Kuhusu “Imani”, Uelewa Wako ni Upi?

Ndani ya mwanadamu mna neno tu “imani” linaloonekana kuwepo na kuonekana kutokuwepo, lakini mwanadamu hajui ni nini hasa kinachojumuisha imani, sembuse kwa nini anapaswa kuwa nayo. Mwanadamu anaelewa kidogo sana, na mwanadamu anapungukiwa sana; imani yake Kwangu ni ya kishenzi na ya kijinga tu. Ingawa hajui imani ni nini, wala kwa nini ana imani Kwangu, anaendelea kushikilia imani Kwangu. Kile Ninachotaka kutoka kwa mwanadamu sio tu kwamba ashikilie kuniita Mimi kwa njia hii au kuwa na imani Kwangu kwa mtindo usio na taratibu, kwa maana kazi Ninayofanya ni ili mwanadamu aweze kuniona Mimi, na kunijua Mimi, si ili mwanadamu anitazame Mimi kwa mtazamo mpya. Niliwahi kudhihirisha ishara na maajabu mengi na kufanya miujiza mingi, na Waisraeli wa wakati huo walivutiwa na Mimi sana na waliheshimu sana nguvu Zangu za kipekee za kuponya wagonjwa na kuondosha pepo. Wakati huo, Wayahudi waliona nguvu Zangu za kuponya kuwa za ustadi sana, za kipekee—na kwa sababu Nimefanya kazi nyingi sana, wote waliniheshimu Mimi, na walionea wivu sana nguvu Zangu zote. Hivyo, wote walioniona Nikitenda miujiza walinifuata kwa karibu, kiasi kwamba maelfu walinizunguka kunitazama Nikiponya wagonjwa. Nilidhihirisha ishara na maajabu mengi sana, lakini watu walinitazama tu kama tabibu stadi; vivyo hivyo, Nilinena maneno mengi ya mafundisho kwa watu wakati huo, lakini walinichukulia tu kama mwalimu aliye bora kuliko wanagenzi wake. Hata leo, baada ya watu kuona rekodi za kihistoria za kazi Yangu, fasiri yao inaendelea kuwa kwamba Mimi ni tabibu mkuu anayeponya wagonjwa na mwalimu kwa wajinga, na wameniwekea mipaka kuwa Bwana Yesu Kristo mwenye rehema. Wale wanaotafsiri Maandiko wanaweza kuwa walizidi “ustadi” Wangu katika kuponya, au wanaweza hata kuwa wanagenzi ambao sasa wamemzidi mwalimu wao, lakini watu kama hao wenye sifa kuu, ambao majina yao yanajulikana ulimwenguni kote, wananichukulia kwa njia duni sana kuwa tabibu tu. Matendo Yangu ni mengi sana, ni mengi kwa idadi kuliko chembe za mchanga wa ufukoni, na hekima Yangu ni kuu sana, inazidi ile ya wana wote wa Sulemani, lakini watu wananiamini tu kana kwamba Mimi ni tabibu asiye na maana na mwalimu asiyejulikana wa mwanadamu. Wengi sana wananiamini Mimi ili tu Niwaponye. Wengi sana wananiamini Mimi ili tu Nitumie nguvu Zangu kutoa roho wachafu kutoka katika miili yao, na wengi sana wananiamini Mimi ili tu wapate amani na furaha kutoka Kwangu. Wengi sana wananiamini Mimi ili tu kudai kutoka Kwangu utajiri mkubwa zaidi wa kidunia. Wengi sana wananiamini Mimi ili tu waishi maisha haya kwa amani na kuwa salama salimini katika maisha yafuatayo. Wengi sana wananiamini Mimi ili kuepuka mateso ya jahanamu na kupokea baraka za mbinguni. Wengi sana wananiamini Mimi kwa ajili ya faraja ya muda tu, lakini hawatafuti kupata chochote katika maisha yafuatayo. Ninapowamwagia watu hasira Yangu na kuchukua furaha na amani yote waliyokuwa nayo hapo awali, wanakuwa na shaka. Ninapowapa watu mateso ya jahanamu na kuchukua tena baraka za mbinguni, wanashikwa na ghadhabu. Watu wanaponiomba Niwaponye, na Mimi siwajali na kuwachukia, wanaondoka kutoka Kwangu ili badala yake watafute njia ya dawa za uovu na uchawi. Ninapoondoa yote ambayo watu wamedai kutoka Kwangu, wote wanatoweka bila kupatikana. Hivyo, Ninasema kwamba watu wana imani Kwangu kwa sababu neema Yangu ni tele sana, na kwa sababu kuna faida nyingi mno za kupata. Watu wa nyumba ya Wayahudi waliniamini Mimi kwa sababu ya neema Yangu na walinifuata popote Nilipoenda. Watu hawa wajinga wenye maarifa na uzoefu mdogo walitafuta tu kutazama ishara na maajabu Niliyodhihirisha. Walinichukulia kama kichwa cha nyumba ya Wayahudi ambaye angeweza kufanya miujiza mikuu kabisa. Na hivyo Nilipofukuza mapepo kwa ajili ya watu, ilisababisha mjadala mwingi miongoni mwao: Walisema kwamba Mimi nilikuwa Eliya, kwamba Mimi nilikuwa Musa, kwamba Mimi nilikuwa wa kale zaidi kati ya manabii wote, kwamba Mimi nilikuwa mkuu zaidi kati ya matabibu wote. Mbali na Mimi Mwenyewe kusema kwamba Mimi ndimi uzima, njia, na ukweli, hakuna ambaye angeweza kujua nafsi Yangu au utambulisho Wangu. Mbali na Mimi Mwenyewe kusema kwamba mbinguni ndipo mahali anapoishi Baba Yangu, hakuna aliyejua kwamba Mimi ni Mwana wa Mungu, na pia Mungu Mwenyewe. Mbali na Mimi Mwenyewe kusema kwamba Nitawaletea binadamu wote ukombozi na kuwakomboa wanadamu, hakuna aliyejua kwamba Mimi ni Mkombozi wa wanadamu, na watu walinijua tu kama mtu mkarimu na mwenye rehema. Na mbali na Mimi Mwenyewe kuweza kueleza ukamilifu wa kile Nilicho, hakuna aliyenijua, na hakuna aliyeamini kwamba Mimi ni Mwana wa Mungu aliye hai. Hiyo ndiyo imani ya watu Kwangu, na jinsi wanavyojaribu kunidanganya Mimi. Wangewezaje kuwa na ushuhuda Kwangu wanapokuwa na maoni kama hayo kunihusu Mimi?

Watu wananiamini Mimi, lakini hawana uwezo wa kuwa na ushuhuda Kwangu, wala hawawezi kuwa na ushuhuda Kwangu kabla ya Mimi Mwenyewe kufunua. Watu wanaona tu kwamba Ninazidi viumbe walioumbwa na watu wote watakatifu, na wanaona kwamba kazi Ninayofanya haiwezi kufanywa na mwanadamu. Hivyo, kuanzia Wayahudi hadi watu wa wakati wa sasa, wote wanaoona matendo Yangu matukufu wamejawa na udadisi tu kunihusu Mimi, lakini hakuna kinywa cha kiumbe aliyeumbwa hata mmoja ambacho kimeweza kuwa na ushuhuda Kwangu. Baba Yangu pekee ndiye aliyenishuhudia Mimi, na kunitengenezea njia miongoni mwa viumbe wote walioumbwa; kama Asingefanya hivyo, haijalishi Nilifanya kazi vipi, mwanadamu asingewahi kujua kwamba Mimi ni Muumba, kwa maana mwanadamu anajua tu kuchukua kutoka Kwangu na hana imani Kwangu kutokana na kazi Yangu. Mwanadamu ananijua Mimi tu kwa sababu Mimi sina hatia na si mwenye dhambi hata kidogo, kwa sababu Ninaweza kueleza siri nyingi, kwa sababu Niko juu ya wengi, au kwa sababu mwanadamu amefaidika kutoka Kwangu, lakini ni wachache wanaoamini kwamba Mimi ni Muumba. Hii ndiyo sababu Ninasema kwamba mwanadamu hajui kwa nini anapaswa kuwa na imani Kwangu; hajui kusudi au umuhimu wa kuwa na imani Kwangu. Uhalisi wa mwanadamu unapungukiwa sana, kiasi kwamba hastahili hata kuwa na ushuhuda Kwangu. Mna imani ya kweli kidogo sana, na mmepata kidogo sana, kwa hivyo mna ushuhuda mdogo sana. Zaidi ya hayo, mnaelewa kiasi kidogo sana na mnapungukiwa mno, kiasi kwamba karibu kabisa mnakosa kile kinachohitajika ili kuweza kuwa na ushuhuda kwa matendo Yangu. Azimio lenu kwa kweli ni kubwa, lakini, je, kweli mnaweza kuwa na uhakika kwamba mtaweza kuwa na ushuhuda kwa kiini cha Mungu? Kile ambacho mmepitia na kuona kinazidi kile cha watakatifu na manabii kutoka enzi zote, lakini, je, mnaweza kutoa ushuhuda Kwangu ulio mkuu kuliko maneno ya hawa watakatifu na manabii wa nyakati za zamani? Kile Ninachowapa sasa kinazidi kile Nilichompa Musa na Daudi, hivyo vivyo hivyo Ninaomba kwamba ushuhuda wenu uzidi ule wa Musa na kwamba maneno yenu yazidi yale ya Daudi. Ninawapa mara mia—hivyo vivyo hivyo Ninawaomba mnilipe Mimi mara mia. Lazima mjue Mimi ndimi Ninayewapa binadamu uzima, na ni ninyi mnaopokea uzima kutoka Kwangu na lazima muwe na ushuhuda Kwangu. Huu ni wajibu wenu ambao Ninawashushia na ambao mnapaswa kunifanyia Mimi. Nimewapa utukufu Wangu wote, Nimewapa uzima ambao watu wateule wa Israeli hawakuwahi kupokea. Mnapaswa kuwa na ushuhuda Kwangu na mnitolee ujana wenu na kuyatoa maisha yenu Kwangu. Yeyote Ninayempa utukufu Wangu atakuwa na ushuhuda na kuyatoa maisha yake kwa ajili Yangu—hili limeamuriwa kimbele na Mimi kitambo. Ni baraka kwamba Ninawapa utukufu Wangu, na ni wajibu wenu kuwa na ushuhuda kwa utukufu Wangu. Kama mngeniamini kwa ajili ya baraka tu, basi kazi Yangu ingekuwa na umuhimu mdogo, na hamgekuwa mnafanya wajibu wenu. Waisraeli waliona tu rehema Yangu, wema Wangu, na ukuu Wangu, na Wayahudi walishuhudia tu uvumilivu Wangu na ukombozi Wangu. Waliona kidogo mno kuhusu kazi ya Roho Wangu, na hata ikawa kwamba kile walichoelewa kilikuwa tu sehemu moja ya elfu kumi ya kile ambacho mmesikia na kuona. Kile ambacho mmeona kinazidi hata kile ambacho makasisi wakuu miongoni mwao wameona. Ukweli mnaouelewa leo unazidi ule waliouelewa; kile ambacho mmeona leo kinazidi kile kilichoonekana katika Enzi ya Sheria, na pia Enzi ya Neema, na kile ambacho mmepitia kinazidi hata kile ambacho Musa na Eliya walipitia. Kwa maana kile ambacho Waisraeli walielewa kilikuwa tu sheria ya Yehova, na kile walichoona kilikuwa tu mwonekano wa mgongo wa Yehova; kile ambacho Wayahudi walielewa kilikuwa tu ukombozi wa Yesu, kile walichopokea kilikuwa tu neema iliyotawazwa na Yesu, na kile walichoona kilikuwa tu mfano wa Yesu ndani ya nyumba ya Wayahudi. Kile ambacho mnaona leo ni utukufu wa Yehova, ukombozi wa Yesu, na matendo yote Ninayoyafanya sasa. Pia mnasikia kwa masikio yenu wenyewe maneno ya Roho Wangu, na mmepata uthamini wa hekima Yangu, mmekuja kujua ajabu Yangu, na kufahamu tabia Yangu. Pia Nimewaambia mpango Wangu wote wa usimamizi. Kile ambacho mmeona sio tu Mungu mwenye upendo na rehema, bali Mungu aliyejawa na haki. Mmeona maajabu ya kazi Yangu na kuja kujua kwamba Nimejawa na uadhama na ghadhabu kabisa; hata zaidi mnatambua kwamba Niliwahi kushusha hasira Yangu kali juu ya nyumba ya Israeli, na kwamba sasa imekuja juu yenu. Mnafahamu zaidi kuhusu siri Zangu mbinguni kuliko Isaya na Yohana; mnajua zaidi kuhusu upendeza Kwangu na kuheshimika Kwangu kuliko watakatifu wote wa enzi zilizopita. Kile ambacho mmepokea sio tu ukweli Wangu, njia Yangu, na uzima Wangu, bali maono na ufunuo mkuu zaidi kuliko yale yaliyopokelewa na Yohana. Mnaelewa siri nyingi zaidi, na pia mmetazama uso Wangu wa kweli; mmekubali zaidi hukumu Yangu na mnajua zaidi kuhusu tabia Yangu ya haki. Na hivyo, ingawa mlizaliwa katika siku za mwisho, mnaelewa mambo yaliyotangulia na mambo ya zamani, na pia mmepitia mambo ya leo, ambayo yalifanywa na Mimi binafsi. Kile Ninachotaka si kilichozidi mno, kwa maana Nimewapa mengi sana, na mmeona mengi sana Kwangu. Hivyo, Ninawaomba mtoe ushuhuda kwa ajili Yangu kwa watakatifu wa enzi zilizopita, na hili ndilo tamanio pekee la moyo Wangu.

Ni Baba Yangu ndiye aliyenishuhudia Mimi hapo awali, lakini Ningependa kupata utukufu mkuu zaidi, na kwamba maneno ya ushuhuda yatoke vinywani mwa viumbe walioumbwa—kwa hivyo Ninawapa yote Niliyo nayo, ili mweze kutimiza wajibu wenu, ili kazi Yangu miongoni mwa wanadamu ifikie kikomo. Mnapaswa kufahamu kwa nini mnaniamini Mimi; kama mnataka tu kuwa “mwanagenzi” Wangu au “mgonjwa” Wangu, au kuwa mtakatifu Wangu mbinguni, basi kunifuata kwenu hakutakuwa na maana. Kunifuata kwa namna hiyo kungekuwa tu kupoteza nguvu; kuwa na imani ya aina hii Kwangu kungekuwa tu kupoteza siku zenu, kufuja ujana wenu. Na mwishowe, hamngepata chochote. Je, huko kusingekuwa kupiga hesabu bure? Nimeondoka miongoni mwa Wayahudi kitambo na Mimi si tabibu wa mwanadamu tena wala dawa nzuri kwa mwanadamu. Mimi si punda tena wa kuendeshwa au kuchinjwa na mwanadamu apendavyo; badala yake, Nimekuja miongoni mwa wanadamu ili kumhukumu na kumwadibu mwanadamu, ili mwanadamu aweze kunijua Mimi. Unapaswa kujua kwamba Niliwahi kufanya kazi ya ukombozi; Niliwahi kuwa Yesu, lakini Singeweza kubaki Yesu milele, kama vile tu Niliwahi kuwa Yehova lakini baadaye Nikawa Yesu. Mimi ni Mungu wa binadamu, Muumba, lakini Siwezi kubaki Yesu au Yehova milele. Nimekuwa kile ambacho mwanadamu anakichukulia kuwa tabibu, lakini hii haionyeshi kwamba Mungu ni tabibu tu kwa binadamu. Kwa hivyo, ikiwa unashikilia maoni ya zamani katika imani yako Kwangu, basi hutapata chochote. Haijalishi unanisifu vipi leo: “Mungu anampenda mwanadamu sana; Ananiponya na kunipa baraka, amani, na furaha. Mungu ni mwema sana kwa mwanadamu; maadamu tunamwamini Yeye, basi hatuhitaji kuwa na wasiwasi kuhusu pesa...,” Bado Siwezi kuvuruga kazi Yangu ya asili. Ikiwa unaniamini Mimi leo, utapokea tu utukufu Wangu na kuwa na haki ya kuwa na ushuhuda Kwangu, na kila kitu kingine kitakuwa cha baadaye. Hili lazima ulijue waziwazi.

Sasa, je, kweli unajua kwa nini unapaswa kuniamini Mimi? Je, kweli unajua kusudi na umuhimu wa kazi Yangu? Je, kweli unajua wajibu wako? Je, kweli unajua ushuhuda Wangu ni nini? Ikiwa unaniamini Mimi tu, lakini hakuna dalili yoyote ya utukufu au ushuhuda Wangu ndani yako, basi Nimekuondosha zamani sana. Na kwa wale wanaoelewa kila kitu, wao ni miiba zaidi katika jicho Langu, na katika nyumba Yangu, wao si chochote zaidi ya vikwazo katika njia Yangu, wao ni magugu ya kupepetwa kabisa katika kazi Yangu, wao ni nyangarika, hawana uzito wowote, na Nimewachukia kitambo. Mara nyingi hasira Yangu huwashukia wote walioondolea ushuhuda, na fimbo Yangu haiwaepuki kamwe. Nimewakabidhi mikononi mwa yule mwovu kitambo; wameondolea kabisa baraka Zangu. Siku itakapofika, kuadibiwa kwao kutakuwa kukali zaidi hata kuliko kule kwa wanawake wapumbavu, wakaidi. Leo, Ninafanya tu kazi ambayo ni wajibu Wangu kuifanya, Nikifunga ngano yote katika vitita, pamoja na hayo magugu. Hii ndiyo kazi Yangu leo. Magugu hayo yote yatapepetwa wakati wa upepetaji Wangu, kisha punje za ngano zitakusanywa ghalani, na magugu hayo ambayo yamepepetwa yatawekwa motoni ili yachomwe kuwa majivu. Kazi Yangu sasa ni kuwafunga watu wote katika vitita tu; yaani, kuwashinda kabisa. Kisha Nitaanza kupepeta ili kufunua matokeo ya watu wote. Na hivyo unapaswa kujua jinsi unavyopaswa kuniridhisha Mimi sasa, na jinsi unavyopaswa kuingia katika njia sahihi katika imani yako Kwangu. Kile Ninachotamani ni uaminifu na utii wako sasa, upendo wako na ushuhuda wako sasa. Hata kama hujui kwa wakati huu ushuhuda ni nini au upendo ni nini, unapaswa kuniletea yote uliyo nayo, na kunikabidhi hazina pekee ulizo nazo: uaminifu na utii wako. Unapaswa kujua kwamba ushuhuda wa ushindi Wangu kwa Shetani upo ndani ya uaminifu na utii wa mwanadamu, kama ulivyo ushuhuda wa ushindi Wangu kamilifu kwa mwanadamu. Wajibu wa imani yako Kwangu ni kuwa na ushuhuda Kwangu, kuwa mwaminifu Kwangu na si kwa mwingine yeyote, na kuwa mtiifu hadi mwisho. Kabla Sijaanza hatua inayofuata ya kazi Yangu, unapaswa kuwa na ushuhuda Kwangu vipi? Unapaswa kuwa mwaminifu na mtiifu Kwangu vipi? Je, utaonyesha kujitolea kwa jukumu lako, au utaacha tu? Je, afadhali utii kila mpango Wangu (hata kama ni kifo au maangamizi), au ukimbie njiani ili kuepuka kuadibu Kwangu? Ninakuadibu ili uweze kuwa na ushuhuda Kwangu, na uwe mwaminifu na mtiifu Kwangu. Inaweza pia kusemwa kwamba kuadibu kwa sasa ni kwa ajili ya kutekeleza hatua inayofuata ya kazi Yangu, na kwa ajili ya maendeleo yasiyozuiliwa ya kazi ya baadaye. Hivyo, Ninakuhimiza uwe na hekima na usichukulie maisha yako wala umuhimu wa uwepo wako kama mchanga usio na thamani. Je, unaweza kujua hasa kazi Yangu ijayo itakuwa nini? Je, unajua jinsi Nitakavyofanya kazi na jinsi kazi Yangu itakavyotekelezwa katika siku zijazo? Unapaswa kujua umuhimu wa kupitia kazi Yangu, na hata zaidi umuhimu wa kuniamini Mimi. Nimefanya kazi nyingi sana—Ninawezaje kuacha katikati, kama unavyowazia? Nimeanzisha mradi mkuu sana—Ninawezaje kuubomoa? Ni kweli kwamba Nimekuja kuifikisha kikomo enzi hii, lakini muhimu zaidi lazima ujue kwamba Nitaanza enzi mpya, kutekeleza kazi mpya, na hata zaidi, kueneza injili ya ufalme. Kwa hivyo unapaswa kujua kwamba kazi ya wakati wa sasa ni kuanzisha enzi tu na kuweka msingi wa kueneza injili katika wakati ujao na kuitamatisha enzi katika siku za usoni. Kazi Yangu si rahisi sana kama unavyowaza, wala si isiyo na thamani au isiyo na maana kama unavyoweza kuamini. Kwa hivyo, bado lazima Nikwambie: Unapaswa kujitoa kwa kazi Yangu, na hata zaidi kujitoa kwa ajili ya utukufu Wangu. Kile ambacho Nimetamani sana kutoka kitambo ni wewe kuwa na ushuhuda Kwangu; na hata zaidi Nimesubiri kwa muda mrefu sana kukuona ukieneza injili Yangu. Unapaswa kuelewa kile kilicho moyoni Mwangu.

Iliyotangulia: Maana ya Kuwa Mtu Halisi

Inayofuata: Majani Yanayoanguka Yanaporudi Kwenye Mizizi Yake, Utajutia Maovu Yote Ambayo Umefanya

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp