4. Adabu Takatifu Ambayo Waumini wa Mungu Wanapasa Kuwa Nayo

Maneno Husika ya Mungu:

Ni nini kinashirikishwa ndani ya ubinadamu wa kawaida? Utambuzi, hisia, dhamiri na tabia. Iwapo unaweza kufanikisha ukawaida katika kila mojawapo ya vipengele hivi, ubinadamu wako uko katika kiwango kinachostahili. Unapaswa kuwa na mfanano wa binadamu wa kawaida na utende kama anayemwamini Mungu. Sio lazima ufikie viwango vya juu zaidi au kujishughulisha na diplomasia. Unapaswa tu kuwa mwanadamu wa kawaida, na hisia za kawaida za mtu, uweze kung’amua vitu, na kwa kiwango cha chini uonekane kama mwanadamu wa kawaida. Hiyo itakuwa imetosha. Kila kitu kinachohitajika kwako leo kiko katika uwezo wako, na huku si kukulazimisha ufanye kadri ya uwezo wako hata kidogo. Hakuna maneno yasiyo na maana au kazi isiyofaa yatakayotekelezwa kwako. Uovu wote ulioonyeshwa au kufichuliwa katika maisha yako lazima uondolewe. Ninyi mmepotoshwa na Shetani na mna sumu nyingi sana za Shetani. Yote ambayo yanahitajika kwako ni kuiepuka tabia hii potovu ya kishetani, si wewe kuwa mtu mwenye cheo cha juu, au mtu maarufu au mkuu. Hii haina maana. Kazi ambayo imefanyika kwenu inaafikiana na kile ambacho ni cha asili kwenu. Kuna mipaka ya kile Ninachohitaji kutoka kwa watu. Ikiwa watu wa leo wote wangeombwa kutenda kama maafisa wa serikali, na kujizoeza toni ya sauti ya maafisa wa serikali, kujifunza katika namna ya kuzungumza ya viongozi wa serikali wenye cheo cha juu, au kujifunza kwa namna na sauti ya kuzungumza ya waandishi wa insha na waandishi wa riwaya, basi hili halingekubalika pia. Halingeweza kufikiwa. Kwa mujibu wa ubora wa tabia zenu, mnapaswa angalau kuweza kuzungumza kwa hekima na busara na kuelezea mambo wazi. Ni wakati huo ndipo mtakapoyatosheleza mahitaji. Kwa kiwango kidogo sana, utambuzi na hisia vinapaswa kufikiwa. Kwa sasa jambo kuu ni kuitupilia mbali tabia potovu ya kishetani. Lazima uutupilie mbali uovu unaouonyesha. Ikiwa hujavitupilia mbali hivi, unawezaje kugusia hisia na utambuzi wenye mamlaka mkubwa kabisa? Watu wengi wanaona kwamba enzi imebadilika. Hivyo hawajizoezi unyenyekevu au uvumilivu wowote, na pengine pia hawana upendo wowote au mwenendo mwema wa kitakatifu pia. Watu hawa ni wajinga mno! Je, wana kiwango chochote cha ubinadamu wa kawaida? Je, wanao ushuhuda wowote wa kuzungumziwa? Hawana utambuzi na hisia zozote kamwe. Bila shaka, vipengele fulani vya utendaji wa watu vilivyopotoka na vyenye makosa vinapaswa kurekebishwa. Kama vile maisha ya watu ya kiroho yasiyopindika ya zamani au mwonekano wao wenye ganzi na upumbavu—vitu hivi vyote vinapaswa kubadilika. Mabadiliko hayamaanishi kukuruhusu uwe mpotovu au kujiingiza katika mwili, kusema chochote utakacho. Kuzungumza kiholela hakuwezi kukubalika. Kutenda kama mwanadamu wa kawaida ni kuzungumza kwa kueleweka. Ndiyo inamaanisha ndiyo, na la inamaanisha la. Kuwa mwenye ukweli kwa uhakika na uzungumze inavyofaa. Usilaghai, usidanganye. Inapaswa kujulikana ni mipaka gani mtu wa kawaida anaweza kufikia kuhusu mabadiliko ya tabia. Ikiwa hiyo haijulikani, hutaweza kuingia katika uhalisi.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kuboresha Ubora wa Tabia ni Kwa Ajili ya Kupokea Wokovu wa Mungu

Katika tabia za watu wa kawaida hakuna uhalifu au udanganyifu, watu wana uhusiano wa kawaida kati yao, hawafanyi mambo pekee yao, na maisha yao si duni wala ya kufifia. Kwa hiyo, vilevile, Mungu huinuliwa miongoni mwa wote, maneno Yake hupenya miongoni mwa wanadamu, watu huishi katika amani kati yao na chini ya utunzaji na ulinzi wa Mungu, dunia imejaa upatanifu, bila kuingilia kwa Shetani, na utukufu wa Mungu huwa na umuhimu mkuu sana miongoni mwa wanadamu. Watu kama hao ni kama malaika: watakatifu, wa kusisimua, wasiolalamika kamwe kuhusu Mungu, na hutoa juhudi zao zote kwa utukufu wa Mungu duniani pekee.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Ufafanuzi wa Mafumbo ya “Maneno ya Mungu kwa Ulimwengu Mzima”, Sura ya 16

Nina matamanio mengi. Natamani muweze kutenda kwa njia inayofaa na yenye mwenendo mzuri, muwe waaminifu kutimiza wajibu wenu, muwe na ukweli na ubinadamu, muwe watu ambao wanaweza kuacha vitu vyote na kuyatoa maisha yao kwa ajili ya Mungu, na mengineyo. Matumaini haya yote yanatokana na upungufu wenu na upotovu na kutotii kwenu.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Dhambi Zitamwelekeza Mwanadamu Jahanamu

Watu ambao Mungu huwatumia huonekana kwa nje kama watu wasio na akili na kama wasio na uhusiano wa kawaida na wengine, ingawa wao huzungumza na adabu, hawazungumzi kiholela, na wanaweza daima kuwa na moyo uliotulia mbele ya Mungu. Lakini ni mtu wa aina hiyo tu ndiye anatosha kutumiwa na Roho Mtakatifu. Mtu huyu asiye na akili anayezungumziwa na Mungu huonekana kama asiye na uhusiano wa kawaida na wengine, na hana upendo wa kuelekea nje au matendo ya juu juu, lakini anapokuwa akieleza mambo ya kiroho anaweza kufungua roho yake na kwa kujinyima awatolee wengine mwangaza na nuru ambayo amepata kutoka kwa uzoefu wake wa hakika mbele za Mungu. Hivi ndivyo anavyodhihirisha upendo wake kwa Mungu na kuridhisha mapenzi ya Mungu. Wengine wote wanapokuwa wanamkashifu na kumdhihaki, ana uwezo wa kutoelekezwa na watu wa nje, matukio, au vitu, na bado anaweza kutulia mbele za Mungu. Mtu wa aina hii inavyooneka yuko na utambuzi wake mwenyewe wa pekee. Bila kujali wengine, moyo wake kamwe haumwachi Mungu. Wengine wanapokuwa wakizungumza kwa furaha na kwa vichekesho, moyo wake bado unasalia mbele za Mungu, kutafakari neno la Mungu au kusali kwa kimya kwa Mungu aliye moyoni mwake, akitafuta makusudi ya Mungu. Kamwe hawatilii maanani udumishaji wa uhusiano wa kawaida na wengine. Mtu wa aina hii inavyoonekana hana falsafa ya maisha. Kwa nje, mtu huyu ni mchangamfu, anayependwa, asiye na hatia, lakini pia anamiliki hisia ya utulivu. Huu ni mfano wa mtu ambaye Mungu anamtumia. Mambo kama falsafa ya kuishi au “mantiki ya kawaida” hayawezi kufanya kazi kwa mtu wa aina hii; mtu wa aina hii ameutoa moyo wake wote kwa neno la Mungu, ambaye anaonekana kuwa na Mungu tu katika moyo wake. Hii ni aina ya mtu ambaye Mungu anamrejelea kama mtu “bila mantiki,” naye tu ni mtu ambaye anatumiwa na Mungu. Alama ya mtu ambaye anatumiwa na Mungu ni: Haijalishi ni lini au wapi, moyo wake daima uko mbele za Mungu, na haijalishi jinsi gani wengine ni wenye anasa, jinsi gani wanavyoshiriki katika tamaa, wanajiingiza katika anasa za kimwili—moyo wake kamwe haumwachi Mungu, naye hafuatani na umati. Aina hii ya mtu pekee ndiye anafaa kwa ajili ya matumizi ya Mungu, naye hasa ni yule ambaye amekamilika na Roho Mtakatifu. Ikiwa huwezi kufikia hatua hii, basi hustahili kupatwa na Mungu, ili kukamilishwa na Roho Mtakatifu.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Ni Muhimu Sana Kuanzisha Uhusiano wa Kawaida na Mungu

Watu ambao wana ukweli ni wale ambao, katika matukio wanayopitia ya kweli, wanaweza kusimama imara katika ushuhuda wao, kusimama imara katika nafasi zao, kusimama katika upande wa Mungu, bila kurudi nyuma, na ambao wanaweza kuwa na uhusiano wa kawaida na watu wanaompenda Mungu, wale ambao, mambo yakishawatokea, wanaweza kumtii Mungu kabisa, na wanaweza kumtii Mungu hadi kifo. Matendo na ufunuo wako katika maisha halisi ndio ushuhuda wa Mungu, ni kuishi kwa kudhihirisha maisha ya mwanadamu na ushuhuda wa Mungu, na huku ni kufurahia upendo wa Mungu; unapopitia hadi kiwango hiki, matukio unayopitia yatakuwa yamekuwa na athari. Watu ambao wameuona upendo wa Mungu kwa kweli ni wale ambao wanaishi kwa kudhihirisha kwa kweli, ambao kila matendo yao yanapongezwa na wengine. Mavazi na kuonekana kwenu kwa nje hakupendezi, lakini wanaoishi kwa kudhihirisha maisha ya utiifu wa hali ya juu, ambao wanawasiliana kwa karibu maneno ya Mungu na huelekezwa na Mungu, na kupata nuru kutoka kwa Mungu, ambao huweza kuongea mapenzi ya Mungu katika maneno yao, na wanawasiliana kwa karibu uhalisi, ambao huelewa zaidi kuhusu kuhudumu katika Roho, wanaongea kwa wazi, ambao ni wenye heshima na kuaminika, ambao hawakabiliki na wana tabia nzuri, ambao wanaweza kutii mipango ya Mungu na kusimama imara katika ushuhuda wakati mambo yanapowatokea, ambao wana utulivu bila kujali wanachokumbana nacho. Watu wengine wangali wachanga, lakini wanatenda kama mtu mzima; wamekomaa, wana ukweli, wanapendwa na wengine—na hawa ndio watu ambao wana ushuhuda, na ndio udhihirisho wa Mungu.

Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Wanaompenda Mungu Wataishi Milele Katika Mwangaza Wake

Madondoo ya Mahubiri na Ushirika kwa ajili ya Marejeo:

Mtu anayemwamini Mungu kwa hakika atatekeleza angalau vipengele hivi vitano vya maisha ya kiroho kila siku: kusoma neno la Mungu, kumwomba Mungu, kuwa na ushirika kuhusu ukweli, kuimba nyimbo na sifa, na kutafuta ukweli katika kila kitu. Ikiwa pia una maisha ya mikutano, utakuwa na furaha kuu zaidi. Mtu akiwa na uwezo wa jumla wa kupokea, kumaanisha anaweza kuelewa dhamira za Mungu baada ya kusoma maneno ya Mungu yeye mwenyewe, ataweza kuelewa ukweli, na kujua jinsi ya kutenda kulingana na ukweli, basi inaweza kusemwa kwamba mtu wa aina hii atafaulu katika imani yake. Iwapo mtu hana maisha ya kiroho ya aina hii, au iwapo maisha yake ya kiroho ni yasiyofaa kupindukia na yanaonekana tu mara chache sana, basi mtu huyo ni muumini aliyechanganyikiwa. Waumini waliochanganyikiwa hawawezi kupata matokeo mazuri kutoka kutimiza jukumu lao. Kuamini katika Mungu bila kuishi maisha ya kiroho ni kuwa na imani kwa maneno pekee; kwa watu kama hao, hakuna Mungu mioyoni mwao, sembuse uchaji wowote wa Mungu. Wanawezaje kuwa na mfano wa binadamu wa kufaa?

…………

Kuna vitu 10 vya kuzingatiwa na kuingiwa inapofikia kwa jinsi mtu wa kufaa anastahili kuwa:

1. Fuata adabu, jua masharti, na uwaheshimu wazee na kuwajali wadogo.

2. Kuwa na hali ya maisha inayofaa; iliyo na manufaa kwako mwenyewe na kwa wengine.

3. Valia kwa namna ya heshima na nyoofu; mavazi ya ajabu au ya urembo yamepigwa marufuku.

4. Usiwahi, kwa sababu yoyote ile, kuomba pesa kutoka kwa ndugu, na usitumie vitu vya watu wengine kama ni jambo la kawaida tu.

5. Kukutana na watu wa jinsia tofauti lazima kuwe na mipaka; vitendo vinahitajika kuwa vya heshima na vinyoofu.

6. Usibishane na watu; jifunze kuwasikiliza wengine kwa uvumilivu.

7. Dumisha usafi mzuri, lakini kwa kuzingatia hali halisi.

8. Jihusishe katika ushirika na uhusiano wa kufaa na wengine, jifunze kuwaheshimu na kuwa mwenye kuwajali watu, na pendaneni.

9. Fanya kila uwezalo kuwasaidia wale walio na mahitaji; usiitishe au kukubali vitu kutoka kwa watu wengine.

10. Usiwaruhusu wengine wakuhudumie; usiwaruhusu wengine wafanye kazi unayofaa kuwa ukifanya mwenyewe.

Masharti kumi ya hapo juu yanafaa kuwa ya msingi yanayofuatwa na waumini wote katika maisha yao, yeyote anayevunja masharti haya ni wa tabia duni. Unaweza kusema kuwa haya ni masharti ya nyumba ya Mungu na wale wanaoyaasi mara kwa mara bila shaka watatupwa kando.

Wale wote wanaoutafuta ukweli pia wanahitaji kufuata mienendo kumi mizuri ya watakatifu wa kale. Watu wanaoweka katika vitendo mara kwa mara na kudumisha haya bila shaka watapata thawabu kubwa za binafsi. Ni yenye manufaa makubwa mno kwa wanadamu.

Kanuni kumi za kuambatana na adabu takatifu:

1. Fanya ibada za kiroho kila asubuhi kwa kusali na kusoma neno la Mungu kwa takriban nusu saa.

2. Tafuta madhumuni ya Mungu katika kila kitu kila siku ili uweze kuuweka ukweli katika matendo kwa usahihi zaidi.

3. Kuwa na ushirika na kila unayekutana naye, mkifunzana kutoka kwa uwezo wa kila mmoja ili nyote muweze kuendelea.

4. Kuwa na mtazamo wa matumaini kuhusu maisha, huku mara nyingi ikiimba nyimbo na sifa na utoe shukrani kwa ajili ya neema ya Mungu.

5. Usitegwe na dunia ya kilimwengu; jongea karibu na Mungu moyoni mwako kwa kawaida na usiingilie mambo ya wengine.

6. Weka hekima moyoni mwako na ukae mbali na uovu na sehemu zenye hatari.

7. Usibishane na watu, kuwa na ushirika kuhusu ukweli, na uelewane na wengine.

8. Kuwa radhi kufanya kila uwezalo kuwasaidia wengine, watulizie mashaka yao, na uwasaidie kutatua ugumu wao katika kuingia katika kumwamini Mungu.

9. Jifunze jinsi ya kutii wengine, usiwatawale watu na kuwalazimisha; waruhusu watu wapate faida kiasi katika kila kitu.

10. Mara nyingi mwabudu Mungu moyoni mwako, ukimwacha Awe na ukuu katika kila kitu na kumridhisha Yeye katika kila kitu.

Kanuni kumi za hapa juu za maisha na namna kumi za kuambatana na adabu takatifu yote ni vitu ambavyo watu wana uwezo wa kuvifanya. Watu wanaweza kuweka vitu hivi katika vitendo alimradi vinaeleweka na makosa ya mara kwa mara si magumu kusuluhisha. Bila shaka, watu fulani ambao ubinadamu wao ni mbaya zaidi wameondolewa katika hili.

Kimetoholewa kutoka katika Ushirika kutoka kwa Aliye Juu

Ubinadamu wa kufaa huashiria hasa kuwa na dhamiri, mantiki, unyoofu na heshima. Dhamiri na mantiki zinajumuisha kuonyesha ustahimilivu, kuwa na uvumilivu kwa wengine, kuwa mwaminifu, kutendea watu kwa hekima, na kuwa na upendo wa kweli kwa ndugu. Hizi ndizo sifa tano ambazo binadamu wa kufaa lazima wawe nazo.

Sifa ya kwanza ni kuwa na moyo wa ustahimilivu. Unamaanisha haijalishi dosari tunazoona ndani ya ndugu zetu, tunafaa kuwatendea vema, tukionyesha uvumilivu na uelewa. Hatupaswi kuwatenga au kuwashambulia kwa maneno. Tunapoona dosari au upotovu ukijifichua ndani ya watu wengine, tunafaa kukumbuka kuwa huu ni wakati wa kazi ya Mungu ya wokovu, kwa hivyo ni jambo la kawaida kwa wateule wa Mungu kufichua upotovu, na tunapaswa kuelewa. Mbali na hayo, tunahitaji kuangalia upotovu wetu sisi wenyewe, si lazima kuwa tunafichua upotovu wa kiwango cha chini kuliko wa watu wengine. Tunapaswa kuchukulia jinsi wengine wanavyofichua upotovu jinsi tunavyochukulia wetu kabisa. Kwa njia hiyo, tunaweza kuwastahimili wengine. Iwapo huwezi kustahimili watu wengine inamaanisha kuna shida na mantiki yako; inathibitisha kwamba huelewi ukweli na hujui kazi ya Mungu. Kutojua kazi ya Mungu kunamaanisha nini? Ni kutojua kwamba kazi ya Mungu bado haijakamilika na kwamba binadamu bado anaishi katika wakati wa kazi ya Mungu ya wokovu—bado hatujafanywa kuwa kamili. Kwa hivyo, kila mtu bila kuzuilika atafichua upotovu. Sasa kila mtu anaufuatilia ukweli kwa njia inayofaa, akipata kuelewa upotovu wake mwenyewe, na kupitia neno la Mungu. Kila mtu yuko kwenye kipindi cha kuingia katika ukweli na bado hajapata ukweli kikamilifu. Ni wakati tu watu wanapopata ukweli ndio tabia ya maisha yao itaanza kubadilika. Watu wanapoelewa jambo hili watakuwa na busara ya mtu wa kawaida, na basi watawatendea wengine na busara pia. Ikiwa watu hawana busara hawatawatendea wengine kwa busara.

Sifa ya pili ni kuonyesha uvumilivu kwa wengine. Kuwa mstahimilivu tu hakutoshi; lazima pia uwe mvumilivu. Wakati mwingine unaweza kuwa mstahimilivu na mwenye kuelewa tu, lakini haiwezekani kuepuka ndugu fulani kufanya jambo linaloweza kukusononesha au kukukosea. Katika hali kama hizo ni rahisi kwa tabia potovu ya binadamu kulipuka, kwa sababu sote tunapenda kupigana na kulinda fahari yetu, na sisi sote ni wenye ubinafsi na bure. Hivyo mtu akisema kitu kinachokusononesha au kufanya kitu kinachokukosea, unafaa kuwa mvumilivu. Uvumilivu pia unajumuishwa katika mawanda ya busara. Watu watakuza uvumilivu tu ikiwa wana busara. Lakini tunawezaje kuwa wavumilivu? Ukitaka kuwa mvumilivu kwa wengine, unahitaji kwanza kuwaelewa, “kumaanisha bila kujali anayesema kitu kinachokusononesha, unafaa kutambua hili: Maneno yake yamenisononesha. Alichosema kilionekana kufunua udhaifu wangu na kilionekana kunilenga mimi. Ikiwa maneno yake yananilenga mimi, anamaanisha nini anapoyasema? Je, anajaribu kunidhuru? Je, ananiona mimi kama adui yake? Je, ananichukia? Je, analipiza kisasi dhidi yangu? Mimi sijamkosea, kwa hivyo majibu ya maswali haya hayawezi kuwa ndiyo.” Kwa kuwa hiyo ndiyo hali, basi haijalishi kile alichosema ndugu huyu, yeye hakuwa na madhumuni ya kukusononesha au kukutendea kama adui yake. Hilo ni bila shaka. Aliposema maneno haya alikuwa anadhihirisha tu yale ambayo binadamu wa kawaida hufikiri, alikuwa anashiriki juu ya ukweli, kujadili maarifa, kufichua upotovu wa watu, au kukubali hali yake mwenyewe ya upotovu; bila shaka hakuwa anamlenga mtu yeyote yule kwa kujua. Kwanza unamwelewa, kisha hasira yako inaweza kutoweka, halafu unaweza kupata uvumilivu. Wengine watauliza: “Mtu akinishambulia kwa kujua na anilenge, na aseme mambo haya kwa makusudi ya kufanikisha kusudi fulani, basi nitawezaje kuwa mvumilivu?” Unapaswa kuwa mvumilivu jinsi hii: “Hata mtu akinishambulia kwa makusudi, bado nafaa kuwa mvumilivu. Hii ni kwa sababu yeye ni ndugu yangu na sio adui yangu, na bila shaka sio ibilisi, Shetani. Haiwezi kuepukika kwamba ndugu watafichua upotovu kiasi na kuwa na makusudi fulani katika mioyo yao. Hii ni kawaida. Napaswa kuelewa, na ninafaa kuhisi maono yake na kuwa mvumilivu.” Unapaswa kuwaza kwa njia hii, kisha usali kwa Mungu na kusema: “Mungu, mtu fulani ametoka kuumiza fahari yangu. Siwezi kukubali aibu hii; kila mara nataka kuwa mwenye hasira na kumshambulia. Huu kwa hakika ni ufichuzi wa upotovu. Nilikuwa nikidhani kuwa nilikuwa na upendo kwa wengine, lakini sasa kwa kuwa maneno ya mtu fulani yamenichoma moyoni siwezi kuvumilia. Nataka kumrudishia pia. Nataka kulipiza kisasi. Uko wapi upendo wangu? Je, hii yote si ni chuki tu? Bado niko na chuki moyoni mwangu! Mungu, jinsi Ulivyo na huruma kwetu na kutusamehe sisi dhambi zetu ndio jinsi tunavyofaa kuwa na huruma kwa wengine. Hatufai kuwa na kisasi dhidi ya wengine. Mungu, tafadhali nikinge, Usiache asili yangu ilipuke. Natamani kukutii Wewe na niishi kwenye upendo Wako. Tunampinga na kumkataa Kristo na Mungu sana katika kila kitu tukifanyacho, lakini Kristo bado Anakuwa mvumilivu nasi. Mungu anafanya hatua hii ya kazi Yake kwa uvumilivu mkubwa na upendo. Je, Kristo Alilazimika kuvumilia mateso, fedheha na kashfa kiasi gani? Ikiwa Kristo Alivumilia hayo, basi kiasi kidogo cha uvumilivu tunaofaa kuwa nao si kitu! Uvumilivu wetu umepungukiwa sana ukilinganishwa na ule wa Kristo....” Mara unapoomba kwa njia hii utajisikia ni kama wewe ni mpotovu mno, asiye wa maana kabisa, aliyepungukiwa katika kimo kabisa, na huo ndio wakati ambapo hasira yako itazimwa. Hivyo ndivyo unavyoweza kufikia uvumilivu.

Sifa ya tatu ni kuwatendea watu kwa uaminifu. Kuwa waaminifu kwa watu kuna maana kwamba bila kujali tunachofanya, iwe ni kuwasaidia wengine au kutoa huduma kwa ndugu zetu au kushiriki kuhusu ukweli, lazima tuzungumze kutoka moyoni. Zaidi ya hayo, usihubiri kile ambacho hujafanya. Wakati wowote ndugu wanahitaji msaada wetu tunapaswa kuwasaidia. Tunapaswa kutimiza wajibu wowote tunaohitaji kuutimiza. Kuwa mwaminifu, wala si muongo au wa kujidai. ... Bila shaka, kuwa mtu mwaminifu kunahitaji hekima kiasi wakati unaposhughulika na watu fulani. Ukiona kwamba mtu fulani si wa kutegemewa kwa sababu upotovu wake ni wa kina kabisa, kama huwezi kumbaini na hujui anachoweza kufanya, basi unahitaji kuwa mwenye hekima na uepuke kumweleza kila kitu. Kuwa mtu mwaminifu kunahitaji maadili. Usizungumze kwa upofu kuhusu mambo usiyofaa kuwa ukizungumzia. Zaidi ya hayo, kuwa mtu mwaminifu kunahitaji kuongea na mantiki na usahihi. Watu wengine wanasisitiza kutenda uaminifu na kumfungulia mtu moyo licha ya shughuli nyingi alizo nazo. Huko ni kuwa mtu mwaminifu vipi? Je, huu sio upumbavu? Kuwa mtu wa kweli ni kutokuwa mjinga. Kunahusu kuwa mwerevu, wa kawaida na wazi, na usiyedanganya. Lazima uwe wa heshima na mwenye busara. Uaminifu hujengwa juu ya msingi wa busara. Hii ndiyo maana ya kuwa mwaminifu wakati unaposhughulika na watu, na kuwa mtu mwaminifu. Bila shaka, jambo muhimu sana kuhusu kuwa mtu mwaminifu ni kuwa mwaminifu kwa Mungu. Je, si lingekuwa tatizo kubwa kama wewe ni mtu mwaminifu mbele ya watu wengine tu, lakini wewe si mwaminifu mbele ya Mungu na umdanganye Yeye? Mkitafuta kuwa watu waaminifu mbele ya Mungu, basi kwa kawaida mtakuwa waaminifu mbele ya wengine. Iwapo huwezi kufanya hivyo mbele ya Mungu, basi kwa kweli huwezi kufanya hivyo mbele ya watu wengine. Haijalishi ni kipengele kipi cha ukweli au ni kitu kipi chema ambacho unaingia, lazima kwanza ukifanye mbele ya Mungu. Punde ambapo umepata matokeo mbele ya Mungu, kwa kiasili utaweza kuishi kwa kukidhihirisha mbele ya watu wengine. Usijichoshe kufanya hiki au kile mbele ya wengine, lakini kisha bila kujali ufanye chochote unachotaka mbele ya Mungu. Hili halitakuwa sawa. Jambo muhimu zaidi ni kulifanya mbele ya Mungu, ambaye huwajaribu binadamu na kuchunguza mioyo yao. Una uhalisi kwa hakika ikiwa unaweza kupita jaribio hili mbele ya Mungu. Huna uhalisi ikiwa huwezi kupita jaribio hili mbele ya Mungu—hii ndiyo kanuni ya kutenda ukweli.

Sifa ya nne ni kutendea watu kwa hekima. Baadhi ya watu husema: “Je, kuelewana na ndugu kunahitaji hekima?” Ndiyo, kunahitaji, kwa sababu kutumia hekima hutoa hata manufaa makubwa zaidi kwa ndugu zako. Baadhi watauliza: “Je, si kutumia hekima kwa ndugu ni kuwa mwenye hila?” Hekima si hila. Badala yake, ni kinyume kabisa na hila. Kutumia hekima kuna maana ya kuwa makini kwa jinsi unavyozungumza na ndugu wakati kimo chao ni kidogo, ikija kuwa wao wasiweze kukubali kile unachosema. Pia, kwa watu wenye kimo kidogo, hasa wale ambao hawana ukweli, wanaofichua upotovu fulani na kuwa na tabia fulani za upotovu, kama wewe ni wa kawaida na wazi sana na uwaambie kila kitu, inaweza kuwa rahisi kwao kuwa na kitu dhidi yako au kukutumia vibaya. Hivyo, ni lazima kwa kadiri uchukue tahadhari kiasi na uwe na mbinu fulani unapozungumza. Hata hivyo, kuwa na tahadhari dhidi ya watu hakumaanishi kutowasaidia au kutokuwa na upendo kwao—kunamaanisha tu kutowaambia mara moja baadhi ya mambo muhimu kuhusu nyumba ya Mungu, na kushiriki tu ukweli kwao. Kama wanahitaji msaada wa kiroho katika maisha, kama wanahitaji ruzuku ya na ukweli, lazima tufanye kila kitu tuwezalo ili kuwakidhi katika suala hili. Lakini iwapo wanauliza kuhusu hili na lile kuhusu nyumba ya Mungu, au hili na lile kuhusu viongozi na wafanyakazi wake, basi hakuna haja ya kuwaambia. Ukiwaambia, kuna uwezekano watafichua habari hii na hii itaathiri kazi ya nyumba ya Mungu. Kwa maneno mengine, ikiwa ni kitu ambacho hawafai kujua au kitu ambacho hawana haja ya kujua, basi usiwaruhusu kujua kukihusu. Kama ni kitu ambacho wanapaswa kujua, basi fanya kila uwezalo kuwafanya wajue kukihusu, kwa uthabiti na bila shaka. Kwa hivyo ni mambo yapi wanayopaswa kujua? Ufuatiliaji wa ukweli ndio watu wanapaswa kujua: Ni ukweli upi wanaopaswa kuwa nao, ni vipengele vipi vya ukweli wanafaa kuelewa, ni majukumu yapi wanapaswa kutimiza, ni majukumu yapi yanawafaa wao kutimiza, ni jinsi gani wanafaa kutimiza majukumu hayo, jinsi ya kuishi kwa kudhihirisha ubinadamu wa kawaida, jinsi ya kuishi maisha ya kanisa—haya yote ni mambo ambayo watu wanapaswa kujua. Kwa upande mwingine, masharti na kanuni za nyumba ya Mungu, kazi ya kanisa na hali za ndugu zako haviwezi kuwekwa wazi kwa kawaida kwa watu wa nje wala wasioamini katika familia yako. Hii ni kanuni ambayo ni lazima ifuatwe tunapotumia hekima. Kwa mfano, hupaswi kamwe kuzungumza kuhusu majina ya viongozi wako au wanapoishi. Ukizungumza kuhusu mambo haya, huwezi kujua wakati habari hii inaweza kufikia masikio ya watu wa nje, na mambo yanaweza kuwa ya taabu sana kama yatapishwa kwa baadhi ya wapelelezi wabaya au maajenti wa siri. Hili linahitaji hekima, na hii ndiyo maana nasema kuwa na hekima ni muhimu. Zaidi ya hayo, unapokuwa wa kawaida na wazi, kuna mambo fulani ya binafsi ambayo huwezi tu kumwambia mtu yeyote. Unafaa kupima kimo cha ndugu zako ili uone kama, baada ya kuwaeleza, wanaweza kuwa waovu na wafanye utani kuhusu kile unachosema, wakikusababishia matatizo baada ya hayo mambo kusambazwa, na hili likaharibu heshima yako. Hii ndiyo maana kuwa wa kawaida na wazi pia kunahitaji hekima. Hicho ndicho kiwango cha nne ambacho binadamu sawa lazima wamiliki—kutendea watu kwa hekima.

Sifa ya tano ni kuwa na upendo wa kweli kwa ndugu ambao hakika wanaamini katika Mungu. Hii inahusisha utunzaji kiasi, msaada halisi, na roho ya huduma. Tunapaswa hasa kuwa na ushirika zaidi na hao ndugu wanaofuatilia ukweli, na kuwapa ruzuku zaidi. Haijalishi kama wao ni waumini wapya au wamekuwa waumini kwa miaka kadhaa. Kuna kanuni moja hasa ya maisha ya kanisa: Watunze hasa wale ambao wanafuatilia ukweli. Shiriki na wao zaidi, wape ruzuku zaidi, na uwanyunyizie zaidi ili waweze kusaidiwa kuinuka haraka iwezekanavyo, kuwasaidia wakue katika maisha yao haraka wawezavyo. Kwa wale ambao hawafuatilii ukweli, kama itakuwa wazi kuwa hawaupendi ukweli baada ya kipindi cha unyunyizaji, basi hakuna haja ya kuweka juhudi kubwa kwao. Si lazima kwa sababu tayari umeshafanya kila kitu kiwezekanacho kwa mwanadamu. Inatosha kuwa umetimiza wajibu wako. ... Unahitaji kuona ni nani unapaswa kulenga kazi yako kwake. Je, Mungu atawakamilisha wale wasiofuatilia ukweli? Kama Roho Mtakatifu hatafanya hivyo, basi kwa nini watu waendelee kufanya hilo kwa upofu? Huelewi kazi ya Roho Mtakatifu ilhali daima umejiamini sana—je, huo si upumbavu na ujinga wa binadamu? Hivyo, toa usaidizi zaidi kwa ndugu ambao kwa kweli wanaufuatilia ukweli, kwa sababu wao ni vyombo vya wokovu wa Mungu na wateule Wake walioamuliwa kabla. Tukishiriki kuhusu ukweli mara nyingi na watu hawa kwa moyo mmoja na mawazo na kusaidiana na kupeana ruzuku, mwishowe sisi wote tutapata wokovu. Wewe unayasaliti mapenzi ya Mungu usipojiunga na watu hawa. ... Wale walio ndani ya kanisa walio na ubinadamu unaofaa wanapaswa kujiweka miongoni mwa wale ambao wanafuatilia ukweli, waingiliane kwa amani na watu hawa, na kwa njia ya ufuatiliaji wa ukweli hatua kwa hatua kujitumia kwa ajili ya Mungu kwa moyo na mawazo sawa. Kwa njia hiyo, wale wanaofuatilia ukweli wataokolewa na wewe pia utaokolewa, kwa sababu Roho Mtakatifu anafanya kazi kati ya wale wanaofuatilia ukweli. ...

Ushirika ambao tumetoka kuwa nao ni juu ya vipengele vitano ambavyo binadamu wa kawaida lazima wamiliki. Kama una sifa hizi zote tano, utaweza kuingiliana kwa amani na ndugu zako, utapata nafasi yako katika kanisa, na utatimiza wajibu wako kwa njia bora zaidi kadri ya uwezo wako.

Kimetoholewa kutoka katika Mahubiri na Ushirika Kuhusu Kuingia Katika Maisha

Iliyotangulia: 3. Katika Kumwamini Mungu, Unapaswa Kuweka Uhusiano wa Kawaida na Mungu

Inayofuata: 5. Imani Katika Mungu Haipasi Kuwa kwa ajili ya Kutafuta Amani na Baraka Pekee

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp