Maono ya Kazi ya Mungu (1)
Yohana alimfanyia Yesu kazi kwa miaka saba, na alikuwa tayari ameandaa njia Yesu Alipowasili. Kabla ya haya, injili ya ufalme wa mbinguni kama ilivyohubiriwa na Yohana ilisikika kote nchini, ilienea kote Yudea, na kila mtu alimwita nabii. Wakati huo, Mfalme Herode alitaka kumuua Yohana, lakini hakuthubutu, kwa maana watu walimheshimu Yohana sana, na Herode aliogopa kwamba kama angemuua Yohana wangeasi dhidi yake. Kazi iliyofanywa na Yohana ilikita mizizi miongoni mwa watu wa kawaida, na Wayahudi wote walishawishika na yeye. Kwa miaka saba aliandaa njia kwa ajili ya Yesu, hadi wakati ambapo Yesu alianza kutekeleza huduma Yake. Kwa sababu hii, Yohana alikuwa mkuu zaidi kati ya manabii wote. Ilikuwa tu baada ya Yohana kufungwa gerezani ndipo Yesu Alianza kazi Yake rasmi. Kabla ya Yohana, hakukuwa kamwe na nabii aliyemwandalia Mungu njia, kwa sababu kabla ya Yesu, Mungu alikuwa hajawahi kupata mwili. Kwa hivyo, kati ya manabii wote hadi wakati wa Yohana, yeye ndiye aliyekuwa wa pekee kumwandalia njia Mungu mwenye mwili, na kwa namna hii, Yohana akawa nabii mkuu zaidi wa Agano la Kale na Jipya. Yohana alianza kuhubiri injili ya ufalme wa mbinguni kwa upana miaka saba kabla ya ubatizo wa Yesu. Kwa watu, kazi aliyofanya ilionekana kuzidi kazi iliyofuata ya Yesu, lakini yeye, hata hivyo, bado alikuwa tu nabii. Hakufanya kazi na kuzungumza ndani ya hekalu, bali katika miji na vijiji nje ya hekalu. Bila shaka, alifanya hili miongoni mwa watu wa Kiyahudi, hasa wale waliokuwa maskini. Ilikuwa nadra sana kwa Yohana kutangamana na watu kutoka matabaka ya juu ya jamii, na alihubiri injili kwa upana tu miongoni mwa watu wa kawaida wa Yudea ili kuandaa watu wanaofaa kwa ajili ya Bwana Yesu, na kuandaa maeneo yanayofaa kwa ajili Yake kufanyia kazi. Kukiwa na nabii kama Yohana wa kuandaa njia, Bwana Yesu aliweza kuanza moja kwa moja njia Yake ya msalaba mara tu Alipowasili. Mungu alipopata mwili kufanya kazi Yake, Hakulazimika kufanya kazi ya kuwachagua watu, wala Hakuhitaji binafsi kuwatafuta watu, au mahali pa kufanyia kazi. Hakufanya kazi kama hiyo Alipokuja; mtu aliyefaa alikuwa tayari amemwandalia mambo kama hayo kabla ya Yeye kuwasili. Yohana alikuwa tayari amekamilisha kazi hii kabla ya Yesu kuanza kazi Yake, kwa maana Mungu mwenye mwili Alipowasili kufanya kazi Yake, Alianza moja kwa moja kufanya kazi ndani ya wale ambao walikuwa wamemngoja kwa muda mrefu. Yesu hakuwa amekuja kufanya kazi ya mwanadamu ya kurekebisha. Alikuwa amekuja tu kutekeleza huduma ambayo ilikuwa Yake kutekeleza; kila kitu kingine hakikuwa na uhusiano na Yeye. Yohana alipokuja, hakufanya chochote ila kuleta kutoka hekaluni na miongoni mwa Wayahudi kundi la wale waliokubali injili ya ufalme wa mbinguni, ili waweze kuwa walengwa wa kazi ya Bwana Yesu. Yohana alifanya kazi kwa miaka saba, yaani alihubiri injili kwa miaka saba. Wakati wa kazi yake, Yohana hakufanya ishara nyingi, kwa maana kazi yake ilikuwa kuandaa njia; kazi yake ilikuwa kazi ya maandalizi. Kazi nyingine yote, kazi ambayo Yesu alikuwa anaenda kufanya, haikuhusiana na yeye kabisa; aliwaambia tu watu wakiri dhambi zao na watubu, na akawabatiza, ili waweze kuokolewa. Ingawa alifanya kazi mpya na kufungua njia ambayo mwanadamu alikuwa hajawahi kuitembea hapo awali, bado alimwandalia tu Yesu njia. Alikuwa tu nabii aliyefanya kazi ya maandalizi, na hakuwa na uwezo wa kufanya kazi ya Yesu. Ingawa Yesu hakuwa wa kwanza kuhubiri injili ya ufalme wa mbinguni, na ingawa Aliendelea kwenye njia ambayo Yohana alikuwa ameanza kuitembea, bado hakukuwa na mtu mwingine ambaye angeweza kufanya kazi Yake, na ilizidi kazi ya Yohana. Yesu hakuweza kuandaa njia Yake mwenyewe; kazi Yake ilitekelezwa moja kwa moja kwa niaba ya Mungu. Na hivyo, haijalishi Yohana alifanya kazi kwa miaka mingapi, bado alikuwa nabii, na bado alikuwa yule aliyeandaa njia. Miaka mitatu ya kazi iliyofanywa na Yesu ilizidi miaka saba ya kazi ya Yohana, kwa maana kiini cha kazi Yake hakikuwa sawa na cha Yohana. Yesu alipoanza kutekeleza huduma Yake, ambao pia ulikuwa wakati kazi ya Yohana ilipofika mwisho, Yohana alikuwa ameandaa watu na maeneo ya kutosha kwa matumizi ya Bwana Yesu, kiasi cha kumtosha Bwana Yesu kutekeleza miaka mitatu ya kazi. Na hivyo, mara tu kazi ya Yohana ilipokamilika, Bwana Yesu alianza kazi Yake mwenyewe rasmi, na maneno yaliyozungumzwa na Yohana yalibatilishwa. Hiyo ni kwa sababu kazi iliyofanywa na Yohana ilikuwa tu kwa ajili ya mpito, na maneno yake hayakuwa maneno ya uzima ambayo yangemwongoza mwanadamu kwenye ukuaji mpya; maneno yake, baada ya yote, yalikuwa ya matumizi ya muda tu.
Kazi aliyofanya Yesu haikuwa ya kimiujiza; kulikuwa na mchakato kuihusu, na yote yaliendelea kulingana na sheria za kawaida za mambo. Kufikia miezi sita ya mwisho ya maisha Yake, Yesu alijua kwamba kwa kweli alikuwa amekuja kufanya kazi hii, na Alijua kwamba Alikuwa amekuja kupigiliwa misumari msalabani. Kabla ya kusulubiwa Kwake, Yesu aliomba kwa Mungu Baba mfululizo, kwa mfano, maombi Yake matatu katika Bustani ya Gethsemane. Baada ya kubatizwa, Yesu alitekeleza huduma Yake kwa miaka mitatu na nusu, na kazi Yake rasmi ilidumu kwa miaka miwili na nusu. Katika mwaka wa kwanza, Alishtakiwa na Shetani, akasumbuliwa na mwanadamu, na akapitia vishawishi vya mwanadamu. Alishinda vishawishi vingi Alipotekeleza kazi Yake. Katika miezi sita ya mwisho, wakati Yesu alipokuwa karibu kusulubiwa, kutoka kinywani mwa Petro yalitoka maneno kwamba Yeye alikuwa Mwana wa Mungu aliye hai, kwamba Yeye alikuwa Kristo. Ni hapo tu ndipo kazi Yake ilipojulikana kwa mwanadamu, na ni hapo tu ndipo utambulisho Wake ulipofichuliwa kwa umma. Baadaye, Yesu aliwaambia wanafunzi Wake kwamba alipaswa kusulubiwa kwa ajili ya mwanadamu, kwamba siku tatu baadaye Angefufuka tena, kwamba Alikuwa amekuja kutekeleza kazi ya ukombozi, na kwamba Yeye alikuwa Mwokozi. Ni katika miezi sita ya mwisho tu ndipo alipofichua utambulisho Wake na kazi aliyokusudia kufanya. Huu pia ulikuwa wakati wa Mungu, na hivi ndivyo kazi ilivyopaswa kutekelezwa. Wakati huo, sehemu ya kazi ya Yesu ilikuwa kulingana na Agano la Kale, pamoja na maneno ya Yehova wakati wa Enzi ya Sheria na sheria za Musa. Mambo haya yote, Yesu aliyatumia kufanya sehemu ya kazi Yake. Aliwahubiria watu na kuwafundisha katika masinagogi, na Alitumia unabii wa manabii katika Agano la Kale kuwakemea Mafarisayo waliokuwa na uhasama na Yeye, na akatumia maneno kutoka katika Maandiko kufichua uasi wao na hivyo kuwahukumu. Kwa maana walichukia kile ambacho Yesu alikuwa amefanya; hasa, sehemu kubwa ya kazi ya Yesu haikufanywa kulingana na sheria katika Maandiko, na, zaidi ya hayo, kile Alichofundisha kilikuwa juu kuliko maneno yao wenyewe, na hata juu kuliko kile ambacho kilikuwa kimetabiriwa na manabii katika Maandiko. Kazi ya Yesu ilikuwa tu kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu na kwa ajili ya kusulubiwa, na hivyo hakukuwa na haja ya Yeye kusema maneno zaidi ili kumshinda mwanadamu yeyote. Mengi ya yale Aliyomfundisha mwanadamu yalitoka katika maneno ya Maandiko, na hata kama kazi Yake haikuzidi Maandiko, bado Aliweza kukamilisha kazi ya kusulubiwa. Kazi Yake haikuwa kazi ya neno, wala kazi iliyofanywa kwa ajili ya kuwashinda binadamu, bali kazi iliyofanywa ili kuwakomboa binadamu. Alikuwa tu sadaka ya dhambi kwa ajili ya binadamu, na hakuwa chanzo cha neno kwa ajili ya binadamu. Hakufanya kazi ya Mataifa, ambayo ilikuwa kazi ya kumshinda mwanadamu, bali kazi ya kusulubiwa, kazi ambayo ilifanywa miongoni mwa wale walioamini kwamba kuna Mungu. Hata ingawa kazi Yake ilitekelezwa juu ya msingi wa Maandiko, na hata ingawa Alitumia kile ambacho kilikuwa kimetabiriwa na manabii wa kale kuwahukumu Mafarisayo, hii ilitosha kukamilisha kazi ya kusulubiwa. Ikiwa kazi ya leo bado ingetekelezwa juu ya msingi wa unabii wa manabii wa kale katika Maandiko, basi isingewezekana kuwashinda ninyi, kwa maana Agano la Kale halina rekodi ya uasi na dhambi zenu ninyi watu wa China, na hakuna historia ya dhambi zenu. Kwa hivyo, ikiwa kazi hii bado ingesalia katika Biblia, ninyi hamngejisalimisha kamwe. Biblia inarekodi tu historia yenye ukomo ya Waisraeli, ambayo haina uwezo wa kuthibitisha kama ninyi ni waovu au wema, au wa kuwahukumu ninyi. Fikirieni kwamba Ningewahukumu ninyi kulingana na historia ya Waisraeli—je, bado mngenifuata kama mnavyofanya leo? Je, mnajua jinsi mlivyo wagumu? Kusingekuwa na maneno ambayo yamezungumzwa wakati wa hatua hii, basi isingewezekana kukamilisha kazi ya ushindi. Kwa sababu Sijakuja kupigiliwa misumari msalabani, lazima Ninene maneno yaliyo nje ya Biblia, ili mweze kushindwa. Kazi iliyofanywa na Yesu ilikuwa tu hatua ya juu kuliko Agano la Kale; ilitumika kuanzisha enzi, na kuongoza enzi hiyo. Kwa nini Alisema, “Sikuja kuiharibu sheria, bali kuitimiza sheria”? Lakini katika kazi Yake kulikuwa na mengi yaliyotofautiana na sheria zilizotendwa na amri zilizofuatwa na Waisraeli wa Agano la Kale, kwa maana Hakuja kuitii sheria, bali kuitimiza. Mchakato wa kuitimiza ulijumuisha mambo mengi ya vitendo: Kazi Yake ilikuwa ya vitendo na halisi zaidi, na, zaidi ya hayo, ilikuwa hai zaidi, na haikuwa ufuasi mkali wa kanuni. Je, Waisraeli hawakushika Sabato? Yesu alipokuja, hakuishika Sabato, kwa maana Alisema kwamba Mwana wa Adamu alikuwa Bwana wa Sabato, na Bwana wa Sabato alipowasili, Angefanya jinsi Apendavyo. Alikuwa amekuja kutimiza sheria za Agano la Kale na kubadilisha sheria. Yote yanayofanywa leo yanategemea wakati wa sasa, lakini bado yanategemea msingi wa kazi ya Yehova katika Enzi ya Sheria, na hayakiuki upeo huu. Kuchunga ulimi wako, na kutozini, kwa mfano—je, hizi si sheria za Agano la Kale? Leo, kile kinachohitajika kwenu hakikomei tu kwa Amri Kumi, bali kinajumuisha amri na sheria za utaratibu wa juu zaidi kuliko zile zilizotangulia. Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba kile kilichotangulia kimefutwa, kwa maana kila hatua ya kazi ya Mungu inatekelezwa juu ya msingi wa hatua iliyotangulia. Kuhusu kazi ambayo Yehova alifanya wakati huo katika Israeli, kama vile kuwataka watu watoe dhabihu, kuwaheshimu wazazi wao, kutoabudu sanamu, kutowapiga au kuwalaani wengine, kutozini, kutovuta sigara au kunywa pombe, na kutokula vitu vilivyokufa au kunywa damu—je, hii haiundi msingi wa utendaji wenu hata leo? Ni juu ya msingi wa wakati uliopita ndiyo kazi imetekelezwa hadi leo. Ingawa sheria za wakati uliopita hazitajwi tena na matakwa mapya yamefanywa kwako, sheria hizi, mbali na kutofutwa, badala yake zimeinuliwa juu zaidi. Kusema kwamba zimefutwa kunamaanisha kwamba enzi iliyopita imepitwa na wakati, ilhali kuna amri fulani ambazo lazima uziheshimu kwa umilele wote. Amri za wakati uliopita tayari zimewekwa katika vitendo, tayari zimekuwa kile mwanadamu alicho, na hakuna haja ya kusisitiza kwa namna maalum juu ya amri kama vile “Usivute sigara,” “Usinywe pombe,” na kadhalika. Juu ya msingi huu, amri mpya zinawekwa kulingana na mahitaji yenu leo, kulingana na kimo chenu, na kulingana na kazi ya leo. Kutoa amri kwa ajili ya enzi mpya hakumaanishi kufuta amri za enzi ya zamani, bali ni kuziinua juu zaidi juu ya msingi huu, ili kufanya matendo ya mwanadamu kuwa kamili zaidi, na ya vitendo zaidi. Ikiwa, leo, mngetakiwa tu kufuata amri na kutii sheria za Agano la Kale, na kutenda kwa namna sawa na Waisraeli, na ikiwa mngetakiwa hata kukariri sheria zilizowekwa na Yehova, isingewezekana kwamba mngeweza kubadilika. Ikiwa mngetii tu amri hizo chache zenye ukomo au kukariri sheria zisizohesabika, tabia yenu ya zamani ingebaki imejikita sana, na isingewezekana kuing’oa. Hivyo mngekuwa wapotovu zaidi na zaidi, na hakuna hata mmoja wenu ambaye angekuwa mtiifu. Yaani, amri chache rahisi au sheria zisizohesabika hazina uwezo wa kuwasaidia kujua matendo ya Yehova. Ninyi si sawa na Waisraeli: Kwa kufuata tu sheria na kukariri amri, waliweza kushuhudia matendo ya Yehova na kumpa uaminifu wao Yeye pekee. Lakini ninyi hamwezi kabisa kufikia hili, na amri chache za enzi ya Agano la Kale si tu kwamba hazina uwezo wa kuwafanya mtoe mioyo yenu, au kuwalinda, bali badala yake zitawafanya mlegee, na zitawafanya mwanguke Kuzimu. Kwa maana kazi Yangu ni kazi ya ushindi, na inalenga uasi wenu na tabia yenu ya zamani. Maneno ya fadhila ya Yehova na Yesu hayawezi kuyafikia maneno makali ya hukumu ya leo. Bila maneno makali kama hayo, isingewezekana kuwashinda ninyi “wataalamu,” ambao mmekuwa waasi kwa maelfu ya miaka. Sheria za Agano la Kale zilipoteza nguvu zao juu yenu kitambo sana, na hukumu ya leo ni ya kutisha zaidi kuliko sheria za wakati huo. Kile kinachowafaa zaidi ninyi ni hukumu, na si vizuizi vidogo vya sheria, kwa maana ninyi si binadamu wa mwanzo kabisa, bali ni binadamu ambao wamekuwa wapotovu kwa maelfu ya miaka. Kile ambacho mwanadamu anahitajika kufikia sasa kinategemea hali halisi ya mwanadamu leo, kulingana na ubora wa tabia na kimo halisi cha binadamu leo, na huambiwi ufuate kanuni. Hili ni ili mabadiliko yaweze kufikiwa katika tabia yako ya zamani, na ili uweze kutupilia mbali dhana zako. Je, unafikiri amri ni kanuni? Inaweza kusemwa kuwa ni matakwa ya kawaida kwa mwanadamu. Si kanuni ambazo lazima ufuate. Chukulia kutokuruhusu kuvuta sigara, kwa mfano—je, hiyo ni kanuni? Si kanuni! Ni jambo linalohitajika na ubinadamu wa kawaida; si kanuni, bali ni kitu kilichowekwa kwa ajili ya binadamu wote. Leo, amri kumi na mbili au zaidi ambazo zimewekwa pia si kanuni; ni kile kinachotakiwa ili kufikia ubinadamu wa kawaida. Watu hawakuwa na mambo kama hayo au kuyajua zamani, na hivyo watu wanatakiwa kuyafikia leo, na mambo kama hayo hayahesabiwi kama kanuni. Sheria haziwakilishi kanuni. Kanuni Ninazozungumzia zinarejelea ibada, taratibu au matendo yaliyopotoka ya mwanadamu; ni itifaki ambazo hazina msaada kwa mwanadamu. Kanuni hizi hazina faida kwa mwanadamu; ni mienendo ambayo haina maana. Hiki ndicho kifano halisi cha kanuni, na kanuni kama hizo lazima zifutwe, kwa maana hazitoi faida yoyote kwa mwanadamu; ilhali, kile ambacho kina faida kwa mwanadamu lazima kitiwe katika vitendo.