Kuhusu Maisha ya Kawaida ya Kiroho
Imani katika Mungu husababisha maisha ya kawaida ya kiroho, ambayo ndiyo msingi wa kupitia maneno ya Mungu na kuingia katika uhalisi. Je, matendo yenu yote ya sasa ya maombi, ya kumkaribia Mungu, ya kuimba nyimbo za dini, sifa, taamali na kutafakari maneno ya Mungu yanajumuisha “maisha ya kawaida ya kiroho”? Hakuna mmoja kati yenu anayeonekana kujua. Maisha ya kawaida ya kiroho hayazuiliwi katika matendo kama kuomba, kuimba nyimbo za kidini, kushiriki katika maisha ya kanisa, na kula na kunywa maneno ya Mungu. Badala yake, yanahusisha kuishi maisha mapya na machangamfu ya kiroho. Kilicho muhimu si jinsi unavyotenda, lakini matunda yanayozalishwa na kutenda kwako. Watu wengi sana huamini kwamba maisha ya kawaida ya kiroho ni lazima yahusishe kuomba, kuimba nyimbo za kidini, kula na kunywa maneno ya Mungu ama kutafakari maneno Yake, bila kujali iwapo matendo kama haya kweli yana athari yoyote ama yanasababisha ufahamu wa kweli. Watu hawa hulenga kufuata taratibu za kijuujuu bila kufikiria matokeo yake, wao ni watu wanaoishi katika kaida za kidini, sio watu wanaoishi ndani ya kanisa, sembuse watu wa ufalme. Maombi yao, kuimba nyimbo za kidini, na kula na kunywa maneno ya Mungu ni kufuata kanuni tu, vitu vinavyofanywa kwa sababu ya kulazimishwa na kuwa sambamba na mitindo, sio kwa sababu ya kutaka wala kutoka moyoni. Bila kujali jinsi watu hawa wanavyoomba ama kuimba, juhudi zao hazitazaa matunda, kwa kuwa kile wanachotenda ni kanuni na kaida za kidini tu; kwa kweli hawatendi maneno ya Mungu. Wanalenga tu kulalamika kuhusu jinsi ya kutenda, na wanayachukulia maneno ya Mungu kama kanuni za kufuatwa. Watu kama hawa hawatii maneno ya Mungu katika vitendo; wanaridhisha tu mwili, na kutenda ili watu wengine wawaone. Kanuni na kaida hizi za kidini zote zina asili yake kwa binadamu; hazitoki kwa Mungu. Mungu hafuati sheria, wala Haathiriwi na sheria yoyote. Badala yake, Yeye hufanya mambo mapya kila siku, Akitimiza kazi ya vitendo. Kama watu katika Kanisa la Kanuni Tatu za Binafsi, wanaojiwekea mipaka kwa matendo kama vile kuhudhuria ibada za asubuhi kila siku, kutoa sala za jioni na sala za shukrani kabla ya milo, na kutoa shukrani katika vitu vyote—bila kujali kiasi wanachofanya ama wanakifanya kwa muda gani, hawatakuwa na kazi ya Roho Mtakatifu. Watu wanapoishi kati ya kanuni na kuzingatia mbinu za utendaji, Roho Mtakatifu hawezi kufanya kazi, kwa sababu mioyo yao imejazwa na kanuni na fikira za kibinadamu. Kwa hivyo, Mungu hawezi kuingilia kati na kuwafanyia kazi, na wanaweza tu kuendelea kuishi wakidhibitiwa na sheria. Watu kama hawa daima hawawezi kupokea sifa ya Mungu.
Maisha ya kawaida ya kiroho ni maisha ambayo mtu anaishi mbele za Mungu. Mtu anapoomba, anaweza kuutuliza moyo wake mbele za Mungu, na kupitia maombi, mtu anaweza kutafuta nuru ya Roho Mtakatifu, ayajue maneno ya Mungu na aelewe mapenzi ya Mungu. Kwa kula na kunywa maneno Yake, watu wanaweza kupata ufahamu dhahiri na kamili zaidi wa kazi ya sasa ya Mungu. Pia wanaweza kupata njia mpya ya kutenda, na hawatashikilia ile ya kale; yote wanayotenda yatakuwa ili kufanikisha ukuaji katika maisha. Kuhusiana na maombi, hayahusu kunena maneno machache yanayosikika kuwa mazuri ama kulia kwa ghafla mbele za Mungu ili kuonyesha jinsi unavyowiwa naye; badala yake, lengo lake ni kujifunza kutumia roho, ikimwezesha kuutuliza moyo wake mbele za Mungu, kujifunza kutafuta mwongozo kutoka kwa maneno ya Mungu katika masuala yote, ili moyo wake uweze kukaribia mwanga mpya na safi kila siku, na ili mtu asiwe mwenye kukaa tu ama mzembe na aweze kuingia kwenye njia sahihi ya kuyaweka maneno ya Mungu katika vitendo. Watu wengi siku hizi wanalenga mbinu za utendaji, lakini hawafanyi hivyo ili kuufuatilia ukweli na kufanikisha ukuaji wa maisha. Hapa ndipo walipopotoka. Pia kuna wengine wanaoweza kupokea mwanga mpya, lakini mbinu zao za utendaji hazibadiliki. Wao hutumia fikira zao za kale wanapotazamia kupokea maneno ya Mungu ya leo, kwa hivyo kile wanachopokea bado ni mafundisho yaliyoathiriwa na fikira za kidini; hawapokei mwanga wa leo hata kidogo. Kwa hiyo, matendo yao yametiwa doa; ni matendo yale yale ya kale katika kifurushi kipya. Bila kujali wanaweza kutenda vyema jinsi gani, wao ni wanafiki. Mungu huwaongoza watu katika kufanya mambo mapya kila siku, Akitaka kwamba kila siku wapate umaizi na ufahamu mpya, na kuwahitaji wasiwe waliopitwa na wakati na wenye kurudiarudia. Ikiwa umemwamini Mungu kwa miaka mingi, lakini mbinu zako za utendaji hazijabadilika hata kidogo, na ikiwa wewe bado ni mwenye raghba na mwenye shughuli nyingi kuhusu masuala ya nje, lakini huna moyo mtulivu wa kuleta mbele za Mungu ili uyafurahie maneno Yake, basi hutapata chochote. Inapofikia kuikubali kazi mpya ya Mungu, usipopanga kwa njia tofauti, usipotenda kwa njia mpya, na usifuatilie ufahamu wowote mpya, lakini badala yake ushikilie ya kale na kupokea tu mwanga finyu mpya, bila kubadili jinsi unavyotenda, basi watu kama wewe wako katika mkondo huu kwa jina tu; kwa kweli, wao ni Mafarisayo wa kidini walio nje ya mkondo wa Roho Mtakatifu.
Ili kuishi maisha ya kawaida ya kiroho, lazima mtu aweze kupokea mwanga mpya kila siku na afuatilie ufahamu wa kweli wa maneno ya Mungu. Ni lazima mtu aone ukweli vyema, apate njia ya utendaji katika masuala yote, agundue maswali mapya kupitia kusoma maneno ya Mungu kila siku, na atambue upungufu wake mwenyewe ili aweze kuwa na moyo unaotamani na kutafuta ambao unaigusa nafsi yake nzima, na ili aweze kutulia mbele za Mungu nyakati zote, akiogopa sana kubaki nyuma. Mtu aliye na moyo kama huu unaotamani na kutafuta, aliye tayari kupata kuingia bila kusita, yuko kwenye njia sahihi ya maisha ya kiroho. Wale wanaoguswa na Roho Mtakatifu, wanaotaka kufanya vizuri zaidi, walio tayari kufuatilia kukamilishwa na Mungu, wanaotamani ufahamu wa kina wa maneno ya Mungu, wasiofuatilia jambo la mwujiza lakini badala yake wanalipa gharama ya kweli, wanaoyajali mapenzi ya Mungu kwa kweli, ambao kwa kweli wanapata kuingia ili uzoefu wao uwe wa kweli na halisi zaidi, wasiofuatilia maneno na mafundisho matupu ama kufuatilia kuhisi jambo la mwujiza, wasiomwabudu mtu yeyote mashuhuri—hawa ndio wale ambao wameingia katika maisha ya kawaida ya kiroho. Kila kitu wanachofanya kinanuiwa kufanikisha ukuaji zaidi katika maisha na kuwafanya wawe wapya na wachangamfu katika roho, na daima wanaweza kupata kuingia kwa shauku. Bila wao kujua, wanakuja kuuelewa ukweli na kuingia katika uhalisi. Wale walio na maisha ya kawaida ya kiroho hupata ukombozi na uhuru wa roho kila siku, na wanaweza kutenda maneno ya Mungu kwa njia huru mpaka Aridhike. Kwa watu hawa, kuomba si jambo la kidesturi ama utaratibu; kila siku, wanaweza kuwa sambamba na mwanga mpya. Kwa mfano, watu hujifunza kuituliza mioyo yao mbele za Mungu, na mioyo yao inaweza kutulia mbele za Mungu kwa kweli, na hawawezi kusumbuliwa na yeyote. Hakuna mtu, tukio ama jambo linaloweza kuzuia maisha yao ya kawaida ya kiroho. Mafunzo kama hayo yananuiwa kuleta matokeo; hayanuiwi kuwafanya watu wafuate kanuni. Utendaji huu hauhusu kufuata kanuni, lakini badala yake unahusu kukuza ukuaji katika maisha ya watu. Ikiwa unaona utendaji huu kuwa kanuni za kufuatwa tu, maisha yako hayatawahi kubadilika. Unaweza kuwa umeshiriki katika matendo sawa kama wengine, lakini wakati wao wanaweza hatimaye kuwa sambamba na kazi ya Roho Mtakatifu, unaondolewa kutoka katika mkondo wa Roho Mtakatifu. Je, hujidanganyi? Lengo la maneno haya ni kuwawezesha watu waitulize mioyo yao mbele za Mungu, waigeuze mioyo yao kumwelekea Mungu, ili kazi ya Mungu ndani yao iweze kutozuiwa na iweze kuzaa matunda. Ni baada ya hayo tu ndiyo watu wataweza kukubaliana na mapenzi ya Mungu.