Hatimaye Naelewa Maana ya Kutimiza Wajibu Wangu

24/01/2021

Na Xunqiu, Korea ya Kusini

Mwenyezi Mungu anasema, “Mwanadamu kufanya wajibu wake ni, kwa uhakika, kutimiza yote yaliyo ya asili yake, yaani, yale yawezekanayo kwa mwanadamu. Hapo ndipo wajibu wake hutimizika. Dosari za mwanadamu wakati wa huduma ya mwanadamu hupunguzwa taratibu kupitia kwa uzoefu uongezekao na mchakato wa uzoefu wake wa hukumu; hayazuii au kuathiri wajibu wa mwanadamu. Wanaoacha kutoa huduma au kuzalisha na kurudi nyuma kwa kuogopa makosa yanayoweza kuwepo katika huduma ndio waoga zaidi miongoni mwa wanadamu wote. Ikiwa mwanadamu haonyeshi anachopaswa kuonyesha wakati wa kutoa huduma au kutimiza kile kilicho katika uwezo wake kiasili, na badala yake huzembea na kufanya tu bila ari yoyote, atakuwa amepoteza majukumu yake ambayo kiumbe anapaswa kuwa nayo. Mwanadamu kama huyu anachukuliwa kuwa mtu hafifu na duni apotezaye nafasi; itakuaje kwamba mtu kama huyu aitwe kiumbe? Je, hao si ni vyombo vya upotovu ving’aavyo kwa nje ila vimeoza kwa ndani?(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Tofauti Kati ya Huduma ya Mungu Mwenye Mwili na Wajibu wa Mwanadamu).

Maneno ya Mungu yamenisaidia kuelewa maana ya kweli ya kufanya wajibu wetu. Inamaanisha kuwa bila kujali tulivyo na talanta au vipaji, hatuna budi kutumia kikamilifu kila kitu tunachoelewa. Hatuwezi kutumia njia za mkato au kufanya tu mambo kwa namna isiyo ya dhati. Lazima tuendelee kujitahidi kulingana na kile ambacho Mungu anataka. Kwa njia hiyo, tutaweza kufidia udhaifu au kasoro zozote katika utendaji wa wajibu wetu na tutazidi kupata matokeo bora.

Hivi majuzi, kanisa lilitaka kupiga picha za video fulani za solo za maneno ya Mungu. Kiongozi wa timu yetu alitaka niongoze na nicheze gita katika wimbo mmoja. Aliponiambia juu ya hili, nilifadhaika kidogo. Kuimba na kucheza gita ni vigumu zaidi kuliko kuimba pekee. Aidha, nilikuwa nimejaribu kuimba hivyo peke yangu hapo awali, lakini nilipokuwa nikiimba nilizingatia utendaji wangu na nikakosea katika kordi zangu, lakini nilipozingatia kordi, nilikosea katika maonyesho yangu. Mwishowe, hawakuweza kutumia video hiyo. Nilipokabiliwa na kazi hiyo hiyo, nilitaka kukataa, lakini niliona kwamba kufanya hivyo hakukupatana na mapenzi ya Mungu. Ndugu zangu wote walidhani kwamba nilistahili kuimba wimbo huo, kwa hivyo nilidhani kwamba nilipaswa kukubaliana na hilo na kufanya wajibu wangu. Kwa hivyo, nilikubali wajibu huo. Baada ya kufanya mazoezi kwa siku mbili, nilielewa sehemu za uimbaji na utendaji vizuri sana. Lakini ilikuwa vigumu kukumbuka kordi za gita na zilitatanisha sana. Ikiwa imesalia siku moja tu kabla ya kupiga picha za video, nilipatwa na wasiwasi sana. Niliogopa kwamba wakati wa kufanya mazoezi ulikuwa umeisha, na iwapo ningeendelea kufanya mazoezi, je, mikono yangu isingevimba? Bila kutilia maanani usumbufu, labda hata sitakumbuka hayo. Baada ya kufikiria hayo, sikutaka kulipa gharama, kwa hivyo niliendelea kujaribu kufikiria suluhisho kamili la tatizo hili gumu. Wakati huo ndipo nilipopata wazo fulani: Naweza kumsihi mpiga picha asipige mikono yangu picha nyingi sana, kisha sitahitaji kujitahidi kujua kordi hizi zinazokera, siyo? Na bado tutaweza kupiga picha za video. Hilo lilionekana kama wazo zuri. Kwa kweli, nilipatwa na wasiwasi kidogo nilipopata wazo hili. Nilihisi kana kwamba sikuwa mwenye kuaminika. Itakuwa vipi iwapo kutakuwa na tatizo la kordi na tulazimike kurudia kupiga picha za video? Lakini nikawaza baadaye: “Hakuna muda wa kutosha na wimbo huu ni mgumu sana. Kucheza wimbo huu vizuri kutaelemea na kutafadhaisha sana. Siwezi kutenda kuzidi kiwango changu. Mbali na hilo, sababu ni ili tuweze kutoa video hii haraka iwezekanavyo. Kila mtu anapaswa kuelewa.” Baada ya hapo, nililenga uimbaji na utendaji wangu bila kuona wasiwasi sana juu ya kordi. Nilidhani kwamba hilo lilipaswa kutosha.

