Kuonekana kwa Mungu Kumeileta Enzi Mpya

Mpango wa usimamizi wa Mungu wa miaka elfu sita unaelekea kufika mwisho, na lango la ufalme tayari limefunguliwa kwa wale wote wanaotafuta kuonekana Kwake. Ndugu wapendwa, mnangoja nini? Ni nini ambacho mnatafuta? Je, mnangoja Mungu aonekane? Je, mnatafuta hatua Zake? Kuonekana kwa Mungu kunatamaniwa sana! Ni vigumu namna gani kupata hatua za Mungu! Katika enzi kama hii, katika dunia kama hii, lazima tufanye nini ili tushuhudie siku ambayo Mungu anaonekana? Lazima tufanye nini ili twende sambamba na hatua za Mungu? Wale wote wanaongoja kuonekana kwa Mungu wanakabiliwa na maswali ya aina hii. Ninyi nyote mmeyafikiria kwa zaidi ya mara moja—lakini matokeo yamekuwa yapi? Mungu anaonekana wapi? Hatua za Mungu ziko wapi? Je, mmepata majibu? Watu wengi wangejibu kwa namna hii: “Mungu anaonekana miongoni mwa wale wote wanaomfuata na hatua Zake ziko katikati yetu; ni rahisi hivyo!” Mtu yeyote anaweza kutoa jibu la kikanuni, lakini, je, mnaelewa ni nini maana ya kuonekana kwa Mungu au hatua Zake? Kuonekana kwa Mungu kunarejelea Mungu kuja duniani Mwenyewe kufanya kazi, kushuka miongoni mwa wanadamu kuendesha kazi ya kuanzisha enzi na kuhitimisha enzi kwa utambulisho Wake mwenyewe na tabia Yake mwenyewe, na kwa namna ambayo ni ya asili Kwake. Kuonekana kwa aina hii si aina ya utaratibu wa kidini. Si ishara, picha, muujiza, au aina ya maono makuu, na sembuse aina ya mchakato wa kidini. Badala yake, ni ukweli halisi na wa vitendo ambao unaweza kuguswa na kutazamwa na yeyote. Kuonekana kwa aina hii si kwa ajili ya kufanya mambo kwa namna isiyo ya dhati, au kwa ajili ya aina ya kazi ya muda mfupi. Badala yake, ni kwa ajili ya hatua ya kazi katika mpango wa usimamizi wa Mungu. Kuonekana kwa Mungu daima ni jambo la maana na daima kuna uhusiano fulani na mpango Wake wa usimamizi. Kile kinachoitwa “kuonekana” hapa ni tofauti kabisa na aina ya “kuonekana” ambapo Mungu humwelekeza, humwongoza, na humtia nuru mwanadamu. Kila wakati Mungu anapoonekana, Yeye hutekeleza hatua ya kazi Yake kuu. Kazi hii ni tofauti na ile ya enzi nyingine yoyote. Ni isiyofikirika na mwanadamu, na haijawahi kupitiwa na mwanadamu hapo awali. Ni kazi inayoanzisha enzi mpya na kuhitimisha enzi ya zamani, na ni hatua mpya zaidi na ya juu zaidi ya kazi kwa ajili ya wokovu wa wanadamu; zaidi ya hayo, ni kazi inayowaongoza wanadamu kuingia katika enzi mpya. Huu ndio umuhimu wa kuonekana kwa Mungu.

Punde mnapoelewa maana ya kuonekana kwa Mungu, mnapaswa kutafutaje hatua za Mungu? Swali hili si gumu kueleza: Popote anapoonekana Mungu, hapo mtapata hatua Zake. Maelezo kama hayo yanasikika kuwa ya moja kwa moja kabisa, lakini si rahisi sana katika utendaji, kwa kuwa watu wengi hawajui Mungu anaonekana wapi, sembuse mahali ambapo Yeye yuko radhi, au mahali Anapaswa, kuonekana. Wengine wanaamini kwa msukumo kwamba popote ambapo Roho Mtakatifu anafanya kazi, hapo Mungu anaonekana. Au vinginevyo wanaamini kwamba popote palipo na watu wa kiroho, hapo Mungu anaonekana. Au vinginevyo wanaamini kwamba popote palipo na watu wenye umashuhuri mkubwa, hapo Mungu anaonekana. Kwa sasa, hebu tuweke kando iwapo imani kama hizo ni sahihi au si sahihi. Ili kueleza swali kama hilo, lazima kwanza tuwe na lengo la wazi: Tunatafuta hatua za Mungu. Hatutafuti watu wa kiroho, sembuse kufuata watu wenye umashuhuri; tunazifuata hatua za Mungu. Kwa sababu hii, kwa kuwa tunatafuta hatua za Mungu, hatuna budi kutafuta nia ya Mungu, maneno ya Mungu, na matamko Yake. Hii ni kwa sababu popote palipo na maneno mapya yanayonenwa na Mungu, sauti ya Mungu ipo hapo, na popote palipo na hatua za Mungu, matendo ya Mungu yapo hapo; popote palipo na maonyesho ya Mungu, Mungu anaonekana hapo, na popote anapoonekana Mungu, ukweli, njia, na uzima vipo hapo. Katika kutafuta hatua za Mungu, ninyi mmeyapuuza maneno “Mungu ni ukweli, njia, na uzima.” Na hivyo, watu wengi, hata wanapopata ukweli, hawaamini kwamba wamepata hatua za Mungu, na sembuse kukiri kuonekana kwa Mungu. Hili ni kosa zito kiasi gani! Kuonekana kwa Mungu hakuwezi kukubaliana na mawazo ya mwanadamu, sembuse Mungu kuonekana kwa jinsi mwanadamu anavyodai Yeye aonekane. Mungu hufanya uchaguzi Wake mwenyewe na mipango Yake mwenyewe Anapofanya kazi Yake; zaidi ya hayo, Yeye ana malengo Yake mwenyewe na njia Zake mwenyewe. Kazi yoyote Anayofanya, Yeye hana haja ya kuijadili na mwanadamu au kutafuta ushauri wake, sembuse kumwarifu kila mtu kuhusu kazi Yake. Hii ni tabia ya Mungu, na inapaswa, hata zaidi, kutambuliwa na kila mtu. Ikiwa mnatamani kushuhudia kuonekana kwa Mungu, kufuata hatua za Mungu, basi lazima kwanza muyaache mawazo yenu wenyewe. Msidai kwamba Mungu afanye hili au lile, sembuse wewe kumweka Yeye ndani ya mipaka yako mwenyewe na kumwekea mipaka katika mawazo yako mwenyewe. Badala yake, mnapaswa kudai kutoka kwenu wenyewe jinsi mnavyopaswa kutafuta hatua za Mungu, jinsi mnavyopaswa kukubali kuonekana kwa Mungu, na jinsi mnavyopaswa kuitii kazi mpya ya Mungu: Hiki ndicho anachopaswa kufanya mwanadamu. Kwa kuwa mwanadamu si ukweli, na hana ukweli, anapaswa kutafuta, kukubali, na kutii.

Haijalishi wewe ni Mmarekani, Mwingereza, au wa utaifa mwingine wowote, unapaswa kutoka nje ya mipaka ya utaifa wako mwenyewe, ukivuka nafsi yako mwenyewe, na uitazame kazi ya Mungu kutoka katika mtazamo wa utambulisho wa kiumbe aliyeumbwa—kwa njia hiyo, hutaziwekea hatua za Mungu mipaka katika mawanda yoyote mahususi. Hii ni kwa sababu, kulingana na mawazo yao, watu wengi siku hizi wanaamini kuwa haiwezekani kwa Mungu kuonekana katika nchi mahususi au kati ya taifa fulani. Maana ya kazi ya Mungu ni ya kina jinsi gani, na kuonekana kwa Mungu ni muhimu jinsi gani! Je, mawazo na fikira za mwanadamu zinawezaje kuvipima? Na kwa hivyo Ninasema, unapaswa kuvunja mawazo yako ya utaifa na kabila ili utafute kuonekana kwa Mungu. Hapo tu ndipo hutafungwa na mawazo yako mwenyewe; hapo tu ndipo utakuwa na sifa za kukaribisha kuonekana kwa Mungu. Vinginevyo, utabaki katika giza la milele, na kamwe hutapata kibali cha Mungu.

Mungu ni Mungu wa mbari nzima ya wanadamu. Yeye hajichukulii Mwenyewe kama mali ya kibinafsi ya nchi au taifa lolote, bali hufanya kazi Yake kama Alivyopanga, bila kuzuiliwa na umbo, nchi, au taifa lolote. Pengine wewe hujawahi kuwazia umbo hili, au pengine mtazamo wako kwa umbo hili ni wa kukanusha, au pengine nchi ambayo na taifa ambalo kati yake Mungu anaonekana yanatokea tu kubaguliwa na kila mtu na yanatokea tu kuwa yaliyo nyuma zaidi duniani. Hata hivyo Mungu ana hekima Yake. Kwa nguvu Zake kuu, na kupitia ukweli Wake na tabia Yake, Yeye hakika amelipata kundi la watu wenye moyo na mawazo sawa na Yeye, na kundi la watu ambao Alitaka kuwafanya kuwa kamili—kundi ambalo Amelishinda, ambalo limevumilia kila namna ya majaribu na taabu na kila namna ya mateso, na linaweza kumfuata Yeye hadi mwisho kabisa. Lengo la kuonekana kwa Mungu, ambalo haliwekewi mipaka kwa umbo au nchi yoyote, ni kumwezesha Yeye akamilishe kazi Yake kama Alivyopanga. Hii ni kama tu wakati Mungu alipopata mwili huko Yudea: Lengo Lake lilikuwa kukamilisha kazi ya kusulubiwa katika kuwakomboa wanadamu wote. Hata hivyo Wayahudi waliamini kwamba haikuwezekana kwa Mungu kufanya hivi, na walifikiri kuwa haiwezekani kwamba Mungu angeweza kupata mwili na kuchukua mfano wa Bwana Yesu. “Haiwezekani” yao ikawa msingi ambao kwao walimshutumu na kumpinga Mungu, na hatimaye ilisababisha kuangamizwa kwa Israeli. Leo, watu wengi wamefanya kosa kama hilo. Wanatangaza kwa nguvu zao zote kuonekana kwa Mungu kunakokaribia, lakini wakati huo huo wanashutumu kuonekana Kwake; “haiwezekani” yao kwa mara nyingine tena inawekea mipaka kuonekana kwa Mungu ndani ya mipaka ya fikira zao. Na kwa hivyo Nimeona watu wengi wakiangua kicheko cha fujo na kelele baada ya kukutana na maneno ya Mungu. Lakini, je, kicheko hiki ni tofauti na shutuma na kufuru ya Wayahudi? Ninyi hamna kicho mbele ya ukweli, sembuse kuwa na mtazamo wa kutamani sana. Mnalofanya tu ni kuchunguza kwa ukaidi, na kungoja kwa moyo mwepesi wa kutojali. Mnaweza kupata nini kutokana na kuchunguza kwa makini na kusubiri namna hii? Je, mnafikiri mtapokea mwongozo wa kibinafsi kutoka kwa Mungu? Ikiwa huwezi kutambua matamko ya Mungu, unastahili kwa njia gani kushuhudia kuonekana kwa Mungu? Popote anapoonekana Mungu, hapo ukweli utaonyeshwa, na hapo sauti ya Mungu itakuwepo. Ni wale tu wanaoweza kukubali ukweli ndio wanaoweza kuisikia sauti ya Mungu, na ni watu kama hao tu ndio wanaostahili kushuhudia kuonekana kwa Mungu. Weka kando mawazo yako! Tuliza nafsi yako na usome maneno haya kwa makini. Mradi una moyo unaotamani sana ukweli, Mungu atakutia nuru ili uelewe nia Zake na maneno Yake. Wekeni kando hoja zenu za “haiwezekani”! Kadiri watu wanavyoamini jambo fulani haliwezekani, ndivyo kuna uwezekano mkubwa wa jambo hilo kutokea, kwa sababu hekima ya Mungu iko juu kuliko mbingu, mawazo ya Mungu yako juu kuliko mawazo ya mwanadamu, na Mungu hufanya kazi Yake kupita mipaka ya fikira na mawazo ya mwanadamu. Kadiri jambo fulani lisivyowezekana, ndivyo kuna ukweli wa kutafutwa ndani ya jambo hilo; kadiri jambo fulani lisivyoweza kuwaziwa na mawazo ya mwanadamu, ndivyo linavyokuwa na nia za Mungu. Hii ni kwa sababu, haijalishi Anaonekana wapi, Mungu bado ni Mungu, na kiini Chake hakitabadilika kabisa kwa sababu ya mahali au namna ya kuonekana Kwake. Tabia ya Mungu haitabadilika bila kujali hatua Zake ziko wapi, na haijalishi hatua za Mungu ziko wapi, Yeye ni Mungu wa wanadamu wote, kama vile tu Bwana Yesu si Mungu wa Waisraeli pekee, bali pia ni Mungu wa watu wote wa Asia, Ulaya, na Amerika, na hata zaidi ya hayo, Yeye ni Mungu mmoja pekee Aliye juu na kote ulimwenguni. Kwa hivyo hebu tutafute nia za Mungu na tugundue kuonekana Kwake katika matamko Yake na maneno Yake, na twende sambamba na hatua Zake! Mungu ni ukweli, njia, na uzima. Maneno Yake na kuonekana Kwake vipo kwa wakati mmoja, na tabia Yake na hatua Zake zinaonyeshwa hadharani kwa wanadamu wakati wote. Ndugu wapendwa, Ninatumai kwamba ninyi nyote mnaweza kuona kuonekana kwa Mungu katika maneno haya, muanze kwenda sambamba na hatua Zake na kupiga hatua mbele kuingia katika enzi mpya, na kuingia katika mbingu mpya na nchi mpya nzuri ambayo Mungu amewatayarishia wale wanaongoja kuonekana Kwake!

Iliyotangulia: Kutanafusi kwa Mwenye Uweza

Inayofuata: Mungu Anashikilia Mamlaka Juu ya Hatima ya Binadamu Wote

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp