Utendaji (1)

Hapo awali, kulikuwa na mikengeuko mingi na hata mambo ya kipuuzi katika namna ambazo watu walipata uzoefu. Hawakuelewa kabisa viwango vya mahitaji ya Mungu, kwa hiyo kulikuwa na sehemu nyingi ambapo uzoefu wa watu ulienda kombo. Kile Mungu anachohitaji kutoka kwa mwanadamu ni kwa yeye kuweza kuishi kwa kudhihirisha ubinadamu wa kawaida. Kwa mfano, ni sawa kwa watu kufuata desturi za kawaida kuhusia na chakula na mavazi kuvaa suti na tai, kujifunza kiasi kuhusu sanaa ya kisasa, na wanaweza kufurahia sanaa, utamaduni na burudani katika muda wao wa ziada. Wanaweza kupiga picha kadhaa za kukumbukwa, wanaweza kusoma na kupata maarifa fulani yenye maana, na kuwa na mazingira mazuri kiasi ya kuishi. Haya ndiyo mambo yote ambayo yanastahili maisha ya ubinadamu wa kawaida, ilhali watu wanayaona kama mambo yanayochukiwa na Mungu na wao wanajizuia wasiyafanye. Utendaji wao unahusu kufuata kanuni chache tu, jambo ambalo husababisha maisha yasiyo machangamfu na yasiyo na maana yoyote hata kidogo. Kwa kweli, Mungu hajawahi kuhitaji watu watende mambo kwa namna hii. Watu wote wanataka kukatiza tabia zao wenyewe, wakiomba bila kukoma rohoni mwao ili wawe karibu na Mungu, mawazo yao yakifikiria daima kile Mungu anachokusudia, macho yao yakiangalia huku na kule mara kwa mara, wakihofu sana kwamba uhusiano wao kwa Mungu utaharibika kwa namna fulani. Haya yote ni maoni ambayo watu wameibua wao wenyewe; ni sheria ambazo zimewekwa na watu kwa ajili yao wenyewe. Ikiwa hujui kiini na asili yako mwenyewe na huelewi kile kiwango ambacho utendaji wako mwenyewe unaweza kufikia, basi hutakuwa na namna yoyote ya kuwa na hakika ni viwango vipi hasa ambavyo Mungu anahitaji kutoka kwa mwanadamu, na wala hutakuwa na njia mwafaka ya utendaji. Kwa kuwa huwezi kuelewa ni nini hasa ambacho Mungu anahitaji kutoka kwa mwanadamu, akili yako inavurugika daima, unatafakari ukichanganua nia za Mungu na kubabaika ukitafuta namna fulani ya kuguzwa na kupatiwa nuru na Roho Mtakatifu. Hivyo, unakuza njia fulani za kutenda ambazo unaamini kuwa zinafaa. Huna habari hata kidogo kuhusu kile hasa Mungu anachohitaji kutoka kwa mwanadamu; unatekeleza utendaji wako mwenyewe kwa wepesi wa moyo tu, bila kujali sana kuhusu matokeo sembuse kuhusu iwapo kunayo mikengeuko au makosa katika utendaji wako. Kwa njia hii, bila shaka utendaji wako unakosa usahihi na kukosa maadili. Kile kinachokosa hasa ni mantiki ya kawaida ya kibinadamu na dhamiri inayostahili, pamoja na pongezi ya Mungu na uthibitisho wa Roho Mtakatifu inakuwa rahisi sana kufuata njia yako tu. Aina hii ya kutenda ni kufuata sheria tu au kuchukua mzigo zaidi kimakusudi ili ujizuie na kujidhibiti. Ilhali unafikiri kuwa utendaji wako uko sahihi kabisa, bila kujua kwamba sehemu kubwa ya utendaji wako unahusu michakato au kanuni ambazo si za lazima. Kuna wengi ambao wanatenda hivi kwa miaka mingi hasabila mabadiliko katika tabia zao, bila ufahamu mpya, na bila kuingia kupya. Wanatenda tena makosa yale yale ya zamani bila kujua na kutekeleza asili zao za kinyama wapendavyo, hata hadi kiwango ambapo mara nyingi wanafanya matendo ya kinyama, yasiyo ya busara na kutenda kwa njia ambazo zinawaacha watu wakichanganyikiwa na kushangazwa kabisa. Je, watu kama hao wanaweza kusemwa kuwa wamepitia mabadiliko katika tabia?

Sasa, imani katika Mungu imeingia katika Enzi ya Neno la Mungu. Tukizungumza kwa kulinganisha, watu hawaombi kadiri walivyokuwa wakiomba awali; maneno ya Mungu yamewasilisha wazi vipengele vyote vya ukweli na njia za utendaji, kwa hivyo hakuna tena haja wa watu kujitahidi na kutafuta kwa kupapasa papasa. Katika maisha ya Enzi ya Ufalme, maneno ya Mungu yanawaongoza watu mbele, nayo ni maisha ambamo kila kitu kinaelezwa waziwazi kwao ili waone—kwa kuwa Mungu ameweka kila kitu wazi, na mwanadamu haachwi tena kutafuta njia katika maisha. Kuhusu ndoa, mambo ya kidunia, maisha, chakula, mavazi na malazi, mahusiano kati ya watu, jinsi mtu anavyoweza kuhudumu kwa njia ambayo inayakidhi mapenzi ya Mungu, jinsi mtu anavyopaswa kuunyima mwili, na kadhalika, Mungu hajawaelezea yepi kati ya mambo haya? Je, bado mnahitaji kwenda kuomba na kutafuta? Hakuna haja kweli! Kama bado unafanya mambo haya, unatenda tu kwa kupita kiasi. Huu ni ujinga na upumbavu, na hauhitajiki kabisa! Ni wale tu waliopungukiwa kabisa katika ubora wa tabia na wasioweza kuelewa maneno ya Mungu ndio wanaoomba maombi ya kipumbavu bila kukoma. Jambo la muhimu katika kuutekeleza ukweli ni kama una azimio au la. Baadhi ya watu wanasisitiza kufuata mambo ya kimwili wanayoyapendelea katika matendo yao hata kama wanapojua wazi kuwa hayapatani na ukweli. Hili basi linazuia kuendelea kwao wenyewe katika maisha, na hata baada ya kuomba na kutafuta bado wanataka kutenda kwa kuustahi mwili. Wanapofanya hivi, je, hawatendi dhambi kwa kujua? Kama wale wanaotamani anasa za mwili na kutamani pesa, na wale wamaomwomba Mungu baadaye, wakisema: “Mungu! Je, Utaniruhusu nitamani anasa za mwili na kutamani utajiri? Je, ni mapenzi Yako nipate fedha kwa njia hii?” Je, hii ni njia inayofaa ya kuomba? Watu wanaofanya hivi hujua vizuri kabisa kwamba Mungu hafurahii mambo haya, na kwamba wanapaswa kuyaacha, lakini mambo wanayoyashikilia mioyoni mwao yameshaamuliwa, na wanapoomba na kutafuta wanajaribu kumlazimisha Mungu awaruhusu kutenda kwa namna hii. Mioyoni mwao, hata wanaweza kumtaka Mungu aseme jambo ili kuthibitisha hili—huu ndio unaoitwa uasi. Pia kuna wale ambao huwaleta ndugu wa kanisa kwa upande wao na kuanzisha falme zao huru wenyewe. Unajua vizuri sana kwamba matendo haya yanampinga Mungu, lakini pindi tu unapoazimia kutenda jambo kama hili bado unaenda kumtafuta na kumwomba Mungu kwa utulivu na bila hofu. Huna aibu hata kidogo! Kuhusu kuyaacha nyuma mambo ya kidunia, jambo hili lilizungumziwa zamani. Kuna baadhi ya watu wanaojua wazi kuwa Mungu anachukia mambo ya kidunia, lakini bado wanaomba, wakisema: “Ee Mungu! Ninaelewa kuwa Hutanikubalia niendelee kutenda mambo ya kidunia, lakini ninafanya hili ili jina Lako lisiaibishwe; ninalifanya ili watu wa kidunia waweze kuona utukufu Wako ndani yangu.” Haya ni maombi ya aina gani? Mnaweza kujua? Ni aina ya maombi yanayokusudia kumlazimisha na kumshurutisha Mungu. Je, huoni aibu kuomba kwa namna hii? Watu wanaoomba kwa namna hii humpinga Mungu kwa makusudi, na maombi ya aina hii ni suala la utata kabisa; ni maonyesho ya tabia ya kishetani kweli. Maneno ya Mungu yako dhahiri kabisa, hasa yale yanayonenwa kuhusiana na mapenzi Yake, tabia Yake, na jinsi Yeye huwatendea watu wa aina tofauti. Ikiwa huuelewi ukweli, basi unapaswa kuyasoma maneno ya Mungu zaidi—matokeo ya kufanya hivi ni bora zaidi kuliko kuomba na kutafuta bila kutafakari. Kuna nyakati nyingi ambapo kutafuta na kuomba kunapaswa kubadilishwa na kusoma maneno ya Mungu zaidi na kushiriki kuhusu ukweli. Katika maombi yako ya kawaida, unapaswa kutafakari na kujaribu kujijua zaidi kutoka ndani ya maneno ya Mungu. Hili ni lenye manufaa zaidi kwa ajili ya maendeleo yako katika maisha. Ikiwa, sasa, bado unatafuta kwa kuinua macho yako mbinguni, je, hiyo haionyeshi kuwa bado unamwamini Mungu asiye dhahiri? Awali, uliona matokeo kutokana na kutafuta na kuomba kwako na Roho Mtakatifu aligusa roho yako kwa kiasi fulani kwa sababu huo ulikuwa wakati wa Enzi ya Neema. Hukuweza kumwona Mungu, kwa hivyo hukuwa na chaguo ila kuitafuta njia yako kuelekea mbele na kutafuta kwa namna hiyo. Sasa Mungu amekuja kati ya wanadamu, Neno limeonekana katika mwili, na umemwona Mungu; kwa hiyo Roho Mtakatifu hafanyi kazi tena kama Alivyofanya mbeleni. Enzi imebadilika na pia namna ambavyo Roho Mtakatifu hufanya kazi imebadilika. Ingawa huenda watu hawaombi sana kama walivyofanya awali, kwa sababu Mungu yuko duniani, mwanadamu sasa anayo nafasi ya kumpenda Mungu. Wanadamu wameingia katika enzi ya kumpenda Mungu na wanaweza kwa kawaida kumkaribia Mungu vizuri zaidi ndani yao wenyewe: “Ee Mungu! Hakika Wewe ni mzuri sana, nami natamani kukupenda!” Maneno machache tu ya wazi na rahisi hudhihirisha upendo kwa Mungu ndani ya mioyo ya watu; ombi hili linasemwa tu kwa ajili ya kuimarisha upendo kati ya mwanadamu na Mungu. Wakati mwingine unaweza kujiona ukionyesha uasi kiasi, na kusema: “Ee Mungu! Mbona mimi ni mpotovu sana?” Unatamani sana kujipiga mara kadhaa, na machozi yanakulengalenga. Katika nyakati kama hizi, unahisi kujuta na kuwa na dhiki moyoni mwako, lakini huna namna ya kuonyesha hisia hizi. Hii ndiyo kazi ya sasa ya Roho Mtakatifu, lakini ni wale tu wanaofuatilia maisha ndio wanaoweza kuifikia. Unahisi kwamba Mungu anakupenda sana nawe unao hisia maalum. Ingawa huna maneno ya kuomba kwa uwazi, daima unahisi kwamba upendo wa Mungu ni wa kina kama bahari. Hakuna maneno sahihi ya kuonyesha hali hii, na hali hii ndiyo hutokea mara nyingi rohoni. Maombi na ushirika wa aina hii, yanayolenga kumvuta mtu karibu na Mungu moyoni mwake, ni ya kawaida.

Ingawa wakati ambao watu walibabaika na kutafuta sasa umepita, hilo halimaanishi kwamba hawastahili kuomba kutafuta tena, wala si kwamba watu hawahitaji kuyasubiri mapenzi ya Mungu yajifichue kabla ya kuendelea na kazi; huku ni kuelewa mambo tu kwa mwanadamu. Mungu amekuja miongoni mwa wanadamu ili Aishi nao, awe mwanga wao, maisha yao na njia yao: Huu ni ukweli. Bila shaka, katika kuja kwa Mungu duniani, kwa kweli Yeye huwaletea wanadamu njia na maisha ya vitendo ambayo yanafaa kimo chao kwa ajili yao kufurahia—Hajaja kuharibu njia zote za matendo ya mwanadamu. Mwanadamu haishi tena kwa kupapasapapasa na kutafuta kwa sababu mambo haya yamebadilishwa na Mungu kuja duniani ili kufanya kazi na kunena neno Lake. Amekuja kumweka mwanadamu huru kutoka kwa maisha ya giza na mashaka ambayo amekuwa akiishi na kumwezesha awe na maisha yaliyojawa mwanga. Kazi ya sasa ni ya kuonyesha mambo kwa uwazi, kusema kwa uwazi, kufahamisha moja kwa moja, na kufafanua mambo haya waziwazi, ili watu waweze kuyaweka mambo haya katika matendo, jinsi Yehova Mungu alivyowaongoza watu wa Israeli, Akiwaambia jinsi ya kutoa sadaka na jinsi ya kulijenga hekalu. Kwa hiyo, hakuna haja tena ya ninyi kuishi maisha ya kutafuta kwa dhati kama mlivyofanya baada ya Bwana Yesu kuondoka. Je, mnapaswa kuihisi njia yenu kupitia kazi ya kueneza injili katika siku za baadaye? Je, mnapaswa kupapasapapasa mkijaribu kutafuta njia mwafaka ya kuishi? Je, mnapaswa kupapasa papasa ili mtambue jinsi mnavyofaa kutekeleza wajibu wenu wenyewe? Je, ni lazima ninyi msujudu ardhini na kutafuta, ili mjue jinsi mnavyopaswa kushuhudia? Je, ni lazima ninyi mfunge na kuomba ili mjue jinsi mnavyopaswa kuvaa au kuishi? Je, ni lazima ninyi muombe kwa Mungu aliye mbinguni bila kukoma ili mjue jinsi mnavyopaswa kukubali kushindwa na Mungu? Je, ni lazima muombe bila kukoma, usiku na mchana, ili mjue jinsi mnavyopaswa kumtii Mungu? Kuna wengi miongoni mwenu wanaosema kwamba hamwezi kutenda kwa sababu hamwelewi. Watu hawaizingatii kazi ya Mungu siku hizi hata kidogo! Nilisema maneno mengi muda mrefu uliopita, lakini hamkuwahi kuzingatia kuyasoma hata kidogo, hivyo si ajabu kwamba hamjui jinsi ya kutenda. Bila shaka, katika enzi ya leo Roho Mtakatifu bado Huwagusa watu ili kuwasababisha wahisi starehe, Naye anaishi pamoja na mwanadamu. Hiki ndicho chanzo cha hisia hizo[a] maalum zenye kuanisi ambazo mara nyingi hutokea katika maisha yako. Kila baada ya muda fulani, siku huja ambapo unahisi kwamba Mungu ni wa kupendeza sana nawe huwezi kujizuia kumwomba: “Ee Mungu! Upendo Wako ni mzuri sana na sura Yako ni nzuri sana. Natamani kukupenda kwa undani zaidi. Natamani kujitoa kabisa ili kuyatumia maisha yangu yote. Nitatoa kila kitu Kwako, mradi ni kwa ajili Yako, mradi kwa kufanya hivi ninaweza kukupenda….” Hii ni hisia ya furaha uliyopewa na Roho Mtakatifu. Si nuru, wala si mwangaza; ni uzoefu wa kuguswa. Uzoefu unaofanana na huu utatokea mara kwa mara: Wakati mwingine unapoelekea kazini, utaomba na kumkaribia Mungu, nawe utasisimuliwa hadi kiwango ambapo machozi yataulowesha uso wako na hutaweza kujidhibiti, nawe utakuwa na hamu ya kupata mahali pa kufaa ambapo unaweza kuonyesha hamasa zote zilizo moyoni mwako…. Kutakuwa na nyakati utakapokuwa hadharani na utahisi kwamba unaufurahia upendo mwingi mno wa Mungu, kwamba bahati yako si ya kawaida, na hata zaidi kwamba unaishi maisha yako na kusudi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote. Utajua kwa undani zaidi kwamba Mungu amekuinua, na kwamba huu ni upendo mkuu wa Mungu kwako. Katika maficho ya ndani kabisa ya moyo wako utahisi kuwa kuna upendo fulani ndani ya Mungu usioweza kuonyeshwa na usioweza kueleweka kwa mwanadamu, kana kwamba unaujua lakini huna namna ya kuueleza, ukikufanya ufikirie kwa makini siku zote lakini ukikuacha usiweze kuuonyesha kabisa. Wakati kama huu, hata utasahau ulipo, nawe utaita: “Ee Mungu! Wewe huwezi kueleweka nawe Unapendwa sana!” Hili litawaacha watu kwa mshangao, lakini hayo yote hutendeka mara kwa mara. Nyinyi mmepitia mambo kama haya mara nyingi sana. Haya ndiyo maisha ambayo Roho Mtakatifu amekupa leo na maisha ambayo unapaswa kuishi sasa. Jambo hili halinui kukufanya uache kuishi maisha, bali kubadilisha jinsi unavyoishi maisha yako. Ni hisia ambayo haiwezi kuelezeka au kuonyeshwa. Pia ndiyo hisia ya kweli ya mwanadamu na hata zaidi ndiyo kazi ya Roho Mtakatifu. Unaweza kuielewa katika moyo wako, lakini huna namna ya kuionyesha wazi kwa mtu yeyote hata kidogo. Hii si kwa sababu wewe si mwepesi wa kusema au kwamba wewe ni kigugumizi, lakini kwa sababu ni aina ya hisia ambayo haiwezi kuelezwa katika maneno. Unaruhusiwa kufurahia mambo haya leo, na haya ndiyo maisha unayopaswa kuishi. Bila shaka, vipengele vingine vya maisha yako haviko tupu; ni kwamba tu uzoefu huu wa kusisimuliwa unakuwa aina ya furaha katika maisha yako ambao unakufanya utake kufurahia uzoefu kama huo kutoka kwa Roho Mtakatifu siku zote. Lakini unapaswa kujua kwamba kuguswa kwa namna hii hakufanyiki ili uweze kuuzidi mwili na kwenda katika mbingu ya tatu au kusafiri kote duniani. Badala yake, ni ili uweze kuhisi na kuonja upendo wa Mungu ambao unafurahia leo, upate uzoefu wa umuhimu wa kazi ya Mungu leo na ufahamiane tena na utunzaji na ulinzi wa Mungu. Mambo haya yote ni ili upate kuwa na maarifa zaidi ya kazi ambayo Mungu hufanya leo—hili ndilo lengo katika kufanya kazi hii.

Kutafuta na kupapasa papasa ilikuwa ndiyo namna ya maisha kabla ya Mungu kupata mwili. Wakati huo watu hawakuweza kumwona Mungu na hivyo hawakuwa na chaguo ila kutafuta na kupapasa papasa. Leo umemwona Mungu naye Anakwambia moja kwa moja jinsi unavyopaswa kutenda; hii ndiyo sababu huhitaji tena kupapasa papasa au kutafuta. Njia ambayo Anamwongoza mwanadamu ni njia ya ukweli, na mambo Anayomwelezea mwanadamu na ambayo mwanadamu anapokea ni maisha na ukweli. Unayo njia, uzima na ukweli, hivyo kuna haja gani ya kutafuta kila mahali? Roho Mtakatifu hatatenda hatua mbili za kazi kwa pamoja. Ikiwa, wakati Nimemaliza kunena neno Langu, watu hawali na kunywa neno la Mungu kwa uangalifu na kuufuatilia ukweli ifaavyo, bado wakitenda jinsi walivyotenda katika Enzi ya Neema, wakipapasapapasa kana kwamba wao ni vipofu, wakiomba na kutafuta siku zote, hiyo haitamaanisha kwamba hatua hii ya kazi Yangu—kazi ya maneno—inafanywa bure? Ingawa Naweza kuwa Nimemaliza kunena neno Langu, watu bado hawaelewi kabisa, na hii ni kwa sababu wamekosa ubora wa tabia. Tatizo hili linaweza kutatuliwa kwa kuishi maisha ya kanisa na kupitia kushiriki sisi kwa sisi. Awali, katika Enzi ya Neema, ingawa Mungu alikuwa mwili, hakufanya kazi ya maneno, ambayo ndiyo sababu Roho Mtakatifu alifanya kazi kwa njia hiyo wakati huo ili kuidumisha kazi. Wakati huo ilikuwa hasa Roho Mtakatifu aliyeifanya kazi, lakini sasa ni Mungu mwenye mwili Mwenyewe ambaye Anaifanya, baada ya kuchukua nafasi ya kazi ya Roho Mtakatifu. Awali, mradi watu waliomba mara kwa mara, walipata amani na furaha; kulikuwa na lawama pamoja na nidhamu. Hii yote ilikuwa kazi ya Roho Mtakatifu. Sasa hali hizi ni chache na nadra. Roho Mtakatifu anaweza tu kufanya aina moja ya kazi katika enzi yoyote ile. Kama Angefanya aina mbili za kazi wakati huo huo, mwili ukifanya aina moja na Roho Mtakatifu akifanya aina nyingine ndani ya watu, na kama kile mwili ulisema hakikuwa na thamani na kile Roho alifanya ndicho kilikuwa na thamani tu, basi Kristo asingekuwa na ukweli wowote, njia au uzima wowote hata kidogo. Huku kungekuwa kujipinga na kungekuwa makosa katika chanzo chake kabisa. Roho Mtakatifu anaweza kutenda kwa njia hii? Mungu ni mwenyezi na mwenye hekima yote, mtakatifu na mwenye haki, na Hatendi makosa yoyote kamwe.

Kulikuwa na mikengeuko na makosa mengi mno katika uzoefu wa zamani wa watu. Kulikuwa na mambo fulani ambayo watu wa ubinadamu wa kawaida walikuwa wamenuiwa kuwa nayo au kufanya, au kulikuwa na makosa ambayo yalikuwa magumu kuepuka katika maisha ya binadamu, na wakati mambo hayo yalishughulikiwa vibaya, watu walimlaumu Mungu. Kulikuwa na dada ambaye alikuwa na wageni nyumbani kwake. Maandazi yake ya kuchemshwa hayakuchemshwa vyema, hivyo akafikiri: “Labda hii ni nidhamu ya Mungu. Mungu anaushughulika moyo wangu usiofaa tena; kiburi changu kweli ni kibubwa mno.” Kwa kweli, tukizingatia jinsi mwanadamu hufikiria kwa kawaida, wageni wanapokuja, unasisimka na kukimbia huku na kule, bila kuwa na utaratibu katika kila kitu unachofanya, na kwa hiyo bila shaka wali utaungua au vyakula vitaishia kuwa na chumvi nyingi sana. Hii hutokea kwa sababu ya kusisimka sana, lakini watu huishia kudhania kuwa ni “nidhamu ya Mungu.” Kwa kweli, haya yote ni makosa tu yanayotendwa katika maisha ya binadamu. Je, hungekumbana pia na aina hii ya jambo mara kwa mara iwapo hungemwamini Mungu? Shida ambazo hutokea mara nyingi hutokana na makosa yaliyotendwa na watu—haiwezekani kabisa kwamba makosa kama haya yametendwa na Roho Mtakatifu. Makosa kama haya hayamhusu Mungu. Kwa mfano unapojiuma ulimi unapokula—hiyo inaweza kuwa ni nidhamu ya Mungu? Nidhamu ya Mungu ina kanuni na kwa kawaida huonekana wakati unatenda kosa kwa kujua. Ni wakati tu unatenda mambo yanayohusu jina la Mungu ama yanayohusu ushuhuda au kazi Yake ndipo Atakufundisha nidhamu. Watu wana ufahamu wa ndani wa mambo wanayoyafanya kwa sababu wanaelewa ukweli vya kutosha sasa. Kwa mfano: Je, unaweza kutohisi chochote ukibadhiri fedha za kanisa au kuzitumia bila kujali? Utahisi jambo unapofanya hivyo. Haiwezekani tu kuhisi jambo fulani kitendo kitakapokuwa kishafanywa. Unaelewa moyoni mwako kuhusu mambo unayoyatenda yanayoenda kinyume na dhamiri yako. Kwa kuwa watu wanayo mambo yao wenyewe wanayoyapenda au kuyapendelea, wao hujifurahisha tu ingawa wanajua wazi jinsi ya kuuweka ukweli katika vitendo. Hivyo, baada ya wao kutenda jambo, hawahisi shutuma yoyote au kupitia nidhamu yoyote dhahiri. Hii ni kwa sababu wametenda kosa kwa makusudi, kwa hiyo Mungu hawafundishi nidhamu; mara tu wakati wa hukumu ya haki ufikapo, adhabu ya Mungu italetwa juu ya kila mmoja kulingana na matendo yake. Kwa sasa kunao baadhi ya watu kanisani ambao hubadhiri fedha, baadhi wasioweka mipaka dhahiri kati ya wanaume na wanawake, na baadhi wanaohukumu, kupinga na kujaribu kuiharibu kazi ya Mungu kwa siri. Kwa nini bado kila kitu kiko sawa nao? Wanapotenda mambo kama hayo, wanao ufahamu na wanahisi aibu mioyoni mwao na kwa sababu ya hii, wakati mwingine wanaadibiwa na kutakaswa, lakini wao hawana aibu hata kidogo! Jinsi tu watu wanaposhiriki katika uzinzi—wanajua wanachokifanya wakati huo, lakini tamaa yao ni kubwa mno na hawawezi kujidhibiti. Hata Roho Mtakatifu akiwafundisha nidhamu, itakuwa bure, kwa hiyo Roho Mtakatifu hatafundisha nidhamu. Roho Mtakatifu asipowafundisha nidhamu wakati huo, wasipohisi shutuma yoyote na hakuna chochote kinachotendekea miili yako, kutakuwa na shutuma gani baadaye? Kitendo kimefanyika—kutakuwa na nidhamu gani? Inathibitisha tu kwamba hawana aibu kabisa nao wamepungukiwa na ubinadamu, na kwamba wanastahili laana na adhabu! Roho Mtakatifu hafanyi kazi bila sababu. Ikiwa unaujua ukweli vizuri sana lakini huutii katika vitendo, ikiwa unaweza kutenda uovu wowote, basi unachoweza kusubiri tu ni kuwasili kwa siku ile ambapo utaadhibiwa pamoja na yule mwovu. Huu ndio mwisho bora kwako! Sasa Nimehubiri nikirudia kuhusu dhamiri, ambacho ni kigezo cha chini kabisa. Watu wakikosa dhamiri, basi wamepoteza nidhamu ya Roho Mtakatifu; wanaweza kufanya chochote wanachotaka na Mungu hawazingatii. Wale ambao kwa kweli wana dhamiri na mantiki wataifahamu wanapotenda jambo baya. Watahisi wasiwasi mara tu wanapohisi shutuma kidogo katika dhamiri yao; watapitia pigano la ndani na mwishowe kuutelekeza mwili. Hawatafika kiwango ambapo wanatenda jambo linalompinga Mungu pakubwa. Haijalishi ikiwa Roho Mtakatifu anafundisha nidhamu na kuwaadibu, watu wote watakuwa na hisia fulani wanapotenda jambo baya. Kwa hiyo, watu sasa wanaelewa aina zote za ukweli na kama hawautendi basi hilo ni suala la kibinadamu. Siwajibu watu kama hawa hata kidogo, wala siwaonei tumaini lolote. Unaweza kufanya utakavyo!

Watu wengine wanapokuja pamoja, wanaliweka neno la Mungu upande mmoja na daima wanazungumza kuhusu jinsi mtu huyu au mtu yule alivyo. Bila shaka ni vizuri kuwa na utambuzi kidogo, ili bila kujali unapokwenda hutadanganywa kwa urahisi, wala hautalaghaiwa au kupumbazwa kwa urahisi—hiki pia ni kipengele ambacho watu wanapaswa kumiliki. Lakini usilenge tu suala hili. Hii inahusiana na upande mbaya wa mambo, na huwezi kuwakazia watu wengine macho daima. Unao ufahamu kidogo sana sasa kuhusu jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi, imani yako katika Mungu ni ya juujuu sana, nawe unayo mambo machache mno yaliyo mazuri. Yule unayemwamini ni Mungu, na Yule unayehitaji kumwelewa ni Mungu, si Shetani. Ikiwa unatambua tu jinsi Shetani anavyofanya kazi na njia zote ambazo kwazo roho mbaya zinafanya kazi, lakini huna ufahamu wa Mungu hata kidogo, hiyo itakuwa na maana gani? Je, si ni Mungu unayemwamini leo? Kwa nini ufahamu wako hauhusishi mambo haya mazuri? Hutilii maanani kipengele kizuri cha kuingia hata kidogo, wala hukifahamu, hivyo ni nini hasa unachotaka kupata katika imani yako? Je, hujui jinsi unavyopaswa kufuatilia? Unajua mengi kuhusu vipengele vilivyo hasi, lakini unaambulia patupu kuhusu kipengele kizuri cha kuingia, kwa hiyo kimo chako kitawezaje kuwahi kukua? Mtu kama wewe anayezungumza tu kuhusu vita na Shetani atakuwa na matarajio yapi ya baadaye ya maendeleo? Kuingia kwako hakutakuwa kumepitwa na wakati sana? Utaweza kupata nini kutokana na kazi ya sasa kwa kufanya hili? Kilicho muhimu sasa ni wewe uelewe nini Mungu anataka kufanya sasa, jinsi binadamu wanavyopaswa kushirikiana, jinsi wanavyopaswa kumpenda Mungu, jinsi wanavyopaswa kuielewa kazi ya Roho Mtakatifu, jinsi wanavyopaswa kuingia katika maneno yote ambayo Mungu anasema leo, jinsi wanavyopaswa kuyala na kuyanywa, kuyapitia, na kuyaelewa, jinsi yanavyopaswa kuyakidhi mapenzi ya Mungu, washindwe kabisa na Mungu na kumtii Mungu…. Haya ndiyo mambo unayopaswa kuyalenga na yanayopaswa kuingiwa sasa. Je, unaelewa? Kuna faida gani kulenga tu utambuzi wa watu wengine? Unaweza kumtambua Shetani hapa, kuzitambua roho mbaya huko—unaweza kuwa na ufahamu kamili wa roho mbaya, lakini kama huwezi kusema chochote kuhusu kazi ya Mungu, je, utambuzi kama huo unaweza kuchukua nafasi ya kumfahamu Mungu? Hapo awali Nimeshiriki kuhusu maonyesho ya kazi ya roho mbaya, lakini hili halijakuwa sehemu kubwa ya ushirika huo. Bila shaka watu wanapaswa kuwa na ufahamu kiasi na hiki ni kipengele ambacho wale wanaomtumikia Mungu wanapaswa kumiliki ili kuepuka kufanya mambo ya kipuuzi na kuikatiza kazi ya Mungu. Hata hivyo, jambo muhimu zaidi linabaki kuwa na maarifa ya kazi ya Mungu na kuelewa mapenzi ya Mungu. Ni ufahamu gani kuhusu hatua hii ya kazi ya Mungu iko ndani yako? Je, unaweza kuzungumza kuhusu kile ambacho Mungu hufanya, mapenzi ya Mungu ni yepi, mapungufu yako ni yapi na mambo unayopaswa kujiandaa nayo? Je, unaweza kusema kuingia kwako kupya zaidi ni kupi? Unapaswa kuweza kuvuna matunda na kutimiza ufahamu katika kuingia huko kupya. Usijifanye kuwa na kiwewe; lazima ufanye juhudi zaidi katika kuingia huko kupya ili uimarishe uzoefu na ufahamu wako mwenyewe, na hata zaidi lazima upate ufahamu wa kuingia kupya zaidi kwa sasa na njia sahihi zaidi ya kupata uzoefu. Aidha, kupitia kazi na kuingia kupya, lazima uwe na utambuzi kuhusu mazoea yako ya zamani yaliyopitwa na wakati na yaliyopotoka, na utafute jinsi ya kuyatupilia mbali ili uingie katika uzoefu mpya. Haya ni mambo ambayo sasa unahitaji kuyaelewa na kuingia ndani yake kwa haraka. Lazima uelewe tofauti na uhusiano kati ya kuingia kwa zamani na kuingia kupya. Kama huna ufahamu wa mambo haya, basi hutakuwa na njia yoyote ya kuendelea, kwa kuwa hutaweza kuendelea sambamba na kazi ya Roho Mtakatifu. Lazima uweze kula na kunywa kwa kawaida maneno ya Mungu na kufanya ushirika wa kawaida, na kuyatumia kubadilisha njia zako za zamani za kutenda na fikira zako za desturi za jadi, ili uweze kuingia katika utendaji upya, na kuingia katika kazi mpya ya Mungu. Haya ni mambo unayopaswa kutimiza. Sikusihi tu sasa uelewe hasa kama una sifa zinazostahili; hili silo lengo. Badala yake Ninakusihi kuchukulia kwa makini kutenda kwako ukweli na kuelewa kwako kuhusu kuingia katika maisha. Uwezo wako wa kujijua si mfano wa kimo chako cha kweli. Ikiwa unaweza kupitia kazi ya Mungu, upitie na kuelewa ukweli ndani ya maneno ya Mungu, na uweze kutambua fikira na makosa yako ya awali, basi hiki ni kimo chako cha kweli nacho ni kitu ambacho kila mmoja wenu anapaswa kutimiza.

Kuna hali nyingi ambamo ninyi hamjui hasa jinsi ya kutenda, sembuse kujua jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi. Wakati mwingine unatenda jambo ambalo ni dhahiri kwamba halimtii Roho Mtakatifu. Kupitia wewe kula na kunywa maneno ya Mungu, tayari unao ufahamu wa kanuni iliyo karibu katika suala hilo, kwa hiyo unayo hisia ya ndani ya lawama na kufadhaika; bila shaka hii ni hisia ambayo mtu atahisi tu kwa kigezo cha kujua ukweli fulani. Watu wasiposhirikiana au kutenda kulingana na neno la Mungu la leo, basi wanaipinga kazi ya Roho Mtakatifu na hakika watahisi kufadhaika ndani yao. Huenda unaelewa kanuni ya kipengele fulani lakini hutendi ipasavyo, kwa hiyo utapata hisia ya lawama ndani yako. Ikiwa huelewi kanuni hiyo na hujui kipengele hiki cha ukweli hata kidogo, basi haimaanishi kuwa lazima utahisi lawama kuhusu suala hili. Lawama ya Roho Mtakatifu huwa katika maudhui yanayofaa daima. Unafikiri kwamba kwa kuwa hujaomba na hujashirikiana na kazi ya Roho Mtakatifu kwamba umeichelewesha kazi. Kwa hakika, haiwezi kucheleweshwa. Roho Mtakatifu atamgusa mtu mwingine; kazi ya Roho Mtakatifu haizuiliwi na yeyote. Unahisi kwamba umemtahayarisha Mungu, na hii ndiyo hisia unayopaswa kuwa nayo katika dhamiri yako. Kama unaweza kuupata ukweli au la ni shauri yako mwenyewe na haihusiani na Mungu. Wakati mwingine ni dhamiri yako mwenyewe inayohisi kushutumiwa, lakini hii si nuru au mwangaza wa Roho Mtakatifu, wala si lawama ya Roho Mtakatifu. Badala yake ni hisia iliyo ndani ya dhamiri ya mwanadamu. Ukitenda kwa utukutu katika mambo yanayohusu jina la Mungu, ushuhuda wa Mungu au kazi ya Mungu, basi Mungu hatakuachilia. Lakini kuna mpaka—Mungu hatajishughulisha nawe katika mambo madogo ya kawaida. Atakupuuza. Ukikiuka kanuni, na uivuruge kazi ya Mungu, utakabiliwa na ghadhabu Yake na hatakuachilia kabisa. Baadhi ya makosa unayoyatenda hayawezi kuepukika katika maisha ya binadamu. Kwa mfano, huchemshi maandazi kwa njia ifaayo na kusema kuwa ni Mungu anakufundisha nidhamu—hili ni jambo lisilo na mantiki kabisa kusema. Kabla ya kuja kumwamini Mungu, jambo la aina hii halikutokea mara nyingi? Unahisi kwamba inaonekana kuwa nidhamu ya Roho Mtakatifu, lakini kwa kweli hivi sivyo ilivyo (bila kuzingatia baadhi ya hali za kipekee), kwa sababu kazi hii haitoki kwa Roho Mtakatifu kabisa, lakini badala yake inatokana na hisia za binadamu. Hata hivyo, ni kawaida kwa watu walio na imani kufikiria kwa namna hii. Hungeweza kufikiria hivi wakati ambapo hukumwamini Mungu. Mara ulipokuja kumwamini Mungu, ulianza kutumia muda mwingi ukitafakari mambo haya na kwa hiyo kwa kawaida ulifikiri kwa namna hii. Hili linatokana na mawazo ya kawaida ya watu na linahusiana na akili zao. Lakini hebu Nikwambie, kufikiri kwa aina hii hakuko katika eneo la kazi ya Roho Mtakatifu. Huu ni mfano wa Roho Mtakatifu kuwapa watu mjibizo wa kawaida kupitia mawazo yao; lakini lazima uelewe kwamba mjibizo huu si kazi ya Roho Mtakatifu. Kuwa na aina hii ya “maarifa” hakuthibitishi kwamba unayo kazi ya Roho Mtakatifu. Maarifa yako hayatokani na nuru ya Roho Mtakatifu, sembuse kazi ya Roho Mtakatifu. Ni matokeo ya wazo la kawaida kibinadamu tu na hayahusiani kamwe na nuru au mwanga wa Roho Mtakatifu—bila shaka haya ni mambo mawili tofauti kabisa. Wazo la kawaida kama hili la kibinadamu halitoki kwa Roho Mtakatifu kikamilifu. Roho Mtakatifu anapofanya kazi ili kuwapa watu nuru, kwa ujumla Yeye huwapa ufahamu wa kazi ya Mungu, na ufahamu wa kuingia kwao kwa kweli na hali yao ya kweli. Yeye pia huwasababisha waelewe nia za dharura za Mungu na madai Yake kwa mwanadamu leo, ili wawe na azimio la kudhabihu kila kitu ili wamridhishe Mungu, wampende Mungu hata wakikumbana na mateso na dhiki, na kuwa shahidi kwa Mungu hata ikimaanisha kumwaga damu yao au kutoa maisha yao, na kufanya hivyo bila majuto. Ukiwa na azimio la aina hii, inamaanisha unayo misisimko na kazi ya Roho Mtakatifu—lakini jua kwamba huna misismko ya aina hii kila wakati. Wakati mwingine katika mikutano unapoomba na kula na kunywa maneno ya Mungu, unaweza kuhisi kuguswa na kupata msukumo mno. Linaonekana jambo la kuburudisha kabisa wakati watu wengine wanashiriki baadhi ya uzoefu na ufahamu wao wa maneno ya Mungu, na moyo wako uko wazi na mchangamfu kabisa. Hii yote ni kazi ya Roho Mtakatifu. Kama wewe ni kiongozi na Roho Mtakatifu anakupa nuru na mwangaza usio wa kawaida unapoenda kanisani kufanya kazi, Anakupa umaizi wa shida ambazo zipo katika kanisa, Anakuwezesha kujua jinsi ya kushiriki kuhusu ukweli ili kuzitatua, Anakufanya uwe mwenye bidii ya ajabu sana, mwenye kuwajibika na uliye makini katika kazi yako, hii yote ni kazi ya Roho Mtakatifu.

Tanbihi:

a. Maandiko ya asili yanasoma “Hizi ni baadhi”

Iliyotangulia: Kuhusu Biblia (4)

Inayofuata: Utendaji (2)

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp