Jinsi Unavyopaswa Kuitembea Sehemu ya Mwisho ya Njia

Ninyi sasa mko katika kipindi cha mwisho cha njia, na ni sehemu muhimu ya njia. Labda umepitia mateso mengi, umefanya kazi nyingi, umesafiri barabara nyingi, na umesikiliza mahubiri mengi; labda haijakuwa rahisi kufika pale ulipo sasa. Ikiwa huwezi kuvumilia mateso unayokabiliwa nayo kwa sasa na ukiendelea kama ulivyofanya hapo zamani, basi huwezi kukamilishwa. Maneno haya hayajakusudiwa kukuogofya—ni ukweli. Baada ya Petro kupitia kazi nyingi ya Mungu, alipata ufahamu wa mambo fulani, na pia utambuzi mwingi. Alikuja kuelewa mambo mengi kuhusu kanuni ya huduma, na baadaye aliweza kujitoa kikamilifu kwa yale ambayo Yesu alimwaminia. Usafishaji mkubwa ambao alipokea kwa kiasi kikubwa ulikuwa kwa sababu, kwa mambo ambayo alikuwa amefanya mwenyewe, alihisi kwamba alikuwa na deni kubwa la Mungu, na kwamba hangeweza kumlipa kamwe. Petro alitambua pia kwamba mwanadamu ni mpotovu sana, jambo ambalo lilimfanya ahisi hatia katika dhamiri yake. Yesu alikuwa amemwambia Petro mambo mengi, lakini katika wakati ambapo mambo haya yalisemwa, aliweza kuwa na ufahamu mdogo tu, na wakati mwingine bado alikuwa na upinzani na uasi kiasi. Baada ya Yesu kusulubiwa msalabani, mwishowe alipitia mwamko fulani, na ndani mwake alihisi maumivu makali ya kujilaumu mwenyewe. Mwishowe, ilifikia hatua ambapo alihisi haikukubalika kuwa na maoni yoyote ambayo hayakuwa sahihi. Aliijua hali yake mwenyewe vizuri sana, na pia alijua utakatifu wa Bwana vizuri sana. Kwa sababu hiyo, moyo wa kumpenda Bwana ulikua ndani yake hata zaidi, na akazingatia zaidi maisha yake mwenyewe. Kwa sababu ya hili alipitia shida nyingi, na ingawa wakati mwingine ilikuwa kama kwamba alikuwa na ugonjwa hatari na hata ilionekana kama kwamba alikuwa amekufa, baada ya kusafishwa kwa njia hii mara nyingi, alijielewa zaidi, na akawa na upendo wa kweli kwa Bwana. Inaweza kusemekana kuwa maisha yake yote yalitumika katika usafishaji, na hata zaidi ya hayo, katika kuadibu. Uzoefu wake ulikuwa tofauti na wa mtu mwingine yeyote, na upendo wake ulizidi ule wa mtu yeyote ambaye hajakamilishwa. Sababu ya kuchaguliwa kwake kama mfano ni kwa sababu alipitia uchungu mwingi kabisa katika maisha yake, na yale aliyoyapitia yalifanikiwa zaidi. Kama mnaweza kweli kuitembea sehemu ya mwisho ya njia kama vile Petro alivyofanya, basi hakuna kiumbe yeyote anayeweza kuwanyang’anya baraka zenu.

Petro alikuwa mtu mwenye dhamiri, lakini hata akiwa na ubinadamu aliokuwa nao, bila kuzuilika, alikuwa na maoni mengi ya upinzani na ya uasi katika wakati huo alipoanza kumfuata Yesu kwa mara ya kwanza. Lakini alipokuwa akimfuata Yesu, hakuchukulia mambo haya kwa uzito, akiamini kuwa hivi ndivyo watu walipaswa kuwa. Kwa hivyo, mwanzoni hakuhisi lawama yoyote na wala hakushughulikiwa. Yesu hakuchukulia majibu ya Petro kwa uzito, wala Hakuyatilia maanani, bali Aliendelea tu na kazi ambayo Alipaswa kufanya. Hakuwahi kutafuta makosa madogo madogo kwa Petro na wengine. Unaweza kusema: “Inawezekana kwamba Yesu hakujua kuhusu maoni haya waliyokuwa nayo?” La