Majani Yanayoanguka Yanaporudi Kwenye Mizizi Yake, Utajutia Maovu Yote Ambayo Umefanya
Ninyi nyote mmeona kwa macho yenu wenyewe kazi Niliyofanya miongoni mwenu, ninyi wenyewe mmesikiliza maneno Niliyonena, na ninyi nyote mmejua mtazamo Wangu kuwaelekea ninyi, kwa hivyo mnapaswa kujua kwa nini Ninafanya kazi hii kwenu. Ninawaambia kwa dhati kabisa, ninyi si chochote ila vyombo kwa ajili ya kazi Yangu ya ushindi katika siku za mwisho, vifaa vya kueneza kazi Yangu miongoni mwa nchi za Mataifa. Ninanena kupitia ukosefu wenu wa haki, uchafu, upinzani, na uasi wenu ili kueneza vyema zaidi kazi Yangu, na ili jina Langu liweze kuenezwa miongoni mwa Mataifa, yaani, kuenezwa miongoni mwa taifa lolote nje ya Israeli. Hii ni ili jina Langu, matendo Yangu, na sauti Yangu viweze kuenezwa kote katika Mataifa, na hivyo mataifa hayo yote ambayo si ya Israeli yaweze kushindwa na Mimi na yaweze kuniabudu Mimi, yawe nchi Zangu takatifu nje ya nchi za Israeli na Misri. Kuenezwa kwa kazi Yangu kwa kweli ni kuenezwa kwa kazi Yangu ya ushindi na upanuzi wa nchi Yangu takatifu; ni upanuzi wa mahali Pangu pa kidato cha uthabiti duniani. Mnapaswa kuelewa wazi kwamba ninyi ni viumbe walioumbwa tu Ninaowashinda miongoni mwa Mataifa. Mwanzoni, hamkuwa na hadhi wala thamani yoyote ya kutumiwa, na hamkuwa na faida yoyote kabisa. Ni kwa sababu tu Niliwainua funza kutoka kwenye lundo la samadi ili wawe vielelezo vya ushindi Wangu wa nchi nzima, kuwa "vifaa vya marejeleo" pekee kwa ajili ya ushindi Wangu wa nchi nzima, ndiyo maana mmekuwa na bahati ya kutosha kukutana na Mimi, na kukusanyika pamoja na Mimi sasa. Ni kwa sababu ya hadhi yenu ya chini ndiyo maana Nimewachagua ninyi muwe vielelezo na mifano ya kazi Yangu ya ushindi. Ni kwa sababu hii tu ndiyo maana Ninafanya kazi na kunena miongoni mwenu, na kwamba Ninaishi na kukaa pamoja nanyi kwa muda. Mnapaswa kujua kwamba ni kwa sababu ya usimamizi Wangu na kutokana na chuki Yangu kuu kwa funza walio katika lundo la samadi ndiyo maana Ninanena miongoni mwenu—imefikia hatua kwamba Nina ghadhabu. Kufanya kazi Kwangu miongoni mwenu si sawa kabisa na utendaji kazi wa Yehova katika Israeli, na hata zaidi si sawa na utendaji kazi wa Yesu katika Yudea. Ninanena na kufanya kazi kwa uvumilivu mkuu, na ni kwa hasira na vile vile hukumu ndiyo Ninawashinda wapotovu hawa. Ni tofauti kabisa na Yehova kuwaongoza watu Wake katika Israeli. Kazi Yake katika Israeli ilikuwa kuwajalia chakula na maji ya uzima, na Alikuwa amejaa rehema na wema kwa watu Wake huku Akiwaruzuku. Kazi ya leo inafanywa miongoni mwa taifa lililolaaniwa la watu ambao hawajachaguliwa. Hakuna chakula kingi, wala hakuna lishe ya kukata kiu ya maji ya uzima, na sembuse utoaji wa bidhaa nyingi za maada; kuna tu utoaji wa hukumu, laana, na kuadibu kwingi. Funza hawa wanaoishi katika lundo la samadi hawastahili kabisa kupata milima iliyojaa ng'ombe na kondoo, utajiri mkuu, na watoto wazuri zaidi katika nchi yote, kama vile Nilivyoijalia Israeli. Israeli ya sasa inatoa juu ya madhabahu sadaka ya ng'ombe na kondoo na vitu vya dhahabu na fedha ambavyo kwavyo Ninawalisha watu wake, ikizidi sehemu ya kumi iliyohitajika na Yehova chini ya sheria, na hivyo Nimewapa hata zaidi—zaidi ya mara mia moja ya kile kilichopatwa na Israeli chini ya sheria. Kile ambacho Ninailisha Israeli nacho kinazidi yote ambayo Ibrahimu alipata, na yote ambayo Isaka alipata. Nitaifanya familia ya Israeli izaane na iongezeke, na Nitawafanya watu Wangu wa Israeli waenee kote duniani. Wale Ninaowabariki na kuwatunza bado ni watu wateule wa Israeli—yaani, watu wanaonitolea kila kitu ambacho wamepata kutoka Kwangu. Ni kwa sababu wananiweka akilini ndiyo maana wanatoa dhabihu ya ndama na wanakondoo wao wazaliwa wa kwanza kwenye madhabahu Yangu takatifu na kutoa kila kitu walicho nacho mbele Yangu, hata kufikia hatua ya kutoa wana wao wa kwanza waliozaliwa karibuni kwa kutarajia kurudi Kwangu. Na ninyi, je? Mnachochea hasira Yangu, mnatoa matakwa Kwangu, na mnaiba dhabihu za wale wanaotoa vitu Kwangu, na hamjui kwamba mnanikosea Mimi; hivyo, yote mnayopata ni kilio na adhabu gizani. Mmechochea hasira Yangu mara nyingi, na Nimenyesha kutoka juu moto Wangu unaowaka kiasi kwamba watu wasio wachache wamefikia mwisho wa kuhuzunisha, na nyumba zenye furaha zimekuwa makaburi yenye ukiwa. Kile Nilicho nacho kwa funza hawa ni hasira isiyo na mwisho tu, na Sina nia ya kuwabariki. Ni kwa ajili ya kazi Yangu tu ndiyo maana Nimefanya jambo la kipekee na kuwainua ninyi, na kuvumilia fedheha kuu na kufanya kazi miongoni mwenu. Isingekuwa kwa ajili ya mapenzi ya Baba Yangu, Ningewezaje kuishi katika nyumba moja na funza wanaobiringika katika lundo la samadi? Ninahisi chuki kuu kwa matendo na maneno yenu yote, na hata hivyo, kwa sababu Nina "raghba" fulani katika uchafu na uasi wenu, huu umekuwa mkusanyiko mkuu wa maneno Yangu. Vinginevyo, Nisingebaki kabisa miongoni mwenu kwa muda mrefu hivi. Kwa hivyo, mnapaswa kujua kwamba mtazamo Wangu kwenu ni wa huruma na kuonea huruma, bila hata tone la upendo, na kile Nilicho nacho kwenu ni uvumilivu tu, kwa sababu Ninafanya hili kwa ajili tu ya kazi Yangu. Na mmeona matendo Yangu kwa sababu tu Nimechagua uchafu na uasi kama "mali ghafi"; vinginevyo, Nisingedhihirisha kabisa matendo Yangu kwa funza hawa. Ninafanya kazi kwenu shingo upande tu, tofauti kabisa na utayari na hiari Niliyokuwa nayo Nilipofanya kazi Yangu katika Israeli. Ninavumilia hasira Yangu huku Nikijilazimisha kunena miongoni mwenu. Isingekuwa kwa ajili ya kazi Yangu kuu zaidi, macho Yangu yangewezaje kuvumilia kuendelea kuwepo kwa funza kama hao? Isingekuwa kwa ajili ya jina Langu, Ningekuwa nimepanda mpaka upeo wa juu kitambo na kuwateketeza kabisa funza hawa pamoja na lundo lao la samadi! Isingekuwa kwa ajili ya utukufu Wangu, Ningewezaje kuwaruhusu pepo hawa waovu wanipinge waziwazi wakitikisa vichwa vyao mbele ya macho Yangu? Isingekuwa kwa ajili ya kazi Yangu kutekelezwa vizuri bila kizuizi chochote hata kidogo, Ningewezaje kuwaruhusu watu hawa walio kama funza wanidhulumu kiholela? Kama watu mia moja katika kijiji nchini Israeli wangeinuka kunipinga hivi, hata kama wangenitolea sadaka, bado Ningewafutilia mbali na kuwatupa chini katika nyufa ardhini ili kuzuia watu katika miji mingine wasipinge tena kamwe. Mimi ni moto unaoteketeza kila kitu na Sivumilii kosa. Kwa sababu wanadamu wote waliumbwa na Mimi, chochote Ninachosema na kufanya, lazima watii, na hawapaswi kupinga. Watu hawana haki ya kuingilia kazi Yangu, sembuse kuwa na sifa za kuchambua yaliyo sawa au makosa katika kazi Yangu na katika maneno Yangu. Mimi ni Muumba, na viumbe walioumbwa wanapaswa kutimiza kila kitu Ninachohitaji kwa moyo wa kuniogopa Mimi; hawapaswi kujaribu kubishana na Mimi, na hasa hawapaswi kupinga. Kwa mamlaka Yangu ninawatawala watu Wangu, na viumbe wote walioumbwa na Mimi wanapaswa kutii mamlaka Yangu. Ingawa leo ninyi ni wafidhuli na wenye kujidai mbele Yangu, ingawa mnayaasi maneno Ninayotumia kuwafundisha na hamjui kuwa na hofu, Ninakabili uasi wenu kwa uvumilivu tu; Sitalipuka kwa hasira kwa sababu funza wadogo, wasio na maana wamekoroga samadi, Nikiiacha kazi Yangu iathirike. Ninavumilia kuendelea kuwepo kwa kila kitu Ninachokichukia na vitu vyote Ninavyokirihi kwa ajili ya mapenzi ya Baba Yangu, na Nitafanya hivyo hadi matamko Yangu yakamilike, hadi wakati Wangu wa mwisho kabisa. Usiwe na wasiwasi! Sitashuka hadi kiwango sawa na funza asiye na jina, na Sitalinganisha ustadi Wangu na wako. Ninakuchukia, lakini Ninaweza kuvumilia. Unaniasi, lakini huwezi kuepuka siku ambayo Nitakuadibu, ambayo Niliahidiwa na Baba Yangu. Je, funza aliyeumbwa anaweza kumshinda Muumba? Katika majira ya kupukutika, majani yanayoanguka yanarudi kwenye mizizi yake; utarudi nyumbani kwa "baba" yako, na Mimi Nitarudi kando ya Baba Yangu. Nitaambatana na upendo Wake mwororo, nawe utafuatwa na kukanyagwa na baba yako. Nitakuwa na utukufu wa Baba Yangu, nawe utakuwa na aibu ya baba yako. Nitatumia kuadibu ambako Nimekuwa nikizuia kwa muda mrefu kuandamana na wewe, nawe utakutana na kuadibu Kwangu ukiwa na mwili wako unaonuka ambao umekuwa mpotovu kwa makumi ya maelfu ya miaka. Nitakuwa nimehitimisha juu yako kazi Yangu ya maneno inayoambatana na uvumilivu, nawe utaanza kutimiza jukumu la kuteseka kwa ole lililozungumziwa katika maneno Yangu. Nitafurahi sana na kufanya kazi katika Israeli; utalia na kusaga meno yako, ukiwepo na kufia matopeni. Nitarudia umbo Langu la asili na Sitabaki tena katika uchafu pamoja nawe, huku wewe ukirudia ubaya wako wa asili na kuendelea kuchimbachimba katika lundo la samadi. Kazi na maneno Yangu yatakapokamilika, itakuwa siku ya furaha Kwangu. Upinzani na uasi wako utakapokwisha, itakuwa siku ya kilio kwako. Sitakuhurumia, na hutaniona tena kamwe. Sitafanya mazungumzo nawe tena, na hutakutana na Mimi tena kamwe. Nitachukia uasi wako, nawe utakumbuka uzuri Wangu. Nitakupiga, nawe utanikumbuka. Nitaondoka kwako kwa furaha, nawe utahisi kuwa mdeni Wangu. Sitakuona tena kamwe, lakini utanitamani daima. Nitakuchukia kwa sababu unanipinga sasa hivi, nawe utanikumbuka kwa sababu Ninakuadibu sasa hivi. Sitakuwa radhi kuishi pamoja nawe, lakini utatamani sana jambo hilo kwa uchungu na kulia hata milele, kwa maana utajutia yote ambayo umenitendea. Utahisi majuto kwa sababu ya uasi na upinzani wako, hata utalala kifudifudi ardhini kwa majuto na kuanguka mbele Yangu na kuapa kutoniasi tena kamwe. Hata hivyo, moyoni mwako, utanipenda Mimi tu, lakini hutaweza kamwe kuisikia sauti Yangu. Nitakufanya uhisi aibu kujihusu.
Sasa Ninautazama mwili wako unaoendekeza anasa ambao unajaribu kunibembeleza kwa hila, na Nina onyo dogo tu kwako, ingawa "Sitakuhudumia" kwa kuadibu. Unapaswa kujua ni jukumu gani unalotekeleza katika kazi Yangu, na kisha Nitaridhika. Katika mambo yaliyo nje ya haya, ukinipinga au utumie pesa Zangu, au ule dhabihu zilizotolewa kwa ajili Yangu, Yehova, au ninyi funza mkiumana, au ikiwa ninyi viumbe kama mbwa mnazozana au kudhulumiana—Sijali lolote kuhusu hayo. Mnapaswa tu kujua ninyi ni vitu vya aina gani, na Nitaridhika. Kando na haya yote, ikiwa mnataka kutoleana silaha au kupigana kwa maneno, hiyo ni sawa; Sina hamu ya kuingilia mambo kama hayo, na mambo ya binadamu hayana uhusiano wowote na Mimi kabisa. Si kwa sababu Sijali kuhusu mizozo kati yenu, bali ni kwa sababu Mimi si mmoja wenu, ndiyo maana Sishiriki katika mambo yaliyo kati yenu. Mimi Mwenyewe si kiumbe aliyeumbwa na si wa ulimwengu, kwa hivyo Ninachukia maisha ya pilikapilika ya watu na mahusiano ya fujo, yasiyofaa kati yao. Ninachukia hasa umati wenye kelele. Hata hivyo, Nina ujuzi wa kina wa uchafu katika mioyo ya kila kiumbe aliyeumbwa, na kabla Sijawaumba ninyi, tayari Nilijua kuhusu ukosefu wa haki uliokuwepo kilindini mwa moyo wa mwanadamu, na Nilijua udanganyifu na upotovu wote katika moyo wa mwanadamu. Kwa hivyo, ingawa hakuna dalili zozote kabisa wakati watu wanatenda mambo yasiyo ya haki, bado Ninajua kwamba ukosefu wa haki uliofichika ndani ya mioyo yenu unazidi utajiri wa vitu vyote Nilivyoviumba. Kila mmoja wenu ameinuka hadi kileleni mwa umati; mmeinuka hadi kuwa mababu wa umati. Ninyi hufanya mambo kiholela mno, na mnakimbia huku na kule kwa fujo miongoni mwa funza wote, mkitafuta mahali pa starehe na kufikiri kwa kujidanganya kuwameza funza ambao ni wadogo kuliko ninyi. Ninyi ni wenye nia ya uovu na wenye hila mioyoni mwenu, mkiizidi mizimu ambayo imezama hadi chini ya bahari. Mnakaa katika sehemu ya chini kabisa ya samadi, mkiwasumbua funza kutoka juu hadi chini hadi wanakosa amani, mkipigana kwa muda na kisha kutulia. Hamjui nafasi yenu, lakini bado mnapigana ninyi kwa ninyi ndani ya samadi. Mnaweza kupata nini kutokana na mapambano kama hayo? Kama kweli mngekuwa na mioyo inayoniogopa Mimi, mngewezaje kushindana ninyi kwa ninyi nyuma Yangu? Haijalishi hadhi yako ni ya juu kiasi gani, je, si wewe bado ni mdudu mdogo anayenuka ndani ya samadi? Je, utaweza kuota mabawa na kuwa njiwa angani? Ninyi wadudu wadogo mnaonuka mnaiba matoleo kutoka kwenye madhabahu Yangu Mimi, Yehova; kwa kufanya hivyo, je, mnaweza kuokoa sifa yenu iliyoharibiwa, iliyoangamizwa na kuwa watu wateule wa Israeli? Ninyi ni watu duni wasio na aibu! Dhabihu hizo zilizo kwenye madhabahu zilitolewa Kwangu na watu, kama ishara ya upendo kutoka kwa wale wanaoniogopa Mimi. Ziko chini ya udhibiti Wangu na kwa matumizi Yangu, kwa hivyo unawezaje kunipokonya hua wadogo ambao watu wamenipa Mimi? Je, huogopi kuwa Yuda? Je, huogopi kwamba ardhi yako inaweza kuwa uwanja wa damu? Wewe kiumbe usiye na aibu! Je, unafikiri kwamba hua waliotolewa na watu ni kwa ajili ya kulisha tumbo lako wewe funza? Kile Nilichokupa ni kile Ninachoridhika na kuwa tayari kukupa; kile ambacho Sijakupa kinapaswa kuwa chini ya uamuzi Wangu. Hupaswi kamwe kuiba matoleo Yangu. Yule anayefanya kazi ni Mimi, Yehova—Muumba—na watu wanatoa dhabihu kwa sababu Yangu. Je, unafikiri hii ni fidia kwa ajili ya kukimbia kwako huku na kule? Wewe kwa kweli huna aibu! Unakimbia huku na kule kwa ajili ya nani? Je, si kwa ajili yako mwenyewe? Kwa nini unaiba sadaka Zangu? Kwa nini unaiba pesa kutoka kwenye mfuko Wangu wa pesa? Je, wewe si mwana wa Yuda Iskariote? Sadaka Kwangu, Yehova, zinapaswa kufurahiwa na makasisi. Je, wewe ni kasisi? Unathubutu kula sadaka Zangu kwa majivuno, na hata kuziweka mezani; wewe huna thamani yoyote! Wewe mtu duni usiye na thamani! Moto Wangu, moto wa Yehova, utakuteketeza!