Wale Wanaompenda Mungu Wataishi Milele Ndani ya Nuru Yake
Kiini cha imani ya watu wengi katika Mungu ni kusadiki sana kidini: Hawawezi kumpenda Mungu na wanamfuata Mungu tu kama roboti, hawawezi kumtamani sana Mungu kwa kweli au kumpenda sana. Wanamfuata Yeye kimyakimya tu. Watu wengi wanamwamini Mungu, lakini kuna wachache sana wanaompenda Mungu; wao “humwogopa” Mungu tu kwa sababu wanaogopa maafa, vinginevyo wao “humstahi” Mungu kwa sababu Yeye ni mkuu na wa juu—lakini katika hofu na kuvutiwa kwao, hakuna upendo au kutamani kwa kweli. Katika uzoefu wao watu hutafuta maelezo madogo ya ukweli au siri fulani zisizo na maana. Watu wengi hufuata tu, na wao hufanya hivyo tu ili wajinufaishe kwa hila ili wapate baraka, si ili kutafuta ukweli, au kumtii Mungu kwa kweli ili wapokee baraka za Mungu. Maisha ya imani ya watu wote katika Mungu hayana maana, hayana thamani, na ndani yake mna mazingatio na mambo wanayoyafuatilia ya kibinafsi; hawamwamini Mungu ili kumpenda Mungu, bali kwa ajili ya kubarikiwa. Watu wengi hutenda wapendavyo; wao hufanya chochote wanachotaka na hawazingatii kamwe masilahi ya Mungu, au kama kile wanachofanya kinalingana na nia za Mungu. Watu kama hao hawawezi hata kufikia imani ya kweli, sembuse kumpenda Mungu. Kiini cha Mungu si tu kwa ajili ya mwanadamu kumwamini, bali hata zaidi ni kwa ajili ya mwanadamu kumpenda. Lakini wengi wa wale wanaomwamini Mungu hawawezi kugundua “siri” hii. Watu hawathubutu kumpenda Mungu, wala hawajaribu kumpenda Yeye. Hawajawahi kugundua kwamba kuna mengi sana ya kupendeza kumhusu Mungu; hawajawahi kugundua kwamba Mungu ni Mungu anayempenda mwanadamu, na kwamba Yeye ni Mungu ambaye mwanadamu anapaswa kumpenda. Kupendeza kwa Mungu kunaonyeshwa katika kazi Yake: Ni wakati tu wanapopitia kazi Yake ndipo watu wanaweza kugundua kupendeza Kwake; ni katika uhalisi tu ndipo wanaweza kupitia kupendeza kwa Mungu; na bila kupitia na kutazama katika maisha halisi, hakuna anayeweza kugundua kupendeza kwa Mungu. Kuna mengi sana ya kupenda kuhusu Mungu, lakini bila kuhusiana na Yeye kwa kweli watu hawawezi kuyagundua. Yaani, Mungu asingekuwa mwili, watu wasingeweza kuingiliana na Yeye kwa kweli, na kama hawangeweza kuingiliana na Yeye kwa kweli, pia wasingeweza kupitia kazi Yake—na hivyo upendo wao kwa Mungu ungetiwa madoa na uwongo mwingi na mawazo mengi. Upendo wa watu kwa Mungu aliye mbinguni si wa vitendo kama upendo wao kwa Mungu aliye duniani, kwa maana maarifa ya watu juu ya Mungu aliye mbinguni yamejengwa juu ya mawazo yao, badala ya kile ambacho wamekiona kwa macho yao wenyewe na kile ambacho wamekipitia wao binafsi. Mungu anapokuja duniani, watu wanaweza kutazama matendo Yake ya vitendo na kupendeza Kwake, na wanaweza kuona kila kitu cha tabia Yake ya vitendo na ya kawaida, yote ambayo ni ya vitendo mara maelfu zaidi kuliko maarifa yao juu ya Mungu aliye mbinguni. Bila kujali watu wanampenda Mungu aliye mbinguni kiasi gani, hakuna chochote cha vitendo kuhusu upendo huu, na umejaa mawazo ya binadamu. Haijalishi upendo wao kwa Mungu aliye duniani ni mdogo kiasi gani, upendo huu ni wa vitendo; hata kama kuna kiasi kidogo tu cha upendo huo, bado ni wa vitendo. Mungu huwafanya watu wamjue kupitia kazi ya vitendo, na kupitia maarifa haya Yeye hupata upendo wao. Ni kama Petro: Asingeishi na Yesu, isingewezekana kwake kumpenda sana Yesu. Vivyo hivyo, uaminifu wake kwa Yesu ulijengwa juu ya kuhusiana kwake na Yesu. Kwa kuwa Mungu anamtaka mwanadamu ampende, Yeye binafsi amekuja miongoni mwa wanadamu na anaishi pamoja na mwanadamu, na yote Anayomfanya mwanadamu aone na kupitia ni uhalisi wa Mungu.
Mungu hutumia uhalisi na ujio wa ukweli wa mambo kuwafanya watu kuwa watimilifu; maneno ya Mungu hutimiza sehemu ya kufanya Kwake watu kuwa watimilifu, na hii ni kazi ya mwongozo na kufungua njia. Yaani, katika maneno ya Mungu mwanadamu anaweza kupata njia ya kutenda na maarifa ya maono. Kwa kuelewa mambo haya, mwanadamu atakuwa na njia na maono katika utendaji wake halisi, na ataweza kutiwa nuru kupitia maneno ya Mungu; ataweza kuelewa kwamba jambo hilo limetoka kwa Mungu na ataweza kutambua mengi. Baada ya kufahamu, mwanadamu lazima aingie mara moja katika uhalisi huu na lazima atumie maneno ya Mungu kumridhisha Mungu katika maisha yake halisi. Mungu atakuelekeza katika mambo yote na atakupa njia ya kutenda, na kukufanya uhisi kwamba Yeye ni mwenye kupendeza hasa, na kukuruhusu uone kwamba kila hatua ya kazi ya Mungu kwako inakusudiwa kukufanya uwe mtimilifu. Ikiwa ungependa kuona upendo wa Mungu, ikiwa ungependa kupitia kwa kweli upendo wa Mungu, basi lazima uingie ndani kabisa katika uhalisi, lazima uingie ndani kabisa katika maisha halisi na uone kwamba kila kitu Anachofanya Mungu ni upendo na wokovu, kwamba yote Anayofanya ni kuwawezesha watu watupe mbali kile ambacho ni kichafu, na kusafisha mambo yaliyo ndani ya mwanadamu ambayo hayawezi kuridhisha nia za Mungu. Mungu humkimu mwanadamu akitumia maneno; wakati huo huo, Yeye huandaa mazingira ya maisha halisi ili watu wayapitie, na watu wakila na kunywa maneno mengi ya Mungu, basi katika utendaji wao halisi, wanaweza kutatua matatizo yote katika maisha yao wakitumia maneno mengi ya Mungu. Yaani, lazima uwe na maneno ya Mungu ili uingie ndani kabisa katika uhalisi; usipokula na kunywa maneno ya Mungu na uwe bila kazi ya Mungu, basi hutakuwa na njia katika maisha halisi. Ikiwa kamwe huli wala hunywi maneno ya Mungu, basi utachanganyikiwa jambo linapokutendekea. Utajua tu kwamba unapaswa kumpenda Mungu, lakini hutakuwa na uwezo wa utambuzi wowote na hutakuwa na njia ya kutenda; utakanganyika na kuchanganyikiwa, na wakati mwingine hata utaamini kwamba kwa kuuridhisha mwili unamridhisha Mungu. Haya yote ni matokeo ya kutokula na kunywa maneno ya Mungu. Yaani, usipokuwa na msaada wa maneno ya Mungu na unapapasa tu ndani ya uhalisi, basi kimsingi huwezi kupata njia ya kutenda. Watu kama hawa hawaelewi kabisa maana ya kumwamini Mungu, sembuse kuelewa maana ya kumpenda Mungu. Ikiwa, ukitumia nuru na mwongozo wa maneno ya Mungu, wewe mara nyingi unaomba, unapapasa-papasa, unatafuta, unagundua kile unachopaswa kutenda, unapata fursa kwa ajili ya kazi ya Roho Mtakatifu, unashirikiana na Mungu kwa kweli, na hukanganyiki wala huchanganyikiwi, basi utakuwa na njia katika maisha halisi, na utamridhisha Mungu kweli. Unapomridhisha Mungu, ndani yako kutakuwa na mwongozo wa Mungu, na utabarikiwa hasa na Mungu, jambo ambalo litakupa hisia ya kufurahia: Utahisi heshima hasa kwamba umemridhisha Mungu, utahisi mwangaza wa pekee ndani yako, na moyoni mwako utakuwa wazi na utahisi utulivu. Dhamiri yako italiwazwa na kuwa huru kutokana na mashtaka, na utahisi furaha ndani yako unapowaona akina ndugu zako. Hii ndiyo maana ya kufurahia upendo wa Mungu, na huku tu ndiko kumfurahia Mungu kwa kweli. Watu kufurahia upendo wa Mungu kunapatikana kupitia uzoefu: Kwa kupitia mateso, na kupitia kutia ukweli katika vitendo, wanapata baraka za Mungu. Ikiwa unasema tu kwamba Mungu anakupenda kweli, kwamba Mungu amelipa gharama kubwa kweli kwa ajili ya watu, kwamba Yeye kwa subira na kwa dhati amezungumza maneno mengi sana na daima huwaokoa watu, kutamka kwako maneno haya ni upande mmoja tu wa kumfurahia Mungu. Hata hivyo, kufurahia zaidi—kufurahia kwa kweli—ni wakati watu wanapotia ukweli katika vitendo katika maisha yao halisi, ambapo baada ya hapo wanahisi utulivu na uwazi mioyoni mwao. Wanahisi kuguswa sana ndani yao na kuhisi kwamba Mungu ni mzuri hasa. Utahisi kwamba gharama ambayo umelipa inastahili kabisa. Baada ya kutumia damu ya moyo wako, utakuwa na mwanga ung’aao hasa ndani yako: Utahisi kwamba unafurahia upendo wa Mungu kwa kweli na utaelewa kwamba Mungu amefanya kazi ya wokovu kwa watu, kwamba usafishaji Wake kwa watu unakusudiwa kuwatakasa, na kwamba Mungu huwajaribu watu ili kupima kama wanampenda Yeye kwa kweli. Ikiwa daima unatenda ukweli kwa njia hii, basi polepole utakuza maarifa ya wazi ya kazi nyingi ya Mungu, na wakati huo daima utahisi kwamba maneno ya Mungu ni dhahiri kama fuwele mbele yako. Unapofahamu waziwazi ukweli mwingi, utahisi kwamba jambo hili na lile ni rahisi kutia katika vitendo, kwamba unaweza kushinda suala lolote na kushinda kishawishi chochote, na utaona kwamba hakuna kitu kilicho tatizo kwako, jambo ambalo litakuweka huru sana na kukukomboa. Wakati huu, utakuwa unafurahia upendo wa Mungu, na upendo wa kweli wa Mungu utakuwa umekujia. Mungu huwabariki wale walio na maono, walio na ukweli, walio na maarifa, na wanaompenda Yeye kwa kweli. Ikiwa watu wangependa kutazama upendo wa Mungu, lazima watende ukweli katika maisha halisi, lazima wawe tayari kuvumilia uchungu na kutelekeza kile wanachokipenda ili kumridhisha Mungu, na licha ya machozi machoni mwao, lazima bado waweze kuuridhisha moyo wa Mungu. Kwa njia hii, hakika Mungu atakubariki, na ukivumilia ugumu kama huu, utafuatiwa na kazi ya Roho Mtakatifu. Kupitia maisha halisi, na kwa njia ya upitiaji wa maneno ya Mungu, watu wanaweza kuona kupendeza kwa Mungu, na ni ikiwa tu wameonja upendo wa Mungu ndiyo wanaweza kumpenda Yeye kwa kweli.
Wale wanaompenda Mungu ni wale wanaopenda ukweli, na kadiri wale wanaopenda ukweli wanavyoutia katika vitendo, ndivyo wanavyokuwa nao zaidi; kadiri wanavyoutia katika vitendo, ndivyo wanavyokuwa na upendo wa Mungu zaidi; na kadiri wanavyoutia katika vitendo, ndivyo wanavyobarikiwa zaidi na Mungu. Ukitenda daima kwa njia hii, utaweza kuuona upendo wa Mungu juu yako hatua kwa hatua, kama vile Petro alivyokuja kumjua Mungu: Petro alisema kwamba Mungu hana tu hekima ya kuumba mbingu na ardhi na vitu vyote, bali, zaidi ya hayo, kwamba Yeye pia ana hekima ya kufanya kazi ya vitendo kwa watu. Petro alisema kwamba Yeye hastahili tu upendo wa watu kwa sababu ya uumbaji Wake wa mbingu na ardhi na vitu vyote, bali, zaidi ya hayo, kwa sababu ya uwezo Wake wa kumuumba mwanadamu, kumwokoa mwanadamu, kumfanya mwanadamu kuwa mtimilifu, na kumpa mwanadamu upendo Wake. Pia, Petro alisema kwamba kuna mengi ndani Yake ambayo yanastahili upendo wa mwanadamu. Petro alimwambia Yesu, “Je, kuumba mbingu na ardhi na vitu vyote ndiyo sababu pekee inayofanya Ustahili upendo wa watu? Kuna mengi zaidi ndani Yako ambayo ni ya kupendeka. Wewe hutenda na kuenenda katika maisha halisi, Roho Wako hunigusa ndani, Wewe hunitia adabu, Wewe hunikemea—mambo haya yanastahili upendo hata zaidi.” Ikiwa ungependa kuona na kupitia upendo wa Mungu, basi lazima upapase huku na huko na utafute katika maisha halisi na lazima uwe tayari kuuachilia mwili wako mwenyewe. Lazima ufanye azimio hili. Lazima uwe mtu mwenye azimio ambaye anaweza kumridhisha Mungu katika mambo yote, bila kuwa mvivu au kutamani starehe za mwili, si kuishi kwa ajili ya mwili bali kuishi kwa ajili ya Mungu. Pengine humridhishi Mungu wakati huu kwa sababu huelewi nia za Mungu; wakati ujao, hata kama itabidi utie bidii kiasi, lazima umridhishe Yeye na hupaswi kuuridhisha mwili. Unapopitia kwa njia hii, utakuwa umekuja kumjua Mungu. Utaona kwamba Mungu anaweza kuumba mbingu na ardhi na vitu vyote, kwamba Yeye amekuwa mwili ili watu waweze kumwona kwa njia halisi na inayogusika, na kwamba Yeye huhusiana nao kwa njia halisi na inayogusika; utaona kwamba Yeye anaweza kutembea miongoni mwa wanadamu, na kwamba Roho Wake anaweza kuwafanya watu kuwa watimilifu katika maisha halisi; utaona kwamba haya yote yanawaruhusu watu waone kupendeza Kwake na wapitie adabu Yake, kurudi Kwake, na baraka Zake. Daima ukipitia kwa njia hii, katika maisha halisi hutatenganishwa na Mungu, na siku moja uhusiano wako na Mungu ukikoma kuwa wa kawaida, utaweza kupitia shutuma na kuhisi majuto. Unapokuwa na uhusiano wa kawaida na Mungu, hutatamani kamwe kumwacha Mungu, na siku moja Mungu akisema Atakutelekeza, utaogopa, na utasema kwamba afadhali ufe kuliko kutelekezwa na Mungu. Mara tu unapohisi hili, utahisi kwamba huwezi kumwacha Mungu, na kwa njia hii, utakuwa na msingi, na utafurahia upendo wa Mungu kwa kweli.
Watu mara nyingi huzungumza juu ya kumruhusu Mungu awe uzima wao, lakini uzoefu wao bado haujafikia hatua hiyo. Unasema tu kwamba Mungu ni uzima wako, na kwamba Yeye hukuongoza kila siku, na unakula na kunywa maneno Yake kila siku, na unamwomba kila siku, na hivyo Yeye amekuwa uzima wako. Maarifa ya wale wanaosema hivi ni ya kijuujuu sana. Ndani ya watu wengi hakuna msingi; maneno ya Mungu yamepandwa ndani yao, lakini bado hayajaota, sembuse kuzaa matunda yoyote. Leo, umepitia hadi kiwango gani? Sasa tu, baada ya Mungu kukulazimisha kufika hapa, ndipo unahisi kwamba huwezi kumwacha Mungu. Siku moja, uzoefu wako utakapofikia hatua fulani, kama Mungu angekufanya uondoke, hungeweza. Daima utahisi kwamba huwezi kuwa bila Mungu ndani yako; unaweza kuwa bila mume, mke, au watoto, bila familia, bila mama au baba, bila starehe za mwili, lakini huwezi kuwa bila Mungu. Kuwa bila Mungu kutakuwa kama kupoteza uzima wako; hutaweza kuishi bila Mungu. Unapopitia hadi hatua hii, utakuwa umefikia lengo katika imani yako kwa Mungu, na kisha, Mungu atakuwa amekuwa uzima wako, Yeye atakuwa amekuwa msingi wa uwepo wako. Hutaweza kamwe kumwacha Mungu tena. Unapokuwa umepitia hadi kiwango hiki, utakuwa umefurahia upendo wa Mungu kwa kweli, na uhusiano wako na Mungu utakuwa wa karibu hadi kufikia hatua kwamba Yeye atakuwa uzima wako, upendo wako, na wakati huo, utamwomba Mungu na kusema, “Mungu! Siwezi Kukuacha. Wewe ni uzima wangu. Ninaweza kuwa bila kila kitu kingine—lakini bila Wewe, siwezi kuendelea kuishi.” Hiki ndicho kimo cha kweli cha watu; ni uzima halisi. Watu wengine wamelazimishwa kufika hapa walipo leo: Wamelazimika kuendelea mbele wapende wasipende, na daima wamehisi kana kwamba wamekwama kati ya pande mbili ngumu. Lazima upitie kiasi kwamba Mungu ni uzima wako, kiasi kwamba kama Mungu angeondolewa kutoka moyoni mwako, ingekuwa kama kupoteza uzima wako; Mungu lazima awe uzima wako, na lazima uwe huna uwezo wa kumwacha Yeye. Kisha, utakuwa umepata upitiaji wa vitendo wa Mungu kwa kweli, na wakati huu, unapompenda Mungu, utampenda Mungu kwa kweli, na utakuwa upendo wa nia moja, ulio safi. Siku inaweza kuja katika uzoefu wako ambapo uzima wako umefikia hatua fulani ambapo unamwomba Mungu, unakula na kunywa maneno ya Mungu, unashindwa kumwacha Mungu ndani yako, na unashindwa kumsahau Yeye hata kama ungetaka. Mungu atakuwa amekuwa uzima wako; utaweza kuisahau dunia, utaweza kumsahau mke, mume, au watoto wako, lakini utapata shida kumsahau Mungu—kufanya hivyo hakutawezekana. Huu utakuwa uzima wako wa kweli na upendo wako wa kweli kwa Mungu. Upendo wako kwa Mungu unapokuwa umefikia hatua fulani ambapo hauwezi kuzidiwa na upendo wako kwa kitu kingine chochote, na unachukua nafasi ya kwanza, basi utaweza kuacha kila kitu kingine, na kuwa tayari kukubali upogoaji wote kutoka kwa Mungu. Unapofikia upendo kwa Mungu unaozidi kila kitu kingine, utaishi katika uhalisi na katika upendo wa Mungu.
Mara tu Mungu anapokuwa uzima ndani ya watu, watu wanashindwa kumwacha Mungu. Je, hili si tendo la Mungu? Hakuna ushuhuda mkuu zaidi ya huu! Mungu amefanya kazi hadi hatua fulani; Amesema watu watoe huduma, waadibiwe au wafe, na watu hawajarudi nyuma, jambo ambalo linaonyesha kwamba wameshindwa na Mungu. Watu walio na ukweli ni wale ambao, katika upitiaji wao halisi, wanaweza kusimama imara katika ushuhuda wao, kusimama imara katika msimamo wao, kusimama upande wa Mungu, bila kurudi nyuma kamwe, na ambao wanaweza kuwa na uhusiano wa kawaida na watu wanaompenda Mungu, ambao, mambo yanapowatendekea, wanaweza kumtii Mungu kikamilifu, na wanaweza kumtii Mungu hadi kifo. Utendaji na ufunuo wako katika maisha halisi ni ushuhuda kwa Mungu, ni kuishi kwa kudhihirisha kwa mwanadamu na ushuhuda kwa Mungu, na huku ndiko kufurahia upendo wa Mungu kwa kweli; unapokuwa umepitia mpaka hatua hii, matokeo yanayostahili yatakuwa yamefikiwa. Unakuwa na kuishi kwa kudhihirisha kwa kweli na kila kitendo chako kinatazamwa kwa kuvutiwa na wengine. Mavazi yako na mwonekano wako wa nje ni wa kawaida tu, lakini unaishi kwa kudhihirisha maisha ya uchaji Mungu wa juu, na unapofanya ushirika kuhusu maneno ya Mungu, unaelekezwa na kutiwa nuru na Yeye. Unaweza kuzungumza nia za Mungu kupitia maneno yako, kushiriki uhalisi, na unafahamu mambo mengi kuhusu kutumikia katika roho. Unazungumza kwa madaha, wewe ni mwenye adabu na mnyofu, hujiingizi katika mabishano na wewe si mpotovu, unaweza kutii mipango ya Mungu na kusimama imara katika ushuhuda wako mambo yanapokutendekea, na wewe ni mtulivu na mwenye kufanya kwa kiasi haijalishi unashughulika na nini. Mtu wa aina hii ameona upendo wa Mungu kwa kweli. Watu wengine bado ni vijana, lakini wao hutenda kama mtu wa makamo; wamekomaa, wana ukweli, na wanastahiwa na wengine—na hawa ndio watu walio na ushuhuda na ni udhihirisho wa Mungu. Yaani, watu wanapopitia hadi hatua fulani, ndani yao watakuwa na umaizi kumhusu Mungu, na tabia yao ya nje pia itatengemaa. Watu wengi hawatendi ukweli na hawasimami imara katika ushuhuda wao. Ndani ya watu kama hao hakuna upendo kwa Mungu, au ushuhuda kwa Mungu, na hawa ndio watu wanaochukiwa zaidi na Mungu. Wanasoma maneno ya Mungu katika mikutano, lakini kile wanachoishi kwa kudhihirisha ni Shetani, na huku ni kumfedhehesha Mungu, kumwakilisha Mungu visivyo, na kumkufuru Mungu. Ndani ya watu kama hao, hakuna dalili ya upendo wa Mungu, na hawana kazi ya Roho Mtakatifu hata kidogo. Kwa hivyo, maneno na matendo yao yanamwakilisha Shetani. Ikiwa moyo wako daima umetulia mbele za Mungu, na daima unazingatia watu, matukio, na vitu vinavyokuzunguka, na ikiwa unajali mzigo wa Mungu, na daima una moyo umwogopao Mungu, basi Mungu mara nyingi atakutia nuru kwa ndani. Katika kanisa kuna watu ambao ni “wasimamizi”: Wanakusudia kutazama makosa ya wengine na kisha wanayaiga na kuyafuata. Hawana uwezo wa utambuzi, hawachukii dhambi na hawakirihi au kuhisi kuchukizwa na mambo ya Shetani. Watu kama hao wamejaa mambo ya Shetani, na hatimaye watatelekezwa kabisa na Mungu. Unapaswa daima kuwa na moyo umwogopao Mungu mbele za Mungu, unapaswa kuwa mwenye kutenda kwa kiasi katika maneno na matendo yako na usitamani kamwe kumpinga au kumfadhaisha Mungu. Hupaswi kamwe kukubali kazi ya Mungu kwako iwe ya bure, au kuruhusu ugumu wote ambao umevumilia na yote ambayo umetenda yawe ya bure. Lazima uwe tayari kutia bidii zaidi na kumpenda Mungu zaidi katika njia iliyo mbele yako. Hawa ndio watu walio na maono kama msingi wao. Hawa ndio watu wanaotafuta maendeleo.
Ikiwa watu wanamwamini Mungu na wanapitia maneno ya Mungu kwa moyo umwogopao Mungu, basi ndani ya watu kama hao wokovu wa Mungu na upendo wa Mungu unaweza kuonekana. Watu hawa wanaweza kumshuhudia Mungu; wanaishi kwa kudhihirisha ukweli, na kile wanachoshuhudia pia ni ukweli, kile Mungu alicho, na tabia ya Mungu. Wanaishi ndani ya upendo wa Mungu na wameona upendo wa Mungu. Ikiwa watu wanataka kumpenda Mungu, lazima wapitie kupendeza kwa Mungu na waone kupendeza kwa Mungu; ni hapo tu ndipo moyo umpendao Mungu unaweza kuamshwa ndani yao, na moyo wa kujitumia kwa ajili ya Mungu kwa kujitoa. Mungu hawafanyi watu wampende kupitia maneno au kupitia mawazo yao, na Yeye hawashurutishi watu wampende. Badala yake, Yeye huwaruhusu wampende kwa hiari yao wenyewe, na Yeye huwaruhusu waone kupendeza Kwake katika kazi na maneno Yake, ambapo baada ya hapo upendo kwa Mungu huzaliwa ndani yao. Ni kwa njia hii tu ndiyo watu wanaweza kuwa na ushuhuda kwa Mungu kwa kweli. Watu hawampendi Mungu kwa sababu wamehimizwa kufanya hivyo na wengine, wala si msukumo wa kihisia wa muda mfupi. Wanampenda Mungu kwa sababu wameona kupendeza Kwake, wameona kwamba kuna mengi sana kumhusu Yeye ambayo yanastahili upendo wa watu, kwa sababu wameona wokovu wa Mungu, hekima, na matendo ya ajabu—na matokeo yake, wanamsifu Mungu kwa kweli na kumtamani kwa kweli, na ndani yao mnaamshwa shauku kubwa kiasi kwamba hawawezi kuendelea kuishi bila kumpata Mungu. Sababu inayofanya wale wanaomshuhudia Mungu kwa kweli waweze kufanya hivyo kwa kishindo ni kwamba ushuhuda wao unategemea msingi wa maarifa ya kweli na shauku ya kweli kwa Mungu. Ushuhuda kama huo hautolewi kulingana na msukumo wa kihisia, bali kulingana na maarifa yao juu ya Mungu na tabia Yake. Kwa sababu wamekuja kumjua Mungu, wanahisi kwamba hakika lazima wawe na ushuhuda kwa Mungu na kuwafanya wale wote wanaomtamani Mungu wamjue Mungu, na wafahamu kupendeza kwa Mungu na uhalisi Wake. Kama upendo wa watu kwa Mungu, ushuhuda wao ni wa hiari; una uhalisi na una umuhimu halisi na thamani. Si wa kutochukua hatua au mtupu na usio na maana. Sababu ya kusema kwamba ni wale tu wanaompenda Mungu kwa kweli ndio walio na thamani na maana kubwa zaidi katika maisha yao, na wanamwamini Mungu kwa kweli, ni kwamba watu hawa wanaweza kuishi katika nuru ya Mungu na wanaweza kuishi kwa ajili ya kazi na usimamizi wa Mungu. Ni kwa sababu hawaishi gizani, bali wanaishi katika nuru; hawaishi maisha yasiyo na maana, bali maisha ambayo yamebarikiwa na Mungu. Ni wale tu wanaompenda Mungu ndio wanaoweza kumshuhudia Mungu, ni wao tu ndio mashahidi wa Mungu, ni wao tu ndio wanaobarikiwa na Mungu, na ni wao tu ndio wanaoweza kurithi ahadi za Mungu. Wale wanaompenda Mungu ni wandani wa Mungu; wao ni watu wanaopendwa na Mungu, na wanaweza kufurahia baraka pamoja na Mungu. Ni watu kama hawa tu ndio watakaoishi milele, na ni wao tu ndio watakaoishi milele chini ya utunzaji na ulinzi wa Mungu. Mungu ni wa kupendwa na watu, na Yeye anastahili upendo wa watu wote, lakini si watu wote wanaoweza kumpenda Mungu, na si watu wote wanaoweza kuwa na ushuhuda kwa Mungu na kutawala pamoja na Mungu. Kwa sababu wanaweza kutoa ushuhuda kwa Mungu na kujitolea juhudi zao zote kwa kazi ya Mungu, wale wanaompenda Mungu kwa kweli wanaweza kutembea ulimwenguni kote bila mtu yeyote kuthubutu kuwapinga, na wanaweza kutawala juu ya dunia na kuwatawala watu wote wa Mungu. Watu hawa wanakusanyika pamoja kutoka kote ulimwenguni. Wao ni watu kutoka kote ulimwenguni wanaozungumza lugha tofauti na walio na rangi tofauti za ngozi, lakini ambao uwepo wao una maana sawa, na walio na moyo uleule umpendao Mungu; wao wote ni watu wanaotoa ushuhuda uleule, na walio na azimio la pamoja na matamanio ya pamoja. Wale wanaompenda Mungu wanaweza kutembea ulimwenguni kote, na wale wanaotoa ushuhuda kwa Mungu wanaweza kusafiri kote ulimwenguni. Watu hawa wanapendwa na Mungu, wamebarikiwa na Mungu, na wataishi milele ndani ya nuru Yake.