Kupata Mwili Mara Mbili Kunakamilisha Umuhimu wa Kupata Mwili

Kila hatua ya kazi iliyofanywa na Mungu ina umuhimu wake mkubwa. Yesu alipokuja zamani, Alikuwa mwanaume, lakini Mungu anapokuja wakati huu Yeye ni mwanamke. Kutokana na hili, unaweza kuona kwamba Mungu aliwaumba mwanaume na mwanamke kwa ajili ya kazi Yake na Kwake hakuna tofauti ya jinsia. Roho Wake anapowasili, Anaweza kuchukua mwili wowote kwa matakwa Yake na mwili huo unaweza kumwakilisha Yeye. Uwe wa kiume au kike, unaweza kumwakilisha Mungu alimradi tu ni mwili Wake wa nyama. Kama Yesu angeonekana kama kike alipokuja, kwa maneno mengine, iwapo mtoto wa kike, sio wa kiume, angezaliwa kwa njia ya Roho Mtakatifu, hatua hiyo ya kazi ingekuwa imekamilika pia. Kama hali ingekuwa hivyo, basi hatua ya leo ya kazi ingelazimika kukamilishwa badala yake na mwanaume, lakini kazi ingekamilika pia. Kazi inayofanywa katika hatua hizi zote ni muhimu kwa kiwango sawa; hakuna hatua yoyote ya kazi inayojirudia au kupingana na nyingine. Wakati huo, Yesu alipokuwa akifanya kazi Yake aliitwa Mwana wa pekee, na “Mwana” inaashiria jinsia ya kiume. Basi kwa nini Mwana wa pekee halikutajwa katika hatua hii? Hii ni kwa sababu mahitaji ya kazi yamelazimisha badiliko la jinsia ambayo ni tofauti na ile ya Yesu. Kwa Mungu hakuna tofauti ya jinsia. Kazi Yake inafanywa kama Anavyotaka na katika kufanya kazi Yake hazuiliwi na kitu chochote kile, lakini hasa yupo huru. Hata hivyo, kila hatua ya kazi ina umuhimu wake mkubwa. Mungu alipata mwili mara mbili, na ni dhahiri kwamba kupata mwili Kwake katika siku za mwisho ni mara ya mwisho. Amekuja kufichua matendo Yake yote. Ikiwa katika hatua hii Hakupata mwili ili Yeye binafsi afanye kazi kwa ajili ya mwanadamu kushuhudia, mwanadamu milele angeshikilia fikra kwamba Mungu ni wa kuime tu, na si wa kike. Kabla ya hili, wanadamu wote waliamini kwamba Mungu angeweza kuwa tu mwanaume na kwamba mwanamke hawezi kuitwa Mungu, maana wanadamu wote walimchukulia mwanamume kuwa na mamlaka juu ya mwanamke. Waliamini kwamba hakuna mwanamke anayeweza kuchukua mamlaka, bali ni mwanamume tu. Aidha hata walisema kwamba mwanamume alikuwa ni mkuu wa mwanamke na kwamba mwanamke anapaswa kumtii mwanaume na asimshinde. Iliposemwa hapo nyuma kwamba mwanamume alikuwa mkuu wa mwanamke, ilielekezwa kwa Adamu na Hawa ambao walikuwa wamedanganywa na yule nyoka, na wala sio kwa mwanamume na mwanamke kama walivyoumbwa na Yehova hapo mwanzo. Bila shaka, mwanamke anapaswa kumtii na kumpenda mume wake, na mume anapaswa kujifunza kuilisha na kuiruzuku familia yake. Hizi ni sheria na kanuni zilizowekwa na Yehova ambazo kwazo wanadamu wanapaswa kuzifuata katika maisha yao ya hapa duniani. Yehova alimwambia mwanamke “Ashiki yako itakuwa kwa mume wako, na atatawala juu yako.” Alisema hivyo tu ili kwamba wanadamu (yaani, mwanamume na mwanamke) waweze kuishi maisha ya kawaida chini ya utawala wa Yehova, na tu ili kwamba maisha ya wanadamu yaweze kuwa na mfumo na yasipoteze mwelekeo. Kwa hivyo, Yehova alitengeneza kanuni zinazofaa ya namna ambavyo mwanamume na mwanamke wanavyopaswa kutenda, lakini hili lilihusu tu viumbe wote wanaoishi duniani na halikuhusiana na mwili wa Mungu wa nyama. Inawezekanaje Mungu awe sawa na viumbe Wake? Maneno Yake yalielekezwa tu kwa wanadamu wa viumbe Wake; Alianzishia mwanamume na mwanamke kanuni ili wanadamu waweze kuishi maisha ya kawaida. Hapo mwanzo, Yehova alipoumba wanadamu, Aliwaumba wanadamu wa aina mbili, mwanamume na mwanamke; na kwa hiyo, kuna mgawanyo wa kike na kiume katika miili Yake. Hakuamua juu ya kazi Yake kulingana na maneno aliyozungumza kwa Adamu na Hawa. Mara mbili Alipopata mwili kuliamuliwa kwa kuzingatia kabisa mawazo Yake alipowaumba wanadamu kwa mara ya kwanza, yaani, Alikamilisha kazi ya kupata Kwake mwili mara mbili, kwa msingi wa mwanamke na mwanamume kabla ya wao kupotoshwa. Ikiwa wanadamu wangechukua maneno yaliyozungumzwa na Yehova kwa Adamu na Hawa, ambao walikuwa wamedanganywa na yule nyoka, na kuyatumia katika kazi ya mwili wa Mungu, je, si Yesu pia angepaswa kumpenda mke Wake kama Alivyotakiwa? Je, kwa njia hii, Mungu bado ni Mungu? Na ikiwa ni hivyo, je, bado Angeweza kukamilisha kazi Yake? Ikiwa ni vibaya kwa mwili wa Mungu kuwa mwanamke, je, basi lisingekuwa kosa kubwa sana pia kwa Mungu kumuumba mwanamke? Ikiwa mwanadamu bado anaamini kwamba Mungu kupata mwili kama mwanamke ni vibaya, je, basi Yesu, ambaye hakuoa na hivyo hakuweza kumpenda mke Wake, angekuwa na makosa kama kupata mwili wa sasa? Kwa kuwa unatumia maneno yaliyozungumzwa na Yehova kwa Hawa ili kupima ukweli wa Mungu kupata mwili leo, basi unapaswa kutumia maneno ya Yehova kwa Adamu kumhukumu Bwana Yesu ambaye alipata mwili katika Enzi ya Neema. Je, hawa wawili sio sawa? Kwa kuwa unampima Bwana Yesu kulingana na mwanamume ambaye hakuwa amedanganywa na yule nyoka, basi hupaswi kuhukumu ukweli wa kupata mwili leo hii kulingana na mwanamke ambaye alikuwa amedanganywa na yule nyoka. Hili si haki! Ikiwa umefanya hukumu ya namna hiyo, inathibitisha kukosa urazini kwako. Yehova alipopata mwili mara mbili, jinsia ya mwili Wake ilikuwa inahusiana na mwanamume na mwanamke ambaye hakuwa amedanganywa na yule nyoka; Alipata mwili mara mbili kulingana na mwanamume na mwanamke ambaye hakuwa amedanganywa na yule nyoka. Usifikiri kwamba uanaume wa Yesu ulikuwa sawa na uanaume wa Adamu ambaye alidanganywa na yule nyoka. Hahusiani naye kabisa, na ni wanaume wawili wa asili tofauti. Hakika haiwezi kuwa kwamba uanaume wa Yesu unathibitisha Yeye ni mkuu wa wanawake wote lakini sio mkuu wa wanaume wote? Je, Yeye si Mfalme wa Wayahudi wote (ikiwa ni pamoja na wanaume na wanawake)? Yeye ni Mungu Mwenyewe, sio tu mkuu wa mwanamke bali mkuu wa mwanamume pia. Yeye ni Bwana wa viumbe vyote, na mkuu wa viumbe vyote. Unawezaje kuamua uanaume wa Yesu kuwa ishara ya mkuu wa mwanamke? Huku si kukufuru? Yesu ni mwanamume ambaye hajapotoshwa. Yeye ni Mungu; Yeye ni Kristo; Yeye ni Bwana. Anawezaje kuwa mwanamume kama Adamu ambaye alipotoshwa? Yesu ni mwili uliovaliwa na Roho wa Mungu aliye mtakatifu sana. Unawezaje kusema kuwa Yeye ni Mungu aliye na uanaume wa Adamu? Kama ni hivyo, kazi yote ya Mungu haingekuwa si sahihi? Je, Yehova angeweza kuuweka ndani ya Yesu uanaume wa Adamu ambaye alidanganywa na yule nyoka? Je, si kupata mwili kwa wakati huu ni tukio jingine la kazi ya Mungu mwenye mwili ambaye ni tofauti kijinsia na Yesu lakini aliye kama Yeye katika asili? Bado unathubutu kusema kwamba Mungu mwenye mwili hawezi kuwa mwanamke kwa kuwa mwanamke ndiye aliyedanganywa kwanza na yule nyoka? Bado unathubutu kusema kwamba, kwa kuwa mwanamke ndiye mwenye najisi sana na ni chanzo cha upotovu wa wanadamu, Mungu hawezi kabisa kupata mwili kama mwanamke? Bado unathubutu kuendelea kusema kwamba “mwanamke siku zote atamtii mwanamume na hawezi kamwe kudhihirisha au kumwakilisha Mungu moja kwa moja”? Hukuelewa hapo nyuma; lakini sasa bado unaweza kuendelea kukufuru kazi ya Mungu, hususan mwili wa nyama wa Mungu? Kama huwezi kuona hili kwa uwazi kabisa, ni vizuri zaidi ukawa makini na ulimi wako, la sivyo upumbavu na ujinga wako ufichuliwe na ubaya wako uwekwe wazi. Usidhani kwamba unaelewa kila kitu. Nakueleza kwamba yote uliyokwishayaona na kuyapitia hayakutoshelezi wewe kuelewa hata sehemu ndogo kabisa ya mpango Wangu wa usimamizi. Hivyo kwa nini basi unakuwa mwenye kiburi sana? Talanta ndogo hiyo uliyonayo na maarifa kidogo hayo uliyonayo hayatoshelezi kutumika na Yesu hata katika sekunde moja ya kazi Yake! Je, una uzoefu kiasi gani hasa? Yale uliyoyaona na yote uliyoyasikia katika maisha yako yote na yale uliyoyafikiria ni kidogo kuliko kazi Ninayoifanya kwa muda mfupi sana! Ni bora usichambue na kutafuta kosa. Haijalishi una kiburi kiasi gani, wewe bado ni kuimbe tu mdogo kuliko mchwa! Vyote vilivyomo katika tumbo lako ni vichache zaidi ya vile vilivyomo katika tumbo la mchwa! Usifikiri kwamba kwa kuwa tu umepata uzoefu na ukubwa kiasi, unaweza kuashiria kiburi na kuzungumza kwa maringo. Je, uzoefu wako na ukubwa wako sio matokeo ya maneno Niliyoyazungumza? Je, unaamini kwamba yalikuwa mbadala wa kufanya kwako kazi kwa bidii na kutokwa jasho? Siku hii, unaona kuwa nimepata mwili, na kwa sababu ya hili pekee unajawa na dhana nyingi hizo, na kutoka kwalo unakuwa na fikira nyingi isiyohesabika. Isingekuwa kwa kupata mwili Kwangu, bila kujali talanta ulizo nazo ni za ajabu kiasi gani, usingekuwa na dhana hizi nyingi; si ni kutoka hapa ndipo fikira zako zinatoka hapa? Kama si kupata mwili kwa Yesu mara hiyo ya kwanza, je, hata ungejua kuhusu kupata mwili? Je, si kwa sababu ya maarifa yako kutoka kwa kupata mwili mara ya kwanza ndio una ufidhuli kuthubutu kuhukumu kupata mwili kwa mara ya pili? Kwa nini ukuchunguze badala ya kuwa mfuasi mtiifu? Wakati umeingia katika mkondo huu na kuja mbele ya Mungu mwenye mwili, je, Angekuruhusu kuchunguza hili? Ni sawa kwako kuchunguza historia ya familia yako, lakini ukijaribu kuchunguza “historia ya familia” ya Mungu, inawezekanaje Mungu wa leo akuruhusu kufanya uchunguzi kama huo? Je, wewe si kipofu? Je, hujiletei dharau kwako mwenyewe?

Ikiwa tu kazi ya Yesu ingefanywa bila kukamilishwa na kazi katika hatua hii ya siku za mwisho, basi mwanadamu milele angeshikilia fikira kwamba Yesu tu ndiye Mwana wa pekee wa Mungu, yaani, Mungu ana mwana mmoja tu, na kwamba yeyote anayekuja baada yake akiwa na jina jingine hawezi kuwa Mwana pekee wa Mungu, sembuse Mungu Mwenyewe. Mwanadamu ana fikira kwamba yeyote ambaye anajitoa sadaka kwa ajili ya dhambi au yule ambaye anachukua mamlaka kwa niaba ya Mungu na anayewakomboa wanadamu wote ni Mwana wa Mungu wa pekee. Kuna baadhi ambao wanaamini kwamba alimradi Yeye anayekuja ni mwanamume, Anaweza kuchukuliwa kuwa ni Mwana wa Mungu wa pekee na mwakilishi wa Mungu, na hata kuna wale wanaosema kwamba Yesu ni Mwana wa Yehova, Mwana Wake wa pekee. Je, hii kweli siyo tu fikira iliyopita kiasi ya mwanadamu? Ikiwa hatua hii ya kazi haingefanywa katika enzi ya mwisho, basi wanadamu wote wangekuwa gizani sana kumhusu Mungu. Ingekuwa ni hivyo, mwanamume angejidhania kuwa ni wa juu sana kuliko mwanamke, na wanawake hawangeweza kamwe kuinua vichwa vyao juu na hivyo, hakuna mwanamke angeweza kuokolewa. Watu siku zote wanaamini kwamba Mungu ni mwanamume, na aidha kwamba siku zote Amemchukia mwanamke na asingempa wokovu. Ingekuwa ni hivyo, isingekuwa ukweli kwamba wanawake wote walioumbwa na Yehova na pia ambao wamepotoshwa, wasingeweza kuwa na fursa ya kuokolewa? Je, basi isingekuwa bure kwa Yehova kumuumba mwanamke, yaani, kumuumba Hawa? Na je, mwanamke asingeangamia milele? Kwa hiyo, hatua ya kazi katika siku za mwisho inafanywa ili kuwaokoa wanadamu wote, sio mwanamke tu Ikiwa kunaye anayefikiria kwamba ikiwa Mungu angepata mwili kama kike, ingekuwa kwa ajili ya kumwokoa mwanamke pekee, basi mtu huyo bila shaka angekuwa mpumbavu!

Kazi inayofanywa kwa sasa imesukuma mbele kazi ya Enzi ya Neema; yaani, kazi katika mpango mzima wa usimamizi wa miaka elfu sita imesonga mbele. Ingawa Enzi ya Neema imeisha, kazi ya Mungu imeendelea mbele. Kwa nini Ninasema mara kwa mara kwamba hatua hii ya kazi inajengwa juu ya Enzi ya Neema na Enzi ya Sheria? Hii ina maana kwamba kazi ya siku hii ni mwendelezo wa kazi iliyofanyika katika Enzi ya Neema na maendeleo ya kazi iliyofanyika katika Enzi ya Sheria. Hatua hizi tatu zinaingiliana kwa karibu na kuunganika moja kwa inayofuata kwa karibu. Kwa nini pia Ninasema kwamba hatua hii ya kazi inajengwa juu ya ile iliyofanywa na Yesu? Tuseme kwamba hatua hii haingejengwa juu ya kazi iliyofanywa na Yesu, ingebidi kusulubiwa kwingine kufanyike katika hatua hii, na kazi ya ukombozi ya hatua iliyopita ingelazimika kufanywa upya tena. Hii isingekuwa na maana yoyote. Kwa hiyo, sio kwamba kazi imekamilika kabisa, bali ni kwamba enzi imesonga mbele, na kiwango cha kazi kimewekwa juu kabisa kuliko kilivyokuwa kabla. Inaweza kusemwa kwamba hatua hii ya kazi imejengwa juu ya msingi wa Enzi ya Sheria na kwenye mwamba wa kazi ya Yesu. Kazi hii inajengwa hatua kwa hatua, na hatua hii sio mwanzo mpya. Ni muungano tu wa hatua tatu za kazi ndio unaweza kuchukuliwa kuwa mpango wa usimamizi wa miaka elfu sita. Kazi ya hatua hii inafanywa kwa msingi wa kazi ya Enzi ya Neema. Ikiwa hatua hizi mbili za kazi hazikuhusiana, kwa nini basi kusulubiwa hakurudiwi katika hatua hii? Kwa nini Sibebi dhambi za mwanadamu, lakini badala yake Naja kumhukumu na kumwadibu mwanadamu moja kwa moja? Ikiwa kazi Yangu ya kumhukumu na kumwadibu mwanadamu na kuja Kwangu saa hii si kwa njia ya Roho Mtakatifu na hakukufuata kusulubiwa, basi Nisingekuwa na sifa zinazostahili kumhukumu na kumwadibu mwanadamu. Kazi katika hatua inajenga kabisa juu ya kazi katika hatua iliyotangulia. Hiyo ndiyo maana ni kazi kama hii tu ndiyo inaweza kumleta mwanadamu katika wokovu hatua kwa hatua. Yesu pamoja na Mimi tunatoka kwa Roho Mmoja. Ingawa miili Yetu haina uhusiano, Roho Zetu ni moja; ingawa kile Tunachofanya na kazi Tulizo nazo hazifanani, kwa asili Tunafanana; Miili Yetu ina maumbo tofauti, lakini hii ni kwa sababu ya mabadiliko ya enzi na mahitaji tofauti ya kazi Yetu; huduma Zetu hazifanani, hivyo kazi Tunayoileta na tabia Tunayoifichua kwa mwanadamu pia ni tofauti. Ndiyo maana kile ambacho mwanadamu anakiona na kukielewa leo hii si kama kile cha wakati uliopita; ni hivyo kwa sababu ya mabadiliko ya enzi. Ingawa jinsia na maumbo ya miili Yao ni tofauti, na kwamba hawakuzaliwa katika familia moja, sembuse katika kipindi kimoja, hata hivyo Roho Zao ni moja. Ingawa miili Yao haina uhusiano wa damu au kimwili kwa namna yoyote ile, haipingiki kwamba Wao ni Mungu kupata mwili katika vipindi viwili tofauti vya nyakati. Ni ukweli usiopingika kwamba Wao ni miili ya nyama ya Mungu, ingawa hawatoki katika ukoo mmoja na hawatumii lugha moja ya binadamu (mmoja alikuwa mwanamume aliyezungumza lugha ya Wayahudi na mwingine ni mwanamke anayezungumza Kichina pekee). Ni kwa sababu hizi ndiyo Wameishi katika nchi tofauti kufanya kazi ambayo inampasa kila mmoja kufanya, na katika nyakati tofauti vilevile. Licha ya ukweli kwamba Wao ni Roho moja, wakiwa na asili inayofanana, hakuna mfanano wa wazi kabisa kati ya ngozi za nje za miili Yao. Wanashiriki tu ubinadamu sawa, lakini sura ya nje ya miili Yao na kuzaliwa Kwao hakufanani. Mambo haya hayana athari katika kazi Zao au maarifa aliyonayo mwanadamu juu Yao, maana, kimsingi, Wao ni Roho moja na hakuna anayeweza kuwatenganisha. Ingawa Hawana uhusiano wa damu, nafsi Zao zote zinaongoza Roho Zao, ambazo zinawapa kazi tofauti katika nyakati tofauti, na miili Yao kwa ukoo tofauti. Roho wa Yehova si baba wa Roho wa Yesu na Roho wa Yesu si mwana wa Roho wa Yehova: Ni Roho moja. Vile vile Kama vile Mungu mwenye mwili wa leo na Yesu. Ingawa Hawahusiani kwa damu, ni Wamoja; hii ni kwa sababu Roho Zao ni moja. Mungu anaweza kufanya kazi ya rehema na wema, vilevile na ile kazi ya hukumu ya haki na kumwadibu mwanadamu, na ile ya kuleta laana kwa mwanadamu; na hatimaye, Anaweza kufanya kazi ya kuuharibu ulimwengu na kuwaadhibu waovu. Je, hafanyi haya yote Mwenyewe? Je, hii si kudura ya Mungu? Aliweza kutangaza sheria kwa ajili ya mwanadamu na kumpa amri, na aliweza pia kuwaongoza Waisraeli wa awali katika kuishi maisha yao duniani na kuwaongoza kujenga hekalu na madhabahu, Akiwatawala Waisraeli wote. Kwa kutegemea mamlaka Yake, Aliishi pamoja na Waisraeli duniani kwa miaka elfu mbili. Waisraeli hawakuthubutu kumwasi; wote walimheshimu Yehova na walifuata amri Zake. Hii ilikuwa Kazi iliyofanywa kwa kutegemea mamlaka Yake na kudura Yake. Kisha, katika Enzi ya Neema, Yesu alikuja kuwakomboa wanadamu wote walioanguka (sio Waisraeli pekee). Alionyesha rehema na wema kwa mwanadamu. Yesu ambaye mwanadamu alimwona katika Enzi ya Neema Alikuwa amejazwa na wema na siku zote Alikuwa mwenye upendo kwa mwanadamu, maana Alikuwa amekuja kuwakomboa wanadamu kutoka dhambini. Aliweza kuwasamehe wanadamu dhambi zao hadi pale ambapo kusulubiwa Kwake kuliwakomboa wanadamu kutoka dhambini kabisa. Wakati huo, Mungu alionekana kwa mwanadamu kwa rehema na wema; yaani, Alijitoa sadaka kwa ajili ya mwanadamu na Alisulubiwa kwa ajili ya dhambi za mwanadamu ili kwamba ziweze kusamehewa milele. Alikuwa mwenye rehema, mwenye huruma, mwenye upendo na mstahimilivu. Na wale wote waliomfuata Yesu katika Enzi ya Neema nao pia walitafuta kuwa wastahimilivu na wenye upendo katika mambo yote. Walistahimili mateso kwa muda mrefu, na hawakuwahi kulipiza kisasi hata walipopigwa, kulaaniwa au kupigwa mawe. Lakini haya hayawezi kuwa hivyo tena katika hatua ya mwisho. Vivyo hivyo, hata ingawa Roho Zao zilikuwa moja, kazi ya Yesu na Yehova hazikufanana kabisa. Kazi ya Yehova haikuwa kwa ajili ya kukamilisha enzi bali kuiongoza, kukaribisha maisha ya wanadamu duniani. Hata hivyo, kazi sasa ni kuwashinda wale walio katika mataifa yasiyo ya Wayahudi na ambao wamepotoshwa sana, sio tu watu wateule wa Mungu nchini China, bali ulimwengu mzima na wanadamu wote. Inaweza kuonekana kwako kwamba kazi hii inafanywa Uchina pekee, lakini kwa kweli imekwishaanza kusambaa katika nchi za ughaibuni. Ni kwa nini wageni mara kwa mara wanatafuta njia ya kweli? Hiyo ni kwa sababu Roho tayari amekwishaanza kazi, na maneno yanayonenwa sasa yanaelekezwa kwa watu ulimwenguni kote. Na hili, nusu ya kazi tayari inafanywa. Kutoka kuumbwa kwa dunia hadi sasa, Roho wa Mungu ameendeleza hii kazi kubwa, na aidha Amefanya kazi tofauti katika enzi tofauti, na katika mataifa tofauti. Watu wa kila enzi wanaiona tabia Yake tofauti, ambayo kwa asili inafichuliwa kupitia kazi tofauti Anazozifanya. Yeye ni Mungu, aliye mwingi wa rehema na wema; Yeye ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mwanadamu na mchungaji wa mwanadamu; lakini pia Yeye ni hukumu, kuadibu, na laana kwa mwanadamu. Angeweza kumwongoza mwanadamu kuishi duniani kwa miaka elfu mbili na pia Angeweza kuwaokoa wanadamu waliopotoka kutoka dhambi. Leo, pia Anaweza kuwashinda wanadamu ambao hawamjui na kuwafanya wawe chini ya miliki Yake, ili kwamba wote wajinyenyekeze kwake kikamilifu. Mwishowe, Atachoma yote ambayo si safi na ambayo ni dhalimu ndani ya wanadamu katika ulimwengu mzima, ili kuwaonyesha kwamba Yeye si Mungu wa Rehema, na upendo tu, si Mungu wa hekima, na maajabu tu, si Mungu mtakatifu tu, bali, hata zaidi ni Mungu anayemhukumu mwanadamu. Kwa waovu miongoni mwa wanadamu, Yeye ni mwenye kuchoma, kuhukumu na kuadhibu; kwa wale ambao wanapaswa kukamilishwa, Yeye ni mateso, usafishaji, na majaribu, na vilevile faraja, ruzuku, utoaji wa maneno, kushughulika na kupogoa. Na kwa wale ambao wanaondolewa, Yeye ni adhabu na vilevile malipo. Niambie, je, Mungu si mwenye enzi? Anaweza kufanya kazi yoyote na yote, sio tu kusulubiwa kama ulivyokuwa ukifikiri. Unamfikiria Mungu kuwa ni wa chini sana! Je, unaamini kwamba chote Anachoweza kufanya ni kukomboa wanadamu wote kupitia kusulubiwa kwako pekee? Na baada ya hilo, utamfuata mbinguni kula tunda kutoka mti wa uzima na kunywa kutoka mto wa uzima? … Je, inaweza kuwa rahisi hivyo? Niambie, umekamilisha nini? Je, una uzima wa Yesu? Ni kweli ulikombolewa naye, lakini kusulubiwa kulikuwa ni kazi ya Yesu Mwenyewe. Ni wajibu gani umeukamilisha kama mwanadamu? Una uchaji Mungu wa nje pekee lakini huielewi njia Yake. Hivyo ndivyo unavyomdhihirisha? Ikiwa hujapata maisha ya Mungu au kuona tabia Yake yote ya haki, basi huwezi kudai kuwa mtu aliye na uzima, na hustahili kupitia katika lango la ufalme wa mbinguni.

Mungu si Roho pekee, Anaweza pia kuwa mwili. Aidha, Yeye ni mwili wa utukufu. Yesu, ingawa hamjamwona, alishuhudiwa na Waisraeli, yaani, Wayahudi wa wakati huo. Mwanzoni alikuwa mwili wa nyama, lakini baada ya kusulubiwa, Aligeuka mwili wa utukufu. Yeye ni Roho anayezunguka mambo yote na Anaweza kufanya kazi katika kila mahali. Anaweza kuwa Yehova, au Yesu au Masihi; hatimaye, Anaweza pia kuwa Mwenyezi Mungu. Yeye ni haki, hukumu, na kuadibu; Yeye ni laana na ghadhabu, lakini pia Yeye ni rehema na wema. Kazi zote ambazo Amezifanya zinaweza kumwakilisha. Unasema Yeye ni Mungu ni wa aina gani? Huwezi kuelezea kabisa. Iwapo huwezi kweli kueleza, hufai kufanya mahitimisho kumhusu Mungu. Usihitimishe kwamba Mungu milele ni Mungu wa rehema na wema, kwa sababu tu Yeye alifanya kazi ya ukombozi katika hatua moja. Je, unaweza kuwa na uhakika kwamba Yeye ni Mungu wa rehema na upendo pekee? Ikiwa Yeye ni Mungu tu wa rehema na mwenye upendo, kwa nini Ataikomesha enzi katika siku za mwisho? Kutokana na fikira na mawazo ya watu Mungu anastahili kuwa mwenye rehema na upendo hadi katika enzi ya mwisho, ili kwamba kila mmoja wa wanadamu aweze kuokolewa. Lakini kwa nini, katika enzi za mwisho, ndipo Atatuma chini majanga makubwa kama vile mitetemeko ya ardhi, tauni na njaa ili kuwaangamiza wanadamu waovu, wanaomchukulia Mungu kama adui? Kwa nini anamruhusu mwanadamu kuteseka majanga haya? Hakuna yeyote kati wenu anayethubutu kusema Yeye ni Mungu wa aina gani, na hakuna anayeweza kuelezea. Je, unaweza kuwa na uhakika kwamba Yeye ni Roho? Je, unathubutu kusema kuwa Yeye ni mwili wa Yesu pekee? Na unathubutu kusema kuwa Yeye ni Mungu ambaye milele atasulubiwa kwa ajili ya mwanadamu?

Iliyotangulia: Fumbo la Kupata Mwili (4)

Inayofuata: Je, Utatu Upo?

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp