XII. Maneno Juu ya Katiba, Agizo za Utawala na Amri za Enzi ya Ufalme

595. Kazi Niliyopanga inaendelea kusonga mbele bila kukoma hata kwa muda kidogo. Baada ya kuingia katika Enzi ya Ufalme, na baada ya kukuingiza katika ufalme Wangu kama watu Wangu, Nitakuwa na madai mengine ya kuweka dhidi yenu; hiyo ni kusema, Nitaanza kutangaza rasmi mbele yenu katiba ambayo Nitatumia kuongoza enzi hii:

Kwa sababu mnaitwa watu Wangu, mnapaswa kuwa na uwezo wa kulitukuza jina Langu, yaani, kushuhudia wakati wa majaribio. Mtu yeyote akijaribu kunirairai na kunificha ukweli, au kushiriki katika shughuli zisizo za heshima nyuma Yangu, bila ubaguzi Nitamfukuza nje, aondolewe kutoka katika nyumba Yangu akisubiri Mimi nimshughulikie. Wale ambao hawajakuwa waaminifu na wasio na upendo wa mtoto kwa mzazi Kwangu zamani, na leo hii wanainuka tena kunihukumu hadharani, wao pia watafukuzwa kutoka kwa nyumba Yangu. Wale ambao ni watu Wangu lazima wajali kuhusu mizigo Yangu kila mara na vile vile kutafuta kujua maneno Yangu. Ni watu kama hawa tu ndio Nitakaowapa nuru, na wao kwa hakika wataishi chini ya uongozi Wangu na nuru, na kamwe hawatakutana na kuadibu. Wale ambao, kwa kutojali mizigo Yangu, wanamakinika na kupanga mustakabali yao wenyewe, yaani, wale ambao hawalengi kwa matendo yao kukidhi Moyo Wangu bali wanataka kuomba omba vya bure, viumbe hawa walio kama waombaji, Ninakataa kata kata kuwatumia, kwa sababu tangu walipozaliwa hawajui chochote kuhusu maana ya kujali mizigo Yangu. Wao ni watu wasiokuwa na akili ya kawaida; watu kama hawa wanaugua kutokana na “utapiamlo” wa ubongo, na wanahitaji kwenda nyumbani wapate “lishe.” Siwahitaji watu wa aina hii. Miongoni mwa watu Wangu, kila mtu atatakiwa kuzingatia kunijua kama wajibu wa lazima unaotakiwa kutekelezwa mpaka mwisho, kama kula, kuvaa, na kulala, mambo ambayo mtu kamwe hawezi kusahau hata kwa muda mfupi, ili kwamba mwishowe kunijua litakuwa jambo la kawaida kama vile kula, jambo ambalo wewe hufanya bila jitihada yoyote, kwa mkono uliozoea. Kuhusu maneno Ninayoyanena, kila neno lazima lichukuliwe kwa uhakika mkubwa na lichukuliwe kikamilifu; hakuwezi kuwa na hatua nusu za uzembe. Yeyote asiyekuwa makini na maneno Yangu ataonekana kama ananipinga Mimi moja kwa moja; mtu yeyote asiyeyala maneno Yangu, au hatafuti kuyajua, ataonekana kama ambaye hanizingatii, na moja kwa moja atafagiliwa nje ya mlango wa nyumba Yangu. Kwa maana, kama Nilivyosema zamani, Ninachotaka sio watu wengi ila wateule wachache. Kati ya watu mia, kama mmoja tu anaweza kunijua kupitia maneno Yangu, basi bila kusita Ningewatupilia mbali wengine wote ili Nizingatie kumpa nuru na mwangaza mmoja huyu. Kutokana na hili unaweza kuona kuwa, si lazima iwe ukweli kwamba idadi kubwa pekee ndio inaweza kunidhihirisha, kuishi kulingana na Mimi. Ninachotaka ni ngano (hata ingawa viini vya mbegu huenda havijajaa) na sio magugu (hata wakati viini vya mbegu vimejaa vya kutosha kutamanika). Na kuhusu wale wasiojali kuhusu kutafuta lakini badala yake kuwa na tabia za kuzembea, wanapaswa kuondoka kwa hiari yao wenyewe; Mimi sitaki kuwaona tena, wasije wakaleta aibu kwa jina Langu.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Maneno ya Mungu kwa Ulimwengu Mzima, Sura ya 5

