Tatizo Kubwa Sana: Usaliti (1)
Hivi karibuni, kazi Yangu itakamilika, na miaka yetu mingi pamoja imekuwa kumbukumbu isiyovumilika. Nimerudia maneno Yangu bila kukoma na kuendeleza kazi Yangu mpya daima. Bila shaka, nasaha Zangu hutumika kama sehemu ya lazima kila wakati Ninapofanya kazi. Bila nasaha hiyo, ninyi nyote mngepotea na hata zaidi mngejikuta hamjui la kufanya kabisa. Kazi Yangu sasa inakaribia kumalizika na iko katika hatua yake ya mwisho. Bado Ninatamani kufanya kazi fulani ya kutoa nasaha, yaani, kutoa maneno ya nasaha ili ninyi myasikie. Ninatumaini tu kwamba ninyi mnaweza kutoruhusu juhudi Zangu ziwe za bure, na, zaidi ya hayo, kwamba mnaweza kuelewa nia Zangu za kujitahidi, na kuyachukulia maneno Yangu kama msingi wa mwenendo wenu wa kibinafsi. Iwe ni aina ya maneno ambayo ninyi mko tayari kuyasikiliza au la, iwe ni maneno ambayo ninyi mnafurahia kuyakubali au ambayo mnayakubali shingo upande, lazima myachukulie kwa uzito. Vinginevyo, tabia na mienendo yenu ya kijuujuu na ya kutojali vitaniumiza Mimi sana, na hata zaidi vitanifanya Mimi nihisi chuki kubwa. Ninatumaini sana ninyi nyote mnaweza kusoma maneno Yangu tena na tena—maelfu ya mara—hata yafikie hatua ya kuchongwa mioyoni mwenu. Ni kwa namna hii tu ndiyo hamtashindwa kuyatimiza matarajio Yangu kwenu. Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishi kwa namna hii sasa. Kinyume chake, ninyi nyote mmezama katika maisha ya upotovu, maisha ya kula na kunywa kwa kadiri ya tamaa ya mioyo yenu, na hakuna hata mmoja wenu anayetumia maneno Yangu kuutajirisha moyo na roho yake. Kwa sababu hii, Nimefikia hitimisho kuhusu sura ya kweli ya binadamu: Mwanadamu anaweza kunisaliti Mimi wakati wowote, na hakuna anayeweza kuwa mwaminifu kabisa kwa maneno Yangu.
“Mwanadamu amepotoshwa sana na Shetani kiasi kwamba hana tena mfano wa mwanadamu.” Idadi kubwa sana ya watu sasa wanalitambua fungu hili la maneno kwa kiasi. Ninasema hivi kwa sababu “utambuzi” Ninaourejelea ni aina tu ya kukiri kwa juu juu, kinyume na maarifa ya kweli. Kwa kuwa hakuna hata mmoja wenu anayeweza kujitathmini kwa usahihi wala kujichanganua kikamilifu, ninyi huyamini maneno Yangu nusu nusu tu. Lakini wakati huu, Ninatumia ukweli wa mambo kueleza tatizo kubwa kabisa ambalo lipo ndani yenu. Tatizo hilo ni usaliti. Ninyi nyote mnalifahamu neno “usaliti,” kwa sababu watu wengi wamefanya jambo ambalo linamsaliti mwingine, kama vile mume kumsaliti mke wake, mke kumsaliti mume wake, mwana kumsaliti baba yake, binti kumsaliti mama yake, mtumishi kumsaliti bwana wake, marafiki kusalitiana, jamaa kusalitiana, wauzaji kuwasaliti wanunuzi, na kadhalika. Mifano hii yote ina kiini cha usaliti. Kwa ufupi, usaliti ni aina ya mwenendo unaovunja kiapo, unaokiuka kanuni za maadili, au unaotenda kinyume na maadili ya binadamu, ukionyesha kupoteza ubinadamu. Kama binadamu, haijalishi kama ninyi mnakumbuka kuwa mlifanya jambo la kumsaliti mtu mwingine, au kama ninyi mmewasaliti wengine mara nyingi hapo awali, kwa kuzaliwa katika dunia hii, ninyi nyote mmefanya jambo ambalo linajumuisha ukiukaji wa ukweli. Kwa kuwa wewe una uwezo wa kuwasaliti wazazi au marafiki zako, basi una uwezo wa kuwasaliti wengine, na hata zaidi una uwezo wa kunisaliti Mimi na kufanya mambo Ninayoyachukia. Yaani usaliti si mwenendo tu wa kijuujuu usio wa kimaadili, bali zaidi ya hayo, ni jambo linalokinzana na ukweli. Hiki hasa ndicho chanzo cha upinzani na uasi wa binadamu dhidi Yangu. Hii ndiyo sababu Nimeufupisha katika kauli ifuatayo: Usaliti ni asili ya mwanadamu ya kuzaliwa nayo, na asili hii ni adui wa asili wa kila mtu katika kufikia uwiano na Mimi.
Mwenendo usioweza kunitii Mimi kabisa ni usaliti. Mwenendo usioweza kuwa mwaminifu Kwangu ni usaliti. Kunidanganya Mimi na kutumia uwongo kunihadaa Mimi ni usaliti. Kuwa na dhana nyingi na kuzieneza kila mahali ni usaliti. Kutoweza kutetea shuhuda na masilahi Yangu ni usaliti. Kutoa tabasamu za uwongo ukiwa mbali na Mimi moyoni ni usaliti. Haya yote ni matendo ya usaliti ambayo ninyi mmekuwa na uwezo wa kuyafanya daima, nayo ni ya kawaida miongoni mwenu. Huenda kusiwe na hata mmoja wenu anayeliona hili kama tatizo, lakini hivyo sivyo Ninavyofikiri. Siwezi kuchukulia usaliti wa mtu dhidi Yangu kuwa jambo dogo, na hata zaidi Siwezi kuupuuza. Hata sasa, Ninapokuwa kazini miongoni mwenu, ninyi mnatenda kwa namna hii—ikiwa itafika siku ambapo hakuna mtu wa kuwasimamia ninyi, je, ninyi hamtakuwa kama majambazi ambao wamejitangaza kuwa wafalme wa maeneo yao madogo? Hilo litakapotokea na ninyi msababishe janga, ni nani atakuwepo kusafisha baada yenu? Ikiwa ninyi mnafikiri baadhi ya matendo ya usaliti ni matendo tu ya mara chache badala ya mwenendo wenu wa kudumu, ambayo hayapaswi kutajwa kwa uzito kama huo, kiasi kwamba heshima yenu inaumizwa, na ikiwa hili ndilo ninyi mnaliamini kweli, basi ninyi hamna busara kabisa. Kadiri mtu anavyofikiri hivi, ndivyo anavyozidi kuwa kielelezo na mfano wa uasi. Asili ya mwanadamu ni maisha yake; ni kanuni anayoitegemea ili kuendelea kuishi, na hawezi kuibadilisha. Chukua asili ya usaliti kama mfano. Ikiwa unaweza kufanya mambo ya kumsaliti yeyote kati ya jamaa au marafiki zako, inathibitisha kwamba ni sehemu ya maisha yako na asili uliyozaliwa nayo. Hili ni jambo ambalo hakuna anayeweza kulikana. Kwa mfano, ikiwa mtu anafurahia kuwaibia wengine, basi furaha hii ya kuiba ni sehemu ya maisha yake, ingawa wakati mwingine anaiba na wakati mwingine haibi. Iwe anaiba au la, haiwezi kuthibitisha kwamba wizi wake ni aina tu ya mwenendo. Badala yake, inathibitisha kwamba wizi wake ni sehemu ya maisha yake—yaani, asili yake. Wengine watauliza: Kwa kuwa ni asili yake, basi kwa nini, anapoona vitu vizuri, wakati mwingine haviibi? Jibu ni rahisi sana. Kuna sababu nyingi zinazomfanya asiibe. Huenda asiibe kitu kwa sababu ni kikubwa sana kuweza kukipokonya mbele ya macho ya watu, au kwa sababu hakuna wakati unaofaa wa kutenda, au kitu ni ghali sana, kinalindwa vikali sana, au pengine hapendezwi nacho hasa, au haoni kinaweza kuwa na matumizi gani kwake, na kadhalika. Sababu hizi zote zinawezekana. Lakini haijalishi chochote, iwe anaiba kitu au la, haliwezi kuthibitisha kwamba wazo hili lipo tu kama wazo la muda mfupi, linalopita haraka. Kinyume chake, ni sehemu ya asili yake—asili ambayo ni ngumu kufanywa upya. Mtu wa aina hii hatosheki na kuiba mara moja tu; fikira kama hizo za kuchukua mali za wengine kuwa zake huibuka kila anapokumbana na kitu kizuri, au hali inayofaa. Hii ndiyo sababu Ninasema kwamba wazo hili si jambo ambalo mtu huyu hulipata nyakati fulani tu, bali ni jambo linalotokana na asili yake.
Mtu yeyote anaweza kutumia maneno na matendo yake mwenyewe kuwakilisha sura yake ya kweli. Sura hii ya kweli, bila shaka, ni asili yake. Ikiwa wewe ni mtu anayezungumza kwa njia ya kupindapinda, basi una asili ya kupindapinda. Ikiwa asili yako ni danganyifu, basi unatenda kwa njia ya ujanja, na unafanya iwe rahisi sana kwa wengine kudanganywa na kuhadaiwa na wewe. Ikiwa asili yako ni ya unyama, maneno yako yanaweza kuwa ya kufurahisha kusikia, lakini matendo yako hayawezi kuficha hila zako za unyama. Ikiwa asili yako ni ya uvivu, basi kwa kila unachosema utakuwa ukijaribu kujiondolea lawama kwa kuwa wa kijuujuu tu na mvivu, na matendo yako yatakuwa ya polepole na ya kijuujuu tu, na mahiri sana katika kuficha ukweli. Ikiwa asili yako ni ya uelewa na kujali wengine, basi maneno yako yatakuwa ya busara, na matendo yako pia yatalingana vyema na ukweli. Ikiwa asili yako ni kuwa mwaminifu kwa kila mtu, basi maneno yako hakika ni ya dhati na jinsi unavyotenda ni kwa uthabiti, bila chochote kinachoweza kumfanya bwana wako awe na wasiwasi. Ikiwa asili yako ni yenye tamaa ya mwili au tamaa ya pesa, basi moyo wako mara nyingi utajazwa na mambo haya, nawe bila kujua utafanya matendo yaliyopotoka, yasiyo ya kimaadili ambayo watu hawatayasahau kwa urahisi na ambayo yatawachukiza watu. Kama tu ambavyo Nimesema, ikiwa una asili ya usaliti, basi ni vigumu kwako kujinasua kutoka kwayo. Usiwe na mawazo ya kujaribu bahati yako, ukidhani kwamba kwa sababu hujawakosea wengine, huna asili ya usaliti. Ikiwa hivyo ndivyo unavyofikiri basi, kwa kweli, unachukiza. Kila wakati Ninaponena, maneno Yangu yanalenga watu wote, si mtu mmoja tu au aina moja ya mtu. Ukweli kwamba hujanisaliti Mimi katika jambo moja hauthibitishi kwamba hutanisaliti Mimi katika jambo lolote. Watu wengine, wakati wa vikwazo katika ndoa zao, wanapoteza imani yao katika kutafuta ukweli. Watu wengine hutelekeza wajibu wao wa kuwa waaminifu Kwangu wakati wa kuvunjika kwa familia. Watu wengine huniacha Mimi ili kutafuta muda mfupi wa furaha na msisimko. Watu wengine afadhali waanguke katika bonde lenye giza kuliko kuishi katika nuru na kupata furaha ya kazi ya Roho Mtakatifu. Watu wengine hupuuza ushauri wa marafiki kwa ajili ya kuridhisha tamaa yao ya utajiri, na hata sasa hawawezi kukiri kosa lao na kubadili mwelekeo wao. Watu wengine wanaishi kwa muda tu chini ya jina Langu ili wapokee ulinzi Wangu, huku wengine wakijitolea Kwangu kidogo tu shingo upande kwa sababu wanang’ang’ania maisha na kuogopa kifo. Je, haya na matendo mengine kama haya, ambayo si ya kimaadili na, hata zaidi, yasiyo na hulka, si mienendo tu ambayo kwayo watu wamekuwa wakinisaliti Mimi kwa muda mrefu kilindini mwa mioyo yao? Bila shaka, Ninajua kuwa watu hawapangi mapema kunisaliti Mimi, lakini usaliti wao ni ufunuo wa kiasili wa asili yao. Hakuna anayetaka kunisaliti Mimi, sembuse mtu yeyote kuwa na furaha kwa sababu amefanya tendo la usaliti dhidi Yangu. Kinyume chake, wanatetemeka kwa hofu, sivyo? Kwa hivyo, je, mnafikiria jinsi ya kurekebisha matendo haya ya usaliti, na jinsi ya kubadili hali ya sasa?