Wale Wanaomtii Mungu kwa Moyo wa Kweli Hakika Watapatwa na Mungu

Kazi ya Roho Mtakatifu inabadilika kutoka siku hadi siku, ikipanda juu kwa kila hatua; ufunuo wa kesho unakuwa hata juu kuliko wa leo, hatua kwa hatua ukikwea hata juu zaidi. Hii ndiyo kazi anayotumia Mungu kumkamilisha mwanadamu. Iwapo mwanadamu hawezi kwenda sambamba, basi anaweza kuachwa nyuma wakati wowote. Kama mwanadamu hana moyo wa kutii, basi hawezi kufuata hadi mwisho. Enzi ya kale imepita; hii ni enzi mpya. Na katika enzi mpya, kazi mpya lazima ifanywe. Hasa katika enzi ya mwisho ambapo mwanadamu atakamilishwa, Mungu atafanya kazi mpya hata haraka zaidi. Hivyo, bila utii moyoni mwake, mwanadamu ataona vigumu kufuata nyayo za Mungu. Mungu hafuati kanuni zozote, wala hachukulii hatua yoyote ya kazi Yake kama isiyobadilika. Badala yake, kazi Anayofanya daima ni mpya zaidi na daima ni juu zaidi. Kazi Yake inazidi kuwa ya utendaji kwa kila hatua, sambamba zaidi na matendo halisi ya mwanadamu. Baada tu ya mwanadamu kuwa na uzoefu wa aina hii ya kazi ndipo anaweza kufikia mabadiliko ya mwisho ya tabia yake. Maarifa ya mwanadamu ya maisha yanakua hata juu zaidi, na vivyo hivyo kazi ya Mungu pia inakuwa juu zaidi. Mwanadamu anaweza kufikia ukamilifu kwa njia hii tu na kufaa kwa matumizi ya Mungu. Kwa upande mmoja, Mungu anafanya kazi hivi ili kupinga na kubadilisha fikira za mwanadamu, na kwa upande mwingine, kumwongoza mwanadamu katika hali ya juu zaidi na kweli zaidi, hadi katika ulimwengu wa juu zaidi wa imani katika Mungu, ili mwishowe, mapenzi ya Mungu yaweze kufanyika. Wote walio na asili isiyotii wanaopinga kwa kusudi wataachwa nyuma na hatua hii ya kazi ya Mungu ya haraka na yenye kusonga mbele kwa nguvu; wale tu walio na moyo mtiifu na wako tayari kuwa wanyonge wataendelea hadi mwisho wa njia. Katika kazi kama hii, nyote mnapaswa kujua jinsi ya kutii na kuweka kando fikira zenu. Mnapaswa kuwa waangalifu katika kila hatua mnayochukua. Kama wewe ni mzembe, hakika utakuwa mmoja wa wale wanaochukiwa na kukataliwa na Roho Mtakatifu na yule anayemkatiza Mungu katika kazi Yake. Kabla ya kufanyiwa hatua hii ya kazi, kanuni na sheria za mwanadamu za zamani zilikuwa nyingi sana hadi akawa na msisimko zaidi, na mwishowe, akawa mwenye majivuno na kujisahau. Hivi vyote ni vikwazo vinavyomzuia mwanadamu kuikubali kazi mpya ya Mungu; vinakuwa pingamizi kwa mwanadamu kuja kumjua Mungu. Iwapo mwanadamu hana utii katika moyo wake wala tamaa ya ukweli, basi atakuwa hatarini. Ukitii tu kazi na maneno yaliyo rahisi, na huwezi kukubali yoyote yaliyo na ugumu zaidi, basi wewe ni yule anayeendelea na njia za zamani na hawezi kwenda sambamba na kazi ya Roho Mtakatifu. Kazi inayofanywa na Mungu ni tofauti kutoka kipindi kimoja hadi kingine. Ukionyesha utii mkubwa katika awamu moja, lakini katika awamu ifuatayo uonyeshe utii mdogo ama usionyeshe wowote, basi Mungu atakuacha. Ukienda sambamba na Mungu anapopaa hatua hii, basi lazima uendelee kuwa sambamba Anapopaa ifuatayo. Ni hapo tu ndipo utakuwa mtu ambaye ni mtiifu kwa Roho Mtakatifu. Kwa sababu unamwamini Mungu, lazima ubakie daima katika utii wako. Huwezi tu kutii unapotaka na kutotii usipotaka. Namna hii ya utii haikubaliki na Mungu. Kama huwezi kwenda sambamba na kazi mpya Ninayoshiriki na uendelee kuyashikilia maneno ya zamani, basi kutakuaje na ukuaji katika maisha yako? Kazi ya Mungu ni kukuruzuku kupitia neno Lake. Unapotii na kulikubali neno Lake, basi Roho Mtakatifu hakika atafanya kazi ndani yako. Roho Mtakatifu anafanya kazi kwa njia Ninayozungumza kabisa. Fanya Nilivyosema, na Roho Mtakatifu atafanya kazi ndani yako mara moja. Natoa mwangaza mpya ili muweze kuona na kuwaleta kwa mwangaza wa wakati wa sasa. Unapotembea katika mwangaza huu, Roho Mtakatifu ataanza kazi ndani yako mara moja. Kuna wengine wanaoweza kuwa wakaidi na kusema, “Sitafanya tu Usemavyo.” Basi Nakwambia kwamba sasa umefika mwisho wa njia umenyauka na huna maisha zaidi. Hivyo, kwa kupitia mabadiliko ya tabia yako, ni muhimu kabisa kwenda sambamba na mwangaza wa sasa. Roho Mtakatifu hafanyi kazi tu kwa baadhi ya wanadamu wanaotumiwa na Mungu, lakini hata zaidi kanisani. Anaweza kuwa akifanya kazi kwa yeyote. Anaweza kufanya kazi ndani yako sasa, na baada ya wewe kuwa na uzoefu nayo, Anaweza kufanya kazi ndani ya mtu mwingine ajaye. Fanya hima ufuate; unapozidi kufuata mwangaza wa sasa, ndivyo maisha yako yanaweza ku kua. Haijalishi yeye ni mwanadamu wa aina gani, alimradi Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani yake, kuwa na hakika kufuata. Chukua uzoefu wake kupitia wako mwenyewe, na utapokea mambo ya juu hata zaidi. Kwa kufanya hivyo utaona ukuaji haraka zaidi. Hii ni njia ya ukamilifu kwa mwanadamu na njia ambayo maisha hukua. Njia ya ukamilifu inafikiwa kupitia utii wako wa kazi ya Roho Mtakatifu. Hujui ni kupitia kwa mtu wa aina gani ndiyo Mungu Atafanya kazi kukukamilisha, wala kupitia mtu yupi, tukio, ama jambo ndiyo Atakuwezesha kuingia katika umiliki na kupata ufahamu fulani. Ukiweza kutembea kwenye njia hii sawa, hii inaonyesha kwamba kuna matumaini makubwa kwako kukamilishwa na Mungu. Kama huwezi kufanya hivyo, inaonyesha kwamba maisha yako ya baadaye ni ya dhalili na giza. Mara unapoenda kwenye njia iliyo sahihi, utapata ufunuo katika mambo yote. Bila kujali yale ambayo Roho Mtakatifu atafichua kwa wengine, ukiendelea kupitia mambo wewe mwenyewe kwa msingi wa maarifa yao, basi uzoefu huu utakuwa sehemu ya maisha yako, na utaweza kuwakimu wengine kwa sababu ya huu uzoefu. Wale wanaowakimu wengine kwa kuyarudia maneno ni wale wasio na uzoefu wowote; lazima ujifunze kupata, kupitia mwangaza na nuru ya wengine, njia ya kutenda kabla ya kuzungumza kuhusu uzoefu na maarifa yako halisi. Hii itakuwa ya manufaa zaidi kwa maisha yako binafsi. Unapaswa kuwa na uzoefu kwa njia hii, kutii yote yatokayo kwa Mungu. Unapaswa kutafuta mapenzi ya Mungu katika vitu vyote na kujifunza masomo katika vitu vyote, ili maisha yako yaweze kukua. Vitendo vya aina hii huleta ukuaji wa haraka zaidi.

Roho Mtakatifu anakupa nuru kupitia uzoefu wa vitendo vyako na kukukamilisha kupitia imani yako. Uko tayari kweli kukamilishwa? Kama kweli uko tayari kukamilishwa na Mungu, basi utakuwa na ujasiri kuweka kando mwili wako, na utaweza kutekeleza maneno ya Mungu na kutokuwa mtu anayekaa tu ama mnyonge. Utaweza kutii yote yatokayo kwa Mungu, na vitendo vyako vyote, viwe vimefanywa hadharani au faraghani, vitastahiki kwa Mungu. Kama wewe ni mtu mwaminifu, na unatenda ukweli katika mambo yote, basi utakamilishwa. Wale wanadamu wadanganyifu wanaotenda njia moja mbele ya wengine na nyingine nyuma yao hawako tayari kukamilishwa. Wote ni wana wa maangamizo na uharibifu; wao si wa Mungu lakini ni wa Shetani. Hao si aina ya wanadamu waliochaguliwa na Mungu! Kama vitendo na tabia yako haviwezi kustahiki mbele ya Mungu ama kufikiriwa na Roho wa Mungu, hii ni thibitisho kwamba wewe una shida. Ukikubali tu hukumu na kuadibu kwa Mungu, na kuweka umuhimu katika mabadiliko ya tabia yako ndipo utafika kwenye njia ya kukamilishwa. Ikiwa kweli uko tayari kukamilishwa na Mungu na kufanya mapenzi ya Mungu, basi unapaswa kutii kazi yote ya Mungu na kutotoa neno lolote la kulalamika, wala hupaswi kutathmini ama kuhukumu kazi ya Mungu utakavyo. Haya ni masharti ya msingi kabisa ya kukamilishwa na Mungu. Mahitaji ya lazima kwa wale wanaotaka kukamilishwa na Mungu ni haya: fanya mambo yote kwa moyo unaompenda Mungu. Inamaanisha nini “kufanya mambo kwa moyo unaompenda Mungu”? Inamaanisha kwamba vitendo na tabia yako yote inaweza kuletwa mbele ya Mungu. Kwa sababu una nia sawa, iwapo vitendo vyako ni sawa ama vibaya, huogopi vikionyeshwa kwa Mungu ama kwa ndugu zako; unathubutu kuapa mbele ya Mungu. Lazime uonyeshe kila nia, fikra, na wazo lako mbele ya Mungu ili ayachunguze; ukitenda na kuingia kwa njia hii, basi maendeleo katika maisha yako yatakuwa mepesi.

Kwa sababu unamwamini Mungu, basi lazima uweke imani ndani ya maneno yote ya Mungu na ndani ya kazi Yake yote. Hii ni kusema kwamba, kwa sababu unamwamini Mungu, ni lazima umtii. Kama huwezi kufanya hivi, basi haijalishi iwapo unamwamini Mungu. Kama umemwamini Mungu kwa miaka mingi, lakini hujawahi kumtii ama kuyakubali maneno Yake, na badala yake umemwuliza Mungu anyenyekee kwako na kufuata dhana zako, basi wewe ni mtu mwasi zaidi ya wote, na wewe si muumini. Mtu kama huyu anawezaje kutii kazi na maneno ya Mungu ambayo hayafuati fikira za mwanadamu? Mtu mwasi zaidi ni yule anayemkataa na kumpinga Mungu makusudi. Yeye ni adui wa Mungu na ni mpinga Kristo. Mtu kama huyu daima anakuwa na mtazamo wa kikatili kwa kazi mpya ya Mungu, hajawahi kuonyesha nia hata ndogo ya kutii, na hajawahi kuonyesha utii ama kujinyenyekeza kwa furaha. Anajisifu mbele ya wengine na kamwe haonyeshi utii kwa mwingine. Mbele ya Mungu, anajiona kuwa hodari zaidi katika kuhubiri neno na mwenye ujuzi zaidi katika kufanya kazi kwa wengine. Kamwe hatupi “hazina” anazomiliki tayari, lakini anazichukua kama vitu vinavyorithiwa kwa familia vya kuabudiwa, vya kuhubiri kuhusu wengine, na huvitumia kuhutubia wale wapumbavu wanaomwabudu. Hakika kuna baadhi ya watu kama hawa kanisani. Inaweza kusemwa kwamba wao ni “mashujaa wasioshindwa,” kizazi baada ya kizazi kinachokaa kwa muda mfupi ndani ya nyumba ya Mungu. Wanachukua kuhubiri neno (mafundisho ya dini) kama wajibu wao wa juu zaidi. Mwaka baada ya mwaka na kizazi baada ya kizazi, wao huenenda kwa nguvu wakitekeleza wajibu wao “mtakatifu na usiokiukwa”. Hakuna anayethubutu kuwaguza na hakuna mtu hata mmoja anayethubutu kuwashutumu kwa uwazi. Wanakuwa “wafalme” katika nyumba ya Mungu, wakienea kote wakiwaonea wengine kutoka enzi hadi enzi. Hili kundi la mapepo linataka kuungana mikono na kuharibu kazi Yangu; Nawezaje kuwaruhusu ibilisi hawa waishio kuwepo mbele Yangu? Hata wale walio tu na moyo nusu wa utii hawawezi kutembea hadi mwisho, sembuse hawa wadhalimu wasio na utii hata kidogo kwa mioyo yao. Kazi ya Mungu haipatwi virahisi na mwanadamu. Hata mwanadamu akitumia nguvu yake yote, ataweza kupata kipande tu na kufikia ukamilifu mwishowe. Na vipi basi kuhusu watoto wa malaika mkuu wanaotaka kuharibu kazi ya Mungu? Je, hawana hata matumaini madogo zaidi ya kupatwa na Mungu? Madhumuni Yangu katika kufanya kazi ya ushindi si tu kushinda kwa sababu ya ushindi, lakini kushinda ili kufichua haki na udhalimu, kupata ushahidi kwa ajili ya adhabu ya mwanadamu, kulaani waovu, na hata zaidi, kushinda kwa sababu ya kuwakamilisha wale walio radhi kutii. Mwishowe, wote watatengwa kulingana na aina, na mawazo ya wale wote waliokamilishwa yatajazwa na utii. Hii ndiyo kazi itakayokamilishwa mwishowe. Lakini waliojawa na uasi wataadhibiwa, kutumwa kuchomeka motoni na milele kulaaniwa. Wakati huo utakapofika, wale “mashujaa wakubwa wasioshindwa” wa awali watakuwa “waoga wanyonge na wasio na maana” wa chini zaidi na wanaoepukwa zaidi. Hii tu ndiyo inaweza kuonyesha kila kipengele cha haki ya Mungu na kufichua tabia Yake ambayo hairuhusu kosa lolote. Hili tu ndilo linaloweza kutuliza chuki iliyo moyoni Mwangu. Je, hamkubali kwamba hili ni la busara sana?

Sio wote walio na uzoefu wa kazi ya Roho Mtakatifu wanaweza kupata uzima, na sio wote katika mkondo huu wanaweza kupata uzima. Uzima sio mali ya kawaida inayoshirikisha binadamu wote, na mabadiliko ya tabia ni kitu ambacho hakifikiwi na wote kwa urahisi. Kujisalimisha kwa kazi ya Mungu lazima kugusike na kuishi kwa kudhihirishwa. Kujisalimisha kwa kiwango cha juu juu hakuwezi kupokea idhini ya Mungu, na kutii tu vipengele vya juujuu vya neno la Mungu bila kutaka mgeuzo wa tabia ya mtu, hakutaweza kuufurahisha moyo wa Mungu. Utiifu kwa Mungu na kujinyenyekeza kwa kazi ya Mungu ni kitu kimoja. Wale wanaomtii Mungu tu lakini hawatii kazi Yake hawawezi kudhaniwa kuwa watiifu, sembuse wale wasiotii kwa kweli na kwa nje hao ni wa kujipendekeza. Wale ambao kweli wanajinyenyekeza kwa Mungu wote wanaweza kufaidika kutokana na kazi na kupata ufahamu wa tabia na kazi ya Mungu. Wanadamu kama hawa tu ndio kweli wanajinyenyekeza kwa Mungu. Wanadamu kama hawa wanaweza kupata maarifa mapya kutokana na kazi mpya na kuwa na uzoefu wa mabadiliko mapya kutoka hayo. Wanadamu kama hawa tu ndio wana idhini ya Mungu; mwanadamu wa aina hii tu ndiye amekamilishwa, ndiye amepitia mabadiliko ya tabia yake. Wale wanaopokea idhini ya Mungu ni wale wanaojisalimisha kwa Mungu kwa furaha, na pia kwa neno na kazi Yake. Mwanadamu wa aina hii tu ndiye yuko sahihi; mwanadamu wa aina hii tu ndiye kweli anamtamani Mungu, na anamtafuta Mungu kwa dhati. Na kwa wale wanaozungumzia tu imani yao kwa Mungu kwa vinywa vyao lakini kwa hakika wanamlaani, ni wanadamu waliovaa barakoa, walio na sumu ya nyoka, ni wanadamu wasaliti zaidi. Siku moja hawa waovu watavuliwa barakoa zao mbovu. Je, hiyo si kazi inayofanywa leo? Wanadamu waovu daima watakuwa waovu na hawataepuka kamwe siku ya adhabu. Wanadamu wazuri daima watakuwa wazuri na watafichuliwa kazi itakapoisha. Hakuna hata mmoja wa waovu atakayedhaniwa kuwa wenye haki, wala yeyote mwenye haki atakayedhaniwa kuwa mwovu. Je, Ningemruhusu yeyote ashtakiwe kimakosa?

Maisha yako yanapoendelea, lazima daima uwe na kiingilio kipya na ufahamu mpya na wa juu zaidi, unaokua kwa kina na kila hatua. Hiki ndicho wanadamu wote wanapaswa kuingia ndani. Kupitia kuwasiliana, kusikiliza ujumbe, kusoma neno la Mungu, ama kushughulikia suala, utapata ufahamu mpya na kupata nuru upya. Huishi ndani ya kanuni za zamani na nyakati za zamani. Unaishi daima ndani ya mwangaza mpya, na hupotei mbali na neno la Mungu. Huku ndiko kunaitwa kwenda katika njia sahihi. Kulipa tu gharama ya juu juu hakutakubalika. Siku baada ya siku, neno la Mungu linaingia katika ulimwengu wa juu zaidi na mambo mapya yanajitokeza kila siku. Ni muhimu pia kwa mwanadamu kuingia upya kila siku. Mungu anavyozungumza, ndivyo Anavyotimiza yote ambayo Amezungumza; kama huwezi kwenda sambamba, basi unabaki nyuma. Lazima uende kwa kina zaidi katika maombi yako; kula na kunywa neno la Mungu hakuwezi kuwa kuna kosa mfululizo. Imarisha nuru na mwangaza unayopokea, ufunuo unaopokea, na dhana zako na fikira zako lazima zipungue hatua kwa hatua. Lazima pia uimarishe hekima yako, na chochote unachopitia, lazima uwe na mawazo yako kukihusu na uwe na mtazamo wako. Kwa kuelewa mambo fulani katika roho, lazima upate ufahamu wa mambo ya nje na kuelewa kiini cha suala lolote. Kama hujajiandaa na mambo haya, utawezaje kuliongoza kanisa? Iwapo unazungumzia tu barua na mafundisho ya dini bila uhalisi wowote na bila njia ya kutenda, unaweza tu kuendelea kwa muda mfupi. Inaweza kukubalika kidogo kwa waumini wapya, lakini baada ya muda, wakati waumini wapya wanapata tajriba halisi, basi hutaweza tena kuwakimu. Basi unafaa vipi kwa matumizi ya Mungu? Bila kupata nuru upya, huwezi kufanya kazi. Walio bila nuru upya ni wale wasiojua jinsi ya kuwa na uzoefu, na wanadamu kama hao kamwe hawapati maarifa mapya ama tajriba. Na katika suala la kuleta maisha, hawawezi kamwe kufanya jukumu lao la kusambaza uhai, wala hawawezi kufaa kwa ajili ya matumizi na Mungu. Mwanadamu kama huyu ni dhaifu na hana maana. Kwa kweli, wanadamu kama hawa hawawezi kufanya jukumu lao kabisa kwa kazi na wote hawana faida. Wanashindwa kufanya jukumu lao na pia kwa kweli wanaweka mzigo mwingi usiohitajika juu ya kanisa. Nawahimiza hawa “wanaume wazee” kuharakisha na kuondoka kanisani ili wengine wasilazimishwe kuwaona tena. Wanadamu kama hawa hawaelewi kazi mpya lakini wamejawa na fikira zisizokoma. Hawafanyi chochote kanisani; badala yake, wanachochea na kusambaza uhasi kila pahali, hata kushiriki katika kila namna ya utovu wa nidhamu na vurugu kanisani, na hivyo kuwarusha wale wasiobagua katika vurugu na machafuko. Haya ibilisi wanaoishi, hawa mapepo mabaya wanapaswa kuondoka kanisani haraka iwezekanavyo, kanisa lisije likaharibiwa kwa sababu yako. Labda huogopi kazi ya leo, lakini huogopi adhabu ya haki ya kesho? Kuna idadi kubwa ya watu kanisani ambao ni vimelea, na pia kuna idadi kubwa ya mbwa mwitu wanaotafuta kuvuruga kazi ya kawaida ya Mungu. Vitu hivi vyote ni mapepo yaliyotumwa na Ibilisi, ni mbwa mwitu wakali wanaotafuta kuwala kondoo wasiojua. Iwapo wanadamu kama hawa hawatafukuzwa, basi wanakuwa vimelea kwa kanisa na nondo wanaokula sadaka. Hawa mabuu wenye kudharauliwa wajinga, duni, na wenye kuchukiza wataadhibiwa siku moja karibuni!

Iliyotangulia: Mungu Anawakamilisha Wale Wanaoupendeza Moyo Wake

Inayofuata: Enzi ya Ufalme Ni Enzi ya Neno

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp