Ukweli wa Ndani wa Kazi ya Ushindi (4)
Inamaanisha nini kufanywa kuwa mtimilifu? Inamaanisha nini kushindwa? Ni vigezo vipi vinavyopaswa kutimizwa ili watu washindwe? Na ni vigezo vipi vinavyopaswa kutimizwa ili wafanywe kuwa watimilifu? Kumshinda na kumfanya kuwa mtimilifu kote ni kwa madhumuni ya kumfanya mwanadamu kuwa kamili ili aweze kurejeshwa katika mfano wake wa asili, na kuwekwa huru kutokana na tabia zake potovu za kishetani na ushawishi wa Shetani. Kushinda huku kunakuja mapema katika mchakato wa kumfinyanga mwanadamu; ndiko hatua ya kwanza ya kazi. Kufanya kuwa mtimilifu ndiyo hatua ya pili, na ndiyo kazi ya kuhitimisha. Watu wote lazima wapitie mchakato wa kushindwa. La sivyo, hawangekuwa na njia ya kumjua Mungu, wala hawangejua kwamba kuna Mungu, ambayo ni kusema, isingewezekana kwao kumkiri Mungu. Na watu wasipomkiri Mungu, pia haiwezekani kwao kufanywa kuwa kamili na Mungu, kwa kuwa hawafikii vigezo vya ukamilisho huu. Ikiwa hata humkiri Mungu, basi unawezaje kumjua Yeye? Unaweza kumfuatiliaje Yeye? Hutaweza kumshuhudia Yeye, pia, sembuse kuwa na imani ya kumridhisha Yeye. Kwa hivyo, kwa yeyote anayetaka kufanywa kuwa kamili, hatua ya kwanza lazima iwe kupitia kazi ya ushindi. Hili ndilo sharti la kwanza. Lakini kushinda na kufanya kuwa mtimilifu kote ni ili kuwafinyanga watu na kuwabadilisha, na kila mojawapo ni sehemu ya kazi ya kumsimamia mwanadamu. Hizi ndizo hatua mbili za kumfanya mtu kuwa mtu mkamilifu, na zote mbili ni za lazima. Ni kweli kwamba “kushindwa” hakusikiki vizuri sana, lakini kwa kweli, mchakato wa kumshinda mtu ni mchakato wa kumbadilisha. Punde tu unapokuwa umeshindwa, huenda tabia zako potovu zisiwe zimetupwa mbali kabisa, lakini utakuwa umezijua. Kupitia kazi ya ushindi, utakuwa umejua ubinadamu wako duni, pamoja na kiasi kikubwa cha uasi wako mwenyewe. Ingawa hutaweza kutupa mbali au kubadilisha mambo haya ndani ya kipindi kifupi cha kazi ya ushindi, utapata kuyajua, na hili litaweka msingi kwa ajili ya kufanywa kwako kuwa mtimilifu. Kwa hivyo, kuwashinda na kuwafanya kuwa watimilifu kote kunafanywa ili kuwabadilisha watu, kuwaondolea tabia zao potovu za kishetani ili waweze kujitoa kikamilifu kwa Mungu. Ni kwamba tu kushindwa ni hatua ya kwanza katika kubadilisha tabia za watu, na pia hatua ya kwanza katika watu kujitoa kikamilifu kwa Mungu, na iko chini kuliko hatua ya kufanywa kuwa watimilifu. Tabia ya maisha ya mtu aliyeshindwa inabadilika kwa kiasi kidogo sana kuliko ya mtu aliyefanywa kuwa mtimilifu. “Kushindwa” na “kufanywa kuwa mtimilifu” yanaitwa tofauti kwa sababu ni awamu tofauti za kazi na kwa sababu yanawawekea watu viwango tofauti vinavyohitajika; ushindi unawawekea watu viwango vya chini, huku ukamilisho ukiwawekea viwango vya juu. Waliofanywa kuwa watimilifu ni watu wenye haki, wametakaswa; wao ni mazao ya mwisho ya kazi ya kuwasimamia binadamu, au matokeo ya mwisho. Ingawa wao si watu wakamilifu, wao ni watu wanaotafuta kuishi maisha yenye maana. Walioshindwa, wakati huo huo, wanakiri tu kwa maneno uwepo wa Mungu, na wanakiri tu kwamba Mungu amepata mwili, kwamba Neno limeonekana katika mwili, na kwamba Mungu amekuja duniani kufanya kazi ya hukumu na kuadibu. Zaidi ya hayo, wanakiri kwamba hukumu ya Mungu na kuadibu Kwake, na kupiga Kwake na usafishaji Wake, yote ni yenye manufaa kwa mwanadamu. Wameanza tu kuwa na mfano fulani wa mwanadamu. Wana umaizi kiasi kuhusu maisha, lakini bado yanabaki kuwa yasiyo wazi kwao. Kwa maneno mengine, wanaanza tu kuwa na ubinadamu kiasi. Hayo ndiyo matokeo ya kushindwa. Watu wanapoanza kuitembea njia ya utimilifu, tabia zao za zamani zina uwezo wa kubadilika. Zaidi ya hayo, maisha yao yanaendelea kukua, na hatua kwa hatua wanaingia kwa kina zaidi katika ukweli. Wanaweza kuichukia dunia na wale wote wasiofuatilia ukweli. Hasa, hawajichukii wenyewe tu, bali zaidi ya hayo, wanajijua waziwazi. Wako radhi kuishi kwa ukweli, wanafanya kufuatilia ukweli kuwa lengo lao, na hawako radhi kuishi ndani ya mawazo ya akili zao wenyewe. Wanahisi chuki kwa kujihesabia haki, kiburi, na majivuno ya mwanadamu, wanazungumza kwa hisia kali ya adabu, wana utambuzi na hekima wanapokumbana na mambo, na ni waaminifu na watiifu kwa Mungu. Wakipitia tukio la kuadibu na hukumu, mbali na wao kutokuwa hasi au dhaifu, wao pia wanakuwa na shukrani kwa kuadibu na hukumu hii kutoka kwa Mungu, wakiamini kwamba hawawezi kuwa bila kuadibu kwa Mungu na hukumu Yake, kwamba vinawalinda. Hawafuatilii imani ya amani na furaha na ya kutafuta kula mikate mpaka washibe. Wala hawafuatilii starehe za kimwili za muda. Haya ndiyo ambayo wale waliofanywa kuwa watimilifu wanamiliki. Baada ya watu kushindwa, wanakiri kwamba kuna Mungu, lakini kukiri huko kunadhihirishwa ndani yao kwa njia chache. Kuonekana kwa Neno katika mwili kunamaanisha nini hasa? Kupata mwili kunamaanisha nini? Mungu mwenye mwili amefanya nini? Lengo na umuhimu wa kazi Yake ni nini? Baada ya kupitia kazi Zake nyingi sana, baada ya kupitia matendo Yake katika mwili, umepata nini? Ni baada tu ya kuelewa mambo haya yote ndipo utakuwa mtu aliyeshindwa. Ukisema tu kwamba unakiri kuna Mungu, lakini hutelekezi kile unachopaswa kutelekeza, na unashindwa kuacha starehe za kimwili wakati unapofika wa kuziacha, badala yake unaendelea kutamani faraja za kimwili kama ulivyofanya daima, na ikiwa huwezi kuachilia ubaguzi wowote dhidi ya akina ndugu, na hulipi gharama yoyote katika kutekeleza matendo mengi rahisi, basi hili linathibitisha kwamba bado hujashindwa. Katika hali hiyo, hata kama kuna mengi unayoelewa, yote yatakuwa ya bure. Walioshindwa ni watu ambao wamefikia mabadiliko kiasi ya awali na kuingia kwa awali. Kupitia hukumu ya Mungu na kuadibu Kwake kunawapa watu maarifa ya awali kumhusu Mungu, na ufahamu wa awali wa ukweli. Huenda ukawa huna uwezo wa kuingia kikamilifu katika uhalisi wa ukweli mwingi wa kina zaidi, na uliofafanuliwa zaidi, lakini unaweza kutia katika vitendo ukweli mwingi wa kimsingi, kama vile ule unaohusisha starehe zako za kimwili au hadhi yako binafsi katika maisha yako halisi. Yote haya, bila shaka, ni matokeo yanayofikiwa ndani ya watu wakati wa mchakato wa kushindwa. Mabadiliko katika tabia pia yanaweza kuonekana ndani ya walioshindwa; kwa mfano, jinsi wanavyovalia na kujitengeneza, na jinsi wanavyoishi—haya yote yanaweza kubadilika. Mtazamo wao juu ya imani katika Mungu unabadilika, wako wazi kuhusu malengo ya ufuatiliaji wao, na wana maazimio makuu zaidi. Wakati wa kazi ya ushindi, mabadiliko yanayolingana pia hutokea katika tabia yao ya maisha. Kuna mabadiliko, lakini ni ya juu juu, ya awali, na duni sana yakilinganishwa na mabadiliko katika tabia na malengo ya ufuatiliaji ya wale ambao wamefanywa kuwa watimilifu. Ikiwa, katika mchakato wa kushindwa, tabia ya mtu haibadiliki hata kidogo, na hapati ukweli wowote, basi mtu huyu ni takataka, na ni bure kabisa! Watu ambao hawajashindwa hawawezi kufanywa kuwa watimilifu! Ikiwa mtu anatafuta tu kushindwa, basi hawezi kufanywa kuwa kamili kabisa, hata kama tabia zake zinaonyesha mabadiliko fulani yanayolingana wakati wa kazi ya ushindi. Pia atapoteza ukweli wa awali alioupata. Kuna tofauti kubwa kati ya mabadiliko katika tabia ya wale walioshindwa na wale waliofanywa kuwa watimilifu. Lakini kushindwa ni hatua ya kwanza katika mabadiliko; ni msingi. Kutokuwepo kwa mabadiliko haya ya awali ni thibitisho kwamba kwa kweli mtu hamjui Mungu hata kidogo, kwa kuwa maarifa haya yanatokana na hukumu, na hukumu kama hiyo ni sehemu kuu ya kazi ya ushindi. Kwa hivyo, wote wanaofanywa kuwa watimilifu lazima kwanza washindwe; la sivyo, hakuna njia kwao kufanywa kuwa watimilifu.
Unasema kwamba unakiri kupata mwili kwa Mungu, na kwamba unakiri kuonekana kwa Neno katika mwili, lakini unafanya mambo fulani nyuma Yake, mambo ambayo yanakwenda kinyume na kile Anachotaka, na moyoni mwako humwogopi Yeye. Je, huku ni kumkiri Mungu? Unakiri kile Anachosema, lakini hutendi kile unachoweza, wala hufuati njia Yake. Je, huku ni kumkiri Mungu? Na ingawa unamkiri Yeye, unahifadhi moyo wa hadhari Kwake, kamwe si moyo wa hofu. Ikiwa umeona na kukiri kazi Yake na kujua kwamba mtu huyu ni Mungu, lakini unabaki vuguvugu na bila kubadilika kabisa, basi wewe ni aina ya mtu ambaye bado hajashindwa. Wale ambao wameshindwa lazima wafanye yote wawezayo, na ingawa hawawezi kuingia katika ukweli wa juu zaidi, na ukweli huu unawazidi uwezo, watu kama hao wako tayari mioyoni mwao kufikia hili. Ni kwa sababu kuna mipaka kwa kile wanachoweza kufahamu ndiyo maana kuna vizuizi na mipaka kwa kile wanachoweza kutenda. Angalau, hata hivyo, lazima wafanye yote wawezayo. Ikiwa unaweza kufikia hilo, haya ni matokeo ambayo yametimizwa kwa sababu ya kazi ya ushindi. Chukulia unasema, “Kwa kuwa Anaweza kunena maneno mengi sana ambayo mwanadamu hawezi, ikiwa Yeye si Mungu, ni nani ndiye Mungu?” Kuwa na ufahamu wa aina hii hakumaanishi kwamba unamkiri Mungu. Ikiwa unamkiri Mungu, lazima uonyeshe hilo kupitia matendo yako halisi. Ikiwa unaongoza kanisa, lakini hutendi haki, ikiwa unatamani sana pesa na utajiri, na kila mara unatia mfukoni fedha za kanisa kwa ajili yako mwenyewe, je, huku ni kukiri kwamba kuna Mungu? Mungu ni Mwenyezi, na Yeye anastahili kuogopwa. Unawezaje kukosa kuogopa ikiwa unakiri kweli kwamba kuna Mungu? Ikiwa una uwezo wa kufanya vitendo vya kudharauliwa kama hivyo, je, unamkiri Yeye kweli? Je, ni Mungu ambaye unamwamini? Kile unachokiamini ni mungu asiye dhahiri; ndiyo maana huogopi! Wale wanaomkiri na kumjua Mungu kweli wote wanamwogopa Yeye na hawathubutu kufanya chochote kinachompinga Yeye au ambacho kinakiuka dhamiri zao; wanaogopa hasa kufanya chochote wanachojua hakilingani na nia za Mungu. Hili pekee ndilo linaloweza kuchukuliwa kuwa kukiri uwepo wa Mungu. Unapaswa kufanya nini wazazi wako wanapojaribu kukuzuia kumwamini Mungu? Unapaswa kumpendaje Mungu wakati mume wako asiyeamini ni mwema kwako? Na unapaswa kumpendaje Mungu wakati akina ndugu wanakuchukia? Ukimkiri Yeye, basi katika mambo haya utatenda ipasavyo na kuishi kwa kudhihirisha uhalisi. Ukishindwa kuchukua hatua thabiti lakini unasema tu kwamba unakiri uwepo wa Mungu, basi wewe ni mzungumzaji tu! Unasema unamwamini Yeye na kumkiri Yeye, lakini unamkiri Yeye kwa njia gani? Unamwamini Yeye kwa njia gani? Je, unamwogopa Yeye moyoni mwako? Je, unamhofu Yeye? Je, una moyo wa upendo Kwake ndani mwako kabisa? Unapofadhaika na huna mtu wa kumtegemea, unahisi kupendeza kwa Mungu, lakini baadaye unasahau kabisa. Huko si kumpenda Mungu, wala si kumwamini Mungu! Hatimaye, Mungu anatamani mwanadamu afikie nini? Hali zote Nilizotaja, kama vile kuhisi kuvutiwa sana na umuhimu wako mwenyewe, kuhisi kwamba wewe ni mwepesi wa kuelewa mambo, kuwabana wengine, kuwadharau wengine, kuwahukumu watu kwa sura yao ya nje, kuwadhulumu watu wapole, kutamani pesa za kanisa, na kadhalika—ni wakati tu ambapo tabia hizi zote potovu za kishetani zimeondolewa kwako, kwa kiasi fulani, ndipo kushindwa kwako kutadhihirishwa.
Kazi ya ushindi inayofanywa kwenu ninyi watu ni yenye umuhimu wa kina kabisa: Kwa upande mmoja, madhumuni ya kazi hii ni kulifanya kundi la watu kuwa watimilifu, yaani, kuwafanya kuwa watimilifu, ili waweze kuwa kundi la washindi—kama kundi la kwanza la watu waliofanywa kuwa kamili, ikimaanisha malimbuko. Kwa upande mwingine, ni ili kuwaruhusu viumbe walioumbwa wafurahie upendo wa Mungu, wapokee wokovu mkubwa kabisa wa Mungu na neema Yake kamili iokoayo, kumruhusu mwanadamu afurahie si tu rehema na wema, bali muhimu zaidi kuadibu na hukumu. Tangu uumbaji wa dunia hadi sasa, yote ambayo Mungu amefanya katika kazi Yake ni upendo, bila chuki yoyote kwa mwanadamu. Hata kuadibu na hukumu ambavyo umeviona pia ni upendo, upendo wa kweli na halisi zaidi, upendo unaowaongoza watu kwenye njia sahihi ya maisha ya mwanadamu. Katika upande mwingine tena, ni ili kuwa na ushuhuda mbele ya Shetani. Na katika mwingine tena, ni ili kuweka msingi kwa ajili ya kueneza kazi ya injili ya baadaye. Kazi yote ambayo Amefanya ni kwa madhumuni ya kuwaongoza watu kwenye njia sahihi ya maisha ya mwanadamu, ili waweze kuishi maisha ya kawaida ya mwanadamu, kwa kuwa watu hawajui jinsi ya kuishi, na bila maelekezo haya, utaishi tu maisha matupu; maisha yako yatakuwa hayana thamani au maana, nawe hutakuwa na uwezo kabisa wa kuwa mtu wa kawaida. Huu ndio umuhimu wa kina kabisa wa kumshinda mwanadamu. Ninyi nyote ni dhuria ya Moabu; kazi ya ushindi inayofanywa kwenu ni wokovu wenu mkuu. Ninyi nyote mnaishi katika nchi ya dhambi na uasherati, nanyi nyote ni waasherati na wenye dhambi. Leo si kwamba tu mnaweza kumwona Mungu, bali lililo muhimu zaidi, mmepokea kuadibu na hukumu, mmepokea wokovu huu wa kina zaidi, yaani, mmepokea upendo mkuu zaidi wa Mungu. Yote ambayo Mungu anafanya ni upendo wa kweli kwenu. Hana nia mbaya. Ni kwa sababu ya dhambi zenu ndiyo maana Anawahukumu, ili muweze kujitafakari na kupokea wokovu huu mkubwa. Kazi hii yote inafanywa kwa madhumuni ya kumfanya mwanadamu kuwa kamili. Tangu mwanzo hadi mwisho, Mungu amekuwa akifanya yote awezayo ili kumwokoa mwanadamu, na Yeye hana nia kabisa ya kuwaangamiza kabisa watu Aliowaumba kwa mikono Yake Mwenyewe. Leo, Amekuja miongoni mwenu kufanya kazi; je, huu si wokovu hata zaidi? Kama Angewachukia, je, bado Angefanya kazi ya ukubwa kama huo ili kuwaongoza binafsi? Kwa nini Ateseke hivi? Mungu hawachukii wala hana nia zozote mbaya kwenu. Mnapaswa kujua kwamba upendo wa Mungu ni halisi kabisa. Ni kwa sababu tu watu ni waasi ndiyo maana inambidi awaokoe kupitia hukumu; la sivyo, bado haingewezekana kuwaokoa. Kwa sababu hamjui jinsi ya kuishi maisha yenu na hamfahamu jinsi ya kuishi, na kwa sababu mnaishi katika nchi hii ya uasherati na dhambi, na ninyi wenyewe ni mapepo waasherati na wachafu, Hawezi kuvumilia kuwaacha mzidi kuzama chini zaidi, Hawezi kuvumilia kuwaona mkiishi katika nchi hii chafu kama mnavyofanya sasa, mkikanyagwa na Shetani apendavyo, na Hawezi kuvumilia kuwaacha mtumbukie kuzimu. Anataka tu kulipata kundi hili la watu na kuwaokoa kikamilifu. Hili ndilo kusudi kuu la kufanya kazi ya ushindi kwenu—ni kwa ajili ya wokovu. Ikiwa huwezi kuona kwamba kila kitu kinachofanywa kwako ni upendo na wokovu, ukifikiri kwamba ni mbinu tu, njia ya kumtesa mwanadamu, na kitu kisichoaminika, basi ni afadhali urudi kwenye ulimwengu wako ili uteseke kwa maumivu na ugumu! Ikiwa uko radhi kufurahia, ndani ya mkondo huu, hukumu hii na hii neema kubwa iokoayo, baraka hizi zote ambazo haziwezi kupatikana popote katika ulimwengu wa binadamu, na upendo huu, basi kuwa mtiifu: Salia katika mkondo huu ili ukubali kazi ya ushindi ili uweze kufanywa kuwa mtimilifu. Leo, unateseka kwa maumivu kidogo na usafishaji kwa sababu ya hukumu ya Mungu, lakini kuna thamani na maana katika kuteseka kwa maumivu haya. Ingawa kwa mwanadamu, kuadibu kwa Mungu na hukumu Yake ni usafishaji, ufichuzi usio na huruma, na mambo yanayofanywa kwa madhumuni ya kumuadhibu kwa dhambi zake na kuuadhibu mwili wake, hakuna hata moja ya kazi hizi inayonuiwa kuuhukumu mwili wake na kuuangamiza. Ufichuzi mkali wa neno wote ni kwa madhumuni ya kukuongoza kwenye njia sahihi. Mmepitia binafsi kazi hizi nyingi sana na, ni wazi, hazijawaongoza kwenye njia mbaya! Yote ni kwa ajili ya kukufanya uishi kwa kudhihirisha ubinadamu wa kawaida, na yote yanaweza kufikiwa na ubinadamu wako wa kawaida. Kila hatua ya kazi ya Mungu inategemea mahitaji yako, kulingana na udhaifu wako, na kulingana na kimo chako halisi, na hakuna mzigo usiostahimilika mnaolazimishwa kubeba. Hili si wazi kwako leo, na unahisi kana kwamba Ninakuwa mkali kwako, na daima wewe unaamini kwamba sababu ya Mimi kukuadibu, kukuhukumu, na kukukemea kila siku ni kwa sababu Ninakuchukia. Lakini ingawa kile unachopokea ni kuadibu na hukumu, huu kwa kweli ni upendo kwako, na ndio ulinzi mkuu kabisa. Ikiwa huwezi kufahamu maana ya kina zaidi ya kazi hii, haitawezekana kwako kuendelea kuipitia. Unapaswa kupata faraja kutokana na wokovu huu. Usikatae kurudiwa na fahamu zako. Baada ya kufika hapa, umuhimu wa kazi ya ushindi unapaswa kuwa wazi kwako, na hupaswi tena kuwa na maoni kuihusu kwa njia moja au nyingine!