1. Mwenyezi Mungu Ndiye Mungu Mmoja wa Kweli Anayetawala Juu ya Vitu Vyote

Maneno Husika ya Mungu:

Kila kitu cha ulimwengu huu kinabadilika haraka sawasawa na mawazo ya Mwenyezi, na chini ya macho Yake. Mambo ambayo wanadamu hawajawahi kuyasikia yanaweza kuja kwa ghafla, ilhali vitu ambavyo wanadamu wamevimiliki kwa muda mrefu vinaweza kutoweka bila wao kujua. Hakuna anayeweza kutambua mahali alipo Mwenyezi, sembuse mtu yeyote anayeweza kuhisi kule kwenda zaidi ya uwezo wa binadamu na ukuu wa nguvu za maisha za Mwenyezi. Yeye ni Mkuu kwa kuwa Anaweza kutambua kile ambacho wanadamu hawawezi. Yeye ni Mkuu kwa kuwani Yeye anayekataliwa na wanadamu na bado Anawaokoa wanadamu. Yeye anajua maana ya uzima na mauti na, isitoshe, Anajua sheria za kuishi ambazo wanadamu, ambao wameumbwa, wanapaswa kuzifuata. Yeye ndiye msingi wa kuwepo kwa mwanadamu, na Yeye ndiye Mkombozi anayewafufua wanadamu tena. Anailemea mioyo yenye furaha kwa huzuni, na kuiinua mioyo yenye huzuni kwa furaha, yote ni kwa ajili ya kazi Yake, na kwa ajili ya mpango Wake.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kutanafusi kwa Mwenye Uweza

Katika upana wa ulimwengu na anga, viumbe wasiohesabika wanaishi na kuzaliana, hufuata sheria ya mzunguko wa maisha na kufuata sheria isiyobadilika. Wanaokufa huenda na hadithi za walio hai, na walio hai hurudia historia hii yenye huzuni ya wale waliokufa. Na kwa hivyo wanadamu hawawezi kujizuia ila kujiuliza wenyewe; Kwa nini tunaishi? Na kwa nini inatulazimu kufa? Nani anayeitawala dunia hii? Na ni nani aliyemuumba mwanadamu huyu? Je, kweli wanadamu waliumbwa na mazingira asilia? Je, kweli wanadamu wana uamuzi juu ya hatima yao? … Wanadamu hawajui kabisa Mkuu wa ulimwengu na vitu vyote ni nani, sembuse kujua mwanzo na mustakabali wa wanadamu. Wanadamu wanaishi tu, bila budi, katikati ya hii sheria. Hakuna anayeweza kuiepuka wala kuibadilisha kwani katika vitu vyote na katika mbingu kuna Mmoja kutoka milele hadi milele ambaye ni Mkuu wa kila kitu. Ni Yeye ambaye Hajawahi kuonekana na mwanadamu, ambaye wanadamu hawajawahi kumjua, ambaye wanadamu hawajawahi kuamini kuwepo Kwake, na bado ni Yeye Aliyewapulizia pumzi mababu wa wanadamu na kuwapa wanadamu uhai. Ni Yeye ndiye Huruzuku na kustawisha wanadamu kwa kuishi kwao, na huwaongoza wanadamu hadi siku ya leo. Aidha, Yeye na Yeye pekee ni wa kutegemewa na wanadamu ili kuendelea kuishi. Ni Mkuu wa kila kitu na Hutawala viumbe vyote vyenye uhai chini ya dunia. Huamrisha misimu yote minne, na ni Yeye huita upepo, jalidi, theluji na mvua. Huwapa wanadamu mwangaza wa jua na huleta machweo ya jioni. Ni Yeye Aliyeumba mbingu na ardhi, Akampa mwanadamu milima, maziwa na mito na kila kitu kilicho na uhai ndani yake. Matendo Yake yako kila mahali, nguvu Zake ziko kila mahali, busara Zake ziko kila mahali na mamlaka Yake yako kila mahali. Kila mojawapo ya hizi sheria na kanuni ni mfano mzuri wa matendo Yake, na kila mojawapo inafichua hekima na mamlaka Yake. Nani anayeweza kujiondoa kutoka kwa ukuu Wake? Na ni nani anayeweza kujitoa mwenyewe katika njia Zake? Kila kitu kinaishi chini ya uangalizi Wake, zaidi ya hayo, kila kitu huishi chini ya ukuu Wake. Matendo na nguvu Zake huwaacha wanadamu bila chaguo ila kutambua ukweli kwamba ni Yeye pekee Anayeishi na Ana ukuu juu ya kila kitu. Hakuna kitu chochote ila Yeye kinachoweza kuamuru dunia, wala kuwajibikia wanadamu bila kukoma. Bila kujali kama unaweza kutambua vitendo vya Mungu, bila kujali kama unaamini katika kuwepo kwa Mungu, hakuna shaka kuwa hatima yako inaegemea katika mipango ya Mungu, na hakuna shaka kuwa Mungu atakuwa na ukuu juu ya kila kitu. Uwepo na utawala Wake haviwezi kutabiriwa ikiwa vinatambulika na kufahamika na binadamu au la. Ni Yeye pekee Anayejua kuhusu yaliyopita ya mwanadamu, yaliyopo na yanayojiri, na Yeye pekee ndiye mwamuzi wa hatima ya wanadamu. Haijalishi kama unaukubali huu ukweli, haitachukua muda mrefu kabla mwanadamu kushuhudia haya yote kwa macho yake mwenyewe, na huu ni ukweli ambao hivi karibu Mungu Ataudhihirisha. Wanadamu huishi na hufa chini ya macho yake Mungu. Wanadamu anaishi kwa ajili ya usimamizi wa Mungu, na macho Yake yanapofumba kwa mara ya mwisho, hiyo pia ni kwa ajili ya usimamizi huo huo. Tena na tena, mwanadamu huja na kwenda, nyuma na mbele. Bila mapendeleo, yote ni sehemu ya mamlaka ya Mungu na muundo Wake. Usimamizi wa Mungu unaendelea mbele kwa kudumu; haujawahi kusimama. Atawafanya wanadamu wafahamu uwepo Wake, waamini katika mamlaka Yake, watazame matendo Yake, na warudi katika ufalme Wake. Huu ndio mpango Wake, na kazi ambayo Amekuwa akiitekeleza kwa maelfu ya miaka.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kiambatisho 3: Mwanadamu Anaweza tu Kuokolewa Katikati ya Usimamizi wa Mungu

Njia ya uzima si kitu ambacho mtu yeyote anaweza kumiliki, wala si kitu ambacho kila mtu anaweza kufikia kwa urahisi. Hii ni kwa sababu uzima unaweza kutoka tu kwa Mungu, ambayo ni kusema, ni Mungu Mwenyewe pekee ndiye Anayemiliki kiini cha uzima, na ni Mungu Mwenyewe pekee aliye na njia ya uzima. Na hivyo Mungu tu ndiye chanzo cha uzima, na kijito cha maji ya uzima kinachotiririka nyakati zote. Tangu uumbaji wa dunia, Mungu amefanya kazi kubwa sana inayobeba pamoja nayo uzima uhai wa uzima, Amefanya kazi nyingi ambayo inamletea mwanadamu uzima, na Amelipa gharama kubwa inayomwezesha mwanadamu apate uzima. Hii ni kwa sababu Mungu Mwenyewe ni uzima wa milele, na Mungu Mwenyewe ndiye njia ambayo kwayo mwanadamu anaweza kufufuliwa. Mungu kamwe hajawahi kosa kuwepo moyoni mwa mwanadamu, na Anaishi miongoni mwa wanadamu wakati wote. Yeye ndiye nguvu ya kuendesha maisha ya mwanadamu, chanzo cha kuendelea kuishi kwa mwanadamu, na rasilmali kubwa ya kuwepo kwa mwanadamu baada ya kuzaliwa. Yeye huwasababisha watu kuzaliwa upya, na kuwawezesha kuishi kwa ushupavu katika jukumu lao binafsi. Akitegemea uwezo Wake, na nguvu Yake ya uzima isiyozima, mwanadamu ameishi kwa kizazi baada ya kizazi, huku nguvu ya uzima wa Mungu imekuwa ikitoa utegemezi miongoni mwa binadamu, na Mungu amelipa gharama ambayo hakuna mtu wa kawaida amewahi kulipa. Nguvu za Mungu za maisha zinaweza kutawala juu ya nguvu zozote; hata zaidi ya hayo, zinapita mamlaka yoyote. Uzima Wake ni wa milele, nguvu Zake ni za ajabu, na nguvu Zake za uzima haziwezi kuzidiwa na kiumbe yeyote au nguvu za adui. Nguvu za uzima wa Mungu zipo na hung’aa kwa mwangaza ulio mzuri sana, bila kujali muda au mahali. Mbingu na dunia zinaweza kupitia mabadiliko ya ajabu, lakini uzima wa Mungu ni ule ule daima. Mambo yote yanaweza kupita, lakini uzima wa Mungu bado utakuwepo. Hii ni kwa sababu Mungu ndiye chanzo cha kuwepo kwa vitu vyote, na mzizi unaotegemewa na kila kitu ili kiendelee kuishi. Asili ya maisha ya mwanadamu hutoka kwa Mungu, kuwepo kwa mbingu ni kwa sababu ya Mungu, na kuwepo kwa ardhi kunatokana na nguvu ya uhai wa Mungu. Hakuna kitu kinachomiliki nguvu kinachoweza kuzidi ukuu wa Mungu, na hakuna kitu chenye nguvu kinachoweza kuvunja mipaka ya mamlaka ya Mungu. Kwa njia hii, bila kujali wao ni nani, kila mtu lazima ajiwasilishe kwa utawala wa Mungu, kila mtu lazima aishi chini ya amri za Mungu, na hakuna mtu anayeweza kutoroka kutoka katika utawala Wake.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Ni Kristo wa Siku za Mwisho Pekee Ndiye Anayeweza Kumpa Mwanadamu Njia ya Uzima wa Milele

Kabla ya binadamu hawa kuwepo, viumbe vyote—sayari zote, nyota zote kule mbinguni—tayari vilikuwepo. Kwenye kiwango cha vitu vikubwa, vyombo hivi vya mbinguni vimekuwa vikizunguka mara kwa mara chini ya udhibiti wa Mungu, kwa kuwepo kwao kote, hata hivyo miaka mingi imepita. Ni sayari gani inaenda wapi na wakati gani haswa; ni sayari gani inafanya kazi gani, na lini; ni sayari gani inazunguka katika mzingo gani, na ni lini inatoweka au inabadilishwa—vitu hivi vyote vinasonga mbele bila ya kosa lolote dogo. Nafasi za sayari na umbali kati yazo ni masuala yanayofuata mifumo maalum, ni masuala ambayo yanaweza kufafanuliwa kwa data sahihi; njia ambazo zinasafiria, kasi na mifumo ya mizunguko yao, nyakati ambapo zinapatikana kwenye nafasi mbalimbali zinaweza kufafanuliwa kwa usahihi na kufafanuliwa kwa sheria maalum. Kwa miaka na mikaka sayari zimefuata sheria hizi na hazijawahi kukosea hata kidogo. Hakuna nguvu inayoweza kubadilisha au kuharibu njia zao au mifumo ambayo zinafuata. Kwa sababu sheria maalum ambazo zinaongoza mizunguko yao na data maalum inayozifafanua ziliamuliwa kabla na mamlaka ya Muumba, zinatii sheria hizi zenyewe, kulingana na ukuu na udhibiti wa Muumba. Kwenye kiwango cha mambo makubwamakubwa, si vigumu kwa binadamu kujua zaidi kuhusu mifumo fulani, data fulani, pamoja na sheria au matukio fulani yasiyoeleweka au yasiyoelezeka. Ingawaje binadamu hawakubali kwamba Mungu yupo, haukubali hoja kwamba Muumba aliumba na anatawala kila kitu na zaidi ya yote hautambui uwepo wa mamlaka ya Muumba, wanasayansi wa kibinadamu, wanafalaki, nao wanafizikia wanachunguza na kugundua zaidi na zaidi kwamba uwepo wa kila kitu kwenye ulimwengu, na kanuni na mifumo inayoamuru mizunguko yao, vyote vinatawaliwa na kudhibitiwa na nishati nyeusi kubwa na isiyoonekana. Ukweli huu unamlazimisha mwanadamu kukabiliana na kukiri kwamba kuna Mwenye Nguvu katikati ya mifumo hii ya mizunguko, Anayepangilia kila kitu. Nguvu zake si za kawaida, na ingawaje hakuna anayeweza kuona uso Wake wa kweli, Yeye hutawala na kudhibiti kila kitu kila dakika. Hakuna binadamu au nguvu zozote zile zinazoweza kuuzidi ukuu Wake. Huku binadamu akiwa amekabiliwa na hoja hii, lazima atambue kwamba sheria zinazotawala uwepo wa kila kitu haziwezi kudhibitiwa na binadamu, haziwezi kubadilishwa na yeyote; na wakati uo huo binadamu lazima akubali kwamba, binadamu hawezi kuelewa kikamilifu sheria hizi. Na hizi sheria hazitokei kiasili lakini zinaamrishwa na Mtawala. Haya yote ni maonyesho na mamlaka ya Mungu yanayoonyesha kwamba mwanadamu anaweza kuelewa katika kiwango cha mambo makubwa.

Kwenye kiwango cha mambo madogomadogo, milima, mito, maziwa, bahari, na maeneo ya ardhi yote ambayo binadamu anatazama nchini, misimu yote ambayo yeye anapitia, mambo yote yanayopatikana kwenye ulimwengu, kukiwemo mimea, wanyama, vijiumbe na binadamu, vyote viko chini ya ukuu wa Mungu na vinadhibitiwa na Mungu Mwenyewe. Katika ukuu na udhibiti wa Mungu, vitu vyote vinakuwepo au vinatoweka kulingana na fikira Zake, maisha ya vitu hivi yanatawaliwa na sheria fulani, na vinakua na kuzaana kulingana nazo. Hakuna binadamu au kiumbe chochote kilicho juu ya sheria hizi.

Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee III

Mungu alipoviumba vitu vyote, Aliweka mipaka kwa ajili ya milima, tambarare, majangwa, vilima, mito, na maziwa. Duniani kuna milima, tambarare, majangwa, vilima, vilevile vyanzo mbalimbali vya maji. Je, hayo si mandhari tofautitofauti? Mungu aliweka mipaka kati ya mandhari haya yote tofautitofauti. Tunapozungumza juu ya kuweka mipaka, ina maana kwamba milima ina mipaka yake, tambarare zina mipaka yake, majangwa yana mawanda fulani, na vilima vina eneo mahususi. Pia kuna kiwango mahususi cha vyanzo vya maji kama vile mito na maziwa. Yaani, Mungu alipoumba vitu vyote aligawanya kila kitu vizuri kabisa. … Ndani ya mandhari haya yote tofautitofauti na mazingira ya kijiografia yaliyoumbwa na Mungu, Anasimamia kila kitu kwa njia iliyopangwa na kwa mpangilio. Kwa hiyo mazingira haya yote ya kijiografia bado yapo kwa miaka elfu kadhaa, makumi elfu ya miaka baada ya kuwa yameumbwa na Mungu. Bado yanatimiza kila wajibu wao. Ingawa wakati wa vipindi fulani volkano hulipuka, wakati wa vipindi fulani matetemeko ya ardhi hutokea, na kuna mabadiliko makubwa ya ardhi, hakika Mungu hataruhusu aina yoyote ya mandhari kupoteza kazi yake ya asili. Ni kwa sababu tu ya usimamizi huu unaofanywa na Mungu, utawala Wake na udhibiti wa sheria hizi, kwamba yote haya—yote haya yanayofurahiwa na binadamu na kuonwa na binadamu—yanaweza kuendelea kuwepo duniani kwa njia ya mpangilio. …

…………

… kando na kuanzisha mipaka kwa ajili ya mazingira mbalimbali ya kijiografia, Mungu pia Aliweka mipaka kwa ajili ya ndege na wanyama, samaki, wadudu mbalimbali, na mimea yote. Pia alianzisha sheria. Kwa sababu ya tofauti za mazingira mbalimbali ya kijiografia na kwa sababu ya uwepo wa mazingira tofauti ya kijiografia, aina tofautitofauti za ndege na wanyama, samaki, wadudu, na mimea vina mazingira tofauti kwa ajili ya kuendelea kuishi. Ndege na wanyama na wadudu huishi katikati ya mimea mbalimbali, samaki wanaishi majini, na mimea inakua kwenye nchi kavu. … vitu vyote vilivyoumbwa na Mungu—haijalishi kama vimewekwa katika sehemu moja au iwapo vinapumua kupitia pua—vina sheria zao kwa ajili ya kuendelea kuishi. Zamani kabla Mungu hajaumba viumbe hai hivi Alikuwa ameviandalia makazi yao, mazingira yao kwa ajili ya kuendelea kuishi. Viumbe hai hivi vilikuwa na mazingira yao yasiyobadilika kwa ajili ya kuendelea kuishi, chakula chao, makazi yao yasiyobadilika, sehemu zao zisizobadilika zinazowafaa kwa ajili ya kuendelea kuishi, maeneo yenye halijoto inayowafaa kwa ajili ya kuendelea kuishi. Kwa njia hiyo wasingezungukazunguka au kudhoofisha hali ya mwanadamu kuendelea kuishi au kuathiri maisha yao. Hivi ndivyo Mungu anavyoongoza vitu vyote, akiwaandalia wanadamu mazingira mazuri kabisa kwa ajili ya kuendelea kuishi. Viumbe hai chini ya vitu vyote kila kimoja kina chakula chao kinachokimu maisha yao wenyewe ndani ya mazingira yao wenyewe kwa ajili ya kuendelea kuishi. Kwa chakula hicho, vinajifunga katika mazingira yao ya asili kwa ajili ya kuendelea kuishi. Katika aina hiyo ya mazingira bado vinaendelea kuishi, kuzaliana, na kuendelea kulingana na sheria za Mungu alizozianzisha kwa ajili yao. Kwa sababu ya aina hizi za sheria, kwa sababu ya majaaliwa ya Mungu, vitu vyote vinaishi kwa upatanifu na wanadamu, na wanadamu huishi pamoja na vitu vyote kwa kutegemeana.

Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee IX

Kuanzia wakati unapokuja ulimwenguni humu ukilia, unaanza kutimiza majukumu yako. Kwa ajili ya mpango wa Mungu na kutawaza Kwake, unafanya wajibu wako na kuanza safari yako ya maisha. Haijalishi ulikokulia kulivyo, na haijalishi safari iliyo mbele yako ilivyo, kwa vyovyote vile, hakuna anayeweza kuepuka mipango na mipangilio ya Mbinguni, na hakuna anayeweza kudhibiti hatima yake mwenyewe, kwani ni Yeye tu aliye na mamlaka juu ya vitu vyote ndiye Anayeweza kufanya kazi hiyo. Tangu kuwepo kwa mwanadamu hapo mwanzo, Mungu daima amekuwa Akifanya kazi Yake kwa namna hii, Akiusimamia ulimwengu, na kuelekeza sheria za mabadiliko kwa vitu vyote na mweleke wa kusonga kwao. Kama vitu vyote, mwanadamu kwa ukimya na bila kujua anastawishwa kwa utamu na mvua na umande kutoka kwa Mungu; kama vitu vyote, mwanadamu bila kujua, anaishi chini ya mpango wa mkono wa Mungu. Moyo na roho ya mwanadamu vimo katika mshiko wa Mungu, na kila kitu cha maisha yake kinatazamwa machoni pa Mungu. Bila kujali kama unaamini haya yote au la, chochote na vitu vyote, viwe vilivyohai au vilivyokufa, vitahamishwa, vitabadilishwa, kufanywa vipya, na kupotea kulingana na fikira za Mungu. Hivi ndivyo ambavyo Mungu anashikilia mamlaka juu ya vitu vyote.

Usiku unapoingia polepole, mwanadamu huwa hafahamu, kwani moyo wa mwanadamu hauwezi kujua jinsi giza linavyoingia au ni wapi linakotokea. Usiku unapotoweka polepole, mwanadamu hukaribisha mwanga wa mchana, lakini kuhusu mahali ambapo nuru imetokea, na jinsi imeliondoa giza la usiku, mwanadamu anajua machache, na hata anafahamu mchache zaidi Mabadiliko haya ya kawaida ya mchana na usiku humpitisha mwanadamu kutoka kipindi kimoja hadi kingine, kutoka kipindi kimoja cha kihistoria hadi kingine, wakati huu wote zinahakikisha kwamba kazi ya Mungu katika kila kipindi na mpango Wake wa kila enzi unatekelezwa.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Mungu Ndiye Chanzo cha Uzima wa Mwanadamu

Tangu uumbaji wa ulimwengu Nimeanza kuamulia kabla na kuchagua kundi hili la watu, yaani, ninyi leo. Tabia yako, ubora wa tabia, sura, kimo, familia ambayo ulizaliwa kwayo, kazi yako na ndoa yako, nafsi yako yote, hata rangi ya nywele zako na ngozi yako, na wakati wa kuzaliwa kwako vyote vilipangwa na mikono Yangu. Hata mambo unayofanya na watu unaokutana nao kila siku hupangwa na mikono Yangu, sembuse ukweli kwamba kukuleta katika uwepo Wangu leo kwa kweli ni mpango Wangu. Usijitupe katika vurugu; unapaswa kuendelea kwa utulivu.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 74

Hatima za binadamu na zile za ulimwengu zimeingiliana kwa undani na ukuu wa Muumba, zimefungamanishwa na haziwezi kutenganishwa na mipango ya Muumba; na hatimaye, haziwezi kutenganishwa na mamlaka ya Muumba. Kupitia kwenye sheria za mambo yote binadamu huja kuelewa mipango ya Muumba na ukuu Wake; kupitia kwenye sheria za namna ya kuishi ambazo anaona katika utawala wa Muumba; kutoka kwenye hatima za mambo yote anapata hitimisho kuhusu njia ambazo Muumba huonyesha ukuu Wake na kuvidhibiti; na katika mizunguko ya maisha ya wanadamu na vitu vyote, mwanadamu kwa kweli huja kupitia ile mipango na mipangilio ya Muumba kwa mambo yote na kwa viumbe vyote vilivyo hai na anashuhudia kwa kweli namna ambavyo mipango na mipangilio hiyo inavyozidi sheria zote za nchi, kanuni, na taasisi, mamlaka na nguvu zingine zote. Kwa mujibu wa haya, binadamu wanashawishiwa kutambua kwamba, ukuu wa Muumba hauwezi kukiukwa na kiumbe chochote kilichoumbwa, kwamba hakuna nguvu zinazoweza kuharibu au kubadilisha matukio na mambo yaliyoamuliwa kabla na Muumba. Ni kupitia kwenye sheria na kanuni hizi takatifu ambapo binadamu na viumbe vyote wanaweza kuishi na kuzaliana, kizazi baada ya kizazi. Je, huu si mfano halisi wa mamlaka ya Muumba?

Neno, Vol. 2. Kuhusu Kumjua Mungu. Mungu Mwenyewe, Yule wa Kipekee III

Mungu Ana Mamlaka Juu ya Hatima ya Wanadamu Wote

(Sura Iliyochaguliwa ya Neno la Mungu)

Kama washiriki wa jamii ya wanadamu na Wakristo waaminifu, ni jukumu na wajibu wetu sote kutoa akili na miili yetu kwa ajili ya kutimiza agizo la Mungu, kwa maana asili yetu yote inatoka kwa Mungu, na tunaishi kwa sababu ya ukuu wa Mungu. Kama akili na miili yetu haipo kwa ajili ya agizo la Mungu na kwa ajili ya kusudi la haki ya wanadamu, basi roho zetu hazitastahili mbele ya wale waliokufa kishahidi kwa ajili ya agizo la Mungu, na zaidi sana hazistahili kwa Mungu, aliyetupa kila kitu.

Mungu aliumba ulimwengu huu, Alimuumba mwanadamu huyu na, zaidi ya hayo, Alikuwa muasisi wa utamaduni wa kale wa Kigiriki na ustaarabu wa binadamu. Ni Mungu pekee Anayewafariji wanadamu hawa, na ni Mungu pekee Anayewajali wanadamu hawa usiku na mchana. Ukuaji na maendeleo ya binadamu hayatenganishwi na ukuu wa Mungu, na historia na mustakabali wa mwanadamu hauwezi kuepuka mipango inayofanywa na mikono ya Mungu. Kama wewe ni Mkristo wa kweli, basi kwa hakika utaamini kwamba kupanda na kushuka kwa nchi ama taifa lolote kunafanyika chini ya mipango ya Mungu. Mungu pekee ndiye Anayejua hatima ya nchi ama taifa lolote, na ni Mungu pekee ndiye Anayedhibiti mwenendo wa wanadamu hawa. Ikiwa wanadamu wanataka kuwa na hatima nzuri, ikiwa nchi inataka kuwa na hatima nzuri, basi mwanadamu lazima amsujudie Mungu katika ibada, na aje mbele za Mungu akitubu na kuungama, kama sivyo majaliwa na hatima ya mwanadamu hayataepuka kumalizika kwa janga.

Angalia nyuma wakati Nuhu alipojenga safina: Wanadamu walikuwa wamepotoka sana, walikuwa wamepotea kutoka katika baraka za Mungu, hawakuwa wanatunzwa na Mungu tena, na walikuwa wamepoteza ahadi za Mungu. Waliishi gizani, bila mwangaza wa Mungu. Hivyo wakawa waasherati kwa asili, wakajiachilia katika mkengeuko wa kutisha. Watu kama hao hawangeweza tena kupokea ahadi za Mungu; hawakufaa kushuhudia uso wa Mungu, wala kusikia sauti ya Mungu, kwani walikuwa wamemwacha Mungu, waliweka kando yote Aliyowapa, na kusahau mafunzo ya Mungu. Mioyo yao ilienda mbali zaidi na zaidi kutoka kwa Mungu, na ilivyofanya hivyo, wakawa wapotovu zaidi ya mantiki na ubinadamu wote na wakazidi kuwa waovu. Hivyo walisogelea kifo zaidi, na kukabiliwa na ghadhabu na adhabu ya Mungu. Ni Nuhu tu aliyemwabudu Mungu na kuepukana na uovu, na hivyo aliweza kusikia sauti ya Mungu, na kusikia maagizo ya Mungu. Alijenga safina kulingana na maagizo ya neno la Mungu, na akakusanya aina zote za viumbe hai. Na kwa njia hii, wakati kila kitu kilikuwa kimetayarishwa, Mungu aliangamiza dunia. Nuhu tu na wanachama saba wa familia yake walinusurika maangamizi, kwani Nuhu alimwabudu Yehova na kuepukana na uovu.

Kisha angalia enzi ya sasa: Hawa watu wenye haki kama Nuhu, ambao wangeweza kumwabudu Mungu na kuepuka uovu, wamekoma kuwepo. Lakini bado Mungu ana fadhili kwa mwanadamu huyu, na Anamsamehe mwanadamu wakati huu wa enzi ya mwisho. Mungu anawatafuta wale wanaotamani Aonekane. Anawatafuta wale wanaoweza kuyasikia maneno Yake, wale ambao hawajasahau agizo Lake na wanatoa mioyo na miili yao Kwake. Anawatafuta wale walio watiifu kama watoto wachanga mbele Zake, na hawampingi. Kama hujazuiliwa na nguvu zozote katika ibada yako Kwake, basi Mungu atakutazama kwa upendeleo na Ataweka baraka Zake juu yako. Kama wewe ni wa cheo cha juu, mwenye sifa ya kuheshimika, mwenye maarifa mengi, mwenye mali nyingi, na kuungwa mkono na watu wengi, lakini mambo haya hayakuzuii kuja mbele za Mungu kuukubali wito Wake na agizo Lake, kufanya kile Mungu anachokuambia ufanye, basi yote unayoyafanya yatakuwa yenye umuhimu zaidi duniani na yenye haki zaidi kwa binadamu. Ukiukataa wito wa Mungu kwa sababu ya hadhi yako na malengo yako mwenyewe, yote utakayoyafanya yatalaaniwa na hata kudharauliwa na Mungu. Pengine wewe ni rais, ama mwanasayansi, ama mchungaji, ama mzee, lakini bila kujali ukuu wa ofisi yako, ukitegemea maarifa yako na uwezo katika shughuli zako, basi daima utakuwa wa kushindwa na kamwe utanyimwa baraka za Mungu, kwa sababu Mungu hakubali chochote unachofanya, na Hakubali kwamba kazi yako ni yenye haki, wala kukubali kwamba unafanya kazi kwa manufaa ya wanadamu. Atasema kwamba kila kitu unachofanya, ni kutumia maarifa na nguvu za wanadamu ili kumwondolea mwanadamu ulinzi wa Mungu, ambapo ni kukataa baraka za Mungu. Atasema kuwa unamwongoza mwanadamu kuelekea gizani, kuelekea kifo, na kuelekea mwanzo wa maisha yasiyo na mipaka ambapo mwanadamu amempoteza Mungu na baraka Zake.

Tangu uvumbuzi wa wanadamu wa sayansi ya kijamii, akili ya mwanadamu imechukuliwa na sayansi na maarifa. Kisha sayansi na maarifa zikawa zana za kuwatawala wanadamu, na hakuna tena nafasi ya kutosha kwa mwanadamu kumwabudu Mungu, na hakuna hali nzuri zaidi kwa kumwabudu Mungu. Nafasi ya Mungu ikashuka chini kabisa katika moyo wa mwanadamu. Bila Mungu mioyoni mwao, ulimwengu wa ndani wa mwanadamu ni giza, usio na tumaini na ni mtupu. Na hivyo kukatokea wanasayansi wa jamii, wataalamu wa historia na wanasiasa wengi kueleza nadharia ya sayansi ya jamii, nadharia ya mageuko ya binadamu, na nadharia nyingine zinazopinga ukweli kwamba Mungu alimuumba mwanadamu, ilikujaza mioyo na akili za wanadamu. Na kwa njia hii, wanaoamini kwamba Mungu aliumba kila kitu wanakuwa wachache zaidi, na wale wanaoamini nadharia ya mageuko wanakuwa hata wengi kwa nambari. Watu zaidi na zaidi wanachukulia rekodi za kazi ya Mungu na maneno Yake wakati wa enzi ya Agano la Kale kuwa hadithi na hekaya. Katika mioyo yao, watu wanakuwa wasiojali adhama na ukuu wa Mungu, wasiojali kwamba Mungu yupo, na kanuni kwamba Mungu ana ukuu juu ya vitu vyote. Kuendelea kuishi kwa wanadamu na hatima ya nchi na mataifa si muhimu tena kwao, na mwanadamu anaishi katika ulimwengu ulio mtupu unaojishughulisha tu na kula, kunywa, na kutafuta raha. … Ni watu wachache wanaojishughulisha kutafuta mahali ambapo Mungu anafanya kazi Yake leo, au kutafuta jinsi Anavyosimamia na kupanga hatima ya mwanadamu. Na kwa njia hii, bila ya mwanadamu kujua, ustaarabu wa mwanadamu unashindwa zaidi na zaidi kuendana na matakwa ya mwanadamu, na hata kuna watu wengi zaidi ambao wanahisi kwamba, kuishi katika ulimwengu kama huu, hawana furaha kuliko wale ambao tayari wamekufa. Hata watu wa nchi zilizokuwa na ustaarabu wa hali ya juu wanatoa malalamiko kama hayo. Kwani bila mwongozo wa Mungu, hata kama watawala na wanasosholojia wataumiza akili zao ili kuhifadhi ustaarabu wa mwanadamu, haitakuwa na mafanikio. Hakuna anayeweza kujaza utupu katika moyo wa mwanadamu, kwani hakuna anayeweza kuwa uzima wa mwanadamu, na hakuna nadharia ya kijamii inayoweza kumwokoa kutokana na utupu unaomtesa. Sayansi, maarifa, uhuru, demokrasia, starehe na faraja, haya yote yanamletea mwanadamu faraja ya muda tu. Pamoja na mambo haya, mwanadamu bado haepuki kutenda dhambi na kulalamika kuhusu ukosefu wa haki kwa jamii. Mambo haya hayawezi kupunguza tamaa ya mwanadamu na hamu ya kuchunguza. Kwa sababu mwanadamu aliumbwa na Mungu na kujitoa kwao na uchunguzi usio na maana wa mwanadamu vitamwongoza tu kwenye dhiki zaidi. Mwanadamu daima atakuwa katika hali ya hofu isiyoisha, hatajua jinsi ya kuukabili mustakabali wa wanadamu, ama jinsi ya kuikabili njia iliyo mbele, hadi kufikia kiwango ambacho mwanadamu hata anaogopa sayansi na maarifa, na hata zaidi anahofia hisia ya utupu iliyo ndani yake. Katika ulimwengu huu, bila kujali kama unaishi katika nchi huru ama isiyo na haki za binadamu, huwezi kabisa kuponyoka majaliwa ya mwanadamu. Kama wewe ni kiongozi ama anayeongozwa, huwezi kabisa kuponyoka hamu ya kuchunguza majaliwa, mafumbo, na hatima ya wanadamu, sembuse kuwa na uwezo wa kutoroka hisia ya utupu inayotatiza. Matukio kama haya, yaliyo kawaida kwa wanadamu wote, yanaitwa matukio ya kijamii na wanasosholojia, lakini hakuna mtu mkuu anayeweza kuja kutatua shida kama hizi. Mwanadamu, hata hivyo, ni mwanadamu. Nafasi na maisha ya Mungu hayawezi kubadilishwa na mwanadamu yeyote. Mwanadamu hahitaji tu jamii iliyo na haki, ambapo kila mtu analishwa vyema na ana uhuru na usawa, lakini wokovu wa Mungu na utoaji Wake wa uzima kwa mwanadamu. Ni pale tu mwanadamu anapopokea utoaji wa Mungu wa uzima na wokovu Wake ndipo mahitaji yao, shauku yao ya kuchunguza, na utupu wa mioyo yao utaweza kutatuliwa. Ikiwa watu wa nchi ama taifa hawawezi kupokea wokovu na utunzaji wa Mungu, basi nchi ama taifa kama hilo litatembelea njia inayoelekea uharibifuni, inayoelekea gizani, na litaangamizwa na Mungu.

Pengine nchi yako inafanikiwa kwa sasa, lakini ukiruhusu watu wako waende mbali na Mungu, basi nchi yako itazidi kujipata bila baraka za Mungu. Ustaarabu wa nchi yako utazidi kukanyagiwa chini, na kabla ya muda mrefu watu watamwasi Mungu na kuilaani Mbingu. Kwa njia hii, bila mwanadamu kujua, hatima ya nchi itaharibiwa. Mungu ataziinua nchi zenye nguvu ili kukabiliana na nchi hizo zilizolaaniwa na Mungu, na Anaweza hata kuzifuta kutoka kwa uso wa dunia. Kupanda na kushuka kwa nchi ama taifa kunategemea kama viongozi wao wanamwabudu Mungu, na kama wanawaongoza watu wao karibu na Mungu na kumwabudu. Lakini, katika enzi hii ya mwisho, kwa sababu wale wanaomtafuta na kumwabudu Mungu kwa kweli wanazidi kuwa wachache, Mungu anatoa upendeleo wa pekee kwa nchi ambazo Ukristo ni dini ya serikali. Anazikusanya nchi hizo pamoja ili kuunda kambi ya ulimwengu yenye haki, wakati nchi zisizomwamini Mungu na zile nchi ambazo hazimwabudu Mungu wa kweli zinakuwa wapinzani wa kambi hiyo ya haki. Kwa njia hii, Mungu hana tu mahali miongoni mwa wanadamu pa kufanyia kazi Yake, lakini pia Anapata nchi zinazoweza kutumia mamlaka ya haki, Akiruhusu vizuizi na vikwazo kuwekwa kwa nchi hizo zinazompinga Mungu. Lakini licha ya hayo, bado hakuna watu zaidi wanaokuja kumwabudu Mungu, kwa sababu mwanadamu amepotea mbali sana kutoka Kwake, na mwanadamu amemsahau Mungu kwa muda mrefu sana, na katika dunia hii kumebaki tu nchi ambazo zinatenda haki na kupinga udhalimu. Lakini hii ipo mbali na kufikia matakwa ya Mungu, kwa kuwa hakuna viongozi wa nchi watakaomruhusu Mungu awaongoze watu wao, na hakuna chama cha kisiasa cha nchi kitakachokusanya pamoja watu wake ili wamwabudu Mungu; Mungu amepoteza nafasi Yake inayostahili katika moyo wa kila nchi, taifa, chama tawala, na hata katika moyo wa kila mtu. Ingawa baadhi ya nguvu za haki zipo katika ulimwengu huu, utawala wowote ambao Mungu hana nafasi ndani ya moyo wa mwanadamu ni mdhaifu sana, na uwanja wa kisiasa, ambao hauna baraka za Mungu, upo katika mkanganyiko na hauwezi kustahimili hata pigo moja. Kwa wanadamu, kutokuwa na baraka za Mungu ni sawa na kutokuwa na jua. Bila kujali jinsi watawala wanavyotoa michango kwa bidii kwa watu wao, bila kujali ni mikutano mingapi ya haki ambayo wanadamu wanafanya pamoja, hakuna hata moja kati ya haya litakaloweza kugeuza wimbi hilo au kubadilisha hatima ya wanadamu. Mwanadamu anaamini kwamba nchi ambayo watu wanalishwa na kuvishwa, ambayo watu wanaishi pamoja kwa amani, ndio nchi nzuri, na yenye uongozi mzuri. Lakini Mungu hafikirii hivyo. Anaamini kuwa nchi ambayo hakuna mtu anayemwabudu ndiyo Atakayoiangamiza. Njia ya mwanadamu ya kufikiria ni tofauti kabisa na ya Mungu. Kwa hiyvo, kama mkuu wa nchi hamwabudu Mungu, basi majaliwa ya nchi hii yatakuwa mabaya sana, na nchi hii haitakuwa na hatima.

Mungu hashiriki katika siasa za mwanadamu, lakini majaliwa ya nchi ama taifa yanadhibitiwa na Mungu, Mungu anadhibiti dunia hii na ulimwengu mzima. Majaliwa ya mwanadamu na mpango wa Mungu vimeunganishwa kwa karibu, na hakuna mtu, nchi au taifa linaloweza kuepuka ukuu wa Mungu. Ikiwa mwanadamu anatamani kujua hatima yake, basi lazima aje mbele za Mungu. Mungu atawafanya wanaomfuata na kumwabudu kufanikiwa, na Atawashusha na kuwaangamiza wale wanaompinga na kumkataa.

Kumbuka tukio katika Biblia ambapo Mungu aliangamiza Sodoma, na fikiria pia jinsi mke wa Lutu alivyokuwa nguzo ya chumvi. Fikiria nyuma jinsi watu wa Ninawi walivyotubu dhambi zao wakiwa kwenye magunia na majivu, na kumbuka kilichofuata baada ya Wayahudi kumsulubisha Yesu miaka 2,000 iliyopita. Wayahudi walifukuzwa kutoka Israeli na kukimbilia nchi za ulimwengu. Wengi waliuawa, na taifa zima la Kiyahudi lilipatwa na uchungu usio na kifani wa kuangamizwa kwa nchi yao. Walikuwa wamempigilia Mungu msalabani—walifanya uhalifu wa kutisha—na kuichokoza tabia ya Mungu. Walifanywa kulipia kile walichofanya, na walifanywa kubeba matokeo yote ya vitendo vyao. Walimhukumu Mungu, walimkataa Mungu, na hivyo walikuwa na hatima moja tu: kuadhibiwa na Mungu. Haya ndiyo matokeo machungu na maafa ambayo viongozi wao walileta juu ya nchi na taifa lao.

Leo, Mungu amerudi duniani kufanya kazi Yake. Na kituo Chake cha kwanza katika kazi Yake ni kielelezo cha juu cha udikteta: Uchina, ngome kali ya ukanaji Mungu. Mungu amepata kundi la watu kwa hekima na nguvu Zake. Wakati huu, Anawindwa na chama tawala cha Uchina kwa kila namna na kukabiliwa na mateso ya kila aina, bila mahala pa kupumzisha kichwa Chake na kutoweza kupata makazi. Licha ya haya, Mungu bado anaendelea kufanya kazi Aliyonuia kufanya: Anatamka sauti Yake na kueneza injili. Hakuna anayeweza kuelewa uweza wa Mungu. Uchina, nchi inayomchukulia Mungu kama adui, Mungu hajawahi kukoma kazi Yake. Badala yake, watu wengi zaidi wamekubali kazi na neno Lake, kwani Mungu anafanya yote Awezayo kuokoa kila mshiriki wa ubinadamu. Sote tunaamini kwamba hakuna nchi au nguvu inayoweza kuzuia kile ambacho Mungu anataka kutimiza, na kwamba wale wanaojaribu kuzuia kazi ya Mungu, wanaopinga neno la Mungu, na wale wanaovuruga na kujaribu kuharibu mpango wa Mungu hatimaye wataadhibiwa na Mungu. Mtu yeyote anayepinga kazi ya Mungu atapelekwa kuzimu; nchi yoyote inayoasi kazi ya Mungu itaangamizwa; taifa lolote linaloinuka kupinga kazi ya Mungu litafutwa kutoka kwa dunia hii na Mungu, na litakoma kuwepo. Ninawahimiza watu wa mataifa yote na wa nchi zote, na hata wa tasnia zote wasikilize sauti ya Mungu, waitazame kazi ya Mungu, na wazingatie hatima ya wanadamu, na hivyo kumfanya Mungu kuwa kitu kitakatifu zaidi, chenye kuheshimiwa zaidi, cha juu, na kitu pekee cha kuabudiwa miongoni mwa wanadamu, na kuwawezesha binadamu wote waishi katikati ya baraka za Mungu, kama tu vile uzazi wa Ibrahimu walivyoishi chini ya ahadi ya Yehova, na kama tu vile Adamu na Hawa, ambao Mungu aliwaumba hapo mwanzo, walivyoishi katika Bustani ya Edeni.

Kazi ya Mungu inasonga mbele kama wimbi kubwa. Hakuna anayeweza kumzuia, na hakuna anayeweza kusimamisha mwendo Wake. Ni wale tu wanaosikiliza maneno Yake kwa makini, na wanaomtafuta na kuwa na shauku na Yeye, ndio wanaoweza kufuata nyayo Zake na kupokea ahadi Yake. Wale wasiofanya hivyo watakabiliwa na maafa makubwa na adhabu wanayostahili kabisa.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu

Iliyotangulia: Kutazama Kuonekana kwa Mungu katika Hukumu na Kuadibu Kwake

Inayofuata: 2. Mwenyezi Mungu Ndiye Bwana Yesu Aliyerudi

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp