Mnapaswa Kutafakari Matendo Yenu

Kila tendo na kitendo chenu maishani kinaonyesha kwamba ni lazima mpewe kifungu cha maneno Yangu kila siku ili kuwajaza tena ninyi, kwa maana ninyi ni mliopungukiwa sana, na maarifa yenu na uwezo wenu wa kufahamu ni duni sana. Katika maisha yenu ya kila siku, mnaishi katikati ya hali na mazingira ambayo hayana ukweli au busara. Mnakosa mtaji wa kuendelea kuishi, na hamna msingi wa kunijua Mimi au kuujua ukweli. Imani yenu imejengwa juu ya imani isiyo dhahiri na ya dhahania tu au maarifa ya kimafundisho sana na mila za kidini. Kila siku Ninatazama mienendo yenu, Nikichunguza nia zenu na matunda ya uovu wenu, na Sijawahi kumpata mtu hata mmoja ambaye kwa kweli anaweka moyo na roho yake juu ya madhabahu Yangu isiyotikiswa kamwe. Hivyo Siko tayari kumimina maneno yote Ninayotaka kuonyesha kwa binadamu kama hao bure; mipango pekee moyoni Mwangu ni kwa ajili ya kazi Yangu ambayo haijakamilika na kwa ajili ya wale miongoni mwa binadamu ambao Sijawaokoa bado. Hata hivyo, Ninatamani wote wanaonifuata Mimi wapate wokovu Wangu na ukweli ambao neno Langu linampa mwanadamu. Ninatumai kwamba siku moja utakapofumba macho yako, utaona ulimwengu ambapo harufu nzuri inajaza hewa na vijito vya maji yaliyo hai vinatiririka—sio dunia yenye giza, baridi ambapo mawingu meusi yanaficha anga na sauti za vilio haziishi kamwe.

Kila siku, matendo na mawazo ya kila mtu yanatazamwa na macho ya Yule Mmoja, na, wakati huo huo, yanatayarisha kesho yao wenyewe. Hii ndiyo njia ambayo lazima itembewe na wote wanaoishi; ni njia ambayo Nimeiamua kabla kwa ajili ya wote, na hakuna anayeweza kuiepuka au kuepushwa. Maneno ambayo Nimenena hayana idadi, na kazi ambayo Nimefanya ni zaidi sana isiyo na kipimo. Kila siku, Ninatazama jinsi kila mtu kiasili anavyotekeleza yote anayopaswa kufanya kulingana na asili yake ya ndani na maendeleo ya asili yake. Bila kujua, wengi tayari wameingia kwenye “njia sahihi,” ambayo Nimeiweka ili kufunua aina tofauti za watu. Watu hawa wa aina tofauti Nimewaweka tangu kitambo katika mazingira tofauti na, katika nafasi zao husika, kila mmoja anaonyesha aina yake ya asili. Hakuna wa kuwafunga, hakuna wa kuwashawishi. Wako huru kwa ukamilifu wao na kile wanachofunua huja kiasili. Ni kitu kimoja tu kinachowadhibiti: maneno Yangu. Hivyo ndivyo baadhi ya watu husoma maneno Yangu shingo upande, bila kuyatenda kamwe, wakifanya hivyo tu ili waambulie matokeo ya kuepuka kifo; wengine, wakati huo huo, wanaona ni vigumu kuvumilia siku bila maneno Yangu kuwaongoza na kuwakimu, na hivyo kiasili wanashikilia maneno Yangu wakati wote. Kadiri muda unavyosonga, wanagundua siri ya maisha ya binadamu, hatima ya binadamu, na thamani ya kuwa binadamu. Hivi ndivyo binadamu alivyo mbele ya maneno Yangu, na Mimi huruhusu tu mambo yafuate mkondo wake. Sifanyi kazi yoyote inayowalazimisha watu wayafanye maneno Yangu kuwa msingi wa uwepo wao. Kwa hivyo wale ambao hawajawahi kuwa na dhamiri, na ambao uwepo wao haujawahi kuwa na thamani yoyote, hutupa kando maneno Yangu kwa ujasiri na kufanya wapendavyo baada ya kutazama kimya kimya jinsi mambo yanavyoenda. Wanaanza kuchukia ukweli na yote yanayotoka Kwangu, na wanakuwa na chuki kubwa hata zaidi kuhusu kukaa katika nyumba Yangu. Kwa ajili ya hatima yao, na ili kuepuka adhabu, watu hawa hukaa ndani ya nyumba Yangu kwa muda, hata wakitumikia. Hata hivyo, nia na matendo yao hayabadiliki kamwe. Hili linaongeza tamaa yao ya baraka, na kuongeza tamanio lao la kuingia katika ufalme mara moja na kubaki milele baada ya hapo—hata kuingia katika mbingu ya milele. Kadiri wanavyotamani siku Yangu ije hivi karibuni, ndivyo wanavyohisi zaidi kwamba ukweli umekuwa kizuizi, kikwazo katika njia yao. Wana hamu kubwa ya kuingia katika ufalme ili wafurahie milele baraka za ufalme wa mbinguni—yote hayo bila kuhitaji kufuatilia ukweli au kukubali hukumu na kuadibu na, zaidi ya yote, bila kuhitaji kujidhalilisha ndani ya nyumba Yangu na kufanya kama Ninavyoamuru. Watu hawa wanaingia katika nyumba Yangu si ili kuridhisha matamanio yao ya kutafuta ukweli, wala kushirikiana na usimamizi Wangu; lengo lao ni kuwa tu miongoni mwa wale ambao hawaangamizwi katika enzi itakayokuja. Kwa hivyo mioyo yao haijawahi kujua ukweli ni nini, au jinsi ya kuukubali ukweli. Hii ndiyo sababu watu kama hao hawajawahi kutenda ukweli au kutambua kina cha upotovu wao, na bado wamekaa katika nyumba Yangu kama “watumishi” wakati wote. Wao husubiri “kwa uvumilivu” kuja kwa siku Yangu na hawachoki wanaporushwa huku na kule na namna ya kazi Yangu. Lakini haijalishi juhudi zao ni kubwa kiasi gani au wanalipa gharama gani, hakuna mtu ambaye amewahi kuwaona wakiteseka kwa ajili ya ukweli au kutoa chochote kwa ajili Yangu. Mioyoni mwao, wana hamu kubwa ya kuona siku Ninapoitamatisha enzi ya zamani na, zaidi ya hayo, hawawezi kusubiri kujua jinsi nguvu na mamlaka Yangu yalivyo makuu. Kile ambacho hawajawahi kufanya kwa haraka ni kujibadilisha wenyewe na kufuatilia ukweli. Wanapenda kile Ninachokichukia, na wanachukia kile Ninachokipenda. Wanatamani kile Ninachokichukia, lakini wanaogopa kupoteza kile Ninachokichukia sana. Wanaishi katika ulimwengu huu mwovu, bila kuuchukia kamwe, na bado wanaogopa sana kwamba Nitauangamiza. Katikati ya nia zao zinazokinzana, wanaupenda ulimwengu huu Ninaouchukia sana, lakini pia wanatamani Niuangamize haraka iwezekanavyo, ili waweze kuepushwa na janga la maangamizi na kugeuka mara moja kuwa mabwana wa enzi itakayokuja, kabla hawajaondoka katika njia ya kweli. Hii ni kwa sababu hawaupendi ukweli na wanachukia yote yanayotoka Kwangu. Wanaweza kuwa “watu watiifu” kwa muda mfupi kwa ajili ya kutopoteza baraka, lakini shauku yao ya kubarikiwa, na hofu ya kuangamia na kuingia katika ziwa la moto unaowaka, haviwezi kufichwa kamwe. Siku Yangu inapokaribia, tamanio lao linazidi kuwa na nguvu. Na kadiri janga linavyokuwa kubwa, ndivyo linavyowaacha wasijue la kufanya, wasijue pa kuanzia ili wanifanye Nifurahi na waepuke kupoteza baraka ambazo wamezitamani kwa muda mrefu. Watu kama hao wana hamu ya kuchukua hatua ili kuhudumu kama kikosi cha mbele punde tu mkono Wangu unapoanza kazi yake. Wanafikiria tu kukimbilia mstari wa mbele kabisa wa majeshi, wakiogopa sana kwamba Sitawaona. Wanafanya na kusema kile wanachofikiri kuwa sahihi, bila kujua kamwe kwamba matendo na vitendo vyao havijawahi kuhusiana na ukweli, na kwamba matendo yao yanahujumu na kusumbua tu mpango Wangu. Wanaweza kuwa wameweka juhudi kubwa, na wanaweza kuwa wa kweli katika azimio na nia yao ya kuvumilia magumu, lakini hakuna wanachofanya kinachohusiana na Mimi, kwa maana Sijawahi kuona kwamba matendo yao yanafanywa kwa nia njema, sembuse kuwaona wakiweka chochote juu ya madhabahu Yangu. Haya ndiyo matendo ambayo wamefanya mbele Yangu kwa miaka hii mingi.

Mwanzoni, Nilitamani kuwakimu ninyi kwa ukweli zaidi, lakini Nimelazimika kujizuia kufanya hivi kwa sababu mtazamo wenu kuelekea ukweli ni baridi na wa kutojali mno; Sitaki damu ya moyo Wangu ipotee bure, wala Sitaki kuona watu wakishikilia maneno Yangu lakini katika mambo yote wakifanya kile kinachonipinga, kunikashifu, na kunikufuru. Kwa sababu ya mitazamo yenu na ubinadamu wenu, Ninawapatia ninyi sehemu ndogo tu ya maneno Yangu na ambayo kwenu ni sehemu muhimu sana, ambayo inatumika kama kazi Yangu ya majaribu miongoni mwa wanadamu. Sasa tu ndipo Nimethibitisha kweli kwamba maamuzi na mpango Nilivyovifanya vinakidhi mahitaji yenu, na Nimethibitisha hata zaidi kwamba mtazamo Wangu kuwaelekea binadamu ni ule sahihi. Miaka yenu mingi ya mwenendo mbele Yangu imenipa jibu ambalo halijawahi kutokea, na swali la jibu hili ni: “Mtazamo wa mwanadamu mbele ya ukweli na Mungu wa kweli ni upi?” Damu ya moyo ambayo Nimemwaga kwa ajili ya mwanadamu inathibitisha kiini Changu cha upendo kwa mwanadamu, na vitendo na matendo ya mwanadamu mbele Yangu vinathibitisha kiini chake cha kuchukia ukweli na kuwa na uadui Kwangu. Wakati wote, Ninawajali wote walionifuata, lakini hakuna wakati ambapo wale wanaonifuata wanaweza kukubali maneno Yangu; hawawezi hata kukubali mapendekezo Yangu. Hili ndilo linalonihuzunisha zaidi ya yote. Hakuna mtu ambaye amewahi kuweza kunielewa, sembuse mtu yeyote kuweza kunikubali, hata ingawa mtazamo Wangu ni wa dhati, na maneno Yangu ni ya upole. Kila mtu anafanya kazi Niliyomwagiza kulingana na nia zake mwenyewe, bila kutafuta nia Zangu, sembuse kuuliza kile Ninachotaka kutoka kwake. Bado wanadai kunitumikia kwa uaminifu, huku wote wakiniasi. Wengi wanaamini kwamba ukweli ambao haukubaliki kwao au ambao hawawezi kuutenda si ukweli. Ndani ya watu kama hao, ukweli Wangu unakuwa kitu kinachokanushwa na kutupwa kando. Wakati huo huo, watu wananikubali kama Mungu kwa maneno, lakini pia wananiamini kuwa mtu wa nje ambaye si ukweli, njia, au uzima. Hakuna anayejua ukweli huu: Maneno Yangu ni ukweli usiobadilika milele; Mimi ndimi ruzuku ya uzima wa mwanadamu na kiongozi pekee kwa wanadamu; thamani na maana ya maneno Yangu haviamuliwi na iwapo yanakubaliwa na kupokelewa na wanadamu, bali na kiini cha maneno yenyewe; na hata kama hakuna mtu hata mmoja duniani anayeweza kukubali maneno Yangu, thamani ya maneno Yangu na msaada wa maneno hayo kwa wanadamu haviwezi kukadiriwa na mwanadamu yeyote. Kwa hivyo, Ninapokabiliwa na watu wengi wanaoasi dhidi ya, wanaokanusha, au wanaodharau kabisa maneno Yangu, mtazamo Wangu ni huu tu: Acha muda na ukweli wa mambo viwe mashahidi Wangu na vithibitishe kwamba maneno Yangu ni ukweli, njia, na uzima. Acha vithibitishe kwamba yote Niliyosema ni sahihi, kwamba ni kile ambacho mwanadamu anapaswa kuwa nacho na, hata zaidi, kile ambacho mwanadamu anapaswa kukubali. Nitawajulisha wote wanaonifuata ukweli huu: Wale ambao hawawezi kukubali kikamilifu maneno Yangu, wale ambao hawawezi kutenda maneno Yangu, wale ambao hawawezi kupata lengo katika maneno Yangu, na wale ambao hawawezi kupokea neema ya wokovu kupitia maneno Yangu, ni wale wanaohukumiwa na maneno Yangu; hata zaidi, wao ni wale ambao wamepoteza neema ya wokovu Wangu, na fimbo Yangu haitawaacha kamwe.

Aprili 16, 2003

Iliyotangulia: Tatizo Kubwa Sana: Usaliti (2)

Inayofuata: Mungu Ndiye Chanzo cha Uzima wa Mwanadamu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp