IX. Tofauti Kati ya Kazi ya Mungu na Ile ya Mwanadamu

1. Kazi ya Mungu Mwenyewe inahusisha kazi ya wanadamu wote, na pia inawakilisha kazi ya enzi nzima. Hii ni kusema kwamba, kazi ya Mungu mwenyewe inawakilisha harakati na mwelekeo wa kazi yote ya Roho Mtakatifu, ilhali kazi ya mitume inafuata kazi ya Mungu na wala haiongozi enzi, na wala haiwakilishi mitindo ya kazi ya Roho Mtakatifu katika enzi nzima. Huwa wanafanya tu kazi ambayo mwanadamu anapaswa kufanya, ambayo haihusishi kabisa kazi ya usimamizi. Kazi ya Mungu ni mradi ndani ya kazi ya usimamizi. Kazi ya mwanadamu ni wajibu tu wa wanadamu kuweza kutumika na wala haina uhusiano na kazi ya usimamizi. Kwa sababu ya utambulisho na uwakilishaji tofauti wa kazi hii, licha ya ukweli kwamba zote ni kazi za Roho Mtakatifu, kuna tofauti za wazi na bainifu kati ya kazi ya Mungu na kazi ya mwanadamu.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

2. Kazi ya Mungu mwenye mwili huanzisha enzi mpya, na wale wanaoiendeleza kazi Yake ni watu wanaotumiwa naye. Kazi inayofanywa na mwanadamu yote ipo ndani ya huduma ya Mungu mwenye mwili, na haina uwezo wa kwenda zaidi ya mawanda haya. Ikiwa Mungu mwenye mwili haji kufanya kazi Yake, mwanadamu hana uwezo wa kuhitimisha enzi ya zamani, na hana uwezo wa kuikaribisha enzi mpya. Kazi inayofanywa na mwanadamu ipo tu ndani ya wajibu wake ambao unawezekana kibinadamu, na haiwakilishi kazi ya Mungu. Ni Mungu mwenye mwili pekee ndiye anayeweza kuja na kukamilisha kazi ambayo Anapaswa kuifanya, na mbali na Yeye, hakuna anayeweza kuifanya kazi hii badala Yake. Bila shaka, kile Ninachozungumzia ni kuhusiana na kazi ya kufanyika mwili.

Kimetoholewa kutoka katika “Mwanadamu Aliyepotoka Anahitaji Zaidi Wokovu wa Mungu Mwenye Mwili” katika Neno Laonekana katika Mwili

3. Mungu mwenye mwili ana tofauti kubwa na wanadamu wanaotumiwa na Mungu. Mungu mwenye mwili Anaweza kufanya kazi ya uungu, lakini wanadamu wanaotumiwa na Mungu hawawezi. Mwanzoni mwa kila enzi, Roho wa Mungu huongea binafsi kuzindua enzi mpya na kuleta mwanadamu kwenye mwanzo mpya. Wakati Yeye Amemaliza kuongea, hili linaashiria kwamba kazi ya Mungu katika uungu Wake imekamilika. Baada ya hapo, wanadamu wote hufuata mwongozo wa wale ambao wametumiwa na Mungu kuingia katika uzoefu wa maisha.

Kimetoholewa kutoka katika “Tofauti Muhimu Kati ya Mungu Mwenye Mwili na Watu Wanaotumiwa na Mungu” katika Neno Laonekana katika Mwili

4. Kazi ya Mungu hufanywa na Mungu Mwenyewe. Ni Yeye ndiye Anayeweka kazi katika mwendo, na pia Yeye ndiye Anayemaliza. Ni Yeye ndiye hupanga kazi, na pia Yeye ndiye Anayesimamia, na zaidi ya hayo, ni Yeye ndiye Anayeleta kazi kuzaa matunda. Ni ilivyoandikwa katika Biblia, “Mimi ndiye Mwanzo na Mwisho: Mimi ndiye Mpanzi na Mvunaji.” Yote yanayohusiana na usimamizi wa kazi Yake yanafanywa na mkono Wake. Yeye ndiye Mtawala wa mpango wa miaka elfu sita; hakuna anayeweza kufanya kazi Yake kwa niaba Yake ama kuleta kazi Yake hadi mwisho, kwani Yeye ndiye Aliye katika uongozi wa yote. Kwa kuwa Aliumba dunia, Ataongoza ulimwengu mzima kuishi katika nuru Yake, na Atamaliza enzi yote na kuleta mpango Wake wote kwa mafanikio!

Kimetoholewa kutoka katika “Fumbo la Kupata Mwili (1)” katika Neno Laonekana katika Mwili

5. Kazi yote ambayo Mungu Mwenyewe hufanya ni kazi Anayolenga Kufanya katika mpango Wake wa usimamizi na inahusiana na usimamizi mkuu. Kazi ifanywayo na mwanadamu (mwanadamu anayetumiwa na Roho Mtakatifu) hukidhi uzoefu wake binafsi. Anapata njia mpya ya uzoefu mbali na ile iliyotembelewa na wale waliomtangulia na anawaongoza ndugu zake chini ya uongozi wa Roho Mtakatifu. Kinachotolewa na watu hawa ni uzoefu wao ama maandishi ya kiroho ya watu wa kiroho. Ingawa wanatumiwa na Roho Mtakatifu, kazi ya watu kama hao haina uhusiano na kazi ya usimamizi mkuu katika mpango wa miaka elfu sita. Wamesimamishwa na Roho Mtakatifu katika wakati tofauti kuongoza watu katika mkondo wa Roho Mtakatifu hadi wakamilishe kazi yao ama maisha yao yafike mwisho. Kazi wanayofanya ni kutayarisha njia ifaayo kwa ajili ya Mungu Mwenyewe ama kuendeleza kitu kimoja kwa usimamizi wa Mungu Mwenyewe katika dunia. Watu hao hawawezi kufanya kazi kuu katika usimamizi Wake, na hawawezi kufungua njia mpya, ama kumaliza kazi yote ya Mungu kutoka enzi ya kitambo. Kwa hivyo, kazi wafanyayo inawakilisha kiumbe aliyeumbwa pekee akifanya kazi Yake na hawezi kuwakilisha Mungu Mwenyewe Akifanya huduma Yake. Hii ni kwa sababu kazi wanayofanya haifanani na ile inayofanywa na Mungu Mwenyewe. Kazi ya kukaribisha enzi mpya haiwezi kufanywa na mwanadamu kwa niaba ya Mungu. Haiwezi kufanywa na mwingine ila Mungu Mwenyewe. Kazi yote inayofanywa na mwanadamu ni kufanya wajibu wake kama mmoja wa viumbe na inafanywa akiguswa au kupewa nuru na Roho Mtakatifu. Uongozi ambao watu hao hupeana ni jinsi ya kuzoea katika kila siku ya maisha ya mwanadamu na jinsi mwanadamu anapaswa kutenda kwa maelewano na mapenzi ya Mungu. Kazi ya mwanadamu haihusishi usimamizi wa Mungu ama kuwakilisha kazi ya Roho. … Kwa hivyo, kwa sababu kazi ya wanadamu wanaotumiwa na Roho Mtakatifu si sawa na kazi ifanywayo na Mungu Mwenyewe, utambulisho wao na wanayefanya kazi kwa niaba yake ni tofauti. Hii ni kwa sababu kazi ambayo Roho Mtakatifu Analenga Kufanya ni tofauti, na hapo kutoa utambulisho tofauti na hadhi kwa wale wote wafanyao kazi. Wanadamu wanaotumiwa na Roho Mtakatifu wanaweza kufanya kazi mpya na wanaweza kutoa kazi iliyofanywa katika enzi iliyopita, lakini kazi yao haiwezi kueleza tabia na mapenzi ya Mungu kwa enzi mpya. Wanafanya kazi ili kuondoa kazi ya enzi iliyopita tu, sio kufanya kazi mpya kuwakilisha moja kwa moja tabia ya Mungu Mwenyewe. Hivyo, haijalishi matendo mangapi yaliyopitwa na wakati wanakomesha ama matendo mapya wanaanzisha, bado wanawakilisha mwanadamu na viumbe vilivyoumbwa. Mungu Mwenyewe Akifanya kazi, hata hivyo, Hatangazi wazi kukomeshwa kwa matendo ya enzi ya zamani au kutangaza moja kwa moja kuanzishwa kwa enzi mpya. Yeye hufanya kazi Yake moja kwa moja na kwa njia ya moja kwa moja. Yeye hufanya kazi Anayolenga kufanya moja kwa moja; hivyo, yeye hueleza moja kwa moja kazi Aliyoleta, Anafanya kazi Yake moja kwa moja Alivyolenga hapo awali, Akieleza uwepo Wake na tabia Yake. Mwanadamu anavyoona, tabia Yake na kazi Yake pia hazifanani na zile ya kitambo. Hata hivyo, kutoka kwa mtazamo wa Mungu Mwenyewe, huku ni kuendelea na ujenzi zaidi wa kazi Yake. Mungu Mwenyewe Akifanya kazi, Anaeleza neno Lake na Analeta kazi mpya moja kwa moja. Tofauti ni, mwanadamu akifanya kazi, ni kwa ukombozi na kusoma, ama ni kwa maendeleo ya maarifa na mpangilio wa mazoezi iliyojengwa juu ya msingi wa kazi za wengine. Hiyo ni kusema, umuhimu wa kazi inayofanywa na mwanadamu ni ya kuweka mkataba na “kutembea njia za kitambo kwa vitu mpya.” Hii inamanisha kuwa hata njia ambayo inatembelewa na watu wanaotumiwa na Roho Mtakatifu imejengwa juu ya yale yalifunguliwa na Mungu Mwenyewe. Kwa hivyo mwanadamu ni baada ya yote mwanadamu, na Mungu ni Mungu.

Kimetoholewa kutoka katika “Fumbo la Kupata Mwili (1)” katika Neno Laonekana katika Mwili

6. Maneno na kazi za manabii na za wale waliotumiwa na Roho Mtakatifu zote zilikuwa zinafanya wajibu wa mwanadamu, kutekeleza jukumu lake kama kiumbe na kufanya ambacho mwanadamu anapaswa kufanya. Hata hivyo, maneno na kazi za Mungu mwenye mwili ilikuwa ni kuendeleza huduma Yake. Ingawa umbo Lake lilikuwa lile la kiumbe, kazi Yake haikuwa kutimiza majukumu Yake bali Huduma Yake. Dhana “wajibu” inarejelea viumbe ilhali “huduma” inarejelea mwili wa Mungu mwenye mwili. Kuna tofauti kubwa kati ya haya mawili, na haya mawili hayabadilishani nafasi. Kazi ya mwanadamu ni kufanya wajibu wake, ilhali kazi ya Mungu ni kusimamia, na kuendeleza huduma Yake. Kwa hivyo, ingawa mitume wengi walitumiwa na Roho Mtakatifu na manabii wengi wakajazwa na Yeye, kazi zao na maneno yao yalikuwa tu kutimiza wajibu wao kama viumbe. Ingawa unabii wao ungeweza kuwa mkubwa kuliko maisha kama yanavyozungumziwa na Mungu mwenye mwili, na hata ubinadamu wao ulikuwa wa hali ya juu kuliko wa Mungu kuwa mwenye mwili, walikuwa bado wanafanya wajibu wao na wala si kutimiza huduma yao. Wajibu wa mwanadamu unarejelea majukumu yake, na ni kitu kinachoweza kupatwa kwa mwanadamu. Hata hivyo, huduma ifanywayo na Mungu mwenye mwili inahusiana na usimamizi Wake, na haiwezi kufanikishwa na mwanadamu. Hata kama Mungu mwenye mwili hunena, kufanya kazi, au kutenda miujiza, Anafanya kazi kubwa katika usimamizi Wake, kazi ambayo haiwezi kufanywa na mwanadamu kwa niaba Yake. Kazi ya mwanadamu ni kufanya tu wajibu wake kama kiumbe katika hatua fulani ya usimamizi wa Mungu. Bila usimamizi kama huo, yaani, ikiwa huduma ya Mungu mwenye mwili itapotea, pia wajibu wa viumbe utapotea. Kazi ya Mungu kuendeleza huduma Yake ni kumsimamia mwanadamu, ilhali mwanadamu afanyapo wajibu wake ni kutimiza wajibu wake ili kuafikia masharti ya Muumba na haiwezi kwa vyovyote vile kuchukuliwa kwamba ameendeleza huduma ya mtu yeyote. Kwa kiini asili cha Mungu, yaani, Roho, kazi ya Mungu ni usimamizi wake, bali kwa Mungu mwenye mwili akiwa na umbile la nje la kiumbe, kazi yake ni kuendeleza huduma Yake. Kazi yoyote Aifanyayo ni ya kuendeleza huduma Yake, na mwanadamu anaweza tu kufanya awezalo ndani ya upeo Wake wa usimamizi na chini ya uongozi Wake.

Kimetoholewa kutoka katika “Tofauti Kati ya Huduma ya Mungu Mwenye Mwili na Wajibu wa Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

7. Yesu aliwakilisha Roho wa Mungu, na Alikuwa Roho wa Mungu Akifanya kazi moja kwa moja. Alifanya kazi ya enzi mpya, kazi ambayo hakuna aliyekuwa amefanya mbeleni. Yeye Alifungua njia mpya, Alimwakilisha Yehova, na Alimwakilisha Mungu Mwenyewe. Ilhali kwa Petro, Paulo na Daudi, bila kujali walichoitwa, waliwakilisha tu utambulisho wa kiumbe wa Mungu, na walitumwa na Yesu na Yehova. Kwa hivyo bila kujali kiasi cha kazi walichofanya, bila kujali jinsi walivyofanya miujiza kubwa, walikuwa bado tu viumbe wa Mungu, na hawakuweza kuwakilisha Roho Mtakatifu. Walifanya kazi kwa jina la Mungu ama baada ya kutumwa na Mungu; zaidi ya hayo, walifanya kazi katika enzi iliyoanzishwa na Yesu ama Yehova, na kazi waliyoifanya haikutengwa. Walikuwa, hatimaye, viumbe wa Mungu tu.

Kimetoholewa kutoka katika “Kuhusu Majina na Utambulisho” katika Neno Laonekana katika Mwili

8. Yohana alifanya tu kazi ya mwanzo; nyingi ya kazi mpya ilifanywa na Yesu. Yohana alifanya kazi mpya pia, lakini sio yeye aliyeianzisha enzi mpya. … Ingawa Yohana alisema kuwa, “Ninyi tubuni: kwa kuwa ufalme wa mbinguni uko karibu,” na kuhubiri pia injili ya ufalme wa mbinguni, kazi yake haikuwa yenye kina na ilijumuisha tu mwanzo. Kinyume, Yesu Alikaribisha enzi mpya na kuikamilisha enzi ya kitambo, lakini pia Alitimiza sheria ya Agano la Kale pia. Kazi Aliyofanya ni kubwa kuliko ile ya Yohana, na Alikuja kuwakomboa wanadamu wote—Alifanya hatua hii ya kazi. Yohana alitayarisha tu njia. Ingawa kazi yake ilikuwa kubwa, maneno yake mengi, na wale wafuasi waliomfuata wengi, kazi yake haikufanya kitu kingine ila kuletea mwanadamu mwanzo mpya. Mwanadamu hakupokea maisha, njia, ama ukweli wa ndani kutoka kwake, wala mwanadamu hakupata kupitia kwake ufahamu wa mapenzi ya Mungu. Yohana alikuwa nabii mkuu (Eliya) aliyeanza msingi mpya wa kazi ya Yesu na kutayarisha aliyeteuliwa; alikuwa mtangulizi wa Enzi ya Neema. Mambo kama haya hayawezi kutambuliwa kirahisi kwa kuchunguza kuonekana kwao kwa kawaida. Hasa sana, Yohana alifanya kazi kubwa; zaidi ya hayo, alizaliwa kutoka kwa ahadi ya Roho Mtakatifu, na kazi yake ikashikiliwa na Roho Mtakatifu. Hivyo, kutofautisha kati ya utambulisho wao inaweza kufanywa tu kupitia kazi yao, kwa kuwa sura tu ya nje ya mwanadamu haiwezi kuonyesha dutu yake, na mwanadamu hawezi kuhakikisha ushuhuda wa kweli wa Roho Mtakatifu. Kazi iliyofanywa na Yohana na ile iliyofanywa na Yesu si sawa na ilikuwa ya asili tofauti. Hii ndiyo inafaa kuonyesha kama yeye ni Mungu ama sio Mungu. Kazi ya Yesu ilikuwa kuanza, kuendelea, kuhitimisha na kukamilisha. Kila moja ya hatua hizi zilichukuliwa na Yesu, ilhali kazi ya Yohana haikuwa zaidi ya kuanzisha. Hapo mwanzo, Yesu Alieneza injili na kuhubiri njia ya kutubu, na Akaendelea mpaka kumbatiza mwanadamu, kuponya magonjwa, na kukemea mapepo. Mwishowe, Alimkomboa mwanadamu kutoka kwa dhambi na kukamilisha kazi Yake ya enzi yote. Alimhubiria mwanadamu na kueneza injili ya ufalme wa mbinguni katika sehemu zote. Hii ilikuwa sawa na Yohana, tofauti ikiwa kwamba Yesu Alikaribisha enzi mpya na kuleta Enzi ya Neema kwa mwanadamu. Kutoka kwa Mdomo Wake lilitoka neno jinsi mwanadamu anavyopaswa kutenda na njia mwanadamu anayopaswa kufuata Enzi ya Neema, na mwishowe, Akamaliza kazi ya Wokovu. Kazi kama hiyo haingeweza kutekelezwa na Yohana. Kwa hivyo, ni Yesu ndiye Aliyefanya Kazi Ya Mungu Mwenyewe, na ni Yeye ndiye Mungu Mwenyewe na Anamwakilisha Mungu moja kwa moja.

Kimetoholewa kutoka katika “Fumbo la Kupata Mwili (1)” katika Neno Laonekana katika Mwili

9. Maneno ya Mungu mwenye mwili yanaanzisha enzi mpya, yanaongoza wanadamu wote, yanafichua mafumbo, na kumwonyesha mwanadamu mwelekeo mbele katika enzi mpya. Nuru anayoipata mwanadamu ni utendaji au elimu rahisi. Haiwezi kuelekeza binadamu wote kuingia enzi mpya au kufichua fumbo la Mungu Mwenyewe. Mungu, hata hivyo, ni Mungu, na mwanadamu ni mwanadamu.

Kimetoholewa kutoka katika Dibaji ya Neno Laonekana katika Mwili

10. Kile ambacho mwanadamu anakisema ni kile alichokipitia. Ni kile ambacho wamekiona, kile ambacho akili zao zinaweza kukifikia, na kile ambacho milango yao ya fahamu inaweza kuhisi. Hicho ndicho wanachoweza kukifanyia ushirika. Maneno yaliyosemwa na mwili wa Mungu ni onyesho la moja kwa moja la Roho na huonyesha kazi ambayo imefanywa na Roho. Mwili haujaipitia au kuiona, lakini bado huonyesha asili Yake kwa sababu kiini cha mwili ni Roho, na huonyesha kazi ya Roho. Ingawa mwili hauwezi kuifikia, ni kazi ambayo tayari imefanywa na Roho. Baada ya kufanyika mwili, kupitia uonyeshaji wa mwili, Anawasaidia watu kujua asili ya Mungu na kuwafanya watu kuiona tabia ya Mungu na kazi ambayo Ameifanya. Kazi ya mwanadamu inawawezesha watu kuelewa kwa uwazi kuhusu kile wanachopaswa kuingia kwacho na wanachopaswa kukielewa; inahusisha kuwaongoza watu kupata ufahamu na kuujua ukweli. Kazi ya mwanadamu ni kuwaendeleza watu; kazi ya Mungu ni kufungua njia mpya na kufungua enzi mpya kwa ajili ya binadamu, na kuwafunulia watu kile ambacho hakijafahamika kwa watu wenye mwili wa kufa, ikiwasaidia kuelewa tabia Yake. Kazi ya Mungu ni kuwaongoza wanadamu wote.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

11. Manabii wa Agano la Kale walitoa unabii, na vivyo hivyo, pia na Yesu. Ni kwa nini iwe hivi? Tofauti hapa inapatikana katika aina ya kazi zao. Ili kutambua suala hili, huwezi kuangazia asili ya mwili na hufai kuangazia upurukushani wa maneno ya mtu. Daima ni sharti kwanza uangazie kazi yake na athari ambayo kazi yake inafanikisha ndani ya mwanadamu. Unabii uliotolewa na manabii wakati ule, haukuyaruzuku maisha ya mwanadamu, na ujumbe uliopokelewa na watu kama Isaya na Danieli ulikuwa tu unabii na si njia ya uzima. Ingekuwa si kuonekana moja kwa moja kwa Yehova, hakuna ambaye angefanya hiyo kazi, ambayo haiwezekani kwa wanadamu. Yesu pia Alisema mengi, lakini maneno yake yalikuwa njia ya uzima ambayo kwayo mwanadamu angepata njia ya kutenda. Hii ni kusema kuwa, kwanza, Angeukimu uzima wa mwanadamu, kwa kuwa Yesu ni uzima; pili, Angeweza kuugeuza upotovu wa mwanadamu; tatu, kazi Yake ingeweza kuifuata ile ya Yehova ili kuendeleza enzi; nne, Angeweza kutambua mahitaji ya mwanadamu kwa ndani na kufahamu anachokosa mwanadamu; tano, Angeweza kuanzisha enzi mpya na kutamatisha enzi ya zamani. Ndiyo maana Anaitwa Mungu na Kristo; Yeye si tofauti na Isaya tu; bali pia na manabii wengine wote. Chukua Isaya kama ulinganisho wa kazi za manabii. Kwanza, asingeweza kuukimu uzima wa mwanadamu; pili, asingeweza kuanzisha enzi mpya. Alikuwa akifanya kazi chini ya uongozi wa Yehova wala si kuanzisha enzi mpya. Tatu, alichokizungumza yeye mwenyewe kilikuwa nje ya ufahamu wake. Alikuwa akipata ufunuo moja kwa moja kutoka kwa Roho wa Mungu, na wengine wasingeelewa hata baada ya kuusikiliza ufunuo huo. Haya machache yanatosha kuthibitisha kuwa kazi yake haikuwa zaidi ya unabii, si zaidi ya kazi iliyofanywa kwa niaba ya Yehova. Hata hivyo, asingeweza kumwakilisha Yehova kikamilifu. Alikuwa mtumishi wa Yehova, chombo katika kazi ya Yehova. Aidha alikuwa anafanya kazi katika Enzi ya Sheria tu na katika mawanda ya kazi ya Yehova; hakufanya kazi nje ya Enzi ya Sheria. Kinyume na haya, kazi ya Yesu ilikuwa tofauti. Alivuka mipaka ya kazi ya Yehova; Alifanya kazi kama Mungu mwenye mwili na kupitia mateso ili amkomboe mwanadamu. Hiyo ni kusema kuwa Alifanya kazi mpya nje ya ile iliyofanywa na Yehova. Huku kulikuwa kukaribisha kwa enzi mpya. Jambo jingine ni kuwa Aliweza kuyazungumzia mambo ambayo mwanadamu asingeweza kupata. Kazi Yake ilikuwa kazi ndani ya usimamizi wa Mungu na ilijumuisha wanadamu wote. Hakufanya kazi miongoni mwa watu wachache tu, na wala kazi yake haikuwa kuwaongoza watu wachache tu. … Kutokana na kazi Yake, inaweza kuonekana kuwa, kwanza, Anaweza kufungua enzi mpya; pili, Yeye ana uwezo wa kuyaruzuku maisha ya mwanadamu na kumwonyesha mwanadamu njia ya kufuata. Hii inatosha kuthibitisha kuwa Yeye ni Mungu Mwenyewe. Angalau kazi Aifanyayo yaweza kumwakilisha kikamilifu Roho Mtakatifu wa Mungu na kutokana na kazi hiyo inaonekana kuwa Roho wa Mungu yupo ndani Yake. Kwa kuwa kazi iliyofanywa na Mungu mwenye mwili ilikuwa kuanzisha enzi mpya, kuongoza kazi mpya, na kuanzisha na kufungua mazingira mapya, haya mambo machache tu yanatosha kuthibitisha kuwa Yeye ni Mungu Mwenyewe. Hili kwa hivyo linamtofautisha na Isaya, Danieli, na manabii wengine wakuu.

Kimetoholewa kutoka katika “Tofauti Kati ya Huduma ya Mungu Mwenye Mwili na Wajibu wa Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

12. Mnapaswa kujua jinsi ya kutofautisha kazi ya Mungu na kazi ya mwanadamu. Mnaweza kuona nini katika kazi ya mwanadamu? Kuna vitu vingi ambavyo ni uzoefu wa mwanadamu katika kazi ya mwanadamu; kile ambacho mwanadamu anakionyesha kile alicho. Kazi ya Mungu pia inaonyesha kile Alicho, lakini kile Alicho ni tofauti na mwanadamu alivyo. Kile mwanadamu alicho ni kiwakilishi cha uzoefu na maisha ya mwanadamu (kile ambacho mwanadamu anakipitia au kukabiliana nacho katika maisha yake, au falsafa za kuishi alizo nazo), na watu wanaoishi katika mazingira tofauti huonyesha nafsi tofauti. Kama una uzoefu wa kijamii au la na jinsi ambavyo unaishi na kupitia uzoefu katika familia yako inaweza kuonekana katika kile unachokionyesha, wakati ambapo huwezi kuona kutoka kwa kazi ya Mungu mwenye mwili kama Ana uzoefu wa maisha ya kijamii au Hana. Anatambua vizuri asili ya mwanadamu, Anaweza kufunua aina za matendo yote yanayohusiana na kila aina ya watu. Ni mzuri hata katika kufunua tabia ya dhambi ya mwanadamu na tabia yake ya uasi. Haishi miongoni mwa watu wa kidunia, lakini Anatambua asili ya watu wenye mwili wa kufa na upotovu wote wa watu wa duniani. Hicho ndicho Alicho. Ingawa Hashughuliki na dunia, Anajua kanuni za kushughulika na dunia, kwa sababu Anaielewa vizuri asili ya mwanadamu. Anajua kuhusu kazi ya Roho ambayo jicho la mwanadamu haliwezi kuiona na kwamba masikio ya mwanadamu hayawezi kusikia, wanadamu wa leo na wanadamu wa enzi zote. Hii inajumuisha hekima ambayo sio falsafa ya kuishi na makuu ambayo ni ngumu kwa watu kuelewa. Hiki ndicho Alicho, kuwekwa wazi kwa watu na pia kufichika kwa watu. Kile Anachoonyesha sio kile ambacho mwanadamu asiye wa kawaida alicho, bali ni tabia za asili na uungu wa Roho. Hasafiri ulimwenguni mzima lakini anajua kila kitu kuhusu ulimwengu. Anawasiliana na “sokwe” ambao hawana maarifa au akili, lakini Anaonyesha maneno ambayo ni ya kiwango cha juu kuliko maarifa na juu ya watu wakubwa duniani. Anaishi miongoni mwa kundi la wanadamu wapumbavu na wasiojali ambao hawana ubinadamu na ambao hawaelewi mila na desturi za ubinadamu na maisha, lakini Anaweza kumwambia mwanadamu kuishi maisha ya kawaida, na kwa wakati uo huo kufichua ubinadamu duni na wa chini wa binadamu. Haya yote ndiyo kile Alicho, mkuu kuliko vile ambacho mwanadamu yeyote wa damu na nyama alicho. Kwake Yeye, si lazima kupitia maisha ya kijamii magumu na changamani, ili Aweze kufanya kazi Anayotaka kufanya na kwa kina kufichua asili ya mwanadamu aliyepotoka. Maisha duni ya kijamii ambayo hayauadilishi mwili Wake. Kazi Yake na maneno Yake hufichua tu kutotii kwa mwanadamu na hayampi mwanadamu uzoefu na masomo kwa ajili ya kushughulika na ulimwengu. Hahitaji kuipeleleza jamii au familia ya mwanadamu wakati Anapompa mwanadamu uzima. Kumweka wazi na kumhukumu wanadamu sio maonyesho wa uzoefu wa mwili Wake; ni kufichua vile mwanadamu asivyokuwa na haki baada ya kufahamu kutotii kwa mwanadamu na kuchukia upotovu wa mwanadamu. Kazi yote Anayoifanya ni kufichua tabia Yake kwa mwanadamu na kuonyesha asili Yake. Ni Yeye tu ndiye anayeweza kuifanya kazi hii, sio kitu ambacho mtu mwenye mwili na damu anaweza kukipata. Kwa kuangalia kazi Yake, mwanadamu hawezi kuelezea Yeye ni mtu wa aina gani. Mwanadamu hawezi kumwainisha kama mtu aliyeumbwa kwa misingi ya kazi Yake. Kile Alicho pia kinamfanya Asiweze kuainishwa kama mtu aliyeumbwa. Mwanadamu anaweza kumwona tu kama Asiye mwanadamu, lakini hajui amwainishe katika kundi gani, kwa hivyo mwanadamu analazimika kumwainisha katika kundi la Mungu. Si busara kwa mwanadamu kufanya hivi, kwa sababu Amefanya kazi kubwa miongoni mwa watu, ambayo mwanadamu hawezi kufanya.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

13. Wakati Mungu Anakuja duniani, Yeye Anafanya tu kazi Yake ndani ya uungu. Hili ndilo Roho wa mbinguni amemwaminia Mungu mwenye mwili. Anapokuja, anakwenda tu kuzungumza kila mahali, kutamka matamshi Yake kwa njia tofauti na kutoka kwa mitazamo tofauti. Yeye kimsingi Anachukulia kumruzuku mwanadamu na kumfundisha mwanadamu kama malengo Yake na kanuni Zake za kazi na hajihusishi na vitu kama uhusiano kati ya wanadamu au maelezo ya maisha ya wanadamu. Huduma Yake kuu ni kuzungumza kwa niaba ya Roho. Wakati Roho wa Mungu Anaonekana katika mwili kwa hali iliyo wazi, Yeye hukimu uzima wa mwanadamu na kuuweka wazi ukweli tu. Yeye hajihusishi katika kazi ya mwanadamu, yaani, Yeye hashiriki katika kazi ya binadamu. Binadamu hawezi kufanya kazi ya uungu, na Mungu hashiriki katika kazi za binadamu.

Kimetoholewa kutoka katika “Tofauti Muhimu Kati ya Mungu Mwenye Mwili na Watu Wanaotumiwa na Mungu” katika Neno Laonekana katika Mwili

14. Shetani anaweza tu kushindwa kabisa ikiwa Mungu mwenye mwili anahukumu upotovu wa mwanadamu. Kuwa sawa na mwanadamu akiwa na ubinadamu wa kawaida, Mungu mwenye mwili anaweza kumhukumu mwanadamu asiye na haki; hii ni ishara ya utakatifu Wake wa ndani na hali Yake ya kutokuwa wa kawaida. Ni Mungu pekee ndiye anayestahili, na aliye katika nafasi ya kumhukumu mwanadamu, maana Ana ukweli, na mwenye haki, na kwa hivyo Ana uwezo wa kumhukumu mwanadamu. Wale ambao hawana ukweli na haki hawafai kuwahukumu wengine.

Kimetoholewa kutoka katika “Mwanadamu Aliyepotoka Anahitaji Zaidi Wokovu wa Mungu Mwenye Mwili” katika Neno Laonekana katika Mwili

15. Kazi inayofanywa na mwanadamu inawakilisha tu mawanda finyu, na Mungu anapofanya kazi Yake hazungumzi na watu fulani, bali Anazungumza na wanadamu wote, na wale wote wanaoikubali kazi Yake. Mwisho Anaoutangaza ni mwisho wa wanadamu wote, na sio mwisho wa mtu fulani tu. Hamtendei mtu yeyote kwa umahususi, wala hampendelei mtu yeyote, na Anafanya kazi kwa ajili ya, na Anazungumza na wanadamu wote.

Kimetoholewa kutoka katika “Mwanadamu Aliyepotoka Anahitaji Zaidi Wokovu wa Mungu Mwenye Mwili” katika Neno Laonekana katika Mwili

16. Kazi ya Mungu haina masharti na haifungwi na muda au mipaka ya kijiografia. Anaweza kuonyesha kile Alicho wakati wowote, mahali popote. Anafanya kazi vile Anavyopenda. Kazi ya mwanadamu ina masharti na muktadha; vinginevyo hana uwezo wa kufanya kazi na hawezi kuonyesha ufahamu wake wa Mungu au uzoefu wake wa ukweli. Unatakiwa tu kulinganisha tofauti baina yao ili kuonyesha kama ni kazi ya Mungu mwenyewe au kazi ya mwanadamu.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

17. Kazi ya mwanadamu ina mipaka na kadiri inavyoweza kufika. Mtu mmoja anaweza tu kufanya kazi ya wakati fulani na hawezi kufanya kazi ya enzi nzima—vinginevyo, angewaongoza watu katika kanuni. Kazi ya mwanadamu inaweza kufaa tu katika kipindi au awamu fulani. Hii ni kwa sababu uzoefu wa mwanadamu una mawanda. Mtu hawezi kulinganisha kazi ya mwanadamu na kazi ya Mungu. Njia za mwanadamu kutenda na maarifa yake ya ukweli yote yanatumika tu katika mawanda fulani. Huwezi kusema kwamba njia ambayo mwanadamu anaiendea ni matakwa ya Roho Mtakatifu kabisa, kwa sababu mwanadamu anaweza kupewa nuru na Roho Mtakatifu tu na hawezi kujazwa kikamilifu na Roho Mtakatifu. Vitu ambavyo mwanadamu anaweza kuvipitia vyote vipo ndani ya mawanda ya ubinadamu na haviwezi kuzidi mawanda ya fikira katika akili ya kawaida ya mwanadamu. Wale wote wanaoweza kuishi kwa kudhihirisha uhalisi wa ukweli hupitia ndani ya mawanda haya.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

18. Mawanda ambayo ukweli unaeleweka kwa mwanadamu siku zote umejikita katika hali tofauti tofauti za watu, na hivyo hazifanani. Kwa njia hii, maarifa yanayoonyesha ukweli ule ule na watu tofauti havifanani. Huu kusema, uzoefu wa mwanadamu siku zote una mipaka, na hauwezi kuwakilisha kikamilifu matakwa ya Roho Mtakatifu, na kazi ya mwanadamu haiwezi kuchukuliwa kama kazi ya Mungu, hata kama kile kinachoonyeshwa na mwanadamu kinafanana kwa karibu sana na mapenzi ya Mungu, hata kama uzoefu wa mwanadamu unakaribiana sana na kazi ya ukamilifu itakayofanywa na Roho Mtakatifu. Mwanadamu anaweza kuwa tu mtumishi wa Mungu, akifanya kazi ambayo Mungu amemwaminia. Mwanadamu anaweza kuonyesha maarifa tu chini ya nuru ya Roho Mtakatifu na ukweli alioupata kutokana na uzoefu wake binafsi. Mwanadamu hana sifa na hana vigezo vya kuwa njia ya Roho Mtakatifu. Hana uwezo wa kusema kuwa kazi ya mwanadamu ni kazi ya Mungu. Mwanadamu ana kanuni za kufanya kazi za mwanadamu, na wanadamu wote wana uzoefu tofauti na wana hali zinazotofautiana. Kazi ya mwanadamu inajumuisha uzoefu wake wote chini ya nuru ya Roho Mtakatifu. Uzoefu huu unaweza tu kuwakilisha asili ya mwanadamu na hauwakilishi asili ya Mungu, au mapenzi ya Roho Mtakatifu. Kwa hivyo, njia anayoipita mwanadamu haiwezi kusemwa kuwa njia anayoipita Roho Mtakatifu, kwa sababu kazi ya mwanadamu haiwezi kuwakilisha kazi ya Mungu na kazi ya mwanadamu na uzoefu wa mwanadamu sio matakwa ya Roho Mtakatifu.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

19. Kazi ya mwanadamu ina hatari ya kuangukia katika kanuni, na mbinu za kazi yake zimefinywa katika uelewa wake finyu na hawezi kuwaongoza watu katika njia huru. Wafuasi wengi wanaishi ndani ya mawanda finyu, na uzoefu wao pia unakuwa ni finyu. Uzoefu wa mwanadamu siku zote ni finyu; mbinu ya kazi yake pia ni finyu na haiwezi kulinganishwa na kazi ya Roho Mtakatifu au kazi ya Mungu Mwenyewe—hii ni kwa sababu uzoefu wa mwanadamu, hatimaye, ni finyu. Hata hivyo Mungu anafanya kazi Yake, hakuna kanuni kwa kazi yake; vyovyote vile inavyofanywa, haifungwi na njia moja. Hakuna kanuni za aina yoyote ile katika kazi ya Mungu—kazi Yake yote ni huru na ni bure. Haijalishi ni muda kiasi gani mwanadamu anatumia kumfuata Yeye, hawawezi kutengeneza sheria zozote za njia anavyofanya kazi. Ingawaje kazi Yake inaongozwa na kanuni, siku zote inafanywa katika njia mpya na siku zote inakuwa na maendeleo mapya ambayo yanazidi uwezo wa mwanadamu. Katika kipindi fulani, Mungu anaweza kuwa na njia nyingi tofauti tofauti za kazi na njia tofauti za kuongoza, Akiruhusu watu siku zote kuwa na kuingia kupya na mabadiliko mapya. Huwezi kuelewa sheria za kazi Yake kwa sababu siku zote Anafanya kazi katika njia mpya. Ni kwa njia hii tu ndiyo wafuasi wa Mungu hawawezi kuanguka katika kanuni. Kazi ya Mungu Mwenyewe siku zote inaepuka mitazamo ya watu na kupinga mitazamo yao. Ni wale tu ambao wanamfuata Yeye kwa moyo wote ndio wanaoweza kubadilishwa tabia zao na wanaweza kuishi kwa uhuru bila kuwa chini ya kanuni zozote au kufungwa na mitazamo yoyote ya kidini. Madai ambayo kazi ya mwanadamu inawawekea watu yamejikita katika uzoefu wake mwenyewe na kile ambacho yeye mwenyewe anaweza kutimiza. Kiwango cha matakwa haya kimejifunga ndani ya mawanda fulani, na mbinu za kutenda pia ni finyu sana. Kwa hivyo wafuasi bila kutambua huishi ndani ya matakwa finyu; kadiri muda unavyokwenda, yanakuwa kanuni na taratibu za kidini.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

20. Watu wanapofanya kazi, wao hutafuta na kupapasa huku na kule, kila mara wakiiga na kufikiria sana kwa kutegemea msingi uliowekwa na wengine ili kutimiza kuingia kwa ndani zaidi. Kazi ya Mungu ni utoaji wa kile Alicho, na Yeye hufanya kazi ambayo Yeye Mwenyewe anapaswa kufanya. Hatoi riziki kwa kanisa kwa kutumia ufahamu kutoka katika kazi ya mwanadamu yeyote. Badala yake, Yeye hufanya kazi ya sasa kwa kutegemea hali za watu. Hivyo, kufanya kazi kwa njia hii ni mara elfu huru zaidi kuliko kazi ambayo watu hufanya. Kwa watu, inaweza hata kuonekana kwamba Mungu hazingatii wajibu Wake na Hufanya kazi kwa namna yoyote Apendayo—lakini kazi yote ambayo Yeye hufanya ni mpya. Lakini, unapaswa kujua kwamba kazi ya Mungu mwenye mwili kamwe haitegemezwi kwa hisia.

Kimetoholewa kutoka katika “Utendaji (5)” katika Neno Laonekana katika Mwili

21. Kazi ya mwanadamu inawakilisha uzoefu wake na ubinadamu wake. Kile ambacho mwanadamu anatoa na kazi ambayo anafanya vinamwakilisha yeye. Kuona kwa mwanadamu, kufikiri kwa mwanadamu, mantiki ya mwanadamu na uwezo wake mkubwa wa kufikiri vyote vinajumuishwa katika kazi yake. Kimsingi, uzoefu wa mwanadamu, unaweza zaidi kuwakilisha kazi yake na kile ambacho mtu amekipitia kitakuwa ni sehemu ya kazi yake. Kazi ya mwanadamu inaweza kuonyesha uzoefu wake. … Na kazi ya Roho Mtakatifu mara nyingi inabadilika kulingana na hali ya mwanadamu. Anafanya kazi kulingana na uzoefu wa mwanadamu na wala hamshurutishi mwanadamu bali anamsihi mwanadamu kulingana na hali yake ya kawaida ya uzoefu wake. Hii ni kusema kwamba ushirika wa mwanadamu unatofautiana na neno la Mungu. Kile ambacho mwanadamu hushiriki kinaeleza vile anavyotazama mambo na uzoefu wake, kinaonyesha kile wanachokiona na kupitia uzoefu kwa msingi wa kazi ya Mungu. Wajibu wao ni kutafuta, baada ya Mungu kufanya kazi au kuzungumza, kile wanachopaswa kufanya au kuingia kwacho, halafu kukiwasilisha kwa wafuasi. Hivyo, kazi ya mwanadamu inawakilisha kuingia au matendo yake. Bila shaka, kazi hiyo imechanganyika na masomo ya kibinadamu na uzoefu au mawazo ya kibinadamu. … Kile ambacho mwanadamu huonyesha ni kile anachokiona, kupitia uzoefu na kukitafakari. Hata kama ni mafundisho au fikira, haya yote hufikiwa na fikira za mwanadamu. Bila kujali ukubwa wa kazi ya mwanadamu, haiwezi kuzidi mawanda ya uzoefu wa mwanadamu, kile ambacho mwanadamu huona, au kile ambacho mwanadamu anaweza kukitafakari au kuingia akilini mwake. Kile ambacho Mungu anaonyesha ndivyo hivyo Mungu Mwenyewe alivyo, na hii ni nje ya uwezo wa mwanadamu, yaani, nje ya uwezo wa kufikiri kwa mwanadamu. Anaonyesha kazi Yake ya kuwaongoza wanadamu wote, na hii haihusiani na undani wa uzoefu wa mwanadamu, badala yake inahusu usimamizi Wake. Mwanadamu anaonyesha uzoefu wake wakati Mungu anaonyesha nafsi Yake—nafsi hii ni tabia Yake ya asili na iko nje ya uwezo wa mwanadamu. Uzoefu wa mwanadamu ni kuona kwake na kupata maarifa kulingana na uonyeshaji wa Mungu wa nafsi Yake. Kuona kama huko na maarifa kama hayo yanaitwa asili ya mwanadamu. Yanaonyeshwa kwa msingi wa tabia asili ya mwanadamu na ubora wa tabia yake halisi; hivyo pia vinaitwa nafsi ya mwanadamu.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

22. Kazi katika akili ya mwanadamu inafikiwa kwa urahisi sana na mwanadamu. Wachungaji na viongozi katika ulimwengu wa kidini, kwa mfano, wanategemea karama zao na nafasi zao katika kufanya kazi zao. Watu wanaowafuata kwa muda mrefu wataambukizwa na karama zao na kuvutwa na vile walivyo. Wanalenga karama za watu, uwezo na maarifa ya watu, na wanamakinikia mambo ya kimiujiza na mafundisho mengi yasiyokuwa na uhalisi (kimsingi, haya mafundisho ya kina hayawezi kutekelezeka). Hawalengi mabadiliko ya tabia za watu, badala yake wanalenga kuwafundisha watu uwezo wao wa kuhubiri na kufanya kazi, kuboresha maarifa ya watu na mafundisho yao mengi ya kidini. Hawalengi kuona ni kwa kiasi gani tabia ya watu imebadilika au ni kwa kiasi gani watu wanauelewa ukweli. Wala hawajali kuhusu viini vya watu, wala kujua hali za watu za kawaida na zisizo za kawaida. Hawapingi mitazamo ya watu au kufichua fikira zao, sembuse kuwapogoa watu kwa ajili ya upungufu wao wa dhambi. Wengi wanaowafuata wanahudu kwa vipaji vyao, na yote wanayotoa ni fikira za kidini na nadharia za theolojia, ambazo haziambatani na uhalisi na haziwezi kabisa kuwapa watu uzima. Kwa kweli, kiini cha kazi yao ni kulea talanta, kumlea mtu kuwa mhitimu mwenye talanta aliyemaliza mafunzo ya kidini ambaye baadaye anakwenda kufanya kazi na kuongoza. Kwa miaka elfu sita ya kazi ya Mungu unaweza kupata sheria zozote kuihusu? Kuna kanuni na vizuizi vingi katika kazi ambayo mwanadamu hufanya, na ubongo wa mwanadamu umejazwa na mafundisho mengi ya kidini. Hivyo mwanadamu anachokionyesha ni kiasi cha maarifa na utambuzi ndani ya uzoefu wake wote. Mwanadamu hawezi kuonyesha kitu chochote zaidi ya hiki. Uzoefu au maarifa ya mwanadamu hayaibuki kutoka ndani ya karama zake za ndani au tabia yake; vinaibuka kwa sababu ya uongozi wa Mungu na uchungaji wa moja kwa moja wa Mungu. Mwanadamu ana ogani tu ya kupokea uongozi huu na sio ogani ya kuonyesha moja kwa moja uungu. Mwanadamu hana uwezo wa kuwa chanzo, anaweza kuwa tu chombo ambacho hupokea maji kutoka kwa chanzo; hii ni silika ya mwanadamu, ogani ambayo mtu anapaswa kuwa nayo kama mwanadamu. Ikiwa mtu anapoteza ogani ya kukubali neno la Mungu na kupoteza silika ya kibinadamu, mtu huyo anapoteza pia kile ambacho ni cha thamani sana, na anapoteza wajibu wa mwanadamu aliyeumbwa. Ikiwa mtu hana maarifa au uzoefu wa neno la Mungu au kazi Yake, mtu huyo anapoteza wajibu wake, wajibu anaopaswa kuutimiza kama kiumbe aliyeumbwa, na kupoteza heshima ya kiumbe aliyeumbwa.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

23. Hata hivyo, kazi ya Mungu ni tofauti na kazi ya mwanadamu, na aidha, maonyesho Yake yanawezaje kuwa sawa na ya mwanadamu? Mungu ana tabia Yake Mwenyewe ya pekee, ilhali mwanadamu ana wajibu ambao anapaswa kutimiza. Tabia ya Mungu inaonyeshwa katika kazi Yake, ilhali wajibu wa mwanadamu unadhihirishwakatika uzoefu wa mwanadamu na kuonyeshwa katika kazi za mwanadamu. Kwa hiyo inakuwa dhahiri kupitia kazi inayofanywa iwapo jambo fulani ni maonyesho ya Mungu ama maonyesho ya mwanadamu. Halihitaji kufafanuliwa na Mungu Mwenyewe, wala halihitaji mwanadamu ajitahidi kushuhudia; aidha, halimhitaji Mungu Mwenyewe kumkandamiza mtu yoyote. Yote haya yanakuja kama ufunuo wa kawaida; hayalazimishwi wala silo jambo ambalo mwanadamu anaweza kuingilia kati. Wajibu wa mwanadamu unaweza kujulikana kupitia uzoefu wake, na hauhitaji watu wafanye kazi yoyote ya ziada inayohusu uzoefu wao. Nafsi yote ya mwanadamu inaweza kufichuliwa wakati anapotimiza wajibu wake, wakati Mungu anaweza kuonyesha tabia Yake ya asili anapotekeleza kazi Yake. Ikiwa ni kazi ya mwanadamu basi haiwezi kufichika. Ikiwa ni kazi ya Mungu, basi haiwezekani hata zaidi kwa tabia ya Mungu kufichwa na yeyote, sembuse kudhibitiwa na mwanadamu. Hakuna mwanadamu anayeweza kusemekana kuwa Mungu, wala kazi na maneno yake kuonekana kuwa matakatifu ama kuchukuliwa kuwa yasiyobadilika. Mungu anaweza kusemekana kuwa mwanadamu kwa sababu Amejivika mwili, lakini kazi Yake haiwezi kuchukuliwa kuwa kazi ya mwanadamu ama wajibu wa mwanadamu. Aidha, matamshi ya Mungu na nyaraka za Paulo hayawezi kulinganishwa, wala hukumu na kuadibu kwa Mungu na maneno ya mwanadamu ya kuagiza kuzungumziwa kuwa sawa. Kwa hiyo, kuna kanuni zinazotofautisha kazi ya Mungu na kazi ya mwanadamu. Zinatofautishwa kulingana na viini vyao, sio kwa upana wa kazi ama ustadi wake wa muda. Watu wengi hufanya makosa ya kanuni kuhusiana na hili.

Kimetoholewa kutoka katika “Msimamo Wako Kuhusu Nyaraka Kumi na Tatu ni Upi?” katika Neno Laonekana katika Mwili

24. Kwa sababu binadamu ni, kwa hakika, binadamu, na wanaweza tu kuangalia kila kitu kutoka kwa mtazamo na kutoka katika kimo cha mtu. Hata hivyo, Mungu mwenye mwili ni tofauti kabisa na mtu aliyepotoka. Bila kujali ni vipi ambavyo mwili wa Mungu mwenye mwili ulivyo wa kawaida, ulivyo kama wengine, ulivyo wa chini, au hata namna ambavyo watu wanamdharau Yeye, fikira Zake na mwelekeo Wake kwa wanadamu ni mambo ambayo hakuna binadamu angeweza kufuatisha na wala hakuna binadamu angeweza kuiga. Siku zote Atawaangalia wanadamu kutoka kwa mtazamo wa uungu, kutoka katika kimo cha madaraka Yake kama Muumba. Siku zote Atawaona wanadamu kupitia katika kiini na akili ya Mungu. Hawezi kabisa kuwaona wanadamu kutoka katika kimo cha mtu wa kawaida na kutoka kwa mtazamo wa mtu aliyepotoka. Watu wanapowaangalia wanadamu, wanawaangalia kwa mtazamo wa binadamu, na wanatumia mambo kama vile maarifa ya binadamu na masharti na nadharia za binadamu kama kipimo. Hali hii imo ndani ya mawanda ya kile ambacho watu wanaweza kuona kwa macho yao; ni ndani ya upana ambao watu waliopotoka wanaweza kutimiza. Mungu anapowatazama wanadamu, Anawatazama kwa macho ya kiungu, na Anatumia kiini Chake na kile Alicho nacho na kile Alicho kama kipimo. Mawanda haya yanajumuisha mambo ambayo watu hawawezi kuona, na hapo ndipo Mungu mwenye mwili na wanadamu waliopotoka walivyo tofauti kabisa. Tofauti hii inaamuliwa na viini tofauti vya wanadamu na vya Mungu na ndivyo vinavyoamua utambulisho na nafasi zao pamoja na mtazamo na kimo ambacho wanaona mambo.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe III” katika Neno Laonekana katika Mwili

25. Pengine uzoefu wa mtu katika kazi yake ni mkubwa sana, au mawazo na fikira zake ni za juu sana, na ubinadamu wake ni mzuri hasa; hivi vinaweza kutamaniwa na watu tu, lakini visiamshe kicho na hofu yao. Watu wote wanawatamani wale ambao wana uwezo wa kufanya kazi na ambao wana uzoefu wa kina na wanaweza kuutenda ukweli, lakini hawawezi kuvuta kicho, bali kutamani na kijicho. Lakini watu ambao wamepitia uzoefu wa kazi ya Mungu hawamtamani Mungu, badala yake wanahisi kwamba kazi Yake haiwezi kufikiwa na mwanadamu na haiwezi kueleweka na mwanadamu, na kwamba ni nzuri na ya kushangaza. Watu wanapopitia uzoefu wa kazi ya Mungu, ufahamu wao wa kwanza kumhusu ni kwamba Yeye ni asiyeeleweka, ni mwenye hekima na wa ajabu na wanamcha bila kujua na kuihisi siri ya kazi Anayoifanya, ambayo inapita akili ya mwanadamu. Watu wanataka tu kuwa na uwezo wa kukidhi matakwa Yake, kuridhisha matamanio Yake; hawatamani kumpita Yeye, kwa sababu kazi anayoifanya inazidi fikira za mwanadamu na haiwezi kufanywa na mwanadamu kama mbadala. Hata mwanadamu mwenyewe hayajui mapungufu yake, wakati Amefungua njia mpya na kumleta mwanadamu katika dunia mpya zaidi na nzuri zaidi, kwamba mwanadamu amefanya maendeleo mapya na kuwa na mwanzo mpya. Kile ambacho watu wanahisi kumhusu Mungu, sio matamanio, au sio matamanio tu. Uzoefu wake wa kina ni kicho na upendo, hisia zake ni kwamba Mungu kweli ni wa ajabu sana. Anafanya kazi ambayo mwanadamu hawezi kufanya na kusema mambo ambayo mwanadamu hawezi kusema. Watu ambao wamepitia kazi ya Mungu daima wana hisia isiyoweza kuelezeka. Watu wenye uzoefu wa kina kutosha wanaweza kuelewa ukweli wa Mungu; wanaweza kuhisi uzuro Wake, kwamba kazi Yake ni ya hekima sana, ya ajabu sana, na hivyo hii inazalisha nguvu isiyokoma ndani yao. Si woga au upendo wa mara moja moja na heshima, bali hisia za ndani za upendo wa Mungu na uvumilivu kwa mwanadamu. Hata hivyo, watu ambao wamepata uzoefu wa kuadibu na hukumu Yake wanamhisi kuwa Yeye mtukufu na asiyekosewa. Hata watu ambao wamepitia uzoefu mkubwa wa kazi Yake pia hawawezi kumwelewa; watu wote wanaomcha wanajua kwamba kazi Yake hailingani na fikira za watu lakini siku zote inakwenda kinyume na fikira zao. Haihitaji watu wamtamani kabisa au kuwa na kuonekana kwa kujikabidhi Kwake, badala yake anataka wawe na uchaji wa kweli na kutii kikamilifu. Katika nyingi ya kazi Yake, mtu yeyote mwenye uzoefu wa kweli anahisi heshima Kwake, ambayo ni ya juu kuliko matamanio. Watu wameiona tabia Yake kwa sababu ya kazi Yake ya kuadibu na hukumu, na kwa hiyo wanamcha mioyoni mwao. Mungu anapaswa kuchiwa na kutiiwa, kwa sababu uungu Wake na tabia Yake havifanani kama ule wa watu walioumbwa na vikuu juu ya vile vya watu walioumbwa. Mungu hategemei chochote kuwepo na ni wa milele, Yeye siye kiumbe Aliyeumbwa, na ni Mungu tu anayestahili uchaji na utiifu; mwanadamu hana sifa ya kupewa hivi. Hivyo, watu wote waliopitia uzoefu wa kazi Yake na kweli wanamjua wanampatia heshima. Hata hivyo, wale ambao hawaachani fikira zao kumhusu, yaani, wale ambao hawamwoni kuwa Mungu, hawana uchaji wowote Kwake, na hata ingawa wanamfuata hawajashindwa; ni watu wasiotii kwa asili yao. Anafanya kazi hii ili apate matokeo kwamba viumbe vyote vilivyoumbwa vinaweza kumcha Muumbaji, vimwabudu Yeye, na kujikabidhi katika utawala Wake bila masharti. Haya ni matokeo ya mwisho ambayo kazi Yake yote inalenga kuyapata.

Kimetoholewa kutoka katika “Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu” katika Neno Laonekana katika Mwili

26. Kama mwanadamu ndiye ambaye angefanya kazi hii, basi kazi hii ingekuwa kidogo sana. Ingemchukua mwanadamu hadi kiwango fulani, lakini haingekuwa na uwezo wa kumleta mwanadamu katika hatima ya milele. Mwanadamu hana uwezo wa kuamua hatima ya mwanadamu, wala, zaidi ya hayo, hana uwezo wa kuhakikisha matarajio na hatima ya baadaye ya binadamu. Kazi inayofanywa na Mungu, hata hivyo, ni tofauti. Tangu Yeye amuumbe mwanadamu, Yeye anamwongoza; kwa sababu Yeye humwokoa mwanadamu, atamwokoa mwanadamu kwelikweli, na atampata kikamilifu; kwa kuwa Yeye humwongoza mwanadamu, atamleta kwenye hatima inayofaa; na kwa kuwa Yeye alimuumba mwanadamu na humsimamia mwanadamu, ni sharti Achukue jukumu la hatima ya mwanadamu na matarajio yake. Ni hii ndio kazi ambayo hufanywa na Muumba.

Kimetoholewa kutoka katika “Kurejesha Maisha ya Kawaida ya Mwanadamu na Kumpeleka Kwenye Hatima ya Ajabu” katika Neno Laonekana katika Mwili

Iliyotangulia: VIII. Kuna Mungu Mmoja Tu: Utatu Haupo

Inayofuata: X. Jinsi ya Kutambua Wachungaji wa Uongo, Wapinga Kristo, na Makristo wa Uongo

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Maudhui Yanayohusiana

Kuhusu Maisha ya Petro

Petro ni mfano ambao Mungu aliutambulisha kwa wanadamu, na yeye ni mtu mashuhuri anayejulikana vizuri. Kwa nini mtu mnyonge kama huyo...

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp