Ahadi kwa Wale Wanaofanywa Kuwa Watimilifu
Njia ambayo kwayo Mungu humfanya mwanadamu kuwa mtimilifu ni ipi? Inajumuisha vipengele vipi? Je, uko tayari kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu? Je, uko tayari kukubali hukumu na kuadibu Kwake? Unajua nini kuhusu maswali haya? Ikiwa huna ufahamu wowote wa kuzungumzia, basi hili ni thibitisho kwamba bado huijui kazi ya Mungu, kwamba hujatiwa nuru na Roho Mtakatifu hata kidogo. Haiwezekani kwa watu kama hao kufanywa kuwa watimilifu. Wanapewa tu kiasi kidogo cha neema ili wafurahie kwa muda mfupi, na haitadumu kwa muda mrefu. Watu hawawezi kufanywa kuwa watimilifu na Mungu ikiwa wanafurahia tu neema Yake. Wengine huwa wametosheka wakati mwili wao una amani na starehe, wakati maisha yao ni rahisi na yasiyo na dhiki au balaa, wakati familia yao yote inaishi kwa upatanifu, bila ugomvi wala migogoro—na wanaweza hata kuamini kwamba hii pekee ndiyo baraka ya Mungu. Kwa kweli, ni neema ya Mungu tu. Hampaswi kutosheka na kufurahia tu neema ya Mungu. Fikira kama hizo ni duni sana. Hata ukisoma maneno ya Mungu kila siku, na ukiomba kila siku, na roho yako ihisi furaha kuu na iwe na amani hasa, ikiwa hatimaye huna la kusema kuhusu ufahamu wako wa Mungu na kazi Yake, na hujapitia chochote, na haijalishi umekula na kunywa neno la Mungu kiasi gani, ikiwa unachohisi tu ni amani na furaha za kiroho, na kwamba neno la Mungu ni tamu kupita kiasi, kana kwamba huwezi kutosheka nalo, lakini huna upitiaji wowote halisi wa maneno ya Mungu na huna kabisa uhalisi wa maneno Yake, basi unaweza kupata nini kutokana na imani kama hiyo katika Mungu? Ikiwa huwezi kuishi kwa kudhihirisha kiini cha maneno ya Mungu, basi kula na kunywa kwako maneno haya na maombi yako si chochote ila imani ya kidini. Watu kama hao hawawezi kufanywa kuwa watimilifu na Mungu na hawawezi kupatwa na Yeye. Watu wanaopatwa na Mungu ni wale wanaofuatilia ukweli. Kile ambacho Mungu anapata si mwili wa mwanadamu, si vitu ambavyo ni vyake, bali ni sehemu iliyo ndani yake ambayo ni ya Mungu. Hivyo, Mungu anapowafanya watu kuwa watimilifu, Hafanyi miili yao kuwa mitimilifu, bali mioyo yao, Akiiruhusu mioyo yao ipatwe na Mungu; yaani, Mungu kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, kimsingi, ni Mungu kuufanya moyo wa mwanadamu kuwa mtimilifu ili moyo huu uweze kumgeukia Mungu na ili uweze kumpenda Yeye.
Mwili wa mwanadamu ni wa nyama na damu. Haina maana kwa Mungu kuupata mwili wa mwanadamu, kwa maana mwili wa mwanadamu ni kitu ambacho bila shaka huharibika na hakiwezi kupokea urithi au baraka Zake. Ikiwa mwili wa mwanadamu ungepatwa, na mwili wa mwanadamu pekee ndio ungekuwa katika mkondo huu, basi ingawa mwanadamu angekuwa katika mkondo kwa jina tu, moyo wake ungekuwa wa Shetani. Hilo likiwa hivyo, mbali na watu kutoweza kuwa udhihirisho wa Mungu, pia wangekuwa mzigo Wake, na hivyo uteuzi wa Mungu wa watu usingekuwa na maana. Wale ambao Mungu anakusudia kuwafanya kuwa watimilifu wote watapokea baraka Zake na urithi Wake. Yaani, wanakubali kile Mungu anacho na alicho ili kiwe kile walicho nacho ndani; wana maneno yote ya Mungu yaliyofanyiwa kazi ndani yao; na chochote kile Mungu alicho, wanaweza kukikubali chote jinsi kilivyo. Kwa njia hii, wanaishi kwa kudhihirisha ukweli. Hii ndiyo aina ya mtu anayefanywa kuwa mtimilifu na Mungu na anayepatwa na Mungu. Ni mtu kama huyu tu ndiye anayestahili kurithi baraka zilizotolewa na Mungu:
1. Kupata upendo wote wa Mungu.
2. Kutenda kulingana na nia za Mungu katika mambo yote.
3. Kupata mwongozo wa Mungu, kuishi katika mwangaza wa Mungu, na kupata nuru ya Mungu.
4. Kuishi kwa kudhihirisha duniani mfano ambao Mungu anaupenda; kuwa kama Petro, aliyempenda Mungu kwa kweli, aliyesulubiwa kwa ajili ya Mungu na aliyestahili kufa kwa ajili ya Mungu; kuwa na utukufu sawa na wa Petro.
5. Kupendwa, kuheshimiwa, na kustahiwa na kila mtu duniani.
6. Kushinda kila kipengele cha vifungo vya kifo na Kuzimu, kutompa Shetani fursa ya kufanya kazi yake, kumilikiwa na Mungu, kuishi ndani ya roho mpya na changamfu, na kutohisi kuchoshwa.
7. Kuwa na hisia isiyoelezeka ya furaha na msisimko nyakati zote katika maisha yote, kana kwamba mtu ameshuhudia kuwasili kwa siku ya utukufu wa Mungu.
8. Kupata utukufu pamoja na Mungu na kuwa na sura inayofanana na watakatifu wapendwa wa Mungu.
9. Kuwa yule ambaye Mungu anampenda duniani, yaani, mwana mpendwa wa Mungu.
10. Kubadilisha umbo na kupaa pamoja na Mungu hadi mbingu ya tatu na kuvuka mipaka ya mwili.
Ni watu wanaoweza kurithi baraka za Mungu tu ndio wanaofanywa kuwa watimilifu na kupatwa na Mungu. Je, umepata chochote kwa sasa? Mungu amekufanya kuwa mtimilifu kwa kiwango gani? Mungu hamfanyi mwanadamu kuwa mtimilifu bila utaratibu; kumfanya Kwake mwanadamu kuwa mtimilifu kuna masharti, na kuna matokeo wazi, yanayoonekana. Si kama mwanadamu anavyowaza, kwamba maadamu ana imani katika Mungu, anaweza kufanywa kuwa mtimilifu na kupatwa na Mungu, na anaweza kupokea duniani baraka na urithi wa Mungu. Mambo kama hayo ni magumu mno—sembuse kubadilika kwa umbo la watu. Katika wakati wa sasa, kile mnachopaswa kufuatilia hasa ni kufanywa kuwa watimilifu na Mungu katika mambo yote, kufanywa kuwa watimilifu na Mungu kupitia watu, matukio, na vitu vyote mnavyokumbana navyo, na kuwa na mengi zaidi ya kile Mungu alicho kikifinyangwa ndani yenu na Yeye. Ni lazima kwanza mpokee urithi wa Mungu duniani; ndipo tu mtakapostahili kurithi baraka nyingi zaidi, na kubwa zaidi, kutoka kwa Mungu. Haya yote ni mambo ambayo mnapaswa kuyafuatilia, na ambayo mnapaswa kuyaelewa kabla ya mambo mengine yote. Kadiri mnavyofuatilia kufanywa kuwa watimilifu na Mungu katika mambo yote, ndivyo mtakavyoweza kuona mkono wa Mungu katika mambo yote, na matokeo yake, kupitia mitazamo tofauti na katika mambo tofauti, mtafuatilia kwa bidii kuingia katika kile neno la Mungu lilicho na kuingia katika uhalisi wa neno Lake. Hamwezi kutosheka na hali hasi kama vile kutotenda dhambi tu, au kutokuwa na dhana, kutokuwa na falsafa za shughuli za kidunia, na kutokuwa na mapenzi ya mwanadamu. Mungu humfanya mwanadamu kuwa mtimilifu kwa njia nyingi; kuna uwezekano wa wewe kufanywa kuwa mtimilifu katika mambo yote, na Anaweza kukufanya kuwa mtimilifu si tu kwa njia chanya bali pia kwa njia hasi, ili kufanya kile unachopata kiwe kingi zaidi. Kila siku kuna fursa za kufanywa kuwa mtimilifu na nyakati za kupatwa na Mungu. Baada ya kupitia mambo kwa njia hii kwa muda, utabadilishwa kwa kiasi kikubwa, na kiasili utakuja kuona wazi mambo mengi ambayo hapo awali hukuelewa. Hakutakuwa na haja ya maelekezo kutoka kwa wengine; bila wewe kujua, Mungu atakutia nuru, ili upokee nuru katika mambo yote na kuingia katika vipengele vyote vya upitiaji wako. Hakika Mungu atakuongoza ili usikengeuke kwenda kushoto au kulia, na hivyo utaanza kuitembea njia ya kufanywa kuwa mtimilifu na Yeye.
Kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu hakuwezi kuwekewa mipaka kwa kufanywa kuwa mtimilifu kwa kula na kunywa neno la Mungu. Kupitia mambo kwa njia hii kungekuwa kuegemea upande mmoja mno, kungejumuisha machache mno, na kungeweza tu kuwazuia watu katika upeo mdogo sana. Hili likiwa hivi, watu wangekosa lishe nyingi ya kiroho wanayohitaji. Mkitaka kufanywa kuwa watimilifu na Mungu, lazima mjifunze jinsi ya kupitia katika mambo yote, na kuweza kupata nuru katika kila kitu kinachowafanyikia. Kiwe kizuri au kibaya, kinapaswa kukuletea faida, na hakipaswi kukufanya uwe hasi. Hata iweje, unapaswa kuweza kutazama mambo ukiwa umesimama upande wa Mungu, na si kuyachanganua au kuyachunguza kutoka katika mtazamo wa mwanadamu (huu utakuwa mkengeuko katika upitiaji wako). Ukipitia mambo kwa njia hii, basi moyo wako utajazwa na mizigo ya uzima wako; utaishi daima katika mwanga wa uso wa Mungu, na itakuwa vigumu kuwa na mikengeuko katika utendaji wako. Watu kama hao wana mustakabali mzuri mbele yao. Kuna fursa nyingi sana za kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu. Yote yanategemea iwapo ninyi ni watu wanaompenda Mungu kwa kweli na iwapo mna azimio la kufanywa kuwa watimilifu na Mungu, kupatwa na Mungu, na kupokea baraka na urithi Wake. Azimio pekee halitoshi; lazima muwe na maarifa mengi, la sivyo daima mtakuwa na mikengeuko katika utendaji wenu. Mungu yuko tayari kumfanya kuwa mtimilifu kila mmoja wenu. Jinsi ilivyo sasa, ingawa watu wengi tayari wamekubali kazi ya Mungu kwa muda mrefu sana, wamejiwekea mipaka kwa kufurahia tu neema ya Mungu, na wako tayari tu kumruhusu Mungu awape faraja kidogo ya mwili, lakini hawako tayari kupokea ufunuo mwingi, na wa juu zaidi. Hili linaonyesha kwamba moyo wa mwanadamu bado uko upande wa nje daima. Hata ingawa kazi ya mwanadamu, huduma yake, na moyo wake umpendao Mungu vina kiasi kidogo zaidi cha uchafu, kadiri kiini chake cha ndani na fikira zake zilizopitwa na wakati zilivyo, mwanadamu bado anatafuta daima amani na starehe ya mwili, na hajali chochote kuhusu masharti na makusudi ya kumfanya Kwake mwanadamu kuwa mtimilifu yanaweza kuwa yapi. Na hivyo, maisha ya watu wengi kabisa bado ni duni na yaliyopotoka. Maisha yao hayajabadilika hata kidogo; hawachukulii imani katika Mungu kama jambo la maana, ni kana kwamba wana imani kwa ajili ya wengine tu, wakifanya mambo kwa namna isiyo ya dhati, na kuishi kiholela na kuendeleza maisha yasiyo ya kuheshimika. Ni wachache wale wanaoweza kutafuta kuingia katika neno la Mungu katika mambo yote, wakipata mambo mengi zaidi na yenye utele zaidi, wakiwa watu wenye utajiri mkubwa zaidi katika nyumba ya Mungu leo, na wakipokea baraka nyingi zaidi za Mungu. Ikiwa unatafuta kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu katika mambo yote, na unaweza kupokea kile ambacho Mungu ameahidi duniani, ikiwa unatafuta kutiwa nuru na Mungu katika mambo yote na usiporuhusu miaka ipite bure, hii ndiyo njia bora zaidi ya kuingia kwa bidii. Ni hivyo tu ndivyo utakavyokuwa umefuzu na kustahili kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu. Je, wewe kweli ni mtu anayetafuta kufanywa kuwa mtimilifu na Mungu? Je, wewe kweli ni mtu aliye makini katika mambo yote? Je, una roho sawa ya upendo kwa Mungu kama aliyokuwa nayo Petro? Je, una azimio la kumpenda Mungu kama alivyofanya Yesu? Umekuwa na imani katika Yesu kwa miaka mingi; je, umeona jinsi Yesu alivyompenda Mungu? Je, ni Yesu kweli unayemwamini? Unamwamini Mungu wa vitendo wa leo; je, umeona jinsi Mungu wa vitendo katika mwili anavyompenda Mungu wa mbinguni? Una imani katika Bwana Yesu Kristo; hiyo ni kwa sababu kusulubiwa kwa Yesu kwa ajili ya kuwakomboa binadamu na miujiza Aliyofanya ni ukweli unaokubalika kwa ujumla. Hata hivyo imani ya mwanadamu haitokani na maarifa na ufahamu wa kweli wa Yesu Kristo. Unaamini tu katika jina la Yesu, lakini huamini katika Roho Wake, kwa sababu hutilii maanani hata kidogo jinsi Yesu alivyompenda Mungu. Imani yako katika Mungu ni ya kitoto mno. Licha ya kumwamini Yesu kwa miaka mingi, hujui jinsi ya kumpenda Mungu. Je, hili halikufanyi kuwa mpumbavu mkubwa kabisa duniani? Hili ni thibitisho kwamba kwa miaka mingi, umekuwa ukila “chakula cha Bwana Yesu Kristo” bure. Sio tu kwamba Siwapendi watu kama hao, Ninaamini kwamba Bwana Yesu Kristo—unayemwabudu—pia asingewapenda. Watu kama hao wanawezaje kufanywa kuwa watimilifu? Je, hujawa mwekundu kwa ajili ya aibu? Je, huhisi aibu? Je, bado una ujasiri wa kumkabili Bwana wako Yesu Kristo? Je, ninyi nyote mnaelewa maana ya kile Nilichosema?