2. Jua madhumuni ya hatua tatu za kazi ya usimamizi wa Mungu wa wanadamu

Maneno Husika ya Mungu:

Mpango Wangu mzima wa usimamizi, mpango ambao una urefu wa miaka elfu sita, unashirikisha hatua tatu, au enzi tatu: Enzi ya Sheria mwanzoni; Enzi ya Neema (ambayo pia ni Enzi ya Ukombozi); na katika siku za mwisho, Enzi ya Ufalme. Kazi Yangu katika enzi hizi tatu hutofautiana katika maudhui kulingana na asili ya kila enzi, lakini katika kila hatua huambatana na mahitaji ya mwanadamu—au, kwa usahihi zaidi, inafanywa kulingana na ujanja ambao Shetani hutumia katika vita Vyangu dhidi yake. Madhumuni ya Kazi Yangu ni kumshinda Shetani, ili kudhihirisha hekima Yangu na kudura, kufichua ujanja wote wa Shetani na hivyo kuokoa wanadamu wote, wanaoishi chini ya miliki yake. Ni ili kuonyesha hekima Yangu na kudura na wakati uo huo kufichua ubovu wa Shetani usiovumilika. Aidha, ni ili kufundisha viumbe Wangu kutofautisha kati ya mema na mabaya, kutambua kwamba Mimi ndiye Mtawala wa vitu vyote, kuona wazi kwamba Shetani ni adui wa binadamu, wa chini kuliko wote, yule mwovu, na kujua, kwa uhakika kabisa tofauti kati ya mema na mabaya, ukweli na uwongo, utakatifu na uchafu, kilicho kikuu na kilicho cha aibu. Kwa njia hii, binadamu wasiofahamu wataweza kunishuhudia kwamba si Mimi Ninayewapotosha wanadamu, na kwamba ni Mimi tu—Bwana wa viumbe—Ninayeweza kumwokoa binadamu, Ninayeweza kumpa mwanadamu vitu kwa ajili ya raha yake; na atapata kujua kwamba Mimi Ndimi Mtawala wa vitu vyote na Shetani ni mmoja tu wa viumbe niliowaumba na ambaye baadaye alinigeuka. Mpango Wangu wa usimamizi wa miaka elfu sita umegawanywa katika hatua tatu ili kufikia matokeo yafuatayo: kuwezesha viumbe Wangu wawe mashahidi Wangu, kuelewa mapenzi Yangu, na wajue kwamba Mimi Ndimi ukweli.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Maelezo ya Kweli ya Kazi Katika Enzi ya Ukombozi

Leo kwanza kabisa tutafanya muhtasari wa fikira, mawazo, na kila hatua ya Mungu tangu Alipomuumba binadamu, na kuangalia ni kazi gani Alitekeleza kuanzia uumbaji wa ulimwengu hadi mwanzo rasmi wa Enzi ya Neema. Tunaweza kisha kugundua ni fikira na mawazo yapi ya Mungu ambayo hayajulikani kwa binadamu, na kuanzia hapo tunaweza kuweka wazi mpangilio wa mpango wa usimamizi wa Mungu na kuelewa kwa kina muktadha ambao kwao Mungu alianzisha kazi Yake ya usimamizi, chanzo chake na mchakato wake wa maendeleo, na pia kuelewa kwa undani ni matokeo yapi Anayotaka kutoka katika kazi Yake ya usimamizi—yaani, kiini na kusudio la kazi Yake ya usimamizi. Kuelewa mambo haya tunahitaji kurudi hadi ule wakati wa kitambo, mtulivu na kimya ambapo hakukuwa na binadamu …

Mungu Mwenyewe Amuumba Mtu wa Kwanza Aliye Hai

Wakati Mungu aliinuka kutoka kitandani Mwake, fikira ya kwanza Aliyokuwa nayo ilikuwa hii: kumuumba binadamu hai, halisi, binadamu anayeishi—mtu wa kuishi naye na kuwa mwandani Wake wa kudumu. Mtu huyu angemsikiliza, na Mungu angempa siri Zake na kuongea na yeye. Kisha, kwa mara ya kwanza, Mungu aliuchukua udongo kwenye mkono na kuutumia kumuumba mtu wa kwanza kabisa aliye hai ambaye Alikuwa amemfikiria, na kisha Akakipa kiumbe hiki hai jina—Adamu. Mara tu Mungu alipompata mtu huyu aliye hai na anayepumua, je, Alihisi vipi? Kwa mara ya kwanza, Alihisi furaha ya kuwa na mpendwa, na mwandani. Aliweza kuhisi pia kwa mara ya kwanza uwajibikaji wa kuwa baba pamoja na kujali kunakoandamana na hisia hizo. Mtu huyu aliye hai na anayepumua alimletea Mungu furaha na shangwe; Alihisi kufarijika kwa mara ya kwanza. Hili lilikuwa jambo la kwanza ambalo Mungu aliwahi kufanya ambalo halikukamilishwa kwa fikira Zake au hata matamshi Yake, lakini lilifanywa kwa mikono Yake miwili. Wakati kiumbe wa aina hii—mtu aliye hai na anayepumua—aliposimama mbele wa Mungu, aliyeumbwa kwa nyama na damu, aliye na mwili na umbo, na aliyeweza kuongea na Mungu, Alihisi aina ya shangwe ambayo Hakuwa amewahi kuihisi kabla. Kwa kweli alihisi kwamba uwajibikaji Wake na kiumbe huyu aliye hai haukuwa na uhusiano tu katika moyo Wake, lakini kila jambo dogo alilofanya pia lilimgusa na likaupa moyo Wake furaha. Kwa hivyo wakati kiumbe huyu aliye hai aliposimama mbele ya Mungu, ilikuwa ndiyo mara ya kwanza Alipowahi kufikiria kuwapata watu wengi zaidi kama hawa. Huu ndio uliokuwa msururu wa matukio ulioanza kwa fikira hii ya kwanza ambayo Mungu alikuwa nayo. Kwa Mungu, matukio haya yote yalikuwa yakifanyika kwa mara ya kwanza, lakini katika matukio haya ya kwanza, haijalishi vile Alivyohisi wakati huo—furaha, uwajibikaji, kujali—hakukuwa na yeyote yule wa kushiriki furaha hii na Yeye. Kuanzia wakati huo, Mungu alihisi kwa kweli upweke na huzuni ambayo Hakuwahi kupata hapo awali. Alihisi kwamba binadamu wasingekubali au kuelewa upendo Wake na kujali Kwake, au nia Zake kwa mwanadamu, hivyo basi Alihisi huzuni na maumivu katika moyo Wake. Ingawa Alikuwa amefanya mambo haya kwa binadamu, binadamu hakuwa na habari na hakuelewa. Mbali na furaha, shangwe na faraja ambayo binadamu alimletea pia viliandamana kwa haraka na hisia Zake za kwanza za huzuni na upweke. Hizi ndizo zilizokuwa fikira na hisia za Mungu wakati huo. Mungu alipokuwa akifanya mambo haya yote, moyoni Mwake Alitoka katika furaha Akaingia katika huzuni na kutoka katika huzuni Akaingia katika maumivu, vyote vikiwa vimechanganyika na wasiwasi. Kile Alichotaka kufanya tu kilikuwa kuharakisha kumruhusu mtu huyu, kizazi hiki cha binadamu kujua ni nini kilichokuwa moyoni Mwake na kuelewa nia Zake haraka iwezekanavyo. Kisha, wangekuwa wafuasi Wake na kupatana na Yeye. Wasingemsikiliza tena Mungu akiongea na kubakia kimya; wasingeendelea kutojua namna ya kujiunga na Mungu katika kazi Yake, na zaidi ya yote, wasingekuwa tena watu wasiojali matakwa ya Mungu. Mambo haya ya kwanza ambayo Mungu alikamilisha ni yenye maana sana na yanashikilia thamani kubwa kwa minajili ya mpango Wake wa usimamizi na ule wa binadamu leo.

Baada ya kuviumba vitu vyote na binadamu, Mungu hakupumzika. Asingesubiri kuutekeleza usimamizi Wake wala Asingeweza kusubiri kuwapata watu Aliowapenda mno miongoni mwa wanadamu.

Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe III

Mungu anachukulia tukio hili la usimamizi Wake wa wanadamu, la wokovu Wake kwa wanadamu, kuwa ya muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote. Anafanya mambo haya yote si kwa kutumia akili Zake tu, wala si kwa kutumia maneno Yake tu, na vilevile Yeye hafanyi hivi hususan kwa juujuu tu—Yeye huyafanya mambo haya yote kwa mpango, wa lengo, kwa viwango, na kwa mapenzi Yake. Ni wazi kwamba kazi hii ya kumwokoa binadamu imeshikilia umuhimu mkubwa kwa Mungu na hata binadamu. Haijalishi jinsi kazi ilivyo ngumu, haijalishi changamoto ni kubwa jinsi gani, haijalishi wanadamu ni wadhaifu kiasi gani, au uasi wa wanadamu ni wa kiasi gani, hakuna chochote kati ya haya ambacho ni kigumu kwa Mungu. Mungu hujibidiisha Mwenyewe, Akitumia jitihada Zake nyingi na kusimamia kazi ambayo Yeye Mwenyewe Anataka kutekeleza. Yeye pia Anapanga kila kitu na kuwatawala watu wote na kazi ambayo Anataka kukamilisha—hakuna chochote kati ya haya ambacho kimefanywa awali. Ndiyo mara ya kwanza Mungu ametumia mbinu hizi na kulipa gharama kubwa kwa minajili ya mradi huu mkubwa wa kumsimamia na kumwokoa mwanadamu. Wakati Mungu akiwa Anatekeleza kazi hii, hatua kwa hatua Anawaonyesha na kuachilia kwa wanadamu bila kuficha juhudi Zake nyingi, kile Anacho na Alicho, hekima na uweza, na kila kipengele cha tabia Yake. Anaachilia na kuonyesha haya yote kwa mwanadamu kidogo kidogo, Akifichua na kuonyesha mambo haya kwa namna ambayo Hajawahi kufanya hapo awali. Kwa hivyo, katika ulimwengu mzima, mbali na watu ambao Mungu analenga kuwasimamia na kuwaokoa, hakujawahi kuwepo na viumbe vyovyote vilivyo karibu na Mungu, ambavyo vinao uhusiano wa karibu sana na Yeye. Katika moyo Wake, yule mwanadamu Anayetaka kumsimamia na kumwokoa ndiye muhimu zaidi, na Anamthamini mwanadamu huyu zaidi ya kitu kingine chochote; hata ingawa Amelipa gharama kubwa kwa ajili yao na ingawa Anaumizwa na kutosikilizwa kila mara na wao, Hakati tamaa juu yao na Anaendelea bila kuchoka katika kazi Yake bila ya malalamiko au majuto. Hii ni kwa sababu Anajua kwamba hivi karibuni au baadaye, binadamu siku moja wataitikia mwito Wake na kuguswa na maneno Yake, kutambua kwamba Yeye ndiye Bwana wa uumbaji, na kurudi upande Wake …

Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe III

Licha ya kile ambacho Mungu anafanya au mbinu ambazo Anatumia kuifanya, licha ya gharama, au lengo Lake, dhumuni la matendo Yake halibadiliki. Kusudi Lake ni kufanya kazi ya maneno ya Mungu ndani ya mwanadamu, pamoja na mahitaji ya Mungu na mapenzi ya Mungu kwa mwanadamu; kwa maneno mengine, ni kufanya kazi ndani ya mwanadamu kwa yale yote ambayo Mungu anayaamini kuwa ni chanya kulingana na hatua Zake, ili kumwezesha binadamu kuuelewa moyo wa Mungu na kufahamu kiini cha Mungu, na kumruhusu aweze kutii ukuu na mipangilio ya Mungu, na hivyo basi kumruhusu binadamu kuweza kufikia kiwango cha kumcha Mungu na kujiepusha na maovu—yote haya ni kipengele kimoja cha kusudi la Mungu katika kila kitu Anachofanya. Kipengele kingine ni kwamba, kwa sababu Shetani ndiye foili na chombo cha huduma katika kazi ya Mungu, mara nyingi binadamu hukabidhiwa kwa Shetani; hizi ndizo mbinu ambazo Mungu hutumia ili kuwaruhusu watu kuweza kuona maovu, ubaya, nakudharaulika kwa Shetani katikati ya majaribu na mashambulizi ya Shetani na hivyo basi kuwasababisha watu kumchukia Shetani na kuweza kutambua kile ambacho ni kibaya. Mchakato huu unawaruhusu kwa utaratibu kuanza kuwa huru dhidi ya udhibiti wa Shetani, na dhidi ya mashtaka, uingiliaji kati, na mashambulizi ya Shetani—hadi, kwa sababu ya maneno ya Mungu, maarifa yao na utiifu wao kwa Mungu, na imani yao kwa Mungu na kuweza kwao kumcha Mungu, wanashinda dhidi ya mashambulizi ya Shetani na kushinda dhidi ya mashtaka ya Shetani; hapo tu ndipo watakapokuwa wamekombolewa kabisa dhidi ya utawala wa Shetani. Ukombozi wa watu unamaanisha kwamba Shetani ameshindwa, unamaanisha kwamba wao si chakula tena katika kinywa cha Shetani—kwamba badala ya kuwameza wao, Shetani amewaachilia. Hii ni kwa sababu watu kama hao ni wanyofu, kwa sababu wanayo imani, utiifu na wanamcha Mungu, na kwa sababu wako huru kabisa dhidi ya Shetani. Wamemletea Shetani aibu, wamemfanya Shetani kuwa mwoga, na wamemshinda kabisa Shetani. Imani yao katika kumfuata Mungu, na utiifu na kumcha Mungu kunamshinda Shetani, na kumfanya Shetani kukata tamaa kabisa na wao. Watu kama hawa ndio ambao Mungu amewapata kwa kweli, na hili ndilo lengo kuu la Mungu katika kumwokoa binadamu.

Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Kazi ya Mungu, Tabia ya Mungu, na Mungu Mwenyewe II

Huu ni mfano wa usimamizi wa Mungu: kuwakabidhi wanadamu kwa Shetani—binadamu ambaye hajui Mungu ni nini, Muumba ni nini, jinsi ya kumwabudu Mungu, na kwa nini ni muhimu kunyenyekea kwa Mungu—na kutoa uhuru kwa upotovu wa Shetani. Hatua kwa hatua, Mungu kisha anamponya mwanadamu kutoka kwa mikono ya Shetani, hadi mwanadamu amwabudu Mungu kikamilifu na kumkataa Shetani. Huu ndio usimamizi wa Mungu. Hili linasikika kama hadithi ya visasili; na inaonekana inatatanisha. Watu wanahisi kwamba ni kama hadithi ya visasili, na hii ni kwa sababu hawana fununu kuhusu yaliyomtokea mwanadamu katika maelfu ya miaka iliyopita, sembuse kujua hadithi ngapi ambazo zimetokea katika ulimwengu na anga. Na zaidi ya hayo, hii ni kwa sababu hawawezi kufahamu kinachostaajabisha sana, dunia inayoibua hofu zaidi ambayo iko zaidi ya dunia yakinifu, lakini ambayo macho yao ya mwili yanawazuia kuiona. Inasikika ya kutofahamika kwa mwanadamu. Na hii ni kwa sababu mwanadamu hana ufahamu wa umuhimu wa Mungu kumwokoa na umuhimu wa kazi ya usimamizi wa Mungu, na hafahamu jinsi Mungu Anavyotamani zaidi wanadamu wawe. Je, ni wanadamu mfano wa Adamu na Hawa, wasiopotoshwa na Shetani? Hapana! Usimamizi wa Mungu ni kwa ajili ya kupata kikundi cha watu ambao humwabudu Mungu na kujitoa kwake. Hawa wanadamu wamepotoshwa na Shetani, lakini hawamwoni Shetani kama baba yao: hutambua uso usiopendeza wa Shetani, na kuukataa, na kuja mbele Zake Mungu na kukubali hukumu na kuadibu Kwake. Hujua kisichopendeza na jinsi kinavyotofautiana na kile kilicho kitakatifu, na hutambua ukubwa wa Mungu na uovu wa Shetani. Wanadamu kama hawa hawatamfanyia Shetani kazi tena, au kumwabudu Shetani, au kumsetiri Shetani. Hii ni kwa sababu wao ni kikundi cha watu ambao wamemilikiwa na Mungu. Huu ndio umuhimu wa Mungu kuwasimamia wanadamu.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kiambatisho 3: Mwanadamu Anaweza tu Kuokolewa Katikati ya Usimamizi wa Mungu

Mungu aliumba binadamu na Akawaweka duniani, ambao Amewaongoza mpaka siku ya leo. Kisha Akaokoa binadamu na kuhudumu kama sadaka ya dhambi kwa binadamu. Mwishowe lazima bado ashinde binadamu, aokoe binadamu kabisa na kuwarejesha kwa mfano wao wa awali. Hii ndiyo kazi Amekuwa akifanya kutoka mwanzo hadi mwisho—kurejesha mwanadamu kwa sura yake halisi na kwa mfano wake wa awali. Ataanzisha ufalme Wake na kurejesha mfano wa awali wa mwanadamu, kumaanisha kwamba Atarejesha mamlaka Yake duniani na kurejesha mamlaka Yake miongoni mwa viumbe vyote. Mwanadamu alipoteza moyo wake wa kumcha Mungu baada ya kupotoshwa na Shetani na kupoteza kazi ambayo kiumbe mmoja wa Mungu anapaswa kuwa nayo, kuwa adui asiyemtii Mungu. Mwanadamu alimilikiwa na Shetani na kufuata amri za Shetani; hivyo Mungu hakuwa na njia ya kufanya kazi miongoni mwa viumbe Wake, na hakuweza zaidi kuwafanya viumbe Wake kumcha. Mwanadamu aliumbwa na Mungu, na anapaswa kumwabudu Mungu, lakini mwanadamu kwa kweli alimpuuza Mungu na kumwabudu Shetani. Shetani alikuwa sanamu katika moyo wa mwanadamu. Hivyo Mungu alipoteza nafasi yake katika moyo wa mwanadamu, kusema kwamba Alipoteza maana ya uumbaji Wake wa mwanadamu, na ili kurejesha maana ya uumbaji Wake wa mwanadamu lazima arejeshe mfano wa awali wa mwanadamu na kumtoa mwanadamu tabia yake potovu. Ili kumrejesha mwanadamu kutoka kwa Shetani, lazima Amwokoe mwanadamu kutoka kwa dhambi. Kwa njia hii tu ndiyo Anaweza kurejesha mfano wa awali wa mwanadamu polepole na kurejesha kazi halisi ya mwanadamu, na mwishowe kurejesha ufalme Wake. Maangamizo ya mwisho ya wale wana wa uasi pia yatafanywa ili kumruhusu mwanadamu kumwabudu Mungu vizuri zaidi na kuishi duniani vizuri zaidi. Kwa sababu Mungu alimuumba mwanadamu, Atamfanya mwanadamu amwabudu; kwa sababu Anataka kurejesha kazi halisi ya mwanadamu, Atairejesha kabisa, na bila ughushi wowote. Kurudisha mamlaka Yake kunamaanisha kumfanya mwanadamu amwabudu na kumfanya mwanadamu amtii; kunamaanisha kwamba Atamfanya mwanadamu aishi kwa sababu Yake na kufanya adui zake waangamie kwa sababu ya mamlaka Yake; kunamaanisha kwamba Atafanya kila sehemu Yake kuendelea miongoni mwa binadamu na bila upinzani wowote wa mwanadamu. Ufalme Anaotaka kuanzisha ni ufalme Wake Mwenyewe. Binadamu Anaotaka ni wale wanaomwabudu, wale wanaomtii kabisa na wana utukufu Wake. Asipookoa binadamu wapotovu, maana ya uumbaji Wake wa mwanadamu hautakuwa chochote; Hatakuwa na mamlaka yoyote miongoni mwa mwanadamu, na ufalme Wake hautaweza kuweko tena duniani. Asipoangamiza wale adui wasiomtii, Hataweza kupata utukufu Wake wote, wala Hataweza kuanzisha ufalme Wake duniani. Hizi ndizo ishara za ukamilishaji wa kazi Yake na ishara za ukamilishaji wa utimilifu Wake mkubwa; kuangamiza kabisa wale miongoni mwa binadamu wasiomtii, na kuwaleta wale waliokamilika rahani. Wakati binadamu wamerejeshwa katika mfano wake wa awali, wakati binadamu wanaweza kutimiza kazi yao husika, kuwa na nafasi zao wenyewe na kutii mipango yote ya Mungu, Mungu atakuwa amepata kundi la watu duniani wanaomwabudu, na Atakuwa pia Ameanzisha ufalme duniani unaomwabudu. Atakuwa na ushindi wa milele duniani, na wale wanaompinga wataangamia milele. Hii itarejesha nia Yake ya asili ya kumuumba mwanadamu; itarejesha nia Yake ya kuumba vitu vyote, na pia itarejesha mamlaka Yake duniani, mamlaka Yake miongoni mwa vitu vyote na mamlaka yake miongoni mwa adui Zake. Hizi ni ishara za ushindi Wake wote. Tangu sasa na kwendelea binadamu wataingia katika raha na kuingia katika maisha yafuatayo njia sahihi. Mungu pia ataingia katika raha ya milele na mwanadamu na kuingia katika maisha ya milele yanayoshirikisha Mungu na mwanadamu. Uchafu na kutotii duniani vitatoweka, na pia maombolezo duniani. Wote walio duniani wanaompinga Mungu hawatakuweko. Mungu na wale Aliowaokoa pekee ndio watabaki; viumbe Wake tu ndio watabaki.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Mungu na Mwanadamu Wataingia Rahani Pamoja

Baada ya kufanya kazi Yake ya miaka 6,000 hadi leo, Mungu tayari amefichua matendo Yake mengi, sababu ya msingi ikiwa ni kumshinda Shetani na kuleta wokovu kwa binadamu wote. Anatumia fursa hii kuruhusu kila kitu mbinguni, kila kitu kilicho duniani, kila kitu kinachopatikana baharini, pamoja na kila kitu cha mwisho ambacho Mungu alikiumba ulimwenguni kiweze kuona uweza wa Mungu na kushuhudia matendo yote ya Mungu. Anachukua fursa ya kumshinda Shetani ili kufichua matendo Yake kwa binadamu na kuwaruhusu watu waweze kumsifu Yeye na kuitukuza hekima Yake kwa kumshinda Shetani. Vitu vyote vilivyomo duniani, mbinguni na ndani ya bahari vinamletea utukufu, vinasifu uweza Wake, vinasifu matendo Yake yote na kutamka kwa sauti jina Lake takatifu. Huu ni uthibitisho wa ushindi Wake dhidi ya Shetani; huu ni uthibitisho wa Yeye kumshinda Shetani; na la muhimu zaidi, ni uthibitisho wa wokovu Wake kwa binadamu. Viumbe vyote vya Mungu vinamletea utukufu, vinamsifu Yeye kwa kumshinda adui Yake na kurudi kwa ushindi, na vinamsifu Yeye kama Mfalme mkuu Aliyeshinda. Dhumuni Lake si kumshinda Shetani tu, na ndio maana kazi Yake imeendelea kwa miaka 6,000. Anatumia kushindwa kwa Shetani kuwaokoa binadamu; Anakutumia kushindwa kwa Shetani kufichua vitendo Vyake vyote na kufichua utukufu Wake wote. Atapata utukufu, na umati wote wa malaika utaweza kushuhudia utukufu Wake wote. Wajumbe walio mbinguni, wanadamu walio duniani na viumbe wote walio duniani watauona utukufu wa Muumba. Hii ndiyo kazi Aifanyayo. Viumbe vyake kule mbinguni na duniani vyote vitauona utukufu Wake, na Atarudi kwa ushindi baada ya kumshinda Shetani kabisa na kuwaruhusu binadamu wamsifu Yeye, kwa hivyo Atapata ushindi maradufu katika kazi Yake. Hatimaye binadamu wote watashindwa na Yeye, na Atamwondoa yeyote yule anayepinga au kuasi, hivi ni kusema, Atawaondoa wale wote wanaomilikiwa na Shetani.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Unapaswa Kujua Namna Ambavyo Binadamu Wote Wameendelea Hadi Siku ya Leo

Iliyotangulia: 1. Ni kwa Nini Mungu Hufanya Kazi ya Kumuokoa Mwanadamu?

Inayofuata: 3. Kusudi na Umuhimu wa Kazi ya Mungu katika Enzi ya Sheria

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp