Maisha ya Kiroho ya Kawaida Humwongoza Mwanadamu Kuingia Katika Njia Sahihi
Mmetembea sehemu ndogo sana tu ya njia ya imani katika Mungu, na bado hamjaingia katika njia sahihi, kwa hivyo bado mko mbali na kufikia kiwango cha Mungu. Sasa hivi, kimo chenu hakitoshi kufikia matakwa Yake. Kwa sababu ya ubora wenu wa tabia na asili yenu potovu mliyozaliwa nayo, daima huichukulia kazi ya Mungu kijuujuu; hamuichukulii kwa uzito. Huu ndio upungufu wenu mkubwa kabisa. Sembuse kuwe na yeyote anayeweza kuelewa njia anayotembea Roho Mtakatifu; wengi wenu hamuielewi na hamwezi kuiona waziwazi. Zaidi ya hayo, wengi wenu hamtilii maanani jambo hili, sembuse kulichukulia kwa umakini. Mkiendelea kwa namna hii, bila kujua kazi ya Roho Mtakatifu, basi njia mnayochukua kama waumini katika Mungu itakuwa ya bure. Hii ni kwa sababu hamfanyi yote mnayoweza ili kutafuta kufikia nia za Mungu na ni kwa sababu hamshirikiani vyema na Mungu. Si kwamba Mungu hajafanya kazi juu yako, wala si kwamba Roho Mtakatifu hajakugusa. Ni kwamba wewe unafanya mambo kijuujuu sana hivi kwamba huichukulii kazi ya Roho Mtakatifu kwa uzito. Ni lazima ubadilishe hali hii mara moja na kutembea katika njia inayoongozwa na Roho Mtakatifu. Hii ndiyo mada kuu kwa leo. “Njia inayoongozwa na Roho Mtakatifu” inarejelea kupata nuru katika roho; kuwa na maarifa ya neno la Mungu; kupata uwazi kuhusu njia iliyo mbele; kuweza kuingia hatua kwa hatua katika ukweli; na kuwa na maarifa zaidi ya Mungu. Njia inayoongozwa na Roho Mtakatifu hasa ni njia ya kuwa na ufahamu ulio wazi zaidi wa neno la Mungu, bila mikengeuko wala upuuzi, na wale wanaotembea katika njia hiyo hutembea moja kwa moja ndani yake. Ili kufanikisha hili mtahitaji kushirikiana kwa upatano na Mungu, kupata njia sahihi ya utendaji, na kutembea katika njia inayoongozwa na Roho Mtakatifu. Hili linahusisha ushirikiano kwa upande wa mwanadamu: yaani, kile mnachopaswa kufanya ili kufikia matakwa ya Mungu kwenu, na jinsi ambavyo sharti mtende ili kuingia katika njia sahihi ya imani katika Mungu.
Kuingia katika njia inayoongozwa na Roho Mtakatifu kunaweza kuonekana kuwa jambo changamano, lakini utaona kuwa ni rahisi sana wakati njia ya utendaji inapokuwa wazi kwako. Ukweli ni kwamba watu wanaweza kufanya yote ambayo Mungu anataka kutoka kwao—si kana kwamba Anajaribu kuwalazimisha samaki kuishi nchi kavu. Katika hali zote, Mungu hutafuta kutatua matatizo ya watu na kuondoa mahangaiko yao. Ninyi nyote mnapaswa kuelewa hili; msimwelewe Mungu vibaya. Watu wanaongozwa kulingana na neno la Mungu katika njia anayotembea Roho Mtakatifu. Kama ilivyotajwa hapo awali, lazima umpe Mungu moyo wako. Hili ni sharti la kutembea katika njia inayoongozwa na Roho Mtakatifu. Ni lazima ufanye hili ili uingie katika njia sahihi. Mtu anawezaje kwa makusudi kufanya kazi ya kumpa Mungu moyo wake? Katika maisha yenu ya kila siku, mnapopitia kazi ya Mungu na kumwomba Yeye, ninyi mnafanya hivyo kijuujuu tu—mnamwomba Mungu huku mkifanya kazi. Je, huku kunaweza kuitwa kumpa Mungu moyo wako? Mnafikiria kuhusu mambo ya nyumbani au mambo ya mwili; daima mna mawazo mawili. Je, hili linaweza kuchukuliwa kuwa ni kuutuliza moyo wenu mbele ya Mungu? Hii ni kwa sababu moyo wako daima umeelekezwa kwenye mambo ya nje, na hauwezi kurudi mbele ya Mungu. Ikiwa ungetaka moyo wako utulie kweli mbele ya Mungu, basi lazima ufanye kazi ya ushirikiano wa makusudi. Hii ni kusema kwamba kila mmoja wenu lazima awe na wakati kwa ajili ya ibada zake za kiroho, na aepuke watu, matukio, na vitu vyote na autulize moyo wake, na awe mtulivu mbele ya Mungu. Kila mmoja wenu lazima awe na madokezo yake binafsi ya ibada ya kiroho, akiandika maarifa yake ya neno la Mungu na jinsi roho yake inavyoguswa, bila kujali kama ni ya kina au ya juu juu tu; kila mmoja wenu lazima kwa makusudi autulize moyo wake mbele za Mungu. Ikiwa unaweza kutenga saa moja au mbili kila siku kwa ajili ya maisha ya kweli ya kiroho, basi maisha yako siku hiyo yatahisi kuwa yenye utimilifu na moyo wako utakuwa wenye nuru na wazi. Ukiishi maisha ya kiroho ya aina hii kila siku, basi moyo wako utaweza kurudi zaidi katika miliki ya Mungu, roho yako itazidi kuwa na nguvu, hali yako itazidi kuwa bora, utaweza zaidi kutembea katika njia inayoongozwa na Roho Mtakatifu, na Mungu atakupa baraka maradufu. Kusudi la maisha yenu ya kiroho ni kupata uwepo wa Roho Mtakatifu kwa makusudi. Si kwa ajili ya kuzingatia taratibu wala kufanya mila za kidini, bali ni kushirikiana kweli na Mungu, kweli kuudhibiti mwili wenu—hili ndilo jambo ambalo mwanadamu anapaswa kufanya, kwa hivyo mnapaswa kufanya hili kwa juhudi zote. Kadiri ushirikiano wako unavyokuwa bora na kadiri unavyotia juhudi zaidi, ndivyo moyo wako utakavyoweza kumrudia Mungu zaidi na ndivyo utakavyoweza kuutuliza moyo wako mbele Yake vyema zaidi. Katika hatua fulani, Mungu ataupata moyo wako kikamilifu. Hakuna mtu atakayeweza kuutikisa wala kuuchukua moyo wako, nawe utakuwa wa Mungu kikamilifu. Ukitembea katika njia hii, basi neno la Mungu litajidhihirisha kwako nyakati zote na kukutia nuru kuhusu kila kitu ambacho huelewi—haya yote yanaweza kufikiwa kupitia ushirikiano wako. Hii ndiyo sababu Mungu daima husema, “Wote wanaoshirikiana na Mimi, Nitawapa maradufu.” Mnapaswa kuiona njia hii waziwazi. Mkitaka kutembea katika njia sahihi, basi lazima mfanye yote mnayoweza ili kumridhisha Mungu. Mnapaswa kufanya yote mnayoweza ili kupata maisha ya kiroho. Mwanzoni, huenda usipate matokeo makubwa katika jambo hili, lakini usiwe hasi, wala usirudi nyuma—endelea kufanya kazi kwa bidii! Kadiri unavyoishi maisha ya kiroho, ndivyo moyo wako utakavyomilikiwa zaidi na maneno ya Mungu, daima ukijishughulisha na mambo haya, daima ukiyabeba kama mzigo wako. Baada ya hapo, kupitia maisha yako ya kiroho mwambie Mungu mawazo yako yote ya ndani kabisa; mwambie kile ambacho uko tayari kufanya, kile unachofikiria, uelewa wako na mtazamo wako wa neno Lake. Usifiche chochote. Jizoeze kumwambia Mungu yaliyo moyoni mwako na kufichua Kwake hisia zako za kweli; sema chochote kilicho moyoni mwako. Kadiri unavyozungumza kwa njia hii, ndivyo utakavyohisi zaidi kupendeza kwa Mungu, na ndivyo moyo wako utakavyovutwa zaidi kwa Mungu. Hili linapotokea, utahisi kwamba Mungu ni wa karibu zaidi kuliko mtu mwingine yeyote, na kwamba huwezi kamwe kuondoka upande wa Mungu, haijalishi kitakachotokea. Ni pale tu unapofanya ibada ya kiroho ya aina hii kila siku, bila kusahau kuifanya kamwe, kana kwamba ni jambo muhimu sana katika maisha yako, ndipo moyo wako unaweza kumilikiwa na neno la Mungu. Hii ndiyo maana ya kuguswa na Roho Mtakatifu. Itakuwa kana kwamba moyo wako daima umemilikiwa na Mungu, kana kwamba kile unachokipenda daima kiko moyoni mwako, na hakuna anayeweza kukichukua kutoka kwako. Hili linapotokea, Mungu ataishi kweli ndani yako na kuwa na nafasi ndani ya moyo wako.