596. Mimi siwi na haraka ya kumwadhibu yeyote, wala Simtendei yeyote bila haki—Natenda haki kwa wote. Kwa hakika Napenda wana Wangu na hakika Nachukia wale waovu wasionitii; hii ndiyo kanuni ya matendo Yangu. Kila mmoja wenu anapaswa kuwa na umaizi wa amri Zangu za utawala. Iwapo sivyo, hamtakuwa na hofu hata kidogo na mtakuwa wazembe mbele Yangu, na hamtajua kile Ninachotaka kutimilisha, kile Ninachotaka kufanya kuwa kamili, kile Ninachotaka kupata ama ufalme Wangu unahitaji mtu wa aina gani.

Amri Zangu za utawala ni:

1) Haijalishi wewe ni nani, ukinipinga Mimi katika moyo wako, utahukumiwa.

2) Kwa wale ambao Nimechagua, watafundishwa nidhamu mara moja kwa sababu ya wazo lolote lisilo sahihi.

3) Nitawaweka wale wasioniamini kwa upande mmoja. Nitawaruhusu wazungumze na kutenda kwa uzembe hadi mwisho kabisa ambapo Nitawaadhibu kabisa na kupambana nao.

4) Kwa wale ambao wananiamini, Nitawatunza na kuwalinda nyakati zote. Nyakati zote Nitawapa uzima kwa kutumia njia ya wokovu. Watu hawa watakuwa na upendo Wangu na hakika hawataanguka ama kupoteza njia yao. Udhaifu wowote ambao wako nao utakuwa wa muda, na kwa hakika Sitaukumbuka.

5) Kwa wale ambao wanaonekana kuamini lakini ambao kwa kweli hawaamini—kumaanisha wale ambao wanaamini kuna Mungu lakini hawamtafuti Kristo, lakini ambao pia hawapingi—watu wa aina hizi ni wa kusikitisha zaidi, na kupitia vitendo Vyangu Nitawafanya waone kwa dhahiri. Kupitia matendo Yangu, Nitawaokoa watu wa aina hizi na kuwarudisha.

6) Wazaliwa wa kwanza ambao walikuwa wa kwanza kukubali jina Langu watabarikiwa! Hakika Nitawapa baraka bora zaidi na mtakuwa na furaha hadi kuridhika kwa mioyo yenu; hakuna atakayethubutu kuizuia. Kila kitu kimetayarishwa kabisa kwa ajili yenu, kwani hii ni amri Yangu ya utawala.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 56

597. Sasa Natamka amri za utawala wa ufalme Wangu: Vitu vyote vimo ndani ya hukumu Yangu, vitu vyote vimo ndani ya haki Yangu, vitu vyote vimo ndani ya uadhama Wangu, na haki inatendwa kwa wote. Wale ambao husema wananiamini Mimi ilhali wananipinga mioyoni mwao, au ambao mioyo yao imeniacha watafukuzwa, lakini yote ni kwa wakati Wangu mzuri. Wale ambao huzungumza kwa kejeli kunihusu, lakini kwa njia ambayo watu hawatambui, watakufa mara moja (watafariki katika roho, mwili na nafsi). Kwa wale ambao huwadhulumu ama kuwadharau wale Ninaowapenda, ghadhabu Yangu itawahukumu mara moja. Hii ni kusema kwamba wale ambao wana mioyo ya wivu kwa wale Ninaowapenda na kufikiri kuwa Mimi si mwenye haki watakabidhiwa kwa wale ambao Ninawapenda ili kuwahukumu. Wale wote wenye tabia nzuri, wanyenyekevu (pamoja na wale ambao hawana hekima) na ambao ni watiifu kwa dhati Kwangu watabaki wote katika ufalme Wangu. Wale ambao hawajapitia katika mafunzo, kumaanisha watu ambao ni waaminifu wanaokosa hekima na ufahamu, watakuwa na uwezo katika ufalme Wangu. Hata hivyo wao pia wamepitia ushughulikiwaji na kuvunjwa. Kwamba hawajapitia mafunzo si hakika, lakini badala yake kupitia mambo hayo Nitaonyesha kila mtu uweza Wangu na hekima Yangu. Nitawafukuza wale ambao bado wananishuku sasa, Sitaki hata mmoja wao (Ninawachukia sana wale ambao bado hunituhumu wakati kama huu). Kwa matendo ambayo Mimi hufanya katika ulimwengu wote, Nitawaonyesha watu waaminifu matendo Yangu ya kustaajabisha, papo kukuza busara zao, ufahamu na utambuzi, na Mimi mara moja Nitasababisha watu wadanganyifu kuharibiwa kwa ajili ya matendo Yangu ya kustaajabisha. Wazaliwa wote wa kwanza waliokuwa wa kwanza kulikubali jina Langu (kumaanisha wale watakatifu wasio na dosari, watu waaminifu) watakuwa wa kwanza kuingia katika ufalme na kutawala mataifa yote na watu wote pamoja na Mimi, kutawala kama wafalme katika ufalme na pamoja kuhukumu mataifa yote na watu wote (kumaanisha wazaliwa wote wa kwanza katika ufalme, na sio wengine). Wale walio katika mataifa yote na watu wote ambao wamekwisha kuhukumiwa na wametubu wataingia katika ufalme Wangu na kuwa watu Wangu, na wale ambao ni wakaidi na wasiotubu watatupwa katika shimo la kuzimu (ili waangamie milele). Hukumu katika ufalme itakuwa mara ya mwisho na itakuwa utakaso Wangu kwa kina duniani. Hakutakuwa tena na udhalimu wowote, huzuni yoyote, machozi yoyote na hata zaidi hakutakuwa na dunia. Kila kitu kitakuwa dhihirisho la Kristo, kila kitu kitakuwa ufalme wa Kristo. Utukufu ulioje! Utukufu ulioje!

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 79

598. Sasa Nawatangazia rasmi amri Zangu za utawala (zinaanza kazi kuanzia siku zilipotangazwa rasmi, kutoa kuadibu tofauti kwa watu tofauti):

Natimiza ahadi Zangu, na kila kitu kiko mikononi Mwangu: Yeyote aliye na shaka hakika atauwawa. Hakuna nafasi ya huruma yoyote; wataangamizwa mara moja, hivyo kuondoa chuki kutoka moyoni Mwangu. (Kuanzia sasa inathibitika kwamba yeyote anayeuwawa lazima asiwe mshiriki wa ufalme Wangu, na lazima awe wa ukoo wa Shetani.)

Kama wazaliwa wa kwanza wa kiume, ni sharti mtunze nafasi zenu na mtimize wajibu wenu vema, na msiwe wadadisi. Ni sharti mjitolee kwa mpango Wangu wa usimamizi, na popote muendapo, ni sharti muwe na ushuhuda mzuri Kwangu na mlitukuze jina Langu. Msitende vitu vya aibu; kuweni mfano kwa wana Wangu wote na watu Wangu. Msiwe waasherati hata kwa muda kidogo: Lazima muonekane kila mara mbele ya kila mtu mkiwa na utambulisho wa wazaliwa wa kwanza wa kiume, na msiwe watumwa; badala yake, mnapaswa kutembea kwenda mbele kwa kujiamini. Nawaomba mlitukuze jina Langu, sio kulitia aibu jina Langu. Wale ambao ni wazaliwa wa kwanza wa kiume kila mmoja wao ana kazi yake binafsi, na hawawezi kufanya kila kitu. Hili ndilo jukumu Nililowapa, na halipaswi kuepukwa. Lazima mjitolee kwa mioyo yenu yote, kwa akili zenu zote na nguvu zenu zote, kwa kutimiza kile ambacho Nimewaaminia.

Kuanzia leo kuendelea, katika Ulimwengu wote, jukumu la kuongoza wana Wangu wote na watu Wangu wote litakabidhiwa wazaliwa Wangu wa kwanza wa kiume walitimize, na Nitamwadibu yeyote asiyeweza kuutoa moyo wake wote na akili katika kulitimiza. Hii ni haki Yangu. Sitawasamehe au kuwabembeleza hata wazaliwa Wangu wa kiume wa kwanza.

Ikiwa kuna yeyote kati ya wana Wangu wote au kati ya watu Wangu wote anayemdhihaki na kumtusi mmoja wa wazaliwa Wangu wa kwanza wa kiume, Nitamwadhibu vikali, kwa sababu wana Wangu wazaliwa wa kwanza wananiwakilisha Mimi Mwenyewe; kile ambacho mtu anawafanyia, ananifanyia Mimi pia. Hii ndiyo kali zaidi kati ya amri Zangu za utawala. Nitawaruhusu wazaliwa Wangu wa kwanza, kulingana na matamanio yao, watoe haki Yangu dhidi ya yeyote kati ya wana Wangu wote na watu Wangu anayeikiuka amri hii.

Taratibu Nitamtenga yeyote anayenitazama kipuuzi na anayelenga tu chakula Changu, mavazi na usingizi anayeshughulikia tu mambo Yangu ya nje na haudhukuru mzigo Wangu, na hatilii maanani kutimiza kazi zake inavyostahili. Hili linaelekezwa kwa wote walio na masikio.

Yeyote amalizaye kunifanyia huduma lazima aondoke kwa utiifu bila vurugu yoyote. Kuwa makini, la sivyo Nitakushughulikia. (Hii ni amri ya ziada).

Wazaliwa Wangu wa kwanza wa kiume watachukua fimbo ya chuma kuanzia sasa na kuendelea na kuanza kutekeleza mamlaka Yangu kutawala mataifa na watu wote, kutembea kati ya mataifa na watu wote na kuzitekeleza hukumu Zangu, haki, na uadhama kati ya mataifa yote na watu. Wana Wangu wote na watu Wangu wote wataniogopa, watanipa sifa, watanishangilia, na kunitukuza bila kukoma kwa sababu mpango wangu wa usimamizi umekamilika na wazaliwa Wangu wa kwanza wa kiume wanaweza kutawala nami.

Hii ni sehemu ya amri Zangu za utawala; baada ya hili, Nitawaambia kuyahusu kazi inapoendelea. Kutokana na amri za utawala zilizoko hapo juu, mtaona kasi ambayo kwayo Nafanya kazi Yangu, na vile vile ni hatua ipi ambayo kazi Yangu imefika. Hili litakuwa thibitisho.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 88

599. Amri Kumi za Utawala Ambazo Lazima Wateule wa Mungu katika Enzi ya Ufalme Wazitii

(Sura Iliyochaguliwa ya Neno la Mungu)

1) Mwanadamu hapaswi kujitukuza wala kujipa sifa. Anapaswa kumwabudu na kumsifu Mungu.

2) Unapaswa kufanya lolote ambalo lina manufaa kwa kazi ya Mungu, na hupaswi kufanya chochote ambacho kitaleta madhara kwa manufaa ya kazi ya Mungu. Unapaswa kutetea jina la Mungu, ushahidi Wake, na kazi ya Mungu.

3) Pesa, vitu vya dunia, na mali yote ambayo yako katika kaya ya Mungu ni sadaka ambazo zinapasa kutolewa na binadamu. Sadaka hizi hazifai kufurahiwa na binadamu yeyote ila kasisi na Mungu Mwenyewe, kwani sadaka zinazotolewa na binadamu ni za kufurahiwa na Mungu, Mungu pekee ndiye Anayeweza kumgawia kasisi sadaka hizi, na hakuna mwingine yeyote aliyehitimu wala kuwa na haki ya kufurahia sehemu yoyote ya sadaka hizi. Sadaka zote zinazotolewa na mwanadamu (ikiwemo pesa na vitu vinavyoweza kufurahiwa) vinapewa Mungu, na sio kwa mwanadamu. Na hivyo, vitu hivi havipaswi kufurahiwa na mwanadamu; iwapo mwanadamu angevifurahia vitu hivi, basi angekuwa anaiba sadaka. Yeyote yule atakayefanya hili ni msaliti kama Yuda, kwa kuwa, zaidi ya Yuda kuwa msaliti. Yuda alijitwalia vilivyokuwa katika mfuko wa hela.

4) Mwanadamu anayo tabia ya upotovu na, zaidi ya hayo, amejawa na hisia. Kwa hivyo, ni marufuku kabisa kwa watu wa jinsia mbili tofauti kufanya pamoja kazi wakati wa kumtumikia Mungu bila kuwepo na mtu mwingine. Yeyote yule atakayepatikana na kosa hili atatupiliwa mbali, bila ubaguzi—na hakuna atakayeepuka hili.

5) Hupaswi kumhukumu Mungu, au kujadili kwa kawaida mambo yanayomuhusu Mungu. Unapaswa kutenda vile mwanadamu anavyopaswa kutenda, na kuzungumza jinsi mwanadamu anapasa kuzungumza, na hupaswi kuvuka upeo wako wala kuvuka mipaka yako. Uchunge ulimi wako na uwe mwangalifu na hatua zako. Yote haya yatakuzuia kufanya jambo lolote linaloweza kukosea tabia ya Mungu.

6) Unapaswa kufanya yale yanayopaswa kufanywa na mwanadamu, na kutenda wajibu wako, na kutimiza majukumu yako, na kushikilia jukumu lako. Kwa sababu unaamini katika Mungu, unapasa kutoa mchango wako kwa kazi ya Mungu; kama huwezi, basi wewe hufai kula na kunywa maneno ya Mungu, na hufai kuishi katika nyumba ya Mungu.

7) Katika kazi na mambo yanayohusiana na kanisa, kando na kumtii Mungu, katika kila kitu unapaswa kufuata maagizo ya mwanadamu anayetumiwa na Roho Mtakatifu. Hata kosa lolote hata liwe dogo kivipi halikubaliwi. Lazima uwe mkamilifu katika kutii kwako, na hupaswi kuchunguza kati ya mazuri na mabaya; yaliyo mazuri au mabaya hayakuhusu. Unapaswa kujishughulisha tu na utiifu kamili.

8) Watu wanaoamini katika Mungu wanapaswa kumtii na kumwabudu. Hupaswi kusifu au kumwabudu mtu yeyote; hupaswi kumpa Mungu nafasi ya kwanza, binadamu unayemheshimu nafasi ya pili, kisha wewe mwenyewe nafasi ya tatu. Mtu yeyote asishikilie nafasi yoyote moyoni mwako, na hufai kuzingatia watu—hasa wale unaowaenzi—kuwa katika kiwango sawa na Mungu, kuwa sawa na Yeye. Mungu hawezi kustahimili hili.

9) Mawazo yako yanapasa kuwa ya kazi ya kanisa. Unapaswa kuweka kando matarajio ya mwili wako, uwe na msimamo thabiti kuhusu mambo ya kifamilia, na ujitoe kwa moyo wako wote kwa kazi ya Mungu, na uiweke kazi ya Mungu kwanza kisha maisha yako katika nafasi ya pili. Huu ndio mwenendo mwema wa utakatifu.

10) Jamaa zako (watoto, mke au mume, dada zako au wazazi wako na kadhalika) wasio wa imani yako hawapaswi kulazimishwa kuja kanisani. Nyumba ya Mungu haina ukosefu wa washirika, na hakuna haja ya kuijaza na watu wasiokuwa na maana katika nyumba Yake. Wale wote wasioamini kwa moyo mchangamfu, hawapaswi kuongozwa kuingia kanisani. Amri hii inaelekezwa kwa kila mwanadamu. Kuhusu hili jambo mnapaswa kuchunguza, mfuatilie na mkumbushane, na hakuna anayepasa kukiuka amri hii. Hata jamaa wako wasio wa imani yako wanapoingia kanisani shingo upande, hawapaswi kupatiwa jina jipya wala kupewa vitabu vya kanisa; watu kama hao si wa kaya ya Mungu, na kuingia kwao kanisani kunapaswa kukomeshwa kwa udi na uvumba. Iwapo matatizo yataletwa kanisani kwa sababu ya uvamizi wa mapepo, basi wewe mwenyewe utafukuzwa au kuwekewa vikwazo. Kwa ufupi, kila mmoja analo jukumu katika hili jambo, lakini pia hupasi kuwa asiyejali, wala kutumia jambo hili kulipiza kisasi cha kibinafsi.

kutoka katika Neno Laonekana katika Mwili

600. Watu lazima wafuate majukumu mengi wanayostahili kuyatekeleza. Hili ndilo watu wanalopaswa kufuata, na wanalostahili kufanya. Mruhusu Roho Mtakatifu afanye linalostahili kufanywa na Roho Mtakatifu; mwanadamu hawezi kulichangia lolote. Mwanadamu sharti ashike yale ambayo lazima yatendwe na mwanadamu, ambayo hayana uhusiano na Roho Mtakatifu. Si lolote bali lile ambalo lazima litendwe na mwanadamu, na lazima lifuatwe kama amri, kama ufuasi wa sheria za Agano la Kale. Ingawa sasa si Enzi ya Sheria, bado kuna maneno mengi yanayolingana na Enzi ya Sheria ambayo yanahitaji kufuatwa, na hayatendwi tu kwa kutegemea kuguswa na Roho Mtakatifu, lakini ni yale yanayostahili kufuatwa na wanadamu. Kwa mfano: Hupaswi kuihukumu kazi ya Mungu wa vitendo. Hupaswi kumpinga mtu anayeshuhudiwa na Mungu. Mbele za Mungu, utahifadhi nafasi yako, na hutakuwa mwovu. Matamshi yako yanapaswa yawe wastani, na maneno yako na matendo yako yanapaswa kufuata mpangilio wa mwanadamu aliyeshuhudiwa na Mungu. Unapaswa kuheshimu ushuhuda wa Mungu. Usipuuze kazi ya Mungu wala maneno kutoka kinywa chake. Usiige sauti na malengo ya matamshi ya Mungu. Kwa nje, usifanye lolote linalodhihirisha kumpinga mtu anayeshuhudiwa na Mungu. Na mengineyo. Haya ndiyo yanayopaswa kufuatwa na kila mmoja.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Amri za Enzi Mpya

601. Leo, hakuna lolote muhimu analopaswa kufuata mwanadamu zaidi ya yafuatayo: Usijaribu kumbembeleza Mungu anayesimama mbele ya macho yako, au kumficha jambo lolote. Usizungumze uchafu ama matamshi ya kiburi mbele ya Mungu aliye mbele yako. Usimdanganye Mungu mbele ya macho yako kwa maneno mazuri wala kwa maneno ya kuridhisha ili uweze kujipatia uaminifu Wake. Usitende bila heshima mbele za Mungu. Tii yote yatokayo kinywani mwa Mungu, wala usikatae, usipinge, ama kusaili maneno Yake. Usitafsiri unavyoona kuwa sawa, maneno yanayonenwa kutoka kinywani mwa Mungu. Chunga ulimi wako ili usikutie katika mtego wa hila danganyifu za yule mwovu. Unapaswa kulinda nyayo zako ili kuepuka kupita mipaka uliyowekewa na Mungu. Kufanya hivyo kutakufanya uzungumze maneno ya majivuno na yenye fahari kuu kulingana na mtazamo wa Mungu, na hivyo kufanya uchukiwe na Mungu. Usieneze maneno kutoka kinywa cha Mungu ovyo ovyo, usije ukadhihakiwa na wengine na kufanywa kuwa mjinga na mapepo. Tii kazi yote ya Mungu wa leo. Hata ikiwa hauifahamu, usiihukumu; unachoweza kufanya ni kutafuta na kushiriki. Hakuna mtu atapatendea dhambi mahali pa Mungu pa asili. Huwezi kufanya lolote ila kumhudumia Mungu wa leo kwa mtazamo wa mwanadamu. Huwezi kumfunza Mungu wa leo kwa mtazamo wa mwanadamu—kufanya hivyo ni kupotoka. Hakuna anayeweza kusimama kwa niaba ya mtu aliyeshuhudiwa na Mungu; katika maneno yako, matendo, na mawazo yako ya ndani, unasimama katika nafasi ya mwanadamu. Hili ni la kufuatwa, ni wajibu wa mwanadamu, hakuna anayeweza kulibadilisha, na kufanya hivyo ni ukiukaji wa amri za utawala. Inapaswa kukumbukwa na kila mtu.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Amri za Enzi Mpya

602. Kila sentensi Ninayotamka huwa na mamlaka na hukumu na hakuna mtu anayeweza kuzibadilisha. Mara tu maneno Yangu yanapotoka, mambo yatafanyika kwa mujibu wa maneno Yangu, na hii ndiyo tabia Yangu. Maneno Yangu ni mamlaka na yeyote anayeyarekebisha hukosea kuadibu Kwangu na ni lazima Nimwangamize. Hali ikiwa mbaya hayo husababisha uharibifu katika maisha yao wenyewe nao huenda kuzimu, au huenda jahanamu. Hii ndiyo njia ya pekee ambayo kwayo Ninawashughulikia wanadamu na mwanadamu hawezi kuibadilisha—hii ni amri Yangu ya utawala. Kumbuka hili! Hakuna mtu anayeruhusiwa kuikosea amri Yangu; lazima hili lifanyike kulingana na mapenzi Yangu! Zamani Nilikuwa mpole sana kwenu nanyi mlikabiliwa na maneno Yangu tu. Maneno Niliyonena kuhusu kuwaangamiza watu hayajatokea bado. Lakini kuanzia leo, majanga yote (haya yanayohusiana na amri Zangu za utawala) yatatokea moja baada ya lingine ili yawaadhibu wale wote wasiotii mapenzi Yangu. Lazima kuwe na ujio wa ukweli, vinginevyo watu hawataweza kuona ghadhabu Yangu lakini watapotoshwa tena na tena. Hii ni hatua ya mpango Wangu wa usimamizi nayo ni njia ambayo kwayo Mimi kushughulikia hatua inayofuata ya kazi Yangu. Nawaambieni hivi mapema ili muweze kuepuka kufanya makosa na kupitia mateso milele. Hiyo ni kusema, kuanzia leo Nitawafanya watu wote ila wazaliwa Wangu wa kwanza kuchukua nafasi zao halisi kwa mujibu wa mapenzi Yangu, nami Nitawaadibu mmoja baada ya mwingine. Sitamsamehe hata mmoja wao. Hebu thubutu tu kuwa wapotovu tena! Hebu thubutu tu kuwa mwasi tena! Nimesema mbeleni kuwa Mimi ni mwenye haki kwa wote bila hisia yoyote, na huu ni mfano kwamba tabia Yangu haipaswi kukosewa. Hii ni nafsi Yangu. Hakuna mtu anayeweza kubadilisha jambo hili. Watu wote husikia maneno Yangu na watu wote huuona uso Wangu mtukufu. Watu wote wanapaswa kunitii kabisa na kwa ukamilifu—hii ni amri Yangu ya utawala. Watu wote katika ulimwengu mzima na katika miisho ya dunia wanapaswa kunisifu na kunitukuza, kwa maana Mimi ni Mungu Mwenyewe wa pekee, kwa maana Mimi ni nafsi ya Mungu. Hakuna mtu anayeweza kubadili maneno na matamshi Yangu, usemi na mwenendo Wangu, kwa kuwa haya ni mambo Yangu peke Yangu, na kile ambacho Nimemiliki tangu milele na kile ambacho kitakuwepo milele.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 100

603. Hukumu Yangu inamjia kila mtu, amri Zangu za utawala zinamgusa kila mtu, na maneno Yangu na nafsi Yangu vinafichuliwa kwa kila mtu. Huu ndio wakati wa kazi kuu ya Roho Wangu (wakati huu wale watakaobarikiwa na wale watakaopitia taabu wanabainishwa). Mara tu maneno Yangu yatakapotamkwa, Nimewabainisha wale watakaobarikiwa na wale watakaopitia taabu. Yote ni dhahiri nami Ninaweza kuyaona mara moja. (Yanasemwa kuhusu ubinadamu Wangu, kwa hiyo hayahitilafiani na majaaliwa na uteuzi Wangu.) Ninatembeatembea hapa na pale milimani na mito na vitu vyote, anga ya ulimwengu, Nikichunguza kila mahali na kutakasa kila mahali, ili yale maeneo yasiyo safi na zile nchi zilizochangamana zote zitakoma kuwepo nazo zitateketea kabisa kwa sababu ya maneno Yangu. Kwangu, kila kitu ni rahisi. Ikiwa wakati huu ungekuwa wakati ambao Niliamua kabla kuiangamiza dunia, Ningeimeza kwa neno moja, lakini sasa si wakati. Lazima kila kitu kiwe tayari kabla Yangu kufanya kazi hii, ili visiuvuruge mpango Wangu na kuingilia usimamizi Wangu. Ninajua jinsi ya kufanya hivyo kwa busara: Nina hekima Yangu nami Nina mpango Wangu wenyewe. Watu hawapaswi kufanya lolote—jihadhari usiuawe kwa mkono Wangu; tayari hii inagusa amri Zangu za utawala. Kutokana na hili mtu anaweza kuona ukali wa amri Zangu za utawala, na mtu anaweza kuona kanuni za amri Zangu za utawala, ikiwa ni pamoja na vipengele viwili: kwa upande mmoja Ninawaua wote wasiokubaliana na mapenzi Yangu na ambao wanazikosea amri Zangu za utawala; kwa upande mwingine, Nikiwa na ghadhabu Ninawalaani wote wanaozikosea amri Zangu za utawala. Vipengele hivi viwili ni muhimu navyo ni kanuni zenye mamlaka ya uamuzi za amri Zangu za utawala. Kila mtu hutendewa kulingana na kanuni hizi mbili, bila hisia, bila kujali jinsi watu walivyo waaminifu. Hii inatosha kuonyesha haki Yangu na inatosha kuonyesha uadhama Wangu na ghadhabu Yangu, ambayo itaviteketeza vitu vyote ya kidunia, vitu vyote vya kidunia, na vitu vyote ambavyo havikubaliani na mapenzi Yangu. Katika maneno Yangu kuna siri zilizofichwa, na katika maneno Yangu pia kuna siri zilizofichuliwa, hivyo katika dhana ya binadamu, katika akili ya binadamu, maneno Yangu hayaeleweki milele na moyo Wangu haueleweki milele. Kwa maneno mengine, lazima Niwaondolee wanadamu dhana na kufikiria kwao. Hiki ni kipengee muhimu zaidi cha mpango Wangu wa usimamizi. Lazima Nifanye hivi ili Niwapate wazaliwa Wangu wa kwanza na ili Niyakamilishe mambo ambayo Nataka kufanya.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 103

604. Lakini ulimwengu wa kitambo ukiendelea kuwepo, Nitavurumisha hasira Yangu kwa mataifa yake, Nikieneza amri Zangu za utawala katika ulimwengu mzima, na kuleta kuadibu kwa yeyote anayezikiuka:

Ninapougeuza uso Wangu kwa ulimwengu kuzungumza, binadamu wote wanasikia sauti Yangu, na hapo kuona kazi yote ambayo Nimefanya katika ulimwengu. Wale wanaoenda kinyume na mapenzi Yangu, hivyo ni kusema, wanaonipinga kwa matendo ya mwanadamu, watapitia kuadibu Kwangu. Nitachukua nyota nyingi mbinguni na kuzitengeneza upya, na kwa mujibu Wangu jua na mwezi vitafanywa upya—anga hazitakuwa tena jinsi zilivyokuwa hapo awali; vitu visivyohesabika duniani vitafanywa kuwa vipya. Yote yatakuwa kamili kupitia maneno Yangu. Mataifa mengi katika ulimwengu yatagawanishwa upya na kubadilishwa kuwa taifa Langu, ili kwamba mataifa yote yaliyomo duniani yatatoweka milele na kuwa taifa linaloniabudu Mimi; mataifa yote ya dunia yataangamizwa, na hayatakuwepo tena. Kati ya binadamu walio ulimwenguni, wale wote walio wa Shetani wataangamizwa; wale wote wanaomwabudu Shetani watalazwa chini na moto Wangu unaochoma—yaani, isipokuwa wale walio ndani ya mkondo, waliobaki watabadilishwa kuwa jivu. Nitakapoadibu watu wengi, wale walio katika dunia ya kidini, kwa kiasi tofauti, watarudi kwa ufalme Wangu, wakiwa wameshindwa na kazi Yangu, kwani watakuwa wameona kufika kwa Aliye Mtakatifu akiwa amebebwa juu ya wingu jeupe. Wanadamu wote watafuata aina yao, na watapokea kuadibu kunakotofautiana kulingana na kile walichofanya. Wale ambao wamesimama kinyume na Mimi wataangamia; na kwa wale ambao matendo yao duniani hayakunihusisha, kwa sababu ya vile wamejiweka huru wenyewe, wataendelea kuwa duniani chini ya uongozi wa wana Wangu na watu Wangu. Nitajionyesha kwa mataifa mengi yasiyohesabika, Nikipaza sauti Yangu kote duniani Nikitangaza kukamilika kwa kazi Yangu kuu ili wanadamu wote waone kwa macho yao.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Maneno ya Mungu kwa Ulimwengu Mzima, Sura ya 26

Iliyotangulia: D. Kuhusu Mungu kama Chanzo cha Uzima wa Vitu Vyote

Inayofuata: XIII. Maneno Juu ya Mahitaji, Ushawishi, Maliwazo na Maonyo ya Mungu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp