Utendaji (2)

Katika nyakati zilizopita, watu walijifunza wenyewe kuwa na Mungu na kuishi ndani ya roho kila wakati. Ukilinganishwa na utendaji wa leo, hayo ni mafundisho rahisi ya kiroho, ni mbinu ya juujuu zaidi na rahisi zaidi ya utendaji kabla ya watu kuingia kwenye njia sahihi ya maisha, na yanaunda hatua ya kwanza kabisa ya utendaji katika imani ya watu. Ikiwa watu watategemea utendaji wa aina hii maishani mwao kila mara, watakuwa na hisia nyingi na huenda wakafanya makosa na hawatakuwa na uwezo wa kuingia katika uzoefu wa kweli wa maisha; wataweza tu kuzifundisha roho zao, kumkaribia Mungu kwa kawaida katika mioyo yao, na kila mara watapata furaha nyingi mno katika kuwa na Mungu pamoja nao. Watajiwekea mipaka katika mawanda madogo ya upamoja wao na Mungu, na hawataweza kufikia kitu chochote cha kina zaidi. Watu ambao huishi katika mipaka hii hawana uwezo wa kupiga hatua yoyote kubwa. Wakati wowote, wanaweza kupaza sauti, “Ee! Bwana Yesu. Amina!” Wako hivi takribani kila siku—ni utendaji wa nyakati zilizopita, utendaji wa kuishi ndani ya roho kila wakati. Huo sio utovu wa adabu? Leo, ufikapo wakati wa kutafakari maneno ya Mungu, zingatia tu kutafakari maneno ya Mungu; ufikapo wakati wa kuuweka ukweli katika vitendo, zingatia tu kuuweka ukweli katika vitendo; na ufikapo wakati wa kutekeleza wajibu wako, tekeleza tu wajibu wako. Utendaji wa aina hii kwa kweli utakuweka huru; unakufungua wewe. Sio kama jinsi wazee wa dini huomba na kusema sala ya mlo. Bila shaka, hapo awali, watu wa imani walitenda hivi, lakini sasa kutenda kwa namna hii ni kuwa nyuma kimaendeleo. Kazi ya Mungu sasa iko katika kiwango cha juu zaidi; kinachozungumziwa leo, “kumleta Mungu katika maisha halisi,” ndicho kipengele muhimu zaidi cha utendaji. Huu ndio ubinadamu wa kawaida ambao watu wanatarajiwa kumiliki katika maisha yao halisi, na kile ambacho watu wanapaswa kuwa nacho katika ubinadamu wao wa kawaida ni maneno yote ambayo Mungu ananena leo. Kuyaleta maneno haya ya Mungu katika maisha ya kweli ndiyo maana halisi ya “kumleta Mungu katika maisha halisi.” Leo, watu wanapaswa hasa kujiandaa na yafuatayo: Kwa upande mmoja, lazima waboreshe ubora wao wa tabia, wapate mafunzo na waboreshe ustadi wao wa usomaji na uelewaji; na katika mwingine, lazima waishi maisha ya mtu wa kawaida. Umerudi tu mbele ya Mungu kutoka ulimwenguni; lazima kwanza uufunze moyo wako kutulia mbele ya Mungu. Huu ndio mwanzo kabisa wa utendaji, na pia ndiyo hatua ya kwanza ya kutimiza mabadiliko katika tabia yako ya maisha. Watu wengine kwa ulinganisho ni wepesi kubadilika katika utendaji wao; wao hutafakari ukweli huku wakifanya kazi, wakijaribu kuelewa ukweli na kanuni za utendaji wanazopaswa kufahamu kwa uhalisi. Kipengele kimoja ni kwamba lazima uwe na maisha ya kawaida ya binadamu, na kingine ni kwamba lazima kuwe na kuingia katika ukweli. Vitu hivi vyote vinajumuisha utendaji bora zaidi wa maisha halisi.

Kumleta Mungu katika maisha halisi ya watu kimsingi kunahitaji kwamba wamwabudu Mungu, watafute kumjua Mungu, na kutekeleza wajibu wa kiumbe wa Mungu ndani ya ubinadamu wa kawaida. Sio kwamba ni lazima wamwombe Mungu kila wakati wanapofanya kitu, kwamba si sawa na kwamba wanapaswa kuhisi ni wadeni Wake wasipoomba. Utendaji wa leo si namna hiyo; ni rahisi sana! Hauwahitaji watu wafuate kanuni. Badala yake, kila mtu anapaswa kutenda kulingana na kimo chake mwenyewe: Ikiwa wanafamilia wako hawamwamini Mungu, wachukulie kama watu wasioamini, na ikiwa wanaamini, wachukulie kama waumini. Usitende kwa upendo na uvumilivu, badala yake tenda kwa hekima. Watu wengine huenda kununua mboga, na huku wakitembea wao hunong’ona: “Ee Mungu! Ni mboga gani ambazo Ungependa ninunue leo? Naomba usaidizi Wako. Mungu anataka tulitukuze jina Lake katika mambo yote na kwamba sote tuwe na ushuhuda, kwa hiyo hata muuzaji akinipa kitu kilichooza, bado nitampa Mungu shukrani—nitavumilia. Sisi tunaomwamini Mungu hatuwezi kuchagua kati ya mboga.” Wanafikiria kwamba kufanya hivi ni ushuhuda, na matokeo ni kwamba wanatumia pesa kununua kibunda cha mboga zilizooza, lakini bado wanaomba na kusema: “Ee Mungu! Bado nitakula mboga hizi zilizooza alimradi Unikubali nifanye jambo hilo.” Je, utendaji kama huo sio wa kipumbavu? Je, huko si kufuata mafundisho ya dini? Hapo awali, watu walijifunza kuishi ndani ya roho kila wakati—hili linahusiana na kazi iliyofanywa awali katika Enzi ya Neema. Uchaji Mungu, unyenyekevu, upendo, uvumilivu, kutoa shukrani kwa ajili ya mambo yote—haya ndiyo yale yaliyohitajika kutoka kwa kila muumini katika Enzi ya Neema. Wakati huo, watu walimwomba Mungu katika mambo yote; wangeomba waliponunua nguo, na walipofahamishwa juu ya mkutano, wangeomba pia na kusema: “Ee Mungu! Je, Utanikubalia niende au la? Ikiwa Utanikubalia niende, basi nitayarishie njia iliyonyooka. Ikiwa hutanikubalia niende, nifanye nijikwae na nianguke.” Wangemsihi Mungu huku wakiomba, na baada ya kuomba wangehisi wasio na utulivu na wangekosa kwenda. Akina dada wengine, wakihofia kwamba baada ya kurudi nyumbani kutoka mikutanoni wanaweza kupigwa na waume wao wasioamini, walihisi wasio na utulivu walipoomba na kwa hivyo hawangeenda kwenye mikutano. Waliamini haya kuwa mapenzi ya Mungu, ilhali ukweli ni kwamba, iwapo wangeenda, hakuna chochote ambacho kingefanyika. Matokeo ni kwamba hawakuhudhuria mkutano. Haya yote yalikuwa matokeo ya ujinga wa watu. Watu wanaotenda kwa njia hii huishi kulingana na hisia zao wenyewe. Njia hii ya utendaji ni yenye makosa na ya kipumbavu sana na imejaa hali ya kutokuwa yakini. Kuna hisia na mawazo yao binafsi mengi sana. Ukiambiwa kuhusu mkutano, basi nenda; hakuna haja zaidi ya kumwomba Mungu. Je, hili si jambo rahisi? Ikiwa unahitaji kununua mavazi fulani leo, basi nenda ukafanye hivyo. Usimwombe Mungu na kusema: “Ee Mungu! Utanikubalia niende au la? Na, je, ndugu au dada mmoja akija hapa nikiwa nimeondoka?” Unahofia huenda ndugu au dada fulani atakuja kwa hivyo huendi, ilhali matokeo ni kwamba jioni inafika na hakuna aliyekuja. Hata katika Enzi ya Neema, njia hii ya utendaji ilikuwa potovu na yenye makosa. Hivyo, watu wakitenda kama katika nyakati zilizopita, hakutakuwa na mabadiliko katika maisha yao. Kwa ujinga watakubali tu chochote kitakachotokea, hawatazingatia utambuzi na hawatafanya lolote ila kutii na kuvumilia pasipo kufikiria. Wakati huo, watu walilenga kumtukuza Mungu—lakini Mungu hakupata utukufu wowote kutoka kwao, kwani hawakuwa wameishi kwa kudhihirisha lolote la vitendo. Walijizuilia tu na kujiwekea mipaka kulingana na mawazo yao wenyewe, na hata miaka mingi ya utendaji haikuleta mabadiliko katika maisha yao. Walijua tu kuvumilia, kuwa wanyenyekevu, kupenda, na kusamehe, lakini hawakuwa na kiwango hata kidogo cha nuru kutoka kwa Roho Mtakatifu. Watu wangemjuaje Mungu kwa njia hiyo? Na wangewezaje kumtukuza Mungu?

Watu wanaweza tu kuingia kwenye njia sahihi ya imani katika Mungu ikiwa watamleta Mungu katika maisha yao halisi, na katika maisha yao ya kawaida ya binadamu. Maneno ya Mungu yanawaongoza ninyi leo; hakuna haja ya ninyi kutafuta na kupapasa kama nyakati zilizopita. Wakati ambapo unaweza kutenda kulingana na maneno ya Mungu, na unaweza kujichunguza na kujitathmini mwenyewe kulingana na hali za binadamu ambazo Nimefichua, basi utaweza kutimiza mabadiliko. Haya siyo mafundisho ya dini, lakini ni kile ambacho Mungu anahitaji kutoka kwa mwanadamu. Leo, hebu Nikuambie jinsi mambo yalivyo: Jishughulishe tu na kutenda kulingana na maneno Yangu. Matakwa Yangu kwako yametegemezwa kwa mahitaji ya mtu wa kawaida. Tayari Nimekwambia maneno Yangu; mradi tu ulenge kuyatenda, utakubaliana na makusudi ya Mungu. Sasa ndio wakati wa kuishi ndani ya maneno ya Mungu. Maneno ya Mungu yameeleza kila kitu, yote yamewekwa wazi, na mradi tu uishi kulingana na maneno ya Mungu, utaishi maisha yaliyo huru kabisa na yaliyokombolewa. Hapo zamani, watu walipomleta Mungu katika maisha yao halisi, walitenda na kupitia mafundisho na kaida nyingi sana za dini; hata katika mambo madogo, wangeomba na kutafuta, wakiweka maneno hayo ya Mungu yaliyosemwa kinaganaga kando na kupuuza kuyasoma. Badala yake, wangeweka juhudi zao zote katika kutafuta—na matokeo yakiwa kwamba hakukuwa na athari. Chukua kwa mfano masuala ya chakula na mavazi: Unaomba na kuyaweka masuala haya mikononi mwa Mungu, ukitaka kwamba Mungu akupangie kila kitu. Mungu anaposikia maneno haya, Atasema: “Je, Napaswa kujishughulisha na mambo madogo kama haya? Ubinadamu wa kawaida na mantiki Niliyokuumbia yameenda wapi?” Wakati mwingine, mtu fulani hufanya makosa katika matendo yake; kisha anaamini kwamba amemkosea Mungu na kisha yeye huanza kujizuia. Hali za watu wengine ni nzuri sana, lakini wanapofanya kitu fulani kidogo kwa njia isiyo sahihi wao huamini kwamba Mungu anawaadibu. Kwa kweli, hayo siyo matendo ya Mungu, lakini ni ushawishi wa akili za watu wenyewe. Wakati mwingine, hakuna kitu kibaya na jinsi unavyopitia tukio, lakini wengine husema kwamba unapitia tukio hilo kwa njia isiyo sahihi, na hivyo unategwa—unakuwa hasi, na mwovu ndani yako. Mara kwa mara, watu wakiwa hasi kwa njia hii, wao huamini kwamba wanaadibiwa na Mungu, lakini Mungu anasema: “Sijafanya kazi yoyote ya kuadibu ndani yako; unawezaje kunilaumu hivyo?” Watu wanakuwa hasi kwa urahisi sana. Wao pia mara kwa mara ni wepesi kuhisi kwa kupindukiana mara nyingi wao hulalamika kuhusu Mungu. Mungu hakutaki wewe uteseke kwa njia hiyo, ilhali wewe unajiruhusu kuingia katika hali hiyo. Hakuna thamani katika kuteseka kwa namna hiyo. Watu hawajui kazi inayofanywa na Mungu, na katika mambo mengi wao ni wajinga na hawawezi kuona vizuri, kwa hiyo wao hunaswa katika dhana na mawazo yao wenyewe, wakiendelea kutegwa kwa kina zaidi. Watu wengine husema kwamba vitu vyote na mambo yote yamo mikononi mwa Mungu—kwa hiyo Mungu hawezi kujua wakati watu wakohasi? Bila shaka Mungu hujua. Unapotegwa katika mawazo ya binadamu, Roho Mtakatifu hana njia ya kufanya kazi ndani yako. Wakati mwingi, watu wengine hutegwa katika hali hasi, lakini Mimi bado huendelea na kazi Yangu. Uwe hasi au chanya, Mimi sizuiliwi na wewe—lakini unapaswa kujua kwamba maneno mengi Ninenayo, na kiasi kikubwa sana cha kazi Nifanyayo, vyote vimeunganika kwa karibu, kimoja kwa kingine, kulingana na hali za watu. Wakati ambapo wewe ni hasi, hili haliizuii kazi ya Roho Mtakatifu. Wakati wa kuadibu na majaribu ya kifo, watu wote walitegwa katika hali hasi, lakini hili halikuizuia kazi Yangu. Ulipokuwa hasi, Roho Mtakatifu aliendelea kufanya kilichohitajika kufanywa ndani ya wengine. Unaweza kuacha kufuatilia kwa mwezi mmoja, lakini Mimi naendelea kufanya kazi—chochote ufanyacho katika siku za sasa au za baadaye, hakiwezi kuizuia kazi ya Roho Mtakatifu. Hali nyingine hasi hutokana na udhaifu wa binadamu; wakati ambapo watu wanaamini kwamba hawawezi kweli kutimiza mahitaji ya Mungu au kuyaelewa, wao hugeuka kuwa hasi. Kwa mfano, katika wakati wa kuadibu, maneno ya Mungu yalizungumza kuhusu kumpenda Mungu hadi kwa kiwango fulani katikati ya kuadibu, lakini watu waliamini kwamba hawawezi wenyewe. Walihisi hasa wenye huzuni na wakaomboleza kwamba miili yao ilikuwa imepotoshwa sana na Shetani, na kwamba ubora wao wa tabia ulikuwa duni sana. Walihisi kwamba lilikuwa jambo la kusikitisha sana kuwa walizaliwa katika mazingira haya. Na watu wengine walihisi kwamba wakati ulikuwa umepita sana kwa wao kumwamini Mungu na kumjua Mungu, na kwamba hawakustahili kufanywa wakamilifu. Hizi zote ni hali za kawaida za binadamu.

Mwili wa mwanadamu ni wa Shetani, umejaa tabia za uasi, ni mchafu kiasi cha kusikitisha, na ni kitu chenye najisi. Watu hutamani raha ya mwili kupita kiasi na kuna maonyesho mengi sana ya mwili; hii ndiyo maana Mungu hudharau mwili wa mwanadamu kwa kiwango fulani. Watu wanapotupa mambo machafu, potovu ya Shetani, wao hupata wokovu wa Mungu. Lakini bado wasipoachana na uchafu na upotovu, basi bado wanamilikiwa na Shetani. Ujanja, udanganyifu, na ukora wa watu yote ni mambo ya Shetani. Wokovu wa Mungu kwako ni ili kukuokoa kutoka katika mambo haya ya Shetani. Kazi ya Mungu haiwezi kuwa na kosa; yote inafanywa ili kuwaokoa watu kutoka gizani. Wakati ambapo umeamini hadi kwa kiwango fulani na unaweza kuachana na upotovu wa mwili, na hufungwi tena pingu na upotovu huu, je, hutakuwa umeokolewa? Wakati ambapo unamilikiwa na Shetani huwezi kumdhihirisha Mungu, wewe ni kitu kichafu, na huwezi kupokea urithi wa Mungu. Mara tu unapotakaswa na kufanywa mkamilifu, utakuwa mtakatifu, utakuwa mtu wa kawaida, na utabarikiwa na Mungu na kuwa mtu anayemfurahisha Mungu. Kazi inayofanywa na Mungu leo ni wokovu, na zaidi ya hayo, ni hukumu, kuadibu, na kulaani. Ina vipengele kadhaa. Nyote mnaona kwamba matamko ya Mungu yana hukumu na kuadibu, na vile vile laana. Nazungumza ili kutimiza athari fulani, kuwafanya watu wajijue, na si kuwafisha watu. Moyo Wangu ni kwa ajili yenu. Kuzungumza ni mbinu mojawapo ambayo Mimi hufanya kazi; kupitia maneno Ninaonyesha tabia ya Mungu na kukuruhusu uelewe mapenzi ya Mungu. Mwili wako waweza kufa, lakini una roho na nafsi. Kama watu wangekuwa na mwili tu, basi hakungekuwa na maana yoyote katika imani yao, wala hakungekuwa na maana yoyote katika kazi hii yote ambayo Nimefanya. Leo, Nazungumza kwa njia moja na kisha nyingine; kwa muda fulani Nawachukia watu mno, na kisha wakati mwingine Mimi ni mwenye upendo wa hali ya juu; Nafanya haya yote kutimiza mabadiliko katika tabia zako, na vile vile kugeuza mawazo yako kuhusu kazi ya Mungu.

Siku za mwisho zimefika na nchi nyingi ulimwenguni ziko katika machafuko. Vurugu ya kisiasa, njaa, ndwele, mafuriko, na ukame unaonekana kila mahali. Kuna maangamizi katika ulimwengu wa mwanadamu; Mbingu pia imetuma msiba hapa chini. Hizi ni ishara za siku za mwisho. Lakini kwa watu, unaonekana kama ulimwengu wa uchangamfu na fahari, ambao unaendelea kuwa hivyo zaidi na zaidi. Mioyo ya watu yote inavutiwa nao, na watu wengi wananaswa na hawawezi kujinasua kutoka kwa ulimwengu; idadi kubwa itadanganywa na wale wanaoshiriki katika hila na uchawi. Usipojitahidi kuendelea mbele, huna maadili, na hujajikita mizizi katika njia ya kweli, utapeperushwa na mawimbi yavumayo ya dhambi. China ni nchi iliyo nyuma zaidi kimaendeleo kuliko zote; ni nchi ambapo joka kuu jekundu hulala likiwa limejiviringisha, ina watu wengi zaidi wanaoabudu sanamu na kushiriki katika uchawi, ina hekalu nyingi zaidi, na ni mahali ambapo pepo wachafu huishi. Ulizaliwa kutoka kwayo, umeelimishwa nayo na ukaloweshwa katika ushawishi wake; umepotoshwa na kuteswa nayo, lakini baada ya kugutushwa unaachana nayo na unapatwa kabisa na Mungu. Huu ni utukufu wa Mungu, na hii ndiyo maana hatua hii ya kazi ina umuhimu mkubwa. Mungu amefanya kazi ya kiwango kikubwa hivi, amenena maneno mengi sana, na hatimaye Atawapata ninyi kabisa—hii ni sehemu moja ya kazi ya usimamizi ya Mungu, na ninyi ndio “mateka wa ushindi” wa vita vya Mungu na Shetani. Kadiri mnavyozidi kuelewa ukweli na kadiri maisha yenu ya kanisa yalivyo bora zaidi, ndivyo joka kuu jekundu linavyotishwa zaidi. Haya yote ni mambo ya ulimwengu wa kiroho—ni vita vya ulimwengu wa kiroho, na Mungu anapokuwa mshindi, Shetani ataaibishwa na kuanguka chini. Hatua hii ya kazi ya Mungu ina umuhimu wa ajabu. Mungu anafanya kazi kwa kiwango kikubwa sana na kukiokoa kabisa kikundi hiki cha watu ili uweze kuponyoka kutoka kwa ushawishi wa Shetani, uishi katika nchi takatifu, uishi katika nuru ya Mungu, na uwe na uongozi na mwongozo wa nuru. Kisha kuna maana katika maisha yako. Mnachokula na kuvaa ni tofauti na wasioamini; mnafurahia maneno ya Mungu na kuishi maisha yenye maana—na wao hufurahia nini? Wao hufurahia tu “urithi wa babu” zao na “fahari yao ya kitaifa.” Hawana hata chembe ndogo kabisa ya ubinadamu! Mavazi, maneno, na matendo yenu yote ni tofauti na yao. Hatimaye, mtatoroka kabisa kutoka katika uchafu, msitegwe tena katika majaribu ya Shetani, na mpate riziki ya Mungu ya kila siku. Mnapaswa kila mara kuwa waangalifu. Ingawa mnaishi mahali pachafu hamjawekwa mawaa na uchafu na mnaweza kuishi ubavuni mwa Mungu, mkipokea ulinzi Wake mkuu. Mungu amewachagua kutoka miongoni mwa wote walio katika nchi hii ya manjano. Je, ninyi sio watu waliobarikiwa zaidi? Wewe ni kiumbe aliyeumbwa—unapaswa bila shaka kumwabudu Mungu na kufuatilia maisha yenye maana. Usipomwabudu Mungu lakini unaishi ndani ya mwili wako mchafu, basi wewe si mnyama tu aliye ndani ya vazi la mwanadamu? Kwa kuwa wewe ni binadamu, unapaswa kujitumia kwa ajili ya Mungu na kuvumilia kila mateso! Unapaswa kukubali kwa furaha na kwa hakika mateso kidogo unayopitia leo na kuishi maisha yenye maana, kama Ayubu na Petro. Katika ulimwengu huu, mwanadamu huvaa mavazi ya ibilisi, hula chakula kutoka kwa ibilisi, na hufanya kazi na kutumika chini ya uelekezi wa Shetani, na kukanyagiwa kabisa ndani ya uchafu wake. Usipoelewa maana ya maisha au kupata njia ya kweli, basi kuna umuhimu gani katika kuishi kwa namna hii? Ninyi ni watu mnaofuatilia njia sahihi, wale mnaotafuta maendeleo. Ninyi ni watu ambao huinuka katika nchi ya joka kuu jekundu, wale ambao Mungu huwaita wenye haki. Je, hayo si maisha yenye maana zaidi?

Iliyotangulia: Utendaji (1)

Inayofuata: Fumbo la Kupata Mwili (1)

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp