Mungu Anawakamilisha Wale Wanaoupendeza Moyo Wake

Kundi la watu ambao Mungu anataka kupata sasa ni wale ambao wanajitahidi kushirikiana na Mungu, wanaoweza kuiheshimu kazi Yake, na wanaoamini kuwa maneno Anayonena Mungu ni ya kweli, wale wanaoweza kuweka mahitaji ya Mungu katika vitendo. Ni wale walio na uelewa wa kweli katika mioyo yao. Ni hao ndio wanaoweza kukamilishwa, na wale ambao bila shaka watatembea katika njia ya ukamilisho. Wale wasio na uelewa wa wazi wa kazi ya Mungu, wale wasiokula na kunywa neno la Mungu, wale wasiotilia maanani neno la Mungu, na wale wasio na upendo wowote kwa Mungu katika mioyo yao. Wale walio na shaka na Mungu mwenye mwili, wasio na uhakika juu Yake, wasioyachukulia maneno ya Mungu kwa uzito na ambao daima humdanganya Mungu ni watu wanaompinga Mungu na ni wa Shetani; hakuna njia ya kukamilisha watu kama hao.

Kama unataka kufanywa mkamilifu, lazima kwanza uwe na neema ya Mungu, kwa sababu Mungu anawakamilisha wale ambao Amewapa neema, wale wanaoupendeza moyo Wake. Kama unataka kuupendeza moyo wa Mungu, lazima uwe na moyo unaotii kazi Yake yote, lazima ujitahidi kuufuata ukweli, na lazima uukubali uchunguzi wa Mungu katika kila kitu. Je, kila kitu unachofanya kimepitia uchunguzi wa Mungu? Je, nia yako iko sawa? Kama nia yako iko sawa, Mungu Atakubaliana nawe; kama nia yako sio sawa, hii inathibitisha kwamba kile moyo wako unapenda sio Mungu, ni mwili na Shetani. Kwa hiyo, lazima utumie maombi kama njia ya kukubali uchunguzi wa Mungu katika kila. Unapoomba, ingawa Mimi mwenyewe sisimami mbele yako, Roho Mtakatifu yuko pamoja nawe, na unaomba kwa Mimi mwenyewe na Roho wa Mungu. Kwa nini unaamini katika mwili huu? Unaamini kwa sababu Yuko na Roho wa Mungu. Je, ungemwamini mtu huyu ikiwa hangekuwa na Roho wa Mungu. Unapoamini katika mtu huyu, unaamini katika Roho wa Mungu. Unapomwogopa mtu huyu, unamwogopa Roho wa Mungu. Imani katika Roho wa Mungu ni imani katika mtu huyu, imani katika mtu huyu pia ni imani katika Roho wa Mungu. Unapoomba, unahisi Roho wa Mungu akiwa pamoja nawe, Mungu yuko mbele yako, kwa hivyo unamwomba Roho wa Mungu. Leo, watu wengi wanaogopa sana kuyaleta matendo yao mbele za Mungu, na ingawa unaweza kuudanganya mwili wa Mungu, huwezi kumdanganya Roho wa Mungu. Yale yote ambayo hayawezi kustahimili uchunguzi wa Mungu hayakubaliani na ukweli nayo lazima yawekwe kando, ama unatenda dhambi dhidi ya Mungu. Kwa hivyo, haijalishi kama ni wakati unaomba, unaponena na kushiriki na ndugu na dada zako, ama unapofanya wajibu wako na kufanya biashara yako, lazima uuweke moyo wako mbele za Mungu. Unapoitimiza kazi yako, Mungu yuko nawe, na bora nia yako iwe sawa, nayo iwe kwa ajili ya kazi ya nyumba ya Mungu, Atakubali kila kitu ufanyacho, kwa hivyo ni lazima uweke bidii kwa dhati kujishughulisha na kuitimiza kazi yako. Unapoomba, kama una upendo kwa Mungu katika moyo wako, na kama unatafuta utunzaji wa Mungu, ulinzi, na uchunguzi, kama haya ndio nia yako, maombi yako yatafaulu. Unapoomba katika mikutano, ndivyo unafaa kufungua moyo wako na kuomba Mungu, ambia Mungu kile kilicho moyoni mwako, na bila kuongea uongo, basi maombi yako yatafaulu. Kama unampenda Mungu moyoni mwako kwa dhati, basi fanya kiapo kwa Mungu: “Mungu, uliye mbinguni na nchini na vitu vyote, naapa Kwako: Hebu Roho Wako achunguze kila kitu ninachofanya na unilinde na kunijali kila wakati. Kinafanya kila kitu nifanyacho kiweze kusimama katika uwepo Wako. Ikiwa moyo wangu utawahi kukoma kukupenda ama kukusaliti Wewe, nipe adhabu Yako na laana kali zaidi. Usinisamehe katika dunia hii ama inayofuata!” Unaweza kuthubutu kula kiapo kama hiki? Kama huwezi, hii inadhibitisha kuwa wewe ni mwoga, na kwamba bado unajipenda. Je, mnao uamuzi huu? Kama kweli huu ndio uamuzi wako, lazima ufanye kiapo hiki. Kama una azimio la kula kiapo kama hiki, Mungu ataridhisha uamuzi wako. Unapoapa kwa Mungu, Mungu anasikiza. Mungu Anaamua kama wewe ni mwenye dhambi ama mwenye haki kupitia maombi yako na matendo yako. Huu sasa ndio mchakato wa kukukamilisha, na kama kweli unayo imani katika kukamilishwa kwako na Mungu, basi utaleta kila kitu ufanyacho mbele za Mungu na kuukubali uchunguzi Wake; ukifanya kitu kinachoasi sana ama ukimsaliti Mungu, basi atatimiza kiapo chako, na kisha haijalishi kitakachokufanyikia, iwe kuangamia ama kuadibu, ni shida yako mwenyewe. Ulikula kiapo, basi lazima ukitekeleze. Ukila kiapo, lakini ukose kukitekeleza, utaangamia. Kwa kuwa unakula kiapo, Mungu atatimiza kiapo chako. Wengine wanaogopa baada ya kuomba, na kusema, “Ee, jamani, nafasi yangu katika ufisadi imepotea, nafasi yangu kufanya mambo maovu imepotea, nafasi yangu ya kujiingiza katika ulafi wangu wa kidunia imepotea!” Watu hawa bado wanaipenda dunia na dhambi, nao ni hakika wataangamia.

Kuwa muumini katika Mungu kunamaanisha kuwa kila kitu ufanyacho lazima kiletwe mbele za Mungu na kupitia uchunguzi wa Mungu. Kama kile ufanyacho kinaweza kuletwa mbele za Roho wa Mungu lakini sio mbele ya mwili wa Mungu, hii inadhibitisha kuwa hujajitiisha katika uchunguzi wa Roho wa Mungu. Roho wa Mungu ni nani? Mtu huyu aliyeshuhudiwa na Mungu ni nani? Je, Wote si sawa? Wengi Huwaona kama nafsi mbili tofauti, wakiamini kwamba Roho wa Mungu ni Roho wa Mungu, naye mtu anayeshuhudiwa na Mungu ni binadamu tu. Lakini, je, hujakosea? Je, mtu huyu anafanya kazi kwa niaba ya nani? Wale ambao hawaujui mwili wa Mungu hawana uelewa ya kiroho. Roho wa Mungu na mwili Wake ni mmoja, kwa sababu Roho wa Mungu anatokea kwa mwili. Kama mtu huyu si mwema kwako, Roho wa Mungu Atakuwa mwema? Ni nini kimekuchanganya? Leo, hakuna asiyekubali uchunguzi wa Mungu anaweza kupokea idhini ya Mungu, na yeyote asiyemjua Mungu mwenye mwili hawezi kukamilishwa. Jiangalie nawe ujiulize kama kila kitu unachofanya kinaweza kuletwa mbele ya Mungu. Iwapo huwezi kuleta kila kitu unachofanya mbele za Mungu, hii inaonyesha kuwa wewe ni mtenda maovu. Je, watenda maovu wanaweza kufanywa wakamilifu? Kila kitu unachofanya, kila tendo, kila nia, na kila jibu lazima kiletwe mbele za Mungu. Hata maisha yako ya kawaida ya kiroho—maombi yako, ukaribu wako kwa Mungu, jinsi unavyokula na kunywa maneno ya Mungu, ushirika wako na kina ndugu zako na maisha yako ndani ya kanisa—na huduma yako katika ushirikiano wako vinaweza kuletwa mbele za Mungu ili Yeye avichunguze. Ni matendo kama hayo ndiyo yatakayokusaidia kustawi katika maisha. Mchakato wa kukubali uchunguzi wa Mungu ni mchakato wa kutakaswa. Kadri unavyoukubali uchunguzi wa Mungu, ndivyo unavyotakaswa zaidi na kadri unavyokubaliana na matakwa ya Mungu, ili kwamba hutajipata katika uasherati, na moyo wako utaishi katika uwepo wa Mungu; kadri unavyokubali uchunguzi wa Mungu, ndivyo unavyomuaibisha Shetani na kuutelekeza mwili. Kwa hivyo, kukubali uchunguzi wa Mungu ni njia ambayo watu wanafaa kutenda. Haijalishi kile unachokifanya, hata katika ushirika na ndugu na dada zako, ukiyaleta matendo yako mbele za Mungu na kutafuta uchunguzi wa Mungu, na kama nia yako ni kumtii Mungu Mwenyewe, unachotenda ni sahihi zaidi. Kama tu wewe ni mtu anayeleta kila kitu anachofanya mbele za Mungu na kukubali uchunguzi wa Mungu ndipo utakapokuwa mtu anayeishi kwa hakika katika uwepo wa Mungu.

Wale wasio na uelewa wa Mungu hawawezi kumtii Mungu kikamilifu. Watu kama hao ni wana wa uasi. Ni wenye kutaka makuu sana, na kunao uasi mwingi sana ndani mwao, kwa hivyo wanajitenga na Mungu na hawana nia ya kukubali uchunguzi wa Mungu. Watu kama hao hawawezi kufanywa wakamilifu na Mungu kwa urahisi. Watu wengine wana uchaguzi katika vile wanavyokula na kunywa neno la Mungu na katika hali yao ya kulikubali. Wanakubali sehemu za neno la Mungu zinazolingana na dhana zao wakikataa zile zisizokubaliana nazo. Je, hawamwasi na kumkataa Mungu kwa uwazi? Kama mtu anaamini katika Mungu kwa miaka mingi bila kupata uelewa hata kidogo wa Mungu, yeye ni mtu asiyeamini. Wale walio tayari kukubali uchunguzi wa Mungu ni wale wanao tafuta uelewano wa Mungu, walio tayari kukubali neno la Mungu. Ni wale ambao watapokea uridhi wa Mungu na mibaraka, nao ni wale waliobarikiwa zaidi. Mungu analaani wale wasio na nafasi Yake katika mioyo yao. Anawaadibu na kuwaacha watu kama hao. Kama humpendi Mungu, Mungu atakuacha, na kama hutasikia Ninachosema, Naahidi kwamba Roho wa Mungu atakuacha. Jaribu hili iwapo hauniamini! Leo Nawaambia njia ya kufuata, lakini kama utafanya hivyo ni juu yako. Kama huamini hilo, kama hulitii katika vitendo, utaona kama Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani yako au la! Kama hautatafuta uelewano wa Mungu, Roho Mtakatifu hatafanya kazi ndani mwako. Mungu anafanya kazi ndani ya wale wanaotafuta na kulithamini neno la Mungu. Kadri unavyolithamini neno la Mungu, ndivyo Roho wa Mungu atakavyofanya kazi zaidi ndani mwako. Kadri mtu anavyolithamini neno la Mungu, ndivyo nafasi yake ya kukamilishwa na Mungu inavyokuwa kubwa. Mungu anawakamilisha wale ambao wanampenda Yeye kwa kweli. Anawakamilisha wale ambao mioyo yao iko katika amani mbele Yake. Ukiithamini kazi yote ya Mungu, yaani, ukiuthamini mwanga wa Mungu, ukiuthamini uwepo wa Mungu, ukithamini kujali na kuwekwa kwa Mungu, ukithamini jinsi neno la Mungu linakuwa ukweli wako na utoaji wa maisha, unafuata zaidi moyo wa Mungu. Ukiithamini kazi ya Mungu, ukiithamini kazi yote ambayo Mungu Amefanya juu yako, Mungu Atakubariki na kufanya kila kitu kilicho chako kuongezeka. Usipoithamini kazi ya Mungu, Mungu Hatafanya kazi kwako, Atakuruhusu tu nyakati za neema kwa imani yako, ama kukubariki na utajiri kidogo ama usalama kwa familia yako. Lazima utie bidii kuyafanya maneno ya Mungu kuwa ukweli wako ili umridhishe Yeye na kuupendeza moyo Wake, sio tu kutia bidii kufurahia neema ya Mungu. Hakuna kitu muhimu zaidi kwa waumini kama kupokea kazi ya Mungu, kupata ukamilifu, na kuwa wanaofanya mapenzi ya Mungu. Hili ndilo lengo unalofaa kufuata.

Kila ambacho mwanadamu alitafuta katika Enzi ya Neema sasa hakiko tena, kwa sababu kiwango cha juu cha ufuatiliaji; kinachofuatiliwa ni cha juu zaidi na cha vitendo zaidi, linalofuatiliwa linaweza kukidhi zaidi kile ambacho mwanadamu anahitaji ndani. Katika enzi zilizopita, Mungu hakuwafanyia watu kazi kama Afanyavyo leo; Hakunena nao sana jinsi Amenena leo, wala mahitaji Yake kwao hayakuwa ya juu kama ya leo. Kwamba Mungu anainua vitu hivi kwenu kunathibitisha kuwa nia ya mwisho ya Mungu, kumelengwa kwenu, kundi hili. Iwapo kweli unataka kufanywa mkamilifu na Mungu, basi lifuate kama lengo lako kuu. Haijalishi kama unakwenda huku na kule, unajitumia, unatenda wajibu, ama kama umepokea agizo la Mungu, nia daima ni kukamilishwa na kuridhisha mapenzi ya Mungu, kutimiza malengo haya. Mtu akisema kuwa hafuati kukamilishwa na Mungu ama kuingia katika maisha, lakini anafuata tu amani na furaha ya kimwili, basi yeye ni kipofu kabisa. Wale wasiofuata ukweli wa maisha, lakini wanafuata maisha ya milele pekee katika maisha ya baadaye na usalama katika maisha haya ni vipofu kabisa. Kwa hivyo, kila kitu ufanyacho lazima kifanywe kwa madhumuni ya kufanywa mkamilifu na kupatwa na Mungu.

Kazi ambayo Mungu anafanya kwa watu ni kuwakimu kulingana na mahitaji yao tofauti. Kadri maisha ya mwanadamu yalivyo makubwa, ndivyo anavyohitaji mengi zaidi, na ndivyo anavyotafuta zaidi. Kama katika awamu hii huna harakati, inathibitisha kuwa Roho Mtakatifu amekuacha. Wale wote wanaofuata maisha hawatawahi kuachwa na Roho Mtakatifu, wao hufuata kila wakati, wanatamani kila wakati. Watu kama hao hawatosheki kamwe kupumzika mahali walipo. Kila awamu ya kazi ya Roho Mtakatifu inalenga kufikia athari ndani mwako, lakini ukikua wa kutojali, kama hauhitaji tena, kama huikubali kazi ya Roho Mtakatifu, Yeye atakuacha. Watu wanahitaji uchunguzi wa Mungu kila siku, wanahitaji kupewa kwa wingi kutoka kwa Mungu kila siku. Je, watu wanaweza kuishi bila kula na kunywa neno la Mungu kila siku? Kama mtu anahisi kuwa hawezi kula ama kunywa neno la Mungu vya kutosha, kama analitafuta kila siku na kuwa na njaa na kiu kwake, Roho Mtakatifu atafanya kazi juu yao. Kadri mtu anavyotamani, ndivyo atakavyokuwa na ushirika kuhusu vitu vya hakika. Kadri mtu anavyoutafuta ukweli sana, ndivyo maisha yake yanavyokua kwa haraka, yakimpa uzoefu wa hali ya juu na kumfanya tajiri katika nyumba ya Mungu.

Iliyotangulia: Jua Kazi Mpya Zaidi ya Mungu na Ufuate Nyayo Zake

Inayofuata: Wale Wanaomtii Mungu kwa Moyo wa Kweli Hakika Watapatwa na Mungu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp