Onyo kwa Wale Wasiotenda Ukweli

Wale miongoni mwa ndugu ambao daima hueneza ubaya wao ni vibaraka wa Shetani, na hulivuruga kanisa. Watu hawa lazima siku moja wafukuzwe na kuondolewa. Katika imani yao kwa Mungu, ikiwa watu hawana moyo wa kumcha Mungu ndani yao, ikiwa hawana moyo ambao ni mtiifu kwa Mungu, basi sio tu kwamba hawatashindwa kufanya kazi yoyote ya Mungu, lakini kinyume na hayo watakuwa watu wanaovuruga kazi ya Mungu na wanaomwasi Mungu. Wakati ambapo mtu anayeamini Mungu hamtii Mungu ama kumcha Mungu lakini badala yake anamwasi, basi hii ndiyo aibu kuu zaidi kwa muumini. Ikiwa usemi na mwenendo wa muumini daima havina mpango na bila kizuizi kama asiyeamini, basi huyu muumini ni mwovu zaidi kumpiku asiyeamini; yeye ni ibilisi halisi. Wale walio kanisani ambao wanaeneza matamshi yao yenye sumu, wale miongoni mwa ndugu ambao wanasambaza uvumi, kuchochea utengano na kufanya magenge wanapaswa kufukuzwa kutoka kanisani. Lakini watu hawa wamezuiwa kwa kuwa sasa ni enzi tofauti ya kazi ya Mungu, kwa sababu wamehukumiwa kuwa vyombo vya kuondolewa. Wale waliopotoshwa na Shetani wote wana tabia iliyopotoka. Hata hivyo, baadhi ya watu wana tabia potovu tu, huku kuna wengine walio tofauti: Si tu kwamba wana tabia potovu za kishetani, lakini asili zao pia ni mbovu kupita kiasi. Si tu kwamba maneno yao na vitendo vyao vinafichua tabia zao potovu za kishetani; watu hawa, aidha ndio Shetani wa kweli. Tabia yao inakatiza na kuvuruga kazi ya Mungu, inaharibu uingiaji wa kina ndugu katika uzima, na kuharibu maisha ya kawaida ya kanisa. Mbwa mwitu hawa waliovalia ngozi ya kondoo lazima waondolewe nje siku moja, na mtu lazima awe na mtazamo usiojizuia kwa vibaraka hawa wa Shetani; mtu lazima awe na mtazamo wa kuachwa kwao. Ni katika kufanya hili pekee ndipo mtu ataweza kusimama upande wa Mungu na wale wasioweza kufanya hili wako katika ushirika na Shetani. Mungu daima yumo mioyoni mwa wale wanaomwamini Mungu kwa kweli na daima wana moyo wa kumcha Mungu, moyo wa kumpenda Mungu. Wale wanaomwamini Mungu lazima wayafanye mambo kwa moyo wa uangalifu na wenye busara, na yote wanayoyafanya yanapasa kulingana na matakwa ya Mungu na yaweze kuuridhisha moyo wa Mungu. Hawapaswi kuwa wabishi, wakifanya watakavyo, hayo hayafai katika utaratibu mtakatifu. Watu hawawezi kuipunga bendera ya Mungu kwa madaha na kucharuka kila mahali, wakienda kwa mikogo na kutapeli kotekote; kutenda haya ni tendo la uasi la juu zaidi. Familia zina masharti zao na mataifa yana sheria zao; je, hali sio hivi hata zaidi katika nyumba ya Mungu? Je, matarajio sio makali hata zaidi? Je, hakuna amri nyingi hata zaidi za utawala? Watu wana uhuru wa kutenda watakayo, lakini amri za usimamizi za Mungu haziwezi kubadilishwa kwa hiari. Mungu ni Mungu asiyewaruhusu watu kumkosea; Yeye ni Mungu anayewaua watu. Je, watu kweli hawajui hili tayari?

Kila moja ya kanisa lina watu wanaolivuruga kanisa, watu wanaokatiza kazi ya Mungu. Watu hawa wote ni Shetani wanaojifanya katika familia ya Mungu. Watu kama hawa ni waigizaji wazuri: wanakuja mbele Yangu na uchaji mkubwa, wakiinama na kuchakura, wakiishi kama mbwa koko, wakijitolea “yote” waliyo nayo ili kufanikisha malengo yao wenyewe—lakini mbele ya kina ndugu, anaonyesha sura yake mbaya. Anapomwona mtu akiutenda ukweli anamshambulia na kumtenga; anapomwona mtu wa kutisha kumpiku yeye mwenyewe, anamsifu mno na kujipendekeza kwake, wakitenda kama viongozi wa kiimla kanisani. Inaweza kusemwa kuwa mengi ya makanisa yana aina hii ya “nyoka mwovu wa ndani,” aina hii ya “mbwa wa kupakata” kati yao. Wanatembea kwa siri kwa pamoja, wakikonyezana na kuashiriana, na hakuna hata mmoja wao anayetenda ukweli. Yeyote aliye na sumu zaidi ndiye “ibilisi mkuu,” na yeyote aliye na hadhi ya juu zaidi huwaongoza, akipeperusha bendera yao juu zaidi. Watu hawa wanakuwa huru na kufanya wanachotaka kanisani, wakieneza ubaya wao, wakiachilia kifo, wakifanya watakavyo, wakisema wanachopenda, bila anayethubutu kuwakomesha, wakijawa na tabia za kishetani. Punde tu wanapoanza kusababisha usumbufu, hewa ya kifo inaingia ndani ya kanisa. Wale wanaotenda ukweli katika kanisa wanaachwa na wanashindwa kufikia uwezo wao, ilhali wale wanaovuruga kanisa na kusambaza kifo wanakuwa huru na kufanya wanachotaka kanisani. Cha ziada ni, watu wengi huwafuata. Aina hii ya kanisa iko chini ya udhibiti wa Shetani na ibilisi ni mfalme wao. Iwapo watu wa kanisa hawataamka na kuwafukuza hao ibilisi wakuu, basi pia watakuja kuangamia siku moja. Kuanzia leo na kuendelea hatua lazima zichukuliwe dhidi ya kanisa la aina hii. Ikiwa wale wanaoweza kutenda ukweli kidogo hawatafuti kufanya hivyo, basi kanisa hilo litaondolewa. Ikiwa hakuna mtu yeyote kanisani aliye radhi kuutenda ukweli, hakuna yeyote anayeweza kuwa shahidi kwa Mungu, basi kanisa hilo linapasa kutengwa kabisa, miunganisho yao na makanisa mengine kukatizwa. Hili linaitwa “kuzika kifo”; hii ndiyo maana ya kumfukuza Shetani. Iwapo kanisa lina waonevu kadhaa wa hapo, na wanafuatwa na “nzi wadogo” wasio na ufahamu kabisa, na ikiwa washiriki wa kanisa, hata baada ya kuona ukweli, bado hawawezi kukataa vifungo na kuchezewa na hawa waonevu—basi hawa wajinga wataondolewa mwishoni. Ingawa nzi hawa wadogo wanaweza kuwa hawajafanya lolote baya, wao ni wenye hila hata zaidi, wadanganyifu hata zaidi na wenye kukwepa hata zaidi na kila mtu aliye namna hii ataondolewa. Hakuna yeyote atakayeachwa! Wale walio wa Shetani watarudishwa kwa Shetani, ilhali wale walio wa Mungu hakika watakwenda kutafuta ukweli; hili linaamuliwa na asili zao. Acheni wale wote wanaomfuata Shetani waangamie! Hakuna huruma watakayoonyeshwa watu hawa. Acheni wale wanaofuata ukweli wapate utoaji na muwakubalie kufurahia neno la Mungu hadi mioyo yao itosheke. Mungu ni mwenye haki; Yeye hawatendei watu kwa udhalimu. Ikiwa wewe ni ibilisi basi hutakuwa na uwezo wa kuutenda ukweli. Ikiwa wewe ni mtu anayetafuta ukweli basi ni wazi kuwa hutatekwa nyara na Shetani—hili halina tashwishi yoyote.

Wale wasiotafuta kuendelea daima wanataka wengine wawe wabaya na watepetevu kama wao wenyewe, wale wasiotenda ukweli wanawaonea gere wale wanaotenda ukweli. Wale wasiotenda ukweli daima wanataka kuwadanganya wale wapumbavu na wasio na ufahamu. Mambo ambayo watu hawa wanaeneza yanaweza kukufanya usawijike, kuteleza kwenda chini, kuwa na hali isiyokuwa ya kawaida na kujawa na kiza ndani yako; yanaweza kukufanya usogezwe mbali na Mungu, na yanakufanya uuthamini mwili na kujihusisha na tamaa. Wale ambao hawapendi ukweli, ambao daima humshughulikia Mungu kwa uzembe hawana maarifa ya binafsi, na tabia zao huwashawishi watu kufanya dhambi na kuasi Mungu. Hawaweki ukweli katika vitendo wala kuwaruhusu wengine kutenda ukweli. Wanathamini dhambi na hawana chuki kwao wenyewe. Hawajifahamu wenyewe na huwakomesha wengine kujifahamu wenyewe, na huwakomesha wengine kuwa na matamanio ya kujua ukweli. Wale wanaowadanganya hawawezi kuona mwangaza na huanguka gizani, hawajijui wenyewe, na ukweli kwao si wazi na wanakuwa mbali zaidi na zaidi na Mungu. Hawaweki ukweli katika vitendo na huwakomesha wengine kutenda ukweli, wakiwaleta watu hao wajinga mbele yao. Badala ya kusema kuwa wanamwamini Mungu ingekuwa vyema kusema kuwa wanawaamini mababu zao, kwamba kile wanachoamini ni sanamu zilizo mioyoni mwao. Ingekuwa vyema kwa wale watu wanaosema kuwa wanamfuata Mungu kufungua macho yao watazame vizuri waone ni nani wanayemwamini hasa: Je, ni Mungu unayemwamini hakika, ama Shetani? Ikiwa unajua kuwa unayemwamini si Mungu ila sanamu zako mwenyewe, basi ni vyema kabisa usiseme kuwa wewe ni muumini. Ikiwa hakika hujui unayemwamini ni nani, basi, pia, ni vyema kabisa usiseme kuwa wewe ni muumini. Kusema hivi kutakuwa kukufuru! Hakuna anayekushurutisha umwamini Mungu. Msiseme kuwa mnaniamini Mimi, kwa kuwa Niliyasikia maneno hayo hapo kale wala Sitamani kuyasikia tena, kwa kuwa mnachoamini ni sanamu zilizo katika mioyo yenu na nyoka waovu wa ndani walio miongoni mwenu. Wale wanaotikisa vichwa vyao wanaposikia ukweli, wanaotabasamu sana wanaposikia mazungumzo ya kifo ni watoto wa Shetani, na wote ni vyombo vya kuondolewa. Kuna watu wengi kanisani ambao hawana ufahamu, na jambo la uongo linapotendeka wanasimama tu upande wa Shetani. Wanapoitwa vibaraka wa Shetani wanahisi kuwa wamekosewa sana. Wanasemekana kuwa hawana ufahamu, lakini daima wanasimama upande usiokuwa na ukweli. Hakujakuwa na wakati muhimu ambapo wamesimama upande wa ukweli, hakuna wakati mmoja ambapo hawasimami na kutetea mjadala juu ya ukweli. Je, kweli hawana ufahamu? Kwa nini daima wao husimama upande wa Shetani isipotarajiwa? Kwa nini hawasemi neno lolote la haki ama lenye mantiki kwa ukweli? Je, hali hii kweli imetokana na kuchanganyikiwa kwao kwa ghafla? Kadri mtu anapokuwa na ufahamu mdogo, ndivyo anavyozidi kushindwa kusimama upande wa ukweli. Je, hili linaonyesha nini? Je, halionyeshi kuwa wale wasio na ufahamu wanapenda uovu? Je, halionyeshi kuwa wale wasio na ufahamu ni watoto waaminifu wa Shetani? Je, ni kwa nini daima wanaweza kusimama upande wa Shetani na kuzungumza lugha moja naye? Kila neno na tendo lao, na maonyesho yao yanathibitisha vya kutosha kuwa wao sio wapenzi wa ukweli kwa namna yoyote, lakini badala yake wao ni watu wanaochukia ukweli. Kwamba wanaweza kusimama upande wa Shetani kunadhihirisha kuwa hakika Shetani anawapenda ibilisi hawa wadogo wanaopigana kwa ajili ya Shetani katika maisha yao yote. Je, taarifa hizi za kweli si wazi sana? Ikiwa hakika wewe ni mtu unayependa ukweli, basi kwa nini huwaheshimu wale wanaotenda ukweli, na mbona unawafuata mara moja wale wasiotenda ukweli punde kwa kuwaangalia tu? Je, hili ni tatizo la aina gani? Sijali iwapo una ufahamu au la, sijali kwamba umelipa gharama kuu kiasi gani, sijali kuwa nguvu zako ni kuu kiasi gani na sijali ikiwa wewe ni nyoka mwovu wa ndani ama kiongozi anayepeperusha bendera. Ikiwa nguvu zako ni kuu basi ni kwa ajili tu ya usaidizi wa nguvu za Shetani; ikiwa hadhi yako iko juu, basi ni kwa sababu kuna wengi waliokuzunguka wasiotenda ukweli; ikiwa hujafukuzwa basi ni kwa kuwa sasa sio wakati wa kazi ya kufukuza, bali ni wakati wa kazi ya kuondoa. Hakuna haraka ya kukufukuza sasa. Ninasubiri tu siku ambayo Nitakuadhibu baada ya wewe kuondolewa. Yeyote asiyetenda ukweli ataondolewa!

Wale wanaomwamini Mungu kwa kweli ni wale walio tayari kuweka neno la Mungu kwenye matendo, na ni wale walio radhi kutenda ukweli. Wale wanaoweza kwa kweli kuwa shahidi kwa Mungu pia ni wale walio radhi kuweka neno Lake kwenye matendo, na ni wale ambao kwa kweli wanaweza kusimama upande wa ukweli. Wale wanaotumia hila na wale wanaotenda yasio haki wote ni watu wasiokuwa na ukweli na wote huleta aibu kwa Mungu. Wale walio kanisani wanaohusika na mabishano ni vibaraka wa Shetani, na ni mfano mwema wa Shetani. Mtu wa aina hii ni mwovu sana. Wale wasio na ufahamu na wasio na uwezo wa kusimama upande wa ukweli wanahifadhi nia mbovu na kufifisha ukweli. Watu hawa hata zaidi ni waakilishi kamili wa Shetani; wamepita hali ya ukombozi na ni wazi mno kuwa wao wote ni vitu vya kuondolewa. Wale wasiotenda ukweli hawapaswi kuruhusiwa kusalia katika familia ya Mungu, wala wale wanaobomoa kanisa kwa makusudi. Lakini sasa Sifanyi kazi ya kufukuza. Watafichuliwa tu na kuondolewa mwishoni. Hakuna kazi nyingine ya bure itakayofanywa kwa watu hawa; wale walio wa Shetani hawana uwezo wa kusimama upande wa ukweli, ilhali wale wanaotafuta ukweli wanaweza kusimama upande wa ukweli. Wale wasiotenda ukweli hawastahili kusikia njia ya kweli na hawastahili kuwa na ushuhuda kwa ukweli. Kimsingi ukweli si kwa ajili ya masikio yao lakini badala yake unazungumzwa kwa ajili ya masikio ya wale wanaoutenda. Kabla ya mwisho wa kila mtu kufichuliwa, wale wanaovuruga kanisa na kukatiza kazi kwanza wataachwa upande moja. Pindi kazi itakapokamilika, watu hawa watafunuliwa mmoja baada ya mwingine kabla ya kuondolewa. Wakati wa kutoa ukweli, Siwatilii maanani kwa sasa. Ukweli wote unapofichuliwa kwa mwanadamu watu hao wanapasa kuondolewa, kwa kuwa huo pia utakuwa wakati ambapo watu wataainishwa kulingana na aina yao. Kwa sababu ya werevu wao mdogo, wale wasio na ufahamu watakuja kuangamia mikononi mwa watu waovu na watapotoshwa na watu waovu na watashindwa kurudi. Watu hawa wanapasa kushughulikiwa kwa njia hii, kwa kuwa hawaupendi ukweli, kwa sababu hawana uwezo wa kusimama upande wa ukweli, kwa sababu wanawafuata watu waovu, wanawaunga mkono watu waovu, na kwa sababu wanashirikiana na watu waovu na kumuasi Mungu. Wanajua vema kuwa watu hao waovu wananururisha uovu lakini wanafanya mioyo yao kuwa migumu na kuwafuata, wakienda kinyume na ukweli. Je, watu hawa wasiotenda ukweli lakini wanaofanya mambo ya uharibifu na ya chukizo wote si wanafanya maovu? Ingawa kuna wale miongoni mwao ambao wanajipa mtindo wenyewe kama “wafalme” na wale wanaofuata msururu nyuma yao, je, asili yao ya kuasi Mungu si ni sawa yote? Je, wanaweza kutoa sababu gani kuwa Mungu hawaokoi? Je, wanaweza kutoa sababu gani kuwa Mungu si mwenye haki? Je, si ni uovu wao wenyewe ambao umewaangamiza? Je, si ni uasi wao ambao utawavuta hadi jahanamu? Wale wanaotenda ukweli mwishowe wataokolewa na kufanywa wakamilifu kwa kupitia ukweli. Wale wasiotenda ukweli mwishowe watakaribisha maangamizi kwa kupitia ukweli. Hii ndio miisho inayowasubiri wale wanaotenda ukweli na wale wasioutenda. Ninawashauri wale ambao hawana mpango wa kutenda ukweli watoke kanisani haraka iwezekanavyo ili kuepuka kutenda dhambi nyingi zaidi. Wakati utakapofika, hata majuto yatakuwa yamechelewa, na hasa wale wanaofanya magenge na kufanya migawanyiko, na wale nyoka waovu wa ndani katika kanisa lazima watoke haraka sana. Watu hawa ambao ni wenye asili ya mbwa mwitu mwovu hawana uwezo wa mabadiliko, ni heri watoke kanisani kwa nafasi inayopatikana mwanzo, wasiweze kuyavuruga maisha mazuri ya ndugu tena, na hivyo kuepuka adhabu ya Mungu. Nyinyi ambao mlienda pamoja nao mtafanya vema kutumia nafasi hii kutafakari juu yenu wenyewe. Je, mtawafuata waovu nje ya kanisa, ama kusalia na kufuata kwa unyenyekevu? Lazima uzingatie jambo hili kwa makini. Ninawapa nafasi moja zaidi ya kuchagua. Ninalisubiri jibu lenu.

Iliyotangulia: Kazi ya Roho Mtakatifu na Kazi ya Shetani

Inayofuata: Je, Wewe ni Mtu Ambaye Amepata Uzima?

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp