Kifo: Awamu ya Sita

10/09/2019

Baada ya mahangaiko mengi na masikitiko mengi, na kuvunjwa moyo kwingi, baada ya furaha nyingi na huzuni nyingi na baada ya misukosuko ya maisha, baada ya miaka mingi sana isiyosahaulika, baada ya kutazama misimu ikipita na kujirudia, mtu hupita kwenye kiungo muhimu sana cha maisha bila ya taarifa, na kwa ghafla tu mtu anajipata kwenye miaka yake ya kufifia. Alama za muda zimejichora kotekote kwenye mwili wa mtu: Mtu hawezi tena kusimama wima, kichwa cha nywele nyeusi kinageuka na kuwa cha nywele nyeupe, macho maangavu na mazuri yanabadilika na kuanza kufifiliza na kuwa na wingu mbele yao, nayo ngozi laini, yenye unyumbufu inageuka na kuwa na makunyanzi na madoadoa. Kusikia kwa mtu kunaanza kufifia, meno yake kulegea na kuanza kujiangukia, mwitikio wa mtu unaanza kuchelewachelewa, kutembea kunakuwa ni kwa kujikokota…. Wakati huu mtu ameaga kwaheri kabisa miaka yake ya nguvu ya ujana wake na kuingia katika maisha yake ya kwaheri: umri wa uzee. Kisha, mtu atakabiliana na kifo, awamu ya mwisho ya maisha ya binadamu.

1. Muumba Pekee Ndiye Anayeshikilia Nguvu za Maisha na Kifo juu ya Binadamu

Kama kuzaliwa kwa mtu kulipangiwa na maisha ya awali ya mtu, basi kifo cha mtu kinaadhimisha mwisho wa hatima hiyo. Kama kuzaliwa kwa mtu ndiyo mwanzo wa kazi maalum ya mtu ya maisha, basi kifo cha mtu kinaadhimisha mwisho wa kazi hiyo maalum. Kwa sababu Muumba amepangilia mseto maalum wa hali mbalimbali za kuzaliwa kwa mtu, ni wazi na dhahiri shahiri kwamba amepangilia pia mseto wa hali zisizobadilika kwa minajili ya kifo cha mtu. Kwa maneno mengine, hakuna anayezaliwa kwa bahati na hakuna kifo cha mtu ambacho hakitarajiwi, na si kuzaliwa, si kufa vyote vina uhusiano na maisha ya mtu ya awali na ya sasa. Hali za kuzaliwa na kifo cha mtu, vyote viliamuliwa kabla na Muumba; hii ni kudura ya mtu, hatima ya mtu. Kama vile tu mengi yanaweza kuzungumzwa kuhusu kuzaliwa kwa mtu, hata kifo cha kila mtu kitafanyika katika mseto tofauti katika hali maalum, hivyo basi urefu wa maisha tofauti miongoni mwa watu na njia tofauti pamoja na nyakati tofauti zinaandama vifo vyao. Baadhi ya watu wana nguvu na afya na ilhali wanakufa mapema; wengine ni wanyonge na wanauguaugua ilhali wanaishi hadi umri wa uzee, na wanaaga dunia kwa amani. Baadhi wanafarakana na dunia kutokana na sababu zisizokuwa za kawaida, wengine kutokana na sababu za kawaida. Baadhi wanakata roho wakiwa mbali na nyumbani, wengine wanayafumba macho yao kwa mara ya mwisho wakiwa na wapendwa wao kando yao. Baadhi ya watu hufia hewani, wengine hufia chini ya nchi. Wengine huzama chini ya maji, wengine nao kwenye majanga. Baadhi hufa asubuhi, wengine hufa usiku. … Kila mtu hutaka kuzaliwa kwa heshima, maisha mazuri, na kifo kitukufu, hakuna mtu anayeweza kufika zaidi ya hatima yake mwenyewe, hakuna mtu anayeweza kukwepa ukuu wa Muumba. Hii ni hatima ya binadamu. Binadamu anaweza kufanya aina zote za mipango ya siku zote za usoni, lakini hakuna mtu anayeweza kupanga njia na muda wa kuzaliwa kwake na kuondoka kwake ulimwenguni. Ingawaje watu hufanya kila wawezalo kuepuka na kuzuia kuja kwa kifo chao, ilhali, bila wao kujua, kifo huwa kinakaribia polepole. Hakuna anayejua ni lini atakapofarakana na dunia au ni vipi, isitoshe hata pale hayo yote yatakapofanyikia. Bila shaka, si binadamu wanaoshikilia nguvu za maisha na kifo, wala si kiumbe fulani kwenye ulimwengu wa kimaumbile, lakini ni Muumba, ambaye mamlaka yake ni ya kipekee. Maisha na kifo cha binadamu si zao la sheria fulani ya ulimwengu wa kimaumbile, lakini athari ya ukuu wa mamlaka ya Muumba.

2. Yule Asiyejua Ukuu wa Muumba Atahangaika kwa Woga wa Kifo

Wakati mtu anapoingia kwenye umri wa uzee, changamoto anazokabiliana nazo si kutosheleza mahitaji ya familia au kuanzisha maono makubwa katika maisha yake, lakini namna ya kuyaaga maisha yake, namna ya kukutana na mwisho wa maisha yake, namna ya kuweka kikomo kwenye mwisho wa uwepo wake binafsi. Ingawaje juujuu inaonekana kwamba watu hutilia makini kidogo kwa kifo, hakuna anayeweza kuepuka kuchunguza suala hili, kwani hakuna anayejua ikiwa ulimwengu mwingine uko kule upande mwingine wa kifo, ulimwengu ambao binadamu hawawezi kung’amua au kuhisi, ulimwengu wasiojua chochote kuuhusu. Hali hii huwafanya watu kuwa na wasiwasi kukabiliana na kifo moja kwa moja, wasiwasi wa kukabiliana nacho kama inavyostahili, na badala yake wanafanya kadri ya uwezo wao kuepuka mada hii. Na kwa hivyo mada hii humfanya kila mmoja kutishika kuhusu kifo, huongezea uzito kwenye fumbo hili kuhusiana na hoja hii isiyokwepeka ya maisha, huweka kivuli kisichoisha juu ya moyo wa kila mmoja.

Wakati mtu anapohisi mwili wake unaanza kudhoofika, wakati mtu anapohisi kwamba kifo chake chakaribia, mtu huhisi tishio, woga usioelezeka. Woga wa kifo humfanya mtu kuhisi kuwa mpweke zaidi na asiyejiweza, na kwa wakati huu mtu hujiuliza: Nilitoka wapi? Ninaenda wapi? Je, hivi ndivyo nitakavyokufa, huku maisha yangu yakinipita kwa haraka hivi? Je, huu ndio wakati unaoadhimisha mwisho wa maisha yangu? Ni nini, hatimaye, maana ya maisha? Maisha yana thamani gani, kwa kweli? Je, yanahusu umaarufu na utajiri? Je, yanahusu kulea familia? … Haijalishi kama mtu amewahi kufikiria maswali haya mahususi, haijalishi ni vipi mtu ana woga wa kifo, katika kina cha moyo wa kila mmoja siku zote kuna tamanio la kutaka kuchunguza zaidi mafumbo, hisia zisizoeleweka kuhusu maisha, pamoja na haya yote, ni uhusiano wa karibu na ulimwengu wenyewe, na kutotaka kuuacha. Pengine hakuna anayeweza kufafanua zaidi ni nini ambacho binadamu huogopa, ni nini ambacho binadamu hutaka kuchunguza zaidi, na nini kile ambacho ana uhusiano wa karibu nacho na kinachomfanya kutotaka kuondoka au kukiacha nyuma …

Kwa sababu wanaogopa kifo, watu huwa na wasiwasi mno; kwa vile wanaogopa kifo, vipo vitu vingi ambavyo hawawezi kuachilia. Wakati wako karibu kufa, baadhi ya watu huhangaika kuhusu hiki au kile; wanakuwa na wasiwasi kuhusu watoto wao, wapendwa wao, utajiri wao, ni kana kwamba kwa kuwa na wasiwasi hivyo wanaweza kuondoa mateso na hofu ambayo kifo huleta, ni kana kwamba kwa kuendeleza aina fulani ya urafiki wa karibu na wale wanaoishi wanaweza kukwepa ile hali ya kutoweza kujisaidia na upweke unaoandamana na kifo. Katika kina cha moyo wa binadamu kunao woga usiokamilika, woga wa kuachwa na wapendwa, woga wa kutowahi kutuliza macho yako kwenye mbingu za samawati, woga wa kutowahi tena kuangalia ulimwengu huu yakinifu. Nafsi pweke, iliyozoeana na wapendwa wake, husita kuachilia mshiko wa maisha na kuondoka, ikiwa pekee, kuelekea kwenye ulimwengu usiojulikana, usiozoeleka.

3. Maisha ya Kuishi Ukitafuta Umaarufu na Utajiri Yatamwacha Mtu Akiwa na Hasara Akikabiliana na Kifo

Kwa sababu ya ukuu na kuamuliwa kabla kwa Muumba, nafsi pweke iliyoanza bila chochote kwa jina lake huweza kupata wazazi na familia, fursa ya kuwa mwanachama wa kizazi cha binadamu, fursa ya kupitia maisha ya binadamu na kuona ulimwengu; na pia inafaidi fursa ya kupitia ukuu wa Muumba, kujua uzuri wa uumbaji wa Muumba, na zaidi kuliko vyote, kujua na kutii mamlaka ya Muumba. Lakini watu wengi zaidi huwa hawatumii vizuri fursa hii nadra na ya kipekee. Mtu hutumia nguvu zake zote maishani akipigana dhidi ya hatima yake, akatumia muda wake wote akihangaika na akijaribu kulisha familia yake na akisafiri huku na kule kati ya kutafuta utajiri na hadhi katika jamii. Mambo ambayo watu huthamini ni familia, pesa, na umaarufu; wanaona mambo haya kuwa mambo yenye thamani zaidi katika maisha. Kila mtu hulalamikia hatima yake, ilhali bado wanazisukuma hatima hizi nyuma ya akili zao na wanabaki na maswali ambayo ni lazima zaidi kuchunguza na kuelewa: kwa nini binadamu yuko hai, namna ambavyo binadamu anafaa kuishi, ni nini maana na thamani ya maisha. Katika maisha yao yote, hata hivyo iwe miaka mingapi, wanakimbilia tu kuhusu kutafuta umaarufu na utajiri, mpaka ujana wao ukawaacha, mpaka wakawa na nywele za kijivu na makunyanzi kwenye uso wao; mpaka wakagundua utajiri na umaarufu ni vitu visivyoweza kusitisha mtu kuelekea katika udhaifu unaotokana na uzee, kwamba pesa haiwezi kujaza utupu wa moyo: mpaka wanapoelewa kwamba hakuna mtu ambaye anaachwa nje kutoka kwenye sheria ya kuzaliwa, kuwa mzee, magonjwa, na kifo, kwamba hakuna mtu anayeweza kutoroka hatima ile inayomsubiri. Mpaka tu pale ambapo anapolazimishwa kukabiliana na awamu ya mwisho maishani ndipo anapong’amua kwa kweli kwamba hata kama mtu anamiliki mamilioni ya mali, hata kama mtu anayo heshima na cheo kikubwa, hakuna anayeweza kutoroka kifo, kwamba kila mtu atarudi kwenye sehemu yake asilia: nafsi pweke, bila chochote kwa jina lake. Wakati mtu anapokuwa na wazazi, mtu husadiki kwamba wazazi wa mtu ni kila kitu; wakati mtu anapokuwa na mali, mtu hufikiri kwamba pesa ndizo kitu cha muhimu, kwamba ndizo namna ambayo kwayo mtu huishi; wakati watu wanapokuwa na hadhi katika jamii, wanaishikilia na hata wanaweza kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya hadhi hiyo. Ni pale tu ambapo watu wanakaribia kuondoka ulimwenguni ndipo wanapotambua kwamba mambo yale waliyoishi katika maisha yao wakifuatilia si chochote bali mawingu yanayopita, hakuna chochote kati ya vitu hivi ambacho wanaweza kushikilia, hakuna hata chochote wanachoweza kwenda nacho, hakuna hata chochote kinachoweza kuwaondolea kifo, hakuna kile kinachoweza kuwapa ushirika au tulizo wakati nafsi yao inapokuwa pweke ikielekea kufa; na hata, hakuna kati ya hivyo vyote vinavyoweza kumpa mtu wokovu, na kuwaruhusu kushinda kifo. Umaarufu na utajiri ambao mtu hupata kwenye ulimwengu yakinifu humpa mtu kutosheka kwa muda, anasa ya kupita, hisia ya uwongo ya utulivu, na kumfanya mtu kupoteza njia. Na kwa hivyo watu, wanapong’ang’ana kila pahali kwenye bahari pana ya binadamu, wakitafuta amani, tulizo na utulivu wa moyo, wanafunikwa zaidi na zaidi na mawimbi. Wakati ambapo watu hawajapata maswali ambayo ni muhimu zaidi kuelewa—ni wapi wametoka, ni kwa nini wako hai, ni wapi wanakoenda na kadhalika—wanashawishiwa na umaarufu na utajiri, wanapotoshwa, wanadhibitiwa na vitu hivyo, na wanaishia kupotea bila kujua njia. Muda huyoyoma; miaka hupita kama kupepeswa kwa jicho; kabla ya mtu kutambua, mtu huaga kwaheri miaka yake bora zaidi ya maisha yake. Wakati mtu anakaribia kuondoka ulimwenguni, mtu anafika katika utambuzi wa taratibu kwamba kila kitu ulimwenguni kinamwacha polepole, kwamba mtu hawezi kushikilia tena vitu alivyomiliki; kisha mtu anahisi kwa kweli kwamba hamiliki chochote kamwe, kama mtoto mchanga anayelia ambaye ndio mwanzo amezaliwa na kubisha mlango ulimwenguni. Wakati huu, mtu anashawishiwa kutafakari kile ambacho amefanya maishani, thamani ya kuwa hai, ni nini maana yake, kwa nini mtu alikuja ulimwenguni; na wakati huu, mtu anaendelea kutaka kujua kama kweli kunayo maisha ya baadaye, kama Mbinguni kweli ipo, kama kweli kunayo adhabu…. Kwa kadri mtu anavyokaribia kifo, ndipo anavyotaka zaidi kuelewa maisha yanahusu nini haswa; kwa kadri mtu anavyokaribia kifo, ndipo moyo wake unapoonekana kuwa mtupu; kwa kadri mtu anavyokaribia kifo, ndipo anapohisi kuwa hawezi kusaidika; na kwa hivyo woga wa mtu kuhusu kifo unazidi kuwa mwingi siku baada ya siku. Kunazo sababu mbili zinazoelezea kwa nini watu huwa hivi wanapokaribia kifo: Kwanza, wako karibu kupoteza umaarufu na utajiri ambao maisha yao yalitegemea, wako karibu kuacha nyuma kila kitu kinachoonekana ulimwenguni; na pili, wako karibu kukabiliana, wakiwa peke yao, na ulimwengu usiojulikana, wenye mafumbo, himaya isiyojulikana ambapo wana woga wa kukanyaga guu lao kule, kule wasikokuwa na wapendwa na mbinu zozote za kupata msaada. Kwa hizo sababu mbili, kila mmoja anayekabiliana na kifo huhisi vibaya, hupitia hali ya wasiwasi na hujipata katika hali ya kutoweza kusaidika ambayo hawajawahi kupitia awali. Kwa hakika punde watu wanapofikia wakati huu ndipo wanapotambua kwamba kitu cha kwanza ambacho mtu lazima aelewe, anapokanyaga guu lake hapa duniani, ni wapi binadamu hutoka, kwa nini watu wako hai, nani anayeamuru hatima ya binadamu, ni nani anayekidhi mahitaji ya binadamu, na Aliye na ukuu juu ya uwepo wa binadamu. Maarifa haya ndiyo njia ya kweli ambayo kwayo mtu huishi, msingi muhimu kwa kuwepo kwa binadamu—kutojifunza namna ya kutosheleza familia ya mtu au namna ya kutimiza umaarufu na utajiri, kutojifunza namna ya kujitokeza katika umati wala namna ya kuishi maisha mazuri zaidi, bila kutaja namna ya kutia fora na kushindana kwa ufanisi dhidi ya wengine. Ingawaje mbinu mbalimbali za kuishi ambazo watu huishi wakijaribu kumiliki zinaweza kumpa wingi wa tulizo la mali, hazijawahi kuleta amani na tulizo la kweli moyoni, lakini badala yake hufanya watu kila wakati kupoteza mwelekeo wao, kuwa na wakati mgumu kujidhibiti, na kukosa kila fursa ya kujifunza maana ya maisha; mbinu hizi za kuishi huleta mawimbi fiche ya wasiwasi kuhusu namna ya kukabiliana na kifo vizuri. Maisha ya watu huharibika kwa njia hii. Muumba hushughulikia kila mmoja bila mapendeleo, huku akipatia kila mmoja wetu fursa ya kutosha maisha yote ili kuweza kupitia na kujua ukuu Wake, ilhali ni mpaka tu kifo kinapokaribia, wakati kivuli cha kifo kinaponing’inia karibu na mtu, ndipo mtu huyu huanza kuona nuru—na kisha muda huwa umeyoyoma mno.

Watu huishi maisha yao wakitafuta pesa na umaarufu; wanashikilia nyuzi hizi, wakifikiri kwamba ndizo mbinu zao pekee za msaada, ni kana kwamba wakiwa nazo wangeendelea kuishi, wangejitoa kwenye hesabu ya wale watakaokufa. Lakini pale tu wanapokuwa karibu kufa ndipo wanapotambua namna ambavyo vitu hivi vilivyo mbali na wao, namna walivyo wanyonge mbele ya kifo, namna wanavyosambaratika kwa urahisi, namna walivyo wapweke na wasivyoweza kusaidika, na hawana popote pa kugeukia. Wanatambua kwamba maisha hayawezi kununuliwa kwa pesa au umaarufu, kwamba haijalishi mtu ni tajiri vipi, haijalishi cheo chake kilivyo cha hadhi, watu wote ni maskini kwa njia sawa na wanaofanya mambo bila mpango mbele ya kifo. Wanatambua kwamba pesa haiwezi kununua maisha, kwamba umaarufu hauwezi kufuta kifo, kwamba si pesa wala umaarufu vinaweza kurefusha maisha ya mtu kwa hata dakika moja, hata sekunde moja. Watu wanapohisi hivi zaidi, ndipo wanapotamani zaidi kuishi; watu wanapohisi hivi zaidi, ndipo wanapohofia kukaribia kwa kifo. Ni katika wakati huu tu ndipo wanapotambua kwa kweli kwamba maisha yao si yao, si yao kudhibiti, na kwamba mtu hana usemi kuhusu iwapo ataishi au atakufa, kwamba haya mambo yote yanapatikana nje ya udhibiti wa mtu.

4. Njoo Chini ya Utawala wa Muumba na Ukabiliane na Kifo kwa Utulivu

Wakati ule ambao mtu anazaliwa, nafsi ya mtu iliyo pweke inaanza kupitia maisha hapa duniani, inapitia mamlaka ya Muumba ambayo Muumba ameipangilia. Ni wazi kwamba, kwa mtu husika, ile nafsi, hii ni fursa nzuri kabisa ya kupata maarifa kuhusu ukuu wa Muumba, kujua mamlaka Yake na kuyapitia binafsi. Watu wanaishi maisha yao kulingana na sheria za hatima zilizowekwa wazi kwao na Muumba, na kwa mtu yeyote mwenye akili razini aliye na dhamiri, kuelewa ukuu wa Muumba na kutambua mamlaka yake kwenye mkondo wa miongo yao mbalimbali hapa nchini si jambo gumu kufanya. Kwa hivyo inafaa kuwa rahisi sana kwa kila mtu kutambua, kupitia kwa yale ambayo yeye mwenyewe amepitia maishani kwa kipindi cha miongo mbalimbali, kwamba hatima zote za binadamu zimeamuliwa kabla, na kung’amua au kujumlisha ni nini maana ya kuishi. Wakati uo huo ambao mtu anakumbatia mafunzo haya ya maisha, mtu ataelewa kwa utaratibu ni wapi maisha yanatokea, kunga’mua hasa ni nini ambacho moyo unahitaji kwa kweli, nini kitaongoza mtu kwenye njia ya kweli ya maisha, kazi maalum na shabaha ya maisha ya binadamu inafaa kuwa nini; na mtu ataanza kutambua kwa utaratibu kwamba kama mtu hataabudu Muumba, kama mtu hataingia kwenye utawala Wake, basi mtu anakabiliana na kifo—wakati nafsi iko karibu kukabiliana na Muumba kwa mara nyingine—moyo wa mtu utajazwa hofu na ugumu usio na mipaka. Kama mtu amekuwepo ulimwenguni kwa miongo kadhaa ilhali hajajua ni wapi maisha ya binadamu hutoka, angali hajatambua ni kwenye viganja vya mikono ya nani hatima ya binadamu huwa, basi si ajabu hataweza kukabiliana na kifo kwa utulivu. Mtu aliyepata maarifa ya ukuu wa Muumba baada ya kupitia miongo kadhaa ya maisha, ni mtu aliye na shukrani sahihi ya maana na thamani ya maisha; mtu aliye na kina cha maarifa kuhusu kusudi la maisha, aliye na hali halisi aliyopitia na anaelewa ukuu wa Muumba; na hata zaidi, mtu anayeweza kunyenyekea mbele ya mamlaka ya Muumba. Mtu kama huyo anaelewa maana ya uumbaji wa Mungu wa mwanadamu, anaelewa kwamba binadamu anafaa kumwabudu Muumba, kwamba kila kitu anachomiliki binadamu kinatoka kwa Muumba na kitarudi kwake siku fulani isiyo mbali sana kwenye siku za usoni; mtu kama huyo anaelewa kwamba Muumba hupangilia kuzaliwa kwa binadamu na ana ukuu juu ya kifo cha binadamu, na kwamba maisha na kifo vyote vimeamuliwa kabla na mamlaka ya Muumba. Kwa hiyo, wakati mtu anapong’amua mambo haya, mtu ataanza kuweza kukabiliana na kifo kwa utulivu na kwa kawaida, kuweka pembeni mali yake yote ya dunia kwa utulivu, kukubali na kunyenyekea kwa furaha kwa yote yatakayofuata, na kukaribisha awamu ya mwisho ya maisha iliyopangiliwa na Muumba badala ya kutishika vivyo hivyo tu na kung’ang’ana dhidi ya kifo. Ikiwa mtu anayaona maisha kama fursa ya kupitia ukuu wa Muumba na kujua mamlaka yake, ikiwa mtu anayaona maisha yake kama fursa nadra ya kutekeleza wajibu wake akiwa binadamu aliyeumbwa na kutimiza kazi yake maalum, basi mtu atakuwa ana mtazamo sahihi wa maisha, ataishi maisha yaliyobarikiwa na yanayoongozwa na Muumba, atatembea kwenye nuru ya Muumba, atajua ukuu wa Muumba, atakuwa katika utawala Wake, atakuwa shahidi wa matendo Yake ya kimiujiza na mamlaka Yake. Ni wazi kwamba, mtu kama huyo atahitajika kupendwa na kukubaliwa na Muumba, na mtu kama huyo ndiye anaweza kushikilia mtazamo mtulivu mbele ya kifo, na anayeweza kukaribisha awamu hii ya mwisho kwa furaha. Bila shaka Ayubu alikuwa na mtazamo kama huu kwa kifo; alikuwa katika nafasi ya kukubali kwa furaha awamu ya mwisho ya maisha, na baada ya kuhitimisha safari yake ya maisha vizuri, baada ya kukamilisha kazi yake maalum alirudi upande wa Muumba.

5. Bidii na Faida za Ayubu katika Maisha Zamruhusu Kukabiliana na Kifo kwa Utulivu

Katika Maandiko imeandikwa kuhusu Ayubu: “Kwa hivyo Ayubu akafariki, akiwa mzee na aliyejawa na siku” (Ayubu 42:17). Hii inamaanisha kwamba wakati Ayubu alipoaga dunia, hakuwa na majuto na hakuhisi maumivu, lakini aliondoka kimaumbile ulimwenguni. Kama vile kila mmoja anavyojua, Ayubu alikuwa mwanamume aliyemcha Mungu na aliyeambaa maovu alipokuwa hai; Mungu alimpongeza kwa matendo yake ya haki, watu waliyakumbuka, na maisha yake, zaidi ya yeyote yule mwingine, yalikuwa na thamani na umuhimu. Ayubu alifurahia baraka za Mungu na aliitwa mtakatifu na Yeye hapa duniani, na aliweza pia kujaribiwa na Mungu na kujaribiwa na Shetani; alisimama kuwa shahidi wa Mungu na alistahili kuwa mtu mtakatifu. Kwenye miongo mbalimbali baada ya kujaribiwa na Mungu, aliishi maisha ambayo yalikuwa yenye thamani zaidi, yenye maana zaidi, yaliyokita mizizi, na yenye amani zaidi kuliko hata awali. Kutokana na matendo yake ya haki, Mungu alimjaribu; kwa sababu ya matendo yake ya haki, Mungu alionekana kwake na kuongea naye moja kwa moja. Kwa hiyo, kwenye miaka yake baada ya kujaribiwa, Ayubu alielewa na kushukuru thamani ya maisha kwa njia thabiti zaidi, aliweza kutimiza ufahamu wa kina zaidi wa ukuu wa Muumba, na akapata maarifa yenye hakika na usahihi zaidi kuhusu namna ambavyo Muumba anavyotoa na kuzichukua baraka zake. Kitabu cha Ayubu kinarekodi kwamba Yehova Mungu alimpa hata baraka nyingi zaidi Ayubu kuliko hapo awali, Akimweka Ayubu katika nafasi bora zaidi ya kujua ukuu wa Muumba na kujua kukabiliana na kifo akiwa mtulivu. Kwa hiyo, Ayubu alipozeeka na kukabiliana na kifo, bila shaka asingekuwa na wasiwasi na mali yake. Hakuwa na wasiwasi wowote, hakuwa na chochote cha kujutia, na bila shaka hakuogopa kifo; kwani aliishi maisha yake akitembea ile njia ya kumcha Mungu, kuepuka maovu, na hakuwa na sababu yoyote ya kuwa na wasiwasi kuhusu mwisho wake mwenyewe. Ni watu wangapi leo wanaweza kuchukua hatua kwa njia zote hizo ambazo Ayubu alitumia alipokabiliwa na kifo chake mwenyewe? Kwa nini hakuna mtu anayeweza kuendeleza mwelekeo wa mtazamo rahisi kama huu? Kunayo sababu moja tu: Ayubu aliishi maisha kwenye harakati ya kutafuta kimsingi kusadiki, utambuzi, na unyenyekevu kwa ukuu wa Mungu, na ilikuwa katika kusadiki huku, utambuzi huu na unyenyekevu huu ambapo aliweza kupitia zile awamu muhimu za maisha, aliishi kwa kudhihirisha miaka yake ya mwisho na akajuliana hali na awamu yake ya mwisho ya maisha. Licha ya kile ambacho Ayubu alipitia, bidii zake na shabaha zake katika maisha zilikuwa za furaha na wala si zenye maumivu. Alikuwa na furaha si tu kwa sababu ya baraka au shukrani aliyopewa yeye na Muumba, lakini muhimu zaidi kwa sababu ya shughuli zake na shabaha za maisha, kwa sababu ya maarifa yaliyoongezeka kwa utaratibu na ufahamu wa kweli wa ukuu wa Muumba ambao alitimiza kupitia kwa kumcha Mungu na kwa kuepuka maovu, na zaidi, kwa sababu ya matendo Yake ya maajabu ambayo Ayubu alipitia kibinafsi wakati huu akiwa chini ya ukuu wa Muumba, na hali aliyopitia yenye uchangamfu na isiyosahaulika na kumbukumbu za kuwepo kwake, kuzoeana na wenzake, na kuzoeana kati yake yeye na Mungu; kwa sababu ya tulizo na furaha zilizotokana na kujua mapenzi ya Muumba; kwa sababu ya kustahi kulikotokea baada ya kuona kwamba Yeye ni mkubwa, ni wa ajabu, Anayependeka, na ni mwaminifu. Sababu ya Ayubu kuweza kukabiliana na kifo bila ya kuteseka ni kwamba alijua kwamba, kwa kufa, angerudi kwenye upande wa Muumba. Na zilikuwa shughuli zake katika maisha zilizomruhusu kukabiliana na kifo akiwa ametulia, kukabiliana na matarajio ya Muumba kuchukua tena maisha yake, kwa moyo mzuri, na zaidi ya yote, kusimama wima, kutotikisika na kuwa huru kutokana na mashaka mbele ya Muumba. Je, watu wanaweza siku hizi kutimiza aina ya furaha ambayo Ayubu alikuwa nayo? Je, nyinyi wenyewe mko katika hali ya kufanya hivyo? Kwa sababu watu siku hizi wako hivyo, kwa nini hawawezi kuishi kwa furaha, kama alivyofanya Ayubu? Kwa nini hawawezi kutoroka mateso yanayotokana na woga wa kifo? Wakati wanapokabiliwa na kifo, baadhi ya watu hujiendea haja ndogo; wengine hutetemeka, wakazirai, na wakalalamika dhidi ya Mbinguni na binadamu vilevile, wengine hata wakalia kwa huzuni na kutokwa machozi. Kwa vyovyote vile, hii ndiyo miitikio ya ghafla inayofanyika wakati kifo kinapokaribia. Watu huwa na tabia hii ya kuaibisha haswa kwa sababu, ndani ya mioyo yao, wanaogopa kifo, kwa sababu hawana maarifa yaliyo wazi na uwezo wa kushukuru ukuu wa Mungu na mipangilio yake, na isitoshe hata kujinyenyekeza mbele ya vitu hivi; kwa sababu watu hawataki chochote ila kupangilia na kutawala kila kitu wenyewe, kudhibiti hatima zao binafsi, maisha yao binafsi na hata kifo. Si ajabu, hivyo basi, kwamba watu hawajawahi kuweza kuacha woga wa kifo.

6. Ni kwa Kukubali tu Ukuu wa Muumba Ndipo Mtu Anaweza Kurejea Upande Wake

Wakati mtu hana maarifa yaliyo wazi na hajapitia ukuu wa Mungu na mipangilio Yake, maarifa ya mtu kuhusu hatima na yale ya kifo yatakuwa yale yasiyoeleweka. Watu hawawezi kuona waziwazi kwamba haya yote yamo kwenye kiganja cha mkono wa Mungu, hawatambui kwamba Mungu ameushika usukani na Anashikilia ukuu juu yao, hawatambui kwamba binadamu hawezi kutupa nje au kutoroka ukuu kama huo; na kwa hivyo wakati wanapokabiliwa na kifo hakuna mwisho wowote katika maneno yao ya mwisho, wasiwasi wao, na hata majuto. Wanalemewa sana na mambo mengi, wanajivuta ajabu, kunakuwa na mkanganyo mkubwa, na haya yote yanawafanya kuogopa kifo. Kwani mtu yeyote aliyezaliwa ulimwenguni humu, kuzaliwa kwake kunahitajika, na kuaga kwake hakuwezi kuepukika, na hakuna mtu anayeweza kuupiga chenga mkondo huu. Kama mtu atataka kuondoka ulimwenguni humu bila maumivu, kama mtu atataka kukabiliana na awamu ya mwisho ya maisha bila kusitasita au wasiwasi, njia pekee ni kutokuwa na majuto. Na njia pekee ya kuondoka bila majuto ni kujua ukuu wa Muumba, kujua mamlaka yake, na kunyenyekea mbele zake. Ni kwa njia hii tu ndipo mtu anaweza kuwa mbali na mahangaiko ya binadamu, maovu, utumwa wa Shetani; ni kwa njia hii ndipo mtu anaweza kuishi maisha kama ya Ayubu, akiongozwa na akibarikiwa na Muumba, maisha yaliyo huru na yaliyokombolewa, maisha yenye thamani na maana, maisha yenye uaminifu na moyo wazi; ni kupitia kwa njia hii tu ndipo mtu anaweza kunyenyekea, kama Ayubu, kujaribiwa na kunyang’anywa na Muumba, kunyenyekeza katika mipango na mipangilio ya Muumba; ni kwa njia hii tu ndipo mtu anaweza kumwabudu Muumba maisha yake yote na kuweza kupata pongezi Lake, kama Ayubu alivyopata, na kusikia sauti Yake, kumwona akionekana; ni kwa njia hii tu ndipo mtu anaweza kuishi na kufa kwa furaha, kama Ayubu, bila ya maumivu, bila wasiwasi, bila majuto; ni kwa njia hii tu ndipo mtu anaweza kuishi kwa nuru, kama Ayubu, kupita kila mojawapo ya awamu ya maisha kwa nuru, na kukamilisha vizuri safari yake kwa nuru, kutimiza kwa ufanisi kazi yake maalum—kupitia, kujifunza, na kujua ukuu wa Muumba kama kiumbe kilichoumbwa—na kuiaga dunia kwa nuru, na milele hadi milele kusimama upande wa Muumba kama kiumbe kilichoumbwa, kilichopongezwa na Yeye.

Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee III

Iliyotangulia: Uzao: Awamu ya Tano

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Maudhui Yanayohusiana

Uhuru: Awamu ya Tatu

Baada ya mtu kupita utoto na wakati wake wa kubaleghe na kwa utaratibu bila kuzuilika kufikia ukomavu, hatua inayofuata ni kwake yeye...

Kuzaliwa: Awamu ya Kwanza

Mahali ambapo mtu amezaliwa, ni familia gani alimozaliwa, jinsia ya mtu, umbo la mtu, na wakati wa kuzaliwa—haya ndiyo maelezo ya awamu ya...

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp