Maonyo Matatu

Kama muumini wa Mungu, unapaswa kuwa mwaminifu kwake Yeye pekee katika vitu vyote, na uweze kulingana na nia Zake katika vitu vyote. Hata hivyo, ingawa kila mtu anaelewa ujumbe huu, kwa sababu ya matatizo mbalimbali ya mwanadamu—kwa mfano, kwa sababu ya ujinga, upumbavu, na upotovu wake—ukweli huu, ambao ni wa kijuujuu na wa msingi kabisa, haudhihiriki kikamilifu ndani yake, na hivyo, kabla matokeo yenu hayajaamuliwa, Ninapaswa kwanza kuwaambia mambo machache ambayo ni ya muhimu sana kwenu. Kabla Sijaendelea, mnapaswa kwanza kuelewa hili: Maneno Ninayonena ni ukweli unaoelekezwa kwa binadamu wote; hayaonyeshwi tu kwa mtu mahususi au aina ya mtu. Kwa hivyo, mnapaswa tu kujishughulisha na kuyafahamu maneno Yangu kutoka katika mtazamo wa ukweli, na lazima muwe na mtazamo wa umakini kamili na unyofu; msipuuze neno hata moja au ukweli Ninaounena, na msiyachukulie maneno yote Ninayonena kwa wepesi. Katika maisha yenu, Ninaona kwamba mmefanya mambo mengi sana ambayo hayahusiani na ukweli, na hivyo Ninahitaji hasa kwamba muwe watumishi wa ukweli, kwamba msiwe watumwa wa uovu na ubaya, na kwamba msikanyage ukweli wala kuinajisi kona yoyote ya nyumba ya Mungu. Hili ndilo onyo Langu kwenu. Sasa Nitazungumzia mada husika.

Kwanza, kwa ajili ya majaliwa yenu, mnapaswa kufikia kutambuliwa na Mungu. Yaani, kwa kuwa mnakiri kwamba ninyi ni washiriki wa nyumba ya Mungu, basi mnapaswa kuutuliza moyo wa Mungu katika vipengele vyote na kumridhisha Yeye katika vitu vyote—yaani, lazima mtende kwa kanuni na kulingana na ukweli. Ikiwa huwezi kufikia hili, basi utabeuliwa na Mungu na kukataliwa kwa dharau na kila mtu. Pindi unapojikuta katika hali ngumu kama hiyo, basi huwezi tena kuhesabiwa miongoni mwa washiriki wa nyumba ya Mungu, jambo ambalo ndilo hasa maana ya kutotambuliwa na Mungu.

Pili, mnapaswa kujua kwamba Mungu anawapenda wale walio waaminifu. Mungu ana kiini cha uaminifu, na hivyo maneno Yake daima yanaweza kuaminiwa; matendo Yake, zaidi ya hayo, hayana makosa na hayana shaka. Hii ndiyo maana Mungu anawapenda wale walio waaminifu Kwake kabisa. Uaminifu unamaanisha kumpa Mungu mioyo yenu, kutokuwa wenye uwongo kwa Mungu katika jambo lolote, kuwa wazi Kwake katika mambo yote, kutoficha ukweli kamwe, kutojaribu kuwadanganya wale walio juu yenu na kuwaficha mambo wale walio chini yenu, na kutofanya mambo ambayo ni majaribio tu ya kujipendekeza kwa Mungu. Kwa ufupi, kuwa waaminifu ni kuwa safi katika matendo na maneno yenu, na kutomdanganya Mungu wala mwanadamu. Kile Ninachosema ni rahisi sana, lakini kwenu ni kigumu maradufu. Watu wengi wanaona afadhali watupwe jahanamu kuliko kuzungumza na kutenda kwa uaminifu. Si ajabu kwamba Nina njia nyingine ya kuwashughulikia wale wasio waaminifu. Bila shaka, Ninajua fika jinsi ilivyo vigumu kwenu kuwa watu waaminifu. Kwa sababu ninyi nyote ni “werevu” sana, stadi sana katika kupima mioyo ya watu waungwana kulingana na mawazo yenu wenyewe yaliyo duni, hili linafanya kazi Yangu iwe rahisi zaidi. Na kwa kuwa kila mmoja wenu anakumbatia siri zake kifuani mwake, basi, Nitawaweka ninyi, mmoja baada ya mwingine, katika janga ili “mfundishwe” kwa moto, ili kwamba baada ya hapo mweze kuwa wenye imani thabiti katika maneno Yangu. Hatimaye, Nitayang’oa kutoka vinywani mwenu maneno “Mungu ni Mungu mwaminifu,” hapo ndipo mtajipiga vifua vyenu na kuomboleza, “Moyo wa mwanadamu ni mdanganyifu sana!” Hali yenu ya akili itakuwaje wakati huo? Hakika hamtakuwa mmejawa na kiburi kama mlivyo sasa! Sembuse mtakuwa “wenye kina na wenye kujifanya kuwa wagumu kueleweka” kama mlivyo sasa. Mbele ya Mungu, watu wengine huonekana kuwa wenye adabu na nidhamu, na hasa “wenye mwenendo mzuri,” lakini wanaonyesha meno yao na kutikisa makucha yao mbele ya Roho. Je, mngewahesabu watu kama hao miongoni mwa safu za waaminifu? Ikiwa wewe ni mnafiki, mtu ambaye ni stadi katika “uhusiano na watu,” basi Ninasema kwamba hakika wewe ni mtu anayejaribu kumchezea Mungu. Ikiwa maneno yako yamejaa visingizio na uthibitisho usio na maana, Basi Ninasema kwamba wewe ni mtu asiyetaka kuutia ukweli katika vitendo. Ikiwa una mambo mengi ya kibinafsi ambayo ni magumu kuyazungumzia, ikiwa unachukia sana kuweka wazi siri zako—matatizo yako—mbele ya wengine ili kutafuta njia ya nuru, basi Ninasema kwamba wewe ni mtu ambaye atakuwa na ugumu mkubwa wa kupata wokovu, na ambaye atakuwa na ugumu wa kutoka gizani. Ikiwa kweli unafurahia kuitafuta njia ya ukweli, basi wewe ni mtu anayekaa daima katika nuru. Ikiwa unafurahi sana kuwa mtendaji huduma katika nyumba ya Mungu, ukifanya kazi kwa bidii na kwa uangalifu bila kujulikana, daima ukitoa na kutochukua kamwe, basi Ninasema kwamba wewe ni mtakatifu mwaminifu, kwa sababu hutafuti malipo na unakuwa tu mtu mwaminifu. Ikiwa uko tayari kuwa mkweli, ikiwa uko tayari kujitumia kikamilifu, Ikiwa unaweza kutoa maisha yako kwa ajili ya Mungu na kusimama imara katika ushuhuda wako, ikiwa wewe ni mwaminifu hadi kufikia hatua ambapo unajua tu kumridhisha Mungu na si kujifikiria mwenyewe au kujinufaisha mwenyewe, basi Ninasema kwamba watu kama wewe ni wale wanaolishwa katika nuru na ambao wataishi milele katika ufalme. Unapaswa kujua kama kuna imani ya kweli na uaminifu wa kweli ndani yako, kama una rekodi ya kuteseka kwa ajili ya Mungu, na kama una utii kamili kwa Mungu. Ikiwa huna haya, basi ndani yako mnasalia uasi, udanganyifu, uchoyo, na malalamiko. Kwa kuwa moyo wako si mwaminifu, hujawahi kuthaminiwa na Mungu na hujawahi kuishi katika nuru. Jinsi majaliwa ya mtu yatakavyokuwa mwishowe inategemea iwapo ana moyo mwaminifu na mwekundu kama damu, na iwapo ana nafsi safi. Ikiwa wewe ni mtu asiye mwaminifu kabisa, mtu aliye na moyo wenye uovu mwingi, mtu aliye na nafsi isiyo safi, basi hakika utaishia mahali ambapo mwanadamu anaadhibiwa, kama ilivyoandikwa katika rekodi ya majaliwa yako. Ikiwa unadai kuwa mwaminifu sana, na bado hufaulu kamwe kutenda kulingana na ukweli wala kuzungumza neno la kweli, basi, je, bado unamngoja Mungu akutuze? Je, bado unatumaini kwamba Mungu atakuona kama mboni ya jicho Lake? Je, fikira kama hizo si za kipuuzi? Ikiwa unamdanganya Mungu katika vitu vyote, nyumba ya Mungu inawezaje kumkaribisha mtu kama wewe, ambaye mikono yake si safi?

Jambo la tatu Ninalotaka kuwaambia ni hili: Kila mtu, katika mchakato wa kuishi maisha yake ya imani katika Mungu, amefanya mambo ambayo yanampinga na kumdanganya Mungu. Baadhi ya mambo hayo hayahitaji kurekodiwa kama makosa, lakini baadhi ya hayo hayasameheki, kwa maana kuna mengi yanayokiuka amri za utawala—mambo ambayo yanaikosea tabia ya Mungu. Wengi ambao wana wasiwasi kuhusu majaliwa yao wenyewe wanaweza kuuliza mambo haya ni yapi. Mnapaswa kujua kwamba ninyi ni wenye kiburi na wenye majivuno kiasili, na hamko tayari kutii ukweli wa mambo. Kwa sababu hii, Nitawaambia kidogo kidogo baada ya ninyi kujitafakari. Ninawahimiza mfanye juhudi ya kweli ili muelewe maudhui ya amri za utawala, na mjitahidi kuijua tabia ya Mungu. Vinginevyo, mtapata ugumu wa kufunga midomo yenu, ndimi zenu zitaongea bila kujizuia, na mtatoa maneno makuu, bila kujua mkiikosea tabia ya Mungu na kuanguka gizani, mkipoteza uwepo wa Roho Mtakatifu na nuru. Kwa sababu hamna kanuni katika matendo yenu, mkifanya na kusema yale msiyopaswa, utapokea malipo unayostahili. Unapaswa kujua kwamba ingawa huna kanuni katika neno na tendo, Mungu ni mwenye kanuni ya kiwango cha juu katika yote mawili. Sababu inayokufanya upokee malipo ni kwa sababu umemkosea Mungu, si mtu. Ikiwa, katika maisha yako, unatenda makosa mengi dhidi ya tabia ya Mungu, basi hakika utaishia kuwa mwana wa jahanamu. Kwa mwanadamu inaweza kuonekana kwamba umetenda tu matendo machache ambayo yanapingana na ukweli, na si zaidi. Hata hivyo, je, unafahamu kwamba machoni pa Mungu tayari wewe ni mtu ambaye kwake hakuna tena sadaka ya dhambi? Kwa sababu umekiuka amri za utawala za Mungu zaidi ya mara moja na, zaidi ya hayo, hujaonyesha dalili yoyote ya toba au kurudi nyuma, hakuna jambo lingine ila wewe kutumbukizwa jahanamu, ambapo Mungu humwadhibu mwanadamu. Idadi ndogo ya watu, walipokuwa wakimfuata Mungu, walitenda matendo fulani yaliyokiuka kanuni, lakini baada ya kupogolewa na kupewa maelekezo, hatua kwa hatua waligundua upotovu wao wenyewe, na baada ya hapo waliingia kwenye njia sahihi ya uhalisi, na wamejikita humo imara hadi sasa. Watu kama hao ndio wale watakaosalia mwishowe. Hata hivyo, ni waaminifu ndio Ninaowataka; ikiwa wewe ni mtu mwaminifu na mtu anayetenda kulingana na kanuni, basi unaweza kuwa msiri wa Mungu. Ikiwa katika matendo yako huikosei tabia ya Mungu, na unatafuta nia ya Mungu, na una moyo umwogopao Mungu, basi imani yako inafikia kiwango kinachostahili. Yeyote asiyemwogopa Mungu na asiye na moyo unaotetemeka kwa hofu ana uwezekano mkubwa wa kukiuka amri za utawala za Mungu. Wengi wanamtumikia Mungu kwa kutegemea shauku yao lakini hawana ufahamu wa amri za utawala za Mungu, sembuse kuwa na ufahamu hata mdogo wa maana ya ndani ya maneno Yake. Na hivyo, kwa nia zao njema, mara nyingi wanaishia kufanya mambo yanayosumbua usimamizi wa Mungu. Katika visa vikali, wanatimuliwa kutoka katika nyumba ya Mungu, wakinyimwa nafasi yoyote zaidi ya kumfuata Yeye, na wanatupwa jahanamu, ushirika wote na nyumba ya Mungu ukiwa umefika mwisho. Watu hawa wanafanya kazi ya nyumba ya Mungu kwa kutegemea nia zao njema zisizo na ufahamu, na mwishowe huikasirisha tabia ya Mungu. Watu huleta njia zao za kuwatumikia maafisa na mabwana katika nyumba ya Mungu na kujaribu kuzitumia, wakijidanganya kwamba zinaweza kutumika kwa urahisi hapa bila juhudi. Kamwe hawawazii kwamba Mungu hana tabia ya mwanakondoo, bali ile ya simba. Kwa hivyo, wale wanaohusiana na Mungu kwa mara ya kwanza hawawezi kuwasiliana na Yeye, kwa maana moyo wa Mungu si kama ule wa mwanadamu. Ni baada tu ya wewe kuelewa ukweli mwingi ndipo unapoweza kuendelea kumjua Mungu. Maarifa haya hayaundwi na maneno na mafundisho bali yanaweza kutumika kama hazina ambayo kwayo unaingia katika uhusiano wa karibu na Mungu, na kama uthibitisho kwamba Yeye anapendezwa nawe. Ikiwa unakosa uhalisi wa maarifa na hujajizatiti na ukweli, basi huduma yako ya shauku inaweza tu kukuletea chukizo na karaha ya Mungu. Kufikia sasa unapaswa kuwa umeelewa kwamba imani katika Mungu si somo la teolojia!

Ingawa maneno Ninayotumia kuwaonya ni mafupi, yote ambayo Nimeyaweka wazi ndiyo yale yanayokosa kabisa ndani yenu. Mnapaswa kujua kwamba Ninanena sasa kwa ajili ya kazi Yangu ya mwisho miongoni mwa wanadamu, kwa ajili ya kuamua matokeo ya mwanadamu. Sitaki kufanya kazi nyingi zaidi isiyozaa matunda, wala Sitaki kuendelea kuwaelekeza watu hao ambao ni kama magogo yaliyokufa, sembuse kuendelea kuwaongoza wale ambao kwa siri wana nia mbaya. Pengine siku moja mtaelewa nia za kujitahidi zilizo nyuma ya maneno Yangu na michango ambayo Nimetoa kwa ajili ya binadamu. Pengine siku moja mtagundua dhana itakayowawezesha kufikia hitimisho kuhusu matokeo yenu wenyewe.

Iliyotangulia: Juu ya Hatima

Inayofuata: Dhambi Zitamwongoza Mwanadamu Jahanamu

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp