VIII. Kuna Mungu Mmoja Tu: Utatu Haupo

1. Mungu ndiye mtawala wa vitu vyote, na anayeendesha vitu vyote. Aliumba vitu vyote, Anaendesha vitu vyote, na pia Anatawala vitu vyote na kukimu vitu vyote. Hii ndiyo hadhi ya Mungu, na utambulisho wa Mungu. Kwa vitu vyote na vyote vilivyopo, utambulisho wa kweli wa Mungu ni Muumbaji, na Mtawala wa vitu vyote. Huo ni utambulisho unaomilikiwa na Mungu, na ni wa kipekee miongoni mwa vitu vyote. Hakuna Kati ya viumbe wa Mungu—wawe miongoni mwa wanadamu, au katika ulimwengu wa kiroho—ambao wanaweza kutumia namna yoyote au kisingizio kuiga au kuchukua nafasi ya utambulisho wa Mungu na hadhi Yake, kwa kuwa kuna mmoja tu kati ya vitu vyote anayemiliki huu utambulisho, nguvu, mamlaka, na uwezo wa kutawala vitu vyote: Mungu wetu wa kipekee Mwenyewe.

Kimetoholewa kutoka katika “Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee X” katika Neno Laonekana katika Mwili

2. Aidha kuna wale wasemao, “je, si Mungu alitaja wazi kuwa Yesu ni Mwanawe mpendwa?” Yesu ni Mwana mpendwa wa Mungu, ambaye anapendezwa naye—haya bila shaka yalitamkwa na Mungu Mwenyewe. Huyu alikuwa Mungu akijitolea ushuhuda Mwenyewe, ila kutoka katika mtazamo tofauti, ule wa Roho aliye mbinguni akitolea ushuhuda kupata Mwili Kwake. Yesu ni kupata mwili Kwake, si Mwanake mbinguni. Je, unaelewa? Je, maneno ya Yesu, “Mimi ni ndani ya Baba naye Baba yu ndani yangu,” hayaonyeshi kuwa Wao ni Roho mmoja? Na si kwa sababu ya kupata mwili kulikosababisha kutenganishwa Kwao kati ya mbinguni na duniani? Uhalisi ni kwamba Wao ni kitu kimoja; hata iweje, ni Mungu anajitolea ushuhuda Mwenyewe. Kutokana na kubadilika kwa enzi, mahitaji ya kazi, na hatua mbalimbali za mpango Wake wa usimamizi, vilevile jina wamwitalo wanadamu hubadilika. Alipokuja kufanya hatua ya kwanza ya kazi, Angeweza kuitwa tu Yehova, mchungaji wa Waisraeli. Katika hatua ya pili, Mungu mwenye mwili Angeweza kuitwa tu Bwana, na Kristo. Lakini wakati huo, Roho aliye mbinguni alikariri tu kwamba Alikuwa Mwana mpendwa wa Mungu, bila kutaja kuwa Alikuwa Mwana wa pekee wa Mungu. Hili halikufanyika kabisa. Mungu angewezaje kuwa na Mwana wa pekee? Basi, Mungu asingekuwa mwanadamu? Kwa kuwa Alikuwa Mwili, Aliitwa Mwana mpendwa wa Mungu na kutokana na hili, kukazuka uhusiano wa Baba na Mwana. Ni kwa sababu tu ya utengano kati ya mbingu na dunia. Yesu aliomba kutokana na msimamo wa mwili. Kwa sababu Alikuwa Amepata mwili wa ubinadamu wa kawaida, ni kutokana na msimamo wa mwili ndipo Alisema: “Umbo Langu la nje ni la kiumbe. Kwa sababu Nilijivisha mwili kuja duniani, sasa Niko mbali, mbali sana na mbinguni.” Kwa sababu hii, Angeomba tu kwa Baba kutokana na msimamo wa mwili. Huu ulikuwa wajibu Wake, ambao ni sharti Roho wa Mungu aliyepata mwili anapaswa kupewa. Haiwezekani kusema kwamba Hawezi kuwa Mungu kwa sababu tu Anamwomba Baba kutokana na msimamo wa mwili. Ijapokuwa Anaitwa Mwana mpendwa wa Mungu, Yeye bado ni Mungu Mwenyewe, ni vile tu Yeye ni mwili wa Roho, na kiini chake bado ni Roho.

Kimetoholewa kutoka katika “Je, Utatu Upo?” katika Neno Laonekana katika Mwili

3. Hili laweza kuwakumbusha watu maneno ya Mungu kutoka katika kitabu cha Mwanzo: “Na tumuumbe mwanadamu katika sura yetu, kwa mfanano wetu.” Ikichukuliwa kuwa Mungu anasema “na tumtengeneze” mtu kwa mfano “wetu,” basi “tu-” inaashiria wawili au wengi; na kwa kuwa anataja “tu-” basi hakuna tu Mungu mmoja. Kwa njia hii, mwanadamu alianza kufikiria udhahania wa nafsi bayana, na kutokana na maneno haya kulitokea dhana ya Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Basi, Baba anafananaje? Je, Mwana anafananaje? Na Roho Mtakatifu anafananaje? Yawezekana kuwa mwanadamu wa leo aliumbwa kwa mfano wa mtu mmoja aliyeunganishwa pamoja kutoka kwa nafsi tatu? Je, sura ya mwanadamu inafanana na ile ya Baba, Mwana, au Roho Mtakatifu? Mwanadamu ni mfano wa nani katika nafsi za Mungu? Mawazo ya mwanadamu ni ya kimakosa na upuuzi! Yanaweza tu Kumgawanya Mungu kuwa Mungu kadhaa. Wakati Musa aliandika kitabu cha Mwanzo, ni baada ya wanadamu kuumbwa baada ya uumbaji wa dunia. Mwanzo kabisa, dunia ilipoanza, Musa hakuwepo. Ni hadi baadaye kabisa ndipo Musa aliandika Biblia, basi angejuaje alichokinena Mungu kutoka mbinguni? Hakuwa na ufahamu wowote jinsi Mungu alivyoumba ulimwengu. Katika Agano la Kale la Biblia, hapakutajwa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, ni Mungu mmoja tu wa kweli, Yehova, akiifanya kazi yake nchini Israeli. Anaitwa majina tofauti kadri enzi zinavyobadilika, ila hili haliwezi kuthibitisha kuwa kila jina linarejelea mtu tofauti. Ingekuwa hivi, basi je, si kungekuwa na nafsi nyingi sana katika Mungu? Kilichoandikwa katika Agano la Kale ni kazi ya Yehova, hatua ya kazi ya Mungu Mwenyewe tangu mwanzo wa Enzi ya Sheria. Ilikuwa ni kazi ya Mungu, ambapo Alinena, ilikuwa, na Alipoamuru, ilitendeka. Hakuna hata wakati mmoja ambapo Yehova alisema kuwa alikuwa Baba aliyekuja kufanya kazi, wala Hakutabiri kuja kwa Mwana kuwakomboa wanadamu. Wakati wa Yesu ulipowadia, ilisemekana tu kwamba Mungu alikuwa Ameupata mwili kuwakomboa wanadamu, si kwamba ni Mwana aliyekuwa amekuja. Kwa sababu enzi hazifanani na kazi ambayo Mungu Mwenyewe hufanya vilevile inatofautiana, Anapaswa kufanya kazi Yake katika milki tofauti, kwa njia hii utambulisho Alionao vilevile unatofautiana. Mwanadamu anaamini kwamba Yehova ndiye Baba ya Yesu, ila hili halijakiriwa na Yesu ambaye alisema: “Hatukubainishwa kamwe kama Baba na Mwana; Mimi na Baba aliye Mbinguni ni kitu kimoja. Baba yu ndani Yangu Nami ni ndani Yake; wanadamu wanapomwona Mwana, wanamwona Baba.” Baada ya yote kusemwa, iwe Baba au Mwana, Wao ni Roho mmoja, Hawajagawanywa kuwa nafsi tofautitofauti. Mara tu wanadamu wanapojaribu kueleza, mambo hutatizwa na wazo la nafsi tofauti, na vilevile na uhusiano kati ya Baba, Mwana na Roho. Mwanadamu akizungumzia nafsi tofauti, je, hili halimfanyi Mungu kuwa kitu? Mwanadamu hata zaidi huziorodhesha nafsi hizi kama nafsi ya kwanza, ya pili, na ya tatu; haya yote ni mawazo ya mwanadamu yasiyofaa kurejelewa, hayana uhalisi kabisa! Ukimwuliza: “Kuna Mungu wangapi?” atasema kuwa Mungu ni Utatu Mtakatifu wa Baba, Mwana na Roho Mtakatifu: Yule mmoja wa kweli. Ukiuliza tena: “Baba ni nani?” atasema: “Baba ni Roho wa Mungu aliye mbinguni; anatawala kila kitu, na kiongozi wa mbinguni.” “Je, Yehova ni Roho?” Atasema: “Ndiyo!” Ukimuuliza tena, “Mwana ni nani?” atasema kuwa Yesu ndiye Mwana, bila shaka. “Basi kisa cha Yesu ni kipi? Alitoka wapi?” Atasema: “Yesu alizaliwa na Maria kupitia kwa utungaji mimba wa Roho Mtakatifu.” “Je, kiini Chake si Roho vilevile? Je, kazi Yake si kiwakilishi cha Roho Mtakatifu? Yehova ni Roho, vivyo hivyo na kiini cha Yesu. Sasa katika siku za mwisho, bila shaka ni Roho Anayeendelea kufanya Kazi; Wangewezaje kuwa nafsi tofauti? Je, si Roho wa Mungu anafanya kazi ya Roho kutoka katika mitazamo tofauti?” Kwa hivyo, hakuna tofauti bayana kati ya nafsi. Yesu alipatikana kwa utungaji mimba wa Roho Mtakatifu, na bila shaka, Kazi Yake hasa ilikuwa ile ya Roho Mtakatifu. Katika hatua ya kwanza ya kazi iliyofanywa na Yehova, Hakuwa mwili au kuonekana kwa mwanadamu. Kwa hivyo mwanadamu hakuona uso Wake. Haijalishi Alikuwa mashuhuri au mrefu kiasi gani, bado Alikuwa Roho, Mungu Mwenyewe aliyemuumba mwanadamu mwanzoni. Yaani, alikuwa Roho wa Mungu. Aliponena na wanadamu kutoka mawinguni, alikuwa Roho tu. Hakuna hata mmoja aliyeuona Uso wake; ni katika Enzi ya Neema tu ambapo Roho wa Mungu alikuwa mwili na Alipata mwili kule Uyahudi ndipo mwanadamu aliona sura ya kupata mwili kama Myahudi. Hisia ya Yehova haingeweza kuhisika. Hata hivyo, Alipatikana kwa utungaji mimba wa Roho Mtakatifu, yaani, Alipatikana kwa utungaji mimba wa Roho wa Yehova Mwenyewe, na Yesu bado alizaliwa kama mfano halisi wa Roho wa Mungu. Alichokiona mwanadamu mwanzoni kilikuwa ni Roho Mtakatifu Akimshukia Yesu kama njiwa; Hakuwa Roho mwenye upekee kwa Yesu tu, badala yake alikuwa Roho Mtakatifu. Basi roho wa Yesu anaweza kutenganishwa na Roho Mtakatifu? Ikiwa Yesu ni Yesu, Mwana, na Roho Mtakatifu ni Roho Mtakatifu, basi wangewezaje kuwa kitu kimoja? Ingekuwa hivyo kazi isingefanywa. Roho ndani ya Yesu, Roho aliye mbinguni, na Roho wa Yehova wote ni mmoja. Anaweza kuitwa Roho Mtakatifu, Roho wa Mungu, Roho aliyezidishwa mara saba, na Roho mwenye vyote. Roho wa Mungu anaweza kufanya kazi nyingi. Ana uwezo wa kuumba na kuiangamiza dunia kwa kuleta mafuriko duniani; Anaweza kuwakomboa wanadamu, aidha, kuwashinda na kuwaangamiza wanadamu wote. Kazi hii yote inafanywa na Mungu Mwenyewe na haiwezi kufanywa na yeyote katika nafsi za Mungu kwa niaba Yake. Roho Wake anaweza kuitwa Yehova na Yesu, na vilevile mwenye Uweza. Yeye ni Bwana na Kristo. Anaweza pia kuwa Mwana wa Adamu. Yuko mbinguni na vilevile duniani; Yuko juu ya dunia na pia miongoni mwa umati. Yeye tu ndiye Bwana wa Mbingu na dunia! Tangu wakati wa uumbaji hadi sasa, kazi hii imekuwa ikifanywa na Roho wa Mungu Mwenyewe. Iwe ni kazi mbinguni au katika mwili, yote hufanywa na Roho Wake Mwenyewe. Viumbe wote, wawe mbinguni au duniani, wamo katika kiganja cha mkono Wake wenye nguvu; yote hii ni kazi ya Mungu na haiwezi kufanywa na yeyote kwa niaba Yake. Mbinguni Yeye ni Roho na vilevile Mungu Mwenyewe; miongoni mwa wanadamu, Yeye ni mwili ila anaendelea kuwa Mungu Mwenyewe. Japo Anaweza kuitwa mamia ya maelfu ya majina, Yeye bado ni Mungu Mwenyewe, na kazi yote ni maonyesho ya moja kwa moja ya Roho Wake. Ukombozi wa wanadamu wote kupitia kwa kusulubiwa Kwake ilikuwa kazi ya moja kwa moja ya Roho Wake, na vilevile tangazo kwa mataifa yote na nchi zote wakati wa siku za mwisho. Wakati wote Mungu anaweza kuitwa mwenye uweza na Mungu mmoja wa kweli, Mungu Mwenyewe mwenye vyote. Nafsi bayana hazipo, aidha dhana ya Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu haipo. Kuna Mungu mmoja mbinguni na duniani!

Kimetoholewa kutoka katika “Je, Utatu Upo?” katika Neno Laonekana katika Mwili

4. Baada ya ukweli wa Yesu aliyepata mwili kutokea, mwanadamu aliamini hili: Si Baba pekee aliye mbinguni, bali pia Mwana, na hata Roho Mtakatifu. Hii ndiyo dhana ya kawaida aliyonayo mwanadamu, kwamba kuna Mungu wa aina hii mbinguni: Utatu ambao ni Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, wote katika nafsi moja. Wanadamu wote wana fikra hizi: Mungu ni Mungu mmoja, ila Anajumuisha sehemu tatu, kile ambacho wale wote waliofungwa kwa huzuni katika hizi dhana za kawaida wanachukulia kuwa kuna Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Ni sehemu hizo tatu pekee ambazo zimefanywa moja ambazo ni Mungu kamili. Bila Baba Mtakatifu, Mungu asingekuwa mkamilifu. Vivyo hivyo, wala Mungu asingekuwa mkamilifu bila Mwana au Roho Mtakatifu. Katika mawazo yao, wanaamini kuwa Baba au Mwana pekee hawezi kuwa Mungu. Ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu tu kwa pamoja wanaoweza kuwa Mungu Mwenyewe. Sasa, waumini wote wa kidini, na hata kila mfuasi miongoni mwenu, anashikilia hii imani. Ilhali, ikiwa hii imani ni sahihi, hakuna anayeweza kuelezea, kwani daima mmechanganyikiwa kuhusu masuala ya Mungu Mwenyewe. Japo hizi ni fikra tu, hamjui kama ni sawa au mbaya, kwani mmeathiriwa vibaya na mawazo ya kidini. Mmeyakubali kwa kina haya mawazo ya kidini yaliyozoeleka, na hii sumu imezama kwa kina ndani yenu. Hivyo basi, hata kwa hili mmeanguka katika huu ushawishi wenye madhara, kwani Utatu haupo. Yaani, Utatu wa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu haupo. Hizi zote ni fikra za kawaida za mwanadamu, na imani za uongo za mwanadamu. Kwa karne nyingi, mwanadamu ameamini katika huu Utatu, ambao umebuniwa na mawazo katika akili za mwanadamu, ukatengenezwa na mwanadamu, na ambao haujawahi kuonekana na mwanadamu. Kwa miaka mingi, kumekuwa na watu maarufu wa kiroho ambao wameeleza “maana ya kweli” ya Utatu, ila maelezo hayo ya Utatu kama nafsi tatu dhahiri yamekuwa si yakini na hayapo wazi na watu wote wamepumbazwa na “ujenzi” wa Mungu. Hakuna mtu maarufu yeyote aliyewahi kutoa maelezo kamili; maelezo mengi yanafaa katika masuala ya mjadala na katika maandishi, ila hakuna hata mtu mmoja ambaye ana ufahamu kamili na wa wazi kuhusu maana ya Utatu. Hii ni kwa sababu huu Utatu huu mkuu ambao mwanadamu anashikilia moyoni kwa hakika haupo.

Kimetoholewa kutoka katika “Je, Utatu Upo?” katika Neno Laonekana katika Mwili

5. Ikiwa yeyote miongoni mwenu anasema kwamba hakika Utatu upo, basi eleza huyu Mungu mmoja katika nafsi tatu ni nini hasa. Baba Mtakatifu ni nini? Mwana ni nini? Roho Mtakatifu ni nini? Je, Yehova ni Baba Mtakatifu? Je, Yesu ni Mwana? Basi, Roho Mtakatifu je? Je, Baba si Roho? Je, kiini cha Mwana vilevile si Roho? Je, kazi ya Yesu haikuwa ya Roho Mtakatifu? Je, kazi ya Yehova haikufanywa wakati ule na Roho sawa tu na kazi ya Yesu? Mungu Anaweza kuwa na Roho wangapi? Kulingana na maelezo yako hizi nafsi tatu, yaani, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu ni mmoja; kama ni hivyo, kuna Roho watatu lakini kuwa na Roho watatu kunamaanisha kuwa kuna Mungu Watatu. Hii inamaanisha kuwa hakuna Mungu Mmoja wa kweli; Mungu wa aina hii anawezaje kuwa kiini asili cha Mungu? Kama unakubali kuwa kuna Mungu mmoja tu, basi Anawezaje kuwa na Mwana na awe Baba? Je, hizi si fikra zako mwenyewe? Kuna Mungu Mmoja tu, nafsi moja katika Mungu huyu, na Roho mmoja tu wa Mungu sawa tu na ilivyoandikwa katika Biblia kwamba “Kuna tu Roho Mtakatifu mmoja na Mungu mmoja tu.” Haijalishi kama Baba na Mwana unaowazungumzia wapo, kuna Mungu mmoja tu, na kiini cha Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu mnaowaamini ni kiini cha Roho Mtakatifu. Kwa maneno mengine, Mungu ni Roho, ila Ana uwezo wa kupata Mwili na kuishi miongoni mwa wanadamu na vilevile kuwa juu ya vitu vyote. Roho Wake anajumuisha kila kitu na Anapatikana kila mahala. Anaweza kuwa katika mwili na wakati huo huo awe ndani na juu ya ulimwengu. Kwa kuwa watu wanasema kwamba Mungu ndiye tu Mungu wa kweli, basi kuna Mungu mmoja, ambaye hawezi kugawanywa kwa mapenzi ya awaye yote! Mungu ni Roho mmoja tu, na nafsi moja; na huyo ni Roho wa Mungu. Ikiwa ni kama usemavyo, Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu, basi Hawa si watatu? Roho Mtakatifu ni kitu kimoja, Mwana ni kingine, na Baba vilevile ni kingine. Nafsi Zao ni tofauti na viini Vyao ni tofauti, iweje basi ziwe kila moja Yao ni sehemu ya Mungu mmoja? Roho Mtakatifu ni Roho; hili ni rahisi kueleweka kwa wanadamu. Ikiwa ni hivyo basi, Baba ni Roho zaidi. Hajawahi kushuka kuja duniani na Hajawahi kupata mwili; Yeye ni Yehova Mungu katika mioyo ya mwanadamu, na kwa hakika Yeye vilevile ni Roho. Basi kuna uhusiano gani kati Yake na Roho Mtakatifu? Je, ni uhusiano kati ya Baba na Mwana? Au ni uhusiano kati ya Roho Mtakatifu na Roho wa Mungu? Je, kiini cha kila Roho ni sawa? Au Roho Mtakatifu ni chombo cha Baba? Hili linaweza kuelezwaje? Aidha kuna uhusiano gani kati ya Mwana na Roho Mtakatifu? Je, ni uhusiano kati ya Roho wawili au ni uhusiano kati ya mwanadamu na Roho? Haya yote ni masuala ambayo hayawezi kuelezewa! Ikiwa Wote ni Roho mmoja, basi hapawezi kuwepo na mjadala kuhusu nafsi tatu, kwani zote zinamilikiwa na Roho mmoja. Kama Zingekuwa nafsi tofauti, basi Roho Zao Zingetofautiana katika nguvu zao na kamwe hawangekuwa Roho mmoja. Hii dhana ya Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu ni upuuzi mtupu! Hili linamweka Mungu katika vitengo na kumgawanya kuwa nafsi tatu, kila moja ikiwa na hadhi na Roho; basi Atawezaje kuwa Roho mmoja na Mungu mmoja?

Kimetoholewa kutoka katika “Je, Utatu Upo?” katika Neno Laonekana katika Mwili

6. Wengine wanaweza kusema: “Baba ni Baba; Mwana ni Mwana; Roho Mtakatifu ni Roho Mtakatifu, na mwishowe, Watafanywa kitu kimoja.” Je, Utawafanyaje kitu kimoja? Baba na Roho Mtakatifu Wawezaje kufanywa kitu kimoja? Ikiwa Walikuwa wawili kiasili, haijalishi Wamewekwa pamoja kwa namna gani, je, Hawataendelea kuwa sehemu mbili? Unaposema kuwa kuwafanya kuwa kitu kimoja, huko si kuunganisha sehemu mbili kutengeneza kitu kamili? Je, Hawakuwa sehemu mbili kabla ya kufanywa kitu kizima? Kila Roho ana kiini kinachotofautiana, na Roho wawili Hawawezi kufanywa kuwa kitu kimoja. Roho si chombo cha kutengenezwa, si kama chombo chochote katika ulimwengu. Kulingana na mitazamo ya wanadamu, Baba ni Roho mmoja, Mwana ni mwingine, na Roho Mtakatifu tena ni mwingine, halafu Roho Hawa huchanganyika sawa na glasi tatu za maji kuunda kitu kimoja kizima. Je, hizo si sehemu tatu zimefanywa kuwa kitu kimoja? Haya bila shaka ni maelezo ya kimakosa! Je, huku si kumgawa Mungu? Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu wanawezaje kufanywa kuwa kitu kimoja? Je, Wao si sehemu tatu zenye asili tofauti?

Kimetoholewa kutoka katika “Je, Utatu Upo?” katika Neno Laonekana katika Mwili

7. Yesu alipomwita Mungu wa mbinguni kwa jina la Baba alipokuwa akiomba, hili lilifanywa katika mitazamo ya mwanadamu aliyeumbwa, kwa sababu Roho wa Mungu alikuwa amevaa mwili wa kawaida na Alikuwa na umbile la nje la mwanadamu aliyeumbwa. Hata ikiwa ndani yake mlikuwa na Roho wa Mungu, umbo Lake la nje bado lilikuwa lile la mtu wa kawaida; kwa maana nyingine, Alikuwa “Mwana wa Adamu” jambo ambalo watu wote, akiwemo Yesu Mwenyewe, walilizungumzia. Na kwa sababu Anaitwa Mwana wa Adamu, Yeye ni mtu (Mwanamke au mwanamume, kwa vyovyote vile mwenye umbo la nje la mwanadamu) aliyezaliwa katika familia ya kawaida ya watu wa kawaida. Kwa hivyo, Yesu kumwita Mungu wa mbinguni kwa jina la Baba kulikuwa sawa na mlivyomwita mara ya kwanza Baba; Alifanya hivyo kutokana na mtazamo wa Mwanadamu aliyeumbwa. Je, mnakumbuka Sala ya Bwana ambayo Yesu aliwafundisha kukariri? “Baba Yetu Uliye mbinguni….” Aliwaambia wanadamu wote wamwite Mungu wa Mbinguni kwa jina la Baba. Na kwa kuwa Naye pia alimwita Baba, alifanya hivyo kutoka kwa mtazamo wa mtu aliye katika daraja moja nanyi nyote. Kwa kuwa mlimuita Mungu wa mbinguni Baba, hili linaonyesha kuwa Yesu alijichukulia kuwa katika daraja sawa nanyi, kama mwanadamu duniani aliyeteuliwa na Mungu (yaani, Mwana wa Mungu). Kama mnamwita Mungu “Baba,” je, hii si kwa sababu nyinyi ni wanadamu walioumbwa? Haijalishi Yesu alikuwa na mamlaka makubwa kiasi gani duniani, kabla ya kusulubiwa, Alikuwa tu Mwana wa Adamu, akiongozwa na Roho Mtakatifu (yaani, Mungu), Akiwa miongoni mwa viumbe wa duniani, kwani bado Alikuwa hajaikamilisha kazi Yake. Kwa hivyo, kumwita kwake Mungu wa mbinguni Baba kulikuwa tu unyenyekevu na utiifu Wake. Yeye kumwita Mungu (yaani, Roho aliye mbinguni) kwa namna ile, hata hivyo, hakudhibitishi kuwa Yeye ni Mwana wa Roho wa Mungu aliye mbinguni. Badala yake, ni kuwa mtazamo wake ni tofauti, si kwamba ni nafsi tofauti. Uwepo wa nafsi tofauti ni uongo. Kabla ya kusulubiwa kwake, Yesu alikuwa Mwana wa Adamu aliyefungwa katika udhaifu wa kimwili, na Hakuwa na mamlaka kamilifu ya Roho. Hiyo ndiyo maana Angeweza tu kutafuta mapenzi ya Mungu Baba kutoka katika mtazamo wa kiumbe. Ni kama tu Alivyoomba mara tatu huko Gethsemane: “Si kama Nitakavyo, bali kama Utakavyo.” Kabla Atundikwe msalabani, Hakuwa zaidi ya Mfalme wa Wayahudi; alikuwa Kristo, Mwana wa Adamu, na wala si mwenye utukufu. Hiyo ndiyo maana, kutokana na mtazamo wa mwanadamu, Alimwita Mungu Baba. Sasa, huwezi kusema kuwa wote wamwitao Mungu Baba ni Wana. Ingekuwa kweli, basi wote si mngekuwa Mwana punde Yesu alipowafundisha Sala ya Bwana? Ikiwa bado hamjaridhika, basi niambieni hili, ni nani mmwitaye Baba? Ikiwa mnamrejelea Yesu, je, Baba ya Yesu ni nani kwenu? Baada ya Yesu kurudi mbinguni, hii dhana ya Baba na Mwana ilikoma. Hii dhana ilifaa tu kipindi ambacho Yesu alikuwa mwili; katika mazingira mengine yoyote, uhusiano ni ule wa kati ya Bwana wa uumbaji na kiumbe mnapomwita Mungu Baba. Hakuna wakati ambapo wazo hili la Utatu wa Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu linaweza kuwa na mashiko; ni uongo ambao ni nadra kuonekana na halipo!

Kimetoholewa kutoka katika “Je, Utatu Upo?” katika Neno Laonekana katika Mwili

8. Hebu Niwaambie hilo, kwa hakika, Mungu wa Utatu hayupo popote katika dunia hii. Mungu hana Baba wala Mwana, na sembuse Baba na Mwana hutumia kwa pamoja Roho Mtakatifu kama chombo. Huu wote ni uongo mkubwa zaidi na haupo kabisa katika dunia hii! Hata hivyo uongo huu una asili yake na haukosi msingi kabisa, kwani akili zenu si punguani, na mawazo yenu hayakosi mantiki. Badala yake, ziko sawa na yenye ubunifu kwa kiasi kikubwa, kwamba haziwezi kuzuiwa hata na Shetani yeyote. La kusikitisha ni kwamba mawazo haya ni uongo mtupu na hayapo kabisa! Hamjaona ukweli halisi haswa; mnabuni na kujiundia dhana, na kuzitengeneza kuwa hadithi ili kuteka imani ya wengine kwa uongo na kupata mamlaka miongoni mwa wanadamu wapumbavu wasio na busara, ili kwamba waamini katika “mafundisho yenu ya kitaaluma” makuu na mashuhuri. Je, huu ni ukweli? Je, hii ndiyo njia ya uzima ambayo wanadamu wanafaa kupokea? Huu ni upuuzi! Hakuna hata neno moja linafaa! Katika miaka hii yote, nyinyi mmegawanya Mungu namna hii, na kuendelea kugawanywa zaidi katika kila kizazi kiasi kwamba Mungu mmoja amegawanywa kuwa Mungu watatu. Na sasa haiwezekani kabisa kwa mwanadamu kumuunganisha Mungu kuwa mmoja kwani mmemgawanya zaidi. Ingekuwa si kazi yangu ya upesiupesi kabla ya muda kuyoyoma, haijulikani mngeishi hivi kwa muda gani! Kuendelea kumgawanya Mungu namna hii, Anawezaje kuendelea kuwa Mungu wenu? Je, bado mngeendelea kumtambua Mungu? Je, bado mngemkiri Yeye kama baba yenu na mumrudie? Ningechelewa hata kidogo, inaonekana kwamba mngewarudisha “Baba na Mwana,” Yehova na Yesu kwenda Israeli na mdai kwamba nyinyi wenyewe ni sehemu ya Mungu. Kwa bahati nzuri, sasa ni siku za mwisho. Hatimaye, siku Niliyoitarajia kwa hamu imewadia, na ni baada tu ya kuifanya hatua hii ya kazi kwa mikono Yangu ndipo kumgawanya kwenu Mungu Mwenyewe kumesitishwa. Isingekuwa hivi, mngezidisha, hadi kuwaweka Mashetani wote miongoni mwenu kwenye meza zenu kwa ajili ya ibada. Hii ndiyo njama yenu! Mbinu yenu ya kumgawanya Mungu! Je, mtaendelea kufanya hivyo sasa? Hebu Niwaulize: Kuna Mungu Wangapi? Ni Mungu Yupi atawaletea wokovu? Je, ni Mungu wa kwanza, wa pili au wa tatu mnayemwomba? Ni nani kati Yao mnayemwamini? Je, ni Baba? Au ni Mwana? Au ni Roho? Niambie ni nani unayemwamini. Ijapokuwa kwa kila neno unasema unamwamini Mungu, mnachokiamini hasa ni akili zenu! Hamna Mungu mioyoni mwenu kabisa! Na bado akilini mwenu mna “Utatu Mtakatifu” kadhaa. Hamkubaliani na hili?

Kimetoholewa kutoka katika “Je, Utatu Upo?” katika Neno Laonekana katika Mwili

Iliyotangulia: VII. Kristo wa Siku za Mwisho ni Bwana wa Hukumu na Mwanakondoo Anayefungua Kitabu

Inayofuata: IX. Tofauti Kati ya Kazi ya Mungu na Ile ya Mwanadamu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Maudhui Yanayohusiana

Kuhusu Maisha ya Petro

Petro ni mfano ambao Mungu aliutambulisha kwa wanadamu, na yeye ni mtu mashuhuri anayejulikana vizuri. Kwa nini mtu mnyonge kama huyo...

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp