Kutazama Kuonekana kwa Mungu katika Hukumu na Kuadibu Kwake

Kama mamia ya mamilioni ya wengine wanaomfuata Bwana Yesu Kristo, tunatii sheria na amri za Biblia, tunafurahia neema tele ya Bwana Yesu Kristo, na tunakusanyika pamoja, tunaomba, tunasifu, na tunahudumu katika jina la Bwana Yesu Kristo—na haya yote tunayafanya chini ya utunzaji na ulinzi wa Bwana. Mara nyingi sisi huwa dhaifu, na pia huwa na nguvu mara nyingi. Tunaamini kwamba matendo yetu yote yanalingana na mafundisho ya Bwana. Ni wazi, basi, kwamba sisi pia tunaamini kwamba tuko kwenye njia ya kufuata mapenzi ya Baba wa mbinguni. Tunatamani sana kurudi kwa Bwana Yesu, ujio wa utukufu Wake, mwisho wa maisha yetu duniani, kuonekana kwa ufalme, na kila kitu kama ilivyotabiriwa katika Kitabu cha Ufunuo: Bwana anawasili, Analeta majanga, Anawatuza wema na kuwaadhibu waovu, na Anawachukua juu wale wote wanaomfuata na wanaokaribisha kurudi Kwake ili kukutana na Yeye hewani. Kila tunapofikiria hili, hatuna budi kuzidiwa na hisia, tukiwa na furaha kwamba tulizaliwa katika siku za mwisho na tuna bahati nzuri ya kushuhudia kushuka kwa Bwana. Ingawa tumeteswa, tumepata “uzito wa utukufu unaozidi kuwa mkuu sana na wa milele” kama malipo. Hii ni baraka iliyoje! Kutamani huku kote na neema anayotupa Bwana hutufanya tuwe wenye busara daima katika maombi na kutufanya tuwe na bidii zaidi katika kukusanyika pamoja. Labda mwaka ujao, labda kesho, na labda ndani ya muda mfupi kuliko mwanadamu anavyoweza kufikiria, Bwana atashuka ghafla, Akionekana miongoni mwa kundi la watu ambao wamekuwa wakimsubiri kwa hamu kuu. Tunakimbia kutanguliana, hakuna aliye tayari kubaki nyuma, yote kwa ajili ya kuwa katika kundi la kwanza kutazama kuonekana kwa Bwana, kuwa miongoni mwa wale wanaonyakuliwa. Tumetoa kila kitu, bila kujali gharama, kwa ajili ya kuja kwa siku hii; wengine wakiacha kazi zao, wengine wakitelekeza familia zao, wengine wakiacha ndoa, na wengine hata wakitoa akiba zao zote. Haya ni matendo ya kujitolea yasiyo na ubinafsi yaliyoje! Unyofu na kujitolea kama huko hakika unazidi hata ule wa watakatifu wa enzi zilizopita! Kwa kuwa Bwana humpa neema yeyote Ampendaye na kumwonyesha rehema yeyote Ampendaye, matendo yetu ya kujitolea na gharama tulizotoa, tunaamini, yameonekana na macho Yake tangu zamani. Vivyo hivyo, maombi yetu ya kutoka moyoni yamefikia masikio Yake, na tunaamini kwamba Bwana atatupa fidia kwa ajili ya kujitolea kwetu. Zaidi ya hayo, Mungu alikuwa ametujalia rehema kabla ya kuumba ulimwengu, na baraka na ahadi Alizotupa hakuna anayeweza kuzichukua. Sisi sote tunapanga kwa ajili ya siku za usoni, na kama jambo la kawaida tumefanya kujitolea kwetu na gharama tulizotoa kuwa kama sarafu za kamari au mtaji wa kubadilishana ili kunyakuliwa na kukutana na Bwana hewani. Zaidi ya hayo, sisi, bila kusita hata kidogo, tumejiweka kwenye kiti cha enzi cha siku za usoni, ili kusimamia mataifa na makabila yasiyohesabika au kutawala kama wafalme. Haya yote tunayachukulia kama jambo la hakika, kama kitu kinachotarajiwa.

Tunawadharau wale wote wanaompinga Bwana Yesu; wote watakumbana na matokeo ya kuangamizwa. Ni nani aliwaambia wasiamini kwamba Bwana Yesu ni Mwokozi? Bila shaka, kuna nyakati ambapo tunamwiga Bwana Yesu katika kuonyesha rehema kwa watu wa ulimwengu, kwa maana hawaelewi, na ni sawa kwamba tuwe wenye ustahimilivu na wenye kuwasamehe. Kila kitu tunachofanya ni kulingana na maneno ya Biblia, kwa maana kila kitu ambacho hakilingani na Biblia ni uzushi na imani potovu. Imani ya aina hii imekita mizizi sana katika akili ya kila mmoja wetu. Bwana wetu yumo katika Biblia, na ikiwa hatutaiacha Biblia, hatutamwacha Bwana; ikiwa tutatii kanuni hii, tutapata wokovu. Tunahimizana, kila mmoja akimtegemeza mwenzake, na kila wakati tunapokusanyika pamoja, tunatumai kwamba kila kitu tunachosema na kufanya kinalingana na nia za Bwana na kitakubaliwa na Bwana. Licha ya uhasama mkali wa mazingira yetu, mioyo yetu imejaa furaha. Tunapofikiria baraka ambazo zinapatikana kwa urahisi hivyo, je, kuna chochote ambacho hatuwezi kukiacha? Je, kuna chochote ambacho tunasita kuachana nacho? Haya yote ni wazi, na haya yote yako chini ya uchunguzi wa macho ya Mungu. Sisi, kundi hili dogo la wanaohitaji ambao tumeinuliwa kutoka kwenye jaa la takataka, ni kama wafuasi wote wa kawaida wa Bwana Yesu, tukiota kuhusu kunyakuliwa, kubarikiwa, na kutawala mataifa yasiyohesabika. Upotovu wetu umewekwa wazi machoni pa Mungu, na matamanio yetu na tamaa yetu vimehukumiwa machoni pa Mungu. Hata hivyo, haya yote yanafanyika kwa kawaida sana, na kwa njia inayoingia akilini sana, kiasi kwamba hakuna hata mmoja wetu anayejiuliza iwapo matamanio yetu ni sahihi, sembuse yeyote kati yetu kutilia shaka usahihi wa kila kitu tunachoshikilia. Ni nani anayeweza kujua nia za Mungu? Ni njia ya aina gani hasa ndiyo mwanadamu anafuata, hatufikirii kutafuta au kuchunguza; na wala hatuna haja kabisa ya kuuliza. Kwa maana tunajali tu kuhusu iwapo tunaweza kunyakuliwa, iwapo tunaweza kubarikiwa, iwapo kuna nafasi kwa ajili yetu katika ufalme wa mbinguni, na iwapo tutakuwa na sehemu ya maji ya mto wa uzima na matunda ya mti wa uzima. Je, si kwa ajili ya kupata mambo haya ndiyo maana tunamwamini Bwana na kuwa wafuasi Wake? Dhambi zetu zimesamehewa, tumetubu, tumekunywa kikombe kichungu cha divai, na tumeweka msalaba migongoni mwetu. Ni nani anayeweza kusema kwamba Bwana hatakubali gharama ambayo tumelipa? Ni nani anayeweza kusema kwamba hatujatayarisha mafuta ya kutosha? Hatutaki kuwa wale wanawali wapumbavu au mmoja wa wale wanaochwa. Zaidi ya hayo, tunaomba daima, tukimwomba Bwana atulinde dhidi ya kupotoshwa na makristo wa uongo, kwa maana inasemwa katika Biblia: “Basi iwapo mtu yeyote atawaambia, Tazameni, Kristo yuko huku, au yuko pale; msiamini hili. Kwa kuwa wataibuka makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao wataonyesha ishara na miujiza mikubwa; ili kwamba, ikiwezekana, watawapotosha walio wateule zaidi” (Mathayo 24:23-24). Sisi sote tumehifadhi mistari hii ya Biblia akilini mwetu; tunaikumbuka kwa moyo, na tunaichukulia kama hazina ya thamani, kama uzima, na kama hati ya dhamana inayoamua iwapo tunaweza kuokolewa au kunyakuliwa …

Kwa maelfu ya miaka, walio hai wameaga dunia, wakienda na matamanio yao na ndoto zao, lakini kuhusu iwapo wameenda katika ufalme wa mbinguni, hakuna anayejua kweli. Wafu wanarudi, wakiwa wamesahau hadithi zote zilizowahi kutokea, na bado wanafuata mafundisho na njia za mababu. Na kwa njia hii, miaka inavyopita na siku zinavyosonga, hakuna anayejua iwapo Bwana wetu Yesu, Mungu wetu, anakubali kweli kila kitu tunachofanya. Kile tunachofanya tu ni kutazamia kuwa na matokeo na kukisia kuhusu kila kitu kitakachotokea. Hata hivyo Mungu amedumisha kimya Chake wakati wote, hajawahi kuonekana kwetu, hajawahi kuzungumza nasi. Na hivyo, tukiifuata Biblia na kulingana na ishara, tunatoa hukumu kwa ukaidi kuhusu nia na tabia ya Mungu. Tumezoea kimya cha Mungu; tumezoea kupima usahihi na makosa ya matendo yetu kwa kutumia njia yetu wenyewe ya kufikiri; tumezoea kutegemea maarifa, mawazo, na maadili yetu badala ya matakwa ambayo Mungu anatuwekea; tumezoea kufurahia neema ya Mungu; tumezoea Mungu kutupa msaada wakati wowote tunapouhitaji; tumezoea kumnyooshea Mungu mikono yetu kwa mambo yote, na kumwamrisha Mungu; tumezoea pia kufuata kanuni, bila kutilia maanani jinsi Roho Mtakatifu anavyotuongoza; na, hata zaidi, tumezoea siku ambazo sisi ndio mabwana wetu wenyewe. Tunamwamini Mungu kama huyu, ambaye hatujawahi kukutana na Yeye uso kwa uso. Maswali kama vile tabia Yake ikoje, kile Anacho na alicho, mfano Wake ukoje, iwapo tutamjua Atakapokuja au la, na kadhalika—hakuna hata moja kati ya haya ambalo ni muhimu. Kile ambacho ni muhimu ni kwamba Yeye yumo mioyoni mwetu na kwamba sote tunamngoja, na inatosha kwamba tunaweza kuwazia kuwa Yeye yuko hivi au vile. Tunathamini imani yetu na tunatunza hali yetu ya roho. Tunachukulia mambo yote kama mavi, na tunakanyaga mambo yote chini ya miguu yetu. Kwa sababu sisi ni waumini wa Bwana mtukufu, haijalishi safari ni ndefu na ngumu kiasi gani, haijalishi ni shida na hatari gani zinazotupata, hakuna kinachoweza kusimamisha hatua zetu tunapomfuata Bwana. “Mto safi wa maji ya uhai, ung’aao kama kioo, ukiondoka katika kiti cha Mungu cha enzi na cha Mwanakondoo. Katika kila upande wa ule mto, ulikuwapo ule mti wa uhai unaozaa matunda ya jinsi kumi na mbili, na kuyatoa hayo matunda yake kila mwezi: na majani ya mti huu yalikuwa ya ajili ya kuyaponya mataifa. Na laana haitakuwepo tena: ila kiti cha Mungu cha enzi na cha Mwanakondoo kitakuwa ndani yake; na watumishi Wake watamhudumia: Na wao wataona uso Wake; nayo mapaji ya nyuso zao yatakuwa na jina Lake. Na hakutakuwa na usiku pale; wala hawahitaji mshumaa, wala mwanga wa jua; kwa sababu Bwana Mungu huwapa mwanga: na wao watatawala daima na milele” (Ufunuo 22:1-5). Kila wakati tunapoimba maneno haya, mioyo yetu hujaa furaha na uradhi usio na mipaka, na machozi hutiririka kutoka machoni mwetu. Shukrani kwa Bwana kwa kutuchagua, shukrani kwa Bwana kwa neema Yake. Ametupa mara mia katika maisha haya na Ametupa uzima wa milele katika dunia ijayo. Kama Angetuomba tufe sasa, tungefanya hivyo bila malalamiko hata kidogo. Bwana! Tafadhali njoo upesi! Ukizingatia jinsi tunavyokutamani sana, na tulivyotelekeza kila kitu kwa ajili Yako, usichelewe hata kwa dakika moja, au sekunde moja zaidi.

Mungu yuko kimya, na hajawahi kuonekana kwetu, hata hivyo kazi Yake haijawahi kusimama. Anachunguza dunia nzima, na Anatawala juu ya vitu vyote, na Anatazama maneno, matendo, na mienendo yote ya mwanadamu. Anafanya usimamizi Wake kwa mpango na kwa hatua, kwa kimya na bila kutikisa mbingu na nchi, hata hivyo hatua Zake zinasonga mbele, moja baada ya nyingine, karibu zaidi na mwanadamu, na kiti Chake cha hukumu kinawekwa katika ulimwengu kwa kasi ya umeme, kufuatia hili kiti Chake cha enzi kinashuka mara moja katikati yetu. Hayo ni mandhari adhimu yaliyoje, picha ya fahari na ya dhati iliyoje! Kama njiwa, na kama simba angurumaye, Roho anakuja katikati yetu sisi umati. Yeye ni hekima, Yeye ni haki na uadhama, na Anashuka kimya kimya katikati yetu, Akishika mamlaka na akijawa na fadhili na rehema. Hakuna anayetambua kuwasili Kwake, hakuna anayekaribisha kuwasili Kwake, na, hata zaidi, hakuna anayejua kila kitu ambacho Yeye yuko karibu kufanya. Maisha ya mwanadamu yanaendelea kama hapo awali, moyo wake hauna tofauti, na siku zinapita kama kawaida. Mungu anaishi miongoni mwetu, kama mtu wa kawaida, kama mmoja wa wafuasi wasio na maana zaidi na mwumini wa kawaida. Ana mambo Yake Mwenyewe anayoyafuatilia, malengo Yake Mwenyewe, na, hata zaidi, Ana uungu ambao haumilikiwi na watu wa kawaida. Hakuna ambaye ametambua kuwepo kwa uungu Wake, na hakuna ambaye ametambua tofauti kati ya kiini Chake na kile cha mwanadamu. Tunaishi pamoja na Yeye, bila kuzuiwa na bila woga, kwa maana machoni petu Yeye ni mwumini asiye na maana tu. Anatazama kila hatua yetu, na mawazo na fikira zetu zote zimewekwa wazi mbele Yake. Hakuna anayependezwa na kuwepo Kwake, hakuna anayewazia chochote kuhusu kazi Anayoifanya, na, hata zaidi, hakuna aliye na shaka hata kidogo kuhusu utambulisho Wake. Kile tunachofanya tu ni kuendelea na ufuatiliaji wetu, kana kwamba Yeye hana uhusiano wowote nasi …

Kwa bahati, Roho Mtakatifu anaonyesha kifungu cha maneno “kupitia” Kwake, na hata ingawa inahisi kana kwamba ni jambo lisilotarajiwa sana, sisi hata hivyo tunaamini kwa dhati kwamba ni tamko linalotoka kwa Mungu na tunalikubali bila kusita kutoka kwa Mungu. Hiyo ni kwa sababu, bila kujali ni nani anayeonyesha maneno haya, mradi tu yanatoka kwa Roho Mtakatifu, tunapaswa kuyakubali na hatuwezi kuyakana. Tamko linalofuata linaweza kuja kupitia kwangu, au kupitia kwako, au kupitia kwa mtu mwingine. Yeyote yule, yote ni neema ya Mungu. Hata hivyo haijalishi ni nani, hatuwezi kumwabudu mtu huyu, kwa maana kwa vyovyote vile, mtu huyu hawezi kamwe kuwa Mungu, wala hatuwezi kwa njia yoyote ile kumchagua mtu wa kawaida kama huyu kuwa Mungu wetu. Mungu wetu ni mkuu na wa kuheshimiwa sana; mtu asiye na maana kama huyu angewezaje kusimama katika nafasi Yake? Zaidi ya hayo, tunatazamia Mungu aje na atuchukue kurudi katika ufalme wa mbinguni, kwa hivyo mtu asiye na maana sana angewezaje kumudu kazi muhimu na ngumu kama hiyo? Bwana akija tena, lazima iwe juu ya wingu jeupe, ili watu wengi sana waweze kuona. Litakuwa tukio la utukufu sana! Inawezekanaje kwamba Anaweza kujificha kwa siri miongoni mwa kundi la watu wa kawaida?

Na bado ni mtu huyu wa kawaida, aliyefichwa katikati ya watu, ambaye anafanya kazi mpya ya kutuokoa. Hatupi maelezo yoyote, wala Hatuambii kwa nini Amekuja, lakini Anafanya tu kazi Anayokusudia kufanya kulingana na mpango Wake na utaratibu Wake. Maneno na matamko Yake yanazidi kuwa ya mara kwa mara. Kuanzia kufariji, kuhimiza, kukumbusha, na kuonya, hadi kushutumu na kutia adabu; kutoka kwa sauti ambayo ni nyororo na ya upole, hadi maneno ambayo ni makali na adhimu—yote yanamfanya mwanadamu ahisi rehema kuu na hofu tupu. Kila kitu Anachosema kinagusa siri zilizofichika ndani yetu kabisa; maneno Yake yanachoma mioyo yetu, yanachoma roho zetu, na yanatuacha tumejawa na aibu isiyovumilika, bila hata kujua mahali pa kujificha. Tunaanza kuwa na shaka kuhusu iwapo Mungu aliye katika moyo wa mtu huyu anatupenda kweli na Anafanya nini hasa. Pengine tunaweza tu kunyakuliwa baada ya kuvumilia mateso haya? Vichwani mwetu, tunapiga hesabu … kuhusu hatima ijayo na kuhusu majaliwa yetu ya siku za usoni. Bado, kama hapo awali, hakuna hata mmoja wetu anayeamini kwamba Mungu tayari amepata mwili kufanya kazi katikati yetu. Hata ingawa Ameandamana nasi kwa muda mrefu sana, hata ingawa tayari Amezungumza maneno mengi sana uso kwa uso nasi, tunabaki tusio radhi kumkubali mtu wa kawaida kama huyu kama Mungu wa siku zetu za usoni, sembuse kuwa tayari kukabidhi udhibiti wa siku zetu za usoni na majaliwa yetu kwa mtu huyu asiye na maana. Kutoka Kwake tunafurahia ruzuku isiyo na mwisho wa maji ya uzima, na kupitia Kwake tunaishi maisha ya mwanadamu na Mungu wakiwa uso kwa uso. Lakini tunashukuru tu kwa neema ya Bwana Yesu aliye mbinguni, na hatujawahi kutilia maanani hisia za mtu huyu wa kawaida ambaye anamiliki uungu. Bado, kama hapo awali, Anafanya kazi Yake kwa unyenyekevu Akiwa amejificha katika mwili, Akionyesha sauti ya moyo Wake, kana kwamba Hajali kukataliwa Kwake na mwanadamu, kana kwamba Anasamehe milele utoto na ujinga wa mwanadamu, na Anavumilia milele mtazamo wa mwanadamu usio na heshima Kwake.

Bila sisi kujua, mtu huyu asiye na maana Ametuongoza katika hatua moja baada ya nyingine ya kazi ya Mungu. Tunapitia majaribu yasiyohesabika na kurudi kusikohesabika, na tunajaribiwa kwa kifo. Tunapata kujua tabia ya Mungu yenye haki na uadhama, tunafurahia, pia, wema na rehema Zake, tunakuja kuthamini nguvu kuu na hekima ya Mungu, tunashuhudia uzuri wa Mungu, na tunatazama nia ya Mungu yenye shauku ya kumwokoa mwanadamu. Katika maneno ya mtu huyu wa kawaida, tunakuja kujua tabia na kiini cha Mungu, kuelewa nia za Mungu, kujua kiini cha asili cha mwanadamu, na kuona njia ya wokovu na ukamilisho. Maneno Yake yanasababisha "tufe," na yanasababisha "tuzaliwe upya"; maneno Yake yanatuletea faraja, lakini pia yanatuacha tukiwa tumejawa na hatia na hisia ya kuwa na deni; maneno Yake yanatuletea furaha na amani, lakini pia maumivu yasiyo na mwisho. Wakati mwingine sisi ni kama wanakondoo mikononi Mwake, wa kuchinjwa jinsi Apendavyo; wakati mwingine sisi ni kama mboni ya jicho Lake, na tunafurahia upendo Wake mwororo; wakati mwingine sisi ni kama adui Yake, na chini ya mtazamo Wake tunageuzwa kuwa majivu na ghadhabu Yake. Sisi ni jamii ya binadamu iliyookolewa na Yeye, sisi ni funza machoni Pake, na sisi ni kondoo waliopotea ambao, mchana na usiku, Amedhamiria kuwapata. Yeye ni mwenye rehema kwetu, Anatuchukia, Anatuinua, Anatufariji na Anatuhimiza, Anatuongoza, Anatutia nuru, Anaturudi na Anatuadhibu, na hata Anatulaani. Usiku na mchana, Haachi kamwe kuwa na wasiwasi kutuhusu na kutulinda na kututunza, bila kutuacha kamwe. Anamwaga damu yote ya moyo Wake na Analipa kila gharama kwa ajili yetu. Ndani ya maneno ya mwili huu usio na maana na wa kawaida, tumefurahia ukamilifu wa Mungu na tumetazama hatima ambayo Mungu ametupa. Licha ya haya, ubatili bado unachochea fadhaa ndani ya mioyo yetu, na bado hatuko tayari kuchukua hatua ya kumkubali mtu kama huyu kama Mungu wetu. Ingawa Ametupa mana nyingi sana, vitu vingi sana vya kufurahia, hakuna hata kimoja kati ya haya kinachoweza kuchukua nafasi ya Bwana katika mioyo yetu. Tunauheshimu utambulisho na hadhi maalum ya mtu huyu kwa kusita sana tu. Mradi tu Hafungui kinywa Chake kutuomba tukiri kwamba Yeye ni Mungu, hatutawahi kuchukua jukumu la kumkiri kama Mungu ambaye anawasili hivi karibuni na bado Amekuwa akifanya kazi katikati yetu kwa muda mrefu.

Mungu Anaendelea na matamko Yake, Akitumia mbinu mbalimbali na mitazamo mingi kutuonya kuhusu kile tunachopaswa kufanya, huku wakati huo huo Akionyesha sauti ya moyo Wake. Maneno Yake yanabeba nguvu ya uzima, yanatupa njia tunayopaswa kufuata, na yanatuwezesha kufahamu ukweli ni nini hasa. Tunaanza kuvutiwa na maneno Yake, tunaanza kutilia maanani sauti na namna ya kuzungumza Kwake, na bila kujua tunaanza kuzingatia sauti ya moyo wa mtu huyu asiyeonekana wazi. Anafanya kazi kwa bidii zote kwa ajili yetu, Anakosa usingizi na hamu ya kula kwa ajili yetu, Analia kwa ajili yetu, Anatanafusi kwa ajili yetu, na Anapiga kite katika ugonjwa kwa ajili yetu; Anavumilia udhalilishaji kwa ajili ya hatima na wokovu wetu; na kufa kwetu ganzi na uasi wetu vinatoa machozi na damu kutoka katika moyo Wake. Hakuna mtu wa kawaida aliye na kile Anacho na alicho, na hakuna mwanadamu mpotovu anayeweza kuwa nacho au kukifikia. Ana ustahimilivu na uvumilivu ambao haumilikiwi na mtu yeyote wa kawaida, na upendo Wake si kitu ambacho kiumbe yeyote aliyeumbwa anacho. Hakuna mwingine ila Yeye anayeweza kujua mawazo yetu yote, au kujua asili na kiini chetu kikamilifu, au kuhukumu uasi na upotovu wa mwanadamu, au kuzungumza nasi na kutufinyanga namna hii kwa niaba ya Mungu aliye mbinguni. Hakuna mwingine ila Yeye anayemiliki mamlaka, hekima, na hadhi ya Mungu; tabia ya Mungu na kile Mungu anacho na alicho vinadhihirishwa, kwa ukamilifu wake, ndani Yake. Hakuna mwingine ila Yeye anayeweza kutuonyesha njia na kutuletea mwanga. Hakuna mwingine ila Yeye anayeweza kufichua siri ambazo Mungu hajazijulisha tangu uumbaji hadi leo. Hakuna mwingine ila Yeye anayeweza kutuokoa kutoka katika utumwa wa Shetani na tabia zetu wenyewe potovu. Anamwakilisha Mungu; Anaonyesha sauti ya moyo wa Mungu, mahimizo ya Mungu, na maneno ya Mungu ya hukumu kuelekea binadamu wote. Amefungua enzi mpya, kipindi kipya, na kuanzisha mbingu na ardhi mpya na kazi mpya, Ametuletea tumaini na kukomesha maisha tuliyoishi katika hali isiyo yakini, na Ameziwezesha nafsi zetu zote zitazame kikamilifu njia ya wokovu. Ameshinda nafsi zetu zote na kupata mioyo yetu. Kuanzia wakati huo na kuendelea, mioyo yetu imepata ufahamu, na roho zetu zinaonekana kufufuliwa: Mtu huyu wa kawaida, asiye na maana, mtu huyu anayeishi miongoni mwetu na amekataliwa na sisi kwa muda mrefu sana—je, huyu si Bwana Yesu, ambaye yumo daima katika mawazo yetu, tukiwa macho au tukiota, na ambaye tunamtamani usiku na mchana? Ni Yeye! Kwa kweli ni Yeye! Yeye ni Mungu wetu! Yeye ni ukweli, njia, na uzima! Ametuwezesha kuishi tena na kuona mwanga na Amezuia mioyo yetu isitangatange. Tumerudi katika nyumba ya Mungu, tumerudi mbele ya kiti Chake cha enzi, tuko uso kwa uso na Yeye, tumeshuhudia uso Wake, na tumeona njia iliyo mbele yetu. Wakati huu, mioyo yetu imeshindwa kikamilifu na Yeye; hatuna shaka tena Yeye ni nani, hatuhisi tena upinzani kuelekea kazi Yake na neno Lake, na tunaanguka kifudifudi mbele Yake. Hatutamani chochote zaidi ya kufuata hatua za Mungu kwa maisha yetu yote yaliyosalia, na kufanywa kuwa watimilifu na Yeye, na kurudisha neema Yake, na kurudisha upendo Wake kwetu, na kutii mipango na mipangilio Yake, na kushirikiana na kazi Yake, na kufanya kila tuwezalo kukamilisha kile Anachotuaminia.

Kushindwa na Mungu ni kama shindano la sanaa ya kijeshi.

Kila neno la Mungu linaupiga kwa kulenga udhaifu wetu mkuu, likituacha tumeumia na kuamsha hofu ndani yetu. Anafichua mawazo yetu, fikira zetu, na tabia zetu potovu. Kuanzia kila neno na tendo letu, kila hatua yetu, hadi kila mojawapo ya mawazo na fikira zetu, kiini chetu cha asili kinafunuliwa katika maneno Yake, kikitutia katika hali ya hofu na kutetemeka bila mahali pa kuficha aibu yetu. Moja baada ya nyingine, Anatuambia kuhusu matendo yetu yote, malengo na nia zetu, hata tabia potovu ambazo sisi wenyewe hatujawahi kuzigundua, Akitufanya tuhisi kufichuliwa katika hali yetu yote ya kusikitisha ya kutokuwa wakamilifu na, hata zaidi, kushawishika kabisa. Anatuhukumu kwa kumpinga, Anatuadibu kwa kumkufuru na kumshutumu, na Anatufanya tuhisi kwamba, machoni Pake, hatuna hata sifa moja nzuri ya kutukomboa, kwamba sisi ni Mashetani walio hai. Matumaini yetu yanavunjwa; hatuthubutu tena kudai matakwa yoyote ya kupita kiasi kutoka Kwake au kuwa na njama zozote juu Yake, na hata ndoto zetu zinatoweka mara moja. Huu ni ukweli ambao hakuna hata mmoja wetu anayeweza kuuwazia na ambao hakuna hata mmoja wetu anayeweza kuukubali. Ndani ya muda mfupi, tunapoteza usawa wetu wa ndani na hatujui jinsi ya kuendelea katika njia iliyo mbele yetu, au jinsi ya kuendelea katika imani yetu. Inaonekana kana kwamba imani yetu imerudi pale ilipoanzia, na kana kwamba hatujawahi kukutana na Bwana Yesu au kupata kumjua. Kila kitu mbele ya macho yetu kinatujaza na mkanganyiko na kutufanya tuyumbayumbe kwa kusita. Tumesikitishwa, tumevunjika moyo, na ndani kabisa ya mioyo yetu kuna ghadhabu isiyozuilika na aibu. Tunajaribu kutoa hisia zetu, kutafuta njia ya kutokea, na, zaidi ya hayo, kuendelea kumngoja Mwokozi wetu Yesu, ili tuweze kumimina mioyo yetu Kwake. Ingawa kuna nyakati ambapo tunaonekana kwa nje kutokuwa na kiburi wala unyenyekevu, mioyoni mwetu tunahisi hisia ya kupoteza ambayo hatujawahi kuhisi hapo awali. Ingawa wakati mwingine tunaweza kuonekana watulivu isivyo kawaida kwa nje, akili zetu zinavurugika kwa mateso kama bahari yenye dhoruba. Hukumu na kuadibu Kwake kumetunyang'anya matumaini na ndoto zetu zote, kukomesha matamanio yetu ya kupita kiasi na kutuacha tukiwa hatuko radhi kuamini kwamba Yeye ni Mwokozi wetu na Ana uwezo wa kutuokoa. Hukumu na kuadibu Kwake kumefungua ufa mkubwa kati yetu na Yeye, ufa mkubwa wenye kina sana kiasi kwamba hakuna aliye radhi kuuvuka. Hukumu na kuadibu Kwake ndiyo mara ya kwanza ambapo tumekumbana na kizuizi kikubwa hivi, udhalilishaji mkubwa hivi katika maisha yetu. Hukumu na kuadibu Kwake kumetusababisha tuhisi kweli heshima ya Mungu na kutovumilia Kwake makosa ya mwanadamu, ambapo tukilinganishwa nayo sisi ni duni mno, wachafu mno. Hukumu na kuadibu Kwake kumetufanya tutambue kiburi na majivuno yetu kwa mara ya kwanza, na jinsi mwanadamu hatakuwa kamwe sawa na Mungu, au kuweza kulinganishwa na Yeye. Hukumu na kuadibu Kwake kumetufanya tutamani kutokuishi tena katika tabia potovu kama hizo, kujiondolea kiini hiki cha asili haraka iwezekanavyo, na kuacha kuchukiwa na Yeye na kuwa wa kuchukiza Kwake. Hukumu na kuadibu Kwake kumetufanya tuwe radhi kutii maneno Yake, bila kuasi tena dhidi ya mipango na mipangilio Yake. Hukumu na kuadibu Kwake kumetupa tena hamu ya kuendelea kuishi na kutufanya tuwe na furaha kumkubali kama Mwokozi wetu…. Tumetoka katika kazi ya ushindi, kutoka kuzimu, kutoka katika bonde la uvuli wa mauti…. Mwenyezi Mungu ametupata, kundi hili la watu! Ameshinda dhidi ya Shetani na Amewashinda halaiki za adui Wake!

Sisi ni kundi la watu wa kawaida tu, tulio na tabia potovu za kishetani, wale walioamuliwa kimbele na Mungu kabla ya enzi, na wanaohitaji ambao Mungu amewainua kutoka kwenye lundo la samadi. Wakati mmoja tulimkataa na kumshutumu Mungu, lakini sasa tumeshindwa na Yeye. Kutoka kwa Mungu tumepokea uzima na njia ya uzima wa milele. Popote pale tulipo duniani, mateso na dhiki yoyote tunayovumilia, hatuwezi kutengwa na wokovu wa Mwenyezi Mungu. Kwa maana Yeye ni Muumba wetu, na ukombozi wetu wa pekee!

Upendo wa Mungu unaenea mbele kama maji ya chemchemi, na unapewa kwako, na kwangu, na kwa wengine, na kwa wale wote wanaotafuta ukweli kwa dhati na kungoja kuonekana kwa Mungu.

Kama vile jua na mwezi vinavyochomoza kwa zamu, kazi ya Mungu haikomi kamwe, na inafanywa juu yako, juu yangu, juu ya wengine, na juu ya wale wote wanaoenda sambamba na hatua za Mungu na kukubali hukumu na kuadibu Kwake.

Machi 23, 2010

Iliyotangulia: Kumjua Mungu Ndiyo Njia ya Kumcha Mungu na Kuepuka Maovu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp