Fumbo la Kupata Mwili (1)

Katika Enzi ya Neema, Yohana alimwandalia Yesu njia. Yohana hangefanya kazi ya Mungu Mwenyewe bali alitimiza tu wajibu wa binadamu. Ingawa Yohana alikuwa mtangulizi wa Bwana, hakuweza kumwakilisha Mungu; alikuwa tu mwanadamu aliyetumiwa na Roho Mtakatifu. Baada ya Yesu kubatizwa, Roho Mtakatifu alimshukia Yeye kama njiwa. Kisha Alianza kazi Yake, yaani, Alianza kutekeleza huduma ya Kristo. Hiyo ndiyo sababu Alichukua utambulisho wa Mungu, kwa maana Alitoka kwa Mungu. Haijalishi imani Yake ilikuwaje kabla ya haya—huenda wakati mwingine ilikuwa dhaifu, au wakati mwingine ilikuwa na nguvu—hayo yote yalikuwa sehemu ya maisha ya kawaida ya binadamu Aliyoishi kabla ya kutekeleza huduma Yake. Baada ya kubatizwa (yaani, kupakwa mafuta), nguvu na utukufu wa Mungu vilikuwa pamoja na Yeye mara moja, na hivyo Akaanza kutekeleza huduma Yake. Aliweza kufanya ishara na maajabu, kufanya miujiza, na Alikuwa na nguvu na mamlaka, kwa maana Alikuwa akifanya kazi kwa niaba ya Mungu Mwenyewe moja kwa moja; Alikuwa akifanya kazi ya Roho badala Yake na kuonyesha sauti ya Roho. Kwa hivyo, Alikuwa Mungu Mwenyewe; hili halina pingamizi. Yohana alikuwa mtu aliyetumiwa na Roho Mtakatifu. Hangeweza kumwakilisha Mungu, wala haikuwezekana kwake kumwakilisha Mungu. Kama angependa kufanya hivyo, Roho Mtakatifu hangeruhusu hilo, kwa maana hangeweza kufanya kazi ambayo Mungu Mwenyewe alikusudia kufanya. Pengine kulikuwa na mengi ndani yake yaliyokuwa ya mapenzi ya mwanadamu, au mikengeuko fulani; kwa vyovyote vile hangeweza kumwakilisha Mungu moja kwa moja. Makosa yake na upuuzi wake vilimwakilisha yeye mwenyewe peke yake, lakini kazi yake ilimwakilisha Roho Mtakatifu. Hata hivyo, huwezi kusema kwamba kila kipengele chake kilimwakilisha Mungu. Je, mambo yake yaliyopotoka yangemwakilisha Mungu pia? Ni kawaida kuwepo na mambo yaliyopotoka katika uwakilishi wa mwanadamu, lakini kukiwa na mkengeuko katika kumwakilisha Mungu, basi, je, hilo halitamfedhehesha Mungu? Je, hilo halitakuwa kufuru dhidi ya Roho Mtakatifu? Roho Mtakatifu hamruhusu mtu asimame mahali pa Mungu kwa urahisi, hata kama anainuliwa na wengine. Kama yeye si Mungu, hawezi kusimama imara mwishowe. Roho Mtakatifu hamruhusu mtu amwakilishe Mungu namna apendavyo! Kwa mfano, ni Roho Mtakatifu aliyemshuhudia Yohana na pia ni Roho Mtakatifu aliyemfunua kuwa yule wa kumwandalia Yesu njia, lakini kazi iliyofanywa juu yake na Roho Mtakatifu ilikuwa imepimwa vizuri. Kila alichotakiwa kufanya Yohana kilikuwa ni kuwa mwandaaji wa njia wa Yesu, kumwandalia njia. Yaani, Roho Mtakatifu aliunga mkono tu kazi yake ya kuandaa njia na kumruhusu tu afanye kazi kama hiyo—hakuruhusiwa kufanya kazi nyingine yoyote. Yohana alimwakilisha Eliya, na alimwakilisha nabii aliyeandaa njia. Roho Mtakatifu alimuunga mkono katika hili; mradi tu kazi yake ilikuwa kuandaa njia, Roho Mtakatifu alimuunga mkono. Hata hivyo, kama angedai kuwa Mungu Mwenyewe na angesema kwamba alikuwa amekuja kutimiza kazi ya ukombozi, Roho Mtakatifu angelazimika kumtia adabu. Haijalishi kazi ya Yohana ilikuwa kuu kiasi gani, na ingawa iliungwa mkono na Roho Mtakatifu, kazi yake haikuwa bila mipaka. Ni kweli kwamba Roho Mtakatifu aliunga mkono kazi yake, lakini nguvu aliyopewa wakati huo ilikomea tu katika kuandaa kwake njia. Hangeweza, hata kidogo, kufanya kazi nyingine yoyote, kwa maana alikuwa tu Yohana aliyeandaa njia, na wala hakuwa Yesu. Kwa hivyo, ushuhuda wa Roho Mtakatifu ni muhimu, lakini kazi ambayo Roho Mtakatifu anamruhusu mwanadamu kufanya ni muhimu hata zaidi. Je, Yohana hakuwa ameshuhudiwa kwa mvumo mkubwa sana wakati huo? Je, kazi yake haikuwa kuu pia? Lakini kazi aliyofanya haingeweza kuishinda ile ya Yesu, kwa maana hakuwa chochote zaidi ya mwanadamu aliyetumiwa na Roho Mtakatifu na hangeweza kumwakilisha Mungu moja kwa moja, na hivyo kazi aliyofanya ilikuwa na mipaka. Baada ya yeye kutimiza kazi ya kuandaa njia, Roho Mtakatifu hakuunga mkono tena ushuhuda wake, hakuna kazi mpya iliyomfuata, na yeye aliondoka wakati kazi ya Mungu Mwenyewe ilipoanza.

Kuna wengine ambao wamepagawa na mapepo waovu na wanapiga kelele kwa sauti kubwa wakisema, “Mimi ni mungu!” Lakini, mwishowe, wanafunuliwa, kwa maana wamekosea katika kile wanachowakilisha. Wanamwakilisha Shetani, na Roho Mtakatifu hawajali hata kidogo. Haijalishi unajiinua kiasi gani au unapiga kelele kwa nguvu kiasi gani, wewe bado ni kiumbe aliyeumbwa na ambaye ni wa Shetani. Mimi sipigi kelele kamwe Nikisema, “Mimi ni Mungu, Mimi ni Mwana mpendwa wa Mungu!” Lakini kazi Ninayofanya ni kazi ya Mungu. Je, Ninahitaji kupiga kelele? Hakuna haja ya kumwinua. Mungu hufanya kazi Yake Mwenyewe na hahitaji mwanadamu ampe hadhi au ampe cheo cha heshima: Kazi Yake inawakilisha utambulisho na hadhi Yake. Kabla ya ubatizo Wake, je, Yesu hakuwa Mungu Mwenyewe? Je, Yeye hakuwa mwili wa umwilisho wa Mungu? Hakika haiwezi kusemwa kwamba ilikuwa tu baada ya kushuhudiwa ndipo Alipokuwa Mwana wa pekee wa Mungu? Muda mrefu kabla ya kuanza kazi Yake, je, hakukuwa tayari na mwanadamu kwa jina la Yesu? Huwezi kutoa njia mpya au kumwakilisha Roho. Huwezi kuonyesha kazi ya Roho au maneno Anayonena. Huwezi kufanya kazi ya Mungu Mwenyewe, na ile ya Roho huwezi kuifanya. Hekima, ajabu, na kutoeleweka kwa Mungu, na ukamilifu wa tabia ambayo kwayo Mungu humwadibu mwanadamu—haya yote yanazidi uwezo wako wa kuyaonyesha. Kwa hivyo itakuwa bure kujaribu kujidai kuwa Mungu; utakuwa na jina tu na wala si kiini. Mungu Mwenyewe amekuja, lakini hakuna anayemtambua, hata hivyo Anaendelea na kazi Yake na Anafanya hivyo kwa kumwakilisha Roho. Iwe unamwita mwanadamu au Mungu, Bwana au Kristo, au umwite dada, haijalishi. Lakini kazi Anayofanya ni ile ya Roho na inaiwakilisha kazi ya Mungu Mwenyewe. Hajali kuhusu jina ambalo mwanadamu anamwita. Je, jina hilo linaweza kuamua kazi Yake? Bila kujali unamwita nini, kwa upande wa Mungu, Yeye ni mwili wa umwilisho wa Roho wa Mungu; Anamwakilisha Roho na Anakubaliwa na Roho. Ikiwa huwezi kutoa njia ya enzi mpya, au kuitamatisha enzi ya kale, au kuileta enzi mpya, au kufanya kazi mpya, basi huwezi kuitwa Mungu!

Hata mtu anayetumiwa na Roho Mtakatifu hawezi kumwakilisha Mungu Mwenyewe. Hili si kusema tu kwamba mtu kama huyo hawezi kumwakilisha Mungu, bali pia kwamba kazi anayofanya haiwezi kumwakilisha Mungu moja kwa moja. Yaani, uzoefu wa binadamu hauwezi kuwekwa moja kwa moja ndani ya usimamizi wa Mungu, na hauwezi kuwakilisha usimamizi wa Mungu. Kazi ambayo Mungu Mwenyewe anafanya ni kwa ukamilifu kazi Anayokusudia kufanya katika mpango Wake wa usimamizi na inahusiana na usimamizi mkuu. Kazi inayofanywa na watu inajumuisha kutoa uzoefu wao binafsi. Inajumuisha kupata njia mpya ya uzoefu kando na zile zilizokanyagwa na wale waliotangulia, na kuwaelekeza ndugu zao wakiwa chini ya mwongozo wa Roho Mtakatifu. Kile ambacho watu hawa wanatoa ni uzoefu wao binafsi au maandishi ya kiroho ya watu wa kiroho. Ingawa watu hawa wanatumiwa na Roho Mtakatifu, kazi wanayofanya haina uhusiano na kazi kuu ya usimamizi katika mpango wa miaka elfu sita. Wao ni wale tu ambao wameinuliwa na Roho Mtakatifu katika vipindi tofauti ili kuwaongoza watu katika mkondo wa Roho Mtakatifu, hadi kazi wanazoweza kutekeleza zifikie kikomo au hadi maisha yao yafikie mwisho. Kazi wanayofanya ni kuandaa tu njia inayofaa kwa ajili ya Mungu Mwenyewe au kuendeleza kipengele fulani cha usimamizi wa Mungu Mwenyewe duniani. Wao wenyewe, watu hawa hawawezi kufanya kazi kuu zaidi ya usimamizi Wake, wala hawawezi kufungua njia mpya za kutokea, sembuse yeyote kati yao kuweza kuhitimisha kazi yote ya Mungu kutoka katika enzi ya awali. Kwa hivyo, kazi wanayofanya inamwakilisha tu kiumbe aliyeumbwa akitekeleza kazi yake na haiwezi kumwakilisha Mungu Mwenyewe akitekeleza huduma Yake. Hii ni kwa sababu kazi wanayofanya ni tofauti na ile inayofanywa na Mungu Mwenyewe. Kazi ya kuanzisha enzi mpya si jambo ambalo linaweza kufanywa na mwanadamu katika nafasi ya Mungu. Haiwezi kufanywa na mwingine yeyote isipokuwa Mungu Mwenyewe. Kazi yote inayofanywa na mwanadamu inajumuisha kutekeleza wajibu wake kama kiumbe aliyeumbwa na inafanywa anapoguswa au kutiwa nuru na Roho Mtakatifu. Mwongozo ambao watu hawa wanatoa unajumuisha kabisa kumwonyesha mwanadamu njia ya utendaji katika maisha ya kila siku na jinsi anavyopaswa kutenda kulingana na nia za Mungu. Kazi ya mwanadamu haihusishi usimamizi wa Mungu wala haiwakilishi kazi ya Roho. Kwa mfano, kazi ya Witness Lee na Watchman Nee ilikuwa ni kuongoza njia. Iwe njia hiyo ni mpya au ya zamani, kazi hiyo ilijengwa juu ya kanuni ya kubaki ndani ya Biblia. Iwe ilikuwa ni kurejesha kanisa la mtaa au kujenga kanisa la mtaa, kazi yao ilihusiana na kuanzisha makanisa. Kazi waliyofanya iliendeleza kazi ambayo Yesu na mitume Wake walikuwa wameiacha bila kukamilika au hawakuwa wameiendeleza zaidi katika Enzi ya Neema. Kile walichofanya katika kazi yao kilikuwa ni kurejesha kile ambacho Yesu, katika kazi Yake ya wakati huo, Alitaka kutoka kwa vizazi vilivyokuja baada Yake, kama vile kufunika vichwa vyao, kupokea ubatizo, kumega mkate, au kunywa divai. Inaweza kusemwa kwamba kazi yao ilikuwa ni kushikamana na Biblia na kutafuta njia ndani ya Biblia. Hawakufanya maendeleo yoyote mapya ya aina yoyote. Kwa hivyo, mtu anaweza kuona katika kazi yao tu ugunduzi wa njia mpya ndani ya Biblia, pamoja na matendo bora na halisi zaidi. Lakini mtu hawezi kupata katika kazi yao nia za sasa za Mungu, sembuse kupata kazi mpya ambayo Mungu katika siku za mwisho Anakusudia kufanya. Hii ni kwa sababu njia waliyotembea ilikuwa bado ni ya zamani—hakukuwa na kufanywa upya na hakukuwa na maendeleo. Waliendelea kushikilia ukweli wa kusulubiwa kwa Yesu, kuzingatia desturi ya kuwaomba watu watubu na kukiri dhambi zao, kushikamana na misemo kwamba yule anayevumilia hadi mwisho ataokolewa na kwamba mwanamume ni kichwa cha mwanamke, na mwanamke lazima amtii mume wake, na hata zaidi kwa wazo la kitamaduni kwamba akina dada hawawezi kuhubiri, bali kutii tu. Kama namna hiyo ya uongozi ingeendelea kuzingatiwa, Roho Mtakatifu hangeweza kamwe kutekeleza kazi mpya, kuwaweka watu huru kutokana na kanuni, au kuwaongoza katika hali ya uhuru na uzuri. Kwa hivyo, hatua hii ya kazi, ambayo inabadilisha enzi, inahitaji kwamba Mungu Mwenyewe afanye kazi na Azungumze; la sivyo hakuna mwanadamu anayeweza kufanya hivyo badala Yake. Kufikia sasa, kazi yote ya Roho Mtakatifu nje ya mkondo huu imesimama, na wale waliotumiwa na Roho Mtakatifu wamepoteza mwelekeo wao. Kwa hivyo, kwa kuwa kazi ya watu wanaotumiwa na Roho Mtakatifu ni tofauti na kazi inayofanywa na Mungu Mwenyewe, utambulisho wao na wale wanaowawakilisha ni tofauti vivyo hivyo. Hii ni kwa sababu kazi ambayo Roho Mtakatifu anakusudia kufanya ni tofauti, na kwa sababu hii wale wote ambao kwa namna sawa wanafanya kazi wana utambulisho na hadhi tofauti. Watu wanaotumiwa na Roho Mtakatifu wanaweza pia kufanya kazi fulani ambayo ni mpya na wanaweza pia kuondoa kazi fulani iliyofanywa katika enzi iliyotangulia, lakini kile wanachofanya hakiwezi kuonyesha tabia na nia za Mungu katika enzi mpya. Wanafanya kazi ili kuondoa tu kazi ya enzi iliyotangulia, na si ili kufanya kazi mpya kwa madhumuni ya kuwakilisha moja kwa moja tabia ya Mungu Mwenyewe. Hivyo, haijalishi ni matendo mangapi yaliyopitwa na wakati wanayokomesha au ni matendo mangapi mapya wanayoanzisha, bado wanawakilisha mwanadamu na viumbe walioumbwa. Hata hivyo, Mungu Mwenyewe anapotekeleza kazi, Hatangazi waziwazi kukomeshwa kwa matendo ya enzi ya kale au kutangaza moja kwa moja kuanzishwa kwa enzi mpya. Yeye hufanya kazi Yake moja kwa moja na waziwazi. Yeye ni wa moja kwa moja katika kutekeleza kazi Anayokusudia kufanya; yaani, Yeye huonyesha moja kwa moja kazi ambayo Ameileta, anafanya kazi Yake moja kwa moja kama ilivyokusudiwa hapo awali, akionyesha nafsi Yake na tabia Yake. Jinsi mwanadamu anavyoiona, tabia Yake na vivyo hivyo kazi Yake hutofautiana na zile za enzi zilizopita. Hata hivyo, kutoka katika mtazamo wa Mungu Mwenyewe, huu ni mwendelezo tu na maendeleo zaidi ya kazi Yake. Mungu Mwenyewe anapofanya kazi, Yeye huonyesha neno Lake na kuleta kazi mpya moja kwa moja. Kinyume chake, mwanadamu anapofanya kazi, ni kupitia tafakari ya kina na utafiti, au ni upanuzi wa maarifa na mpangilio wa utendaji uliojengwa juu ya kazi ya wengine. Yaani, kiini cha kazi inayofanywa na mwanadamu ni kufuata utaratibu uliowekwa na “kutembea njia za zamani kwa viatu vipya.” Hii inamaanisha kwamba hata njia inayotembewa na watu wanaotumiwa na Roho Mtakatifu imejengwa juu ya ile iliyoanzishwa na Mungu Mwenyewe. Kwa hivyo, baada ya yote, mwanadamu angali mwanadamu, na Mungu angali Mungu.

Yohana alizaliwa kwa ahadi, kama vile Isaka alivyozaliwa kwa Abrahamu. Alimwandalia Yesu njia na alifanya kazi nyingi, lakini hakuwa Mungu. Badala yake, alikuwa mmoja wa manabii, kwa sababu alimwandalia Yesu njia tu. Kazi yake ilikuwa kuu pia, na ilikuwa tu baada ya yeye kuandaa njia ndipo Yesu alianza kazi Yake rasmi. Kimsingi, alimtumikia Yesu tu, na kazi aliyofanya ilikuwa katika huduma kwa kazi ya Yesu. Baada ya kumaliza kuandaa njia, Yesu alianza kazi Yake, kazi iliyokuwa mpya zaidi, thabiti zaidi, na ya kina zaidi. Yohana alifanya tu sehemu ya mwanzo ya kazi; sehemu kubwa ya kazi mpya ilifanywa na Yesu. Yohana alifanya kazi mpya pia, lakini hakuwa yule aliyeanzisha enzi mpya. Yohana alizaliwa kwa ahadi, na jina lake lilitolewa na malaika. Wakati huo, wengine walitaka kumpa jina la baba yake Zakaria, lakini mama yake alizungumza, akisema, “Mtoto huyu hawezi kuitwa kwa jina hilo. Anapaswa kuitwa Yohana.” Haya yote yalikuwa kwa maagizo ya Roho Mtakatifu. Yesu pia alipewa jina kwa maagizo ya Roho Mtakatifu, Alizaliwa kwa Roho Mtakatifu, na Aliahidiwa na Roho Mtakatifu. Yesu alikuwa Mungu, Kristo, na Mwana wa Adamu. Lakini, kazi ya Yohana ikiwa kuu pia, kwa nini hakuitwa Mungu? Je, tofauti hasa kati ya kazi iliyofanywa na Yesu na ile iliyofanywa na Yohana ilikuwa nini? Je, sababu pekee ilikuwa kwamba Yohana ndiye aliyeandaa njia kwa ajili ya Yesu? Au kwa sababu hili lilikuwa limeamuriwa kabla na Mungu? Ingawa Yohana pia alisema, “Ninyi tubuni: kwa kuwa ufalme wa mbinguni uko karibu,” na yeye pia alihubiri injili ya ufalme wa mbinguni, kazi yake haikuendelezwa zaidi na ilijumuisha tu mwanzo. Kinyume chake, Yesu alianzisha enzi mpya na pia kuikomesha ile ya kale, lakini pia Alitimiza sheria ya Agano la Kale. Kazi Aliyofanya ilikuwa kuu kuliko ile ya Yohana, na zaidi ya hayo Alikuja kuwakomboa binadamu wote—Alitekeleza hatua hiyo ya kazi. Kuhusu Yohana, yeye aliandaa njia tu. Ingawa kazi yake ilikuwa kuu, maneno yake mengi, na wale wanafunzi waliomfuata walikuwa wengi, kazi yake haikufanya chochote zaidi ya kumletea mwanadamu mwanzo mpya. Mwanadamu hakupokea kamwe kutoka kwake uzima, njia, au ukweli wa kina zaidi, wala mwanadamu hakupata kupitia kwake uelewa wa nia za Mungu. Yohana alikuwa nabii mkuu (Eliya) aliyefungua uwanja kwa ajili ya kazi ya Yesu na kuwatayarisha watu wanaofaa; alikuwa mtangulizi wa Enzi ya Neema. Mambo kama haya hayawezi kamwe kutambuliwa kwa kuchunguza sura zao za kawaida za kibinadamu. Hili linafaa hata zaidi kwa kuwa Yohana pia alifanya kazi ambayo ilikuwa ya kiwango kikubwa sana na, zaidi ya hayo, aliahidiwa na Roho Mtakatifu, na kazi yake iliungwa mkono na Roho Mtakatifu. Hili likiwa hivi, ni kupitia tu kazi waliyofanya ndiyo mtu anaweza kutofautisha kati ya utambulisho wao, kwa maana hakuna njia ya kutambua kiini cha mtu kutokana na sura yake ya nje, wala hakuna namna yoyote kwa mwanadamu kuhakikisha ushuhuda wa Roho Mtakatifu ni nini. Kazi iliyofanywa na Yohana na ile iliyofanywa na Yesu hazikufanana na zilikuwa za asili tofauti. Mtu anapaswa kubainisha kama Yohana alikuwa Mungu au la kulingana na hili. Kazi ya Yesu ilikuwa kuanzisha, kuendeleza, kuhitimisha, na kukamilisha. Alitekeleza kila moja ya hatua hizi, ilhali kazi ya Yohana haikuwa zaidi ya kuanzisha. Hapo mwanzo, Yesu alihubiri injili na akahubiri njia ya toba, na kisha Akaendelea kumbatiza mwanadamu, kuponya wagonjwa, na kutoa mapepo. Mwishowe, Alimkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na kukamilisha kazi Yake ya enzi nzima. Pia Alizunguka kila mahali, Akimhubiria mwanadamu na kuhubiri injili ya ufalme wa mbinguni. Katika hili Yeye na Yohana walifanana, tofauti ikiwa kwamba Yesu Alianzisha enzi mpya na kumletea mwanadamu Enzi ya Neema. Kutoka kinywani Mwake lilitoka neno kuhusu kile ambacho mwanadamu anapaswa kutenda na njia ambayo mwanadamu anapaswa kufuata katika Enzi ya Neema, na mwishowe, Aliitimiza kazi ya ukombozi. Yohana hangeweza kutekeleza kazi hii. Na hivyo ni Yesu ndiye Aliyefanya kazi ya Mungu Mwenyewe, na ni Yeye ndiye Mungu Mwenyewe, na anayemwakilisha Mungu moja kwa moja. Dhana za mwanadamu zinasema kwamba wale wote waliozaliwa kwa ahadi, waliozaliwa kwa Roho, wanaoungwa mkono na Roho Mtakatifu, na wanaofungua njia mpya za kutokea ni Mungu. Kulingana na hoja hii, Yohana pia angekuwa Mungu, na Musa, Abrahamu, na Daudi..., wao pia wangekuwa Mungu. Je, huu si mzaha mkubwa?

Kabla ya kutekeleza huduma Yake, Yesu pia Alikuwa tu mtu wa kawaida aliyetenda kulingana na chochote ambacho Roho Mtakatifu alifanya. Bila kujali kama Alifahamu utambulisho Wake mwenyewe wakati huo, Alitii yote yaliyotoka kwa Mungu. Roho Mtakatifu hakufunua kamwe utambulisho Wake kabla ya huduma Yake kuanza. Ilikuwa tu baada ya Yeye kuanza huduma Yake ndipo Alipokomesha kanuni hizo na sheria hizo, na haikuwa mpaka Alipoanza rasmi kutekeleza huduma Yake ndipo maneno Yake yakajaa mamlaka na kuwa na nguvu. Ni baada tu ya kuanza huduma Yake ndipo kazi Yake ya kuleta enzi mpya ilipoanza. Kabla ya hili, Roho Mtakatifu aliendelea kujificha ndani Yake kwa miaka 29, wakati ambapo Alimwakilisha mtu tu na hakuwa na utambulisho wa Mungu. Kazi ya Mungu ilianza kwa Yeye kufanya kazi na kutekeleza huduma Yake, Alifanya kazi Yake kulingana na mpango Wake wa ndani bila kujali mwanadamu alijua kiasi gani kumhusu Yeye, na kazi Aliyofanya ilikuwa uwakilishi wa moja kwa moja wa Mungu Mwenyewe. Wakati huo, Yesu Aliwauliza wale waliokuwa karibu na Yeye, “Ninyi mnasema Mimi ni nani?” Wakajibu, “Wewe ndiwe mkuu zaidi wa manabii na tabibu wetu bora sana.” Na wengine wakajibu, “Wewe ni kuhani wetu mkuu,” na kadhalika. Majibu ya kila aina yalitolewa, wengine hata wakisema kwamba Alikuwa Yohana, kwamba Alikuwa Eliya. Kisha Yesu akamgeukia Simoni Petro na kuuliza, “Wewe unasema Mimi ni nani?” Petro akajibu, “Wewe ni Kristo, Mwanawe Mungu aliye hai”. Tangu wakati huo kuendelea, watu wakafahamu kwamba Yeye alikuwa Mungu. Utambulisho Wake ulipotambulishwa, ni Petro ndiye aliyekuwa wa kwanza kufahamu hili na ni kutoka kinywani mwake ndipo liliposemwa. Kisha Yesu akasema, “Kile ulichosema hakikufunuliwa na mwili na damu, bali na Baba Yangu.” Baada ya ubatizo Wake, iwe wengine walijua kuhusu hili au la, kazi Aliyofanya ilikuwa kwa niaba ya Mungu. Alikuja ili kutekeleza kazi Yake, si ili kufunua utambulisho Wake. Ilikuwa tu baada ya Petro kuzungumza kuhusu hilo ndipo utambulisho Wake ulipojulikana wazi. Uwe ulikuwa unajua kwamba Alikuwa Mungu Mwenyewe au la, wakati ulipofika, Alianza kazi Yake. Na uwe ulijua kuhusu hilo au la, Yeye aliendelea na kazi Yake vivyo hivyo. Hata kama ungeikana, bado Angetekeleza kazi Yake na Angeifanya wakati ulipofika wa kufanya hivyo. Alikuja ili kufanya kazi Yake na kutekeleza huduma Yake, si ili mwanadamu apate kuujua mwili Wake, bali ili mwanadamu aelewe kazi Yake. Ikiwa umeshindwa kutambua kwamba hatua ya kazi siku ya sasa ni kazi ya Mungu Mwenyewe, ni kwa sababu unakosa maono. Hata hivyo, huwezi kukana hatua hii ya kazi; kushindwa kwako kuitambua hakuthibitishi kwamba Roho Mtakatifu hafanyi kazi au kwamba kazi Yake si sahihi. Kuna wale ambao hata hulinganisha kazi ya sasa na ile ya Yesu katika Biblia na kutumia tofauti zozote kukana hatua hii ya kazi. Je, huku si kuwa kipofu kupindukia? Mambo yaliyoandikwa katika Biblia yana mipaka; hayawezi kuwakilisha kazi ya Mungu kwa ukamilifu wake. Injili Nne zina sura chini ya mia moja kwa jumla, ambamo mmeandikwa idadi yenye kikomo ya matukio, kama vile Yesu kulaani mtini, Petro kumkana Bwana mara tatu, Yesu kuwatokea wanafunzi baada ya kusulubiwa na kufufuka Kwake, kufundisha kuhusu kufunga, kufundisha kuhusu maombi, kufundisha kuhusu talaka, kuzaliwa na nasaba ya Yesu, Yesu kuwateua wanafunzi, na kadhalika. Hata hivyo, mwanadamu huyathamini mambo hayo kama hazina, hata akiilinganisha kazi ya leo nayo. Hata anaamini kwamba kazi yote ambayo Yesu alifanya katika maisha Yake ilikuwa kiasi tu, kana kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kufanya kiasi hiki tu na si zaidi. Je, huu si upuuzi?

Muda ambao Yesu alikuwa nao duniani ulikuwa miaka thelathini na mitatu na nusu, yaani, Aliishi duniani kwa miaka thelathini na mitatu na nusu. Ni miaka mitatu na nusu pekee ya muda huu ndiyo iliyotumiwa katika kutekeleza huduma Yake; muda uliosalia Aliishi tu maisha ya kawaida ya binadamu. Hapo mwanzo, Alihudhuria ibada katika sinagogi na hapo Alisikiliza ufafanuzi wa makuhani wa Maandiko na mahubiri ya wengine. Alipata maarifa mengi ya Biblia: Hakuzaliwa na maarifa kama hayo, na Aliyapata tu kupitia kusoma na kusikiliza. Imeandikwa wazi katika Biblia kwamba Aliwauliza walimu maswali katika sinagogi akiwa na umri wa miaka kumi na miwili: Unabii wa manabii wa kale unahusu nini? Vipi kuhusu sheria za Musa? Na Agano la Kale? Na vipi kuhusu mwanadamu kumtumikia Mungu na kuvaa mavazi ya kikuhani hekaluni? … Aliuliza maswali mengi, kwa maana Hakuwa na maarifa wala uelewa. Ingawa mimba Yake ilitungwa na Roho Mtakatifu, Alizaliwa kama mtu wa kawaida kabisa; licha ya vipengele fulani maalum vya hulka Yake, Yeye bado Alikuwa mtu wa kawaida. Hekima Yake ilikua kwa kuendelea kulingana na kimo Chake na umri Wake, na Alipitia hatua za maisha ya mtu wa kawaida. Katika mawazo ya watu, Yesu Hakupitia utoto na wala ujana; Alianza kuishi maisha ya mtu mwenye umri wa miaka thelathini mara tu Alipozaliwa, na Alisulubiwa baada ya kukamilisha kazi Yake. Pengine Hakupitia hatua katika maisha ya mtu wa kawaida; Hakula wala kushirikiana na watu wengine, na haikuwa rahisi kwa watu kumwona. Pengine Alikuwa mtu wa ajabu, ambaye angewatisha wale waliomwona, kwa sababu Yeye alikuwa Mungu. Watu wanaamini kwamba Mungu anayekuja katika mwili hakika Haishi kama mtu wa kawaida anavyoishi; wanaamini kwamba Yeye ni msafi bila kulazimika kupiga mswaki au kunawa uso Wake, kwa sababu Yeye ni mtu mtakatifu. Je, hizi si dhana za mwanadamu tupu? Biblia haina rekodi ya maisha ya Yesu katika ubinadamu, bali ya kazi Yake tu, lakini hili halithibitishi kwamba Hakuwa na ubinadamu wa kawaida au kwamba Hakuishi maisha ya kawaida ya binadamu kabla ya umri wa miaka thelathini. Alianza kazi Yake rasmi Akiwa na umri wa miaka 29, lakini huwezi kufutilia mbali maisha Yake yote katika ubinadamu kabla ya umri huo. Biblia iliacha tu kipindi hicho kutoka kwenye rekodi zake; kwa kuwa yalikuwa maisha Yake katika ubinadamu wa kawaida na si kipindi cha kazi Yake ya kiungu, hakukuwa na haja ya kukiandika. Kwa maana kabla ya ubatizo wa Yesu, Roho Mtakatifu hakufanya kazi moja kwa moja, bali Alimdumisha tu katika maisha Yake kama mtu wa kawaida hadi siku ambayo Yesu alipaswa kutekeleza huduma Yake. Ingawa Alikuwa Mungu mwenye mwili, Alipitia mchakato wa kukomaa kama mtu wa kawaida anavyofanya. Mchakato huu wa kukomaa uliachwa nje ya Biblia. Uliachwa kwa sababu haungeweza kutoa msaada mkubwa kwa ukuaji wa mwanadamu katika maisha. Kipindi kabla ya ubatizo Wake kilikuwa kipindi kilichofichwa, ambacho ndani yake Hakufanya ishara na maajabu. Ni kazi ya Yesu tu baada ya ubatizo Wake ndiyo iliyokuwa ukombozi wa binadamu—tele na iliyojaa neema, ukweli, na rehema na upendo. Mwanzo wa kazi hii ulikuwa hasa pia kuanza kwa Enzi ya Neema; kwa sababu hii, uliandikwa na kupitishwa hadi sasa. Ulikuwa ni kufungua njia ya kutokea na kukamilisha yote kwa wale walio katika Enzi ya Neema kutembea katika njia ya Enzi ya Neema na njia ya msalaba. Ingawa inatokana na rekodi zilizoandikwa na mwanadamu, kila kitu ni ukweli, isipokuwa kwamba makosa madogo yanapatikana hapa na pale katika sehemu mbalimbali. Hata hivyo, rekodi hizi haziwezi kusemwa kuwa si za kweli. Mambo yaliyoandikwa ni ya uhakika kabisa, ni katika kuyaandika tu ndipo watu walipofanya makosa. Kuna wengine ambao watasema kwamba, kama Yesu ndiye aliyekuwa na ubinadamu wa kawaida na wa desturi, inawezekanaje kwamba Alikuwa na uwezo wa kufanya ishara na maajabu? Siku arobaini za vishawishi ambazo Yesu alipitia zilikuwa ishara ya kimuujiza, ambayo mtu wa kawaida hangeweza kuitimiza. Siku Zake arobaini za vishawishi zilikuwa katika asili ya kazi ya Roho Mtakatifu; basi mtu anawezaje kusema kwamba hakukuwa na chembe ya mambo yasiyo ya kawaida ndani Yake? Uwezo Wake wa kufanya ishara na maajabu hauthibitishi kwamba Alikuwa mtu anayepita mipaka ya binadamu na si wa kawaida; ni kwamba tu Roho Mtakatifu alifanya kazi ndani ya mtu wa kawaida kama Yeye, na hivyo kumwezesha kufanya miujiza na kufanya kazi kuu zaidi. Kabla ya Yesu kutekeleza huduma Yake, au kama Biblia inavyosema, kabla ya Roho Mtakatifu kushuka juu Yake, Yesu alikuwa tu mtu wa kawaida na Hakuwa na mambo yasiyo ya kawaida kwa namna yoyote. Roho Mtakatifu aliposhuka juu Yake, yaani, Alipoanza utekelezaji wa huduma Yake, Alijazwa na mambo yasiyo ya kawaida. Kwa njia hii, mwanadamu anafikia kuamini kwamba mwili wa Mungu hauna ubinadamu wa kawaida; zaidi ya hayo, anafikiri kimakosa kwamba Mungu mwenye mwili ana uungu tu, na si ubinadamu. Hakika, Mungu anapokuja duniani kufanya kazi Yake, yote ambayo watu wanaona ni matukio yasiyo ya kawaida. Yote wanayotazama kwa macho yao na yote wanayosikia kwa masikio yao yote ni yasiyo ya kawaida, kwa maana kazi Yake na maneno Yake hayaeleweki na hayafikiki kwao. Kitu cha mbinguni kikiletwa duniani, kinawezaje kuwa kingine kando na kisicho cha dunia hii? Mafumbo ya ufalme wa mbinguni yanapoletwa duniani, mafumbo ambayo hayaeleweki na yasiyoweza kueleweka kwa mwanadamu, ambayo ni ya ajabu na yenye hekima mno—je, si yote ni yasiyo ya dunia hii? Hata hivyo, unapaswa kujua, haijalishi hayo si ya dunia hii kiasi gani, kila kitu kinatekelezwa ndani ya ubinadamu Wake wa kawaida. Mwili wa Mungu una ubinadamu; Asingekuwa nao, basi Asingekuwa mwili wa Mungu. Yesu alifanya miujiza mingi sana katika wakati Wake. Kile ambacho Waisraeli wa wakati huo waliona kilijaa mambo yasiyo ya dunia hii; waliwaona malaika na wajumbe, na walisikia sauti ya Yehova. Je, haya yote hayakuwa mambo yasiyo ya dunia hii? Hakika, leo kuna baadhi ya pepo waovu ambao wanampotosha mwanadamu kwa mambo yasiyo ya dunia hii; hicho si kingine ila ni uigaji kwa upande wao, ili kumpotosha mwanadamu kupitia kazi ambayo haifanywi na Roho Mtakatifu kwa sasa. Watu wengi hufanya miujiza na kuponya wagonjwa na kutoa mapepo; haya si mengine ila ni kazi ya pepo waovu, kwa maana Roho Mtakatifu hafanyi tena kazi kama hiyo katika siku ya leo, na wale wote ambao wameiga kazi ya Roho Mtakatifu kuanzia wakati huo na kuendelea ni pepo waovu kweli. Kazi yote iliyotekelezwa katika Israeli wakati huo ilikuwa kazi ya asili isiyo ya kawaida, ingawa Roho Mtakatifu sasa hafanyi kazi kwa namna hiyo, na kazi yoyote kama hiyo sasa ni uigaji na udanganyifu wa Shetani na usumbufu wake. Lakini huwezi kusema kwamba chochote kisicho cha kawaida kinatoka kwa mapepo waovu—hili lingetegemea enzi ya kazi ya Mungu. Fikiria kazi inayofanywa na Mungu mwenye mwili katika wakati wa sasa: Ni kipengele chake kipi kisicho cha dunia hii? Maneno Yake hayaeleweki na hayafikiki kwako, na kazi Anayofanya haiwezi kufanywa na mwanadamu yeyote. Kile Anachoelewa mwanadamu hana njia ya kukielewa, na kuhusu maarifa Yake, mwanadamu hajui yanatoka wapi. Kuna wengine wanaosema, “Mimi ni wa kawaida kwa namna sawa na Wewe, lakini inakuwaje kwamba mimi sijui kile Unachojua? Mimi ni mzee zaidi na mwenye uzoefu mwingi, lakini Wewe unawezaje kujua kile ambacho mimi sijui?” Haya yote, kwa upande wa mwanadamu, ni mambo ambayo mwanadamu hana njia ya kuyafikia. Kisha kuna wale wanaosema, “Hakuna anayejua kuhusu kazi iliyotekelezwa katika Israeli, na hata wafafanuzi wa Biblia hawawezi kutoa maelezo yoyote; inakuwaje Wewe unajua?” Je, haya yote si mambo ambayo si ya dunia hii? Hana uzoefu wa maajabu, hata hivyo Anajua yote; Ananena na kuonyesha ukweli kwa urahisi mkubwa. Je, hili si jambo lisilo la dunia hii? Kazi Yake inazidi kile ambacho mwili unaweza kufikia. Haifikiki kwa mawazo ya mwanadamu yeyote aliye na mwili wa nyama na haifikiriki kabisa kwa busara ya akili ya mwanadamu. Ingawa Hajawahi kusoma Biblia, Anaelewa kazi ya Mungu katika Israeli. Na ingawa Anasimama duniani Anapozungumza, Anazungumza kuhusu mafumbo ya mbingu ya tatu. Mwanadamu anaposoma maneno haya, atahisi: “Je, hii si lugha ya mbingu ya tatu?” Je, haya yote si mambo yanayozidi kile ambacho mtu wa kawaida ana uwezo wa kutimiza? Wakati huo, Yesu alipopitia siku arobaini za kufunga, je, hilo halikuwa la dunia hii? Ukisema kwamba siku arobaini za kufunga ni jambo lisilo la dunia hii katika visa vyote, kitendo cha pepo waovu, basi je, hujamhukumu Yesu? Kabla ya kutekeleza huduma Yake, Yesu alikuwa kama mtu wa kawaida. Yeye pia Alienda shuleni; ni vipi vinginevyo Angeweza kujifunza kusoma na kuandika? Mungu alipopata mwili, Roho alijificha ndani ya mwili. Hata hivyo, Akiwa mtu wa kawaida, ilikuwa lazima Kwake kupitia mchakato wa ukuaji na kukomaa, na haikuwa mpaka uwezo Wake wa utambuzi ulipokomaa, na Akaweza kutekeleza mambo, ndipo Angeweza kuchukuliwa kuwa mtu wa kawaida. Ilikuwa tu baada ya ubinadamu Wake kukomaa ndipo Angeweza kutekeleza huduma Yake. Angewezaje kutekeleza huduma Yake ilhali ubinadamu Wake wa kawaida ulikuwa bado haujakomaa na busara Yake haikuwa timamu? Hakika Hangeweza kutarajiwa kutekeleza huduma Yake akiwa na umri wa miaka sita au saba! Kwa nini Mungu hakujidhihirisha Mwenyewe waziwazi Alipopata mwili kwa mara ya kwanza? Ilikuwa kwa sababu ubinadamu wa mwili Wake ulikuwa bado haujakomaa; michakato ya utambuzi ya mwili Wake, pamoja na ubinadamu wa kawaida wa mwili huu, haikuwa katika milki Yake kikamilifu. Kwa sababu hii, ilikuwa lazima kabisa Kwake kuwa na ubinadamu wa kawaida na maarifa ya kawaida ya ubinadamu wa kawaida—hadi kufikia hatua ambapo Alikuwa ametayarishwa vya kutosha kuchukua kazi Yake katika mwili—kabla ya kuanza kazi Yake. Ikiwa Hangekuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo, ingekuwa lazima Kwake kuendelea kukua na kukomaa. Yesu angeanza kazi Yake akiwa na umri wa miaka saba au minane, je, mwanadamu asingemwona kama wa kimuujiza? Je, watu wote wasingemfikiria kuwa mtoto? Ni nani ambaye angemwona kuwa wa kusadikisha? Mtoto wa miaka saba au minane asiye mrefu kuliko mimbari Aliyosimama nyuma yake—je, Angefaa kuhubiri? Kabla ya ubinadamu Wake wa kawaida kukomaa, Hakuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo. Kuhusu ubinadamu Wake ambao ulikuwa bado haujakomaa, sehemu kubwa ya kazi haingeweza kufikiwa kabisa. Pia kuna kanuni za kazi ya Roho wa Mungu katika mwili. Ni pale tu Anapokuwa na ubinadamu wa kawaida ndipo Anapoweza kufanya kazi kwa ajili ya Baba, na kuchukua agizo Alilopewa na Baba. Ni hapo tu ndipo Anaweza kuanza kazi Yake. Katika utoto Wake, Yesu asingeweza kuelewa chochote kuhusu mengi yaliyotukia katika nyakati za kale, na ni kwa kuwauliza walimu katika sinagogi tu ndipo Alipata kuelewa. Kama Angeanza kazi Yake mara tu Alipojifunza kuzungumza, ingewezekanaje Kwake kutofanya makosa? Mungu angewezaje kufanya makosa? Kwa hivyo, ilikuwa tu baada ya kuwa na uwezo wa kufanya kazi ndipo Alipoanza kazi Yake; Hakutekeleza kazi yoyote hadi Alipokuwa na uwezo kamili wa kuichukua. Akiwa na umri wa miaka 29, Yesu alikuwa tayari amekomaa sana na ubinadamu Wake ulitosha kuchukua kazi Aliyopaswa kufanya. Ilikuwa tu wakati huo ndipo Roho wa Mungu alianza rasmi kufanya kazi ndani Yake. Wakati huo, Yohana alikuwa amefanya matayarisho kwa miaka saba ili kumfungulia njia, na baada ya kuhitimisha kazi yake, alitupwa gerezani. Mzigo kisha ukamwangukia Yesu kabisa. Kama Angeanza kazi hii Akiwa na umri wa miaka 21 au 22, wakati ambapo ubinadamu Wake ulikuwa na upungufu mkubwa, wakati Alipokuwa ndio kwanza ameingia katika utu uzima, na kulikuwa na mambo mengi ambayo bado Hakuelewa, basi Hangekuwa na uwezo wa kuchukua udhibiti. Wakati huo, Yohana alikuwa tayari ametekeleza kazi yake kwa muda kabla ya Yesu kuanza kazi Yake, wakati ambapo Alikuwa tayari katika umri wa makamo. Katika umri huo, ubinadamu Wake wa kawaida ulitosha kuchukua kazi Aliyopaswa kufanya. Sasa, Mungu mwenye mwili pia ana ubinadamu wa kawaida na, ingawa hajakomaa kwa kulinganisha na wale wazee miongoni mwenu, ubinadamu huu tayari unatosha jinsi ulivyo kuchukua kazi Yake. Hali zinazozunguka kazi ya leo si sawa kabisa na zile za wakati wa Yesu. Kwa nini Yesu aliwachagua mitume kumi na wawili? Yote yalikuwa kwa ajili ya kuunga mkono kazi Yake na kwa ushirikiano nayo. Kwa upande mmoja, ilikuwa ni kuweka msingi wa kazi Yake wakati huo, huku kwa upande mwingine ilikuwa ni kuweka msingi wa kazi Yake katika siku zilizofuata. Kulingana na kazi ya wakati huo, Yesu aliwachagua mitume kumi na wawili; hii ilikuwa nia ya Yesu, pamoja na nia ya Mungu Mwenyewe. Aliamini kwamba Alipaswa kuwachagua mitume kumi na wawili na kisha kuwaongoza kuhubiri kila mahali. Lakini leo hakuna haja ya hili miongoni mwenu! Mungu mwenye mwili Anapofanya kazi katika mwili, kuna kanuni nyingi, na kuna mambo mengi ambayo mwanadamu haelewi kabisa; mwanadamu hutumia dhana zake mwenyewe kila mara kumpima, au kutoa matakwa ya kupita kiasi kwa Mungu. Hata hivyo hadi leo, watu wengi hawajui kabisa kwamba maarifa yao yanajumuisha dhana zao wenyewe pekee. Haijalishi ni enzi gani au mahali gani ambapo Mungu anapata mwili, kanuni za kazi Yake katika mwili hazibadiliki. Hawezi kupata mwili na bado avuke mipaka ya mwili katika kazi Yake; sembuse Yeye kupata mwili na bado asifanye kazi ndani ya ubinadamu wa kawaida wa mwili. Vinginevyo, umuhimu wa Mungu kupata mwili haungekuwa na umuhimu wowote, na Neno kuwa mwili hata zaidi kungekuwa hakuna maana kabisa. Zaidi ya hayo, ni Baba tu aliye mbinguni (Roho) ndiye Anayejua kuhusu Mungu kupata mwili, na hakuna mwingine, hata mwili Mwenyewe au wajumbe wa mbinguni. Hali ikiwa hivi, kazi ya Mungu katika mwili ni ya kawaida zaidi na ina uwezo bora zaidi wa kuonyesha kwamba Neno kwa kweli limekuwa mwili, na mwili unamaanisha mtu wa kawaida na wa desturi.

Wengine wanaweza kushangaa, “Kwa nini enzi lazima iletwe na Mungu Mwenyewe? Je, kiumbe aliyeumbwa hawezi kusimama mahali Pake?” Ninyi nyote mnafahamu kwamba Mungu anapata mwili kwa madhumuni hasa ya kuleta enzi mpya, na, bila shaka, Anapoileta enzi mpya, Atakuwa amekamilisha enzi ya kale wakati huo huo. Mungu ndiye Mwanzo na Mwisho; ni Yeye Mwenyewe ndiye anayeanzisha kazi Yake na hivyo lazima awe ni Yeye Mwenyewe anayehitimisha enzi iliyotangulia. Huo ndio ushahidi wa Yeye kumshinda Shetani na wa ushindi Wake dhidi ya ulimwengu. Kila wakati Yeye Mwenyewe anapofanya kazi miongoni mwa binadamu, huo ni mwanzo wa mapigano mapya. Bila mwanzo wa kazi mpya, kwa kawaida hakungekuwa na hitimisho la ile ya zamani. Na wakati hakuna hitimisho la ile ya zamani, huu ni ushahidi kwamba vita na Shetani bado havijafikia mwisho. Ni pale tu ambapo Mungu Mwenyewe anakuja, na kutekeleza kazi mpya miongoni mwa binadamu, ndipo mwanadamu anaweza kujinasua kabisa kutoka kwa nguvu za Shetani na kupata maisha mapya na mwanzo mpya. Vinginevyo, mwanadamu ataishi milele katika enzi ya zamani na kuishi milele chini ya ushawishi wa zamani wa Shetani. Katika kila enzi inayoongozwa na Mungu, sehemu ya mwanadamu huwekwa huru, na hivyo mwanadamu husonga mbele pamoja na kazi ya Mungu kuelekea enzi mpya. Ushindi wa Mungu unamaanisha ushindi kwa wale wote wanaomfuata Yeye. Kama wanadamu walioumbwa wangepewa jukumu la kuhitimisha enzi, basi iwe ni kutoka kwa mtazamo wa mwanadamu au wa Shetani, hiki hakingekuwa chochote zaidi ya kitendo cha kumpinga au kumsaliti Mungu, si cha utii kwa Mungu, na kazi ya mwanadamu ingekuwa uwezo wa kushawishi wa Shetani. Ni pale tu mwanadamu anapomtii na kumfuata Mungu katika enzi iliyoletwa na Mungu Mwenyewe ndipo Shetani anaweza kusadikishwa kikamilifu, kwa maana huo ndio wajibu wa kiumbe aliyeumbwa. Kwa hivyo, Ninasema kwamba ninyi mnahitaji tu kufuata na kutii, na hakuna zaidi kinachohitajika kutoka kwenu. Hii ndiyo maana ya kila mmoja kushika wajibu wake na kila mmoja kutekeleza kazi yake husika. Mungu hufanya kazi Yake Mwenyewe na Hahitaji mwanadamu aifanye badala Yake, wala Hajihusishi katika kazi ya viumbe walioumbwa. Mwanadamu hutekeleza wajibu wake mwenyewe na hajihusishi katika kazi ya Mungu. Hii ndiyo maana ya utii, na huu ni ushahidi wa kushindwa kwa Shetani. Baada ya Mungu Mwenyewe kumaliza kuileta enzi mpya, Hashuki tena kufanya kazi katikati ya binadamu Yeye Mwenyewe. Ni wakati huo tu ndipo mwanadamu anaingia rasmi katika enzi mpya kutekeleza wajibu wake na kutekeleza misheni yake kama kiumbe aliyeumbwa. Hizi ndizo kanuni ambazo kwazo Mungu hufanya kazi, ambazo hakuna anayeweza kuzikiuka. Kufanya kazi kwa njia hii pekee ndiko kwenye hekima na kwa busara. Kazi ya Mungu hufanywa na Mungu Mwenyewe. Ni Yeye anayeanzisha kazi Yake, na ni Yeye anayehitimisha kazi Yake. Ni Yeye anayepanga kazi, na ni Yeye anayeisimamia, na hata zaidi, ni Yeye anayekamilisha kazi yote. Kama inavyosemwa katika Biblia, “Mimi ndimi Mwanzo na Mwisho; Mimi ndimi Mpanzi na Mvunaji.” Kazi hii yote inayohusiana na usimamizi wa Mungu hufanywa na Mungu Mwenyewe. Yeye ndiye Mtawala wa mpango wa usimamizi wa miaka elfu sita; hakuna anayeweza kufanya kazi Yake badala Yake na hakuna anayeweza kuhitimisha kazi Yake, kwa maana ni Yeye ndiye anayeshikilia kila kitu mkononi Mwake. Baada ya kuumba ulimwengu, Atauongoza ulimwengu mzima kuishi katika nuru Yake, na pia hakika Atahitimisha enzi nzima, na hivyo kukamilisha mpango Wake mzima!

Iliyotangulia: Maono ya Kazi ya Mungu (3)

Inayofuata: Fumbo la Kupata Mwili (2)

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp