Kujua Hatua Tatu za Kazi ya Mungu Ndiyo Njia ya Kumjua Mungu

Kazi ya kumsimamia mwanadamu imegawanywa katika hatua tatu, na ina maana kuwa kazi ya kumwokoa mwanadamu imegawanywa katika hatua tatu. Hatua hizi tatu hazihusishi kazi ya kuuumba ulimwengu, ila ni hatua tatu za kazi ya Enzi ya Sheria, Enzi ya Neema, na Enzi ya Ufalme. Kazi ya kuiumba dunia ilikuwa kazi ya kusababisha uwepo wa wanadamu wote. Haikuwa kazi ya kumwokoa mwanadamu, na haina uhusiano na kazi ya kumwokoa mwanadamu, kwa kuwa dunia ilipoumbwa mwanadamu hakuwa amepotoshwa na Shetani, na hivyo hakukuwa na haja ya kutekeleza kazi ya kumwokoa mwanadamu. Kazi ya kumwokoa mwanadamu ilianza tu baada ya mwanadamu kupotoshwa na Shetani, na kwa hivyo kazi ya kumsimamia mwanadamu pia ilianza tu punde mwanadamu alipopotoshwa. Kwa maneno mengine, usimamizi wa Mungu wa mwanadamu ulianza kutokana na kazi ya kumwokoa mwanadamu, na wala haukutokana na kazi ya kuiumba dunia. Hakungekuwa na kazi ya kumsimamia mwanadamu pasipo kuwepo na tabia potovu ya mwanadamu, na kwa hivyo kazi ya kumsimamia mwanadamu ina sehemu tatu, badala ya hatua nne, au enzi nne. Hii tu ndio njia sahihi ya kutaja kazi ya Mungu ya usimamizi wa mwanadamu. Enzi ya mwisho itakapofikia kikomo, kazi ya kusimamia mwanadamu itakuwa imekamilika. Hitimisho la kazi ya usimamizi lina maana kuwa kazi ya kuwaokoa wanadamu wote imekamilika kabisa, na kwamba mwanadamu amefika mwisho wa safari yake. Pasipo kazi ya kuwaokoa wanadamu wote, kazi ya usimamizi wa wanadamu haingekuwepo, wala hakungekuwa na hatua tatu za kazi. Ilikuwa ni hasa kwa ajili ya upotovu wa mwanadamu, na kwa sababu mwanadamu alihitaji wokovu kwa dharura, ndipo Yehova alikamilisha uumbaji wa dunia na kuanza kazi ya Enzi ya Sheria. Hapo tu ndipo kazi ya kumsimamia mwanadamu ilipoanza, kumaanisha kwamba hapo tu ndipo kazi ya kumwokoa mwanadamu ilipoanza. “Kumsimamia mwanadamu” haimaanishi kuongoza maisha ya mwanadamu aliyeumbwa upya duniani (ambapo ni kusema, mwanadamu ambaye bado hakuwa amepotoshwa). Badala yake, ni wokovu wa mwanadamu ambaye amepotoshwa na Shetani, ambapo ni kusema kwamba, ni kubadilishwa kwa mwanadamu aliyepotoshwa. Hii ndiyo maana ya kumsimamia mwanadamu. Kazi ya kumwokoa mwanadamu haihusishi kazi ya kuiumba dunia, na kwa hivyo kazi ya kumsimamia mwanadamu haijumuishi kazi ya kuumba ulimwengu, na inahusisha tu hatua tatu za kazi zilizo tofauti na uumbaji wa ulimwengu. Ili kuelewa kazi ya kumsimamia mwanadamu, ni muhimu kuwa na ufahamu wa historia ya hatua tatu za kazi—hili ndilo kila mtu anapaswa kulifahamu ili kuokolewa. Kama viumbe wa Mungu, mnapaswa kutambua kuwa mwanadamu aliumbwa na Mungu, na kufahamu chanzo cha upotovu wa mwanadamu, na, vilevile, kufahamu mchakato wa wokovu wa mwanadamu. Iwapo mnafahamu tu jinsi ya kutenda kulingana na mafundisho ili kupata neema ya Mungu, lakini hamna fununu jinsi Mungu anavyomwokoa mwanadamu, au ya chanzo cha upotovu wa mwanadamu, basi hili ndilo mnalokosa kama viumbe wa Mungu. Hupaswi kutoshelezwa tu na kuelewa kwa ukweli unaoweza kuwekwa katika vitendo, huku ukibakia kutojua upeo mpana wa kazi ya usimamizi ya Mungu—kama hivi ndivyo ilivyo, basi wewe ni mwenye kulazimisha kauli sana. Hatua tatu za kazi ya Mungu ndizo hadithi ya ndani ya usimamizi wa Mungu wa mwanadamu, ujio wa injili ya dunia nzima, fumbo kubwa zaidi kati ya wanadamu, na pia ni msingi wa kueneza injili. Ukizingatia tu kuelewa ukweli sahili unaohusiana na maisha yako, na usijue lolote kuhusu hili, maajabu makuu zaidi na maono, basi maisha yako si ni sawa na bidhaa yenye kasoro, yasio na maana isipokuwa kuangaliwa?

Ikiwa mwanadamu huzingatia tu matendo, na kuona kazi ya Mungu na hekima ya mwanadamu kama za upili, basi si ni sawa na kufikira mambo yasiyokuwa muhimu huku ukipuuza mambo yaliyo muhimu zaidi? Lile ambalo sharti ulijue, lazima ulijue, na kile unachostahili kuonyesha kwa vitendo, lazima ukionyeshe kwa vitendo. Ni hapo tu ndipo utakapokuwa mtu anayejua kufuata ukweli. Siku yako ya kueneza injili itakapowadia, ikiwa utaweza kusema tu kuwa Mungu ni Mkuu na Mwenye haki, kuwa ni Mungu Mkuu, Mungu ambaye hapana mwanadamu yeyote mkuu anayeweza kujilinganisha naye, na kuwa hakuna aliye juu zaidi wa kumpiku…, kama waweza tu kusema maneno haya yasiyofaa na ovyo, na kabisa huwezi kunena maneno yenye umuhimu zaidi, na yaliyo na kiini, kama huna lolote la kusema kuhusu kumjua Mungu, ama kazi ya Mungu, na zaidi ya hapo, huwezi kuelezea ukweli, au kutoa kile ambacho kinakosekana kwa mwanadamu, basi mtu kama wewe hana uwezo wa kutekeleza wajibu wake vyema. Kumshuhudia Mungu na kueneza injili ya ufalme si jambo rahisi. Lazima kwanza uwe na ukweli, na maono yatakayoeleweka. Unapokuwa na uwazi wa maono na ukweli wa masuala tofauti ya kazi ya Mungu, moyoni mwako unapata kujua kazi ya Mungu, na bila kujali anayoyafanya Mungu—iwe ni hukumu ya haki ama kusafishwa kwa mwanadamu—unamiliki maono makuu kama msingi wako, na unamiliki ukweli sahihi wa kuonyesha kwa matendo, basi utaweza kumfuata Mungu hadi mwisho. Lazima ujue kuwa bila kujali kazi ambayo Yeye anatenda, lengo la kazi ya Mungu halibadiliki, kiini cha kazi Yake hakibadiliki, na mapenzi Yake kwa mwanadamu hayabadiliki. Bila kujali maneno Yake ni makali namna gani, haijalishi mazingira ni mabaya kiasi gani, kanuni za kazi Yake, na nia Yake ya kumwokoa mwanadamu hayatabadilika. Mradi tu si ufunuo wa mwisho wa mwanadamu au hatima ya mwanadamu, na si kazi ya awamu ya mwisho, au kazi ya kutamatisha mpango wote wa usimamizi wa Mungu, na mradi tu ni wakati Anapomfinyanga mwanadamu, basi kiini cha kazi Yake hakitabadilika: Daima kitakuwa wokovu wa mwanadamu. Hili linapaswa kuwa msingi wa imani yenu katika Mungu. Lengo la hatua tatu za kazi ni wokovu wa wanadamu wote—ambayo inamaanisha wokovu kamili wa mwanadamu kutoka kwa miliki ya Shetani. Ingawa kila moja ya hatua ya kazi ina madhumuni na umuhimu, kila moja ni sehemu ya kazi ya kumwokoa mwanadamu, na ni kazi tofauti ya wokovu inayotekelezwa kulingana na matakwa ya mwanadamu. Punde unapofahamu lengo la hatua hizi tatu za kazi, basi utafahamu jinsi ya kuthamini umuhimu wa kila hatua ya kazi, na utatambua jinsi ya kutenda ili kutosheleza shauku ya Mungu. Iwapo utaweza kufikia hatua hii, basi hili, ono kubwa kuliko yote, litakuwa msingi wa imani yako katika Mungu. Unapaswa kufuata sio tu njia rahisi za matendo, ama ukweli wenye undani, lakini unapaswa kuunganisha maono na matendo, ili kwamba kuwe na ukweli unaoweza kuwekwa kwenye vitendo, na maarifa yaliyo na msingi wa maono. Ni hapo tu ndipo utakapokuwa mtu anayefuatilia ukweli.

Hatua tatu za kazi ndizo kiini cha usimamizi mzima wa Mungu, na ndani yazo zimeelezwa tabia ya Mungu na kile Alicho. Wale wasiojua kuhusu hatua tatu za kazi ya Mungu hawana uwezo wa kutambua jinsi Mungu anavyoonyesha tabia Yake, wala hawajui hekima ya kazi ya Mungu, na wanasalia kutojua njia nyingi Anazomwokoa mwanadamu, na mapenzi Yake kwa wanadamu wote. Hatua tatu za kazi ndizo maonyesho kamili ya kazi ya kumwokoa mwanadamu. Wale wasiofahamu hatua tatu za kazi watakosa kuelewa njia mbalimbali na kanuni za kazi ya Roho Mtakatifu; wale wanaoshikilia tu imara mafundisho ya dini yanayosalia kutoka katika hatua moja ya kazi ni watu wanaomwekea Mungu mipaka kwa mafundisho ya dini, na wale ambao imani yao kwa Mungu haina udhahiri na uhakika. Watu kama hao kamwe hawawezi kupokea wokovu wa Mungu. Ni hatua tatu tu za Mungu zinazoweza kuonyesha kabisa ukamilifu wa tabia ya Mungu, na kuonyesha kabisa nia ya Mungu ya kuwaokoa wanadamu wote, na mchakato mzima wa wokovu wa mwanadamu. Hili ni dhibitisho kuwa Yeye amemshinda Shetani na kumpata mwanadamu, ni dhibitisho la ushindi wa Mungu, na ni maonyesho ya tabia kamili ya Mungu. Wale wanaoelewa hatua moja tu kati ya hatua tatu za kazi ya Mungu wanajua tu sehemu ya tabia ya Mungu. Katika dhana ya mwanadamu, ni rahisi kwa hatua hii moja kuwa mafundisho ya kidini, panakuwa na uwezekano zaidi wa mwanadamu kuweka amri kumhusu Mungu, na mwanadamu anatumia hii sehemu moja ya tabia ya Mungu kama dhihirisho la tabia nzima ya Mungu. Zaidi ya hayo, mawazo mengi ya mwanadamu yanachanganywa ndani yake, hivi kwamba anaweka vikwazo imara kwa tabia, nafsi, na hekima ya Mungu, na pia kanuni za kazi ya Mungu ndani ya vigezo vyenye mipaka, akiamini kwamba ikiwa Mungu alikuwa hivi wakati mmoja, basi Yeye atasalia kuwa vile daima, na kamwe hatabadilika. Ni wale tu wanaojua na kuthamini hatua tatu za kazi ndio wanaoweza kumjua Mungu kabisa na kwa usahihi. Angalau, hawatamfafanua Mungu kama Mungu wa Waisraeli, ama Wayahudi, na hawatamwona kama Mungu atakayesulubiwa msalabani milele kwa ajili ya mwanadamu. Kama unapata kumjua Mungu kutokana na hatua moja ya kazi Yake tu, basi maarifa yako ni kidogo, kidogo sana. Maarifa yako ni sawa na tone moja katika bahari. Kama si hivyo, kwa nini wengi wa walinzi wa kidini wa kale walimtundika Mungu msalabani akiwa hai? Je, si kwa ajili mwanadamu humwekea Mungu mipaka kwenye vigezo fulani? Je, si watu wengi humpinga Mungu na kuzuia kazi ya Roho Mtakatifu kwa sababu hawajui kazi mbalimbali na tofautitofauti ya Mungu, na, zaidi ya hayo, kwa sababu wanamiliki maarifa na mafundisho duni ya kupima kazi ya Roho Mtakatifu? Ingawa uzoefu wa watu kama hawa ni wa juujuu tu, ni wenye majivuno na wadekezi katika asili yao, na wanatazama kazi ya Roho Mtakatifu kwa dharau, wanapuuza masomo ya Roho Mtakatifu na, hata zaidi, wanatumia hoja zao ndogo ndogo zee kudhibitisha kazi ya Roho Mtakatifu. Pia wanajifanya, na wanashawishika kabisa na elimu yao na maarifa yao, na kuwa wanaweza kusafiri duniani kote. Je, watu hawa si ni wale wanaochukiwa na kukataliwa na Roho Mtakatifu na je, si wataondolewa na enzi mpya? Je, si wale wanaokuja mbele ya Mungu na kumpinga waziwazi ni watu wadogo wasiojua na wasio na habari ya kutosha jinsi na wanajaribu kuonyesha walivyo werevu? Kwa maarifa haba ya Biblia, wanajaribu kupotosha “wasomi”; wa dunia, kwa mafundisho duni ya dini ili kuwafunza watu, wanajaribu kurudisha nyuma kazi ya Roho Mtakatifu, na kujaribu kuifanya ihusu mchakato wao wanavyofikiria, na kwa kuwa hawaoni mbali, wanajaribu kuona kwa mtazamo mmoja miaka 6,000 ya kazi ya Mungu. Watu hawa hawana mantiki yoyote hata kidogo! Kwa kweli, maarifa ya watu kumhusu Mungu yanavyozidi kuwa mengi, ndivyo wanavyokuwa wagumu wa kuhukumu kazi Yake. Zaidi ya hayo, wanazungumzia tu machache kuhusu maarifa yao ya kazi ya Mungu leo, lakini si wepesi wa kuhukumu. Kadri watu wanavyojua machache kumhusu Mungu, ndivyo wanavyozidi kuwa wenye majivuno na wenye kujiamini sana, na ndivyo wanavyozidi kutangaza nafsi ya Mungu kwa utundu—ilhali wanazungumzia tu nadharia, na wala hawapeani ushahidi wowote halisi. Watu kama hawa hawana thamani yoyote kabisa. Wale wanaoona kazi ya Roho Mtakatifu kama mchezo ni wenye upuzi! Wale wasio waangalifu wanapokumbana na kazi mpya ya Roho Mtakatifu, wanaopayuka, ni wepesi wa kuhukumu wanaoruhusu silika yao ya kiasili kukana haki ya kazi ya Roho Mtakatifu, na pia kuitusi na kuikufuru—je, watu hawa wasio na heshima si ni wale wasiojua kazi ya Roho Mtakatifu? Je, si wao ndio, zaidi ya hayo, wale wasiojua, wenye majivuno ya asili na wasioweza kutawalwa? Hata ikiwa siku itakuja ambapo watu hawa watakubali kazi mpya ya Roho Mtakatifu, bado Mungu hatawavumilia. Hawadharau tu wale wanaofanya kazi ya Mungu, bali pia wanamkufuru Mungu Mwenyewe. Watu kama hawa jasiri pasi na hadhari hawatasamehewa, katika enzi hii ama enzi itakayokuja na wataangamia kuzimuni milele! Watu kama hawa wasio na heshima, wenye kujifurahisha, wanajifanya kuwa wanamwamini Mungu, na kadiri wanavyozidi kufanya vile, ndivyo wanavyozidi kukosea amri za utawala wa Mungu. Je, si hao mafidhuli ambao kiasili hawazuiliki, na hawajawahi kumtii yeyote, wote hupitia njia hii? Je, si wao humpinga Mungu siku baada ya siku, Yeye ambaye daima huwa mpya na wala hazeeki? Leo, mnapaswa kuelewa mbona lazima mjue umuhimu wa hatua tatu za kazi ya Mungu. Maneno Ninayosema yana manufaa kwenu, wala si mazungumzo ya bure. Ukiyasoma tu kama mtu anayetazama na kupendezwa na maua anapoendesha farasi shoti, si bidii Yangu yote itakuwa kazi bure? Kila mmoja wenu anapaswa kujua asili yake. Wengi wenu wamebobea katika mabishano, majibu ya maswali ya nadharia yanatoka kinywani mwenu, lakini hamna la kusema kwa maswali kuhusu dutu. Hadi leo, bado mnashiriki mazungumzo duni, na hamuwezi kubadilisha asili yenu ya zamani, na wengi wenu hawana nia ya kubadilisha jinsi mnavyofuatilia ili kupata ukweli wa juu, mnaishi tu maisha yenu shingo upande. Je, watu kama hawa wataweza kumfuata Mungu hadi tamati vipi? Hata ikiwa mtafika mwishoni mwa safari, itakuwa na faida gani kwenu? Ni bora mbadili mawazo yenu kabla hamjachelewa, kufuatilia kwa kweli, au kujitoa mapema. Muda unapokatika utakuwa kimelea doezi—je, mko radhi kutekeleza jukumu kama hili la hali ya chini na lenye aibu?

Hatua tatu za kazi ni rekodi ya kazi nzima ya Mungu, ni rekodi ya wokovu wa Mungu wa mwanadamu, na si porojo tu. Kama kweli mnataka kutafuta kujua tabia nzima ya Mungu, basi sharti mfahamu hatua tatu za kazi inayofanywa na Mungu, na, zaidi, sharti msiache hatua yoyote. Hiki ndicho kiwango cha chini kinachopaswa kufikiwa na wale wanaotafuta kumjua Mungu. Mwanadamu mwenyewe hawezi kuvumbua maarifa ya Mungu. Si kitu ambacho mwanadamu mwenyewe anaweza kufikiria, wala si matokeo ya fadhila za Roho Mtakatifu kwa mtu mmoja. Badala yake, ni maarifa yanayotokea mwanadamu anapopitia kazi ya Mungu, na ni maarifa ya Mungu yanayotokana tu na mwanadamu kupitia ukweli wa kazi ya Mungu. Maarifa kama haya hayawezi kutimizwa kwa ghafla, wala si jambo linaloweza kufundishwa. Inahusiana kabisa na uzoefu wa kibinafsi. Wokovu wa Mungu wa mwanadamu ndiyo kiini cha hatua hizi tatu za kazi, ilhali katika kazi ya wokovu kumejumuishwa mbinu kadhaa za kufanya kazi na namna ambazo tabia ya Mungu imeonyeshwa. Hili ndilo jambo gumu sana kwa mwanadamu kutambua na kwa mwanadamu kuelewa. Mgawanyiko wa enzi, mabadiliko ya kazi ya Mungu, mabadiliko katika eneo la kazi, mabadiliko ya wanaopokea kazi na kadhalika—haya yote yamejumuishwa katika hatua tatu za kazi. Hususan, tofauti katika njia ya utendakazi wa Roho Mtakatifu, na vilevile mabadiliko katika tabia ya Mungu, picha, jina, utambulisho, au mabadiliko mengine, yote ni sehemu ya hatua tatu za kazi. Sehemu moja ya kazi inaweza tu kuwakilisha sehemu moja, na imewekewa mipaka ndani ya wigo fulani. Haihusiani na mgawanyiko wa enzi, ama mabadiliko ya kazi ya Mungu, wala masuala mengine. Huu ni ukweli ulio waziwazi. Hatua tatu za kazi ya Mungu ndizo ukamilifu wa kazi ya Mungu ya kumwokoa mwanadamu. Mwanadamu lazima ajue kazi ya Mungu, tabia ya Mungu katika kazi ya wokovu, na bila ukweli huu, maarifa yako kumhusu Mungu yatakuwa tu maneno matupu, ni mahubiri ya starehe tu. Maarifa kama haya hayawezi kumshawishi au kumshinda mtu, maarifa kama haya yako nje ya uhalisi, na si ukweli. Yanaweza kuwa mengi, na mazuri kwa masikio, lakini kama hayaambatani na tabia ya asili ya Mungu, basi Mungu hatakusamehe. Hatakosa kuyasifu maarifa yako tu, bali pia atakuadhibu kwa kuwa mwenye dhambi aliyemkufuru. Maneno ya kumjua Mungu hayazungumzwi kwa mzaha. Ingawa unaweza kuwa na ulimi laini wenye maneno matamu, na ingawa maneno yako ni ya werevu kiasi kwamba unaweza kubishana kitu kisichowezekana, bado huna elimu ya kuzungumza kuhusu maarifa ya Mungu. Mungu si mtu ambaye unaweza kuhukumu kwa urahisi, ama kusifu bila mpango, ama kupaka tope bila kujali. Unamsifu mtu yeyote na watu wowote, ilhali unajitahidi kupata maneno sahihi ya kuelezea ukuu wa wema na neema za Mungu—hili ndilo mshindwa yeyote hujifunza. Ingawa kuna wataalam wengi wa lugha wanaoweza kumwelezea Mungu, usahihi wa kile wanachoelezea ni asilimia moja ya ukweli unaozungumzwa na watu wa Mungu na wana misamiati michache tu, ilhali wanamiliki tajriba yenye uzito. Basi inaweza kuonekana kuwa maarifa ya Mungu yapo katika usahihi na uhalisi, na wala si utumiaji mzuri wa maneno au misamiati mingine, na kwamba maarifa ya mwanadamu na maarifa ya Mungu kabisa hayahusiani. Somo la kumjua Mungu liko juu zaidi kuliko sayansi za asili za mwanadamu. Ni somo linaloweza kutimizwa tu na idadi ndogo sana ya watu wanaotafuta kumjua Mungu, na haliwezi kutimizwa na mtu yeyote tu mwenye kipaji. Na kwa hivyo lazima msione kumjua Mungu na kufuatilia ukweli kama kwamba kunaweza kupatikana na mtoto mdogo tu. Pengine umekuwa na mafanikio makuu katika maisha yako ya kifamilia, ama kazi yako, ama katika ndoa yako, lakini inapofika kwenye ukweli, na somo la kumjua Mungu, huna lolote la kujivunia, hujatimiza malengo yoyote. Kutia ukweli kwenye vitendo, inaweza kusemwa, ni jambo gumu kwenu, na kumjua Mungu ni tatizo kuu hata zaidi. Hili ni tatizo lenu, na pia ni tatizo linalokabiliwa na wanadamu wote. Kati ya wale wenye mafanikio katika kumjua Mungu, karibu wote hawajafikia kiwango. Mwanadamu hajui maana ya kumjua Mungu, ama kwa nini ni muhimu kumjua Mungu, ama kiasi kipi kinahesabiwa kama kumjua Mungu. Hili ndilo linalomshangaza mwanadamu, na ni kitendawili kikubwa zaidi kinachokabiliwa na mwanadamu—na hakuna awezaye kujibu swali hili, ama aliye na hiari kujibu hili swali, kwa sababu, hadi leo, hamna katika wanadamu aliyefanikiwa katika kusomea kazi hii. Pengine, kitendawili cha hatua tatu za kazi kitakapotambulishwa kwa mwanadamu, kutakuwepo katika mfululizo kundi la watu wenye vipaji wanaomjua Mungu. Bila shaka, Natumaini kuwa hivyo ndivyo ilivyo, na, hata zaidi, Niko katika harakati ya kutekeleza kazi hii, na Ninatumaini kuona kujitokeza kwa vipaji zaidi kama hivi katika siku za hivi karibuni. Watakuwa wale wanaoshuhudia ukweli wa hatua hizi tatu za kazi, na, bila shaka, watakuwa pia wa kwanza kushuhudia hizi hatua tatu za kazi. Kama kutakuwa na aliye na vipaji hivi, siku ambayo kazi ya Mungu itafikia kikomo, ama kuwe na wawili ama watatu, na kibinafsi wamekubali kufanywa wakamilifu na Mungu mwenye mwili, basi hakuna jambo la kuhuzunisha na kujutia kama hili—ingawa ni katika hali mbaya zaidi tu. Kwa vyovyote vile, Ninatumai kuwa wale wote wanaotafuta kwa kweli wanaweza kupata baraka hii. Tangu mwanzo wa wakati, hakujawahi kuwa na kazi kama hii, hapo awali hakujawahi kuwa na kazi kama hii katika historia ya ukuaji wa mwanadamu. Kama kweli unaweza kuwa mmoja wa wale wa kwanza wanaomjua Mungu, je, si hii itakuwa heshima ya juu kuliko viumbe wote? Je, kuna kiumbe mwingine kati ya wanadamu anayeweza kusifiwa na Mungu zaidi? Kazi kama hii ni ngumu kutekeleza, lakini mwishowe bado itapokea malipo. Bila kujali jinsia yao ama uraia wao, wale wote wenye uwezo wa kufikia maarifa ya Mungu, mwishowe, watapokea heshima kuu ya Mungu, na watakuwa tu wenye kumiliki mamlaka ya Mungu. Hii ndiyo kazi ya leo, na pia ndiyo kazi ya siku za usoni; ni ya mwisho na ya juu zaidi kuwahi kutekelezwa katika miaka 6000 ya kazi, na ni njia ya kufanya kazi inayodhihirisha kila kundi la mwanadamu. Kupitia kazi ya kumfanya wanadamu kumjua Mungu, daraja tofauti za mwanadamu zinadhihirishwa: Wale wanaomjua Mungu wamehitimu kupokea baraka za Mungu na kukubali ahadi zake, wakati wale wasiomjua Mungu hawajahitimu kupokea baraka za Mungu wala kupokea ahadi zake. Wale wanaomjua Mungu ni wandani wa Mungu, na wale wasiomjua Mungu hawawezi kuitwa wandani wa Mungu; wandani wa Mungu wanaweza kupokea baraka zozote za Mungu, lakini wale wasio wandani wa Mungu hawastahili kazi yoyote Yake. Iwe ni dhiki, usafishaji, ama hukumu, yote ni kwa ajili ya kumfanya mwanadamu hatimaye kufikia maarifa ya Mungu na ili kwamba mwanadamu amtii Mungu. Hii ndiyo athari pekee itakayofikiwa hatimaye. Hakuna lolote katika hatua tatu za kazi lililofichwa, na hii ni faida kwa maarifa ya mwanadamu kuhusu Mungu, na humsaidia mwanadamu kupata maarifa kamili na mengi ya Mungu. Kazi hii yote ni ya kumfaidi mwanadamu.

Kazi ya Mungu Mwenyewe ni maono ambayo mwanadamu lazima afahamu, kwa kuwa kazi ya Mungu haiwezi kutekelezwa na mwanadamu, wala haimilikiwi na mwanadamu. Hatua tatu za kazi ndizo ukamilifu wa usimamizi wa Mungu, na hakuna ono kuu kuliko hili linalopaswa kufahamika kwa mwanadamu. Kama mwanadamu hafahamu maono haya makuu, basi si rahisi kumjua Mungu, na si rahisi kujua mapenzi ya Mungu, na, zaidi ya hayo, njia ambayo mwanadamu anapitia inazidi kuwa ngumu. Bila maono, mwanadamu hangeweza kufika umbali huu. Ni maono ambayo yamemlinda mwanadamu hadi leo, na ambayo yamempa mwanadamu ulinzi mkuu. Katika siku za usoni, maarifa yenu lazima yawe ya kina, na sharti mfahamu mapenzi Yake yote na umuhimu wa kazi Yake yenye busara katika hatua tatu za kazi. Hiki tu ndicho kimo chenu cha kweli. Hatua ya kazi ya mwisho haisimami peke yake, ila ni sehemu ya yote iliyounganishwa pamoja na hatua mbili za awali, ambayo ni kusema kwamba haiwezekani kukamilisha kazi nzima ya wokovu kwa kufanya kazi ya hatua moja pekee. Ingawa hatua ya mwisho ya kazi inaweza kumwokoa mwanadamu kabisa, hii haimaanishi kwamba ni muhimu tu kutekeleza hatua hii pekee, na kwamba hatua mbili za hapo awali hazihitajiki kumwokoa mwanadamu kutokana na ushawishi wa Shetani. Hakuna hatua moja kati ya zote tatu inayoweza kuwekwa kama maono ya kipekee ambayo lazima yajulishwe mwanadamu, kwa kuwa ukamilifu wa kazi ya wokovu ni hatua tatu za kazi, wala si hatua moja kati ya tatu. Ilimradi kazi ya wokovu bado haijakamilishwa, usimamizi wa Mungu utashindwa kufikia kikomo. Nafsi ya Mungu, tabia, na hekima zimeonyeshwa katika ukamilifu wa kazi ya wokovu, wala hazikufichuliwa kwa mwanadamu hapo mwanzo, lakini zimeonyeshwa hatua kwa hatua katika kazi ya wokovu. Kila hatua ya kazi ya wokovu huonyesha sehemu ya tabia ya Mungu, na sehemu ya nafsi Yake: si kila hatua ya kazi inayoweza moja kwa moja kuonyesha kabisa na kwa ukamilifu nafsi ya Mungu. Kwa hivyo, kazi ya wokovu inaweza tu kuhitimishwa hatua tatu za kazi zitakapokamilika, na kwa hivyo, maarifa ya mwanadamu ya ukamilifu wa Mungu hayawezi kutenganishwa na hatua tatu za kazi ya Mungu. Kile ambacho mwanadamu hupokea kutoka kwa hatua moja ya kazi ni tabia ya Mungu inayoonyeshwa katika sehemu moja ya kazi yake tu. Haiwezi kuwakilisha tabia na nafsi inayoonyeshwa katika hatua ya awali na ijayo. Hii ni kwa sababu kazi ya kumwokoa mwanadamu haiwezi kumalizika mara moja katika kipindi kimoja, ama katika eneo moja, lakini hukuwa kwa kina hatua kwa hatua kulingana na kiwango cha kukua kwa mwanadamu katika wakati na maeneo tofauti. Ni kazi inayofanywa hatua kwa hatua, na haikamilishwi katika hatua moja. Na kwa hiyo, hekima yote ya Mungu imejumuishwa katika hatua tatu, badala ya hatua moja. Nafsi yake yote na hekima yake yote zimewekwa wazi katika hatua hizi tatu, na kila hatua ina nafsi Yake, na ni rekodi ya hekima ya kazi Yake. Mwanadamu anapaswa kujua tabia yote ya Mungu iliyoonyeshwa katika hatua hizi tatu. Nafsi hii ya Mungu ndiyo ina maana zaidi kwa wanadamu wote, na ikiwa watu hawana maarifa haya wanapomwabudu Mungu, basi hawana tofauti na wale wanaoabudu Budha. Kazi ya Mungu kati ya wanadamu haijafichiwa mwanadamu, na inapaswa kujulikana na wale wote wanaomwabudu Mungu. Kwa sababu Mungu ametekeleza hatua tatu za kazi ya wokovu kati ya wanadamu, mwanadamu anapaswa kujua maonyesho ya kile Anacho na alicho wakati wa hatua hizi tatu za kazi. Hili ndilo ambalo ni lazima lifanywe na mwanadamu. Kile ambacho Mungu anamfichia mwanadamu ni kile ambacho mwanadamu hawezi kutimiza, na kile ambacho mwanadamu hapaswi kujua, ilhali yale Mungu anayomfunulia mwanadamu ni yale ambayo mwanadamu anapaswa kujua na yale ambayo mwanadamu anapaswa kumiliki. Kila moja ya hatua tatu za kazi huendelea juu ya msingi wa hatua iliyopita; haitekelezwi peke yake, tofauti na kazi ya wokovu. Ingawa kuna tofauti kubwa katika enzi na aina ya kazi ambayo inafanywa, katika kiini chake bado ni wokovu wa mwanadamu, na kila hatua ya kazi ya wokovu ina kina kuliko iliyopita. Kila hatua inaendelea kutoka kwa msingi wa hatua ya mwisho ambayo haiondolewi. Kwa njia hii, katika kazi Yake ambayo daima huwa mpya na kamwe si kuukuu, Mungu mara kwa mara anaonyesha vipengele vya tabia Yake ambavyo havijawahi kuonyeshwa kwa mwanadamu hapo awali, na daima anamfichulia mwanadamu kazi Yake mpya, na nafsi Yake mpya, na hata ikiwa wazoefu wakongwe wa kidini hufanya juu chini kukinzana na hili, na kulipinga waziwazi, Mungu daima hufanya kazi mpya ambayo anakusudia kufanya. Kazi Yake daima hubadilika, na kwa sababu hii, daima inakabiliwa na upinzani wa mwanadamu. Na hivyo, pia, tabia Yake inabadilika daima, na vilevile enzi na wanaopokea kazi Yake. Zaidi ya hayo, kila mara Yeye hufanya kazi ambayo haijawahi kufanywa tena, hata kufanya kazi ambayo huonekana kwa mwanadamu kuhitilafiana na kazi iliyofanywa awali, kuwa kinyume nayo. Mwanadamu anaweza kukubali tu aina moja ya kazi, ama njia moja ya matendo. Ni vigumu kwa wanadamu kukubali kazi ama njia za matendo, ambayo yanakinzana nao, ama yaliyo juu kuwaliko—lakini Roho Mtakatifu daima anafanya kazi mpya, na kwa hivyo kunakuwepo kikundi baada ya kikundi cha wataalamu wa kidini wanaoipinga kazi mpya ya Mungu. Watu hawa wamekuwa wataalamu hasa kwa sababu mwanadamu hana maarifa ya jinsi Mungu huwa mpya wala hazeeki, na zaidi ya hayo, hana maarifa ya kanuni za kazi ya Mungu, na hata zaidi hawana maarifa ya njia nyingi ambazo Mungu humwokoa mwanadamu. Kwa hivyo, mwanadamu kabisa anashindwa kueleza kama ni kazi inayotoka kwa Roho Mtakatifu, au ni kazi ya Mungu Mwenyewe. Watu wengi hushikilia mtazamo ambao, kama inalingana na maneno yanayokuja kabla, basi wanaweza kuikubali, na kama kuna tofauti na kazi ya awali, basi wanaipinga na kuikataa. Leo, je, nyote hamjafuata katika kanuni hizi? Hatua tatu za kazi ya wokovu hazijakuwa na athari kubwa kwenu, na kuna wale wanaoamini kuwa hatua mbili zilizopita za kazi ni mzigo usiohitaji kufahamika. Wanafikiria kuwa hatua hizi hazifai kutangazwa kwa umati na zinafaa kufutwa haraka iwezekanavyo, ili watu wasihisi kwamba wamezidiwa na hatua mbili za awali za zile hatua tatu za kazi. Wengi wanaamini kuwa kupeana ufahamu kuhusu hatua mbili zilizopita ni hatua ya mbali sana, wala haina faida katika kumjua Mungu—hivyo ndivyo mnavyofikiria. Leo, nyote mnaamini kuwa ni haki kutenda vile, lakini siku itawadia ambapo mtagundua umuhimu wa kazi Yangu: Mjue kuwa Sifanyi kazi yoyote ambayo haina umuhimu. Kwa sababu Ninawatangazia hatua tatu za kazi, kwa hivyo lazima ziwe na faida kwenu; kwa sababu hatua hizi tatu za kazi ndizo kiini cha usimamizi mzima wa Mungu, kwa hivyo lazima ziwe lengo la kila mmoja duniani. Siku moja, nyote mtagundua umuhimu wa kazi hii. Fahamuni kuwa mnapinga kazi ya Mungu, ama mnatumia dhana zenu kupima kazi ya leo, kwa sababu hamjui kanuni za kazi ya Mungu, na kwa sababu hamchukulii kazi ya Roho Mtakatifu kwa makini kutosha. Upinzani wenu kwa Mungu na kuzuia kazi ya Roho Mtakatifu kumetokana na dhana zenu na upumbavu wenu wa kiasili. Si kwa sababu kazi ya Mungu si sawa, lakini ni kwa sababu mna tabia ya kiasili ya kutotii. Baada ya kupata imani yao katika Mungu, watu wengine hawawezi hata kusema kwa uhakika mwanadamu alikotoka, ilhali wanathubutu kuzungumza hadharani wakitathmini haki na makosa ya kazi ya Roho Mtakatifu. Na pia wanawakemea mitume ambao wana kazi mpya ya Roho Mtakatifu, wakitoa maoni huku wakizungumza kwa zamu; ubinadamu wao uko chini sana, na hawana hisia zozote. Je, si siku itawadia ambapo watu kama hawa watakataliwa na kazi ya Roho Mtakatifu, na kuchomwa katika moto wa kuzimu? Hawafahamu kazi ya Mungu, lakini badala yake wanakosoa kazi Yake, na pia wanajaribu kumwagiza Mungu jinsi atakavyofanya kazi. Je, ni kwa namna gani watu hawa wasio na busara watamjua Mungu? Mwanadamu huja kumjua Mungu wakati anapomtafuta na anapokuwa na uzoefu naye; si katika kumkosoa kwa ghafla ndipo anapokuja kumjua Mungu kwa kupitia kutiwa nuru na Roho Mtakatifu. Kadiri maarifa ya watu kuhusu Mungu yanavyozidi kuwa sahihi, ndivyo upinzani wao Kwake unavyopungua. Kinyume na hayo, kadri watu wanavyomjua Mungu kwa kiasi kidogo, ndivyo wanavyokuwa na uwezekano wa kumpinga. Dhana zako, ubinadamu wako wa zamani, na utu wako, tabia na maadili ndiyo “mtaji” ambao unampingia Mungu, na kadri unavyokuwa mpotovu, ama ulivyoshushwa heshima na ulivyo duni, ndivyo unavyozidi kuwa adui wa Mungu. Wale waliomilikiwa na dhana kali na wenye tabia ya unafiki wamo hata zaidi katika uadui wa Mungu mwenye mwili, na watu kama hawa ni wapinga Kristo. Ikiwa dhana zako hazitarekebishwa, basi daima zitakuwa kinyume na Mungu; daima hutalingana na Mungu, na daima utakuwa mbali na Yeye.

Ni katika kuweka dhana zako za kale kando tu ndipo utakapoweza kupata maarifa mapya, ilhali maarifa ya zamani si lazima yawe dhana za zamani. “Dhana” inamaanisha vitu vinavyodhaniwa na mwanadamu ambavyo viko mbali na uhalisi. Kama maarifa ya zamani yalikuwa yamepitwa na wakati katika enzi ya kale, na yalimzuia mwanadamu kuingia katika kazi mpya, basi maarifa kama yale pia ni dhana. Ikiwa mwanadamu ataweza kuchukua mwelekeo mzuri kwa maarifa kama yale, na anaweza pata kumjua Mungu kutoka kwa vipengele tofauti, kuunganisha ya zamani na mapya, basi maarifa ya kale yatamsaidia mwanadamu, na yatakuwa msingi wa mwanadamu kuingia katika enzi mpya. Funzo la kumjua Mungu linahitaji kwamba uwe stadi wa kanuni nyingi: jinsi ya kuingia kwenye njia ya kumjua Mungu, ukweli gani unapaswa kuelewa ili kumjua Mungu, na jinsi ya kuondoa dhana zako na asili yako ya kale ili kwamba uweze kutii mipango yote ya kazi mpya ya Mungu. Ukitumia kanuni hizi kama msingi wa kuingia kwenye somo la kumjua Mungu, basi maarifa yako yatakuwa na kina zaidi na zaidi. Kama una maarifa wazi ya hatua tatu za kazi—ambayo ni kusema kwamba, ya mpango mzima wa usimamizi wa Mungu—na ikiwa utaweza kupatanisha hatua mbili za awali na hatua ya sasa, na unaweza kuona kwamba ni kazi iliyofanywa na Mungu mmoja, basi utakuwa na msingi imara zaidi. Hatua tatu za kazi zilifanywa na Mungu mmoja; haya ndiyo maono makubwa zaidi, na ndiyo njia ya pekee ya kumjua Mungu. Hatua tatu za kazi zingefanywa tu na Mungu Mwenyewe, na hapana mwanadamu yeyote ambaye angeweza kufanya kazi kama hii kwa niaba Yake—ambayo ni kusema kuwa ni Mungu Mwenyewe pekee ambaye angeifanya kazi Yake toka mwanzo hadi leo. Ingawa hatua tatu za kazi ya Mungu zimefanywa katika enzi tofauti na maeneo tofauti, na ingawa kazi ya kila moja ni tofauti, yote ni kazi iliyofanywa na Mungu mmoja. Kati ya maono yote, hili ndilo kuu zaidi ambalo mwanadamu anapaswa kulijua, na ikiwa litaeleweka kabisa na mwanadamu, basi ataweza kusimama imara. Leo, tatizo kuu linalokumba dini na madhehebu kadhaa ni kwamba hazijui kazi ya Roho Mtakatifu, na hazina uwezo wa kutofautisha kati ya kazi ya Roho Mtakatifu na kazi isiyo ya Roho Mtakatifu—na kwa hivyo hawawezi kueleza kama hatua hii ya kazi, kama hatua mbili za awali, pia zimefanywa na Yehova Mungu. Ingawa watu wanamfuata Mungu, wengi hawawezi kueleza kama ni njia sahihi. Mwanadamu anahofia ikiwa hii ndiyo njia inayoongozwa na Mungu Mwenyewe, na kama Mungu kupata mwili ni jambo la hakika, na watu wengi bado hawana dokezo jinsi ya kupambanua ikifikia maneno kama haya. Wale wanaomfuata Mungu hawawezi kujua njia, na kwa hivyo habari zinazozungumzwa zinaathiri sehemu ndogo tu kati ya watu hawa na hayana uwezo wa kufaa kikamilifu, na kwa hivyo, hili basi linaathiri kuingia kwa maisha kwa watu kama hawa. Ikiwa mwanadamu anaweza kuona katika hatua tatu za kazi kuwa zilitekelezwa na Mungu Mwenyewe wakati tofauti, katika maeneo tofauti, na kwa watu tofauti; ikiwa mwanadamu anaweza kuona kuwa ingawa kazi ni tofauti, yote imefanywa na Mungu mmoja, na kwa kuwa ni kazi ambayo imefanywa na Mungu mmoja, basi lazima iwe sawa, na bila dosari, na kwamba ingawa hailingani na dhana za mwanadamu, hakuna kupinga kuwa ni kazi iliyofanywa na Mungu mmoja—ikiwa mwanadamu anaweza kusema kwa hakika kuwa ni kazi ya Mungu mmoja, basi dhana zake zitakuwa duni, na ambazo hazifai kutajwa. Kwa sababu maono ya mwanadamu hayako wazi, na mwanadamu anamjua tu Yehova kama Mungu, na Yesu kama Bwana, na ana mitazamo miwili kumhusu Mungu mwenye mwili wa leo, watu wengi wamejitoa kwa ajili ya kazi ya Yehova na Yesu, na wamezingirwa na dhana kuhusu kazi ya leo, watu wengi daima huwa na shaka na hawachukulii kazi ya leo kwa makini. Mwanadamu hana uelewa kuhusu hatua mbili za mwisho, ambazo hazikuonekana. Hio ni kwa sababu mwanadamu haelewi uhalisi wa hatua mbili za mwisho za kazi, na wala hakuzishuhudia binafsi. Ni kwa sababu haziwezi kuonekana ndiyo mwanadamu anawaza jinsi anavyopenda; bila kujali atakayodhania, hakuna ukweli wa kudhibitisha, na yeyote wa kurekebisha. Mwanadamu anaruhusu silika yake ya asili itawale, huku akikosa kujali na kuachilia mawazo yake yaende popote, kwa kuwa hakuna ukweli wa kudhibitisha, na kwa hivyo dhana za mwanadamu zinakuwa “ukweli,” bila kujali kama zina dhibitisho. Kwa hivyo mwanadamu anaamini Mungu wake aliyemuwazia akilini mwake, na hamtafuti Mungu wa uhalisi. Ikiwa mtu mmoja ana aina moja ya imani, basi kati ya watu mia moja kuna aina mia moja za imani. Mwanadamu ana imani kama hizi kwa maana hajaona uhalisi wa kazi ya Mungu, kwa sababu amesikia tu kwa masikio yake na hajaona kwa macho yake. Mwanadamu amesikia hekaya na hadithi—lakini amesikia kwa nadra kuhusu maarifa ya ukweli ya kazi ya Mungu. Hivyo ni katika dhana zao ndivyo watu ambao wamekuwa waumini kwa mwaka mmoja tu wanaamini Mungu, na hilo ni kweli pia kwa wale ambao wamemwamini Mungu katika maisha yao yote. Wale ambao hawawezi kuona ukweli daima hawawezi kuepuka imani ambayo wana dhana kwazo kumhusu Mungu. Mwanadamu anaamini kuwa amejiweka huru kutokana na vifungo vya dhana zake za kale, na ameingia eneo jipya. Je, mwanadamu hajui kuwa maarifa ya wale wasioweza kuona uso wa kweli wa Mungu kuwa ni dhana na tetesi? Mwanadamu anafikiria kuwa dhana zake ni sawa, na wala hayana kasoro, na hufikiri kuwa hizi dhana zimetoka kwa Mungu. Leo, mwanadamu anaposhuhudia kazi ya Mungu, anaachilia dhana zilizokuwa zimeongezeka kwa miaka mingi. Mawazo na dhana za awali zilikuwa vizuizi vya kazi ya hatua hii, na inakuwa vigumu kwa mwanadamu kuachana na dhana kama hizo na kupinga mawazo kama yale. Dhana kuhusu kazi hii ya hatua kwa hatua ya wengi wa wale wanaomfuata Mungu hadi leo zimekuwa za kuhuzunisha na watu hawa pole pole wamefanya uadui wa kikaidi na Mungu mwenye mwili hatua kwa hatua, na chanzo cha chuki ni mawazo na dhana za mwanadamu. Ni hasa kwa sababu ukweli haumruhusu mwanadamu kuwa na uhuru wa hiari ya mawazo yake, na, zaidi ya hayo, hauwezi kupingwa na mwanadamu kwa urahisi, na mawazo na dhana za mwanadamu hazistahimili uwepo wa ukweli, na hata zaidi ya hayo, kwa sababu mwanadamu hawezi kufikiria kuhusu usahihi na unyofu wa ukweli, na kwa nia moja tu huachilia mawazo yake, na hutumia dhana yake, kwamba dhana na mawazo ya mwanadamu zimekuwa adui wa kazi ya leo, kazi ambayo haiambatani na dhana za mwanadamu. Hili linaweza kusemwa kuwa kasoro ya dhana za mwanadamu, na wala si dosari ya kazi ya Mungu. Mwanadamu anaweza kufikiria lolote atakalo, lakini hawezi kupinga waziwazi hatua yoyote ya kazi ya Mungu au hata sehemu yoyote; ukweli wa kazi ya Mungu hauwezi kukiukwa na mwanadamu. Unaweza kuruhusu mawazo yako yatawale, na unaweza pia kujumuisha hadithi nzuri kuhusu kazi ya Yehova na Yesu, lakini kamwe huwezi kupinga ukweli wa kila hatua ya kazi ya Yehova na Yesu; hii ni kanuni, na pia ni amri ya utawala, na mnapaswa kuelewa umuhimu wa masuala haya. Mwanadamu anaamini kuwa hatua hii ya kazi hailingani na dhana za mwanadamu, na hivi sivyo katika hatua mbili zilizopita za kazi. Katika mawazo yake, mwanadamu anaamini kuwa kazi ya hatua mbili zilizopita kwa hakika si sawa na kazi ya leo—lakini je, umewahi kufikiria kuwa kanuni zote za kazi ya Mungu ni sawa, na kuwa kazi Yake huwa vitendo daima, na kuwa, bila kujali enzi, daima kutakuwa na halaiki ya watu wanaokataa na kuupinga ukweli wa kazi Yake? Wale wote ambao leo wanakataa na kuipinga hatua hii ya kazi bila shaka wangempinga Mungu wakati uliopita, kwa kuwa watu kama hawa daima watakuwa adui za Mungu. Watu wanaoujua ukweli wa kazi ya Mungu wataona hatua tatu za kazi kama kazi ya Mungu mmoja, na watatupilia mbali dhana zao. Hawa ni watu wanaomjua Mungu, na watu kama hawa ndio kwa kweli humfuata Mungu. Wakati ambapo usimamizi mzima wa Mungu utakaribia kufika mwisho, Mungu ataweka vitu vyote kulingana na aina. Mwanadamu aliumbwa kwa mikono ya Muumba, na mwishowe lazima kabisa Amrudishe mwanadamu chini ya utawala Wake; huu ndio mwisho wa hatua tatu za kazi. Hatua ya kazi ya siku za mwisho, na hatua mbili zilizopita katika Israeli na Yudea, ni mpango wa Mungu wa usimamizi katika dunia nzima. Hakuna anayeweza kupinga hili, na ni ukweli wa kazi ya Mungu. Ingawa watu hawajapata uzoefu ama kushuhudia nyingi za kazi hizi, ukweli unabaki kuwa ukweli, na hauwezi kukanwa na mwanadamu yeyote. Watu wanaomwamini Mungu katika nchi zote duniani watakubali hatua tatu za kazi. Kama wajua tu hatua moja ya kazi, na huelewi hatua nyingine mbili za kazi, na huelewi kazi ya Mungu katika wakati uliopita, basi huwezi kuongea ukweli wa mpango mzima wa usimamizi wa Mungu, na maarifa yako ya Mungu yameegemea upande mmoja, kwa kuwa katika imani yako katika Mungu humfahamu, ama kumwelewa, na kwa hivyo hustahili kutoa ushuhuda wa Mungu. Bila kujali kama maarifa yako ya sasa ya mambo haya yana kina kirefu ama cha juujuu tu, mwishowe, lazima muwe na maarifa, na ushawishike kabisa, na watu wote wataona uzima wa kazi ya Mungu na kunyenyekea chini ya utawala wa Mungu. Mwishoni mwa kazi hii, madhehebu yote yatakuwa moja, viumbe wote watarejea chini ya utawala wa Muumba, viumbe wote watamwabudu Mungu mmoja wa kweli, na dini zote ovu zitakuwa bure, na hazitaonekana tena.

Mbona mfululizo huu wa marejeo kwa hatua tatu za kazi? Kupita kwa enzi, maendeleo ya kijamii, na uso wa asili unaobadilika yote hufuata mabadiliko katika hatua tatu za kazi. Mwanadamu hubadilika kwa wakati na kazi ya Mungu, na wala hakui peke yake mwenyewe. Kutajwa kwa hatua tatu za kazi ya Mungu ni kwa ajili ya kuleta viumbe wote, na watu kutoka dini zote, chini ya utawala wa Mungu mmoja. Bila kujali wewe ni wa dini gani, mwishowe nyote mtanyenyekea chini ya utawala wa Mungu. Ni Mungu Mwenyewe tu anayeweza kufanya kazi hii; haiwezi kufanywa na kiongozi yeyote wa kidini. Kuna dini kadhaa kuu duniani, na kila moja ina kichwa, ama kiongozi, na wafuasi wameenea katika nchi tofauti na maeneo yote duniani; kila nchi, iwe ndogo au kubwa, ina dini tofauti ndani yake. Hata hivyo, bila kujali ni dini ngapi zilizo duniani, watu wote wanaoishi duniani mwishowe wanaishi katika uongozi wa Mungu mmoja, na uwepo wao hauongozwi na viongozi wa kidini au vichwa. Ambayo ni kusema kwamba wanadamu hawaongozwi na kiongozi fulani wa kidini ama kiongozi; badala yake wanadamu wote wanaongozwa na Muumba, aliyeziumba mbingu na nchi, na vitu vyote, na ambaye aliwaumba wanadamu—na huu ni ukweli. Hata ingawa dunia ina dini kadhaa kuu, bila kujali jinsi zilivyo kuu, zote zipo chini ya utawala wa Muumba, na hakuna inayoweza kuzidi wigo wa mamlaka hii. Maendeleo ya wanadamu, maendeleo ya kijamii, maendeleo ya sayansi ya asili—kila moja haitengani na mipango ya Muumba, na kazi hii sio kitu kinachoweza kufanywa na uongozi fulani wa dini. Viongozi wa dini ni viongozi tu wa dini fulani, na hawawezi kuwakilisha Mungu, ama Yule aliyeziumba mbingu na nchi na vitu vyote. Viongozi wa kidini wanaweza kuongoza wale wote walio katika dini yote, lakini hawawezi kuamrisha viumbe vyote vilivyo chini ya mbingu—huu ni ukweli uliokubalika ulimwenguni. Viongozi wa dini ni viongozi tu, na hawawezi kuwa sawa na Mungu (Muumba). Vitu vyote vi mikononi mwa Muumba, na mwishowe vyote vitarejea mikononi mwa Muumba. Mwanadamu kiasili aliumbwa na Mungu, na haijalishi dini, kila mtu atarejea katika utawala wa Mungu—hili haliwezi kuepukika. Ni Mungu tu Aliye Juu Zaidi kati ya vitu vyote, na mtawala mkuu kati ya viumbe wote lazima pia warejee chini ya utawala Wake. Bila kujali mwanadamu ana hadhi ya juu kiasi gani, hawezi kumfikisha mwanadamu kwenye hatima inayomfaa, wala hakuna anayeweza kuainisha kila kitu kulingana na aina. Yehova mwenyewe alimuumba mwanadamu na kumwainisha kila mmoja kulingana na aina na siku ya mwisho itakapowadia bado Atafanya kazi Yake Mwenyewe, kuanisha kila kitu kulingana na aina—hili haliwezi kufanywa na mwingine isipokuwa Mungu. Hatua tatu za kazi ambazo zilifanywa tangu mwanzo hadi leo zote zilitekelezwa na Mungu Mwenyewe, na zilitekelezwa na Mungu mmoja. Ukweli wa hatua tatu za kazi ni ukweli wa uongozi wa Mungu kwa wanadamu wote, ukweli ambao hakuna anayeweza kuupinga. Mwishoni mwa hatua tatu za kazi, vitu vyote vitaainishwa kulingana na aina na kurejea chini ya utawala wa Mungu, kwa kuwa duniani kote kuna Mungu mmoja tu, na hakuna dini nyingine. Yule asiyeweza kuiumba dunia hataweza kuiangamiza, ilhali Yule aliyeumba dunia hakika ataiangamiza, na kwa hivyo, kama mtu hana uwezo wa kutamatisha enzi na ni wa kumsaidia mwanadamu kukuza akili zake tu, basi hakika hatakuwa Mungu, na hakika hatakuwa Bwana wa mwanadamu. Hataweza kufanya kazi kuu kama hii; kuna mmoja tu anayeweza kufanya kazi kama hii, na wote wasioweza kufanya hii kazi hakika ni adui wala si Mungu. Dini zote ovu hazilingani na Mungu, na kwa sababu hawalingani na Mungu, wao ni adui za Mungu. Kazi yote inafanywa na huyu Mungu mmoja wa kweli, na ulimwengu mzima unatawaliwa na huyu Mungu mmoja. Bila kujali kama Anafanya kazi Uchina ama Israeli, bila kujali kama kazi inafanywa na Roho ama mwili, yote hufanywa na Mungu Mwenyewe, na haiwezi kufanywa na mwingine yeyote. Ni kabisa kwa sababu Yeye ni Mungu wa wanadamu wote ndiyo kwamba Yeye hufanya kazi kwa njia ya uhuru, pasipo kuwekewa masharti yoyote—na haya ndiyo maono makuu zaidi. Kama kiumbe wa Mungu, kama ungependa kutekeleza jukumu la kiumbe wa Mungu na kuelewa mapenzi ya Mungu, lazima uelewe kazi ya Mungu, lazima uelewe mapenzi ya Mungu kwa viumbe, lazima uelewe mpango Wake wa usimamizi, na lazima uelewe umuhimu wote wa kazi Anayofanya. Wale wasioelewa hivi hawajahitimu kuwa viumbe wa Mungu! Kama kiumbe wa Mungu, kama huelewi ulikotoka, huelewi historia ya mwanadamu na kazi yote iliyofanywa na Mungu, na, hata zaidi, huelewi jinsi mwanadamu ameendelea hadi leo, na huelewi ni nani anayeamuru wanadamu wote, basi huna uwezo wa kutekeleza wajibu wako. Mungu amemwongoza mwanadamu hadi leo, na tangu alipomuumba mwanadamu duniani Hajawahi kumwacha. Roho Mtakatifu daima haachi kufanya kazi, hajawahi kuacha kumwongoza mwanadamu, na hajawahi kumwacha. Lakini mwanadamu hatambui kuwa kuna Mungu, pia hamjui Mungu, na je, kuna jambo la kufedhehesha zaidi kuliko hili kwa viumbe wote wa Mungu? Mungu binafsi humwongoza mwanadamu, lakini mwanadamu haelewi kazi ya Mungu. Wewe ni kiumbe wa Mungu, ilhali huelewi historia yako mwenyewe, na wala hujui ni nani aliyekuongoza katika safari yako, hutambui kazi iliyofanywa na Mungu, na kwa hivyo huwezi kumjua Mungu. Ikiwa hujui sasa, basi hutawahi kuhitimu kutoa ushuhuda kwa Mungu. Leo, Muumba binafsi huwaongoza watu wote kwa mara nyingine, na kuwafanya watu wote kuona hekima Yake, uweza, wokovu, na kustaajabisha Kwake. Ilhali bado hujatambua au kuelewa—na kwa hivyo, je, si wewe ndiwe utakayekosa kupokea wokovu? Wale walio wa Shetani hawaelewi maneno ya Mungu, na wale walio wa Mungu wanaweza kusikia sauti ya Mungu. Wale wote wanaotambua na kuelewa maneno Ninayozungumza ni wale watakaookolewa, na kumshuhudia Mungu; wote wasioelewa maneno Ninayoyazungumza hawawezi kutoa ushuhuda kwa Mungu, na ni wale watakaoondolewa. Wale wasioyaelewa mapenzi ya Mungu na hawaitambui kazi ya Mungu hawawezi kupata maarifa ya Mungu, na watu kama hawa hawawezi kutoa ushuhuda kwa Mungu. Kama ungependa kumshuhudia Mungu, basi lazima umjue Mungu, na maarifa ya Mungu yanapatikana kwa kupitia kazi ya Mungu. Kwa ufupi, kama ungependa kumjua Mungu, basi lazima ujue kazi ya Mungu: Kufahamu kazi ya Mungu ndilo jambo la umuhimu kabisa. Hatua tatu za kazi zitakapofikia tamati, patafanyika kundi la watu wanaomshuhudia Mungu, kundi la wale wanaomjua Mungu. Watu hawa wote watamjua Mungu na wataweza kuonyesha ukweli kwa matendo. Watakuwa na ubinadamu na hisia, na wote watajua hatua tatu za kazi ya wokovu ya Mungu. Hii ndiyo kazi ambayo itatekelezwa mwishowe, na watu hawa ndio dhihirisho la kazi ya miaka 6,000 ya usimamizi, na ndio ushuhuda wenye nguvu zaidi kwa kushindwa kwa Shetani. Wale wanaoweza kumshuhudia Mungu wataweza kupokea ahadi na baraka za Mungu, na litakuwa ndilo kundi litakalosalia pale mwisho kabisa, lile linalomiliki mamlaka ya Mungu na lililo na ushuhuda wa Mungu. Pengine wale kati yenu wanaweza wote kuwa sehemu ya kundi hili, ama pengine nusu tu, ama wachache tu—inategemea radhi yenu na ufuatiliaji wenu.

Iliyotangulia: Kazi ya Mungu na Kazi ya Mwanadamu

Inayofuata: Mwanadamu Aliyepotoka Anahitaji Zaidi Wokovu wa Mungu Mwenye Mwili

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp