Kuhusu Biblia (4)
Watu wengi wanaamini kwamba kuelewa na kuwa na uwezo wa kufasiri Biblia ni sawa na kutafuta njia ya kweli—lakini, kimsingi, je, vitu ni rahisi sana? Hakuna anayejua uhalisia wa Biblia: kwamba si kitu chochote zaidi ya rekodi ya kihistoria ya kazi ya Mungu, na agano la hatua mbili zilizopita za kazi ya Mungu, na haikupatii ufahamu wa malengo ya kazi ya Mungu. Kila mtu ambaye amesoma Biblia anajua kwamba inarekodi hatua mbili za kazi ya Mungu wakati wa Enzi ya Sheria na Enzi ya Neema. Agano la Kale linaandika historia ya Israeli na kazi ya Yehova kuanzia wakati wa uumbaji hadi mwisho wa Enzi ya Sheria. Agano Jipya linarekodi kazi ya Yesu duniani, ambayo ipo katika Injili Nne, vilevile kazi ya Paulo; je, sio rekodi za kihistoria? Kuleta mambo ya zamani leo kunayafanya yawe historia, haijalishi yana ukweli kiasi gani, bado ni historia—na historia haiwezi kushughulikia masuala ya leo. Maana Mungu haangalii historia! Na hivyo, kama unaelewa tu Biblia, na huelewi chochote kuhusu kazi ambayo Mungu anakusudia kufanya leo, na kama unamwamini Mungu, na hutafuti kazi ya Roho Mtakatifu, basi hujui inamaanisha nini kumtafuta Mungu. Ikiwa unasoma Biblia kwa lengo la kujifunza historia ya Israeli, kutafiti historia ya uumbaji wa Mungu wa mbingu na dunia, basi humwamini Mungu. Lakini leo, kwa kuwa unamwamini Mungu, na kutafuta uzima, kwa kuwa unatafuta maarifa juu ya Mungu, na hutafuti nyaraka na mafundisho mfu, au ufahamu wa historia, unapaswa kutafuta mapenzi ya Mungu ya leo, na unapaswa kutafuta uongozi wa kazi ya Roho Mtakatifu. Kama ungekuwa mwanaakiolojia ungeweza kusoma Biblia—lakini wewe sio mwanaakiolojia, wewe ni mmoja wa wale wanaomwamini Mungu, na utakuwa bora zaidi ukitafuta mapenzi ya Mungu ya leo. Kwa kusoma Biblia, angalau utakuwa umeelewa sehemu ndogo ya historia ya Israeli, utajifunza kuhusu maisha ya Abrahamu, Daudi, na Musa, utajua kuhusu namna walivyomheshimu sana Yehova, namna ambavyo Yehova aliwachoma wale waliompinga, na jinsi alivyozungumza na watu wa enzi hiyo. Utaelewa tu kuhusu kazi ya Mungu katika wakati uliopita. Rekodi za Biblia zinahusiana na jinsi ambavyo watu wa awali wa Israeli walivyomheshimu sana Mungu na kuishi chini ya uongozi wa Yehova. Kwa sababu Waisraeli walikuwa ni wateuliwa wa Mungu, katika Agano la Kale unaweza kuona utii wote wa watu wa Israeli kwa Yehova, jinsi ambavyo wale wote waliomtii Yehova walivyokuwa wanaangaliwa na kubarikiwa Naye, unaweza kujifunza kwamba Mungu alipofanya kazi katika Israeli alikuwa mwingi wa rehema na mapenzi, vilevile alikuwa na moto uteketezao, na kwamba Waisraeli wote, kuanzia watu wa chini hadi wakubwa, walimheshimu sana Yehova, na hivyo nchi yote ilibarikiwa na Mungu. Hiyo ni historia ya Israeli iliyorekodiwa katika Agano la Kale.
Biblia ni rekodi ya kihistoria ya kazi ya Mungu katika Israeli, na inaandika utabiri mwingi wa manabii wa kale vilevile baadhi ya matamshi ya Yehova katika kazi Yake wakati huo. Hivyo, watu wote wanakitazama kitabu hiki kama kitakatifu (maana Mungu ni mtakatifu na mkuu). Kimsingi, hii yote ni matokeo ya uchaji wao kwa Yehova na vile walivyokuwa wanampenda Mungu. Watu wanarejelea kitabu hiki kwa namna hii kwa sababu tu viumbe wa Mungu wacha Mungu na wanampenda Muumba wao sana, na hata kuna wale ambao wanakiita kitabu hiki kitabu cha mbinguni. Kimsingi, ni rekodi tu za kibinadamu. Hakikupewa jina na Yehova Mwenyewe, wala Yehova Mwenyewe hakuongoza utengenezaji wake. Kwa maneno mengine, mwandishi wa kitabu hiki sio Mungu, bali ni wanadamu. Biblia Takatifu ni jina la heshima tu lililotolewa na mwanadamu. Jina hili halikuamuliwa na Yehova na Yesu baada ya Wao kujadiliana; si chochote zaidi ya mawazo ya kibinadamu. Maana kitabu hiki hakikuandikwa na Yehova, wala kuandikwa na Yesu. Badala yake, ni maelezo yaliyotolewa na manabii wengi wa kale, mitume na waonaji maono, ambayo baadaye yalipangiliwa na vizazi vilivyofuata na kuwa kitabu cha maandiko ya kale, ambayo kwa watu, yanaonekana kuwa matakatifu, kitabu ambacho wanaamini kimejumuisha siri nyingi ambazo hazieleweki na za kina ambazo zinasubiri kufunguliwa na vizazi vijavyo. Kwa namna hiyo, watu hata wanaamini kwamba kitabu hiki ni kitabu cha mbinguni. Ukijumlisha Injili Nne na Kitabu cha Ufunuo, mtazamo wa watu kuhusu kitabu hicho ni tofauti kabisa na vitabu vingine, na hivyo hakuna mtu anayethubutu kukichambua hiki “kitabu cha mbinguni” kwa sababu ni “kitakatifu” sana.
Kwa nini, mara tu baada ya watu kusoma Biblia wanakuwa na uwezo wa kupata njia sahihi ya kukiweka katika matendo? Kwa nini wanakuwa na uwezo wa kupata mengi ambayo yalikuwa hayafahamiki kwao? Leo, Ninaichambua Biblia kwa namna hii na haimaanishi kwamba Naichukia, au kukana thamani yake kwa ajili ya marejeleo. Ninakuelezea na kukufafanulia thamani ya asili na chanzo cha Biblia ili uweze kuondoka katika giza. Maana watu wana mitazamo mingi kuhusu Biblia, na mingi yao ina makosa; kusoma Biblia kwa namna hii sio tu kunawazuia kupata kile wanachopaswa kupata, lakini, muhimu zaidi, kunazuia kazi Niliyokusudia kufanya. Inaingilia kati kazi ya siku zijazo kwa kiasi kikubwa, na inatoa hasara tu, na wala sio faida. Hivyo, Ninachokufundisha ni hulka tu na kisa cha ndani cha Biblia. Sikwambii kwamba usisome Biblia, au uzunguke ukitangaza kwamba haina thamani kabisa, bali kwamba uweze kuwa na maarifa na mtazamo sahihi juu ya Biblia. Usiegemee upande mmoja sana! Ingawa Biblia ni kitabu cha historia kilichoandikwa na wanadamu, pia kinaandika kanuni nyingi ambazo kwazo watakatifu wa zamani na manabii walimhudumia Mungu, vilevile uzoefu wa hivi karibuni wa mitume katika kumhudumia Mungu—yote haya yalishuhudiwa na kujulikana kwa watu hawa, na inaweza kutumika kama rejeleo kwa ajili ya watu wa enzi hii katika kutafuta njia ya kweli. Hivyo, katika kusoma Biblia watu wanaweza pia kupata njia nyingi za maisha ambazo haziwezi kupatikana katika vitabu vingine. Njia hizi ni njia za maisha ya kazi ya Roho Mtakatifu ambazo manabii na mitume walizipitia katika enzi iliyopita, na maneno mengi ni ya thamani, na yanaweza kutoa kile ambacho watu wanataka. Hivyo, watu wote wanapenda kusoma Biblia. Kwa sababu kuna mambo mengi sana yaliyofichwa katika Biblia, mitazamo ya watu juu ya Biblia ni tofauti na mitazamo yao juu ya maandiko ya viongozi wa kiroho mashuhuri. Biblia ni rekodi na mkusanyiko wa uzoefu na maarifa ya watu ambao walimhudumia Yehova na Yesu katika enzi ya kale na mpya, na pia vizazi vya baadaye vimeweza kupata nuru, mwanga mkubwa na njia za kuweza kutembea kwazo. Sababu ya Biblia kuwa na hadhi ya juu kuliko maandiko ya kiongozi yeyote mkubwa wa kiroho ni kwa sababu maandiko yao yote yanatoka katika Biblia, uzoefu wao wote unatokana na Biblia, na wote wanaelezea Biblia. Na hivyo, ingawa watu wanaweza wakafaidika na vitabu kutoka kwa kiongozi yeyote wa kiroho mashuhuri, bado wanaiabudu Biblia, maana kwao, inaonekana ni ya juu sana na ya kina sana! Ingawa Biblia inaleta pamoja baadhi ya vitabu vya maneno ya uzima, kama vile nyaraka za Paulo na nyaraka za Petro, na ingawa watu wanaweza kusaidiwa na vitabu hivi, vitabu hivi bado vimepitwa na wakati, bado ni vitabu vya enzi ya kale, na haijalishi ni vizuri kiasi gani, vinafaa tu kwa ajili ya kipindi kimoja, na wala sio vya milele. Maana kazi ya Mungu siku zote inaendelea, na haiwezi kusimama tu katika kipindi cha Paulo na Petro, au siku zote ibaki katika Enzi ya Neema, enzi ambayo Yesu alisulubiwa. Na hivyo, vitabu hivi vinafaa tu katika Enzi ya Neema, na wala sio kwa ajili ya Enzi ya Ufalme wa siku za mwisho. Vinaweza tu kuwa na manufaa kwa waumini wa Enzi ya Neema, na sio kwa watakatifu wa Enzi ya Ufalme, na haijalishi ni vizuri kiasi gani, bado havifai kwa kipindi hiki. Ni sawa na kazi ya Yehova ya uumbaji au kazi Yake katika Israeli: Haijalishi kazi hii ilikuwa kubwa kiasi gani, bado imepitwa na wakati, na muda utaendelea kuja wakati umekwishapita. Kazi ya Mungu pia ni ile ile: Ni nzuri, lakini muda utafika ambapo itakoma; siku zote haitaendelea kubaki katikati ya kazi ya uumbaji, wala katikati ya kazi ile ya msalaba. Haijalishi kazi ya msalaba inashawishi kiasi gani, haijalishi ilikuwa ya ufanisi kiasi gani katika kumshinda Shetani, hata hivyo, kazi bado ni kazi, na enzi, hata hivyo bado ni enzi; kazi siku zote haiwezi kubaki katika msingi ule ule, wala nyakati haziwezi kukosa kubadilika, kwa sababu kulikuwa na uumbaji na lazima kuwepo na siku za mwisho. Hii haiepukiki! Hivyo, leo maneno ya uzima katika Agano Jipya—nyaraka za mitume, na Injili Nne—vimekuwa vitabu vya kihistoria, vimekuwa vitabu vya kale, na inawezekanaje vitabu vya kale kuwapeleka watu katika enzi mpya? Haijalishi ni kiasi gani vitabu hivi vinaweza kuwapatia watu uzima, haijalishi vina uwezo kiasi gani katika kuwaongoza watu kwenye msalaba, ndio kwamba havijapitwa na wakati? Havijaondokewa na thamani? Hivyo, Ninasema hupaswi kuviamini vitabu hivi bila kufikiri. Ni vya zamani sana, haviwezi kukupeleka katika kazi mpya, vinaweza kukulemea tu. Sio tu haviwezi kukuleta katika kazi mpya, na katika kuingia kupya, bali vinakupeleka katika makanisa ya dini ya kale na kama ni hivyo, havirudishi nyuma imani yako kwa Mungu?
Kile Biblia inaandika ni kazi ya Mungu huko Israeli, pamoja na baadhi ya kile kilichofanywa na watu wateule wa Israeli. Licha ya ukweli kwamba kulikuwa na uchaguzi kadhaa za sehemu zinazopaswa kujumuishwa au kuachwa, hata ingawa Roho Mtakatifu hakukubali, bado Hakuweka lawama yoyote. Biblia ni historia ya Israeli tu, ambayo pia ni historia ya kazi ya Mungu. Watu, masuala, na mambo inayoyarekodi yote yalikuwa ya kweli, na hakuna kitu kuhusu hayo kilikuwa na maana fiche—mbali na unabii wa Isaya, Danieli, na manabii wengine, au kitabu cha Yohana cha maono. Watu wa awali wa Israeli walikuwa wenye maarifa na watu wenye utamaduni wa hali ya juu, na maarifa yao ya kale na utamaduni ulikuwa wa kiwango cha juu, na hivyo kile walichoandika kilikuwa cha kiwango cha juu kuliko watu wa leo. Na hivyo, walikuwa na uwezo mkubwa wa kuandika vitabu hivi, kwa hiyo sio ajabu, maana Yehova alikuwa amefanya kazi kubwa sana miongoni mwao, na walikuwa wameona mengi sana. Daudi alitazama matendo ya Yehova kwa macho yake mwenyewe, yeye mwenyewe aliyashuhudia, na aliona ishara na maajabu mengi sana, na hivyo aliandika zaburi zote hizo kutukuza matendo ya Yehova. Waliweza kuandika vitabu hivi katika mazingira fulani, sio kwa sababu walikuwa watakatifu. Walimtukuza Yehova kwa sababu walikuwa wamemwona. Kama hamjawahi kuona kitu chochote kwa Yehova, na hamjui juu ya uwepo Wake, mnawezaje kumtukuza? Ikiwa hamjawahi kumwona Yehova, basi hamtajua jinsi ya kumtukuza, wala kumwabudu, wala kuweza kuandika nyimbo za kumsifu, na hata kama mtaombwa kuvumbua baadhi ya matendo ya Yehova hamtakuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Kwamba, leo, mnaweza kumtukuza Mungu na kumpenda Mungu pia ni kwa sababu mmemwona, na pia mmepitia kazi Yake—na ikiwa tabia yenu inaboreka, ninyi pia hamtakuwa na uwezo wa kuandika mashairi ya kumsifu Mungu kama Daudi?
Ili kuielewa Biblia, kuelewa historia, bali sio kuelewa kile ambacho Roho Mtakatifu anafanya leo—hayo ni makosa! Umefanya vizuri sana katika kujifunza historia, umefanya kazi nzuri sana, lakini huelewi chochote juu ya kazi Anayofanya Roho Mtakatifu leo. Je, huu si upumbavu? Watu wengine wanakuuliza: “Mungu anafanya nini leo? Ni kitu gani unapaswa kuingia kwacho leo? Maisha yako yanakwendaje? Je, unaelewa mapenzi ya Mungu?” Hutakuwa na majibu ya kile wanachouliza—sasa unajua nini kwani? Utasema: Ninajua tu kwamba ninapaswa kupuuzia mambo ya mwili na kujitambua. Halafu wakiuliza tena “Ni kitu gani kingine ambacho unakielewa?” Utasema unajua pia kutii mipangilio yote ya Mungu, na kujua kidogo kuhusu historia ya Biblia, basi. Hicho tu ndicho umepata kwa kumwamini Mungu miaka yote hii? Ikiwa hayo tu ndiyo unayoyaelewa, basi unapungukiwa mengi sana. Hivyo, kimo chenu sasa kimsingi hakiwezi kufanikisha yale ambayo Ninayataka kutoka kwenu, na ukweli mnaoufahamu ni mdogo sana, pamoja na uwezo wenu wa kutofautisha—ni sawa na kusema, imani yenu ni ya juujuu sana! Mnapaswa kuwa na kweli zaidi ya hapo, mnahitaji maarifa zaidi, mnapaswa kutazama zaidi, na baada ya hapo tu ndipo mtakuwa mnaweza kusambaza injili, maana hiki ndicho mnapaswa kukipata!