Kazi ya Kueneza Injili Ni Kazi ya Kuokoa Binadamu Pia
Watu wote wanahitaji kuelewa kusudio la kazi Yangu duniani, yaani, lengo la mwisho la kazi Yangu na ni kiwango gani Ninapaswa kufikia katika kazi hii kabla ya kukamilika. Kama, baada ya kutembea na Mimi hadi leo, watu hawaelewi kazi Yangu inahusu nini, basi hawajakuwa wakitembea na Mimi bure? Watu wanaonifuata Mimi wanafaa kujua mapenzi Yangu. Nimekuwa nikifanya kazi ulimwenguni kwa maelfu ya miaka, na hadi leo ningali nafanya kazi Yangu vivyo hivyo sasa. Ingawa kunavyo vipengele vingi hasa vilivyojumuishwa katika kazi Yangu, madhumuni ya kazi hii bado hayajabadilika; kama vile, kwa mfano, ingawa Nimejawa na hukumu na kuadibu kwa mwanadamu, Ninachofanya bado ni kwa ajili ya kumwokoa, na kwa ajili ya kueneza vizuri zaidi injili Yangu na kupanua zaidi kazi Yangu miongoni mwa mataifa, mara tu mwanadamu amekamilika. Kwa hiyo leo, katika wakati ambapo watu wengi tayari wametamauka pakubwa, Naendelea na kazi Yangu, Nikiendeleza kazi ambayo lazima Nifanye ili kuhukumu na kuadibu binadamu. Licha ya ukweli kwamba binadamu amechoshwa na kile Ninachosema na licha ya ukweli kwamba hana tamanio la kujali kuhusu kazi Yangu, Ningali natekeleza wajibu Wangu kwa sababu kusudio la kazi Yangu halijabadilika na mpango Wangu wa asili hautabadilika. Kusudi la hukumu Yangu ni kummwezesha binadamu anitii Mimi kwa njia bora zaidi, na kusudi ka kuadibu Kwangu ni kumwezesha binadamu afikie mabadiliko vema zaidi. Ingawa kila kitu Ninachofanya ni kwa ajili ya usimamizi Wangu, Sijawahi kufanya kazi yoyote ambayo si ya manufaa kwa mwanadamu, kwa maana Ninataka kufanya mataifa yote nje ya Israeli yawe na utii kama tu Waisraeli, kuwafanya wawe binadamu na kuwabadilisha kuwa binadamu halisi, ili Niwe na mahali pa usalama katika nchi zilizo nje ya Israeli. Huu ndio usimamizi Wangu; ndiyo kazi Yangu ninayotimiza katika nchi za Mataifa. Hata sasa, watu wengi bado hawauelewi usimamizi Wangu kwa sababu hawajali kuhusu mambo kama hayo, na badala yake wanafikiria tu kuhusu mustakabali na hatima zao. Haijalishi kile Ninachosema, watu hawajali kazi Yangu, badala yake wanalenga tu hatima zao za baadaye. Mambo yakiendelea kwa namna hii, kazi Yangu itaeneaje? Injili Yangu itahubiriwaje kotekote ulimwenguni? Mnapaswa kujua kwamba kazi Yangu itakapoenea, Nitawatawanya, Nitawaadhibu kama vile tu Yehova alivyoyaadhibu makabila ya Israeli. Haya yote yatafanywa ili kwamba injili Yangu iweze kuenea ulimwenguni kote, ili kwamba kazi Yangu iweze kuenea katika Mataifa, na hivyo jina Langu litukuzwe kama kuu na watu wazima na watoto kwa pamoja na jina Langu takatifu litasifiwa sana katika vinywa vya watu kutoka makabila na mataifa yote. Katika enzi hii ya mwisho, acha jina Langu litatukuzwa kama kuu miongoni mwa Mataifa, acha matendo Yangu yaonekane na watu wa mataifa, acha waniite Mwenyezi kwa sababu ya matendo Yangu, na maneno Yangu yatimie hivi karibuni. Nitawafanya watu wote wajue kwamba Mimi siye tu Mungu wa Waisraeli, lakini pia Mungu wa Mataifa yote, hata yale mataifa ambayo Nimeyalaani. Nitawafanya watu wote waone kwamba Mimi ndimi Mungu wa viumbe vyote. Hii ndiyo kazi Yangu kuu zaidi, ndilo kusudi la mpango wa kazi Yangu katika siku za mwisho, na kazi ya pekee ambayo Natamani kutimiza katika siku za mwisho.
Kazi ambayo Nimekuwa nikisimamia kwa maelfu ya miaka inafichuliwa kabisa tu kwa binadamu katika siku za mwisho. Ni sasa tu ndipo Nimelifumbua fumbo kamili la usimamizi Wangu kwa mwanadamu. Binadamu anajua kusudio la kazi Yangu na zaidi ya yote anapata uelewa wa mafumbo Yangu yote. Na Nimemwambia binadamu kila kitu kuhusu hatima ambayo amekuwa akijali kuhusu. Tayari Nimemfichulia binadamu mafumbo yote yaliyofichwa kwa zaidi ya miaka 5,900. Yehova ni nani? Masiha ni nani? Yesu ni nani? Mnafaa kuyajua haya yote. Mabadiliko makubwa ya kazi Yangu yamo katika majina haya. Je, mmeelewa haya? Jina Langu takatifu linafaa kutangazwa vipi? Jina Langu linafaa kuenezwaje katika taifa lolote ambalo limeniita kwa jina Langu lolote? Kazi Yangu tayari imeanza kupanuka, na Nitaeneza ukamilifu wake katika mataifa yote. Kwa sababu kazi Yangu imetekelezwa ndani yenu, Nitawapiga kama vile Yehova alivyowapiga wale wachungaji wa nyumba ya Daudi kule Israeli, na kuwasababisha kutawanyika miongoni mwa mataifa yote. Kwani katika siku za mwisho, Nitapondaponda mataifa yote kuwa vipande vidogo vidogo na kusababisha watu wao kuenezwa upya. Nitakaporudi tena, mataifa yatakuwa tayari yamegawanywa kwa mipaka iliyowekwa na mwako wa moto Wangu utakaokuwa ukichoma. Katika wakati huo, Nitajionyesha upya kwa binadamu kama jua linalochoma, Nikijionyesha kwao hadharani kwa taswira ya yule Aliye Mtakatifu ambaye hawajawahi kumwona, Nikitembea miongoni mwa mataifa yote, kama vile tu Mimi, Yehova, Nilivyotembea miongoni mwa makabila ya Wayahudi. Kuanzia hapo kuendelea, Nitawaongoza watu huku wakiishi ulimwenguni. Hakika watauona utukufu Wangu hapo na hakika wataona pia nguzo ya wingu hewani ili uwaongoze, kwani Nitaonekana katika sehemu takatifu. Binadamu ataiona siku Yangu ya haki na pia maonyesho Yangu ya utukufu. Hilo litafanyika Nitakapoutawala ulimwengu mzima na kuwaleta wana wengi katika utukufu. Kila pahali duniani, watu watainama, nalo hema Langu takatifu litaundwa miongoni mwao juu ya mwamba wa kazi ambayo Natekeleza sasa. Watu watanihudumia pia hekaluni. Madhabahu, yaliyojaa mambo machafu na ya kuchukiza, Nitayavunjavunja vipandevipande na Nitajenga upya mengine. Madhabahu matakatifu yatarundikwa wanakondoo na ndama waliozaliwa karibuni. Nitaangusha hekalu lililopo leo na kujenga jingine upya. Hekalu lililopo sasa na lililojaa watu wenye chuki litaporomoka na lile Nitakalojenga litajaa watumishi watiifu Kwangu. Kwa mara nyingine watasimama na kunihudumia Mimi kwa utukufu wa hekalu Langu. Kwa hakika mtaiona siku ambayo Nitapokea utukufu mkuu na hakika mtaiona siku ambayo Nitaliangusha hekalu na kujenga lingine upya. Pia, hakika mtaona siku ya kuletwa kwa hema Langu takatifu hapa ulimwenguni mwa binadamu. Huku Nikilibomoa hekalu, ndivyo Nitakavyoleta hema Langu takatifu hapa ulimwenguni mwa binadamu; itakuwa kama vile tu ambavyo watu wanavyoniona Nikishuka. Baada ya kuangamiza mataifa yote, Nitayakusanya pamoja upya, Nikilijenga hekalu Langu na kuandaa madhabahu Yangu, ili wote waweze kutoa kafara zao Kwangu, kunihudumia Mimi hapo, na kujitolea kwa uaminifu katika kazi Yangu kwenye mataifa mengineyo. Itafanywa namna tu ambavyo wana wa Israeli wanavyofanya sasa, na joho la kuhani na taji la mfalme, utukufu Wangu, Yehova, ukiwa miongoni mwao na uadhama Wangu ukivinjari juu yao na ukiwa nao. Kazi Yangu katika Mataifa itatekelezwa pia katika njia hiyo. Kama vile kazi Yangu kule Israeli ilivyokuwa, ndivyo kazi Yangu katika Mataifa itakavyokuwa kwa sababu Nitapanua kazi Yangu kule Israeli na kuieneza katika mataifa yale mengine.
Sasa ndio wakati ambapo Roho Wangu anafanya kazi kuu, na ndio wakati ambapo Ninaanza kazi Yangu kati ya Mataifa. Zaidi ya hayo, ndiyo wakati ambapo Ninaainisha viumbe wote walioumbwa, Nikimweka kila mmoja katika aina yake, ili kazi Yangu iweze kuendelea kwa kasi zaidi na iweze kufikia matokeo zaidi. Na hivyo, kile Ninachowaomba bado ni kwamba utoe nafsi yako yote kwa kazi Yangu yote, na, zaidi ya hayo, kwamba utambue wazi na uone kwa usahihi kazi yote ambayo Nimefanya ndani yako, na kutumia nguvu zako zote ili kazi Yangu iweze kupata matokeo makuu zaidi. Hili ndilo unalopaswa kuelewa. Acha kushindana ninyi kwa ninyi, kutafuta njia ya kutokea, au kutafuta raha kwa ajili ya mwili wako, ili kuepuka kuchelewesha kazi Yangu, na kuzuia mustakabali wako wa ajabu. Badala ya kukulinda, kufanya hivyo kunaweza tu kuleta maangamizi juu yako. Je, si huu utakuwa ujinga kwa upande wako? Kile ambacho unajifurahisha nacho leo ndicho kile kile ambacho kinaharibu mustakabali wako, huku yale maumivu unayostahimili leo ndicho kile kitu ambacho kinakulinda hasa. Lazima ufahamu waziwazi kuhusu jambo hilo, ili uepuke kuwa windo la vishawishi ambavyo utaona ugumu kujinasua kutoka kwavyo, na kuepuka kuingia kwa kijinga kwenye ukungu mzito na kutoweza kupata jua daima. Ukungu huu mzito utakapotoweka, utajipata katikati ya hukumu ya siku kuu. Kufikia wakati huo, siku Yangu itakuwa imemkaribia binadamu. Utatorokaje hukumu Yangu? Utawezaje kuvumilia joto kali la jua? Ninapompa binadamu wingi Wangu, haufurahii kwa dhati, lakini badala yake anautupa nje kwenye sehemu zisizotambulika. Wakati siku Yangu itawadia, binadamu hataweza tena kugundua wingi Wangu au kupata ukweli mkali Niliompa zamani sana. Ataomboleza na kulia, kwa sababu amepoteza uangavu wa mwanga na kuanguka gizani. Kile mnachoona leo ni upanga tu mkali wa kinywa Changu. Bado hamjakiona kiboko kilicho katika mkono Wangu au moto Ninaotumia kumchoma binadamu, na ndiyo maana bado mna kiburi na msio na kiasi mbele Yangu. Ndiyo maana bado mnapigana na Mimi katika nyumba Yangu, huku mkipinga kwa ulimi wa mwanadamu kile ambacho Nimenena na kinywa Changu. Binadamu haniogopi Mimi. Akiwa bado katika uhasama na Mimi hadi leo, bado haniogopi kamwe. Mnao ulimi na meno ya wale wasio na haki vinywani mwenu. Maneno na matendo yenu ni kama yale ya yule nyoka aliyemshawishi Hawa na kumfanya kutenda dhambi. Mnadai nyinyi kwa nyinyi kulipiza kisasi, na mnashindana mbele Yangu kwa ajili ya nafasi, umaarufu, na faida kwa ajili yenu wenyewe, ilhali hamjui kwamba Natazama maneno na matendo yenu kwa siri. Kabla hata ya nyinyi kuja mbele Yangu, Nimejua vina vya nyoyo zenu kabisa. Siku zote binadamu hutamani kutoroka kutoka mfumbato Wangu na kuepuka uangalizi wa macho Yangu, lakini Sijawahi kuepuka maneno au matamshi yake. Badala yake, kwa kusudio kuu huwa Nayaruhusu maneno na matendo hayo yaingie katika macho Yangu, ili Niweze kuadibu udhalimu wake na kuhukumu uasi wake. Kwa hiyo, maneno na matendo fiche ya binadamu siku zote yanawekwa mbele ya kiti Changu cha hukumu, na hukumu Yangu haijawahi kumtoka binadamu, kwa sababu uasi wake ni mwingi mno. Kazi Yangu ni kuteketeza na kusafisha maneno na matendo yote ya binadamu yaliyotamkwa na kufanywa mbele ya Roho Wangu. Kwa njia hiyo, baada ya Mimi kuondoka ulimwenguni, binadamu wataweza bado kuendeleza utiifu Kwangu, na bado watanihudumia kama vile watumishi Wangu watakatifu wanavyofanya katika kazi Yangu, wakiruhusu kazi Yangu hapa ulimwenguni iendelee mpaka siku itakapokamilika.