87. Mateso ya kikatili Yaliimarisha Imani Yangu

Na Zhao Rui, China

Jina langu ni Zhao Rui. Kwa sababu ya neema ya Mungu, familia yangu yote ilianza kumfuata Bwana Yesu mnamo mwaka wa 1993. Mnamo mwaka wa 1996, nilipokuwa na umri wa miaka kumi na sita, nilivutiwa na upendo wa Bwana Yesu na nilianza kufanya kazi kanisani na kutoa mahubiri. Hata hivyo, muda mfupi baadaye, nilianza kuona mambo mengi ndani ya kanisa ambayo yaliniacha nikiwa nimesikitika sana: Wafanyakazi wenzangu walishiriki katika kula njama wao kwa wao, walitengana, na walishindana kwa ajili ya mamlaka na manufaa. Ilikuwa kana kwamba mafundisho ya Bwana ya kwamba tunapaswa kupendana yalikuwa yamesahaulika zamani. Wale waliotoa mahubiri walionekana kutokuwa na chochote cha kusema na hakukuwa na raha ya kufurahia katika kuishi maisha ya kanisa. Ndugu wengi walikuwa wameanza kuwa hasi na dhaifu na hata walikuwa wameacha kuhudhuria mikutano…. Nilipokabiliwa na hali ya huzuni na ya ukiwa ya kanisa, nilihisi hasa mwenye kusikitika na asiyejiweza. Mnamo Julai mwaka wa 1999, kwa mpango na utaratibu wa Mungu wa kimiujiza, nilipokea kwa furaha kurudi kwa Bwana Yesu—Mwenyezi Mungu. Kupitia kusoma maneno ya Mwenyezi Mungu na kushughulika katika maisha ya kanisa, nilifurahia kwa mara nyingine tena kazi ya Roho Mtakatifu. Nilipohudhuria mikutano pamoja na ndugu zangu, mtindo wa maisha ya dini ambao niliokuwa nimeufuata hapo nyuma ulikuwa umefutiliwa mbali; kila mtu angeweza kueleza hisia yake halisi, na tulishirikiana katika nuru iliyotolewa kwetu na nuru ya Roho Mtakatifu na kujadili jinsi tulivyopitia neno la Mungu, na pia jinsi ya kumtegemea Mungu kujiondolea upotovu. Zaidi ya hayo, ndugu waliishi katika njia yenye kumcha Mungu na yenye heshima sana; walikuwa wenye msamaha na wa kuvumiliana dosari na manyesho ya upotovu na walipeana msaada wa upendo. Ikiwa mtu alikuwa akipitia shida, hakuna mtu ambaye angemdharau au kumdunisha, lakini wangetafuta ukweli pamoja naye ili kupata suluhisho la matatizo yake. Haya yalikuwa maisha ya kanisa ambayo nilitaka daima—njia ya kweli ambayo nilikuwa nimeitafuta kwa muda wa miaka mingi! Nilikuwa hatimaye nimerudi mbele za Mungu baada ya kupotea kwa muda wa miaka mingi! Nilifanya azimio kwa Mungu: “Nitawaleta watu wasio na hatia ambao bado wangali wanaishi gizani mbele za Mungu, niwawezeshe kuishi kwa mwongozo na baraka ya kazi ya Roho Mtakatifu, na kunyunyiziwa na maji ya uzima ya Mungu. Huu ni wito wangu kama kiumbe aliyeumbwa na ni njia yenye maana zaidi na ya thamani zaidi ya kuishi maisha yangu.” Kwa ajili ya hayo, nilijitosa katika kutekeleza wajibu wangu.

Hata hivyo, serikali ya CCP, adui huyo wa Mungu wa kweli, serikali hiyo inayochukia ukweli na inayomkana Mungu, haingeturuhusu tumfuate Mungu wala kushuhudia kwa Mungu au kueneza injili ya Mungu, sembuse ingevumilia kuwepo kwa kanisa la Mungu. Katika msimu wa joto wa mwaka wa 2009, CCP ilifanya kampeni kubwa iliyolenga kuwakamata washiriki wa Kanisa la Mwenyezi Mungu. Viongozi kutoka makanisa kote nchini walikamatwa na kutupwa gerezani mmoja baada ya mwingine. Takribani saa tatu jioni tarehe 4 Aprili, mimi na dada mmoja ambaye nilikuwa nikishirikiana naye katika kutekeleza wajibu wetu tulikuwa tumeondoka nyumbani kwa dada Wang na kutembea hadi barabarani wakati wanaume watatu waliokuwa wamevalia nguo za kiraia ghafla waliruka nyuma yetu na kutuvuta kwa nguvu kwa mikono, wakisema kwa sauti kubwa, “Hebu twende! Mtaandamana nasi!” Kabla hata ya kupata wakati wa kuonyesha kujibiza, tuliingizwa kwa nguvu nyuma ya gari dogo jeusi ambalo lilikuwa limeegezwa pembeni mwa barabara. Ilikuwa tu kama kwenye sinema wakati majambazi huja na kumteka mtu nyara kweupe kabisa, isipokuwa sasa ilikuwa ikitufanyikia katika maisha halisi, na ilikuwa ya kutisha sana. Nilizidiwa sana na nilichoweza kufanya tu ni kumwomba Mungu kisirisiri tena na tena: “Mungu Mpendwa! Niokoe! Ee Mungu, tafadhali niokoe….” Kabla ya kupata tena umakini wangu, gari hilo dogo lilisimama katika uga mkubwa wa Ofisi ya Usalama wa Umma ya Manispaa. Ni wakati huo tu ndipo niligundua kuwa tulikuwa tumeangukia mikononi mwa polisi. Muda mfupi baadaye, dada Wang aliletwa pia. Sisi sote watatu tulipelekwa ofisini kwenye ghorofa ya pili na afisa mmoja, bila maelezo hata kidogo, alichukua ngawira mifuko yetu na kutushurutisha tusimame tukiwa tumetazama ukuta. Kisha alitulazimisha tuvue mavazi yetu hadi kuwa uchi na kufanya upekuzi wa mwili, akichukua ngawira vifaa kadhaa kuhusu kazi yangu kanisani, risiti za pesa za kanisa ambazo zilikuwa zimehifadhiwa, simu zetu za rununu, zaidi ya yuani 5,000 pesa taslimu, kadi ya benki na saa, pamoja na mali nyingine za kibinafsi ambazo tulikuwa nazo na kwenye mifuko yetu, katika harakati hiyo. Haya yote yalipokuwa yakijiri, maafisa wa polisi saba au wanane waliendelea kuingia na kutoka katika chumba hicho na maafisa wawili ambao walikuwa wakitusimamia hata waliangua kicheko na kunielekeza, wakisema, “Huyu ni mtu mashuhuri kanisani, inaonekana kuwa tumemkamata mkubwa leo.” Muda mfupi baadaye, maafisa wanne wa polisi wenye kuvalia mavazi ya kiraia walinitia pingu mikononi, wakayafunika macho yangu kwa kitambaa cha kuziba macho, na kunisindikiza hadi katika tawi la Ofisi ya Usalama wa Umma nje ya jiji.

Nilipoingia katika chumba cha mahojiano na kuona dirisha lililokuwa juu, na lenye kiunzi cha nondo ya chuma na kiti cha mateso cha kutisha, na kilichoonekana kuwa kibaya, hadithi za kuogofya za ndugu ambao walikuwa wameteswa hapo zamani ziliingia polepole katika mawazo yangu. Nilipofikiria mateso yasiyojulikana ambayo afisa hao waovu wa polisi wangenitesa baadaye, niliogopa sana na mikono yangu ilianza kutetemeka bila kutaka. Katika hali hii ya kukata tamaa, nilifikiria maneno ya Mungu: “Basi bado unabeba woga moyoni mwako, na moyo wako bado haujazwi na fikira kutoka kwa Shetani? Mshindi ni nini? Wanajeshi wazuri wa Kristo lazima wawe jasiri na kunitegemea kuwa wenye nguvu kiroho; lazima wapigane kuwa wapiganaji na wapambane na Shetani hadi kufa(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 12). Nuru ya maneno ya Mungu ilituliza polepole moyo wangu uliokuwa na wasiwasi na kuniwezesha kutambua kwamba hofu yangu ilikuwa na chanzo chake katika Shetani. Nilijiwazia: “Shetani anataka kuutesa mwili wangu ili niweze kujisalimisha kwa udhalimu wake. Siwezi kudanganywa na njama yake ya hila. Wakati wote, Mungu daima atakuwa tegemeo langu madhubuti na msaada wangu wa milele. Huu ni wakati wa vita vya kiroho na ni muhimu kwamba niwe shahidi kwa Mungu. Sina budi kusimama kwenye upande wa Mungu na siwezi kukubali kushindwa na Shetani.” Baada ya kugundua hayo, nilimwomba Mungu kimoyomoyo: “Ee Mwenyezi Mungu! Ni kwa ajili ya nia yako nzuri ndipo nimeanguka mikononi mwa polisi hawa waovu leo. Hata hivyo, kimo changu ni kidogo sana na nina wasiwasi na hofu. Ninaomba Unipe imani na ujasiri, ili nijikomboe kutoka katika masuto ya ushawishi wa Shetani, nisijisalimishe kwake na niwe shahidi Kwako kwa njia imara!” Baada ya kumaliza maombi yangu, moyo wangu ulijawa na ujasiri, na kamwe sikuhisi kuogopeshwa sana na wale polisi waovu wenye sura zenye nia mbaya.

Wakati huo huo, maafisa wawili walinisukuma kwenye kiti cha mateso na kufunga mikono na miguu yangu. Mmoja wa maafisa, jitu kubwa katili, aliyaelekezea maneno kadhaa ukutani ambayo yaliandikwa “Utekelezaji wa Sheria Uliostaarabika” na kisha akagonga meza kwa kishindo na kufoka, “Unajua uko wapi? Ofisi ya Usalama wa Umma ni tawi la serikali ya China ambalo linabobea katika ukatili! Usiposema ukweli, utapata mateso unayostahili! Ongea! Jina lako ni nani? Una umri wa miaka mingapi? Unatoka wapi? Una cheo kipi kanisani?” Asili yake ya shari pamoja na kukiri kwake binafsi kwa kusema ukweli, kuhusu asili ya kweli ya shirika hili la utekelezaji wa kitaifa, Ofisi ya Usalama wa Umma, kulinijaza ghadhabu. Nilijiwazia: “Wao daima hudai kuwa ‘Polisi wa Umma’ na kwamba lengo lao ni ‘kuwaondoa waovu na kuwaruhusu wafuata sheria kuishi kwa amani,’ lakini kwa kweli wao ni kikundi cha majambazi, maharamia na watu wanaolipwa ili waue. Wao ni pepo wanaoendeleza shambulio la kulenga haki na kuwaadhibu raia wema, waadilifu! Polisi hawa hawatilii maanani wale wanaovunja sheria na kufanya uhalifu, wakiwaruhusu kuishi nje ya mkono wa sheria. Lakini, licha ya ukweli kwamba yote tuyafanyayo ni kumwamini Mungu, kusoma neno la Mungu na kutembea katika njia inayofaa maishani, tumekuwa walengwa wakuu wa kikundi hiki cha wauaji katili. Serikali ya CCP kwa kweli ni mpinduzi potovu wa haki.” Ingawa niliwachukia polisi hao waovu kwa moyo wangu wote, nilijua kuwa kimo changu kilikuwa kidogo sana na singeweza kuhimili adhabu na mateso yao ya kikatili, kwa hivyo nilimwomba Mungu tena na tena, nikimsihi anipe nguvu. Wakati huo tu, maneno ya Mungu yalinipa nuru: “Imani ni kama daraja moja la gogo la mti, wale ambao hushikilia maisha kwa unyonge watakuwa na ugumu katika kulivuka, lakini wale ambao wako tayari kujitolea wenyewe wanaweza kulivuka bila wasiwasi(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 6). Faraja na utiaji moyo wa maneno ya Mungu ulinisaidia kunipa mafunzo ya msingi, na nilijiwazia: “Leo ninapaswa kuwa tayari kuhatarisha kila kitu—ikiwa jambo baya zaidi litatendeka na nife, basi iwe hivyo. Ikiwa kikundi hiki cha pepo kinadhani kuwa kitapata habari kutoka kwangu kuhusu pesa za kanisa, kazi au viongozi wetu, kinapaswa kufikiria tena!” Baadaye, bila kujali jinsi walivyonihoji au kujaribu kupata habari kutoka kwangu kwa kutumia nguvu, sikusema lolote.

Walipoona kwamba nilikuwa nikikataa kuzungumza, mmoja wa maafisa alikasirika sana, na baada ya kubamiza meza, alinishambulia, akakipiga mateke kiti cha mateso ambacho nilikuwa nimekikalia na kisha akakisukuma kichwa changu huku akifoka, “Tuambie unachokijua! Usidhani kuwa hatujui chochote. Ikiwa hatukujua chochote, basi unafikiria ni vipi tuliweza kuwakamata ninyi watatu kwa mkataa?” Afisa mwingine mrefu wa polisi alisema kwa sauti kubwa, “Usiniudhi! Tusipokuonjesha maumivu madogo, utafikiri kwamba tunatoa vitisho visivyo na maana. Simama!” Mara tu alipozungumza, alinivuta kutoka kwenye kiti cha mateso hadi chini ya dirisha mara moja, ambalo lilikuwa juu sana ukutani na lilikuwa na kiunzi cha nondo ya chuma. Walitumia jozi moja ya pingu zilizokuwa na misumari kwa kila mkono, ncha moja ikiwa imefungwa karibu na mikono yangu na nyingine ikishikizwa kwenye kiunzi cha nondo ya chuma ili nining’inie kwa mikono yangu kutoka dirishani na niliweza tu kugusa chini kwa sehemu ya wayo chini ya kidole. Mmoja wa polisi waovu aliwasha kiyoyozi ili kupunguza halijoto chumbani na kisha akanipiga kofi vibaya kichwani kwa kutumia kitabu kilichokunjwa. Alipoona kuwa bado nilikaa kimya, alifoka kwa ghadhabu kubwa sana: “Utazungumza au la? Usipozungumza, ‘tutakuning’iniza’!” Baada ya kusema hayo, alitumia ukanda mrefu wa aina ya kijeshi wa kufunga mizigo kisha akafunga ukanda huo kwenye kiti cha mateso. Maafisa wawili kisha walivuta kiti cha mateso mbali na ukuta ili kwamba nilining’inia hewani. Mwili wangu ulipokuwa ukisonga mbele, pingu ziliteleza chini hadi kwenye sehemu ya chini ya vifundo vya mikono yangu na misumari iliyokuwa ndani ya pingu zilichoma mishipa kwenye sehemu ya nyuma ya mikono yangu. Nilikuwa na maumivu makali, lakini niliuma mdomo wangu kwa nguvu ili kujizuia kupiga mayowe kwa sababu sikutaka kuwaruhusu polisi hao waovu wanicheke. Mmoja wao alisema kwa tabasamu baya, “Inaonekana si chungu! Acha nikuongezee.” Baada ya kusema hivyo, aliinua mguu wake na kuukanyagisha kwa nguvu kwenye mashavu ya miguu yangu kisha alitingisha mwili wangu kutoka upande mmoja hadi mwingine. Hii ilisababisha pingu kushikilia kwa kukaza kandokando ya mikono yangu na hatimaye iliuma sana kiasi kwamba sikuweza kujizuia kupiga mayowe kwa ajili ya maumivu makali, jambo ambalo liliwafanya polisi hao wawili waovu waangue kicheko. Ni wakati huo tu ndipo aliacha kugandamiza miguu yangu, akiniacha nikining’inia hapo hewani. Baada ya muda wa takribani dakika ishirini, afisa huyo ghafla alikipiga teke kiti cha mateso kuelekea kwangu, kikatoa mlio mbaya wa sauti nyembamba na nilipiga uyowe huku mwili wangu ukirudi tena mahali pake, ukining'inia kutoka ukutani na sehemu ya wayo chini ya kidole tu ukigusa chini. Wakati huo huo, pingu ziliteleza na kurudi kwenye vifundo vya mikono yangu. Kwa ajili ya kufunguka kwa ghafla kwa pingu zangu, damu ilizunguka haraka kutoka kwa mikono yangu na kurudi mikononi mwangu, ikisababisha maumivu makali kutokana na shinikizo la damu iliyokuwa ikirudi. Polisi hao wawili wabaya walicheka vibaya kwa sauti kubwa walipoona kuteseka kwangu kisha wakaanza kunihoji, wakiuliza, “Kuna watu wangapi katika kanisa lako? Ninyi huhifadhi pesa wapi?” Swali hili la mwisho lilifichua waziwazi nia ya Shetani ya kustahili dharau: Sababu yao ya kunipitisha katika mateso na maumivu haya yote makali, sababu yao ya kutumia mbinu za ibilisi na za kikatili zote ni ili waweze kuiba pesa za kanisa. Walitarajia bila mafanikio na bila aibu kutumia pesa za kanisa kwa kusudi lao wenyewe. Nilipotazama nyuso zenye uroho, mbovu, nilikasirika Bila kujali jinsi walivyonihoji, nilikataa kuzungumza hadi walikasirika sana kiasi kwamba walianza kutupa matusi: “Ala! Wewe ni mjeuri kushughulikia! Tutaona utavumilia kwa muda gani!” Baada ya hapo, kwa mara nyingine tena walivuta kiti cha mateso mbali na ukuta, wakinining’iniza tena hewani. Wakati huu, pingu zilikamata kwa kukaza kwenye vidonda ambavyo tayari vilikuwa wazi kwenye sehemu ya nyuma ya mkono yangu, na mikono yangu ilivimba kwa kasi na kufurishwa na damu, ikihisi kana kwamba ilikuwa inakaribia kulipuka. Maumivu yalikuwa hata makali zaidi kuliko wakati wa kwanza. Maafisa walielezea picha dhahiri wao kwa wao kuhusu “matendo yao adhimu ya zamani” katika kuwatesa na kuwaadhibu wafungwa. Haya yaliendelea kwa dakika kumi na tano kabla wao hatimaye kupiga mateke kiti tena na nilirudi tena katika mkao wangu wa zamani nikining'inia moja kwa moja kutoka dirishani na sehemu ya wayo chini ya kidole ya miguu yangu tu ikigusa chini. Katika harakati hiyo, maumivu machungu yalinizidi kwa mara nyingine. Wakati huo huo, afisa wa kiume mfupi mnene aliingia na kuuliza, “Hajazungumza bado?” Maafisa hao wawili walijibu, wakisema, “Huyu ni Liu Hulan halisi!” Polisi huyo mnene mwovu alinijia na kunizaba makofi kwa nguvu usoni, akinizomea vibaya, “Hebu tuone wewe ni mjeuri kiasi gani! Hebu nifungue mikono hiyo yako.” Niliangalia chini kwenye mkono wangu wa kushoto na kuona kwamba ilikuwa imevimba vibaya na ilikuwa imegeuka kuwa rangi nyeusi ya zambarau zambarau. Wakati huo huo, polisi huyo mwovu alikamata kwa nguvu vidole vya mkono wangu wa kushoto na kuanza kuvitikisa mbele na nyuma akivisugua na kuvibana mpaka kufa ganzi kwa mara nyingine tena kukabadilishwa kuwa maumivu. Kisha aliweka sawa pingu ili ziwe katika mpangilio wa kukaza zaidi na kuwaashiria maafisa hao wengine wawili wanivute juu angani tena. Nilikuwa, kwa mara nyingine, nimening’inia hewani na niliachwa katika mkao huo kwa muda wa dakika ishirini kabla ya kuteremshwa. Waliendelea kunivuta juu hadi hewani kisha kuniteremsha chini tena na tena, wakinitesa hadi nilitamani ningekufa ili niepe maumivu. Kila wakati pingu ziliteleza juu na chini ya mikono yangu nilikuwa na maumivu makali zaidi kuliko wakati uliopita. Mwishowe, pingu zilizokuwa na misumari zilichoma vifundo vya mikono yangu na kutengua ngozi kwenye sehemu ya nyuma ya mikono yangu, na kusababisha kutokwa na damu kwa wingi. Mzunguko wa damu mikononi mwangu ulikuwa umezuiliwa kabisa na ilikuwa imevimba kama baluni. Kichwa changu kilikuwa kikinigonga kwa sababu ya ukosefu wa oksijeni na nilihisi kana kwamba kilikaribia kulipuka. Kwa kweli nilidhani nitakufa.

Nilipokuwa tu nikifikiria singeweza kustahimili zaidi, kifungu cha maneno ya Mungu akilini mwangu: “Alipokuwa njiani kuelekea Yerusalemu, Yesu alihisi maumivu makali, kama kwamba kisu kilikuwa kimedungwa ndani ya moyo Wake, ilhali hakuwa na nia yoyote ya kwenda kinyume cha Neno lake; kila mara kulikuwa na nguvu zenye uwezo mkuu zilizomvutia Yeye kuelekea mahali ambapo Angesulubiwa(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Jinsi ya Kuhudumu kwa Upatanifu na Mapenzi ya Mungu). Maneno ya Mungu yalinipa ongezeko la ghafla la nguvu na nilifikiria jinsi Bwana Yesu alivyokuwa ameteseka msalabani: Alipigwa mijeledi, alidhihakiwa na kudhalilishwa na askari wa Kirumi na alipigwa hadi akatokwa na damu kwa wingi. Na bado alikuwa akilazimishwa kubeba msalaba huo mzito, ule ule ambao mwishowe walimsulubisha Akiwa hai, hadi kila tone la damu mwilini Mwake lilikuwa limemwagika. Mateso ya kikatili namna gani! Mateso yasiyowazika yalioje! Lakini Bwana Yesu alivumilia yote akiwa kimya. Ijapokuwa maumivu hayo yalikuwa kwa hakika makubwa yasivyoelezeka, Bwana Yesu alijiweka katika mikono ya Shetani kwa hiari kwa ajili ya ukombozi wa wanadamu wote. Nilijiwazia: “Hivi majuzi, Mungu amepata mwili kwa mara ya pili na kuja katika nchi ya China inayomkana Mungu. Hapa, Amekumbana na majanga yenye hatari kubwa sana kuliko yale aliyokumbana nayo katika Enzi ya Neema. Tangu Mwenyezi Mungu alipoonekana na kuanza kutekeleza kazi Yake, serikali ya CCP imetumia kila mbinu inayowezekana kumkashifu, kumkufuru, kumwandama na kumkamata Kristo kwa shauku, wakitarajia bila mafanikio kuiharibu kazi ya Mungu. Mateso ambayo Mungu amepitia katika kupata Kwake kwa mwili mara mbili ni zaidi ya yale ambayo mtu yeyote anaweza kufikiria, sembuse kuvumilia. Kwa kuwa Mungu amevumilia mateso mengi kwa ajili yetu, ninapaswa kuwa na dhamiri zaidi; Sina budi kumridhisha Mungu na kumletea faraja, hata kama inamaanisha kifo changu.” Wakati huo, kutaabika kwa watakatifu na manabii wote kupitia vizazi vyote kulinijia akilini mwangu kwa ghafla: Danieli kwenye tundu la simba, Petro akitundikwa juu chini msalabani, Yakobo kukatwa kichwa…. Bila kumwacha yeyote, watakatifu na manabii hawa wote walikuwa na ushahidi kwa Mungu walipokuwa wakichungulia kifo, na niligundua kuwa nilipaswa kulenga kuiga imani yao, kujitolea kwao, na kujisalimisha kwao kwa Mungu. Kwa hivyo, nilimwomba Mungu kimoyomoyo: “Mungu mpendwa! Huna hatia ya dhambi lakini ulisulubiwa kwa ajili ya wokovu wetu. Kisha ukapata mwili nchini China ili kufanya kazi Yako, na kuhatarisha maisha Yako. Upendo Wako ni mkubwa sana kiasi kwamba kamwe sitaweza kulipa. Ni heshima yangu kubwa kuteseka pamoja nawe leo na niko tayari kuwa shahidi ili kufariji moyo Wako. Hata Shetani akichukua maisha yangu, kamwe sitasema hata neno moja la malalamiko!” Akili yangu ikiwa imelenga upendo wa Mungu, maumivu mwilini mwangu yalionekana kupunguka sana. Katika nusu ya pili ya usiku huo, polisi waovu waliendelea kunitesa kwa zamu. Ilikuwa saa tatu asubuhi, asubuhi iliyofuata ndipo tu mwishowe walifungua miguu yangu na kuniacha nikining'inia kutoka kwenye dirisha. Mikono yangu yote miwili ilikuwa imekufa ganzi kabisa na bila hisia na mwili wangu wote ulikuwa umevimba. Wakati huo, dada ambaye nilikuwa nikitimiza wajibu naye alikuwa ameletwa katika chumba cha mahojiano cha karibu. Kwa ghafla, maafisa nane au tisa waliandamana katika safu wakiingia katika chumba changu cha mahojiano, na afisa wa polisi mfupi na mnene aliingia akiwa amenuna na kuwauliza polisi waovu waliokuwa wakinishughulikia: “Hajazungumza bado?” “Bado,” walijibu. Mara tu aliposikia jibu lao, alinirukia, akanizaba makofi usoni mara mbili na kusema kwa sauti kubwa kwa hasira, “Bado hushirikiani nasi! Tunalijua jina lako, na tunajua wewe ni kiongozi mwenye madaraka makubwa kanisani. Usikosee kwa kufikiria kwamba hatujui chochote! Je, uliweka pesa wapi?” Alipoona nikikaa kimya, alinitishia, akisema, “Usiposema ukweli, hali yako itakuwa mbaya zaidi tukipata habari sisi wenyewe. Kwa kuzingatia cheo chako kanisani, utapewa hukumu ya muda wa miaka ishirini gerezani!” Baadaye, walinipokonya kadi yangu ya benki na kuuliza jina kwenye kadi hiyo na nambari ya siri. Nilijiwazia, “Waache waone, ni nani anayejali. Familia yangu haikuhawilisha pesa nyingi katika akaunti hiyo. Labda ikiwa wataona, hawataendelea kunisumbua kuhusu fedha za kanisa.” Baada ya kuamua, niliwaambia jina na nambari ya siri.

Baadaye, niliomba kwenda msalani na ni wakati huo tu ndipo hatimaye waliniteremsha. Wakati huo, nilikuwa nimeshindwa kabisa kudhibiti matumizi ya miguu yangu, kwa hivyo walinibeba hadi msalani na kuwa walinzi nje. Hata hivyo, tayari nilikuwa nimepoteza hisia zote mikononi mwangu na amri kutoka katika ubongo wangu hazikuwa hasa zikiifikia, kwa hivyo nilisimama tu hapo nikiegemea ukuta, nikashindwa kabisa kufungua suruali yangu. Nilipokuwa bado sijatoka nje baada ya muda, mmoja wa polisi alipiga mlango mateke kuufungua na kusema kwa sauti kubwa akiwa na tabasamu la kiasherati, “Bado hujamaliza?” Alipoona kwamba singeweza kusogeza mikono yangu, alinikaribia na kufungua suruali yangu kisha akafunga tena suruali yangu nilipomaliza. Kikundi cha maafisa wa kiume walikuwa wamekusanyika nje ya msala wakitoa maoni ya dhihaka ya kila aina na kunidhalilisha kwa lugha yao chafu. Dhuluma ya majambazi na pepo hao ya kumdhalilisha msichana asiye na hatia, mwenye umri wa miaka ishirini na kitu kama mimi ghafla ilinizidi na nilianza kulia. Iliniingia pia mawazoni kwamba, ikiwa mikono yangu ilikuwa imepooza kwa kweli na singeweza kujitunza katika siku za usoni, ingekuwa afadhali nife. Ikiwa ningeweza kutembea vizuri wakati huo, ningekuwa nimeruka nje ya jengo hilo na kujitia kitanzi papo hapo. Nilipokuwa tu katika hali yangu dhaifu zaidi, wimbo wa kanisa “Ninatamani Kuona Siku ya Utukufu wa Mungu” ulikuja akili: “Nitampa Mungu upendo na uaminifu wangu na kukamilisha misheni yangu ya kumtukuza Mungu. Nimeazimia kusimama imara katika ushuhuda kwa Mungu, na kamwe kutoshindwa na Shetani. Eh, kichwa changu kinaweza kupasuka na damu kutiririka, lakini ujasiri wa watu wa Mungu hauwezi kupotea. Ushawishi wa Mungu umo moyoni, ninaamua kumwaibisha Shetani Ibilisi. Maumivu na shida vimeamuliwa kabla na Mungu, nitastahimili aibu ili kuwa mwaminifu Kwake. Kamwe sitamsababisha Mungu alie au kusumbuka tena” (Mfuateni Mwanakondoo na Kuimba Nyimbo Mpya). Nuru ya Mungu na mwangaza Wake kwa mara nyingine tena ulinipa imani na roho yangu iliimarishwa. Nilijiwazia: “Siwezi kudanganywa na ujanja wa Shetani na sitaki kujitia kitanzi kwa sababu ya jambo kama hili. Wananidhalilisha na kunidhihaki ili nifanye kitu ambacho kitamuumiza na kumsaliti Mungu. Ikiwa nitakufa, nitakuwa nikitumbukia moja kwa moja katika njama yao. Siwezi kuruhusu njama za Shetani zifanikiwe. Hata kama kwa kweli nimekuwa kiwete, almradi bado nina pumzi moja iliyobaki ndani yangu, lazima niendelee kuishi ili kuwa na ushuhuda wa Mungu.”

Niliporudi kwenye chumba cha mahojiano, nilianguka sakafuni kwa ajili ya uchovu. Polisi kadhaa walinizunguka na kusema kwa sauti kubwa, wakiniamuru nisimame. Yule afisa mfupi, mnene aliyekuwa amenizaba makofi usoni alinirukia, akanipiga mateke mabaya na kunishutumu kwamba nilikuwa nikijisingizia. Wakati huo, mwili wangu ulianza kutetemeka, na nikawa mwenye kuishiwa na pumzi haraka na nikaanza kupumua kupita kiasi. Mguu wangu wa kushoto na upande wa kushoto wa kifua changu ulianza kusukasukana na kubanana. Mwili wangu wote ukawa baridi na mwenye mavune na bila kujali jinsi maafisa wawili waliuvuta na kuuinua, hawakuweza kuninyoosha. Akilini mwangu, nilifahamu kuwa Mungu alikuwa akitumia maumivu na mateso kunifungulia njia, vinginevyo wangekuwa wameendelea kunitesa kikatili. Ni baada tu ya kuona hali yangu ya hatari niliyokuwamo ndipo maafisa hao waovu hatimaye waliacha kunipiga. Kisha walinifunga kwenye kiti cha mateso na wakaenda katika chumba cha pili kumtesa dada yangu wa kanisa, wakiacha nyuma maafisa wawili wa kunilinda. Nilipokuwa nikimsikia dada yangu akipiga mayowe tena na tena kwa ukwenzi wa kuogofya, nilitamani sana kuwaendea kwa nguvu pepo hao na kupigana nao hadi kufa, lakini mambo yalivyokuwa, nilikuwa nimeanguka katika rundo na nilikuwa nimechoka kabisa, kwa hivyo nilichoweza kukifanya tu ni kumwomba Mungu na kumsihi Mungu ampe dada yangu nguvu na Amlinde ili aweze kuwa shahidi. Wakati huo huo, nilikilaani daima chama hicho, kiovu na kibaya ambacho kilikuwa kimewatosa watu wake katika lindi la mateso na nilimwomba Mungu awaadhibu wanyama hawa walio katika umbo la kibinadamu. Baadaye, waliponiona nimeanguka hapo, nikionekana karibu kufa, na hawakutaka kujihusisha na mtu aliyekuwa akifa chini ya ulinzi wao, hatimaye walinipeleka hospitalini. Baada ya kufika hospitalini, miguu yangu na kifua changu kilianza kusukasuka kuelekeana na iliwachukua watu kadhaa kuuvuta mwili wangu urudi katika mkao ulionyooka. Mikono yangu yote miwili ilikuwa imevimba kama baluni na ililowa damu iliyoganda. Mikono yangu yote ilivimba kwa usaha na hawakuweza kuanza matibabu ya kuingiza dawa kupitia mishipa kwa sababu mara tu waliponipiga sindano, damu ilitoka mshipani na kutiririka, ikinyunyiza tishu zilizokuwa karibu na kutokwa na damu kutoka kwenye sehemu iliyopigwa sindano. Daktari alipoona kilichokuwa kikitendeka, alisema, “Tunapaswa kuondoa pingu hizi!” Aliwashauri polisi kwamba nipelekwe katika hospitali ya manispaa kwa uchunguzi zaidi, kwa sababu alikuwa na wasiwasi kuwa nilikuwa na tatizo la moyo. Polisi hao waovu hawakutaka kufanya lolote kunisaidia, lakini baada ya hapo hawakunitia pingu tena, Siku iliyofuata, afisa ambaye alikuwa akinihoji aliandikisha taarifa iliyojawa na kufuru na kashfa kumhusu Mungu ili itumiwe kama ushuhuda wangu wa mdomo na kuniamuru niitie sahihi. Nilipokataa kutia sahihi taarifa hiyo, alighadhabika, akakamata mkono wangu kwa nguvu na kunilazimisha kutia alama ya kidole changu kwenye taarifa hiyo.

Karibu jioni tarehe 9 mwezi Aprili, mkurugenzi wa divisheni pamoja na polisi wengine wawili wa kiume walinisindikiza kwenda kizuizini. Daktari aliyekuwa kizuizini alipoona kuwa mwili wangu wote ulikuwa umevimba, na kwamba sikuweza kutembea, sikuwa na hisia mikononi mwangu na nilionekana kuwa katika hali mahututi, alikataa kunichukua, akiogopa kuwa ninaweza kufa huko. Baadaye, mkurugenzi wa divisheni alijadiliana na gavana wa kizuizi kwa muda wa takribani saa moja na aliahidi kwamba kama kitu chochote kingenitendekea, kizuizi hakingewajibika, na ni wakati huo tu ndipo gavana hatimaye alikubali kunifunga.

Zaidi ya muda wa siku kumi baadaye, polisi waovu zaidi ya 12 walihamishwa kutoka maeneo mengine na kuwekwa kwa muda kizuizini ili kunihoji kwa zamu siku nzima usiku na mchana. Kuna mipaka iliyowekwa kwa muda ambao mfungwa anaweza kuhojiwa, lakini polisi walisema kwamba hii ilikuwa kesi kubwa na muhimu ya asili nzito mno, kwa hivyo hawangeniacha hata kidogo. Kwa sababu waliogopa kwamba, ikiwa wangenihoji kwa muda mrefu sana ningeweza, kwa kuzingatia hali yangu dhaifu, kupata hali fulani ya dharura ya kiafya, wangemaliza mahojiano yao takribani saa saba usiku na kunirudisha kwenye seli yangu ya jela, wakiniita alfajiri ya asubuhi inayofuata. Walinihoji kwa muda wa takribani masaa 18 kwa siku, siku tatu mfululizo. Hata hivyo, bila kujali jinsi walivyonihoji kwa ukali, sikusema lolote. Walipoona kwamba mbinu zao za ukali hazikukuwa zikifanya kazi, walibadilisha kwa mbinu za upole. Walianza kuonyesha kujali majeraha yangu na walininunulia dawa na kupaka dawa za kuchua kwenye vidonda vyangu. Nilipokumbana na onyesho hili la ghafla la “wema,” niliacha kujihadhari, nikiwaza: “Ikiwa nitawaambia tu jambo lisilo la maana kuhusu kanisa, pengine nitakuwa sawa....” Mara, maneno ya Mungu yalitokea akilini mwangu: “Msichukue mtazamo usio mwangalifu, ila mnikaribie zaidi mara nyingi wakati mambo yanapowafika; kuweni makini na kujihadhari zaidi katika mambo yote kuepuka kukosea kuadibu Kwangu, na kuepuka kuwa windo la ujanja za Shetani(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Matamko ya Kristo Mwanzoni, Sura ya 95). Ghafla niligundua kuwa nilikuwa nimedanganywa na njama ya hila ya Shetani. Je, si watu hawa ndio wale wale ambao wamekuwa wakinitesa siku chache zilizopita? Wangeweza kugeuza mienendo yao, lakini asili yao ilikuwa isiyobadilika—pepo, sikuzote ni pepo. Maneno ya Mungu yaliniamsha kwa ukweli kwamba walikuwa ni mbwa mwitu tu katika mavazi ya kondoo, na kwamba kila wakati walikuwa na malengo ya siri. Baadaye, bila kujali jinsi walivyonishawishi au kunihoji vikali, sikusema neno lingine. Muda mfupi baadaye, Mungu alifichua tabia zao za kweli; afisa ambaye walimwita Kapteni Wu aliniuliza kwa ukali: “Wewe ni kiongozi kanisani, ilhali hujui pesa ziko wapi? Usipotuambia, tuna mbinu za kupata habari!” Afisa wa polisi mzee na aliyekonda sana alianza kuangua mfuatano wa matusi, akisema kwa sauti kubwa, “Ala! Tunakupa uhuru mdogo kisha unataka kupata uhuru zaidi! Usipozungumza, tutakupeleka nje na kukuning’iniza tena. Tutaona iwapo bado unataka kuwa Liu Hulan na kutuficha habari tena! Nina njia nyingi za kukushughulikia!” Kadiri alivyoongea kwa namna hii, ndivyo nilivyoazimia zaidi kukaa kimya. Mwishowe alighadhibika na kunijia na kunipiga kikumbo, akisema, “Ukiwa na mwenendo wa aina hii, miaka ishirini itakuwa kifungo kidogo!” Baada ya kusema hivyo, alitoka nje ya chumba hicho kwa nguvu huku akiwa amevunjika moyo. Baadaye, afisa kutoka katika Idara ya Usalama wa Umma aliyesimamia maswala ya usalama wa taifa alikuja kunihoji. Alitoa matamshi mengi yanayomsuta na kumpinga Mungu na alijigamba kila wakati kuhusu jinsi alivyokuwa na uzoefu na mwenye maarifa, ambayo ilisababisha maafisa wengine kumsifu kwa wingi. Nilipoangalia ubaya wake wa kujisikia na wa kujiona, na niliposikia uongo wake wa kupotosha ukweli na wa kueneza uongo na shutuma zake za uongo, nilihisi chuki na karaha kwa afisa huyu. Singeweza hata kuvumilia kumtazama na kwa hivyo nilikaza macho yangu moja kwa moja kwenye ukuta uliokuwa mbele yangu na kukanusha kila moja ya hoja yake kichwani mwangu. Makemeo na matusi yake yalidumu asubuhi nzima na hatimaye alipomaliza, aliniuliza maoni yangu. Nilisema bila stahamala: “Sijasoma, kwa hivyo sielewi kuhusu kile ambacho umekuwa ukizungumzia kwa sauti nzito.” Akiwa na ghadhabu, aliwaambia wahojaji wengine, “Hakuna tumaini kwake. Nadhani tayari amefanywa kumwabudu mungu, amekwisha!” Baada ya hapo aliondoka kimyakimya akiwa mwenye huzuni.

Katika kuteseka kupitia mateso ya kikatili ya ibilisi, nilipitia mabaya ya maisha yasiyo na haki zozote za kibinadamu katika nchi hii iliyotawaliwa na chama kiovu cha CCP. Kulingana na serikali ya CCP, waumini katika Mungu ni kama chembe katika macho yao na miiba kwao; walitumia mbinu zote kuniadhibu na kunitesa kwa tumaini la bure la kuniua. Hata hivyo, Mungu ndiye tegemeo langu thabiti na wokovu wangu; Aliniokoa kutoka katika hatari ya kifo tena na tena, akiniwezesha kupata upendo wa kweli wa Mungu na kuona wema na uzuri wa moyo wa Mungu. Polisi waovu waliponivuta hadi kwenye seli yangu ya jela kizuizini na nikaona kuwa dada Wang alikuwapo ndani ya seli hiyo hiyo, kumwona mpendwa huyu kulinifanya nijawe na uchangamfu moyoni mwangu. Nilijua kuwa huu ulikuwa mpango na utaratibu wa Mungu na kwamba upendo wa Mungu ulikuwa ukinitunza, na nilijua kuwa Mungu alikuwa amefanya hivyo kwa sababu, wakati huo, nilikuwa karibu kuwa kiwete—mikono yangu ilikuwa imevimba na kufutuka kwa usaha, sikuwa na hisia kwenye vidole vyangu, ambavyo vilikuwa vinene kama soseji na vilihisi vigumu kugusa, singeweza kusogeza miguu yangu na mwili wangu wote ulikuwa dhaifu na ulikuwa na maumivu. Kwa muda wa miezi sita, sikuwahi kutoka kwenye kitanda changu cha tofali kilichokuwa na joto na sikuweza kujitunza. Ni baada tu ya muda wa miezi sita ndipo nilipata tena utendaji mikononi mwangu, lakini bado sikuweza kushikilia vitu (hadi leo, nikijaribu kushikilia sahani kwa mkono mmoja, mkono unauma, unakuwa dhaifu na kufa ganzi, na nisipotumia mkono wangu mwingine kuutegemeza, siwezi hata kushikilia sahani juu). Wakati huo, dada yangu alinitunza kila siku—alinisugua meno, akanawisha uso wangu, akaniosha, akachana nywele zangu na kunilisha…. Mwezi mmoja baadaye, dada yangu aliachiliwa, na niliambiwa kwamba nilikuwa nimekamatwa rasmi. Baada ya dada yangu kuachiliwa, nilipofikiria jinsi nilivyokuwa bado siwezi kujitunza na bila kujua kuwa ningefungwa kwa muda gani zaidi, nilihisi asiyejiweza na mwenye ukiwa sana. Sikuweza kujizuia kumwomba Mungu: “Ee Mungu, ninahisi kama kiwete—ninapaswaje kuendelea kwa namna hii? Ninakuomba uulinde moyo wangu, ili niweze kushinda hali hii.” Nilipokuwa tu nikitaka kuchanganyikiwa na kuhisi nimepoteza matumaini, nilifikiria maneno ya Mungu: “Je, mmefikiria kwamba siku moja Mungu atawaweka katika mahali pasipojulikana? Je, mnaweza kuwazia siku ambayo huenda Nikawapokonya kila kitu, ni kipi kingewakumba? Nguvu yenu siku hiyo ingekuwa vile ilivyo sasa? Je, imani yenu ingejitokeza tena?(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Ni Lazima Muielewe Kazi—Msifuate kwa Rabsha!). Maneno ya Mungu yalikuwa kama nguzo inayong'aa ikiangaza moyo wangu na kuniwezesha kuelewa mapenzi Yake. Nilijiwazia: “Hali ambayo ninakabili sasa ndiyo ambayo sina uzoefu nayo kabisa. Mungu anataka nipate uzoefu wa kazi Yake ndani ya hali ya aina hii ili akamilishe imani yangu. Ingawa dada yangu ameniacha, hakika Mungu hajaniacha! Nilipokumbuka kuhusu njia ambayo nimetembea, Mungu ameniongoza katika kila hatua safarini! Kama nitamtegemea Mungu, hakuna shida ambayo haiwezi kushindwa. Niliona kuwa imani yangu ilikuwa kidogo sana, nilimwomba Mungu: “Mungu Mpendwa, niko tayari kujiweka mikononi Mwako kikamilifu na kujisalimisha kwa mipango Yako. Bila kujali ninaweza kukumbana na hali gani siku zijazo. Nitajisalimisha Kwako na sitalalamika.” Baada ya kumaliza maombi yangu, nilihisi hali ya amani na utulivu. Alasiri ya siku iliyofuata, afisa wa marekebisho alileta mfungwa mpya. Alipoona hali yangu, alianza kunitunza bila hata mimi kumsihi. Katika jambo hili, niliona ustaajabishaji na uaminifu wa Mungu; Mungu hakuwa ameniacha—vitu vyote mbinguni na duniani viko mikononi mwa Mungu, ikiwemo mawazo ya mwanadamu. Isingekuwa mipango na utaratibu wa Mungu, kwa nini mwanamke huyu ambaye sikuwahi kukutana naye awe mzuri sana kwangu? Baada ya hapo, nilishuhudia hata upendo zaidi wa Mungu. Mwanamke huyo alipoachiliwa kutoka kizuizini, Mungu alimwinua mwanamke mmoja baada ya mwingine ambaye sikuwahi kukutana naye ili anitunze, na walikabidhiana utunzaji wangu mmoja baada ya mwingine kana kwamba walikuwa wakipokezana kifimbo cha mbio za kupokezana. Kulikuwa hata na wafungwa wengine ambao walihawilisha pesa hadi kwenye akaunti yangu baada ya kuachiliwa. Wakati huu, ingawa mwili wangu uliteseka kwa kiasi fulani, niliweza kujionea ukweli wa upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Bila kujali mwanadamu anatupwa katika hali ya aina gani, Mungu hamwachi kamwe, lakini hutumika kama msaada wake wa siku zote. Alimradi mwanadamu asipoteze imani katika Mungu, hakika ataweza kushuhudia matendo ya Mungu.

Nilizuiliwa kwa muda wa mwaka mmoja na miezi mitatu kisha nikashtakiwa na serikali ya CCP kwa kosa la “kufanya kazi kupitia shirika la xie jiao kuzuia kutekelezwa kwa sharia” na nilihukumiwa kifungo cha muda wa miaka mitatu na miezi sita gerezani. Kufuatia mimi kupatikana na hatia, nilihamishiwa hadi katika Gereza la Wanawake la Mkoa ili kutumikia kifungo changu. Gerezani, tulitendewa kinyama. Tulilazimishwa kufanya kazi ya sulubu kila siku na masharti ya sehemu ya kazi yetu ya kila siku yalizidi kiwango ambacho kila mtu angeweza kukikamilisha. Ikiwa hatungeweza kumaliza kazi yetu, tungepewa adhabu ya kutandikwa. Karibu pesa zote zilizochumwa kupitia kazi yetu ziliingia mifukoni mwa walinzi wa gereza. Tulipewa yuani chache tu kila mmoja kwa mwezi iliyodhaniwa kuwa ruzuku ya kuishi. Msemo rasmi ambao gereza lilitumia ni kwamba lilikuwa likiwaelimisha upya wafungwa kupitia kazi, lakini kwa uhalisi, tulikuwa tu mashine zao za kutengeneza pesa, watumishi wao wasiolipwa. Kadiri ionekanavyo, sheria za gereza za kupunguza hukumu za wafungwa zilionekana kuwa zenye huruma sana—kwa kutimiza masharti fulani, wafungwa walistahili kupunguziwa kifungo chao inavyofaa. Lakini kwa ukweli, hili lilikuwa singizio tu na lilikuwa kwa ajili tu ya sura. Kwa kweli, mfumo wao unaodaiwa kuwa wenye huruma ulikuwa tu maneno matupu yalioandikwa: Amri zilizotolewa na walinzi binafsi ndizo zilikuwa sheria halisi za nchi. Gereza lilidhibiti kabisa jumla ya kupunguzwa kwa hukumu ya kila mwaka ili kuhakikisha idadi ya “wafanyakazi” ni ya kutosha na kutoa uhakikisho kwamba mapato ya walinzi wa gereza hayatapungua. “Orodha ya kupunguza kifungo” ilikuwa mbinu iliyotumiwa na gereza kuongeza tija ya wafanyikazi. Kati ya mamia ya wafungwa waliokuwa gerezani, ni takribani wafungwa kumi tu ndio wangefaulu kuwa katika “orodha ya kupunguziwa kifungo” na kwa hivyo watu wangejitahidi sana kupita kiasi, walishiriki katika kula njama dhidi ya wao kwa wao ili kupata nafasi kwenye orodha. Hata hivyo, wafungwa wengi ambao wangeishia kuwa katika orodha walikuwa wale walio na uhusiano na polisi ambao hawakuhitajika kufanya kazi ya sulubu hapo mwanzoni. Wafungwa hawakuwa na lingine la kufanya ila kuzuia chuki yao kuhusu jambo hili wenyewe. Wengine walijiua wakipinga, lakini baada ya ukweli, gereza lingetunga bila utaratibu maalumu hadithi za kutuliza familia za wahasiriwa, na hivyo vifo vyao vyote vilikuwa vya bure. Huko gerezani, walinzi hawakuwahi kututendea kama wanadamu; ikiwa tulitaka kuzungumza nao, tulilazimika kuchutama na kinua macho yetu juu kuwatazama, na ikiwa lolote halikuwapendeza, wangetukaripia na kututukana kwa matusi machafu ya kuchukiza. Ikiwa maafisa wa ngazi ya juu wangekuja kutukagua, tulilazimishwa kujifanya tunashirikiana nao katika visingizio vyao, kwani wangetutishia hapo awali, wakisema kwamba tulihitajika kusema mambo mazuri kuhusu gereza, kama vile: “Milo yetu ni mitamu, walinzi hutujali daima, kamwe hatufanyi kazi zaidi ya masaa nane kwa siku na burudani mara wa mara huwekwa kwa ajili yetu….” Nyakati kama hizi, nilikasirika sana hadi mwili wangu wote ulitetemeka. Pepo hawa walikuwa wanafiki hivyo: Ni dhahiri kwamba wao tu walikuwa mazimwi wala watu, lakini walisisitiza kujifanya kwamba wao ni watu wema zaidi na wenye huruma zaidi. Jambo baya, la kudharauliwa na la aibu namna gani! Wakati miaka mitatu na nusu ya hukumu yangu hatimaye ilikamilika na nikarudi nyumbani, familia yangu haikuweza kuficha uchungu iliyohisi kwa kuniona nikionekana kama gofu la mtu, dhaifu sana na aliyechoshwa kiasi kwamba sikuweza kutambulika kwa urahisi, na machozi mengi yalimwagwa. Hata hivyo, mioyo yetu ilikuwa imejawa na shukrani kwa Mungu. Tulimshukuru Mungu kwamba nilikuwa bado hai na kwa ajili ya kunilinda ili niweze kuibuka kutoka jehanamu hiyo ya dunia nikiwa salama salmini.

Ni baada tu ya kurudi nyumbani ndipo nilipata habari kwamba nilipokuwa kizuizini, polisi waovu walikuwa wamekuja mara mbili na kupekua nyumba bila kuzuilika. Wazazi wangu, ambao wote wawili wanamwamini Mungu, walikuwa wamekimbia nyumba yao na walikaa karibu miaka miwili wakiwa watoro ili kukwepa kukamatwa na serikali. Hatimaye waliporudi nyumbani, magugu uani yalikuwa yamekua marefu kama nyumba yenyewe, sehemu za paa zilikuwa zimeanguka na mahali pote palikuwa mchafuko usiopendeza. Polisi pia walikuwa wameenda pote kijijini mwetu wakieneza uwongo juu yetu: Walisema kwamba nilikuwa nimemlaghai mtu pesa zake kiasi cha yuani milioni moja hadi zaidi ya milioni mia moja, (takribani dola 150,000 hadi 15,000,000) na kwamba wazazi wangu walikuwa wamemlaghai mtu kiasi cha mamia kadhaa ya melfu ya yuani ili wampeleke kakangu mdogo chuoni. Kundi hili la pepo lilikuwa kundi la waongo wa kitaalamu waliothibitishwa, bora zaidi kwenye taaluma hiyo! Kwa kweli, kwa sababu wazazi wangu walikuwa wamekimbia kutoka nyumbani, kaka yangu mdogo alilazimika kutumia pesa za msaada wa masomo na mikopo kulipa ada ya masomo na kumaliza chuo kikuu. Zaidi ya hayo, wakati aliondoka nyumbani kwenda kazini, kwanza alihitajika kuweka akiba ya gharama ya usafiri kidogo kidogo kwa kuuza mazao ya nafaka ambayo familia yetu ilikuza na kuchuma matunda madogo ya mmea wa ‘hawthorn’ ili kuyauza. Lakini wale pepo walitenda bila kuwa na busara, wakisingizia familia yangu na shutuma za uwongo, uvumi ambao bado unaenea hata leo. Hata hivi sasa, bado ninadharauliwa na kijiji changu kwa sababu ya sifa yangu kama mkosaji wa kisiasa na mdanganyifu stadi. Kundi hili la pepo ambalo linaua bila kujali, serikali hii katili ambayo haiheshimu maisha ya mwanadamu, hawa wadogo wa Shetani wanaoshutumu kwa uwongo na kuchochea maoni ya umma—ninawachukia wote! Ijapokuwa ibilisi anatutia hatarini kwa uwongo, anatukashifu na kututesa, hii iliniruhusu nione waziwazi asili mbovu inayompinga Mungu, potovu, inayokataa Mbingu ya serikali ya CPP na uso wake wa kweli mbaya. Iliniwezesha zaidi kujionea upendo wa Mungu na wokovu Wake. Kadiri ibilisi anavyotutesa, ndivyo anavyoimarisha azimio letu la kumfuata Mwenyezi Mungu hadi mwisho kabisa. Kama singepitia mateso ya kikatili mikononi mwa pepo hao, ni nani anayejua wakati roho yangu ingeamshwa au ni lini ningekuja kumdharau Shetani kwa kweli na kumwacha milele.

Nikikumbuka miaka yangu yote niliyoitumia kumfuata Mungu, nilikuwa nimepokea tu maneno ya Mungu ambayo yalifichua asili na hali katili ya serikali ya CCP kwa kiwango cha nadharia, lakini sikuwahi kuielewa kwa kweli. Kwa sababu, tangu umri mdogo, nilikuwa nimejifundisha mafundisho ya “elimu ya kizalendo,” ambayo ilinishurutisha na kunidanganya kwa utaratibu nifikirie kwa njia fulani, hata nilidhani kwamba maneno ya Mungu yalikuwa ya kutiwa chumvi—sikuweza kabisa kujilazimisha kuacha kuipenda mno nchi yetu, nikidhani kuwa Chama cha Kikomunisti kilikuwa sahihi kila wakati, kwamba jeshi lililinda nchi yetu, na kwamba polisi waliwaadhibu na kuwakomesha waovu kutoka kwa jamii na kulinda masilahi ya umma. Ni kwa kupitia mateso mikononi mwa pepo hao tu ndipo nilikuja kufahamu uso wa kweli wa serikali ya CCP; ni ya kudanganya na ya unafiki sana na imewahadaa watu wa China na ulimwengu mzima kwa uwongo wake kwa muda wa miaka mingi. Inatangaza tena na tena kutetea “uhuru wa imani na haki za kisheria za kidemokrasia,” lakini kwa uhalisi inaadhibu imani ya kidini bila kuzuilika. Kile inachotetea tu ni udhalimu wake mwenyewe, udhibiti wa kutumia nguvu na udikteta. Ingawa mwili wangu ulikuwa umejeruhiwa vibaya wakati wa mateso ya kikatili ya CCP, na nilikuwa nimeumia na mdhaifu maneno ya Mungu kila wakati yalinipa nuru na kunipa imani na nguvu, ili niweze kuona hila za shetani na kwa shahidi wa Mungu. Wakati huo huo, nilipata hisia kubwa ya upendo na wema wa Mungu na imani yangu kumfuata Mungu iliongezeka. Kama vile neno la Mwenyezi Mungu lisemavyo: “Sasa ndio wakati: Mwanadamu ana muda mrefu tangu akusanye nguvu zake zote, amejitolea nguvu zake zote, amelipa kila gharama, kwa hili, kuchana uso uliojificha wa pepo hili na kuwafanya watu, ambao wamepofushwa na kuvumilia kila aina ya mateso na taabu, kuinuka kutoka katika maumivu na kurudi kwa ibilisi huyu wa zamani(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kazi na Kuingia (8)). Sasa nimerudi kanisani na ninatimiza wajibu wangu kwa kuhubiri injili, Asante Mungu.

Iliyotangulia: 86. Siku Baada Ya Nyingine Katika Jela Ya Chama Cha Kikomunisti

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Maudhui Yanayohusiana

62. Kuinuka licha ya kushindwa

Na Fenqi, Korea ya KusiniKabla ya kumwamini Mungu, nilifundishwa na CCP, na sikufikiria chochote ila jinsi ya kufaulu kutokana na juhudi...

3. Jaribu la Foili

Na Xingdao, Korea ya Kusini“Ee Mungu! Kama nina hadhi au la, sasa ninajielewa mwenyewe. Hadhi yangu ikiwa juu ni kwa sababu ya kuinuliwa na...

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp