Sura ya 21

Mwanadamu huanguka katikati ya mwanga Wangu, na anasimama imara kwa sababu ya wokovu Wangu. Niletapo wokovu ulimwenguni kote, mwanadamu hujaribu kutafuta njia za kuingia miongoni mwa mtiririko wa urejesho Wangu, ilhali kuna watu wengi ambao huoshwa wasijulikane waliko na gharika hili la urejesho; kuna watu wengi ambao wamezama na kumezwa na mafuriko haya ya maji; na kuna watu wengi pia ambao husimama imara huku kukiwa na mafuriko, ambao hawajawahi kupoteza hisia zao za mwelekeo, na ambao basi wamefuata mafuriko mpaka sasa. Ninaenda hatua kwa hatua na mwanadamu, lakini yeye hajawahi kunitambua; yeye anajua tu nguo Ninazovaa kwa nje, na hajui utajiri uliofichika ndani Mwangu. Ingawa Mimi humruzuku mwanadamu na kumpa kila siku, hana uwezo wa kukubali kwa kweli, hana uwezo wa kupokea utajiri wote niliompa. Hakuna jambo lolote kuhusu upotovu wa mwanadamu ambalo huniepuka; Kwangu, ulimwengu wake wa ndani ni dhahiri kama mwezi unaong’aa juu ya maji. Mimi Simtendei mwanadamu katika njia iliyo hobelahobela wala kufanya mambo kwake kwa namna isiyo ya dhati; ni kwamba tu mwanadamu hawezi kujiwajibikia, na hivyo wanadamu wote daima wamepotoka, na hata wa leo bado hawana uwezo wa kujitoa wenyewe kutoka upotovu huo. Ole wao, maskini wanadamu! Kwa nini mwanadamu ananipenda lakini hawezi kufuata nia za Roho Wangu? Je, Mimi Sijajifichua kwa wanadamu kwa kweli? Wanadamu kwa kweli hawajapata kuuona uso Wangu kamwe? Je, inawezekana kwamba Nimeonyesha huruma kiasi kidogo sana kwa wanadamu? Enyi waasi wa wanadamu wote! Lazima waharibiwe chini ya miguu Yangu, ni lazima watokomee kabisa katikati ya kuadibu Kwangu, na lazima, siku ambayo mpango Wangu mkubwa utakamilika, watatupiliwa mbali kutoka kati ya wanadamu, ili wanadamu wote wazijue nyuso zao mbaya. Sababu ya mwanadamu kuona uso Wangu na kusikia sauti Yangu mara chache ni kwamba dunia nzima imejawa na machafuko sana, na kelele zake ni kubwa mno, na hivyo mwanadamu ni mvivu mno kutafuta uso Wangu na kujaribu kuelewa Moyo Wangu. Je, hii si sababu ya kupotoshwa kwa mwanadamu? Je, hii si ndiyo sababu mwanadamu yuko na mahitaji? Wanadamu wote daima wamekuwa katikati ya utoaji Wangu; kama isingekuwa hivyo, Nisingekuwa mwenye huruma, nani angenusurika mpaka leo? Utajiri Nilio nao hauna wa kulingana nao, na bado maafa yote yamo mikononi Mwangu—na ni nani awezaye kuepuka maafa wakati wowote apendapo? Je, maombi ya mwanadamu yanaweza kumruhusu afanye hivyo? Au machozi yaliyo moyoni mwa mwanadamu? Mwanadamu hajawahi kuniomba Mimi kwa kweli, na hivyo miongoni mwa wanadamu wote hakuna mwanadamu aliyewahi kuishi maisha yake yote kwenye mwanga wa ukweli, na watu wanaishi katikati ya mwanga unaooneka kwa kipindi pekee. Hii ndiyo imesababisha mahitaji ya mwanadamu leo.

Kila mwanadamu ana hamu kubwa, tayari kufanya jambo lolote kwa sababu Yangu ili apate kitu kutoka Kwangu, na hivyo, nikizingatia saikolojia ya mwanadamu, Mimi humpa ahadi za kuhamasisha upendo wa kweli ndani yake. Je, ni upendo wa kweli wa mwanadamu unaompa nguvu? Je, ni uaminifu wa mwanadamu Kwangu ndio umegusa Roho Wangu mbinguni? Mbingu haijawahi kuathiriwa na matendo ya mwanadamu hata kidogo, na iwapo kumtendea Kwangu mwanadamu kungetegemea matendo yake yote, basi wanadamu wote wangeishi katikati ya kuadibu Kwangu. Nimewaona watu wengi wakitiririkwa na machozi, na Nimewaona watu wengi wakitoa nyoyo zao ili wapate utajiri Wangu. Licha ya “uchaji Mungu” kama huu, Sijawahi kujitoa kwa mwanadamu kikamilifu kwa sababu ya hisia zake za ghafla, kwa sababu mwanadamu hajawahi kuwa radhi kujitoa kwa furaha mbele Yangu. Nimeng’oa barakoa za watu wote na kutupa barakoa hizo katika ziwa la moto, na kama matokeo, unaodaiwa kuwa uaminifu wa mwanadamu na maombi yake hayajawahi kuwa imara mbele Zangu. Mwanadamu ni kama wingu angani: Wakati upepo unavuma, anahofia uwezo mkubwa wa nguvu yake na hivyo huelea kwa haraka kufuata upepo, akiwa na woga sana kuwa ataangamizwa kwa sababu ya uasi wake. Je, huu sio uso mbaya wa mwanadamu? Je, hili silo linalodaiwa kuwa utiifu wa mwanadamu? Je, hii siyo “hisia ya kweli” na nia njema bandia ya mwanadamu? Watu wengi hukataa kushawishiwa na maneno yote yatokayo kwenye kinywa Changu, na wengi hawakubali tathmini Yangu, na hivyo maneno na matendo yao hufichua nia zao za kuasi. Nisemacho ni kinyume cha asili ya zamani ya mwanadamu? Je, si Nimepeana ufafanuzi wa kufaa kwa binadamu kulingana na “sheria za asili”? Mwanadamu hanitii kwa kweli; angenitafuta kwa kweli, haingenibidi kusema mengi. Mwanadamu ni takataka isiyo na maana, na ni lazima Nitumie kuadibu Kwangu kumlazimisha kuendelea mbele; Nisingefanya hivyo, —ingawa ahadi Ninazompa ni za kutosha starehe yake—moyo wake ungeweza kushawishiwa vipi? Mwanadamu ameishi na mapambano machungu kwa miaka mingi; inaweza kusemekana, siku zote ameishi kwa kukata tamaa. Matokeo yake ni kuwa ameachwa kama amekufa moyo, na amechoka kimawazo na kimwili, na hivyo hapokei utajiri Ninaompa kwa furaha. Hata leo, hakuna mwanadamu aliye na uwezo wa kukubali utamu wote wa roho kutoka Kwangu. Watu wanaweza tu kubaki maskini, na kusubiri siku ya mwisho.

Watu wengi wangependa kunipenda kwa kweli, lakini kwa sababu mioyo yao si yao wenyewe, hawawezi kujidhibiti wenyewe; watu wengi hunipenda kwa kweli katika majaribio Ninayotoa, lakini hawana uwezo wa kuelewa kwamba Mimi kwa kweli Nipo, na wananipenda tu katikati ya utupu; na si kwa sababu ya kuwepo Kwangu halisi; watu wengi, baada ya kuweka nyoyo zao mbele Zangu, hawazijali, na hivyo nyoyo zao zinanyakuliwa na Shetani wakati wowote anapopata nafasi, na baada yake huniacha; watu wengi hunipenda kwa dhati Ninapotoa maneno Yangu, lakini hawathamini maneno Yangu katika roho zao, badala yake wakiyatumia kwa kawaida kama mali ya umma na kuyatupa yalipotoka wakati wowote wanapotaka. Mwanadamu hunitafuta akiwa na maumivu, na hunitazamia akiwa na majaribu. Wakati kuna amani yeye hunifurahia, wakati wa hatari yeye hunikana, wakati ana kazi nyingi yeye hunisahau, na asipokuwa na kitu cha kufanya yeye hufanya vitu kwa namna isiyo ya dhati—lakini kamwe hakuna yeyote ambaye amenipenda katika maisha yake yote. Ningependa mwanadamu awe mwenye bidii mbele Zangu: Mimi Simuombi chochote, ila tu watu wote wanichukulie kwa umakini, kwamba, badala ya kunirairai, waniruhusu kurudisha uaminifu wa mwanadamu. Nuru Yangu, mwangaza na gharama ya juhudi Zangu huenea kwa watu wote, ilhali hivyo pia ukweli halisi wa kila tendo la mwanadamu huenea kwa watu wote, kama ufanyavyo wao kunidanganya. Ni kama kwamba viungo vya udanganyifu wa mwanadamu vimekuwa naye tangu tumboni mwa mamake, kama kwamba amekuwa na mbinu hizi maalum za kuhadaa tangu kuzaliwa kwake. Kuzidisha, hajawahi kufichua siri yake; hakuna mwanadamu aliyewahi kutambua chanzo cha ujuzi huu wa udanganyifu. Matokeo yake ni kuwa mwanadamu anaishi katika udanganyifu bila kujua, na ni kana kwamba yeye hujisamehe mwenyewe, kana kwamba ni mipango ya Mungu na sio yeye kunidanganya. Je, hiki sicho chanzo halisi cha mwanadamu kunidanganya? Je, huu sio mpango wake wa ujanja? Sijawahi kuchanganywa na ushawishi na hila za mwanadamu, kwa maana Mimi Nilishatambua kiini chake muda mrefu uliopita. Nani anayejua kiasi cha uchafu ulio katika damu yake, na kiasi gani cha sumu ya Shetani kimo ndani ya mafupa yake? Mwanadamu anapata uzoefu wa sumu hii kila uchao, hata anakosa busara ya kufahamu maafa ya Shetani na hivyo hana nia ya kutambua “sanaa ya uwepo wa afya.”

Wakati mwanadamu yuko mbali nami, na wakati ananijaribu, Mimi hujificha kutoka kwake kati ya mawingu. Na hivyo, hawezi kunipata hata kidogo, na huishi tu mikononi mwa waovu, akifanya yote watakayo. Mwanadamu anaponikaribia, Mimi hujitokeza kwake na sifichi uso Wangu kutoka kwake, na kwa wakati huu, mwanadamu huona hisia ya ukarimu usoni Mwangu. Yeye ghafla hupata fahamu na ingawa hatambui, ndani yake kunazaliwa upendo Kwangu. Katika moyo wake, yeye ghafla huhisi utamu usio na kifani, na hustaajabu jinsi gani hakuweza kutambua kuwepo Kwangu ulimwenguni. Hivyo basi mwanadamu ana hisia kubwa ya uzuri Wangu, na zaidi, ya thamani Yangu kubwa. Matokeo, yake ni kuwa yeye hatamani kamwe kuniacha tena, Ananiona kama mwanga wa maisha yake, na akiwa na woga sana kuwa Naweza kumwacha, hunikumbatia kwa nguvu. Mimi siguswi na bidii ya mwanadamu, lakini ni mwenye rehema kwake kwa sababu ya upendo wake. Kwa wakati huu, mwanadamu mara moja huishi katikati ya majaribio Yangu. Uso Wangu hutoweka kutoka moyo wake, na yeye mara moja huona kuwa maisha yake ni matupu na anafikiria kukimbia. Wakati huu, moyo wa mwanadamu huwekwa wazi. Yeye hanikumbatii kwa sababu ya tabia Yangu, lakini ananiomba Nimlinde kwa sababu ya upendo Wangu. Hata hivyo, upendo Wangu unapomgeukia mwanadamu, yeye mara moja hubadili mawazo yake; yeye hukiuka agano lake nami na hujiweka mbali na hukumu Yangu, asiwe na nia ya kutazamia uso Wangu wa rehema tena, na hivyo hubadilisha mtazamo wake Kwangu na husema kuwa Sijawahi kumwokoa mwanadamu. Je, upendo wa kweli unahusisha huruma pekee? Je, mwanadamu ananipenda tu akiishi chini ya mwanga Wangu unaong’aa? Yeye anaangalia ya jana lakini anaishi katika wakati huu—si hizi ni hali za mwanadamu? Je, kesho mtakuwa jinsi mlivyo bado? Ninachotaka ni mwanadamu awe na moyo unaonitamani kwa kina na sio moyo unaoniridhisha na vitu vya juu juu.

Machi 21, 1992

Iliyotangulia: Sura ya 20

Inayofuata: Sura ya 22

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp