Kazi ya Roho Mtakatifu na Kazi ya Shetani
Mtu huelewaje mambo ya ndani ya roho? Roho Mtakatifu hufanyaje kazi ndani ya mwanadamu? Shetani hufanyaje kazi ndani ya mwanadamu? Roho waovu hufanyaje kazi ndani ya mwanadamu? Udhihirisho ni upi? Jambo linapokutendekea, je, linatoka kwa Roho Mtakatifu, na, je, unapaswa kulitii au kuliasi? Katika utendaji halisi wa watu, mengi hutokana na mapenzi ya binadamu ambayo watu huamini kila wakati kwamba yanatoka kwa Roho Mtakatifu. Mambo mengine hutoka kwa roho waovu, lakini bado watu kila mara hufikiri yametoka kwa Roho Mtakatifu, na wakati mwingine Roho Mtakatifu huwaongoza watu kwa ndani, lakini watu wanaogopa kwamba mwongozo kama huo unatoka kwa Shetani na hivyo hawathubutu kutii, huku katika uhalisi mwongozo huo ni nuru ya Roho Mtakatifu. Kwa hivyo, ikiwa mtu hatumii utambuzi, hataweza kwa kweli kupitia mambo halisi anayopitia; ikiwa mtu hatumii utambuzi katika upitiaji wake, basi hataweza kupata uzima. Roho Mtakatifu hufanyaje kazi? Roho waovu hufanyaje kazi? Ni nini hutokana na mapenzi ya mwanadamu? Na kitu gani ambacho huzaliwa kutokana na mwongozo na nuru ya Roho Mtakatifu? Ikiwa unaelewa mifumo ya kazi ya Roho Mtakatifu ndani ya mwanadamu, basi, katika maisha yako ya kila siku na wakati wa uzoefu wako halisi, utaweza kukuza maarifa yako na kupata utambuzi; utakuja kumjua Mungu, utaweza kumfahamu na kumtambua Shetani; hutachanganyikiwa katika utii au ufuatiliaji wako, na utakuwa mtu ambaye mawazo yake yako wazi, ambaye anatii kazi ya Roho Mtakatifu.
Kazi ya Roho Mtakatifu ni kutoa mwongozo na nuru katika upande chanya. Haitawafanya watu kuwa hasi. Inawaletea faraja, inawapa imani na azimio, na inawawezesha kufuatilia kufanywa kuwa watimilifu na Mungu. Roho Mtakatifu anapofanya kazi, watu wanaweza kuingia kutoka katika upande chanya; wao si wanaokaa bila kuchukua hatua au wa kulazimishwa, bali hutenda kwa hiari yao wenyewe. Roho Mtakatifu anapofanya kazi, watu wanafurahi na wako tayari, wako tayari kutii na wanafurahi kujinyenyekeza. Hata ikiwa wana maumivu na udhaifu kwa ndani, wana azimio la kushirikiana; wanateseka kwa furaha, wanaweza kutii, na hawajachanganywa na mapenzi ya binadamu, hawajachanganywa na fikira za mwanadamu, na hata zaidi hawajachanganywa na matarajio na nia za binadamu. Watu wanapopitia kazi ya Roho Mtakatifu, wanakuwa safi hasa kwa ndani. Wale walio na kazi ya Roho Mtakatifu wanaishi kwa kudhihirisha upendo kwa Mungu na upendo kwa ndugu na dada zao; wanafurahia mambo yanayomfurahisha Mungu na kuchukia mambo anayoyachukia Mungu. Watu wanaoguswa na kazi ya Roho Mtakatifu ni wale walio na ubinadamu wa kawaida, kwa kawaida hufuatilia ukweli, na wana ubinadamu. Roho Mtakatifu anapofanya kazi ndani ya watu, hali yao inakuwa bora zaidi na zaidi, na ubinadamu wao unakuwa wa kawaida zaidi na zaidi, na ingawa ushirikiano wao fulani unaweza kuwa wa kipumbavu, nia zao ni sahihi, wanaingia kutoka katika upande chanya, hawajaribu kusababisha vurugu, na hawana nia zozote mbaya. Kazi ya Roho Mtakatifu ni ya kawaida na ya vitendo, Roho Mtakatifu hufanya kazi ndani ya mwanadamu kulingana na mifumo ya maisha ya watu wa kawaida, na Yeye hutia nuru na kuwaongoza watu kwa ndani kulingana na ufuatiliaji halisi wa watu wa kawaida. Roho Mtakatifu anapofanya kazi ndani ya watu, Yeye huwaongoza na kuwatia nuru kulingana na mahitaji ya watu wa kawaida. Yeye huwakimu kulingana na mahitaji yao, na Yeye huwaongoza na kuwatia nuru kulingana na kile wanachokosa, na kulingana na upungufu wao, kutoka katika upande chanya. Kazi ya Roho Mtakatifu ni kuwatia nuru na kuwaongoza watu katika maisha halisi; wanapopitia maneno ya Mungu katika maisha yao halisi ndipo tu wanapoweza kuona kazi ya Roho Mtakatifu. Ikiwa, katika maisha yao ya kila siku, watu wako katika hali chanya na wana maisha ya kiroho ya kawaida, basi wana kazi ya Roho Mtakatifu. Katika hali kama hiyo, wana imani wanapokula na kunywa maneno ya Mungu, wanatiwa moyo wanapoomba, na hawawi hasi wanapokumbana na jambo fulani—ndani yake, wanaweza kuona mafunzo ambayo Mungu anawataka wajifunze, wao si hasi wala dhaifu, na ingawa wana matatizo halisi, wako tayari kutii mipango yote ya Mungu.
Ni matokeo gani yanayofanikishwa na kazi ya Roho Mtakatifu? Unaweza kuwa mpumbavu, au unaweza kuwa huna utambuzi, lakini Roho Mtakatifu akifanya kazi tu kutakuwa na imani ndani yako, utahisi kila mara kwamba huwezi kumpenda Mungu vya kutosha, na utakuwa tayari kushirikiana. Haijalishi matatizo yaliyo mbele ni makubwa kiasi gani, bado utakuwa tayari kushirikiana. Mambo yanapokutendekea na si wazi kwako iwapo yanatoka kwa Mungu au kwa Shetani, utaweza kusubiri, na hutakuwa hasi wala mzembe. Hii ndiyo kazi ya kawaida ya Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anapofanya kazi ndani yako, bado utakumbana na matatizo halisi: Wakati mwingine utatokwa na machozi, na wakati mwingine kutakuwa na mambo ambayo huwezi kuyashinda—hii yote ni awamu tu ya kazi ya kawaida ya Roho Mtakatifu. Ingawa hutafaulu kuyashinda mambo hayo, na ingawa wakati huo utakuwa dhaifu na utalalamika, baadaye bado utaweza kumpenda Mungu, ukifurikwa na imani. Uhasi wako hautakuzuia kuwa na upitiaji wa kawaida, na bila kujali kile ambacho watu wengine wanasema, na jinsi wengine wanavyokushambulia, bado utaweza kumpenda Mungu. Wakati wa maombi, utahisi kila mara kwamba wakati uliopita ulikuwa na deni kubwa sana kwa Mungu, na utaazimia kumridhisha Mungu na kuuasi mwili utakapokumbana na mambo kama hayo tena. Msukumo huu unaonyesha kwamba kazi ya Roho Mtakatifu iko ndani yako. Hii ndiyo hali ya kawaida ya kazi ya Roho Mtakatifu.
Kazi inayotoka kwa Shetani ni ipi? Katika kazi inayotoka kwa Shetani, maono ndani ya watu sio dhahiri; watu hawana ubinadamu wa kawaida, nia za matendo yao si sahihi, na ingawa wanatamani kumpenda Mungu kila mara kuna mashtaka ndani yao, na mashtaka haya na mawazo husababisha usumbufu wa kila mara ndani yao, yakibana ukuaji wa maisha yao na kuwazuia kuwa katika hali ya kawaida mbele za Mungu. Yaani, punde tu kazi ya Shetani inapokuwa ndani ya watu, mioyo yao haiwezi kuwa na amani mbele za Mungu. Hawajui wafanye nini—wanapoona watu wakikusanyika pamoja, wanataka kutoroka, na hawawezi kufumba macho yao wakati wengine wanaomba. Kazi ya roho waovu inaharibu uhusiano wa kawaida kati ya mwanadamu na Mungu, na kuvuruga maono ya awali ya watu au njia yao ya zamani ya kuingia katika uzima; mioyoni mwao hawawezi kamwe kumkaribia Mungu, wanasumbuliwa na kubanwa kila mara na jambo fulani, na mioyo yao haiwezi kupata amani. Wanaachwa bila nguvu za kumpenda Mungu na roho zao zikishuka. Huo ndio udhihirisho wa kazi ya Shetani. Udhihirisho wa kazi ya Shetani ni: kutoweza kushikilia msimamo wako na kusimama imara katika ushuhuda wako, kukusababisha uwe mtu asiye sahihi mbele za Mungu na mtu asiye na uaminifu kwa Mungu. Shetani anapokusumbua, unapoteza upendo na uaminifu kwa Mungu ndani yako, unanyang’anywa uhusiano wa kawaida na Mungu, hufuatilii ukweli au kujiboresha wewe mwenyewe; unarudi nyuma na kuwa hasi, unajiendekeza, unatoa uhuru kamili kwa kuenea kwa dhambi na huchukii dhambi. Zaidi ya hayo, inakusababisha uwe mpotovu; inasababisha mguso wa Mungu utoweke ndani yako na kukufanya ulalamike kuhusu Mungu na kumpinga Yeye, ikikuongoza kumtilia Mungu shaka; hata kuna hatari kwamba utaondoka. Haya yote yanatoka kwa Shetani.
Jambo linapokutendekea katika maisha yako ya kila siku, unapaswa kutambuaje iwapo linatoka kwa kazi ya Roho Mtakatifu au kwa kazi ya Shetani? Hali za watu zinapokuwa za kawaida, maisha yao ya kiroho na maisha yao katika mwili ni ya kawaida na busara yao ni ya kawaida na yenye mpangilio. Wanapokuwa katika hali hii, kile wanachopitia na kuja kujua ndani yao wenyewe kwa ujumla kinaweza kusemwa kwamba kinatoka kwa mguso wa Roho Mtakatifu. (Kuwa na umaizi au kupata maarifa kiasi ya juu juu wanapokula na kunywa maneno ya Mungu, au kuwa waaminifu katika mambo fulani, au kuwa na nguvu za kumpenda Mungu katika mambo fulani—haya yote yanatoka kwa Roho Mtakatifu.) Kazi ya Roho Mtakatifu kwa mwanadamu ni ya kawaida hasa; mwanadamu hana uwezo wa kuihisi, na inaonekana kana kwamba inatoka kwa mwanadamu mwenyewe, ingawa kwa kweli ni kazi ya Roho Mtakatifu. Katika maisha ya kila siku, Roho Mtakatifu hufanya kazi juu ya kila mtu, ambayo inaweza kuwa kubwa au ndogo, na ni kiwango tu cha kazi hii ndicho kinachotofautiana. Baadhi ya watu wana ubora mzuri wa tabia, na wanafahamu mambo haraka, na Roho Mtakatifu hutoa nuru maalum ndani yao. Wakati huo huo, baadhi ya watu wana ubora duni wa tabia, na inawachukua muda mrefu zaidi kufahamu mambo, lakini Roho Mtakatifu huwagusa kwa ndani na wao, pia, wanaweza kuwa waaminifu kwa Mungu. Roho Mtakatifu hufanya kazi ndani ya wale wote wanaomfuatilia Mungu. Wakati, katika maisha ya kila siku, watu hawampingi au kumwasi Mungu, hawafanyi mambo yanayovuruga usimamizi wa Mungu na hawaisumbui kazi ya Mungu, basi ndani ya kila mmoja wao Roho wa Mungu hufanya kazi kwa kiwango kikubwa au kidogo; Yeye huwagusa, kuwatia nuru, kuwapa imani, kuwapa nguvu, na kuwasukuma kuingia kwa njia chanya, bila kuwa wavivu au kutamani starehe za kimwili, wakiwa tayari kutenda ukweli, na kutamani maneno ya Mungu. Hii yote ni kazi inayotoka kwa Roho Mtakatifu.
Hali za watu zinapokosa kuwa za kawaida, wanatelekezwa na Roho Mtakatifu. Malalamiko ndani ya mioyo yao, nia zao zisizo sahihi, uvivu wao, kuendekeza kwao mwili, na nia yao ya kusaliti ukweli—haya yote yanatoka kwa Shetani. Hali za watu zinapokosa kuwa za kawaida, wanapokuwa na giza kwa ndani na wamepoteza busara yao ya kawaida, wametelekezwa na Roho Mtakatifu, na hawawezi kumhisi Mungu ndani yao wenyewe, huu ndio wakati Shetani anafanya kazi ndani yao. Ikiwa kila mara watu wana nguvu ndani yao na kila mara wanampenda Mungu, basi kwa ujumla, mambo yanapowatendekea, mambo hayo yanatoka kwa Roho Mtakatifu, na yeyote wanayekutana naye, kukutana huko kunatokana na mipango ya Mungu. Hii ni kusema kwamba unapokuwa katika hali ya kawaida, unapokuwa ndani ya kazi kuu ya Roho Mtakatifu, basi haiwezekani kwa Shetani kukufanya uyumbe. Kwa msingi huu inaweza kusemwa kwamba kila kitu kinatoka kwa Roho Mtakatifu, na ingawa unaweza kuwa na mawazo yasiyo sahihi, unaweza kuyaasi na huyafuati. Haya yote yanatoka kwa kazi ya Roho Mtakatifu. Ni katika hali zipi ambapo Shetani huingilia kati? Ni rahisi kwa Shetani kufanya kazi ndani yako hali zako zinapokuwa si za kawaida, wakati hujaguswa na Mungu na huna kazi ya Mungu, unapokuwa mkavu na mtupu kwa ndani, unapomwomba Mungu lakini huhisi chochote, na unapokula na kunywa maneno ya Mungu lakini hutiwi nuru au kuangaziwa. Yaani, wakati ambapo umetelekezwa na Roho Mtakatifu na huwezi kumhisi Mungu, basi mambo mengi yanakutendekea ambayo yanatoka kwa kishawishi cha Shetani. Roho Mtakatifu anapofanya kazi, Shetani pia anafanya kazi wakati wote. Roho Mtakatifu humgusa mwanadamu kwa ndani, huku wakati huo huo Shetani akisababisha usumbufu ndani ya mwanadamu. Hata hivyo, kazi ya Roho Mtakatifu huchukua nafasi ya mbele, na watu ambao hali zao ni za kawaida wanaweza kushinda hili; huu ni ushindi wa kazi ya Roho Mtakatifu dhidi ya kazi ya Shetani. Roho Mtakatifu anapokuwa anafanya kazi, tabia potovu bado zipo ndani ya watu; hata hivyo, wakati wa kazi ya Roho Mtakatifu, ni rahisi kwa watu kugundua na kutambua uasi wao, nia zao, na kuchanganyika kwao na uchafu. Ni hapo tu ndipo watu huhisi majuto na kuwa tayari kutubu. Hivyo, uasi wao na tabia potovu huvuliwa hatua kwa hatua ndani ya kazi ya Mungu. Kazi ya Roho Mtakatifu ni ya kawaida hasa; Anapofanya kazi ndani ya watu, bado wana matatizo, bado wanalia, bado wanateseka, bado ni dhaifu na bado kuna mengi ambayo hayako wazi kwao. Lakini wanapokuwa katika hali hizi, wanaweza kujizuia kurudi nyuma, na bado wanaweza kumpenda Mungu, na ingawa wanalia na kuumia moyoni, bado wanaweza kumsifu Mungu; kazi ya Roho Mtakatifu ni ya kawaida hasa, si ya kupita maumbile hata kidogo. Watu wengi wanaamini kwamba, punde tu Roho Mtakatifu anapoanza kufanya kazi, mabadiliko hutokea katika hali ya watu, na mambo ambayo ni dutu yao huvuliwa. Ufahamu kama huo umepotoka. Roho Mtakatifu anapofanya kazi ndani ya mwanadamu, mambo hasi ya mwanadamu bado yapo na kimo chake kinabaki vile vile, lakini anapata mwangaza na nuru ya Roho Mtakatifu na hivyo anakuwa katika hali chanya wakati mwingi, hali ndani yake zinakuwa za kawaida, na anabadilika kwa haraka zaidi. Katika uzoefu halisi wa watu, kimsingi wao hupitia kazi ya Roho Mtakatifu au ya Shetani, na ikiwa hawawezi kuzielewa hali hizi na hawana utambuzi kuzihusu, basi kuingia katika uzoefu wa vitendo hakuwezekani, sembuse mabadiliko katika tabia. Hivyo, jambo la msingi katika kupitia kazi ya Mungu ni kuweza kung’amua mambo kama hayo; kwa namna hii, itakuwa rahisi kwao kuipitia.
Kazi ya Roho Mtakatifu huwafanya watu wawe chanya na wenye msukumo, ilhali kazi ya Shetani huwafanya wawe hasi na kurudi nyuma, wamwasi Mungu na wampinge Yeye, wapoteze imani Kwake, na wawe dhaifu katika kutekeleza wajibu wao. Kila kitu kinachotokana na nuru ya Roho Mtakatifu ni cha asili kabisa; hakilazimishwi kwako. Ikiwa unakitii, basi utakuwa na amani; usipokitii, basi baadaye utahisi kukemewa. Ikiwa ni nuru ya Roho Mtakatifu, hutasumbuliwa au kubanwa katika chochote unachofanya; utawekwa huru, kutakuwa na njia ya utendaji katika matendo yako, na hutafungwa, na utaweza kutenda kulingana na nia za Mungu. Kazi ya Shetani inakusababishia usumbufu katika mambo mengi; inakufanya usiwe tayari kuomba, mvivu sana kula na kunywa maneno ya Mungu, na inakufanya usiwe tayari kuishi maisha ya kanisa, na inakutenga na maisha ya kiroho. Kazi ya Roho Mtakatifu haiingilii maisha yako ya kila siku na haiingilii maisha yako ya kiroho ya kawaida. Huwezi kutambua mambo mengi wakati uleule yanapotokea, lakini, baada ya siku kadhaa, moyo wako unang’aa zaidi na akili yako inakuwa wazi zaidi. Unakuja kuwa na ufahamu kiasi kuhusu mambo ya roho, na polepole unaweza kutambua iwapo wazo limetoka kwa Mungu au kwa Shetani. Mambo mengine yanakufanya waziwazi umpinge Mungu na kumwasi Mungu, au yanakuzuia kutia maneno ya Mungu katika vitendo; mambo haya yote yanatoka kwa Shetani. Mambo mengine hayaonekani wazi, na huwezi kuyatambua wakati huo; baadaye, unaweza kuona udhihirisho wake na kisha kutumia utambuzi. Ikiwa unaweza kutambua waziwazi ni mambo yapi yanatoka kwa Shetani na yapi yanaelekezwa na Roho Mtakatifu, basi hutapotea kwa urahisi katika upitiaji wako. Wakati mwingine, hali yako si nzuri, na una wazo ambalo linakutoa katika hali yako hasi. Hili linaonyesha kwamba hata wakati hali yako si nzuri, baadhi ya mawazo yako bado yanaweza kutoka kwa Roho Mtakatifu. Si kweli kwamba unapokuwa hasi, mawazo yako yote yanatumwa na Shetani; ikiwa hilo lingekuwa kweli, basi ungeweza lini kubadilika na kuwa katika hali chanya? Unapokuwa hasi kwa kipindi cha muda fulani, Roho Mtakatifu anakupa fursa ya kufanywa kuwa mtimilifu; Yeye anakugusa, akikufanya uibuke kutoka katika hali yako hasi, na unaingia katika hali ya kawaida.
Ukijua kazi ya Roho Mtakatifu ni nini na kazi ya Shetani ni nini, unaweza kulinganisha haya na hali yako mwenyewe wakati wa upitiaji wako, na upitiaji wako mwenyewe, na kwa njia hii kutakuwa na ukweli mwingi zaidi unaohusiana na kanuni katika upitiaji wako. Baada ya kuelewa ukweli huu kuhusu kanuni, utaweza kuelewa hali yako halisi, utaweza kuwatambua watu na matukio, na hutalazimika kutumia juhudi nyingi sana katika kupata kazi ya Roho Mtakatifu. Bila shaka, hili linategemea nia zako kuwa sahihi na utayari wako wa kutafuta na kutenda. Lugha kama hii—lugha inayohusiana na kanuni—ni kitu unachopaswa kuwa nacho katika upitiaji wako. Bila hiyo, upitiaji wako utajaa usumbufu wa Shetani na maarifa ya kipumbavu. Ikiwa huelewi jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi, basi huelewi jinsi ya kumwomba Mungu au jinsi unavyopaswa kuingia, na ikiwa hujui jinsi Shetani anavyotenda ili kuwapotosha na kuwasumbua watu, basi hujui jinsi ya kumkataa Shetani na kusimama imara katika ushuhuda wako. Jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi na jinsi Shetani anavyotenda ni mambo ambayo watu wanapaswa kuelewa, na ni mambo ambayo lazima yapitiwe katika imani ya watu kwa Mungu.