Kuhusu Ayubu (Sehemu 1)

07/09/2019

Baada ya kusikia namna Ayubu alivyopitia majaribio, kunao uwezekano kwamba wengi wenu watataka kujua maelezo zaidi kuhusu Ayubu mwenyewe, hasa kuhusiana na siri iliyomfanya akapata sifa za Mungu. Hivyo basi leo, hebu tuzungumzie kuhusu Ayubu!

Katika Maisha ya Kila Siku ya Ayubu Tunaona Utimilifu, Unyofu, Kumcha Mungu, na Kujiepusha na Maovu Kwake

Kama tutazungumzia Ayubu, basi lazima tuanze na namna ambavyo alitathminiwa kwa mujibu wa matamshi kutoka kwa kinywa cha Mungu mwenyewe: “Hakuna hata mtu kama yeye duniani, mtu mtimilifu na mwaminifu, ambaye anamcha Mungu, na kuepuka maovu.”

Hebu kwanza tujifunze kuhusu utimilifu na unyofu wa Ayubu.

Kuhusu Ayubu (Sehemu 1)

Unaelewa vipi maneno haya “utimilifu” na “unyofu”? Unasadiki kwamba Ayubu hakuwa na lawama, na kwamba aliheshimika? Hili, bila shaka, litakuwa ni ufasiri wa moja kwa moja na uelewa wa “mtimilifu” na “mnyofu.” Muhimu katika uelewa wa kweli wa Ayubu ni maisha halisi—maneno, vitabu, na nadharia pekee haviwezi kutupa majibu yoyote. Tutaanza na kuyaangalia maisha ya Ayubu ya nyumbani, kuangalia namna mwenendo wake wa kawaida ulivyokuwa maishani mwake. Kufanya hivi kutatwambia kuhusu kanuni na malengo yake maishani, pamoja na hulka yake na mambo yale aliyoyafuatilia. Sasa, hebu tuyasome maneno ya mwisho katika Ayubu 1:3: “Mtu huyo alikuwa mkubwa zaidi kuwaliko watu wengine wote wa mashariki.” Kile ambacho maneno haya yanasema ni kwamba hadhi na heshima ya Ayubu ilikuwa ya juu sana, na ingawaje hatuambiwi kama alikuwa ndiye mkubwa zaidi kati ya wanaume wote wa mashariki kwa sababu ya wingi wa rasilimali zake au kwa sababu alikuwa mtimilifu na mnyofu, na kwamba alimcha Mungu na kujiepusha na maovu, kwa ujumla tunajua kwamba hadhi na heshima ya Ayubu vyote vilithaminiwa sana. Kama ilivyorekodiwa kwenye Biblia, picha za kwanza za Ayubu kwa watu zilikuwa kwamba Ayubu alikuwa mtimilifu, kwamba alimcha Mungu na kujiepusha na maovu na kwamba alimiliki utajiri mkubwa na alikuwa na hadhi ya kuheshimika. Kwa mtu wa kawaida anayeishi katika mazingira kama haya na hali kama hizo, mlo wa Ayubu, ubora wa maisha, na vipengele mbalimbali vya maisha yake ya kibinafsi vyote vingekuwa malengo ya umakinifu wa watu wengi; hivyo lazima tuendelee kuyasoma maandiko: “Nao wana wake walienda na kufurahia karamu katika nyumba zao, kila kwa siku yake; na wao wakatuma na kuwaita ndugu zao wa kike watatu ili wakule na kunywa pamoja na wao. Na ilikuwa hivyo, wakati hizo siku zao za karamu ziliisha, Ayubu aliwatuma na kuwatakasa, na akaamka asubuhi mapema, na kutoa sadaka za kuteketezwa kulingana na hesabu yao wote; kwa sababu Ayubu alisema, Inaweza kuwa kwamba wana wangu wametenda dhambi, na kumlaani Mungu mioyoni mwao. Hivyo ndivyo Ayubu alivyofanya kila siku” (Ayubu 1:4-5). Kifungu hiki kinatuambia mambo mawili: Jambo la kwanza ni kwamba watoto wa kiume na wa kike wa Ayubu walishiriki kwenye karamu mara kwa mara, wakila na wakinywa; pili ni kwamba Ayubu mara kwa mara alitoa sadaka za kuteketezwa kwa sababu alikuwa na wasiwasi na wao, akiogopa kwamba walikuwa wakitenda dhambi, kwamba katika mioyo yao walikuwa wamemlaani Mungu. Katika maandiko haya maisha ya watu wa aina mbili tofauti yanafafanuliwa. Maisha ya kwanza, watoto wa kiume na kike wa Ayubu, mara nyingi walishiriki kwenye karamu kwa sababu ya ukwasi wao, waliishi kwa ubadhirifu, wakinywa na wakila hadi mioyo yao kutosheka, wakifurahia maisha ya kiwango cha juu yaliyoletwa na utajiri wa anasa. Wakiishi maisha kama haya, ilikuwa lazima kwamba mara kwa mara wangetenda dhambi na kumkosea Mungu—ilihali hawakujitakasa wala kutoa sadaka za kuteketezwa kutokana na hayo yote. Waona, basi, kwamba Mungu hakuwa na nafasi katika mioyo yao, kwamba hawakufikiria kuhusu neema za Mungu, wala kuogopa kumkosea Mungu, isitoshe hawakuogopa kumuacha Mungu katika mioyo yao. Bila shaka zingatio letu si watoto wa Ayubu, lakini ni kwa kile ambacho Ayubu alifanya alipokabiliwa na mambo kama haya; hili ndilo suala lile jingine lililofafanuliwa katika kifungu, na ambalo linahusisha maisha ya kila siku ya Ayubu na kiini cha ubinadamu wake. Wakati Biblia inapofafanua kushiriki kwa watoto wa kike na kiume katika karamu mbalimbali hakuna mahali ambapo Ayubu anatajwa; yasemekana tu kuwa ni watoto wake wa kiume na wa kike walio kula na kunywa pamoja. Kwa maneno mengine, hakuandaa karamu, wala hakujiunga na watoto wake wa kiume na kike katika karamu hizo ili kuendeleza ubadhirifu. Ingawaje alikuwa tajiri na alimiliki raslimali nyingi na watumishi wengi, maisha ya Ayubu hayakuwa ya anasa. Hakudanganywa na mazingira yake ya juu kabisa aliyoyaishi na wala hakujawa na ulafi wa anasa za mwili au kusahau kutoa sadaka za kuteketezwa kwa sababu za utajiri wake, isitoshe pia haya yote hayakumsababisha kuanza kujiepusha na Mungu ndani ya moyo wake kwa utaratibu. Ni dhahiri, hivyo basi, kwamba Ayubu alikuwa na nidhamu katika hali ya maisha yake, wala hakuwa mlafi au na imani ya kuwa anasa kutokana na baraka za Mungu kwake, na hakushikilia na kupumbazwa na ubora wa maisha. Badala yake, alinyenyekea na akawa asiye na majivuno, hakuwa mwenye kujidai na alikuwa mtulivu na makini mbele ya Mungu. Mara nyingi alifikiria kuhusu neema na baraka za Mungu, na siku zote alimcha Mungu. Katika maisha yake ya kila siku, Ayubu mara nyingi alirauka mapema ili kutoa sadaka zilizoteketezwa kwa niaba ya watoto wake wa kiume na kike. Kwa maneno mengine, Ayubu mwenyewe alimcha Mungu na pia alitumaini kwamba watoto wake wangeweza vilevile kumcha Mungu na kutotenda dhambi dhidi ya Mungu. Utajiri wa anasa wa Ayubu haukuwa na mahali popote ndani ya moyo wake, wala haukusawazisha ile nafasi iliyoshikiliwa na Mungu; haijalishi kama ilikuwa ni kwa ajili yake mwenyewe au watoto wake, vitendo vyote vya kila siku vya Ayubu viliunganishwa katika kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Kumcha Yehova Mungu kwake hakukuishia kwenye kinywa chake lakini kulitiwa katika vitendo, na kukajionyesha katika kila sehemu ya maisha yake. Mwenendo huu halisi wa Ayubu unatuonyesha kwamba alikuwa mwaminifu, na alimiliki kiini kilichopenda haki na mambo yaliyokuwa mazuri. Kwamba Ayubu mara nyingi alituma sadaka ya kuwateketeza na kwa niaba ya watoto wake wa kiume na kike na kuwatakasa kunamaanisha kwamba hakuruhusu wala kuidhinisha tabia ya watoto wake; badala yake katika moyo wake alichoshwa na tabia yao, na akawashutumu vikali. Alikuwa amethibitisha kwamba tabia ya watoto wake wa kike na kiume haikupendeza Yehova Mungu na hivyo basi mara nyingi aliwaita kwenda mbele ya Yehova Mungu na kutubu dhambi zao. Vitendo vya Ayubu vinatuonyesha upande mwingine wa ubinadamu wake: ule ambao unaonyesha kwamba hakuwahi kutembea na wale ambao mara nyingi walitenda dhambi na kumkosea Mungu, lakini badala yake alijiepusha na kutotaka kuwa nao. Hata ingawaje watu hawa walikuwa watoto wake wa kike na kiume, hakuziacha kanuni zake za kibinafsi kwa sababu walikuwa ukoo wake binafsi wala hakujihusisha kwa dhambi zao kwa sababu ya hisia zake binafsi za moyoni. Badala yake aliwasihi kutubu na kupata ustahimilivu wa Yehova Mungu na akawaonya kutomwacha Mungu kwa ajili ya kujifurahisha kwao kwa ulafi. Kanuni za namna ambavyo Ayubu aliwashughulikia wengine haziwezi kutenganishwa na zile kanuni za kumcha Mungu na kujiepusha na maovu. Alipenda kile kilichokubalika na Mungu na kuchukia kile Alichokiona Mungu kuwa mbaya, na akawapenda wale waliomcha Mungu katika mioyo yao, na kuchukia wale waliotenda maovu au kutenda dhambi dhidi ya Mungu. Upendo na chuki kama hiyo zilionyeshwa katika maisha yake ya kila siku, na ndio uliokuwa unyofu wenyewe wa Ayubu ulioonekana katika macho ya Mungu. Kiasili, haya pia ndiyo maonyesho na kuishi kulingana na ubinadamu wa kweli wa Ayubu katika mahusiano yake na wengine katika maisha yake ya kila siku ambao lazima tujifunze kuhusu.

Maonyesho ya Ubinadamu wa Ayubu Wakati wa Majaribio Yake (Kuelewa Utimilifu wa Ayubu, Unyofu, Kumcha Mungu na Kujiepusha na Maovu Wakati wa Majaribio Yake)

Kile tulichozungumzia hapo juu ni vipengele mbalimbali vya ubinadamu wa Ayubu zilizoonyeshwa katika maisha yake ya kila siku kabla ya majaribio yake. Bila shaka, maonyesho haya mbalimbali yanatupa ufahamu wa mwanzo pamoja na uelewa wa unyofu wa Ayubu, kumcha Mungu na kujiepusha na maovu kwake, na unatupa uthibitisho wa mwanzo. Sababu inayonifanya kusema “mwanzo” ni kwa kuwa watu wengi bado hawana uelewa wa kweli wa hulka ya Ayubu na kiwango ambacho alifuatilia njia ya kutii na kumcha Mungu. Hivi ni kusema, ufahamu wa watu wengi kuhusu Ayubu hauendi kwa kina zaidi ya ile picha ambayo kwa kiasi fulani inamfaa yeye kama ilivyoelezewa katika vifungu viwili kwenye Biblia vilivyo na maneno yake “Yehova alinipa, na Yehova amechukua; jina la Yehova libarikiwe” na “tupokee mema kutoka mkononi mwa Mungu, nasi tusipokee mabaya?” Hivyo, kunayo haja kubwa yetu sisi kuelewa namna ambavyo Ayubu aliishi kwa kudhihirisha ubinadamu wake alipokuwa akipokea majaribu ya Mungu; kwa njia hii, ubinadamu wote wa kweli wa Ayubu utaweza kuonyeshwa kwa wote.

Wakati Ayubu aliposikia kwamba mali yake ilikuwa imeibwa, kwamba watoto wake wa kike na kiume walikuwa wameaga dunia, na kwamba watumishi wake walikuwa wameuliwa, aliitikia hivi: “Kutoka hapo Ayubu akainuka, na akalipasua joho lake, na akanyoa kichwa chake, na akaanguka chini, na kuabudu” (Ayubu 1:20). Maneno haya yanatuambia ukweli mmoja: Baada ya kuzisikiza habari hizi, Ayubu hakushikwa na wasiwasi, hakulia au kuwalaumu wale watumishi ambao walikuwa wamempa habari hizo, isitoshe hakukagua eneo la uhalifu ili kuchunguza na kuthibitisha ni kwa nini na ni vipi hali ilikuwa hivyo na kutaka kujua ni nini haswa kilichofanyika. Hakuonyesha maumivu au majuto yoyote kutokana na kupoteza mali yake wala hakuanza kupukutikwa na machozi kutokana na kuwapoteza watoto wake, wapendwa wake. Kinyume ni kwamba, akalirarua joho lake kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kuabudu. Vitendo vya Ayubu ni tofauti sana na vile vya binadamu wa kawaida. Vinawachanganya watu wengi, na kuwaruhusu kumkosoa Ayubu ndani ya mioyo yao kwa “kukosa huruma na rehema”. Kwa kupotea ghafla kwa mali yao, watu wa kawaida wangeonekana wamevunjwa moyo, au wanasikitika kweli—au kama ilivyo kwa baadhi ya watu, wanaweza hata kujipata wakiwa wamefadhaishwa moyo. Hii ni kwa sababu, katika mioyo yao, mali ya watu inawakilisha jitihada ya maisha yao yote—ndiyo ambayo maisha yao yanategemea, ndilo tumaini linalowafanya kuishi; kupoteza mali yao kunamaanisha jitihada zao zimeambulia patupu na kwamba hawana tumaini tena na kwamba pia hawana siku za usoni. Huu ndio mwelekeo wa mtu yeyote wa kawaida kuhusiana na mali yake na uhusiano wa karibu alio na mali hiyo, na huu ndio pia umuhimu wa mali katika macho ya watu. Hivyo, idadi kubwa ya watu wanahisi wakiwa wamechanganyikiwa na mtazamo mtulivu wa Ayubu kuhusiana na kupoteza mali yake. Leo, tutauondoa mkanganyiko ambao watu wote walihisi kwa kuelezea kile kilichokuwa kikipitia moyoni mwa Ayubu.

Akili za kawaida zinakariri kwamba, kwa kuwa alikuwa amepewa rasilimali hizo nyingi na Mungu, Ayubu anafaa kuaibika mbele ya Mungu kwa sababu ya kuzipoteza rasilimali hizi, kwani alikuwa hajazitunza, alikuwa hajashikilia zile rasilimali alizopewa na Mungu. Hivyo, aliposikia kwamba mali yake ilikuwa imeibwa, mwitikio wake wa kwanza ulifaa kuwa kuenda kwenye eneo la uhalifu na kuchukua hesabu ya kila kitu kilichokuwa kimepotea na kisha kutubu kwa Mungu ili aweze kwa mara nyingine kupokea baraka za Mungu. Ayubu, hata hivyo hakufanya hivi, na kiasili alikuwa na sababu zake za kutofanya hivyo. Ndani ya Moyo wake, Ayubu alisadiki pakubwa kwamba kila kitu alichomiliki alikuwa amepewa na Mungu na hakikuwa kimetokana na jitihada zake yeye mwenyewe. Hivyo, hakuziona baraka hizo kama jambo la kutilia maanani, lakini alishikilia ile njia alifaa kuchukua kwa udi na uvumba kama kanuni zake za kuishi. Alizitunza baraka za Mungu, na akatoa shukrani kutokana nazo, lakini hakutamanishwa nazo wala hakutafuta baraka zaidi. Huo ndio uliokuwa mwelekeo wake kuhusu mali. Hakufanya chochote kwa minajili ya kupata baraka, wala kuwa na wasiwasi kuhusu au kuhuzunishwa kutokana na ukosefu au kupoteza baraka za Mungu; hakufurahi kwa njia ya kupindukia na isiyo na mipaka kwa sababu ya baraka za Mungu na wala hakupuuza njia ya Mungu wala kusahau neema ya Mungu kwa sababu ya zile baraka ambazo alifurahia mara kwa mara. Mtazamo wa Ayubu kwa mali yake unafichulia watu ubinadamu wake wa kweli: Kwanza, Ayubu hakuwa binadamu mlafi, na hakuwa na madai katika maisha yake yakinifu. Pili, Ayubu hakuwahi kuwa na wasiwasi au kuogopa kwamba Mungu angechukua kila kitu alichokuwa nacho, na ndio uliokuwa mwelekeo wake wa utiifu kwa Mungu ndani ya moyo wake; yaani, hakuwa na madai au malalamiko kuhusu ni lini au kama Mungu angechukua kutoka kwake, na wala hakuuliza sababu, lakini alilenga tu kutii mipango ya Mungu. Tatu, hakuwahi kusadiki kwamba rasilimali zake zilitokana na jitihada zake, lakini kwamba alipewa yeye na Mungu. Hii ilikuwa imani ya Ayubu kwa Mungu, na onyesho la imani yake. Je, ubinadamu wa Ayubu na ufuatiliaji wake wa kweli wa kila siku umefanywa kuwa wazi katika muhtasari huu wa hoja tatu kumhusu yeye? Ubinadamu na ufuatiliaji wa Ayubu ni vitu vilivyokuwa muhimu katika mwenendo wake mtulivu alipokabiliwa na hali ya kupoteza mali yake. Ilikuwa hasa kwa sababu ya ufuatiliaji wake wa kila siku ndipo Ayubu akawa na kimo na imani ya kusema, “Yehova alinipa, na Yehova amechukua; jina la Yehova libarikiwe,” kwenye majaribio ya Mungu. Maneno haya hayakupatwa kwa mkesha mmoja, na wala hayakujitokeza tu kwa ghafla kwenye kichwa chake Ayubu. Yalikuwa yale ambayo alikuwa ameona na kupata kwa miaka mingi ya kupitia safari ya maisha. Akilinganishwa na wale wote wanaotafuta tu baraka za Mungu na wanaoogopa Mungu atachukua kutoka kwao, nao wanachukia hali hio na wanalalamikia kuhusu hali hiyo, je utiifu wa Ayubu ni wa kweli haswa? Tukilinganisha na wale wote wanaosadiki kwamba Mungu yupo, lakini ambao hawajawahi kusadiki kwamba Mungu anatawala mambo yote, Ayubu anamiliki uaminifu na unyofu mkubwa?

Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe II

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Maudhui Yanayohusiana

Leave a Reply

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp