Huduma ya Kidini Lazima Ipigwe Marufuku
Tangu Mungu alipoanzisha kazi Yake katika ulimwengu, Amewaamua kabla watu wengi kumtumikia Yeye, wakiwemo wale kutoka kila nyanja ya maisha, kwa lengo la kwamba nia Zake ziridhishwe na kazi Yake duniani ikamilishwe kwa wepesi—hili ndilo lengo la Mungu katika kuwachagua watu kumtumikia Yeye. Kila mtu anayemtumikia Mungu anapaswa kuelewa nia Yake hii. Kupitia kazi hii ya Mungu, watu wanaona kwa uwazi zaidi hekima na uweza Wake, na kanuni za kazi Yake duniani. Kwa njia ya vitendo, Mungu amekuja duniani kufanya kazi Yake na kuingiliana na watu, ili waweze kujua matendo Yake kwa uwazi zaidi. Leo, ninyi—kikundi hiki cha watu—mna bahati ya kumtumikia Mungu wa vitendo. Hii ni baraka isiyoweza kupimika kwenu—kwa kweli ni kuinuliwa kwenu na Mungu. Katika kumchagua mtu amtumikie Yeye, Mungu daima huwa na kanuni Zake mwenyewe. Si kweli kabisa, kama watu wanavyofikiria, kwamba mtu anaweza kumtumikia Mungu mradi tu ana shauku. Leo, mnaona kwamba wote wanaotumikia mbele za Mungu wanafanya hivyo kwa sababu ya kuelekezwa na Mungu, na kwamba wana kazi ya Roho Mtakatifu, na ni watu wanaofuatilia ukweli. Haya ndiyo masharti ya chini kabisa kwa wale wote wanaomtumikia Mungu.
Kumtumikia Mungu si kazi rahisi. Wale ambao tabia yao potovu inabaki bila kubadilika hawawezi kamwe kumtumikia Mungu. Ikiwa tabia yako haijahukumiwa na kuadibiwa na maneno ya Mungu, basi tabia yako bado inamwakilisha Shetani, jambo ambalo linathibitisha kwamba huduma yako kwa Mungu ni wewe tu kutoa nia zako njema, kwamba huduma yako inategemea asili yako ya kishetani. Unamtumikia Mungu kwa hulka yako ya asili, na kulingana na mapendeleo yako binafsi. Zaidi ya hayo, wewe hufikiri daima kwamba mambo ambayo uko radhi kufanya ndiyo yanayompendeza Mungu, na kwamba mambo ambayo huko radhi kufanya ndiyo yanayomchukiza Mungu; unatenda kwa ukamilifu kulingana na mapendeleo yako mwenyewe. Je, huku kunaweza kuitwa kumtumikia Mungu? Hatimaye, hakutakuwa na mabadiliko hata kidogo katika tabia yako ya maisha; badala yake, huduma yako itaifanya iwe kaidi hata zaidi, na hivyo kuifanya tabia yako potovu ikite mizizi kwa kina, na kwa hivyo, kutaundwa ndani yako kanuni kuhusu huduma kwa Mungu ambazo kimsingi zinategemea hulka yako mwenyewe, na uzoefu unaotokana na huduma yako kulingana na tabia yako mwenyewe. Huu ndio uzoefu na mafunzo ya mwanadamu. Ni falsafa za shughuli za kidunia za mwanadamu. Watu kama hawa ni Mafarisayo na maafisa wa kidini. Wasipoamka na kutubu sasa, basi hakika watageuka na kuwa makristo wa uongo na wapinga Kristo wanaowapotosha watu katika siku za mwisho. Makristo wa uongo na wapinga Kristo waliozungumziwa watatokea miongoni mwa watu kama hao. Wale wanaomtumikia Mungu wakifuata hulka yao wenyewe na wakitenda kulingana na mapenzi yao wenyewe, wako katika hatari ya kuondoshwa wakati wowote. Wale wanaotegemea miaka yao mingi ya uzoefu kumtumikia Mungu ili kuishinda mioyo ya wengine, kuwakemea na kuwabana, na kujiinua—na ambao hawatubu kamwe, hawakiri dhambi zao kamwe, hawaachilii kamwe manufaa ya hadhi—watu hawa wataanguka mbele za Mungu. Wao ni wa aina moja na Paulo, wakitumia vibaya ukubwa wao na kuwatawala wengine kwa kutumia sifa zao. Mungu hawafanyi watu kama hawa kuwa watimilifu. Huduma kama hiyo ni ya kuvuruga kazi ya Mungu. Watu daima hung’ang’ania mambo ya kale. Wao hung’ang’ania dhana za zamani, hung’ang’ania kila kitu kutoka nyakati zilizopita. Hiki ni kikwazo kikubwa kwa huduma yao. Usipovitupa mbali, vitu hivi vitayaharibu maisha yako yote. Hata ukivunja miguu yako ukikimbia huku na huko, uvunje mgongo wako kwa kazi ngumu, au hata ufe kishahidi kwa ajili ya “kumtumikia” Mungu, Mungu hatakukubali hata kidogo. Kinyume chake kabisa: Atasema kwamba wewe ni mtenda maovu.
Kuanzia leo, Mungu atawafanya kuwa watimilifu rasmi wale ambao hawana dhana za kidini, ambao wako tayari kuweka kando nafsi zao za zamani, na wanaomtii Mungu kwa moyo wa dhati. Yeye atawafanya kuwa watimilifu wale wanaotamani maneno ya Mungu. Watu hawa wanapaswa kusimama na kumtumikia Mungu. Ndani ya Mungu kuna utele usio na mwisho na hekima isiyo na mipaka. Kazi Yake ya ajabu na maneno Yake ya thamani vinasubiri kufurahiwa na idadi kubwa zaidi ya watu. Jinsi ilivyo sasa, wale walio na dhana za kidini, wale wanaojiona wakubwa, na wale wasioweza kujiweka kando wanaona ugumu kukubali mambo haya mapya. Roho Mtakatifu hana fursa ya kuwafanya watu hawa kuwa watimilifu. Ikiwa mtu hana azimio la kutii, na hana kiu ya maneno ya Mungu, basi hana namna ya kukubali mambo haya mapya; atazidi tu kuwa mwasi zaidi na zaidi, mjanja zaidi na zaidi, na hivyo ataishia kwenye njia mbaya. Katika kufanya kazi Yake sasa, Mungu atawainua watu wengi zaidi wanaompenda Yeye kwa kweli na wanaoweza kukubali mwanga mpya, na Yeye atawakatakata kabisa maafisa wa kidini wanaotegemea ukubwa wao; Yeye hataki hata mmoja wa watu kama hao wanaopinga mabadiliko kwa ukaidi. Je, unataka kuwa mmoja wa watu hawa? Je, unatekeleza huduma yako kulingana na mapendeleo yako mwenyewe au kile ambacho Mungu anataka? Hili ni jambo unalopaswa kujua wewe mwenyewe. Je, wewe ni afisa wa kidini, au wewe ni mtoto mchanga ambaye Mungu anamfanya kuwa mtimilifu? Ni kiasi gani cha huduma yako kinachokubaliwa na Roho Mtakatifu? Ni kiasi gani cha huduma ambacho hakitakumbukwa na Mungu kabisa? Kumekuwa na mabadiliko makubwa kiasi gani katika uzima wako kutokana na miaka yako yote ya huduma? Je, unaelewa haya yote? Ikiwa wewe ni wa imani kweli, utatupa mbali dhana zako za zamani za kidini za hapo awali, na utamtumikia Mungu vizuri zaidi kwa njia mpya. Hujachelewa sana kusimama sasa. Dhana za zamani za kidini zinaweza kumpotezea mtu maisha yake yote. Uzoefu ambao mtu anapata unaweza kumsababisha akengeuke kutoka kwa Mungu na kujitegemea mwenyewe kufanya mambo. Usipoweka mambo kama haya kando, yatakuwa vikwazo kwa ukuaji wa uzima wako. Mungu daima huwafanya kuwa watimilifu wale wanaomtumikia Yeye, na hawaondoshi kwa urahisi. Ukikubali kweli hukumu na kuadibu kwa maneno ya Mungu, ukiweza kuweka kando matendo na kanuni zako za kidini za zamani, na uache kutumia dhana zako za kidini za hapo awali kama kipimo cha maneno ya Mungu ya leo, hapo tu ndipo utakapokuwa na matarajio yoyote ya kutajika. Lakini uking’ang’ania mambo ya kale ya hapo awali, ikiwa bado unayathamini, basi hakuna namna ambavyo unaweza kuokolewa. Mungu hawatilii maanani watu kama hao. Ikiwa kweli uko tayari kufanywa kuwa mtimilifu, basi lazima uazimie kuachilia kabisa kila kitu cha hapo awali. Hata kama kile kilichofanywa hapo awali kilikuwa sahihi, hata kama kilifanywa na Mungu, bado lazima uweze kukiweka kando na kutoking’ang’ania. Hata kama ilikuwa wazi kuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu, iliyofanywa moja kwa moja na Roho Mtakatifu, leo lazima uiweke kando. Hupaswi kuishikilia. Hiki ndicho anachotaka Mungu. Kila kitu lazima kifanywe kipya. Katika kazi ya Mungu na maneno ya Mungu, kwa usawa Yeye harejelei mambo ya kale yaliyopita, Yeye harejelei shajara ya mwaka ya zamani; Mungu ni Mungu ambaye daima ni mpya na si wa zamani kamwe, na hang’ang’anii hata maneno Yake Mwenyewe ya zamani—jambo ambalo linaonyesha kwamba Mungu hafuati taratibu zozote. Kwa hivyo ikiwa wewe, kama mwanadamu, daima unang’ang’ania mambo ya zamani na kukataa kuyaachilia, na kuyatumia kwa namna isiyobadilika kwa kufuata mtindo mmoja, lakini Mungu hafanyi kazi akitumia njia Alizotumia hapo awali, basi, je, maneno na matendo yako si ya kuvuruga? Je, hayampingi Mungu? Je, uko radhi kuyaacha maisha yako yote yaharibiwe na kuangamizwa kwa sababu ya mambo haya ya kale? Mambo haya ya kale yatakufanya uwe mtu anayevuruga kazi ya Mungu—je, huyo ndiye aina ya mtu unayetaka kuwa? Ikiwa kweli hutaki hilo, basi acha haraka kile unachofanya na ugeuke; anza upya. Mungu hatakumbuka huduma yako ya zamani.