Hudumu Jinsi Waisraeli Walivyohudumu

Siku hizi, watu wengi hawatilii maanani ni mafunzo yapi wanayopaswa kupata wakati wanaposhirikiana na wengine. Nimegundua kwamba wengi wenu hawawezi kupata mafunzo hata kidogo wakati wanaposhirikiana na wengine; wengi wenu huyashikilia maoni yenu wenyewe. Unapofanya kazi kanisani, unatoa maoni yako na mtu mwingine anatoa yake, na maoni hayo hayana uhusiano; kwa kweli hamshirikiani hata kidogo. Ninyi nyote mnajishughulisha sana na kuwasiliana tu kuhusu utambuzi wenu wenyewe ama kuachilia “mizigo” mliyoibeba ndani yenu, bila kutafuta uzima kwa namna yoyote ile. Unaonekana kufanya kazi kwa njia ya uzembe tu, daima ukiamini kwamba unapaswa kuitembea njia yako mwenyewe bila kujali kile ambacho mtu mwingine anasema ama kufanya; unafikiria kwamba unapaswa kushiriki jinsi Roho Mtakatifu anavyokuongoza, bila kujali hali za wengine zinaweza kuwa zipi. Hamwezi kugundua uwezo wa wengine, na wala hamwezi kujichunguza. Kukubali kwenu mambo kumepotoka na kuna makosa sana. Inaweza kusemwa kwamba hata sasa bado mnaonyesha unyoofu mwingi, kana kwamba mmerudia ugonjwa huo wa zamani. Kwa mfano, hamwasiliani kwa njia inayofanikisha uwazi kamili, kwa mfano, kuhusu aina ya matokeo ambayo mmepata kutoka kwa kazi katika makanisa fulani, ama kuhusu hali zako za ndani za siku hizi na kadhalika; kamwe hamwasiliani hata kidogo kuhusu mambo kama hayo. Hamshiriki hata kidogo katika vitendo kama kuyaacha mawazo yenu wenyewe ama kujikana. Viongozi na wafanyakazi wanafikiri tu kuhusu jinsi ya kuwazuia ndugu zao wasiwe hasi na jinsi ya kuwafanya waweze kufuata kwa juhudi. Hata hivyo, ninyi nyote mnafikiri kwamba kufuata kwa juhudi pekee kunatosha, na kimsingi, hamwelewi maana ya kujijua na kujikana, sembuse kuelewa maana ya kuhudumu kwa kushirikiana na wengine. Mnafikiri tu kuhusu ninyi wenyewe kuwa na nia ya kuulipiza upendo wa Mungu, kuhusu ninyi wenyewe kutaka kuishi kwa kudhihirisha mtindo wa Petro. Hamfikirii kuhusu kitu kingine isipokuwa mambo haya. Hata unasema kwamba bila kujali yale watu wengine wanayofanya, hutatii bila kufikiria, na kwamba bila kujali jinsi watu wengine walivyo, wewe mwenyewe utatafuta kukamilishwa na Mungu, na hiyo itatosha. Hata hivyo, ukweli ni kwamba kutaka kwako hakujapata maonyesho thabiti kwa kweli. Je, haya yote sio mwenendo ambao mnadhihirisha siku hizi? Kila mmoja wenu anashikilia utambuzi wake mwenyewe, na nyote mnatamani kukamilishwa. Naona kwamba mmehudumu kwa muda mrefu sana bila kufanya maendeleo mengi; hasa katika funzo hili la kufanya kazi pamoja kwa upatanifu, hamjafanikisha chochote hata kidogo! Unapokwenda katika makanisa unawasiliana kwa njia yako, na wengine wanawasiliana kwa njia zao. Ushirikiano wa upatanifu unafanyika mara chache sana, na hili ni kweli hata zaidi kwa wafuasi walio chini yako. Yaani, ni mara chache ambapo yeyote kati yenu anaelewa maana ya kumhudumia Mungu, ama jinsi mtu anavyopaswa kumhudumia Mungu. Mmekanganyikiwa na mnayachukulia mafunzo ya aina hii kama mambo madogo. Hata kuna watu wengi ambao hawakosi kutenda kipengele hiki cha ukweli tu, lakini ambao pia wanafanya makosa kwa makusudi. Hata wale ambao wamehudumu kwa miaka mingi wanapigana na kupangiana njama nao ni wenye wivu na wenye kupenda kushindana; ni kila mtu na wake, na hawashirikiani hata kidogo. Je, mambo haya yote hayawakilishi kimo chenu cha kweli? Ninyi watu mnaohudumu pamoja kila siku ni kama Waisraeli, ambao kila siku walimhudumia Mungu Mwenyewe moja kwa moja hekaluni. Inawezekanaje kwamba ninyi watu, mnaomhudumia Mungu, hamjui jinsi ya kushirikiana ama jinsi ya kuhudumu?

Wakati huo, Waisraeli walimhudumia Yehova moja kwa moja hekaluni, na walikuwa na utambulisho wa makuhani. (Bila shaka, si kila mtu alikuwa kuhani; ni baadhi tu ya waliomhudumia Yehova hekaluni ndio waliokuwa na utambulisho huo.) Walijitwika mataji waliyopewa na Yehova (kumaanisha kwamba walitengeneza mataji haya kulingana na matakwa ya Yehova; sio kwamba Yehova aliwapa mataji haya moja kwa moja). Pia walivalia majoho ya ukuhani waliyopewa na Yehova na kumhudumia moja kwa moja hekaluni kutoka asubuhi hadi usiku wakiwa pekupeku. Huduma yao kwa Yehova haikuwa ya ovyo ovyo hata kidogo, na haikuhusisha kuharakisha huku na kule bila kufikiria; badala yake, yote ilifanywa kulingana na sheria ambazo hazingekiukwa na yeyote aliyemhudumia moja kwa moja. Wote walilazimika kufuata kanuni hizi; vinginevyo, wangepigwa marufuku kuingia hekaluni. Iwapo yeyote kati yao angevunja sheria za hekalu—yaani, iwapo yeyote angeasi amri za Yehova—basi ingebidi mtu huyo atendewe kulingana na sheria ambazo Alikuwa ametoa, na hakuna mtu aliyeruhusiwa kupinga jambo hili ama kumlinda huyo mvunja sheria. Bila kujali walikuwa wamemhudumia Mungu kwa miaka mingapi, wote walihitajika kufuata sheria. Kwa sababu hii, makuhani wengi sana walivalia majoho ya ukuhani na kumhudumia Yehova bila kusita kwa njia hii mwaka mzima, hata ingawa hakuwa Amewatendea kwa njia yoyote ya kipekee. Hata waliishi maisha yao yote mbele ya madhabahu na hekaluni. Hili lilikuwa onyesho la uaminifu na utii wao. Si ajabu kwamba Yehova aliwapa baraka kama hizo; ilikuwa ni kwa sababu tu ya uaminifu wao ndipo walipokea fadhila na kuyaona matendo yote ya Yehova. Wakati huo, Yehova alipofanya kazi huko Israeli kati ya wateule Wake, aliwatolea madai makali sana. Wote walikuwa watiifu sana na wakazuiliwa na sheria hizi; sheria hizi zilitumika kulinda uwezo wao wa kumcha Yehova. Hizi zote zilikuwa amri za utawala za Yehova. Iwapo kuhani yeyote kati yao hakuishika Sabato ama kukiuka amri za Yehova, na iwapo angegunduliwa na watu wa kawaida, basi mtu huyo angebebwa mara moja hadi mbele ya madhabahu na kupigwa mawe hadi afe. Maiti hizo hazikuruhusiwa kuwekwa ndani ama karibu na hekalu; Yehova hakuruhusu jambo hilo. Yeyote ambaye angefanya hivyo angechukuliwa kuwa mtu aliyetoa “dhabihu zenye kukufuru,” na angerushwa ndani ya shimo kubwa na kuuawa. Bila shaka, watu wote kama hao wangepoteza maisha yao; hakuna yeyote ambaye angesamehewa. Hata kuna wale ambao walitoa “moto wenye kukufuru”: yaani, watu ambao hawakutoa dhabihu katika siku zilizotengwa na Yehova wangechomwa na moto Wake pamoja na vitu vyao vya kutolewa dhabihu, ambavyo havikuruhusiwa kubaki kwenye madhabahu. Matakwa yaliyotolewa kwa makuhani yalikuwa kama ifuatavyo: Hawakuruhusiwa kuingia hekaluni, ama hata kwenye uwanja wake wa nje bila kuosha miguu yao kwanza; wangeingia hekaluni tu iwapo wangekuwa wamevalia majoho yao ya ukuhani; wangeingia hekaluni tu iwapo wangekuwa wamejitwika mataji yao ya ukuhani; hawangeingia hekaluni iwapo wangekuwa wamechafuliwa na maiti; hawangeingia hekaluni baada ya kugusa mkono wa mtu dhalimu, isipokuwa kama wangenawa mikono yao kwanza; na hawangeingia hekaluni baada ya kujitia unajisi na wanawake (kwa miezi mitatu, si milele), wala hawakuruhusiwa kuuona uso wa Yehova. Muda ulipopita—kumaanisha kwamba baada ya miezi mitatu tu ndipo wangeruhusiwa kuvalia majoho masafi ya ukuhani—kisha walilazimika kuhudumu katika uwanja wa nje kwa siku saba kabla ya kuweza kuingia hekaluni ili kuuona uso wa Yehova. Waliruhusiwa kuvalia haya mavazi yoyote ya ukuhani ndani ya hekalu tu, wala si nje kamwe, ili kuepuka kulinajisi hekalu la Yehova. Iliwabidi wale wote ambao walikuwa makuhani kuwaleta wahalifu ambao walikuwa wamekiuka sheria za Yehova mbele ya madhabahu Yake, ambapo wangeuawa na watu wa kawaida; vinginevyo, moto ungemteketeza kuhani ambaye alikuwa ameshuhudia uhalifu huo. Kwa hivyo, walikuwa waaminifu daima kwa Yehova, kwa sababu sheria Zake zilikuwa kali sana kwao, na kamwe hawangethubutu hata kidogo kukiuka amri Zake za utawala kiholela. Waisraeli walikuwa waaminifu kwa Yehova kwa sababu walikuwa wameuona mwale Wake, na walikuwa wameuona mkono Alioutumia kuwaadibu watu, na pia kwa sababu mwanzoni walikuwa wamemcha sana. Kwa hivyo, walichokipata hakikuwa tu mwale wa Yehova, bali utunzaji, ulinzi na baraka Zake. Uaminifu wao ulikuwa kwamba walifuata maneno ya Yehova katika matendo yao yote, na hakuna mtu aliyeasi. Iwapo uasi wowote ungetokea, wale wengine bado wangetekeleza maneno ya Yehova, wakimuua yeyote aliyempinga Yehova, na kutomficha mtu huyo kutoka kwa Yehova hata kidogo. Wale walioikiuka Sabato, waliokuwa na hatia ya uzinzi, na wale walioiba dhabihu zilizotolewa kwa Yehova wangeadhibiwa vikali hasa. Wale walioikiuka Sabato walipigwa mawe hadi wakafa na wao (watu wa kawaida), ama walipigwa mijeledi hadi kufa, bila yeyote kusamehewa. Wale wote waliotenda uzinzi—hata wale waliotamani wanawake warembo ama walioibua fikira za uasherati baada ya kuwaona wanawake waovu, ama walioshikwa na tamaa walipowaona wanawake vijana—wote wangeuawa. Iwapo mwanamke yeyote kijana ambaye hakujifunika ama kuvalia shela angemshawishi mwanaume kufanya kitendo haramu, mwanamke huyo angeuawa. Ikiwa mwanamume huyo aliyekiuka sheria za aina hii alikuwa kuhani (mtu aliyehudumu hekaluni), angesulubiwa ama kunyongwa. Hakuna mtu kama huyo angeruhusiwa kuishi, na hakuna hata mmoja kati yao angefadhiliwa na Yehova. Jamaa za mtu kama huyu hawangeruhusiwa kumtolea Yehova dhabihu mbele za madhabahu kwa miaka mitatu baada ya kifo chake, wala hawangeruhusiwa kushiriki katika dhabihu ambazo Yehova aliwapa watu wa kawaida. Wangeweza kuweka ng’ombe ama kondoo wa hali ya juu kwenye madhabahu ya Yehova baada tu ya muda huo kuisha. Iwapo makosa mengine yangetendwa, iliwabidi wafunge kwa siku tatu mbele za Yehova, wakiomba neema Yake. Hawakumwabudu Yehova kwa sababu tu sheria Zake zilikuwa kali sana na za shuruti sana; walifanya hivyo kwa sababu ya neema Yake na uaminifu wao Kwake. Kwa hivyo, hadi leo, wameendelea kuwa waaminifu vivyo hivyo katika huduma yao, na hawajawahi kulegeza maombi waliyotoa mbele za Yehova. Siku hizi, Waisraeli bado wanapokea utunzaji na ulinzi Wake, na Yeye bado ndiye neema kati yao, inayowafuata siku zote. Wote wanajua jinsi wanavyopaswa kumcha Yehova, na jinsi wanavyopaswa kumhudumia, na wote wanajua jinsi wanavyopaswa kutenda ili wapokee utunzaji na ulinzi Wake; hii ni kwa sababu wote wanamcha mioyoni mwao. Siri ya mafanikio ya huduma yao yote ni uchaji tu. Kwa hivyo, nyote mko vipi siku hizi? Je, mna mfanano wowote na Waisraeli? Je, unafikiri kwamba kuhudumu siku hizi ni sawa na kufuata uongozi wa mtu mkuu wa kiroho? Hamna uaminifu ama uchaji wowote kabisa. Mnapokea neema nyingi, na mnalingana na makuhani wa Israeli kwa kuwa ninyi nyote mnamhudumia Mungu moja kwa moja. Ingawa hamwingii hekaluni, yale mnayopata na yale mnayoyaona ni mengi zaidi kuliko yale ambayo makuhani waliomhudumia Yehova hekaluni walipokea. Hata hivyo, mnaasi na kupinga mara nyingi zaidi kuliko walivyofanya. Uchaji wenu ni mdogo sana, na kwa hivyo, mnapokea neema kidogo sana. Ingawa mnatoa kidogo sana, mmepokea mengi zaidi kuliko yale ambayo Waisraeli hao waliwahi kupokea. Je, katika haya yote, hamjatendewa kwa ukarimu? Wakati ambapo kazi huko Israeli ilikuwa ikifanyika, watu hawakuthubutu kumhukumu Yehova jinsi walivyotaka. Na kuwahusu ninyi, je? Insingekuwa kwa ajili ya kazi ambayo Ninaifanya sasa ili kuwashinda, Ningewezaje kuvumilia ninyi kuliaibisha jina Langu kwa ukatili sana hivi? Iwapo enzi mnayoishi ingekuwa Enzi ya Sheria, basi kwa kuzingatia maneno na matendo yenu, hakuna hata mmoja wenu angeendelea kuishi. Uchaji wenu ni mdogo sana! Daima mnanilaumu kwa kutowapa fadhila nyingi, na hata mnadai kwamba Siwapi maneno ya kutosha ya baraka, na kwamba Ninawalaani tu. Je, hamjui kwamba kwa kunicha kwa kiasi kidogo hivyo haiwezekani kwenu kukubali baraka Zangu? Je, hamjui kwamba Ninawalaani na kuwahukumu daima kwa sababu ya huduma yenu duni? Je, ninyi nyote mnahisi kwamba mmekosewa? Je, Ninawezaje kulipa baraka Zangu kundi la watu ambao ni waasi na wasiotii? Je, Nawezaje kuwapa neema Yangu kiholela watu wanaolifedhehesha jina Langu? Tayari mmetendewa kwa wema mwingi sana. Waisraeli wangelikuwa waasi kama mlivyo leo, Ningeliwaangamiza kitambo. Hata hivyo, Ninawatendea kwa huruma tu. Je, huu si ukarimu? Je, mnataka baraka nyingi zaidi kuliko hizi? Yehova huwabariki tu wale wanaomcha. Yeye huwaadibu watu wanaomwasi, Asimsamehe hata mmoja wao. Je, ninyi watu wa leo, msiojua jinsi ya kuhudumu, hamhitaji kuadibiwa na kuhukumiwa zaidi, ili mioyo yenu iweze kugeuzwa kabisa? Je, kuadibu na hukumu za aina hii si baraka bora kabisa kuwapa? Je, hizo si ulinzi wenu bora kabisa? Bila hizo, kuna yeyote kati yenu ambaye angeweza kuvumilia moto uchomao wa Yehova? Iwapo kweli mngeweza kuhudumu kwa uaminifu kama Waisraeli, je, pia hamngekuwa na neema kama mwandani wenu wa daima? Je, hamngekuwa na furaha na fadhila ya kutosha kila mara? Je, ninyi nyote mnajua jinsi mnavyopaswa kuhudumu?

Matakwa mnayohitaji kutimiza leo—kufanya kazi pamoja kwa upatanifu—ni sawa na huduma ambayo Yehova alitaka kutoka kwa Waisraeli: Vinginevyo, acheni tu kufanya huduma. Kwa sababu ninyi ni watu wanaomhudumia Mungu moja kwa moja, angalau lazima muweze kuwa waaminifu na watiifu katika huduma yenu, na pia lazima muweze kupata mafunzo kwa njia ya utendaji. Kwa wale kati yenu wanaofanya kazi kanisani hasa, je, kuna yeyote kati ya akina ndugu walio chini yenu anayeweza kuthubutu kuwashughulikia? Je, mtu yeyote anaweza kuthubutu kuwaambia makosa yenu ana kwa ana? Mko juu ya wengine wote, mnatawala kama wafalme! Hata hamchunguzi ama kuingia katika mafunzo ya utendaji ya aina hii, lakini bado mnazungumza kuhusu kumhudumia Mungu! Kwa sasa, unaombwa uyaongoze makanisa kadhaa, lakini hukosi tu kujitolea, bali hata unashikilia mawazo na maoni yako mwenyewe, ukisema mambo kama, “Nadhani suala hili linapaswa kutendwa kwa namna hii, kwa kuwa Mungu amesema kwamba hatupaswi kuzuiliwa na wengine na kwamba siku hizi hatupaswi kutii bila kufikiria.” Kwa hivyo, kila mmoja wenu anashikilia maoni yake mwenyewe, na hakuna anayemtii mwenzake. Ingawa unajua vyema kwamba huduma yako ina shida kubwa, bado unasema, “Jinsi nionavyo, njia yangu ni sahihi kiasi. Haidhuru, kila mmoja wetu ana upande wake: Wewe zungumzia upande wako, nami nitazungumzia upande wangu; wewe shiriki kuhusu maono yako, nami nitazungumzia kuingia kwangu.” Kamwe huwajibikii mambo mengi ambayo yanapaswa kushughulikiwa, ama unaridhika tu, kila mmoja wenu akijadili maoni yake mwenyewe na kuilinda hadhi, sifa na heshima yake mwenyewe kwa uangalifu. Hakuna yeyote kati yenu aliye tayari kujinyenyekeza, na hakuna atakayechukua hatua ya kwanza kujitolea na kufidiana kasoro zenu ili maisha yasonge mbele upesi zaidi. Mnaposhirikiana pamoja, mnapaswa kujifunza kuutafuta ukweli. Unaweza kusema, “Sielewi vyema kuhusu kipengele hiki cha ukweli. Je, una uzoefu upi kuuhusu?” Ama unaweza kusema, “Una uzoefu mwingi kuniliko kuhusu kipengele hiki; tafadhali unaweza kuniongoza kiasi?” Je, hiyo haitakuwa njia nzuri ya kulitatua? Mmesikiliza mahubiri mengi, na mna uzoefu kiasi kuhusu kufanya huduma. Msipojifunza kutoka kwa kila mmoja, msaidiane, na kufidiana dosari zenu mnapofanya kazi makanisani, basi mnawezaje kupata mafunzo yoyote? Wakati wowote mnapokabiliwa na chochote, mnapaswa kufanya ushirika ninyi kwa ninyi ili maisha yenu yaweze kufaidika. Aidha, mnapaswa kufanya ushirika kwa makini kuhusu mambo ya aina yoyote kabla kufanya maamuzi yoyote. Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo mnawajibikia kanisa badala ya kutenda kwa uzembe tu. Baada ya kutembelea makanisa yote, mnapaswa kukusanyika pamoja na kushiriki kuhusu masuala yote mnayogundua na matatizo yoyote mliyokumbana nayo katika kazi yenu, na kisha mnapaswa kuwasiliana kuhusu nuru na mwangaza ambao mmepokea—huu ni utendaji wa msingi wa huduma. Lazima mfanikishe ushirikiano wa upatanifu kwa ajili ya kazi ya Mungu, kwa manufaa ya kanisa, na ili muwahimize ndugu zenu mbele. Mnapaswa kushirikiana, kila mmoja akimrekebisha mwenzake na kufikia matokeo bora ya kazi, ili kuyatunza mapenzi ya Mungu. Hii ndiyo maana ya ushirikiano wa kweli, na ni wale tu wanaoshiriki katika ushirikiano huo ndio watakaopata kuingia kwa kweli. Mnaposhirikiana, baadhi ya maneno mnayozungumza yanaweza kuwa yasiyofaa, lakini hilo si muhimu. Shirikini kulihusu baadaye, na mlielewe vyema; msilipuuze. Baada ya ushirika wa aina hii, mnaweza kufidia kasoro za ndugu zenu. Ni kwa kusonga kwa kina daima katika kazi yenu kwa namna hii ndipo mnaweza kupata matokeo bora. Kama watu wanaomhudumia Mungu, kila mmoja wenu lazima aweze kulinda maslahi ya kanisa katika kila kitu mnachofanya, badala ya kuzingatia tu masilahi yenu wenyewe. Haikubaliki ninyi kutenda kila mtu peke yake, daima mkidhoofishana. Watu wanaotenda kwa namna hiyo hawafai kumhudumia Mungu! Watu kama hao wana tabia mbaya sana; hawana ubinadamu hata kidogo ndani yao. Wao ni Shetani asilimia mia moja! Wao ni wanyama! Hata sasa, mambo kama haya bado hutokea miongoni mwenu; hata mnafika kiasi cha kushambuliana wakati wa ushirika; mkitafuta visingizio kwa makusudi na kughadhabika sana mnapogombana kuhusu suala fulani lisilo la maana, pasiwe na mtu aliye radhi kujiweka kando, kila mtu akimfichia mwenzake fikira zake za ndani, akimtazama yule mwingine kwa makini na kuwa mwangalifu daima. Je, tabia ya aina hii inafaa katika kumhudumia Mungu? Je, kazi kama hiyo yako inaweza kuwapa ndugu zako chochote? Huwezi tu kuwaongoza watu kwenye njia sahihi ya maisha, lakini kwa kweli unawajaza ndugu zako tabia zako potovu. Je, huwadhuru wengine? Dhamiri yako ni mbaya na ni mbovu kabisa! Huingii katika uhalisi, wala huuweki ukweli katika vitendo. Aidha, unawafichulia wengine asili yako mbaya mno bila aibu. Huna aibu hata kidogo! Umeaminiwa ndugu hawa, lakini unawapeleka kuzimuni. Je, wewe si mtu ambaye dhamiri yake imekuwa mbovu? Huna aibu hata kidogo!

Iliyotangulia: Utendaji (8)

Inayofuata: Kuboresha Ubora wa Tabia ni Kwa Ajili ya Kupokea Wokovu wa Mungu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp