Mungu Ana Mamlaka Juu ya Hatima ya Wanadamu Wote
Kama washiriki wa jamii ya wanadamu na Wakristo waaminifu, ni jukumu na wajibu wetu sote kutoa akili na miili yetu kwa ajili ya kutimiza agizo la Mungu, kwa maana asili yetu yote inatoka kwa Mungu, na tunaishi kwa sababu ya ukuu wa Mungu. Kama akili na miili yetu haipo kwa ajili ya agizo la Mungu na kwa ajili ya kusudi la haki ya wanadamu, basi roho zetu hazitastahili mbele ya wale waliokufa kishahidi kwa ajili ya agizo la Mungu, na zaidi sana hazistahili kwa Mungu, aliyetupa kila kitu.
Mungu aliumba ulimwengu huu, Alimuumba mwanadamu huyu na, zaidi ya hayo, Alikuwa muasisi wa utamaduni wa kale wa Kigiriki na ustaarabu wa binadamu. Ni Mungu pekee Anayewafariji wanadamu hawa, na ni Mungu pekee Anayewajali wanadamu hawa usiku na mchana. Ukuaji na maendeleo ya binadamu hayatenganishwi na ukuu wa Mungu, na historia na mustakabali wa mwanadamu hauwezi kuepuka mipango inayofanywa na mikono ya Mungu. Kama wewe ni Mkristo wa kweli, basi kwa hakika utaamini kwamba kupanda na kushuka kwa nchi ama taifa lolote kunafanyika chini ya mipango ya Mungu. Mungu pekee ndiye Anayejua hatima ya nchi ama taifa lolote, na ni Mungu pekee ndiye Anayedhibiti mwenendo wa wanadamu hawa. Ikiwa wanadamu wanataka kuwa na hatima nzuri, ikiwa nchi inataka kuwa na hatima nzuri, basi mwanadamu lazima amsujudie Mungu katika ibada, na aje mbele za Mungu akitubu na kuungama, kama sivyo majaliwa na hatima ya mwanadamu hayataepuka kumalizika kwa janga.
Angalia nyuma wakati Nuhu alipojenga safina: Wanadamu walikuwa wamepotoka sana, walikuwa wamepotea kutoka katika baraka za Mungu, hawakuwa wanatunzwa na Mungu tena, na walikuwa wamepoteza ahadi za Mungu. Waliishi gizani, bila mwangaza wa Mungu. Hivyo wakawa waasherati kwa asili, wakajiachilia katika mkengeuko wa kutisha. Watu kama hao hawangeweza tena kupokea ahadi za Mungu; hawakufaa kushuhudia uso wa Mungu, wala kusikia sauti ya Mungu, kwani walikuwa wamemwacha Mungu, waliweka kando yote Aliyowapa, na kusahau mafunzo ya Mungu. Mioyo yao ilienda mbali zaidi na zaidi kutoka kwa Mungu, na ilivyofanya hivyo, wakawa wapotovu zaidi ya mantiki na ubinadamu wote na wakazidi kuwa waovu. Hivyo walisogelea kifo zaidi, na kukabiliwa na ghadhabu na adhabu ya Mungu. Ni Nuhu tu aliyemwabudu Mungu na kuepukana na uovu, na hivyo aliweza kusikia sauti ya Mungu, na kusikia maagizo ya Mungu. Alijenga safina kulingana na maagizo ya neno la Mungu, na akakusanya aina zote za viumbe hai. Na kwa njia hii, wakati kila kitu kilikuwa kimetayarishwa, Mungu aliangamiza dunia. Nuhu tu na wanachama saba wa familia yake walinusurika maangamizi, kwani Nuhu alimwabudu Yehova na kuepukana na uovu.
Kisha angalia enzi ya sasa: Hawa watu wenye haki kama Nuhu, ambao wangeweza kumwabudu Mungu na kuepuka uovu, wamekoma kuwepo. Lakini bado Mungu ana fadhili kwa mwanadamu huyu, na Anamsamehe mwanadamu wakati huu wa enzi ya mwisho. Mungu anawatafuta wale wanaotamani Aonekane. Anawatafuta wale wanaoweza kuyasikia maneno Yake, wale ambao hawajasahau agizo Lake na wanatoa mioyo na miili yao Kwake. Anawatafuta wale walio watiifu kama watoto wachanga mbele Zake, na hawampingi. Kama hujazuiliwa na nguvu zozote katika ibada yako Kwake, basi Mungu atakutazama kwa upendeleo na Ataweka baraka Zake juu yako. Kama wewe ni wa cheo cha juu, mwenye sifa ya kuheshimika, mwenye maarifa mengi, mwenye mali nyingi, na kuungwa mkono na watu wengi, lakini mambo haya hayakuzuii kuja mbele za Mungu kuukubali wito Wake na agizo Lake, kufanya kile Mungu anachokuambia ufanye, basi yote unayoyafanya yatakuwa yenye umuhimu zaidi duniani na yenye haki zaidi kwa binadamu. Ukiukataa wito wa Mungu kwa sababu ya hadhi yako na malengo yako mwenyewe, yote utakayoyafanya yatalaaniwa na hata kudharauliwa na Mungu. Pengine wewe ni rais, ama mwanasayansi, ama mchungaji, ama mzee, lakini bila kujali ukuu wa ofisi yako, ukitegemea maarifa yako na uwezo katika shughuli zako, basi daima utakuwa wa kushindwa na kamwe utanyimwa baraka za Mungu, kwa sababu Mungu hakubali chochote unachofanya, na Hakubali kwamba kazi yako ni yenye haki, wala kukubali kwamba unafanya kazi kwa manufaa ya wanadamu. Atasema kwamba kila kitu unachofanya, ni kutumia maarifa na nguvu za wanadamu ili kumwondolea mwanadamu ulinzi wa Mungu, ambapo ni kukataa baraka za Mungu. Atasema kuwa unamwongoza mwanadamu kuelekea gizani, kuelekea kifo, na kuelekea mwanzo wa maisha yasiyo na mipaka ambapo mwanadamu amempoteza Mungu na baraka Zake.
Tangu uvumbuzi wa wanadamu wa sayansi ya kijamii, akili ya mwanadamu imechukuliwa na sayansi na maarifa. Kisha sayansi na maarifa zikawa zana za kuwatawala wanadamu, na hakuna tena nafasi ya kutosha kwa mwanadamu kumwabudu Mungu, na hakuna hali nzuri zaidi kwa kumwabudu Mungu. Nafasi ya Mungu ikashuka chini kabisa katika moyo wa mwanadamu. Bila Mungu mioyoni mwao, ulimwengu wa ndani wa mwanadamu ni giza, usio na tumaini na ni mtupu. Na hivyo kukatokea wanasayansi wa jamii, wataalamu wa historia na wanasiasa wengi kueleza nadharia ya sayansi ya jamii, nadharia ya mageuko ya binadamu, na nadharia nyingine zinazopinga ukweli kwamba Mungu alimuumba mwanadamu, ilikujaza mioyo na akili za wanadamu. Na kwa njia hii, wanaoamini kwamba Mungu aliumba kila kitu wanakuwa wachache zaidi, na wale wanaoamini nadharia ya mageuko wanakuwa hata wengi kwa nambari. Watu zaidi na zaidi wanachukulia rekodi za kazi ya Mungu na maneno Yake wakati wa enzi ya Agano la Kale kuwa hadithi na hekaya. Katika mioyo yao, watu wanakuwa wasiojali adhama na ukuu wa Mungu, wasiojali kwamba Mungu yupo, na kanuni kwamba Mungu ana ukuu juu ya vitu vyote. Kuendelea kuishi kwa wanadamu na hatima ya nchi na mataifa si muhimu tena kwao, na mwanadamu anaishi katika ulimwengu ulio mtupu unaojishughulisha tu na kula, kunywa, na kutafuta raha. … Ni watu wachache wanaojishughulisha kutafuta mahali ambapo Mungu anafanya kazi Yake leo, au kutafuta jinsi Anavyosimamia na kupanga hatima ya mwanadamu. Na kwa njia hii, bila ya mwanadamu kujua, ustaarabu wa mwanadamu unashindwa zaidi na zaidi kuendana na matakwa ya mwanadamu, na hata kuna watu wengi zaidi ambao wanahisi kwamba, kuishi katika ulimwengu kama huu, hawana furaha kuliko wale ambao tayari wamekufa. Hata watu wa nchi zilizokuwa na ustaarabu wa hali ya juu wanatoa malalamiko kama hayo. Kwani bila mwongozo wa Mungu, hata kama watawala na wanasosholojia wataumiza akili zao ili kuhifadhi ustaarabu wa mwanadamu, haitakuwa na mafanikio. Hakuna anayeweza kujaza utupu katika moyo wa mwanadamu, kwani hakuna anayeweza kuwa uzima wa mwanadamu, na hakuna nadharia ya kijamii inayoweza kumwokoa kutokana na utupu unaomtesa. Sayansi, maarifa, uhuru, demokrasia, starehe na faraja, haya yote yanamletea mwanadamu faraja ya muda tu. Pamoja na mambo haya, mwanadamu bado haepuki kutenda dhambi na kulalamika kuhusu ukosefu wa haki kwa jamii. Mambo haya hayawezi kupunguza tamaa ya mwanadamu na hamu ya kuchunguza. Kwa sababu mwanadamu aliumbwa na Mungu na kujitoa kwao na uchunguzi usio na maana wa mwanadamu vitamwongoza tu kwenye dhiki zaidi. Mwanadamu daima atakuwa katika hali ya hofu isiyoisha, hatajua jinsi ya kuukabili mustakabali wa wanadamu, ama jinsi ya kuikabili njia iliyo mbele, hadi kufikia kiwango ambacho mwanadamu hata anaogopa sayansi na maarifa, na hata zaidi anahofia hisia ya utupu iliyo ndani yake. Katika ulimwengu huu, bila kujali kama unaishi katika nchi huru ama isiyo na haki za binadamu, huwezi kabisa kuponyoka majaliwa ya mwanadamu. Kama wewe ni kiongozi ama anayeongozwa, huwezi kabisa kuponyoka hamu ya kuchunguza majaliwa, mafumbo, na hatima ya wanadamu, sembuse kuwa na uwezo wa kutoroka hisia ya utupu inayotatiza. Matukio kama haya, yaliyo kawaida kwa wanadamu wote, yanaitwa matukio ya kijamii na wanasosholojia, lakini hakuna mtu mkuu anayeweza kuja kutatua shida kama hizi. Mwanadamu, hata hivyo, ni mwanadamu. Nafasi na maisha ya Mungu hayawezi kubadilishwa na mwanadamu yeyote. Mwanadamu hahitaji tu jamii iliyo na haki, ambapo kila mtu analishwa vyema na ana uhuru na usawa, lakini wokovu wa Mungu na utoaji Wake wa uzima kwa mwanadamu. Ni pale tu mwanadamu anapopokea utoaji wa Mungu wa uzima na wokovu Wake ndipo mahitaji yao, shauku yao ya kuchunguza, na utupu wa mioyo yao utaweza kutatuliwa. Ikiwa watu wa nchi ama taifa hawawezi kupokea wokovu na utunzaji wa Mungu, basi nchi ama taifa kama hilo litatembelea njia inayoelekea uharibifuni, inayoelekea gizani, na litaangamizwa na Mungu.
Pengine nchi yako inafanikiwa kwa sasa, lakini ukiruhusu watu wako waende mbali na Mungu, basi nchi yako itazidi kujipata bila baraka za Mungu. Ustaarabu wa nchi yako utazidi kukanyagiwa chini, na kabla ya muda mrefu watu watamwasi Mungu na kuilaani Mbingu. Kwa njia hii, bila mwanadamu kujua, hatima ya nchi itaharibiwa. Mungu ataziinua nchi zenye nguvu ili kukabiliana na nchi hizo zilizolaaniwa na Mungu, na Anaweza hata kuzifuta kutoka kwa uso wa dunia. Kupanda na kushuka kwa nchi ama taifa kunategemea kama viongozi wao wanamwabudu Mungu, na kama wanawaongoza watu wao karibu na Mungu na kumwabudu. Lakini, katika enzi hii ya mwisho, kwa sababu wale wanaomtafuta na kumwabudu Mungu kwa kweli wanazidi kuwa wachache, Mungu anatoa upendeleo wa pekee kwa nchi ambazo Ukristo ni dini ya serikali. Anazikusanya nchi hizo pamoja ili kuunda kambi ya ulimwengu yenye haki, wakati nchi zisizomwamini Mungu na zile nchi ambazo hazimwabudu Mungu wa kweli zinakuwa wapinzani wa kambi hiyo ya haki. Kwa njia hii, Mungu hana tu mahali miongoni mwa wanadamu pa kufanyia kazi Yake, lakini pia Anapata nchi zinazoweza kutumia mamlaka ya haki, Akiruhusu vizuizi na vikwazo kuwekwa kwa nchi hizo zinazompinga Mungu. Lakini licha ya hayo, bado hakuna watu zaidi wanaokuja kumwabudu Mungu, kwa sababu mwanadamu amepotea mbali sana kutoka Kwake, na mwanadamu amemsahau Mungu kwa muda mrefu sana, na katika dunia hii kumebaki tu nchi ambazo zinatenda haki na kupinga udhalimu. Lakini hii ipo mbali na kufikia matakwa ya Mungu, kwa kuwa hakuna viongozi wa nchi watakaomruhusu Mungu awaongoze watu wao, na hakuna chama cha kisiasa cha nchi kitakachokusanya pamoja watu wake ili wamwabudu Mungu; Mungu amepoteza nafasi Yake inayostahili katika moyo wa kila nchi, taifa, chama tawala, na hata katika moyo wa kila mtu. Ingawa baadhi ya nguvu za haki zipo katika ulimwengu huu, utawala wowote ambao Mungu hana nafasi ndani ya moyo wa mwanadamu ni mdhaifu sana, na uwanja wa kisiasa, ambao hauna baraka za Mungu, upo katika mkanganyiko na hauwezi kustahimili hata pigo moja. Kwa wanadamu, kutokuwa na baraka za Mungu ni sawa na kutokuwa na jua. Bila kujali jinsi watawala wanavyotoa michango kwa bidii kwa watu wao, bila kujali ni mikutano mingapi ya haki ambayo wanadamu wanafanya pamoja, hakuna hata moja kati ya haya litakaloweza kugeuza wimbi hilo au kubadilisha hatima ya wanadamu. Mwanadamu anaamini kwamba nchi ambayo watu wanalishwa na kuvishwa, ambayo watu wanaishi pamoja kwa amani, ndio nchi nzuri, na yenye uongozi mzuri. Lakini Mungu hafikirii hivyo. Anaamini kuwa nchi ambayo hakuna mtu anayemwabudu ndiyo Atakayoiangamiza. Njia ya mwanadamu ya kufikiria ni tofauti kabisa na ya Mungu. Kwa hiyvo, kama mkuu wa nchi hamwabudu Mungu, basi majaliwa ya nchi hii yatakuwa mabaya sana, na nchi hii haitakuwa na hatima.
Mungu hashiriki katika siasa za mwanadamu, lakini majaliwa ya nchi ama taifa yanadhibitiwa na Mungu, Mungu anadhibiti dunia hii na ulimwengu mzima. Majaliwa ya mwanadamu na mpango wa Mungu vimeunganishwa kwa karibu, na hakuna mtu, nchi au taifa linaloweza kuepuka ukuu wa Mungu. Ikiwa mwanadamu anatamani kujua hatima yake, basi lazima aje mbele za Mungu. Mungu atawafanya wanaomfuata na kumwabudu kufanikiwa, na Atawashusha na kuwaangamiza wale wanaompinga na kumkataa.
Kumbuka tukio katika Biblia ambapo Mungu aliangamiza Sodoma, na fikiria pia jinsi mke wa Lutu alivyokuwa nguzo ya chumvi. Fikiria nyuma jinsi watu wa Ninawi walivyotubu dhambi zao wakiwa kwenye magunia na majivu, na kumbuka kilichofuata baada ya Wayahudi kumsulubisha Yesu miaka 2,000 iliyopita. Wayahudi walifukuzwa kutoka Israeli na kukimbilia nchi za ulimwengu. Wengi waliuawa, na taifa zima la Kiyahudi lilipatwa na uchungu usio na kifani wa kuangamizwa kwa nchi yao. Walikuwa wamempigilia Mungu msalabani—walifanya uhalifu wa kutisha—na kuichokoza tabia ya Mungu. Walifanywa kulipia kile walichofanya, na walifanywa kubeba matokeo yote ya vitendo vyao. Walimhukumu Mungu, walimkataa Mungu, na hivyo walikuwa na hatima moja tu: kuadhibiwa na Mungu. Haya ndiyo matokeo machungu na maafa ambayo viongozi wao walileta juu ya nchi na taifa lao.
Leo, Mungu amerudi duniani kufanya kazi Yake. Na kituo Chake cha kwanza katika kazi Yake ni kielelezo cha juu cha udikteta: Uchina, ngome kali ya ukanaji Mungu. Mungu amepata kundi la watu kwa hekima na nguvu Zake. Wakati huu, Anawindwa na chama tawala cha Uchina kwa kila namna na kukabiliwa na mateso ya kila aina, bila mahala pa kupumzisha kichwa Chake na kutoweza kupata makazi. Licha ya haya, Mungu bado anaendelea kufanya kazi Aliyonuia kufanya: Anatamka sauti Yake na kueneza injili. Hakuna anayeweza kuelewa uweza wa Mungu. Uchina, nchi inayomchukulia Mungu kama adui, Mungu hajawahi kukoma kazi Yake. Badala yake, watu wengi zaidi wamekubali kazi na neno Lake, kwani Mungu anafanya yote Awezayo kuokoa kila mshiriki wa ubinadamu. Sote tunaamini kwamba hakuna nchi au nguvu inayoweza kuzuia kile ambacho Mungu anataka kutimiza, na kwamba wale wanaojaribu kuzuia kazi ya Mungu, wanaopinga neno la Mungu, na wale wanaovuruga na kujaribu kuharibu mpango wa Mungu hatimaye wataadhibiwa na Mungu. Mtu yeyote anayepinga kazi ya Mungu atapelekwa kuzimu; nchi yoyote inayoasi kazi ya Mungu itaangamizwa; taifa lolote linaloinuka kupinga kazi ya Mungu litafutwa kutoka kwa dunia hii na Mungu, na litakoma kuwepo. Ninawahimiza watu wa mataifa yote na wa nchi zote, na hata wa tasnia zote wasikilize sauti ya Mungu, waitazame kazi ya Mungu, na wazingatie hatima ya wanadamu, na hivyo kumfanya Mungu kuwa kitu kitakatifu zaidi, chenye kuheshimiwa zaidi, cha juu, na kitu pekee cha kuabudiwa miongoni mwa wanadamu, na kuwawezesha binadamu wote waishi katikati ya baraka za Mungu, kama tu vile uzazi wa Ibrahimu walivyoishi chini ya ahadi ya Yehova, na kama tu vile Adamu na Hawa, ambao Mungu aliwaumba hapo mwanzo, walivyoishi katika Bustani ya Edeni.
Kazi ya Mungu inasonga mbele kama wimbi kubwa. Hakuna anayeweza kumzuia, na hakuna anayeweza kusimamisha mwendo Wake. Ni wale tu wanaosikiliza maneno Yake kwa makini, na wanaomtafuta na kuwa na shauku na Yeye, ndio wanaoweza kufuata nyayo Zake na kupokea ahadi Yake. Wale wasiofanya hivyo watakabiliwa na maafa makubwa na adhabu wanayostahili kabisa.