Amri za Enzi Mpya
Katika kupitia kazi ya Mungu, ni lazima msome maneno ya Mungu kwa uangalifu na mjizatiti na ukweli. Lakini kuhusu kile mnachotaka kufanya au jinsi mnavyotaka kukifanya, hakuna haja ya maombi yenu ya dhati au dua, na mambo haya hayana manufaa. Hata hivyo, matatizo yanayowakabili wakati wa sasa ni kwamba hamjui jinsi ya kupitia kazi ya Mungu, na kwamba kuna uhasi mwingi ndani yenu. Mnajua mafundisho mengi, lakini hamna uhalisi mwingi. Je, hii si dalili ya kupotoka? Kupotoka kwingi kunaonekana ndani yenu, kundi hili. Jinsi mambo yalivyo, hamjakuwa na ushahidi wa majaribu kama “watendaji huduma,” au wa majaribu mengine na usafishaji unaohusiana na maneno ya Mungu. Lazima mfuate mambo mengi mnayopaswa kutia katika vitendo. Hii ni kusema kwamba watu lazima wafuate wajibu mwingi wanaopaswa kutekeleza. Hili ndilo jambo ambalo watu wanapaswa kufuata, na hili ndilo lazima walitekeleze. Mwacheni Roho Mtakatifu afanye kile kinachopaswa kufanywa na Roho Mtakatifu; mwanadamu hawezi kushiriki katika hilo. Mwanadamu anapaswa kufuata kile kinachopaswa kufanywa na mwanadamu, ambacho hakina uhusiano na Roho Mtakatifu. Si chochote ila kile kinachopaswa kufanywa na mwanadamu, na kinapaswa kufuatwa kama amri, kama vile tu kufuata sheria katika Agano la Kale. Ingawa sasa si Enzi ya Sheria, bado kuna maneno mengi yanayopaswa kufuatwa ambayo ni ya aina moja na maneno yaliyonenwa katika Enzi ya Sheria. Maneno haya hayatekelezwi tu kwa kutegemea mguso wa Roho Mtakatifu, bali, ni mambo ambayo mwanadamu anapaswa kuyafuata. Kwa mfano:
Usihukumu kazi ya Mungu wa vitendo.
Usimpinge mtu anayeshuhudiwa na Mungu.
Mbele ya Mungu, dumisha nafasi yako na usiwe mpotovu.
Unapaswa kuwa wa wastani katika usemi, na maneno na matendo yako lazima yafuate mipango ya mtu anayeshuhudiwa na Mungu.
Unapaswa kuuhofu ushuhuda wa Mungu. Usipuuze kazi ya Mungu na maneno yanayotoka kinywani Mwake.
Usiige sauti na malengo ya maneno ya Mungu.
Kwa nje, usifanye chochote kinachompinga waziwazi mtu anayeshuhudiwa na Mungu.
Haya ndiyo kila mtu anapaswa kuyafuata. Katika kila enzi, Mungu hubainisha taratibu nyingi ambazo zinafanana na sheria na zinapaswa kufuatwa na mwanadamu. Kupitia hili, Yeye huzuia tabia ya mwanadamu na kugundua unyofu wake. Kumbuka maneno “Heshimu baba yako na mama yako” ya enzi ya Agano la Kale, kwa mfano. Maneno haya hayatumiki leo; wakati huo, yalizuia tu baadhi ya tabia za nje za mwanadamu, yalitumika kuonyesha unyofu wa imani ya mwanadamu kwa Mungu, na yalikuwa alama ya wale waliomwamini Mungu. Ingawa sasa ni Enzi ya Ufalme, bado kuna taratibu nyingi ambazo mwanadamu lazima azifuate. Sheria za zamani hazitumiki, na leo kuna matendo mengi zaidi yanayofaa kwa mwanadamu kutekeleza, na ambayo ni ya lazima. Hayahusishi kazi ya Roho Mtakatifu na lazima yafanywe na mwanadamu.
Katika Enzi ya Neema, desturi nyingi za Enzi ya Sheria zilitupiliwa mbali kwa sababu sheria hizi hazikuwa na ufanisi hasa kwa kazi ya wakati huo. Baada ya kutupiliwa mbali, desturi nyingi zilianzishwa ambazo zilifaa kwa enzi hiyo na ambazo zimekuwa taratibu nyingi za leo. Mungu wa leo alipokuja, taratibu hizi ziliachwa na haikuhitajika tena kwamba zifuatwe, na desturi nyingi zilianzishwa ambazo zinafaa kwa kazi ya leo. Leo, desturi hizi si taratibu, bali zinakusudiwa kufikia matokeo; zinafaa kwa leo—kesho, pengine zitakuwa taratibu. Kwa maneno machache, unapaswa kufuata kile kilicho na mafanikio kwa kazi ya leo. Usijali kuhusu kesho: Kile kinachofanywa leo ni kwa ajili ya leo. Pengine kesho itakapofika, kutakuwa na desturi bora zaidi ambazo utahitajika kutekeleza—lakini usijali kuhusu hilo. Badala yake, fuata kile kinachopaswa kufuatwa leo ili kuepuka kumpinga Mungu. Leo, hakuna kitu muhimu zaidi ambacho mwanadamu anapaswa kufuata kuliko yafuatayo:
Usijaribu kumrairai Mungu anayesimama mbele ya macho yako, au kumficha chochote.
Usitamke maneno machafu au maneno ya kiburi mbele ya Mungu aliye mbele yako.
Usimdanganye Mungu aliye mbele ya macho yako kwa maneno matamu na hotuba nzuri ili kupata imani Yake.
Usitende bila heshima kuu kwa Mungu. Tii yote yanayonenwa kutoka kinywani mwa Mungu, na usipinge, usikatae, au usibishane dhidi ya maneno Yake.
Usifasiri kiholela maneno yanayonenwa kutoka kinywani mwa Mungu. Unapaswa kuulinda ulimi wako ili uepuke usikusababishe kunaswa na njama za udanganyifu za watu waovu.
Unapaswa kulinda hatua zako ili kuepuka kuvuka mipaka uliyowekewa na Mungu, jambo ambalo litakusababisha usimame katika nafasi ya Mungu na uzungumze maneno ya kiburi, na hivyo kuchukiwa na Mungu.
Usieneze kiholela maneno yanayonenwa kutoka kinywani mwa Mungu, usije ukadhihakiwa na wengine na kufanyiwa mzaha na ibilisi.
Itii kazi yote ya Mungu wa leo. Hata kama huielewi, usiihukumu; kile tu unachoweza kufanya ni kutafuta na kushiriki.
Hakuna mtu anayepaswa kuvuka mpaka wa nafasi asili ya Mungu. Huwezi kufanya chochote zaidi ya kumtumikia Mungu wa leo kutoka katika nafasi ya mwanadamu. Huwezi kumfundisha Mungu wa leo kutoka katika nafasi ya mwanadamu—kufanya hivyo ni kosa.
Hakuna anayeweza kusimama katika nafasi ya mtu anayeshuhudiwa na Mungu; katika maneno, matendo, na mawazo yako ya ndani kabisa, unasimama katika nafasi ya mwanadamu. Hili linapaswa kufuatwa, ni jukumu la mwanadamu, na hakuna anayeweza kulibadilisha; kufanya vinginevyo kutakiuka amri za utawala. Hili linapaswa kukumbukwa na wote.
Mungu kunena na kutamka kwa muda mrefu kumesababisha mwanadamu achukulie kusoma na kukariri maneno ya Mungu kuwa kazi yake kuu. Hakuna anayetilia maanani utendaji, na hata kile mnachopaswa kufuata hamfuati. Hili limeleta matatizo na shida nyingi katika huduma yenu. Ikiwa, kabla ya kutenda maneno ya Mungu, hujafuata kile unachopaswa kufuata, basi wewe ni mmoja wa wale wanaobeuliwa na Mungu. Katika kufuata desturi hizi, unapaswa kuwa wa dhati na mnyofu. Hupaswi kuzichukulia kama pingu, bali uzifuate kama amri. Leo, hupaswi kujishughulisha na ni matokeo gani yanapaswa kufikiwa; kwa ufupi, hivi ndivyo Roho Mtakatifu anavyofanya kazi, na yeyote anayekiuka lazima aadhibiwe. Roho Mtakatifu hana hisia za kimwili, na hajali ufahamu wako wa wakati wa sasa. Ukimkosea Mungu leo, basi Atakuadhibu. Ukimkosea ndani ya upeo wa mamlaka Yake, basi Hatakusamehe. Hajali jinsi ulivyo makini katika ufuataji wako wa maneno ya Yesu. Ukikiuka amri za Mungu za leo, Atakuadhibu, na kulichukulia kama kosa lenye adhabu ya kifo. Inawezaje kukubalika kwako kutofuata? Lazima uzifuate, hata kama inamaanisha kuteseka maumivu kidogo! Haijalishi ni dini, sekta, taifa, au dhehebu gani, katika siku za usoni wote lazima wafuate desturi hizi. Hakuna anayeachwa, na hakuna atakayehurumiwa! Kwa maana ndiyo ambayo Roho Mtakatifu anafanya katika wakati wa sasa, na hakuna anayeweza kuyakiuka. Ingawa si mambo makubwa, lazima yafanywe na kila mtu na ni amri zilizowekwa kwa mwanadamu na Yesu, aliyefufuka na kupaa mbinguni. Je, “Njia … (7)” haisemi kwamba ufafanuzi wa Yesu wa iwapo wewe ni mwenye haki au mwenye dhambi ni kulingana na mtazamo wako kwa Mungu leo? Hakuna anayeweza kupuuza jambo hili. Katika Enzi ya Sheria, kizazi baada ya kizazi cha Mafarisayo kilimwamini Mungu, lakini kwa kuwasili kwa Enzi ya Neema hawakumjua Yesu, na walimpinga. Hivyo basi, yote waliyofanya yaliambulia patupu na yalikuwa ya bure, na Mungu hakukubali matendo yao. Ukiweza kuling’amua hili, basi hutatenda dhambi kwa urahisi. Watu wengi, pengine, wameshindana na Mungu. Kumpinga Mungu kuna ladha gani hasa? Je, ni chungu au tamu? Unapaswa kuelewa hili; usijifanye kwamba hujui. Mioyoni mwao, pengine, watu wengine bado hawajashawishika. Hata hivyo Ninawashauri wajaribu na waone ina ladha gani hasa, watu wengi wasijekuwa na shaka kila wakati kuhusu hilo. Watu wengi husoma maneno ya Mungu lakini wanampinga kwa siri mioyoni mwao. Baada ya kumpinga hivi, je, huhisi kana kwamba kisu kimesokotwa moyoni mwako? Ikiwa si kutotangamana katika familia, ni usumbufu wa kimwili, au mateso ya wana na mabinti. Ingawa mwili wako umeepushwa na kifo, mkono wa Mungu hautakuacha kamwe. Je, unafikiri inaweza kuwa rahisi hivyo? Hasa, ni muhimu hata zaidi kwa wengi walio karibu na Mungu kulenga hili. Kadiri muda unavyopita, utalisahau, na, bila kutambua, utatumbukizwa katika kishawishi na kutojali chochote, na huu utakuwa mwanzo wa wewe kutenda dhambi. Je, hili linaonekana kuwa jambo dogo kwako? Ikiwa unaweza kufanya vizuri, basi itakuwa fursa kwako kufanywa kuwa mtimilifu—kuja mbele ya Mungu na kupokea maelekezo Yake kutoka kinywani Mwake mwenyewe. Ikiwa wewe ni mzembe, basi kutakuwa na shida kwako—hutakuwa na heshima kwa Mungu, maneno na matendo yako yatakuwa ya upotovu, na ni vigumu kusema ni lini utasombwa na dhoruba kali na mawimbi makubwa. Kila mmoja wenu anapaswa kuzingatia kwa karibu amri hizi. Ukizikiuka, basi ingawa mtu anayeshuhudiwa na Mungu huenda asikushutumu, Roho wa Mungu atakuwa na jambo ambalo hajamalizana nawe, na Hatakuhurumia. Je, unaweza kubeba matokeo ya kosa lako? Hivyo, haijalishi Mungu anasema nini, lazima utie maneno Yake katika vitendo, na lazima uyafuate kwa namna yoyote uwezayo. Hili si jambo rahisi!