hasha! Ni kwa sababu alimwelewa Petro vyema—kwa kweli, inaweza kusemwa kwamba Alikuwa na ufahamu wa juu kumhusu—ndiyo maana Yesu hakuchukua hatua yoyote dhidi yake. Aliwachukia wanadamu lakini pia Aliwahurumia. Je, si kuna watu wengi miongoni mwenu sasa ambao ni wapinzani kama tu alivyokuwa Paulo, na walio na maoni mengi kama vile Petro alivyokuwa nayo kwa Bwana Yesu wakati huo? Nakwambia, itakuwa bora usipoamini sana katika hisi yako ya tatu, hisi yako ya mtazamo, ambayo siyo ya kutegemewa na iliyoharibiwa kabisa na upotoshaji wa Shetani zamani. Je, unafikiri kwamba mtazamo wako ni kamili na hauna dosari? Paulo alimpinga Bwana Yesu mara nyingi, lakini Yesu hakujibu. Inawezekana kwamba Yesu aliweza kuponya wagonjwa na kufukuza pepo, lakini hakuweza kumfukuza yule “pepo” aliyekuwa ndani ya Paulo? Ni kwa nini ni kwamba huku Paulo akiendelea kuwakamata wanafunzi wa Yesu kwa ukaidi, ni baada tu ya Yesu kufufuka na kupaa kwenda mbinguni ndipo mwishowe Yesu alimwonekania akiwa njiani kwenda Dameski na kumpiga chini? Inawezekana kwamba Bwana Yesu alijibu polepole sana? Au ni kwa sababu Hakuwa na mamlaka yoyote wakati Alikuwa katika mwili? Je, unafikiri kuwa wakati wewe ni mharibifu kwa siri na mpinzani wakati ambapo Sioni ya kwamba Sijui kuhusu hilo? Je, unafikiri kwamba mabaki ya nuru unayopata kutoka kwa Roho Mtakatifu yanaweza kutumiwa kunipinga Mimi? Wakati Petro hakuwa mkomavu, alikuwa na maoni mengi kumhusu Yesu, kwa hivyo mbona hakulaumiwa? Hivi sasa, watu wengi wanafanya mambo bila lawama, na hata wanapoambiwa wazi kuwa kile wanachofanya si sahihi, bado hawasikilizi. Je, hilo si kwa sababu ya uasi wa mwanadamu kabisa? Nimesema mengi sana sasa, lakini bado huna hata chembe ya mtazamo wa dhamiri, kwa hivyo utawezaje kuitembea sehemu ya mwisho ya njia, kuendelea kutembea hadi njia itakapomalizika? Je, huhisi kuwa hili ni swali lenye uzito mkubwa?

Baada ya watu kushindwa, wanaweza kutii mipango ya Mungu; wana imani yao na ridhaa yao ambayo kwayo wanampenda Mungu, na wanategemea vitu hivi kumfuata. Kwa hivyo sehemu ya mwisho ya njia inaweza kutembewaje? Katika siku zako za kupitia mateso, lazima uvumilie shida zote, na lazima uwe radhi kuteseka; ni kwa njia hii tu ndiyo unaweza kuitembea sehemu hii ya njia vizuri. Je, unafikiri ni rahisi sana kuitembea sehemu hii ya njia? Unapaswa kujua ni kazi gani unayopaswa kutimiza; lazima mwongeze ubora wenu wa tabia na mjiandae na ukweli wa kutosha. Hii siyo kazi ya siku moja au mbili, na siyo rahisi kama vile unavyofikiri! Kuitembea sehemu ya mwisho ya njia kunategemea imani na ridhaa uliyo nayo kweli. Pengine huwezi kumwona Roho Mtakatifu akifanya kazi ndani yako, au pengine huwezi kugundua kazi ya Roho Mtakatifu kanisani, kwa hivyo wewe huna rajua na unasikitika na kukata tamaa sana kwa siku za usoni. Hususani, mashujaa wakuu wa zamani wote wameanguka—je, yote haya si pigo kwako? Je, unapaswa kuyaonaje mambo haya? Je, una imani, au huna? Unaielewa kazi ya leo kikamilifu, au huielewi? Vitu hivi vinaweza kuamua ikiwa unaweza kuitembea sehemu ya mwisho ya njia kwa mafanikio.