Wakati wa kupiga picha za filamu ulipowadia, nilimsihi ndugu aliyekuwa akipiga picha asipige mikono yangu picha nyingi za karibu. Sikufikiri kwamba kungekuwa na tatizo lolote. Lakini siku iliyofuata, mwelekezi alisema kwamba nilikuwa nikicheza vibaya baadhi ya kordi na akaniuliza kilichokuwa kikiendelea. Nilihisi hatia sana na nikashikwa na aibu. Niliwaza, “Lo! Itabidi tupige picha tena?” Nilikurupuka kumuuliza mhariri iwapo kulikuwa na suluhisho lingine. Alitikisa kichwa tu na kusema, “Nilijaribu, si nzuri.” Niliposikia hayo, nilijua kwamba hatukuwa na budi kurudia kupiga picha za video. Nilihisi vibaya kwa kuwa nilijua kwamba nilikuwa nimesababisha tatizo hilo. Baadaye, tulipokutana ili kujadili kilichokuwa kimetokea, nilimwambia kila mtu sababu zangu za kufanya kile nilichokuwa nimefanya. Dada mmoja alinisuta, akisema, “Kwa nini hukutuambia kwamba hukuwa umejifunza kordi? Sasa hatuna budi kupiga tena picha na mradi wote umecheleweshwa. Hukujali wala kuwa mwenye kuwajibika!” Sikuweza kabisa kukubali yale aliyosema. Niliwaza, “Je, sikufanya vizuri kadiri nilivyoweza? Ukweli ni kwamba siwezi kucheza kordi hizo, na nilizicheza ili kuhakikisha kuwa video ilikamilika haraka. Hawakupaswa kabisa kupiga picha mikono yangu, siyo?” Nilitoa visingizio tu bila kutafakari juu yangu mwenyewe. Lakini baadaye dada mwingine aliniambia, “Kama ulikuwa na tatizo, ungefanya mazoezi zaidi hata kama upigaji picha ungeahirishwa kwa siku chache. Lakini huwezi tu kumaliza mambo kwa kubahatisha kwa namna hiyo. Wewe ni mwimbaji anayeongoza—itakuwa vipi tusipoonyesha ukicheza gita? Hukujali wala kuwajibika hata kidogo!” Kumsikia akisema “hata kidogo” kwa namna hiyo, kulinifadhaisha sana. Sikuweza kujizuia kuwaza, “Iwapo ndugu zangu wote wanafikiri kwamba mimi ni mzembe katika wajibu wangu, je, pengine nimekosea kwa kweli? Nilitaka upigaji picha za video uende vizuri pia. Lakini hata hivyo, mradi umecheleshwa na lazima turudie kupiga picha za video kwa sababu kordi zangu hazikuwa sawa. Bila shaka, mimi ndimi wa kulaumiwa.” Nilihisi vibaya nilipofikiria hilo. Niliacha kulalamika na nikaanza kutafakari.

Kilisema hivi: “Je, matokeo ya kutekeleza wajibu wako kwa haraka na kijuujuu na kutouchukulia kwa makini ni nini? Ni utendaji duni wa wajibu wako, ingawa una uwezo wa kuufanya vizuri—utendaji wako hautafikia kiwango kinachotakiwa na Mungu hataridhishwa na mtazamo wako kwa wajibu wako. Kama hapo mwanzoni, ungetafuta na kushirikiana kwa kawaida; kama ungetumia mawazo yako yote; iwapo ungejizatiti na kutia juhudi zako zote katika kuufanya, na iwapo ungetumia bidii yako, jitihada zako, na mawazo yako kuufanya, au ungetumia marejeo zaidi, na kutumia akili yako yote na mwili wako wote kuufanya; kama ungekuwa na uwezo wa kushirikiana kwa njia hii, basi Mungu angetangulia na kukuongoza. Huhitaji kutumia nguvu nyingi; ukifanya kila kitu uwezacho kushirikiana, Mungu tayari atakuwa Amekupangia kila kitu. Iwapo wewe ni mjanja na mwongo, na ubadilishe mawazo yako na upotoke unapokuwa ukifanya kazi, basi Mungu hatavutiwa nawe; utakuwa umepoteza fursa hii, na Mungu atasema, ‘Wewe si hodari kiasi cha kutosha; wewe ni bure. Nenda upande ule. Unapenda kuwa mvivu, siyo? Unapenda kuwa mdanganyifu na mjanja, siyo? Unapenda kupumzika? Haya basi, pumzika.’ Mungu atampa mtu mwingine neema na fursa hii. Je, mnasemaje: Hii ni hasara au ushindi? Ni hasara kubwa!(“Jinsi ya Kusuluhisha Shida ya Kuwa Mvivu na Mzembe Wakati wa Kutekeleza Wajibu Wako” katika Kumbukumbu za Hotuba za Kristo). Maneno ya Mungu yalifichua hali yangu mwenyewe. Nilikuwa nimekubali kufanya mazoezi ili kufanya wajibu wa kuongoza, lakini kwa kweli sikufanya kile nilichoahidi. Sikushughulikia udhaifu wangu au kutafuta habari ili kuboresha kordi zangu. Nilizembea wakati wa mazoezi kwa sababu nilidhani kwamba yatakuwa magumu sana. Nilitoa kisingizio kwamba sikuwa na wakati na nikamtaka mpiga picha aepuke kuipiga mikono yangu picha za karibu. Nilidhani kwamba ningefaulu bila kugunduliwa, lakini hilo liliishia kuchelewesha mradi. Kwa kweli sikujali wala kuaminika! Wajibu wangu ulipojitokeza, sikutaka kujitahidi kucheza wimbo huo vizuri wala kumshuhudia Mungu. Badala yake, nilitumia mbinu rahisi zaidi, na sasa tulilazimika kurudia kila kitu. Je, niliwezaje kutoaminika vile? Kama tu ningefanya mazoezi zaidi kidogo, kama ningejitahidi zaidi kidogo, nisingeidhuru kazi ya nyumba ya Mungu. Nilijichukia kidogo wakati huo. Niliwaza, “Nikipata nafasi nyingine, sitakuwa mzembe sana tena. Hata kama nitalazimika kujichosha nitakapokuwa nikijizoeza kordi hizo, nitafanya kile kinachohitajika kufanywa.”

Wengine waliamua kunipa siku nyingine mbili za kufanya mazoezi. Hilo lilinigusa sana na nilimshukuru Mungu kwa kunipa nafasi ya kufidia kosa langu. Katika mazoezi yangu baada ya hayo, nilijitahidi kukariri kordi zote, lakini nilifadhaika sana. Niliogopa kwamba mbinu yangu haikuwa imefikia kiwango kilichotakiwa na kwamba siku mbili hazikutosha kuiboresha. Nilianza kupata wasiwasi tena. Lakini kadiri nilivyozidi kuwa na wasiwasi, ndivyo nilivyozidi kusahau, na kadiri nilivyozidi kusahau, ndivyo nilivyozidi kuwa na wasiwasi. Muda ulipita haraka asubuhi hiyo. Bado sikuweza kucheza wimbo huo vizuri sana, na mikono yangu ilikuwa na maumivu. Kwa kawaida, nilipumzika baada ya chakula cha mchana, lakini wakati huu, nilijua kwamba sikuwa na budi kuendelea. Nilijua kwamba sikupaswa kupumzika bali ilibidi nitumie kila wakati niliokuwa nao kuelewa kordi vizuri. Mara niliporekebisha mawazo yangu, Mungu aliniongoza. Alasiri hiyo, nilijua jinsi ya kukariri kordi katika mafungu baada ya muda mfupi sana! Nilizidi kufanya vizuri. Lakini nilikuwa nimefanya mazoezi kwa muda mrefu sana kiasi kwamba mikono yangu ilianza kuvimba na nilitamani kuzembea tena. Nilipogundua kwamba nilikuwa nikifikiri kwa namna hii tena, nilikumbuka jambo ambalo Mungu alikuwa Amesema na nikakurupuka kulisoma: “Unapokabiliwa na wajibu ambao unahitaji juhudi yako na kujitumia kwako, na ambao unahitaji utoe mwili, mawazo na wakati wako, sharti usisite, usifiche ujanja wako mdogo au kujipa uhuru wowote wa kufanya matendo tofauti. Iwapo utajipa uhuru wa kufanya matendo tofauti, iwapo wewe ni mlaghai au mjanja na mdanganyifu, basi huna budi kufanya kazi duni. Unaweza kusema, ‘Hakuna aliyeniona nikitenda kwa ujanja. Vyema!’ Je, hii ni fikira ya aina gani? Unadhani kwamba umewahadaa watu na kumhadaa Mungu pia. Kwa kweli, je, Mungu anajua kile ambacho umefanya au la? (Anajua.) Kwa ujumla, watu wanaoingiliana nawe kwa muda mrefu watagundua pia na watasema kwamba wewe ni mtu ambaye hulaghai kila wakati, mtu asiyetia bidii kamwe, na ambaye hujitahidi tu kwa asilimia hamsini au sitini au themanini sanasana. Watasema kwamba wewe hufanya kila kitu kwa namna ya shaghalabaghala, ukipuuza chochote unachofanya; wewe si mwangalifu hata kidogo katika kazi yako. Ukilazimishwa kufanya jambo, basi wakati huo tu ndipo unapotia bidii kidogo; kama kuna mtu anayeangalia iwapo kazi yako imefikia kiwango kinachotakiwa, wakati huo unafanya kazi nzuri zaidi—lakini iwapo hapana mtu wa kuangalia, unazembea kidogo. Ukishughulikiwa, basi unajitahidi; vinginevyo, unasinzia kila wakati kazini na kujaribu kukwepa lawama kadiri uwezavyo, ukidhani kuwa hakuna atakayegundua. Muda unapita, na watu wanagundua. Wanasema, ‘Mtu huyu si wa kutegemewa wala kuaminika; ukimpa wajibu fulani muhimu autekeleze, atahitaji kusimamiwa. Anaweza kufanya kazi za kawaida na kazi ambazo hazihusishi kanuni, lakini ukimpa wajibu wowote muhimu autimize, atauvuruga tu, kisha utakuwa umehadaiwa.’ Watu watambaini kabisa, na atakuwa amepoteza kabisa heshima na uadilifu. Iwapo hakuna mtu anayeweza kumwamini, basi Mungu anawezaje kumwamini? Je, Mungu anaweza kumwaminia kazi yoyote muhimu? Mtu kama huyo haaminiki(“Uingiaji Katika Uzima Lazima Uanze na Uzoefu wa Kutenda Wajibu wa Mtu” katika Kumbukumbu za Hotuba za Kristo). Maneno ya Mungu yalinifanya nigundue jinsi nilivyokuwa mzembe sana katika wajibu wangu. Sikujizoeza kordi kwa bidii sana, na sikuwa nikifikia kiwango cha juu zaidi. Sikuwa nikifanya jitihada kikamilifu. Nilikuwa nikimaliza wajibu wangu kwa kubahatisha na pasipo kujali. Sikuwa na uadilifu. Sikuwa mwaminifu. Nilijiona kila mara kama mtu mwenye shauku na mwenye bidii katika wajibu wangu na kwamba nilikuwa na uaminifu usioisha. Lakini sasa, niliona kwamba sikuwa nimelenga matokeo, bali nilikuwa nimemaliza mambo kwa kubahatisha tu. Je, huko kulikuwaje kufanya wajibu wangu? Kama ningeendelea hivyo, ni nani ambaye angethubutu kuniamini tena? Je, sikuwa nikipoteza uaminifu na heshima yangu? Nilikuwa nimefanya dhambi wakati uliopita. Sikutaka kuirudia. Sikujali iwapo mikono yangu ilivimba au iwapo nilichoka, maadili na heshima yangu ilikuwa ya maana zaidi. Kwa hivyo, niliamua kuendelea kufanya mazoezi ya kordi bila kujali jinsi yalivyonichosha au kuwa magumu. Mara nilipoazimia kutubu kwa kweli, niliona baraka na mwongozo wa Mungu. Siku hiyo hiyo, nilifanya mazoezi hadi usiku wa manane, na nikaweza kukariri karibu kordi zote. Siku iliyofuata, nilifanya mazoezi siku nzima hadi nikajua wimbo wote. Wakati wa upigaji picha za video, nilizingatia kila hatua kwa makini na niliomba kimyakimya na kumtegemea Mungu. Ajabu ni kwamba, tulipiga picha za video nzima kwa zamu moja! Nilipoona mambo yalivyokuwa bora mwishowe, nilihisi amani. Nilionja utamu wa kutenda ukweli.

Baadaye, nilipewa wajibu wa kutunga muziki. Sikuwa nimetunga wimbo kwa muda mrefu, kwa hivyo sikuwa stadi sana. Hasa, tulikuwa tukitunga nyimbo za roki hivi karibuni, ambazo sikuwa nimezitunga hapo awali, kwa hivyo nilikuwa na wasiwasi kidogo. Lakini nilijua kwamba huu ulikuwa wajibu ambao nilihitaji kutimiza na sikuwa na budi kufanya vyema kadiri nilivyoweza. Kwa hivyo, nilifanya mpango wa kukamilisha nyimbo mbili kufikia mwisho wa mwezi. Nilifanya kazi hadi saa za ziada nikitunga nyimbo na nilipochoka, nilimwomba Mungu anisaidie kuukana mwili. Nilipata lahani fulani kwa bahati na nikaigeuza upesi iwe wimbo kamili. Nilipoumliza, niliwaambia kina ndugu zangu wausikilize. Walisema kwamba wimbo huo ulikuwa sawa na kwamba ulikuwa na mtindo sahihi wa muziki wa roki. Lakini niliwaza moyoni: “Nikifanya kazi zaidi na nilainishe sauti ya kiitikio, wimbo huu utakuwa bora zaidi.” Lakini nilibadili mawazo baada ya kufikiria upya. Sikuwa na mwelekeo bayana wakati huo na sikudai mengi kutoka kwangu. Mbali na hilo, ndugu zangu hawakuuonea mashaka. Ulikuwa mzuri kiasi cha kutosha. Aidha, nilikuwa nimejifunza jinsi ya kutunga wimbo wa aina hii karibuni, kwa hivyo ilikuwa kawaida kwa wimbo huo kuwa na dosari. Niliuwasilisha kwa kiongozi wa timu.

Siku chache baadaye, aliniambia kwamba nilitunga wimbo jinsi ilivyofaa, lakini lahani haikuwa nzuri sana. Alipendekeza nifikiri zaidi kidogo kuhusu maneno ya wimbo huo. Nilihisi mwenye ukinzani na nikawaza, “Nimejifunza kutunga wimbo wa aina hii kwa muda mfupi tu. Unadai mengi sana kutokwa kwangu!” Tayari nilikuwa nimetumia muda mwingi kuutunga na siku chache zaidi zikapita huku nikisubiri maoni yake. Nusu ya mwezi tayari ilikuwa imepita. Nilipoona kwamba hakukuwa na maendeleo, nilipata wasiwasi kidogo. Kusahihisha wimbo huo kungechukua juhudi nyingi na sikujua ungeishia kuwa vipi. Kwa hivyo, nilitunga lahani upya. Kiongozi wa timu alisema kwamba wimbo huo ulikosa lahani na ulikuwa kama wimbo wa watoto. Nilivunjika moyo sana. Niliwaza, “Nimejitahidi sana lakini hamna hata wimbo mmoja ambao umekubaliwa. Napaswa kufanya nini?” Baadaye, nilitunga lahani nyingine chache, lakini hakuna hata moja iliyokubaliwa. Nilikanganyikiwa sana. Nilifikiria juu ya jinsi nilivyokuwa nimeamua kutunga nyimbo mbili kufikia mwisho wa mwezi, lakini sikuwa nimemaliza hata mmoja. Nilikuwa nimeshindwa kutimiza wajibu wangu. Je, nilikuwa bure?

Nilipokuwa katika mkutano mmoja baadaye, kiongozi wa timu alinikumbusha, “Nyimbo zako ni za ajabu sana na zina mitindo mizuri, hivyo kwa nini bado hakuna hata wimbo mmoja ambao umekubaliwa? Huzingatii maneno ya wimbo, kwa hivyo maneno na lahani havifaani. Kila unapobaidilisha, wimbo unazidi kuwa mbaya. Hili linachelewesha kazi ya nyumba ya Mungu.” Halafu, ndugu mwingine akaingilia mazungumzo hayo: “Huimbi vizuri unaporekodi wimbo. Baadhi ya lahani hazilingani na noti zilizoandikwa. Wewe ni mzembe!” Kushughulikiwa na kukaripiwa na kina ndugu kulinifedhehesha. Nilitamani ardhi ipasuke niingie ndani. Nilipofika nyumbani, nilimwomba Mungu: “Mungu, nimekuwa mzembe katika wajibu wangu. Sijatia bidii, lakini sijui jinsi ya kutatua tatizo hili. Tafadhali nisaidie na Uniongoze.”

Baadaye, nilisoma maneno haya ya Mungu: “Je, kushughulikia mambo kwa mzaha na pasipo uaminifu si jambo lililo ndani ya tabia potovu? Jambo lipi? Ni uovu; katika masuala yote, wao husema ‘hiyo imekaribia kuwa sawa’ na ‘imekaribia kutosha’; ni mtazamo wa ‘pengine,’ ‘labda,’ na ‘nne kati ya tano’; wao hufanya mambo kwa uzembe, wao huridhishwa na kufanya kazi ya kiwango cha chini zaidi na wanaridhishwa na kubananga mambo kadiri wawezavyo; hawaoni sababu ya kuchukulia mambo kwa makini au kujitahidi kufikia usahihi na hawaoni sababu ya kutafuta kanuni. Je, hili si jambo lililo ndani ya tabia potovu? Je, ni dhihirisho la ubinadamu wa kawaida? Kuliita kiburi ni sahihi, na kuliita upotovu pia kunafaa kabisa—lakini ili kulieleza kikamilifu, neno pekee ambalo litaeleza vizuri ni ‘uovu.’ Uovu kama huu upo katika ubinadamu wa watu wengi sana; katika mambo yote, wao hutaka kujitahidi kwa kiasi kidogo kabisa kadiri iwezekanavyo, ili waone jinsi wanavyoweza kufanikiwa bila kugunduliwa, na kuna kidokezo cha udanganyifu katika kila kitu wanachofanya. Wao huwadanganya wengine wanapoweza, wao hutumia njia za mkato wanapoweza na huchukia kutumia muda mwingi au mawazo kufikiri kuhusu jambo. Almradi waweze kukwepa kufichuliwa, na wasisababishe matatizo yoyote, na wasiitwe wajieleze, wao hufikiri kwamba mambo yote ni mazuri, na hivyo wao husonga mbele kwa kubahatisha. Kwao, kufanya kazi vizuri kunasumbua zaidi kuliko jinsi inavyostahili. Watu kama hawa hawajifunzi lolote hadi wawe stadi na hawatii bidii katika masomo yao. Wao hutaka tu kupata muhtasari wa jumla wa mada fulani na kisha hujiita stadi wa mada hiyo, na kisha wao hutegemea hili kumaliza kazi zao kwa kubahatisha. Je, huu sio mtazamo ambao watu wanao kwa mambo? Je, ni matazamo mzuri? Mtazamo wa aina hii ambao watu kama hao huwa nao kwa watu, matukio na mambo, kwa maneno machache, ni, ‘kumaliza mambo kwa kubahatisha’, na uovu kama huu upo ndani ya wanadamu wote wapotovu.” “Mtu anawezaje kutofautisha kati ya watu waadilifu na waovu? Angalia tu mtazamo wao na jinsi wanavyochukulia watu, matukio, na mambo—angalia jinsi wanavyotenda, jinsi wanavyoshughulikia mambo na jinsi wanavyotenda matatizo yanapotokea. Watu wenye unyoofu na hadhi ni waangalifu sana, wamakinifu na wenye bidii katika matendo yao na wako tayari kujitolea. Watu ambao hawana unyoofu na hadhi ni vigeugeu katika vitendo vyao na hutenda ovyovyo, na wao kila wakati huwa na hila fulani, wakitaka tu kumaliza mambo kwa kubahatisha kila mara. Hawajifunzi ustadi wowote, na bila kujali wanasoma kwa muda gani, wao husalia wakiwa wamekanganywa na ujinga katika masuala ya ustadi au taaluma. Usiposisitiza wakupe majibu, mambo yote huonekana kuwa sawa, lakini, mara unapofanya hivyo, wao hushikwa na hofu—nyuso zao hulowa kwa jasho, na wao hukosa jibu. Hao ni watu wenye tabia duni(Kumbukumbu za Hotuba za Kristo). Niliposoma maneno haya tu ndipo nilipogundua kwamba nilikuwa mzembe katika wajibu wangu, kwa sababu kulikuwa na kitu kilichokengeuka ndani yangu. Nilitaka kutia juhudi kidogo kadiri iwezekanavyo katika kila kitu bila kujali ubora wa kazi yangu. Sikutaka kutafuta kanuni za ukweli wala kutekeleza wajibu wangu kama Mungu anavyotaka. Ninapofikiria wakati huu, iwapo ilikuwa upigaji picha za video au kutunga wimbo, kila nilipokabiliwa na tatizo lililohitaji bidii, kila nilipohitaji kulipa gharama, niliridhishwa na kujitahidi kwa kiasi kidogo sana. Sikujaribu kufanya vizuri zaidi au kujitahidi zaidi. Kwa kweli, nilijua kwamba iwapo ningefanya kazi kwa bidii na kwa makini zaidi, ningefanya wajibu wangu vizuri zaidi. Lakini nilitia juhudi kiasi kidogo mno na kujifurahisha kila wakati. Kwa hivyo sikuweza kusonga mbele katika kazi yangu au kumshuhudia Mungu kupitia kazi yangu, na kama matokeo, niliendelea kuchelewesha kazi ya kanisa. Niliwezaje kusema nilikuwa nimefanya wajibu wangu? Hakika nilikuwa nikizuia kazi ya nyumba ya Mungu. Wakati huo ndipo nilipoona jinsi nilivyokuwa mtu duni kabisa. Nilimaliza mambo kwa kubahatisha, sikujitahidi na nilijaribu kumdanganya Mungu. Sikuwa na unyoofu wala hadhi. Mungu huwapenda wale ambao hufanya wajibu wao kwa uaminifu na bidii, ambao hutafuta kanuni za ukweli wanapokabiliwa na matatizo na kutimiza wajibu wao kama Mungu anavyotaka. Wana heshima na uadilifu, na wanathaminiwa sana machoni pa Mungu. Nikilinganishwa nao, sikustahili kuitwa binadamu. Nilihisi aibu. Wakati huo, nilielewa: Mungu alikuwa Akiniokoa kupitia akina ndugu zangu kunipogoa na kunishughulikia. Vinginevyo, ningekuwa nikimaliza mambo kwa kubahatisha kwa njia hii kila wakati. Nisingefanya kazi yangu vizuri. Ningevuruga kazi ya nyumba ya Mungu na kufukuzwa na Mungu.

Nilisoma maneno mengi zaidi ya Mungu: “Kazi ya Mungu ni kwa ajili ya wanadamu, na ushirika wa mwanadamu ni kwa minajili ya usimamizi wa Mungu. Baada ya Mungu kufanya yale yote Anayopaswa kufanya, mwanadamu anapaswa kufanya vitendo bila kukoma, na kushirikiana na Mungu. Mwanadamu hapaswi kulegeza kamba katika kazi ya Mungu, lazima aonyeshe uaminifu na asijitie katika mawazo mengi au kukaa akisubiri kifo bila kufanya kitu. Mungu Mwenyewe anaweza kujitolea kwa mwanadamu, basi ni kwa nini mwanadamu asiweze kuwa mwaminifu kwa Mungu? Mawazo na moyo wa Mungu vipo kwa mwanadamu, basi ni kwa nini mwanadamu asijitolee katika ushirika? Mungu huwafanyia wanadamu kazi, basi ni kwa nini mwanadamu asifanye wajibu wake kwa minajili ya usimamizi wa Mungu? Kazi ya Mungu imefika umbali huu, bado mnaona ila hutendi, mnasikia ila hamsogei. Je, si watu kama hawa wanafaa kuangamizwa kabisa? Tayari Mungu amejitolea kikamilifu kwa ajili ya mwanadamu, basi ni kwa nini siku hizi mwanadamu hafanyi wajibu wake kwa dhati? Kwa Mungu, kazi Yake ni ya kipaumbele Kwake, na kazi ya usimamizi Wake ni ya umuhimu wa hali ya juu. Kwa mwanadamu, kuweka maneno ya Mungu katika vitendo na kutimiza mahitaji ya Mungu ndiyo kipaumbele kwake. Ni lazima nyote myafahamu haya(Neno, Vol. 1. Kuonekana na Kazi ya Mungu. Kazi ya Mungu na Utendaji wa Mwanadamu). Niliguswa sana nilipoyafikiria tena maneno ya Mungu. Mungu ana moyo mmoja na nia moja kwa mwanadamu. Amepata mwili mara mbili ili kuwaokoa binadamu ambao wamepotoshwa na Shetani. Ameaibishwa, Amekataliwa na vizazi na Amepata mateso mengi mno. Licha ya Mungu kukabiliwa na upotovu wetu mkubwa na kutojali kwetu, Yeye hajawahi kutuacha. Bado Yeye huonyesha ukweli ili kutuokoa. Ubora wetu wa tabia ni duni na sisi si wepesi wa kukubali ukweli, lakini Mungu hushiriki pamoja nasi kwa dhati na kwa bidii sana. Wakati mwingine Yeye hutumia sitiari na mifano na Yeye hutuambia hadithi ili kutuongoza kutoka kila sehemu na kwa kila njia. Yeye hufanya hivi ili tuweze kuelewa ukweli na kuingia ndani ya ukweli. Mungu huwajibikia maisha yetu na Hatapumzika hadi Atakapotukamilisha. Kuona tabia ya Mungu na nia Zake za dhati kulinitia msukumo sana. Lakini nilipofikiria jinsi ambavyo nilikuwa nimemtendea Mungu na jinsi nilivyokuwa nimechukulia wajibu wangu, nilijuta sana. Sikutaka tena kumaliza wajibu wangu kwa kubahatisha. Nilikwenda mbele za Mungu na kuomba, nikimuuliza jinsi ambavyo ningeweza kuacha kuwa mzembe na kutekeleza wajibu wangu vizuri. Kisha nikasoma maneno ya Mungu, ambayo yalisema: “Wajibu ni nini? Ni agizo lililoaminiwa kwa watu na Mungu. Hivyo unapaswaje kutimiza wajibu wako? Kwa kutenda kwa mujibu wa matakwa na viwango vya Mungu, na kutegemeza tabia yako kwa kanuni za ukweli badala ya matamanio ya dhahania ya binadamu. Kwa njia hii, wewe kutimiza wajibu wako kutakuwa kumefikia kiwango kinachohitajika(“Ni kwa Kutafuta Kanuni za Ukweli Tu Ndiyo Mtu Anaweza Kutekeleza Wajibu Wake Vizuri” katika Kumbukumbu za Hotuba za Kristo). “Kuuchukulia kwa uzito kunamaanisha nini? Kuuchukua kwa uzito hakumaanishi kutia bidii kidogo au kuteseka kimwili kwa kiasi. Kilicho muhimu ni kwamba kuna Mungu moyoni mwako, na mzigo. Lazima uzingatie umuhimu wa wajibu wako moyoni mwako, na kisha ubebe mzigo huu na jukumu lako katika yote unayoyatenda na kujitahidi kadiri uwezavyo katika kuutekeleza. Lazima ustahili misheni ambayo Mungu amekupa, na vile vile kila kitu ambacho Mungu amekufanyia, na matarajio Yake kwa ajili yako. Kufanya hivyo tu ndiyo kuchukulia mambo kwa uzito. Hakuna haja ya wewe kufanya mambo kwa namna isiyo ya dhati; unaweza kuwadanganya watu, lakini huwezi kumdanganya Mungu. Ikiwa hakuna gharama halisi na uaminifu wakati unapotekeleza wajibu wako, basi haitoshelezi kiwango(Kumbukumbu za Hotuba za Kristo).

Maneno haya yalinifanya nielewe waziwazi. Mungu hutuaminia wajibu wetu. Lazima tufanye kama Anavyotaka na tutende kulingana na ukweli. Hatuwezi kuchagua au kufuata tamaa zetu wenyewe bila kufikiri. Lazima tufikie kiwango fulani katika wajibu wetu—kuonekana tu kufanya kazi kwa bidii hakutaleta mafanikio. Jambo la muhimu ni kuwajibika, kuwa wenye bidii na ari, kutafuta, kutafakari, na kutafuta njia za kufanya vizuri zaidi. Kisha, tutaweza kufanya wajibu wetu na kumpendeza Mungu. Baadaye, nilipokuwa nikitunga wimbo, nilichambua maneno ya wimbo huo kwa uangalifu, na nikapata nyimbo chache zilizolingana na tuni ya maneno hayo. Nilifikiria sana jinsi watu wengine walivyotumia lahani kuonyesha hisia zile zile, na juu ya maana ya maneno ya wimbo huo, tuni, na mweleko wa lahani. Baada ya kufahamu yote hayo, nilianza kutunga. Niliomba ushauri wa kina ndugu zangu baadaye, nikasahihisha wimbo huo mara mbili na kisha ukawa tayari. Nilimaliza baada ya wiki moja tu. Wimbo mwingine niliousahihisha pia ulikubaliwa. Ninaona kwamba kufanya wajibu wetu kwa makini kulingana na kanuni za ukweli hutupa baraka na mwongozo wa Mungu. Nilipoona jinsi ilivyochukua muda kidogo kumaliza kutunga nyimbo hizo, nilihisi majuto na masikitiko hata zaidi kwa ajili ya kujaribu kumaliza wajibu wangu kwa kubahatisha hapo awali. Niliona jinsi nilivyokuwa nimepotoshwa sana na Shetani, jinsi nilivyokuwa duni sana na jinsi nilivyokuwa mzembe katika kazi yangu. Kwa msaada wa mipango ya Mungu na kina ndugu kunishughulikia, naweza hatimaye kutafuta ukweli ili kutatua tabia zangu potovu na kutekeleza wajibu wangu kwa bidii. Shukrani kwa Mungu!

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Maudhui Yanayohusiana

Ukombozi wa Moyo

Na Zheng Xin, Marekani Mnamo Oktoba ya 2016, mimi na mume wangu tulikubali kazi ya Mungu katika siku za mwisho wakati tulikuwa ughaibuni....

Leave a Reply

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp