Kiini cha Mwili Uliovaliwa na Mungu
Mungu katika kupata mwili Kwake kwa mara ya kwanza Aliishi duniani kwa miaka thelathini na tatu na nusu, lakini Alitekeleza huduma Yake kwa miaka mitatu na nusu pekee ya hiyo miaka yote. Kipindi Alichofanya kazi na kabla Hajaanza kazi Yake, Alikuwa na ubinadamu wa kawaida. Aliishi na ubinadamu Wake wa kawaida kwa miaka thelathini na tatu na nusu. Katika miaka yote mitatu na nusu ya mwisho Alijifichua kuwa Mungu mwenye mwili. Kabla Hajaanza kutekeleza kazi ya huduma Yake, Alikuwa na ubinadamu wa kawaida, bila kuonyesha ishara ya uungu Wake, na ni baada tu ya kuanza rasmi kutekeleza huduma Yake ndipo uungu Wake uliwekwa wazi. Maisha na kazi Zake katika ile miaka ishirini na tisa yote ilidhihirisha kuwa Alikuwa mwanadamu halisi, mwana wa Adamu, na kwamba Alikuwa katika mwili, kwa sababu huduma Yake ilianza rasmi baada tu ya kuwa na umri wa miaka ishirini na tisa. “Kupata mwili” ni kuonekana kwa Mungu katika mwili; Mungu anafanya kazi miongoni mwa binadamu walioumbwa katika mfano wa mwili. Kwa hivyo, kwa kuwa Yeye ni Mungu mwenye mwili, ni lazima kwanza Awe mwili, mwili wenye ubinadamu wa kawaida; hili ndilo sharti la kimsingi kabisa. Kwa kweli, maana ya Mungu kupata mwili ni kwamba Mungu anaishi na kufanya kazi katika mwili, kwamba Mungu katika kiini Chake hasa anakuwa mwili, anakuwa mtu. Maisha Yake ya kimwili na kazi vinaweza kugawanywa katika hatua mbili. Kwanza ni maisha Anayoishi kabla ya kuanza kutekeleza huduma Yake. Anaishi katika familia ya kawaida ya binadamu, katika ubinadamu wa kawaida kabisa, Akifuata maadili na sheria za maisha ya wanadamu, Akiwa na mahitaji ya kawaida ya binadamu (chakula, nguo, makazi, na usingizi), na udhaifu wa kawaida wa binadamu na hisia za kawaida za binadamu. Kwa maneno mengine, katika hatua hii ya kwanza Anaishi maisha yasiyo na uungu, yenye ubinadamu wa kawaida kabisa, Akijishughulisha na shughuli zote za wanadamu. Hatua ya pili ni ya maisha Anayoishi baada ya kuanza kutekeleza huduma Yake. Bado Yumo katika ubinadamu wa kawaida Akiwa na umbo la nje la binadamu bila kuonyesha ishara yoyote ya kawaida kwa nje. Lakini kimsingi Anaishi kwa ajili ya huduma Yake, na wakati huu ubinadamu Wake wa kawaida upo kikamilifu kuhudumia kazi ya kawaida ya uungu Wake; kwani wakati huo, ubinadamu Wake wa kawaida umekomaa kiasi cha kuweza kutekeleza huduma Yake. Kwa hivyo hatua ya pili ya maisha Yake ni ya kutekeleza huduma Yake katika ubinadamu Wake wa kawaida, ni maisha ya ubinadamu wa kawaida na uungu kamili. Sababu ya kuishi katika maisha ya kawaida kabisa ya ubinadamu katika hatua ya kwanza ya maisha Yake ni kwamba ubinadamu Wake bado haujalingana na ukamilifu wa kazi ya uungu, bado haujakomaa; ni baada tu ya kukomaa kwa ubinadamu Wake na kuwa na uwezo wa kustahimili huduma Yake, ndipo Anaweza kuanza kutekeleza huduma Yake. Kwa kuwa Yeye ni mwili, Anahitaji kukua na kukomaa, hatua ya kwanza ya maisha Yake ni ile ya ubinadamu wa kawaida, ilhali katika hatua ya pili, kwa kuwa ubinadamu Wake una uwezo wa kuanza kazi Yake na kutekeleza huduma Yake, maisha ambayo Mungu mwenye mwili Anaishi katika kipindi cha huduma Yake ni ya ubinadamu na ya uungu kamili. Ikiwa, tangu wakati wa kuzaliwa Kwake, Mungu mwenye mwili Angeanza rasmi huduma Yake, Akifanya ishara na maajabu yasiyo ya kawaida, basi Asingekuwa na kiini cha mwili. Kwa hivyo, ubinadamu Wake upo kwa sababu ya kiini Chake cha kimwili; hapawezi kuwa na mwili bila ubinadamu, na mtu bila ubinadamu si mwanadamu. Kwa njia hii, ubinadamu wa mwili wa Mungu ni sifa ya ndani ya mwili wa Mungu. Kusema kwamba “Mungu Anapokuwa mwili Anakuwa na uungu kamili, na si binadamu kabisa,” ni kufuru, kwa kuwa kauli hii haipo kabisa, na inakiuka kanuni ya kupata mwili. Hata baada ya kuanza kutekeleza huduma Yake, bado Anaishi katika uungu Wake akiwa na umbo la nje la binadamu Anapofanya kazi Yake; ni kwamba tu kwa wakati huo, ubinadamu Wake una kusudi la pekee la kuuwezesha uungu Wake kutekeleza kazi katika mwili wa kawaida. Kwa hivyo wakala wa kazi ni uungu unaosetiriwa katika ubinadamu Wake. Ni uungu na wala si ubinadamu Wake unaofanya kazi, lakini uungu huu umefichwa ndani ya ubinadamu Wake; kimsingi kazi Yake inafanywa na uungu Wake kamili, haifanywi na ubinadamu Wake. Lakini mtekelezaji wa kazi ni mwili Wake. Mtu anaweza kusema kuwa Yeye ni mwanadamu na vilevile ni Mungu, kwani Mungu Anakuwa Mungu Anayeishi katika mwili, mwenye umbo la mwanadamu na kiini cha binadamu, lakini pia Ana kiini cha Mungu. Kwa sababu Yeye ni binadamu aliye na kiini cha Mungu, Yuko juu ya binadamu wote walioumbwa, juu ya mtu yeyote anayeweza kutekeleza kazi ya Mungu. Kwa hivyo, miongoni mwa wale wote walio na umbo la binadamu kama Lake, miongoni mwa wale wote walio na ubinadamu, Yeye pekee ndiye Mungu mwenye mwili Mwenyewe—wengine wote ni wanadamu walioumbwa. Japokuwa wote wana ubinadamu, wanadamu walioumbwa hawana chochote ila ubinadamu, ilhali Mungu mwenye mwili ni tofauti: katika mwili Wake, mbali na kuwa na ubinadamu, lililo muhimu kabisa, pia Ana uungu. Ubinadamu Wake waweza kuonekana katika mwonekano wa nje wa mwili Wake na katika maisha Yake ya kila siku; ila uungu Wake ni vigumu kuonekana. Kwa kuwa uungu Wake huonyeshwa pale tu Anapokuwa na ubinadamu, na si wa kimuujiza kama watu wanavyofikiria kuwa, ni vigumu sana kwa watu kuuona. Hata leo, watu wana ugumu mkubwa sana wa kufahamu hasa kiini cha Mungu mwenye mwili ni nini. Hata baada ya Mimi kuzungumza maneno mengi sana, Ninatarajia bado ni siri kwa wengi wenu. Kwa kweli, suala hili ni rahisi sana: Kwa kuwa Mungu anakuwa mwili, kiini Chake ni muunganyiko wa ubinadamu na uungu. Muunganyiko huu unaitwa Mungu Mwenyewe, Mungu Mwenyewe duniani.
Maisha Aliyoishi Yesu duniani yalikuwa maisha ya kimwili ya kawaida. Aliishi katika ubinadamu wa kawaida wa mwili Wake. Mamlaka Yake—kufanya kazi Yake na kuzungumza neno Lake, au kuwaponya wagonjwa au kufukuza mapepo, kufanya hiyo kazi isiyo ya kawaida—haikujidhihirisha yenyewe, kwa sehemu kubwa, hadi Alipoanza huduma Yake. Maisha Yake kabla ya umri wa miaka ishirini na tisa, kabla ya Yeye kuanza kutekeleza huduma Yake, yalikuwa uthibitisho tosha kuwa Alikuwa mwili wa kawaida. Kwa sababu ya hili, na kwa kuwa Alikuwa bado Hajaanza kutekeleza huduma Yake, watu hawakuona chochote cha uungu ndani Yake, hawakuona chochote zaidi ya ubinadamu wa kawaida, mwanadamu wa kawaida—kama vile wakati huo baadhi ya watu walimwamini kuwa mwana wa Yusufu. Watu walidhani kuwa Alikuwa mwana wa mwanadamu wa kawaida, hawakuwa na njia ya kugundua kuwa Alikuwa mwili wa Mungu; hata wakati Alipotenda miujiza mingi katika harakati za kutekeleza huduma Yake, watu wengi bado walisema Alikuwa mwana wa Yusufu, kwani Alikuwa Kristo mwenye umbo la nje la ubinadamu wa kawaida. Ubinadamu Wake wa kawaida pamoja na kazi yake vyote vilikuwepo ili kutimiza umuhimu wa kupata mwili kwa mara ya kwanza, kuthibitisha kwamba Mungu alikuwa Amekuja kikamilifu katika mwili, Akawa mwanadamu wa kawaida kabisa. Kuwa na ubinadamu wa kawaida kabla ya kuanza kazi Yake ulikuwa uthibitisho kuwa Alikuwa mwili wa kawaida; na kwa kuwa Alifanya kazi baadaye ilithibitisha pia kwamba Alikuwa mwili wa kawaida, kwa kuwa Alifanya ishara na miujiza, kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo katika mwili wenye ubinadamu wa kawaida. Sababu za kufanya miujiza ilikuwa kwamba mwili Wake ulikuwa umebeba mamlaka ya Mungu, ulikuwa mwili ambamo Roho wa Mungu Alikuwa amefichwa. Alikuwa na mamlaka haya kwa sababu ya Roho wa Mungu, na haikumaanishi kuwa Hakuwa Mwili. Kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo ilikuwa kazi Aliyopaswa kutekeleza katika huduma Yake, onyesho la uungu Wake uliojificha ndani ya ubinadamu Wake, na haijalishi ni ishara za aina gani Alizoonyesha au jinsi Alivyodhihirisha mamlaka Yake, bado Aliishi katika ubinadamu wa kawaida na bado Alikuwa mwili wa kawaida. Hadi kufikia wakati Alipofufuka baada ya kufa msalabani. Aliishi katika mwili wa kawaida. Akitoa neema, Akiwaponya wagonjwa, na kufukuza mapepo hayo yote yalikuwa sehemu ya huduma Yake, hiyo yote ilikuwa kazi Aliyotekeleza katika mwili Wake wa kawaida. Kabla ya kwenda msalabani, Hakuuacha mwili Wake wa kawaida, haijalishi Alikuwa Anafanya nini. Alikuwa Mungu Mwenyewe, Akifanya kazi ya Mungu, lakini kwa sababu Alikuwa Mwili wa Mungu, Alikula chakula na kuvaa nguo, Alikuwa na mahitaji ya kawaida ya binadamu, Alikuwa na fikira za kawaida za binadamu na akili za kawaida. Haya yote yalikuwa uthibitisho kwamba Alikuwa mwanadamu wa kawaida, ambayo yalithibitisha kuwa mwili wa Mungu ulikuwa mwili wenye ubinadamu wa kawaida, haukuwa wa kiroho. Kazi Yake ilikuwa kukamilisha kazi ya Mungu kupata mwili kwa mara ya kwanza, kutimiza huduma ya kupata mwili kwa mara ya kwanza. Umuhimu wa kupata mwili ni kwamba mtu wa kawaida Anatekeleza kazi ya Mungu Mwenyewe; yaani, kwamba Mungu Anatekeleza kazi Yake ya uungu katika ubinadamu na hivyo kumshinda Shetani. Kupata mwili kunamaanisha kwamba Roho wa Mungu Anakuwa Mwili, yaani, Mungu Anakuwa mwili; kazi Anayoifanya katika mwili ni kazi ya Roho, inayothibitika katika mwili, na kuonyeshwa kwa mwili. Hakuna mwingine isipokuwa tu mwili wa Mungu unaoweza kutimiza huduma ya Mungu mwenye mwili; yaani, ni mwili wa Mungu pekee, ubinadamu huu wa kawaida—na hakuna mwingine yeyote—anayeweza kuonyesha kazi ya uungu. Iwapo, wakati wa kuja Kwake kwa mara ya kwanza, Mungu Hangekuwa na ubinadamu wa kawaida kabla ya umri wa miaka ishirini na tisa—ikiwa mara tu Alipozaliwa Angeweza kufanya miujiza, ikiwa mara tu Alipojifunza kuongea Angeweza kuongea lugha ya mbinguni, ikiwa mara tu Alipokanyaga duniani Angeweza kuyaelewa mambo yote ya kidunia, kung’amua fikira za kila mtu na nia zao—mtu kama huyu asingeitwa mwanadamu wa kawaida, na mwili Wake usingeitwa mwili wa mwanadamu. Iwapo ingekuwa hivi kwa Kristo, basi maana na kiini cha kuwa mwili kwa Mungu ingepotea. Kuwa Yeye ana ubinadamu wa kawaida kunathibitisha kuwa Yeye ni Mungu Aliyejidhihirisha katika mwili; ukweli kwamba Anapitia ukuaji wa kawaida wa binadamu unaonyesha zaidi kuwa Yeye ni mwili wa kawaida; hata zaidi, kazi Yake ni uthibitisho tosha kuwa Yeye ni Neno la Mungu, Roho wa Mungu, kuwa mwili. Mungu Anakuwa mwili kwa sababu ya mahitaji ya kazi; kwa maneno mengine, hatua hii ya kazi inapaswa kufanywa katika mwili, kufanywa katika ubinadamu wa kawaida. Hili ndilo sharti la “Neno kuwa mwili,” la “Neno kuonekana katika mwili,” na ndio ukweli wa Mungu kupata mwili mara mbili. Watu huenda wakaamini kuwa maisha yote ya Yesu yaliambatana na miujiza, kwamba mpaka kufikia mwisho wa kazi Yake duniani Hakudhihirisha ubinadamu wa kawaida, kwamba Hakuwa na mahitaji ya kawaida ya mwanadamu au udhaifu au hisia za binadamu, kwamba Hakuhitaji vitu vya msingi vya maisha au kuwa na fikira za kawaida za binadamu. Wanadhani tu kuwa Alikuwa mwanadamu asiyekuwa na akili ya kawaida, aliyevuka mipaka ya ubinadamu. Wanaamini kuwa kwa sababu Yeye ni Mungu, Hapaswi kufikiria na kuishi kama wanadamu wa kawaida wanavyofanya, kwamba ni mtu wa kawaida tu, mwanadamu halisi, ambaye Anaweza kufikiria mawazo ya kawaida ya kibinadamu na kuishi maisha ya mwanadamu wa kawaida. Haya yote ni mawazo ya wanadamu na maoni ya wanadamu, ambayo yanakinzana na madhumuni asilia ya kazi ya Mungu. Kufikiri kwa mwanadamu wa kawaida kunadumisha mawazo ya kawaida ya mwanadamu na ubinadamu wa kawaida; ubinadamu wa kawaida unadumisha kazi za kawaida za mwili; na kazi za kawaida za mwili zinawezesha maisha ya kawaida ya mwili katika ukamilifu wake. Ni kwa kufanya kazi tu katika mwili kama huo ndipo Mungu Anaweza kutimiza kusudi la kupata mwili Kwake. Kama Mungu mwenye mwili angekuwa na umbo la nje tu la mwili, bila kufikiri fikira za kawaida za binadamu, basi mwili huu usingekuwa na mawazo ya binadamu, sembuse ubinadamu halisi. Ni vipi ambavyo mwili kama huu, usio na ubinadamu, ungeweza kutimiza huduma ambayo Mungu mwenye mwili Anapaswa kutekeleza? Akili za kawaida huwezesha vipengele vyote vya maisha ya binadamu; bila akili ya kawaida, mtu hawezi kuwa mwanadamu. Kwa maneno mengine, mtu asiyefikiria fikra za kawaida ni mgonjwa wa akili. Na Kristo ambaye Hana ubinadamu ila uungu pekee Hawezi kuitwa mwili wa Mungu. Basi, mwili wa Mungu unawezaje kukosa ubinadamu wa kawaida? Je, si kufuru kusema kwamba Kristo hana ubinadamu? Kila shughuli ambazo wanadamu wa kawaida hufanya hutegemea utendaji kazi wa akili ya kawaida ya mwanadamu. Bila hiyo, wanadamu wangekuwa na mienendo iliyopotoka; wangeshindwa hata kutofautisha kati ya nyeupe na nyeusi, wema na uovu; na hawangekuwa na maadili ya binadamu na kanuni za uadilifu. Vivyo hivyo, iwapo Mungu mwenye mwili Asingefikiri kama mwanadamu wa kawaida, basi Asingekuwa mwili halisi, mwili wa kawaida. Mwili usiofikiri kama huo haungeweza kuikabili kazi ya uungu. Haungeweza kushiriki kwa kawaida katika shughuli za mwili wa kawaida, sembuse kuishi na wanadamu duniani. Na kwa hivyo, umuhimu wa kupata mwili kwa Mungu, kiini hasa cha kuja kwa Mungu katika mwili, kingepotea. Ubinadamu wa Mungu mwenye mwili upo ili kudumisha kazi ya kawaida ya uungu katika mwili; Mawazo Yake ya kawaida ya kibinadamu yanadumisha ubinadamu Wake wa kawaida na shughuli Zake zote za kawaida za kimwili. Mtu angeweza kusema kwamba mawazo Yake ya kawaida ya kibinadamu yapo ili kuendeleza kazi yote ya Mungu katika mwili. Ikiwa mwili huu haungekuwa na akili ya kawaida ya mwanadamu, basi Mungu hangeweza kufanya kazi katika mwili, na kile Anachohitaji kufanya katika mwili hakingeweza kutimizwa. Ingawa Mungu mwenye mwili Ana akili ya mwanadamu wa kawaida, kazi Yake haijatiwa doa na mawazo ya binadamu; Anafanya kazi katika ubinadamu na akili ya kawaida chini ya masharti ya awali kuwa atakuwa na ubinadamu na akili ya kawaida, na sio kwa kutumia mawazo ya kawaida ya binadamu. Haijalishi mawazo ya mwili Wake ni bora kiasi gani, kazi Yake haionyeshi alama ya mantiki au kufikiria. Kwa maneno mengine, kazi Yake haifikiriwi na akili ya mwili Wake, ila ni onyesho la moja kwa moja la kazi ya uungu katika ubinadamu Wake. Kazi Yake yote ni huduma Anayohitaji kutimiza, na hakuna hata moja inayofikiriwa kwa akili Zake. Kwa mfano, kuponya wagonjwa, kufukuza mapepo na kusulubishwa hayakuwa mazao ya akili Zake zakibinadamu, yasingeweza kutimizwa na mwanadamu yeyote mwenye akili za kibinadamu. Vivyo hivyo, kazi ya ushindi ya leo ni huduma ambayo ni sharti itekelezwe na Mungu mwenye mwili, lakini si kazi ya mapenzi ya mwanadamu, ni kazi ambayo uungu Wake unapaswa kuifanya, kazi ambayo hakuna mwanadamu mwenye mwili anayeweza kuifanya. Kwa hivyo, Mungu mwenye mwili ni lazima Awe na akili za binadamu, ni lazima Awe na ubinadamu wa kawaida, kwa sababu ni lazima Atekeleze kazi Yake katika ubinadamu akiwa na akili za kawaida. Hiki ndicho kiini cha kazi ya Mungu mwenye Mwili, kiini chenyewe cha Mungu mwenye mwili.
Kabla Yesu Hajatekeleza kazi yake, Aliishi tu katika ubinadamu Wake wa kawaida. Hakuna mtu ambaye angeweza kutambua kuwa Alikuwa Mungu, hakuna aliyegundua kuwa Alikuwa Mungu mwenye mwili; watu walimjua tu kama mwanadamu wa kawaida kabisa. Ubinadamu Wake wa kawaida ulikuwa ni uthibitisho kuwa Mungu Alipata mwili, na kwamba Enzi ya Neema ilikuwa enzi ya kazi ya Mungu mwenye mwili, si enzi ya kazi ya Roho. Ulikuwa uthibitisho kwamba Roho wa Mungu alitambulika kabisa katika mwili, kwamba katika enzi ya kupata mwili kwa Mungu mwili Wake ungefanya kazi yote ya Roho. Kristo aliye na ubinadamu wa kawaida ni mwili ambamo Roho anatambulika, akiwa na ubinadamu wa kawaida, akili ya kawaida, na mawazo ya kibinadamu. “Kutambuliwa” maana yake ni Mungu kufanyika mwanadamu, Roho kuwa mwili; ili kuiweka wazi, ni wakati ambapo Mungu Mwenyewe anaishi katika mwili wenye ubinadamu wa kawaida, na kupitia kwenye huo mwili, Anaonyesha kazi Yake ya Uungu—hii ndiyo maana ya kutambulika, au kupata mwili. Wakati wa kupata mwili Kwake kwa mara ya kwanza, ilikuwa ni lazima kwa Mungu kuponya wagonjwa na kutoa mapepo, kwa sababu kazi Yake ilikuwa kukomboa. Ili kuwakomboa wanadamu wote, Alihitaji kuwa mwenye huruma na mwenye kusamehe. Kazi Aliyoifanya kabla ya kusulubishwa ilikuwa ni kuponya watu na kufukuza mapepo, ambayo iliashiria wokovu Wake wa mwanadamu kutoka katika dhambi na uchafu. Kwa sababu ilikuwa ni Enzi ya Neema, ilikuwa ni muhimu Kwake kuwaponya wagonjwa, na kwa njia hiyo Alionyesha ishara na miujiza, mambo ambayo yalikuwa yakiwakilisha neema katika enzi hiyo; kwani Enzi ya Neema ilikitwa katika kutolewa kwa neema, ikiashiriwa na amani, furaha, na baraka za kimwili, vyote vikiwa zawadi za imani ya watu kwa Yesu. Hii ni kusema kuwa, kuponya wagonjwa, kufukuza mapepo na kutoa neema ilikuwa ni uwezo asilia wa mwili wa Yesu katika Enzi ya Neema, mambo haya yalikuwa ni kazi ya Roho iliyotambulika katika mwili. Lakini Alipokuwa Akitekeleza kazi kama hiyo, Alikuwa Akiishi katika mwili, Hakuenda nje ya mipaka ya mwili. Haijalishi ni matendo gani ya uponyaji Aliyotekeleza, bado Alikuwa na ubinadamu wa kawaida, bado Aliishi maisha ya kawaida ya binadamu. Sababu inayonifanya Niseme kuwa katika enzi ya kupata mwili kwa Mungu mwili ulitekeleza kazi yote ya Roho, ni kuwa haijalishi ni kazi gani Aliyoifanya, Aliifanya katika mwili. Lakini kwa sababu ya kazi Yake, watu hawakuuchukulia mwili Wake kuwa na kiini cha kimwili kabisa, kwani mwili huu ungeweza kufanya maajabu, na katika nyakati fulani maalum ungeweza kufanya mambo ambayo yalivuka uwezo wa kimwili. Kwa hakika, haya matukio yote yalitokea Alipoanza huduma Yake, kama vile Yeye kujaribiwa kwa siku arobaini au kubadilishwa sura kule mlimani. Hivyo kwa Yesu, maana ya kupata mwili kwa Mungu haikukamilishwa, ila tu sehemu yake ilitimizwa. Maisha Aliyoishi katika mwili kabla ya kuanza kazi Yake yalikuwa ya kawaida tu katika hali zote. Baada ya Yeye kuanza kazi, Alibakiza tu ganda la nje la mwili Wake. Kwa sababu kazi Yake ilikuwa onyesho la uungu Wake, ilipita kazi ya kawaida ya mwili. Hata hivyo, Mwili wa Mungu ulikuwa tofauti na wanadamu wenye mwili na damu. Kwa hakika, katika maisha Yake ya kila siku, Alihitaji chakula, nguo, usingizi, na makao kama mtu yeyote yule, Alikuwa na mahitaji ya lazima ya kawaida, na Alikuwa na hisia za mwanadamu wa kawaida, na Aliwaza kama mwanadamu wa kawaida. Bado watu walimchukulia kuwa ni mwanadamu wa kawaida, isipokuwa tu kwamba kazi Aliyoifanya ilikuwa ya kupita akili. Kwa hakika, haijalishi Alifanya nini, Aliishi katika ubinadamu wa kawaida, na hata Alipotekeleza kazi, fikira zake zilikuwa za kawaida, mawazo yake yalikuwa ya wazi, hata zaidi ya wanadamu wa kawaida. Ilikuwa muhimu kwa Mungu mwenye mwili kufikiri kwa njia hii, kwani kazi ya uungu ilipaswa ionyeshwe na mwili ambao fikira zake zilikuwa za kawaida sana na mawazo yake ya wazi kabisa—ni kwa njia hii tu ndiyo mwili Wake ungeweza kuonyesha kazi ya uungu. Wakati wa miaka yote thelathini na tatu na nusu ambayo Yesu Aliishi duniani, Alidumisha ubinadamu Wake wa Kawaida, lakini kwa sababu ya kazi Yake katika huduma Yake ya miaka mitatu na nusu, watu walidhani kuwa Alikuwa Amepita mipaka ya ubinadamu, kwamba Alikuwa wa kimiujiza zaidi kuliko hapo awali. Kwa kweli, ubinadamu wa kawaida wa Yesu haukubadilika kabla na baada ya Yeye kuanza huduma Yake; ubinadamu Wake ulikuwa sawa wakati wote, lakini kwa sababu ya tofauti iliyokuwepo kabla na baada ya Yeye kuanza huduma Yake, mitazamo miwili ilijitokeza kuhusiana na mwili Wake. Haijalishi watu walifikiria nini, Mungu mwenye mwili Alidumisha ubinadamu Wake asilia wa kawaida kipindi chote, kwani kwa sababu Mungu Alikuwa mwili, Aliishi katika mwili, mwili uliokuwa na ubinadamu wa kawaida. Hata ikiwa Alikuwa Anatekeleza huduma Yake au la, ubinadamu Wake wa kawaida usingeweza kufutika, kwani ubinadamu ndio kiini cha msingi cha mwili. Kabla Yesu hajaanza kutekeleza huduma Yake, mwili Wake ulibaki wa kawaida kabisa, ukishiriki katika shughuli zote za binadamu; Hakuonekana hata kidogo kuwa wa kiroho, Hakuonyesha ishara zozote za kimiujiza. Wakati ule Alikuwa tu mwanadamu wa kawaida sana Aliyemwabudu Mungu, japo dhamira Yake ilikuwa adilifu sana, ya kweli zaidi kuliko ya mtu yeyote. Hivi ndivyo ubinadamu Wake wa kawaida ulivyojionyesha wenyewe. Kwa kuwa Hakufanya kazi kabisa kabla ya kuianza huduma Yake, hakuna aliyemtambua, hakuna aliyegundua kuwa mwili Wake ulikuwa tofauti kabisa na miili ya watu wengine, kwa kuwa Hakutenda muujiza hata mmoja, Hakutenda hata sehemu moja ya kazi ya Mungu Mwenyewe. Hata hivyo, baada ya kuanza kutekeleza kazi Yake, Alidumisha umbo la nje la ubinadamu wa kawaida na kuendelea kuishi katika mawazo ya kawaida ya binadamu, lakini kwa kuwa Alikuwa Ameanza kufanya kazi ya Mungu Mwenyewe, kuanzisha huduma ya Kristo na kufanya kazi ambayo wanadamu wa kufa, wanadamu wenye mwili na damu, wasingeweza kuifanya, basi watu walidhani kuwa Hakuwa na ubinadamu wa kawaida na Hakuwa mwili wa kawaida kikamilifu ila mwili usio kamili. Kwa sababu ya yale Aliyotekeleza, watu walisema kuwa Alikuwa Mungu katika mwili Ambaye Hakuwa na ubinadamu wa kawaida. Huu ulikuwa ufahamu wa kimakosa, kwani watu hawakuelewa maana ya Mungu kupata mwili. Huu ufahamu mbaya ulitokana na ukweli kuwa kazi iliyoonyeshwa na Mungu katika mwili ilikuwa kazi ya uungu, iliyoonyeshwa kupitia kwa mwili wenye ubinadamu wa kawaida. Mungu alivaa mwili, Aliishi katika mwili, na kazi Yake katika ubinadamu Wake iliuziba ukawaida wa ubinadamu Wake. Kwa sababu hii, watu walidhani kuwa Mungu hakuwa na ubinadamu bali uungu tu.
Mungu katika kupata mwili Kwake kwa mara ya kwanza Hakukamilisha kazi ya kupata mwili; Alikamilisha tu hatua ya kwanza ya kazi iliyokuwa lazima kwa Mungu kuifanya katika mwili. Kwa hivyo, ili kuimaliza kazi ya kupata mwili, Mungu Amerudi katika mwili kwa mara nyingine tena, Akiishi kulingana na ukawaida na uhalisia wote wa mwili, yaani, anaifanya kazi ya Mungu ijitokeze katika mwili wa kawaida kabisa, na kwa njia hiyo Anahitimisha kazi Aliyoiacha bila kuikamilisha katika mwili. Mwili wa pili uliopatikana kimsingi ni sawa na ule wa kwanza, lakini ni halisi zaidi, wa kawaida kabisa kuliko ule wa kwanza. Kwa sababu hiyo, mateso yanayopitiwa na mwili wa pili uliopatikana ni makubwa kuliko yale ya ule wa kwanza, ila mateso haya ni kwa sababu ya huduma Yake katika mwili, ambayo ni tofauti na mateso ya mwanadamu mwovu. Vilevile yanayotokana na ukawaida na uhalisi wa mwili Wake. Kwa kuwa Anatekeleza huduma Yake katika mwili wa kawaida na halisi kabisa, ni lazima mwili upitie mateso makubwa. Kadiri mwili ulivyo wa kawaida na wa kivitendo, ndivyo unavyoteseka zaidi katika utekelezaji wa huduma Yake. Kazi ya Mungu inaonyeshwa katika mwili wa kawaida sana, mwili ambao si wa kimiujiza kabisa. Kwa kuwa mwili Wake ni wa kawaida, na ni lazima ubebe kazi ya kumwokoa mwanadamu, Anateseka hata zaidi kuliko ambavyo mwili wa kiroho unavyoweza kuteseka—mateso haya yote yanatokana na uhalisi na ukawaida wa mwili Wake. Kutokana na mateso yaliyopitiwa na hii miili miwili iliyopatikana wakati wa kutekeleza huduma Zao, mtu anaweza kuona kiini cha kupata mwili. Kadiri mwili ulivyo wa kawaida, ndivyo Anavyopata mateso mazito Anapofanya kazi, kadri mwili unaofanya kazi unavyokuwa halisi, ndivyo dhana za watu zinavyoendelea kuwa kubwa, na ndivyo hatari nyingi zaidi zinavyoweza kumpata Yeye. Lakini, kadiri mwili ulivyo halisi, kadiri mwili unavyokuwa na mahitaji na hisia kamili za mwanadamu wa kawaida, ndivyo Anavyoweza zaidi kuifanya kazi ya Mungu katika mwili. Ulikuwa mwili wa Yesu ulioangikwa msalabani, mwili Wake Alioutoa kama kafara kwa dhambi; yaani, ni kupitia kwa mwili wenye ubinadamu wa kawaida ndipo Alipoweza kumshinda Shetani na kumkomboa kabisa mwanadamu kutoka msalabani. Ni kwa njia ya mwili kamili ambapo mwili wa pili wa Mungu unafanya kazi ya ushindi na kumshinda Shetani. Ni mwili tu wa kawaida na halisi kabisa unaoweza kutekeleza kazi ya ushindi kwa ukamilifu wake na kutoa ushuhuda wenye nguvu. Hii ni sawa na kusema kwamba, ushindi juu ya mwanadamu unafanywa kuwa bora kupitia uhalisi na ukawaida wa mwili wa Mungu, si kupitia miujiza na mafunuo yasiyo ya kawaida. Huduma inayofanywa na huyu Mungu mwenye mwili ni kuzungumza, na ni kupitia kuzungumza ndipo Anapomshinda na kumkamilisha mwanadamu; kwa maneno mengine, kazi ya Roho inayodhihirika katika mwili ni kuzungumza na kazi ya mwili ni kuzungumza, na hivyo inafikia lengo la kuwashinda, kuwafichua, kuwakamilisha, na kuwaondoa watu kabisa. Kwa hivyo, ni katika kazi ya ushindi ambapo kazi ya Mungu katika mwili itatimizwa kikamilifu. Kazi ya upatanisho kwa ajili ya dhambi za wanadamu iliyofanywa mara ya kwanza ilikuwa tu ni mwanzo wa kazi ya kupata mwili; ni mwili tu unaofanya kazi ya ushindi ndio utakamilisha kazi yote ya kupata mwili. Kijinsia, mmoja ni mwanamke na mwingine ni mwanamume; kwa hili, maana ya kupata mwili kwa Mungu imekamilishwa. Dhana za mwanadamu kumhusu Mungu zimeondolewa: Mungu Anaweza kuwa mwanamke na mwanamume, na kimsingi Mungu mwenye mwili Hana jinsia. Alimuumba mwanamume na mwanamke, na Kwake, hakuna mgawanyiko wa jinsia. Katika hatua hii ya kazi, Mungu Hafanyi ishara na miujiza, ili kwamba kazi iweze kutimiza matokeo yake kupitia kwa maneno. Sababu ya jambo hili, aidha, ni kwa sababu kazi ya Mungu mwenye mwili kwa wakati huu si kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo, ila ni kumshinda mwanadamu kupitia kunena, ikiwa na maana kwamba uwezo wa asili unaomilikiwa na mwili huu uliopatwa na Mungu ni kunena maneno na kumshinda mwanadamu, si kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo. Kazi Yake katika ubinadamu wa kawaida si kutenda miujiza, si kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo, ila ni kunena, na kwa hivyo kupata mwili kwa mara ya pili kunaonekana kwa watu kuwa kwa kawaida zaidi ya mara ya kwanza. Watu wanaona kuwa Mungu kupata mwili si uongo; lakini huyu Mungu mwenye mwili ni tofauti na Yesu Aliyekuwa mwili, na ingawa Wote ni kupata mwili kwa Mungu, Hawako sawa kabisa. Yesu Alikuwa na ubinadamu usio wa tofauti, ubinadamu wa kawaida, lakini Aliambatana na ishara nyingi na miujiza. Katika huyu Mungu mwenye mwili, macho ya mwanadamu hayataona ishara au miujiza, wala kuponya wagonjwa au kufukuza mapepo, wala kutembea juu ya bahari, wala kufunga kwa siku arobaini… Hafanyi kazi sawa na Aliyoifanya Yesu, si kwa kuwa mwili Wake kimsingi ni tofauti na ule wa Yesu, ila ni kwa sababu si huduma Yake kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo. Haharibu kazi Yake mwenyewe, Havurugi kazi Yake mwenyewe. Kwa kuwa Anamshinda mwanadamu kupitia maneno Yake ya kivitendo, hakuna haja ya kumtiisha kwa miujiza, na hivyo hatua hii ni kukamilisha kazi ya kupata mwili. Mungu mwenye mwili unayemwona leo ni mwili kamili, na hakuna kitu kisicho cha kawaida kuhusu Yeye. Anakuwa mgonjwa sawa tu na watu wengine, Anahitaji chakula na nguo sawa tu na watu wengine, kwani Yeye ni mwili kabisa. Ikiwa kwa wakati huu Mungu mwenye mwili Angefanya ishara na miujiza mikubwa, ikiwa Angeponya wagonjwa, kufukuza mapepo, au Angeweza kuua kwa neno moja tu, je, kazi ya kushinda ingefanywaje? Je, kazi ingeenezwa vipi miongoni mwa watu wa Mataifa? Kuponya wagonjwa na kufukuza mapepo ilikuwa kazi ya Enzi ya Neema, hatua ya kwanza katika kazi ya ukombozi, na sasa kwa kuwa Mungu Amemkomboa mwanadamu kutoka msalabani, Hatekelezi kazi hiyo kamwe. Ikiwa katika siku za mwisho “Mungu” sawa na Yesu Angeonekana, Ambaye Anaponya wagonjwa, Anafukuza mapepo na Anayesulubiwa kwa ajili ya wanadamu, “Mungu” huyo, japo Analingana na maelezo ya Mungu katika Biblia, na ni rahisi kwa mwanadamu kumkubali, Hangeweza, katika kiini chake, kuwa mwili uliovaliwa na Roho wa Mungu, bali na roho mwovu. Kwani ni kanuni ya kazi ya Mungu kutorudia Alichokikamilisha. Hivyo basi kazi ya kupata mwili kwa Mungu kwa mara ya pili ni tofauti na kule kwa kwanza. Katika siku za mwisho, Mungu Anafanikisha kazi ya kushinda katika mwili wa kawaida; Haponyi wagonjwa, Hatasulubishwa kwa ajili ya mwanadamu, ila tu Ananena maneno katika mwili, Anamshinda mwanadamu katika mwili. Ni mwili kama huo tu ndio mwili wa Mungu katika mwili; ni mwili kama huo tu ndio unaoweza kukamilisha Kazi ya Mungu katika mwili.
Haijalishi kama katika hatua hii Mungu mwenye mwili Anapitia ugumu au Anatekeleza huduma Yake, Anafanya hivyo ili kukamilisha maana ya kupata mwili, kwani huku ndiko Mungu kupata mwili kwa mara ya mwisho. Mungu anaweza kufanyika mwili mara mbili tu. Hakuwezi kuwa na mara ya tatu. Kupata mwili kwa mara ya kwanza kulikuwa ni mwanamume, mara ya pili ni mwanamke, na kwa hivyo sura ya mwili wa Mungu imekamilika katika akili za mwanadamu; zaidi ya hayo, kupata mwili mara mbili tayari kumekamilisha kazi ya Mungu katika mwili. Mara ya kwanza, Mungu mwenye mwili Alikuwa na ubinadamu wa kawaida, ili kukamilisha maana ya kupata mwili. Mara hii vilevile Ana ubinadamu wa kawaida lakini maana ya kupata mwili huku ni tofauti: ni kwa kina zaidi, na kazi Yake ni ya umuhimu mkubwa. Sababu ya Mungu kufanyika mwili kwa mara nyingine tena ni ili kukamilisha maana ya kupata mwili. Mungu atakapomaliza kabisa hatua hii ya kazi Yake, maana nzima ya kupata mwili, yaani, kazi ya Mungu katika mwili, itakuwa imekamilika, na hakutakuwa na kazi nyingine ya kufanywa katika mwili. Yaani, tangu sasa Mungu Hatawahi tena kuja katika mwili kufanya kazi Yake. Ni kwa kuwaokoa na kuwakamilisha wanadamu ndipo Mungu anafanya kazi ya kupata mwili. Kwa maneno mengine, si jambo la kawaida kwa Mungu kuja katika mwili, isipokuwa kwa ajili ya kazi. Kwa kuja kufanya kazi Akiwa katika mwili, Anamwonyesha Shetani kuwa Mungu ni mwili, mtu wa kawaida—lakini bado Anaweza kuitawala dunia kwa ushindi, Anaweza kumshinda Shetani, kumkomboa mwanadamu na kumshinda mwanadamu! Lengo la kazi ya Shetani ni kuwapotosha wanadamu, ilhali lengo la Mungu ni kuwaokoa wanadamu. Shetani huwateka wanadamu katika shimo lisilo na mwisho, ilhali Mungu anawaokoa kutoka humo shimoni. Shetani huwafanya wanadamu wote wamwabudu, ilhali Mungu anawafanya wawe chini ya utawala Wake, kwani Yeye ndiye Bwana wa viumbe vyote. Kazi hii yote inatekelezwa kupitia Mungu kupata mwili mara mbili. Mwili Wake kimsingi ni muunganiko wa ubinadamu na uungu, na unakuwa na ubinadamu wa kawaida. Kwa hivyo, bila Mungu kupata mwili, Mungu Asingeweza kufikia matokeo katika ukombozi wa mwanadamu, na bila ubinadamu wa kawaida wa mwili Wake, kazi Yake katika mwili bado haingefikia matokeo. Kiini cha kupata mwili kwa Mungu ni kwamba lazima awe na ubinadamu wa kawaida; kwani ingekuwa vinginevyo, ingekuwa kinyume na madhumuni ya awali ya Mungu ya kupata mwili.
Kwa nini Ninasema kuwa maana ya kupata mwili haikukamilishwa katika kazi ya Yesu? Ni kwa sababu Neno halikuwa Mwili kikamilifu. Kilichofanywa na Yesu kilikuwa tu sehemu moja ya kazi ya Mungu katika mwili; Alifanya tu kazi ya ukombozi na Hakufanya kazi ya kumpata mwanadamu kikamilifu. Kwa sababu hii, Mungu amefanyika mwili kwa mara nyingine tena katika siku za mwisho. Hatua hii ya kazi, pia inafanywa katika mwili wa kawaida, ikifanywa na mwanadamu wa kawaida kabisa, ambaye ubinadamu wake haupiti mipaka ya ubinadamu. Kwa maneno mengine, Mungu Amekuwa mwanadamu kamili, na ni mtu ambaye utambulisho wake ni ule wa Mungu, mwanadamu kamili, mwili kamili, Ambaye Anatekeleza kazi. Macho ya mwanadamu huona umbo la mwili ambao haujavuka mipaka ya ubinadamu hata kidogo, ni, mwanadamu wa kawaida kabisa Anayeweza kuzungumza lugha ya mbinguni, Ambaye Haonyeshi ishara za kimiujiza, Hafanyi miujiza, sembuse kuweka wazi ukweli wa ndani kuhusu dini katika kumbi kuu za mikutano. Kazi ya kupata mwili kwa mara ya pili inaonekana kwa wanadamu kuwa tofauti kabisa na ile ya kwanza, kiasi kwamba kazi hizi mbili zinaonekana kutokuwa na uhusiano wowote, na hakuna chochote katika kazi ya kwanza kinachoweza kuonekana wakati huu. Japo kazi ya kupata mwili kwa mara ya pili ni tofauti na ile ya kwanza, hili halithibitishi kuwa chanzo Chao si kimoja na sawa. Iwapo chanzo Chao ni kimoja inategemea aina ya kazi iliyofanywa na miili na si katika maumbo Yao ya nje. Katika hatua tatu za kazi Yake, Mungu amefanyika mwili mara mbili, na mara zote kazi ya Mungu katika mwili inaanzisha enzi mpya, inaanzisha kazi mpya; kupata mwili kwa mara ya kwanza na ya pili kunakamilishana. Macho ya wanadamu hayawezi kugundua kuwa hii miili miwili kwa kweli imetoka kwenye chanzo kimoja. Ni wazi kwamba hili liko nje ya uwezo wa macho ya wanadamu au akili za wanadamu. Lakini katika kiini Chao, ni miili sawa, kwani kazi Zao zinatoka kwa Roho mmoja. Ikiwa hii miili miwili inatoka kwenye chanzo kimoja haiwezi kuamuliwa kutokana na enzi na sehemu Ilipozaliwa, au vigezo vingine kama hivyo, ila kwa kazi ya uungu iliyoonyeshwa Nayo. Kupata mwili kwa pili hakufanyi kazi yoyote iliyofanywa na Yesu, kwani kazi ya Mungu haifuati makubaliano, lakini kila wakati inafungua njia mpya. Kupata mwili kwa mara ya pili hakulengi kuongeza au kuimarisha maono ya kupata mwili kwa mara ya kwanza katika akili za watu, bali inautimiza na kuukamilisha, ili kuongeza maarifa ya mwanadamu kuhusu Mungu, kuvunja sheria zote ambazo zipo katika mioyo ya watu, na kufuta picha za uongo kuhusu Mungu mioyoni mwao. Ni wazi kuwa hakuna hatua moja ya kazi ya Mungu mwenyewe inayoweza kumpa mwanadamu ufahamu kamili wa Mungu; kila moja inatoa kwa sehemu tu, si ufahamu kamili. Ingawa Mungu ameonyesha tabia Yake kikamilifu, lakini kwa sababu ya upungufu wa ufahamu wa mwandamu, ufahamu wake kuhusu Mungu si kamili. Haiwezekani, kutumia lugha ya wanadamu, kuelezea tabia nzima ya Mungu; basi je hatua moja tu ya kazi Yake itawezaje kumwelezea Mungu kikamilifu? Anafanya kazi katika mwili kwa kujificha katika ubinadamu Wake wa kawaida, na mtu anaweza kumjua tu kupitia kwa maonyesho ya uungu Wake, si kupitia kwa umbo Lake la kimwili. Mungu Anakuja katika mwili kumruhusu mwanadamu Amjue kupitia kazi Zake mbalimbali, na hakuna hatua mbili za kazi Yake zinazofanana. Ni kwa njia hii tu mwanadamu anaweza kuwa na ufahamu kamili wa kazi ya Mungu katika mwili, si kwa kujifunga katika kipengele kimoja tu. Japo kazi ya hii miili miwili iliyopatikana ni tofauti, kiini cha hii miili, na chanzo cha kazi Yao vinafanana; ni kwamba tu Ipo ili kutekeleza hatua mbili tofauti za kazi, na inatokea katika enzi mbili tofauti. Licha ya jambo lolote, miili ya Mungu katika mwili inashiriki kiini kimoja na asili moja—huu ni ukweli ambao hauwezi kupingwa na yeyote.