Ni kwa nini inasemekana kwamba sasa mko kwenye sehemu ya mwisho ya njia? Ni kwa sababu mmeelewa kila kitu mnachopaswa kuelewa, na ni kwa sababu Nimewaambia kila kitu ambacho watu wanapaswa kutimiza. Pia, Nimewaambia kuhusu kila kitu ambacho mmeaminiwa nacho. Kwa hivyo, kile mnachokitembea sasa ni sehemu ya mwisho ya njia ambayo kwayo Ninawaongoza watu. Nahitaji tu kwamba mpate uwezo wa kuishi kwa kujitegemea; wewe utakuwa na njia ya kufuata daima na kila wakati, utaongeza ubora wako wa tabia kama zamani, utasoma maneno ya Mungu kwa kawaida, na kuishi maisha ya kawaida ya binadamu. Sasa Ninakuongoza uishi hivi, lakini katika siku za usoni wakati Sikuongozi, bado utaweza kuishi hivi? Je, utaweza kuendelea? Hili ndilo alilopitia Petro: Wakati Yesu alikuwa akimwongoza, hakuwa na ufahamu; alikuwa asiyejali kama mtoto, na hakuyachukulia mambo aliyofanya kwa uzito. Ilikuwa tu baada ya Yesu kuondoka ndipo alianza maisha yake ya binadamu wa kawaida. Maisha yake yenye maana yalianza tu baada ya Yesu kuondoka. Hata ingawa alikuwa na akili fulani ya ubinadamu wa kawaida na mambo fulani ambayo mtu wa kawaida anapaswa kuwa nayo, hata hivyo yale aliyopitia na ufuatiliaji wake wa kweli havikuwa na mwanzo mpya hadi Yesu alipoondoka. Je, hali yenu ya sasa ni ipi? Sasa, Mimi ninakuongoza hivi, na wewe unafikiri hili ni jambo zuri sana. Hakuna mazingira na majaribu yanayokukumba, lakini kwa njia hii hakuna njia ya kuona wewe kweli una kimo cha aina gani, wala hakuna njia yoyote ya kuona kama wewe kweli ni mtu anayefuatilia ukweli. Unasema kwa mdomo wako kwamba unaelewa kiini chako mwenyewe, lakini haya ni maneno matupu. Ni katika siku za usoni tu, ukweli utakapokujia, ndipo ufahamu wako utathibitishwa. Sasa, wewe una ufahamu wa aina hii: “Ninaelewa kwamba mwili wangu umepotoka sana, na kiini cha miili ya watu ni kuasi na kumpinga Mungu. Kuweza kupokea hukumu na kuadibu kwa Mungu ndiyo njia ambayo Yeye huwainua watu. Nimeelewa hilo sasa, na niko tayari kulipa upendo wa Mungu.” Lakini hili ni rahisi kusema. Baadaye wakati dhiki, majaribu, na mateso yatakukumba, haitakuwa rahisi kupitia vitu hivi. Mtafuata hivi kila siku, lakini bado hamwezi kuendelea kupitia matukio yenu. Itakuwa mbaya zaidi ikiwa Nitawaacha na Niwapuuze kabisa; watu wengi wataanguka chini na kugeuka kuwa nguzo ya chumvi, alama ya aibu. Matokeo kama hayo yanawezekana kuwepo sana. Je, huogopi au kuwa wasiwasi kuhusu hili? Petro alipitia mazingira ya aina hiyo na alipitia mateso ya aina hiyo, lakini bado alisimama imara. Ukipitishwa katika mazingira hayo, je, utaweza kusimama imara? Vitu ambavyo Yesu alisema na kazi ambayo Alifanya alipokuwa duniani vilimpa Petro msingi, na ilikuwa kwa msingi huu ndiyo aliitembea njia yake ya baadaye. Je, mnaweza kufikia kiwango hicho? Njia ambazo umetembea na ukweli ambao umeelewa—je, vinaweza kuwa msingi wako ambao kwao unaweza kusimama imara katika siku zijazo? Je, vitu hivi vinaweza kuwa maono yako ya kusimama imara baadaye? Nitawaambia ukweli—mtu anaweza kusema kwamba yale ambayo watu wanaelewa sasa yote ni mafundisho. Hii ni kwa sababu hawana uzoefu wa vitu vyote ambavyo wanaelewa. Kwamba umeweza kuendelea hadi sasa ni kwa sababu umeongozwa na mwanga mpya kikamilifu. Si kwa sababu kimo chako kimefikia kiwango fulani, lakini badala yake ni kwa sababu maneno Yangu yamekuongoza hadi siku ya leo; si kwa sababu wewe una imani kubwa, bali ni kwa sababu ya hekima ya maneno Yangu, ambayo yalikufanya usiweze kufanya chochote ila kufuata wakati huo wote hadi leo. Nisingeweza kunena sasa, Nisingeweza kutamka sauti Yangu, usingeweza kuendelea na ungeacha kusonga mbele mara moja. Je, hiki si kimo chenu halisi? Hamjui mnapaswa kuingia kutoka katika vipengele vipi na mnapaswa kufidia mnachokosa kutoka katika vipengele vipi. Hamwelewi jinsi ya kuishi kwa kudhihirisha maisha ya binadamu yenye maana, jinsi ya kulipa upendo wa Mungu, au jinsi ya kushuhudia kwa njia yenye nguvu na kubwa. Hamuwezi kabisa kufanikisha mambo haya. Ninyi ni wavivu na ni wapumbavu! Kile mnachoweza kufanya ni kuegemea kitu kingine tu, na kile mnachoegemea ni mwanga mpya na Yule aliye mbele, Akiwaongoza. Kwamba umeweza kuendelea kuishi hadi leo ni kwa sababu umeutegemea mwanga mpya kabisa na matamshi ya hivi karibuni kabisa. Ninyi hamko kabisa kama Petro ambaye alikuwa hodari wa kufuatilia njia ya kweli, au kama Ayubu, ambaye aliweza kumwabudu Yehova kwa kujitoa kikamilifu na kuamini kwamba Yehova alikuwa Mungu bila kujali jinsi Yehova alivyomjaribu, na ikiwa Alimbariki au la. Je, wewe una uwezo wa kufanya hilo? Je, ninyi mmeshindwaje? Kipengele kimoja ni hukumu, kuadibu, na laana, na kipengele kingine ni siri zinazowashinda. Ninyi nyote ni kama punda. Ikiwa yale Ninayozungumza kuhusu si ya juu sana vya kutosha kwenu, ikiwa hakuna siri, basi hamwezi kushindwa. Ikiwa ingekuwa ni mtu anayehubiri na kila wakati ahubiri kuhusu mambo yale yale kwa kipindi cha muda, nyote mngeondoka na kutawanyika ndani ya miaka miwili; hamngeweza kuendelea. Hamjui jinsi ya kuingia kwa kina zaidi, wala hamwelewi jinsi ya kufuatilia ukweli au njia ya uzima. Kile mnachoelewa ni kupokea kitu kinachoonekana kuwa kipya kwenu, kama vile kusikia kuhusu siri au maono, au jinsi Mungu alivyokuwa Akifanya kazi, au matukio aliyopitia Petro, au maelezo ya nyuma ya kusulubiwa kwa Yesu…. Mko tayari kusikia kuhusu mambo haya tu, na kadiri mnavyosikiliza zaidi ndivyo mnavyopata nguvu zaidi. Mnayasikiliza haya yote ili muondoe huzuni na uchovu wenu tu. Maisha yenu yanahimiliwa kikamilifu na vitu hivi vipya. Je, unafikiri kwamba umefika mahali ulipo leo kwa ajili ya imani yako mwenyewe? Je, hiki si kimo kidogo cha kusikitisha unachomiliki? Uadilifu wenu uko wapi? Ubinadamu wenu uko wapi? Je, mna uzima wa binadamu? Je, mna vipengele vingapi vinavyohitajika kwa ajili ya kukamilishwa? Je, kile Ninachosema si ukweli? Ninazungumza na kufanya kazi kwa njia hii, lakini bado mnakuwa makini kwa nadra sana. Wakati mnafuata, pia mnachunga. Kila wakati mna mwonekano wa kutojali, na kila wakati mnaongozwa kama wanyama. Hivi ndivyo ninyi nyote mmeendelea; kile kilichowaongoza hadi pale mlipo leo kimekuwa kuadibu, usafishaji, na kurudiwa. Ikiwa mahubiri fulani kuhusu kuingia katika uzima pekee yangehubiriwa, si ninyi nyote mngeponyoka zamani? Kila mmoja wenu ni mwenye kupenda makuu zaidi kuliko mwingine, lakini kwa kweli matumbo yenu yamejaa maji machafu tu! Umeweza tu kuendelea hadi sasa kwa sababu wewe umekuja kuelewa siri chache, mambo fulani ambayo wanadamu hawajawahi kuelewa hapo awali. Hamna sababu ya kutofuata, kwa hivyo mmeweza tu kujikaza na kufuata umati. Haya ni matokeo ambayo yamepatikana tu kupitia maneno Yangu, na hakika silo jambo ambalo ninyi wenyewe mmetimiza. Hamna chochote cha kujivunia. Kwa hivyo, katika hatua hii ya kazi mmeongozwa hadi siku ya leo kimsingi kupitia maneno. Vinginevyo, ni nani kati yenu ambaye angeweza kutii? Ni nani angeweza kuendelea kuwepo hadi leo? Tangu mwanzo mlitaka kuondoka fursa ya kwanza iwezekanayo itokeapo, lakini hamkuthubutu kufanya hivyo; hamkuwa na ujasiri. Hadi leo, mmekuwa mkifuata shingo upande.

Ilikuwa tu baada ya Yesu kusulubiwa msalabani na kuondoka ndiyo Petro alianza kuifuata njia yake mwenyewe na kuanza kuitembea njia aliyopaswa kuitembea; alianza kujiandaa baada tu ya kuona upungufu wake na kasoro zake. Aliona kwamba alikuwa na upendo mdogo sana kwa Mungu na hiari yake ya kuteseka haikutosha, kwamba hakuwa na utambuzi wowote na kwamba hakuwa na akili. Aliona kwamba kulikuwa na mambo mengi ndani yake ambayo hayakulingana na mapenzi ya Yesu, na kwamba kulikuwa na mambo mengi ambayo yalikuwa ya uasi na upinzani na yaliyotiwa najisi mapenzi ya wanadamu. Ilikuwa tu baada ya hili ndiyo alipata kuingia katika kila kipengele. Yesu alipokuwa akimwongoza, Yesu aliifunua hali yake na Petro aliikubali na kukubaliana na kile ambacho Yesu alisema, lakini bado alikosa ufahamu wa kweli mpaka baadaye. Hiyo ilikuwa kwa sababu wakati huo, hakuwa na uzoefu wala maarifa ya hali yake mwenyewe. Hiyo ni kusema, kwa sasa Natumia maneno tu kuwaongoza, na haiwezekani kuwakamilisha katika kipindi kifupi na mtawekewa mipaka katika kuweza kuelewa na kujua ukweli. Hii ni kwa sababu kukushinda wewe na kukushawishi katika moyo wako ndiyo kazi ya sasa na ni baada tu ya watu kushindwa ndiyo wataweza kukamilishwa. Hivi sasa, maono hayo na ukweli huo ambao wewe unaelewa yanaweka msingi kwa ajili ya matukio utakayopitia katika siku zijazo; katika dhiki za siku zijazo nyote mtakuwa na uzoefu wa vitendo wa maneno haya. Baadaye, majaribu yatakapokujia na upitie dhiki, utakumbuka maneno unayosema leo, ambayo ni: “Haijalishi ni dhiki, majaribu au maafa yapi makubwa ninayokumbana nayo, lazima nimridhishe Mungu.” Fikiria matukio aliyopitia Petro na kisha matukio aliyopitia Ayubu—wewe utaamshwa na maneno ya leo. Ni kwa njia hii tu ndiyo imani yako inaweza kutiwa msukumo. Wakati huo, Petro alisema kwamba hakustahili kupokea hukumu na kuadibu kwa Mungu, na wakati utakapofika pia utakuwa tayari kuwafanya watu wote waione tabia ya Mungu ya haki kupitia kwako. Utakubali hukumu na kuadibu Kwake bila kusita, na hukumu, kuadibu na kulaani Kwake vitakuwa faraja kwako. Sasa, haikubaliki kabisa kwako kutojiandaa na ukweli. Bila ukweli, sio tu kwamba hutaweza kusimama imara katika siku zijazo, lakini pia huenda usiweze kuipitia kazi ya sasa. Ikiwa hii ndiyo hali, je, hutakuwa mmoja wa wale watakaotupwa nje na kuadhibiwa? Sasa hivi, hakujakuwa na ukweli wowote ambao umekujia na Nimekuruzuku katika kipengele chochote ambacho umepungukiwa; Nazungumza kutoka katika kila kipengele. Hamjapitia mateso mengi; ninyi huchukua tu kile kinachopatikana bila kulipia gharama ya aina yoyote, na, zaidi ya hayo, hamna matukio mliyopitia au utambuzi wenu halisi. Kwa hivyo, kile mnachoelewa si vimo vyenu halisi. Mmewekewa mipaka kwa ufahamu, maarifa na kuona, lakini hamjapata mavuno mengi. Ikiwa Singejali kuwahusu lakini Niwafanye mpitie matukio nyumbani kwenu wenyewe, mngekuwa mlishakimbia kurudi katika ulimwengu mkubwa wa zamani. Njia mtakayoitembea katika siku za usoni itakuwa njia ya mateso na mkiitembea kwa mafanikio njia hii ya sasa, basi mtakuwa na ushuhuda wakati ambapo mtapitia dhiki kubwa katika siku zijazo. Ikiwa unaelewa umuhimu wa maisha ya binadamu na umechukua njia inayofaas ya maisha ya mwanadamu na ikiwa katika siku za usoni utatii miundo Yake bila malalamiko yoyote au chaguo bila kujali jinsi Mungu anavyokushughulikia, na ikiwa hufanyi madai yoyote kwa Mungu, basi kwa njia hii wewe utakuwa mtu wa thamani. Sasa hivi, hujapitia dhiki, kwa hivyo unaweza kutii chochote bila kutofautisha. Unasema kwamba vyovyote ambavyo Mungu anaongoza, hivyo ni sawa, na kwamba utatii mipango Yake yote. Mungu akuadibu au kukulaani, utakuwa tayari kumridhisha. Hata hivyo, kile unachosema sasa hakiwakilishi kimo chako hasa. Kile ambacho uko tayari kufanya sasa hakiwezi kuonyesha kuwa unaweza kufuata hadi mwisho. Dhiki kubwa zitakapokujia au utakapopitia mateso kiasi au kushurutishwa au kupitia majaribu makubwa zaidi, basi hutaweza kusema maneno hayo. Ikiwa unaweza kuwa na ufahamu wa aina hiyo wakati huo na usimame imara, hiki kitakuwa kimo chako. Je, Petro alikuwa mtu wa aina gani wakati huo? Petro alisema: “Bwana, nitayatoa maisha yangu kwa ajili Yako. Ikiwa Unataka nife, nitakufa!” Hivyo ndivyo alivyokuwa akiomba wakati huo. Alisema pia: “Hata kama wengine hawakupendi, lazima nikupende hadi mwisho. Nitakufuata kila wakati.” Hivyo ndivyo alivyosema wakati huo, lakini punde majaribu yalipomjia, alivurugika na kulia. Ninyi nyote mnajua kuwa Petro alimkana Bwana mara tatu, sivyo? Kuna watu wengi ambao watalia na kuonyesha udhaifu wa kibinadamu wakati majaribu yatakapowapata. Wewe siye bwana wako mwenyewe. Katika hili, huwezi kujidhibiti. Labda leo wewe unaendelea vizuri sana, lakini hiyo ni kwa sababu una mazingira mazuri. Hilo likibadilika kesho, wewe utaonyesha waoga na kutokuwa na uwezo kwako, kustahili dharau na kutostahili kwako. “Ujasiri” wako utakuwa tayari umetoweka, na wakati mwingine unaweza kutupa kazi yako kando na uondoke. Hii inaonyesha kuwa kile ulichoelewa wakati huo hakikuwa kimo chako halisi. Mtu lazima aangalie kimo halisi cha mtu ili aone ikiwa anampenda Mungu kweli, ikiwa ana uwezo kweli wa kutii muundo wa Mungu na ikiwa ana uwezo wa kuweka nguvu zake zote katika kutimiza kile ambacho Mungu anahitaji; na ikiwa anabaki mtiifu kwa Mungu na anampa Mungu vitu vyote vilivyo bora zaidi, hata ikimaanisha kuyatoa maisha yake mwenyewe.

Lazima ukumbuke kwamba maneno haya sasa yamenenwa: Baadaye, utapitia dhiki kubwa na mateso makubwa! Kukamilishwa silo jambo rahisi au jepesi. Angalau lazima uwe na imani ya Ayubu, au hata labda imani kubwa kuliko yake. Unapaswa kujua kwamba majaribu katika siku zijazo yatakuwa makubwa kuliko majaribu ya Ayubu, na kwamba lazima bado upitie kuadibu kwa muda mrefu. Je, hili ni jambo rahisi? Ikiwa ubora wa tabia yako hauwezi kuboreshwa, ikiwa uwezo wako wa kuelewa umepungukiwa, na ikiwa unajua kidogo sana, basi wakati huo hutakuwa na ushuhuda wowote, lakini badala yake utakuwa kichekesho, kitu cha Shetani kuchezea. Ikiwa huwezi kushikilia maono sasa, basi huna msingi hata kidogo na katika siku zijazo utatupwa! Hakuna sehemu ya njia ambayo ni rahisi kutembea, kwa hivyo usiichukulie kwa urahisi. Lipime hili kwa uangalifu sasa na ufanye maandalizi ili uweze kuitembea vizuri sehemu ya mwisho ya njia hii. Hii ndiyo njia ambayo lazima itembewe katika siku zijazo, njia ambayo lazima watu wote waitembee. Lazima usikose kusikiliza maarifa haya; usifikirie kuwa kile Ninachokuambia si chote cha maana. Siku itakuja ambapo utayatumia vizuri—maneno Yangu hayawezi kunenwa bure. Huu ndio wakati wa wewe kujiandaa, wakati wa kuandaa njia kwa ajili ya siku zijazo. Unapaswa kuandaa njia ambayo unapaswa kuitembea baadaye; unapaswa kuwa na hofu na wasiwasi kuhusu jinsi utakavyoweza kusimama imara katika siku zijazo na ujiandae vizuri kwa ajili ya njia yako ya baadaye. Usiwe mlafi na mvivu! Lazima ufanye kila kitu uwezacho kabisa kutumia muda wako vizuri, ili uweze kupata kila kitu unachohitaji. Ninakupa kila kitu ili uweze kuelewa. Umeona kwa macho yako mwenyewe kwamba katika kipindi kisichozidi miaka mitatu, Nimenena mambo mengi sana na kufanya kazi nyingi sana. Sababu moja ya Mimi kufanya kazi kwa njia hii ni kwamba watu wamepungukiwa sana, na sababu nyingine ni kwamba muda ni mfupi sana; hakuwezi kuwa na kuchelewa zaidi. Unadhani kuwa watu lazima kwanza waweze kupata ufahamu kamili wa ndani kabla ya kushuhudia na kutumiwa—lakini hiyo haitakuwa polepole sana? Kwa hivyo, Nitalazimika kuandamana na wewe kwa muda gani? Ukinilazimisha niandamane na wewe hadi nitakapozeeka na niwe na mvi, hilo halitawezekana! Kwa kupitia dhiki kubwa zaidi, ufahamu wa kweli ndani ya watu wote utatimizwa. Hizi ni hatua za kazi. Punde unapofahamu kikamilifu maono yaliyoshirikiwa leo na ufikie kimo cha kweli, basi ugumu wowote utakaopitia katika siku zijazo hautakushinda na utaweza kuustahimili. Nitakapokuwa nimemaliza hatua hii ya mwisho ya kazi na kumaliza kunena maneno ya mwisho, katika siku zijazo watu watahitajika kutembea njia yao wenyewe. Hili litatimiza maneno yaliyonenwa hapo awali: Roho Mtakatifu ana agizo kwa kila mtu, na kazi ya kufanya ndani ya kila mtu. Katika siku zijazo, kila mtu ataitembea njia anayopaswa kuitembea, akiongozwa na Roho Mtakatifu. Ni nani atakayeweza kuwatunza wengine huku akipitia dhiki? Kila mtu ana mateso yake mwenyewe, na kila mmoja ana kimo chake mwenyewe. Hakuna kimo cha mtu yeyote kilicho sawa na cha mtu mwingine yeyote. Waume hawataweza kuwatunza wake zao, au wazazi kuwatunza watoto wao; hakuna mtu atakayeweza kumtunza mtu mwingine yeyote. Haitakuwa kama sasa, wakati ambapo kutunzana na kuhimiliana bado kunawezekana. Huo utakuwa wakati ambapo mtu wa kila aina amefunuliwa. Yaani, Mungu anapowapiga wachungaji, basi kondoo wa kundi watatawanyika, na wakati huo ninyi hamtakuwa na kiongozi yeyote wa kweli. Watu watakuwa wamegawanyika—haitakuwa kama sasa, wakati ambapo mnaweza kukusanyika pamoja kama mkutano. Katika siku zijazo, wale ambao hawana kazi ya Roho Mtakatifu wataonyesha sura zao za kweli. Waume watawasaliti wake zao, wake watawasaliti waume zao, watoto watawasaliti wazazi wao, na wazazi watawatesa watoto wao—moyo wa binadamu ni usioeleweka kabisa! Kile kinachoweza kufanywa ni kwa mtu kushikilia tu kile mtu alicho nacho, na kuitembea vizuri sehemu ya mwisho ya njia. Sasa hivi, ninyi hamwoni hili wazi wazi; nyinyi nyote ni wasiofikiria mambo yajayo. Si jambo rahisi kupitia hatua hii ya kazi kwa mafanikio.

Wakati wa dhiki hautarefushwa sana; kwa kweli, utadumu kwa chini ya mwaka mmoja. Ukidumu kwa mwaka mzima, hatua inayofuata ya kazi itacheleweshwa, na kimo cha watu hakitakuwa cha kutosha. Ukiwa mrefu sana, basi watu hatawaweza kuistahimili. Hata hivyo, kimo cha watu kina mapungufu yake. Baada ya kazi Yangu mwenyewe kukamilika, hatua inayofuata itakuwa kwa watu kuitembea njia wanayopaswa kuitembea. Kila mtu lazima aelewe ni njia gani anayopaswa kuitembea—ni njia na mchakato wa kuteseka, na pia ni njia ya kusafisha dhamira yako ya kumpenda Mungu. Unapaswa kuingia katika ukweli upi, ni ukweli gani unaopaswa kujazilia, jinsi unavyopaswa kupitia na unapaswa kuingia kutoka katika kipengele kipi—sharti uelewe mambo haya yote. Lazima ujiandae sasa. Dhiki itakapokujia, utakuwa umechelewa mno. Kila mtu lazima achukue mzigo kwa ajili ya maisha yake mwenyewe na usingojee kila wakati maonyo ya wengine au wengine kukuvuta na kukuelekeza kila wakati. Nimesema mengi sana lakini wewe bado hujui ni ukweli gani unaopaswa kuingia ndani au kujiandaa nao. Hili linaonyesha kuwa hujafanya jitihada kusoma maneno ya Mungu. Hubebi mzigo wowote kwa ajili ya maisha yako mwenyewe—hilo linawezaje kukubalika? Huelewi kile unachopaswa kuingia katika, huelewi kile unachopaswa kuelewa, na bado huna mwelekeo kuhusu ni njia gani ya baadaye unayopaswa kuchukua. Je, si wewe huna maana kabisa? Una maaana gani? Kile mnachofanya sasa ni kujenga na kuandaa njia zenu wenyewe. Lazima ujue ni nini ambacho watu wanapaswa kutimiza na lazima ujue kiwango cha mahitaji ya Mungu kwa wanadamu. Lazima uwe na ufahamu ufuatao: Haijalishi chochote, hata ingawa mimi ni mpotovu sana, lazima nifidie kasoro hizi mbele za Mungu. Kabla Mungu hajaniambia, sikuelewa, lakini sasa kwa kuwa Ameniambia na ninaelewa, lazima niharakishe kufidia upungufu huo, kuishi kwa kudhihirisha ubinadamu wa kawaida, na kuishi kwa kudhihirisha taswira inayoweza kuyaridhisha mapenzi ya Mungu. Hata kama siwezi kufikia kile ambacho Petro alifanya, angalau lazima niishi kwa kudhihirisha ubinadamu wa kawaida. Kwa njia hii, naweza kuuridhisha moyo wa Mungu.

Sehemu ya mwisho ya njia hii itaongezeka kutoka sasa hadi mwisho wa dhiki ya baadaye. Sehemu hii ya njia itakuwa wakati ambapo kimo cha kweli cha watu kinafichuliwa na vile vile kuonyesha ikiwa wana imani ya kweli au la. Kwa sababu sehemu hii ya njia itakuwa njia ngumu na yenye mabonde zaidi kuliko ile ambayo watu wameongozwa kwayo hapo awali, inaitwa “sehemu ya mwisho ya njia.” Ukweli ni kwamba siyo sehemu ya mwisho kabisa ya njia; hii ni kwa sababu baada ya kupitia dhiki, baadaye utapitia kazi ya kueneza injili na kutakuwa na sehemu ya watu ambao watapitia kazi ya kutumiwa. Kwa hivyo “sehemu ya mwisho ya njia” inazungumziwa tu kwa kurejelea dhiki ya kuwasafisha watu na kwa mazingira magumu. Kwenye sehemu hiyo ya njia ambayo ilitembewa zamani, Mimi binafsi nilikuongoza kwenye safari hiyo ya furaha, Nikikushika mkono kukufundisha, na kukulisha kutoka katika kinywa Changu mwenyewe. Ingawa umepitia hukumu na kuadibu mara nyingi, vimekuwa tu mapigo mepesi kuhusiana na wewe. Bila shaka, hilo limesababisha mitazamo yako juu ya imani yako kwa Mungu ibadilike kwa kiasi kikubwa; pia imesababisha tabia yako kuimarika kwa kiasi kikubwa, na imekuruhusu upate ufahamu mdogo kunihusu. Lakini Ninachosema ni kwamba wakati watu walikuwa wakiitembea sehemu hiyo ya njia hiyo, juhudi angalifu au gharama zilizolipwa na watu zilikuwa ndogo kiasi—ni Mimi ndimi nimekuongoza hadi pale ulipo leo. Hii ni kwa sababu Sikuhitaji ufanye kitu chochote; kwa kweli, matakwa Yangu kwako si ya juu hata kidogo—Ninakuruhusu tu uchukue kile kinachopatikana. Katika kipindi hiki cha muda Nimewapa mahitaji yenu bila kukoma na Sijawahi kuwawekea madai yasiyotimizika. Mmepitia kuadibu kwa kurudiwa, lakini hamjatimiza mahitaji Yangu ya asili. Mnarudi nyuma na mnakata tamaa, lakini Mimi sizingatii hili kwa sababu sasa ndio wakati wa kazi Yangu binafsi, na sichukulii “ibada” yako Kwangu kwa uzito sana. Lakini kwenye njia kuanzia sasa kuendelea, Sitafanya kazi au kunena tena na wakati utakapokuja Sitawaacha muendelee tena kwa njia ya uzembe namna hiyo. Nitawaruhusu mpate mafunzo mengi ya kujifunza na Sitawaruhusu mchukue kile kinachopatikana. Kimo halisi mlicho nacho leo lazima kifunuliwe. Ikiwa juhudi zenu za miaka mingi zimezaa matunda mwishowe au la itaonekana katika jinsi mnavyoitembea sehemu hii ya mwisho ya njia. Hapo zamani, mlidhani kwamba kumwamini Mungu lilikuwa jambo rahisi sana na hiyo ilikuwa kwa sababu Mungu hakuwa Akikutendea kwa ukali. Na sasa, je? Je, mnafikiri kwamba kumwamini Mungu ni rahisi? Je, bado mnahisi kuwa kumwamini Mungu kunawafanya muwe na furaha na wachangamfu kama watoto wanaocheza mitaani? Ni kweli kwamba ninyi ni kondoo; hata hivyo, lazima muweze kuitembea njia mnayopaswa kuitembea ili kulipa rehema ya Mungu, na kumpata kikamilifu Mungu mnayemwamini. Msijidhihaki na msijidanganye! Ikiwa unaweza kuendelea kwenye sehemu hii ya njia, basi utaweza kuona tukio ambalo halijawahi kuonekana hapo awali la kazi Yangu ya injili kuenea katika ulimwengu mzima, na utakuwa na bahati nzuri ya kuwa mwandani Wangu na kufanya wajibu wako katika kupanua kazi Yangu katika ulimwengu mzima. Wakati huo, utaendelea kwa furaha kuitembea njia unayopaswa kuitembea. Siku za usoni zitang’aa bila kikomo, lakini jambo la msingi sasa ni kuitembea vizuri sehemu hii ya mwisho ya njia. Lazima utafute na uandae jinsi ya kufanya hivi. Hili ndilo lazima ufanye sasa; hili ni suala muhimu sasa!

Iliyotangulia: Ni Lazima Muielewe Kazi—Msifuate kwa Rabsha!

Inayofuata: Unapaswa Kushughulikiaje Wito Wako wa Baadaye?

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp