Mungu Ndiye Chanzo cha Uhai wa Mwanadamu

Kuanzia wakati unapokuja ulimwenguni humu ukilia, unaanza kutimiza majukumu yako. Kwa ajili ya mpango wa Mungu na kutawaza Kwake, unafanya wajibu wako na kuanza safari yako ya maisha. Haijalishi ulikokulia kulivyo, na haijalishi safari iliyo mbele yako ilivyo, kwa vyovyote vile, hakuna anayeweza kuepuka mipango na mipangilio ya Mbinguni, na hakuna anayeweza kudhibiti hatima yake mwenyewe, kwani ni Yeye tu aliye na mamlaka juu ya vitu vyote ndiye Anayeweza kufanya kazi hiyo. Tangu kuwepo kwa mwanadamu hapo mwanzo, Mungu daima amekuwa Akifanya kazi Yake kwa namna hii, Akiusimamia ulimwengu, na kuelekeza sheria za mabadiliko kwa vitu vyote na mweleke wa kusonga kwao. Kama vitu vyote, mwanadamu kwa ukimya na bila kujua anastawishwa kwa utamu na mvua na umande kutoka kwa Mungu; kama vitu vyote, mwanadamu bila kujua, anaishi chini ya mpango wa mkono wa Mungu. Moyo na roho ya mwanadamu vimo katika mshiko wa Mungu, na kila kitu cha maisha yake kinatazamwa machoni pa Mungu. Bila kujali kama unaamini haya yote au la, chochote na vitu vyote, viwe vilivyohai au vilivyokufa, vitahamishwa, vitabadilishwa, kufanywa vipya, na kupotea kulingana na fikira za Mungu. Hivi ndivyo ambavyo Mungu anashikilia mamlaka juu ya vitu vyote.

Usiku unapoingia polepole, mwanadamu huwa hafahamu, kwani moyo wa mwanadamu hauwezi kujua jinsi giza linavyoingia au ni wapi linakotokea. Usiku unapotoweka polepole, mwanadamu hukaribisha mwanga wa mchana, lakini kuhusu mahali ambapo nuru imetokea, na jinsi imeliondoa giza la usiku, mwanadamu anajua machache, na hata anafahamu mchache zaidi Mabadiliko haya ya kawaida ya mchana na usiku humpitisha mwanadamu kutoka kipindi kimoja hadi kingine, kutoka kipindi kimoja cha kihistoria hadi kingine, wakati huu wote zinahakikisha kwamba kazi ya Mungu katika kila kipindi na mpango Wake wa kila enzi unatekelezwa. Mwanadamu amepitia vipindi hivi vyote tofauti akimfuata Mungu, lakini bado hafahamu kwamba Mungu ana ukuu juu ya hatima ya vitu vyote na viumbe hai, wala jinsi Mungu anavyopanga na kuelekeza vitu vyote. Hili ni jambo ambalo limekwepa ufahamu wa binadamu tangu enzi za kale mpaka leo. Kuhusu sababu, siyo kwa sababu matendo ya Mungu hayafahamiki, au kwa sababu mpango wa Mungu bado haujakamilika, lakini ni kwa sababu moyo na roho ya mwanadamu viko mbali sana na Mungu, kiasi cha kwamba, mwanadamu anabaki katika huduma ya Shetani wakati ule ule anapomfuata Mungu—na hata halitambui hili. Hakuna anayetafuta kwa bidii nyayo za Mungu na kuonekana kwa Mungu, na hakuna aliye tayari kuishi katika utunzaji na ulinzi wa Mungu. Badala yake wako tayari kutegemea upotoshaji wa Shetani, yule mwovu, ili kubadilishwa kufuatana na dunia hii na kanuni za kuishi ambazo wanadamu waovu wanafuata. Katika hatua hii, moyo na roho ya mwanadamu vinakuwa ushuru ambao mwanadamu anatoa kwa shetani na kuwa riziki ya Shetani. Hata zaidi, moyo wa binadamu na roho yake zimekuwa mahali ambapo Shetani anaweza kuishi na uwanja wake wa kuchezea unaofaa. Kwa njia hii, mwanadamu bila kujua anapoteza ufahamu wake wa kanuni za mwenendo wa mwanadamu, na wa thamani na umuhimu wa kuwepo kwa binadamu. Sheria za Mungu na agano kati ya Mungu na mwanadamu polepole vinakuwa giza katika moyo wa mwanadamu, na anaacha kumtafuta au kumsikiliza Mungu. Wakati unavyopita, mwanadamu haelewi tena kwa nini Mungu alimuumba, wala haelewi maneno yanayotoka katika kinywa cha Mungu na yote yanayotoka kwa Mungu. Kisha mwanadamu anaanza kupinga sheria na amri za Mungu, na moyo wake na roho yake vinakufa ganzi…. Mungu amempoteza mwanadamu ambaye Alimuumba hapo mwanzo, na mwanadamu amepoteza asili aliyokuwa nayo hapo awali: Hii ndio huzuni ya jamii hii ya binadamu. Kwa hakika, tangu mwanzo hadi sasa, Mungu ameandaa janga kwa ajili ya wanadamu, ambapo mwanadamu ndiye mhusika mkuu na mwathirika. Na hakuna anayeweza kujibu kuhusu mwelekezi wa janga hili ni nani.

Katika upana mkubwa wa dunia hii, mabadiliko yasiyohesabika yamefanyika, bahari kujaa hadi kuziba mashamba, mashamba kufurika hadi baharini, tena na tena. Isipokuwa Yule ambaye anatawala kila kitu katika ulimwengu, Hakuna anayeweza kuongoza na kuelekeza jamii hii ya wanadamu. Hakuna mtu hodari wa kufanya kazi au kufanya maandalizi kwa ajili ya jamii hii ya binadamu, sembuse yule anayeweza kuiongoza jamii hii ya wanadamu hadi kwenye hatima yenye mwanga na kuikomboa kutokana na udhalimu wa duniani. Mungu anaombolezea mustakabali wa wanadamu, Anahuzunishwa na anguko la mwanadamu, na Anaumia kwamba wanadamu wanatembea, hatua kwa hatua, kuuelekea uozo na katika njia ambayo hawataweza kurejea. Hakuna mtu ambaye amewahi kufikiria kuhusu hili: Mwanadamu kama huyo, ambaye ameuvunja moyo wa Mungu kabisa na kumkana ili kumfuata yule mwovu, je, anaweza kuelekea wapi? Ni kwa sababu hii hasa kwamba hakuna anayehisi hasira ya Mungu, hakuna anayetafuta njia ya kumpendeza Mungu au kujaribu kuja karibu na Mungu na isitoshe, hakuna anayetafuta kufahamu huzuni na maumivu ya Mungu. Hata baada ya kusikia sauti ya Mungu, binadamu anaendelea tu kwenye njia yake mwenyewe, anazidi kwenda mbali na Mungu, kukwepa neema na utunzaji wa Mungu, na kuuepuka ukweli Wake, akiona ni heri ajiuze kwa Shetani, adui wa Mungu. Na ni nani amewahi kufikiria—kama mwanadamu ataendelea kuwa mkaidi—ni kwa jinsi gani Mungu atawatendea wanadamu hawa ambao wamempuuza bila kusita? Hakuna anayejua kwamba sababu ya ukumbusho wa mara kwa mara na kusihi kwa Mungu ni kwa sababu Yeye anayo katika mikono yake maafa yasiyokuwa ya kawaida ambayo ameyaandaa, maafa ambayo yatakuwa magumu kwa mwili na nafsi ya mwanadamu kuyastahimili. Maafa haya siyo tu adhabu ya mwili bali pia yanalenga nafsi ya mwanadamu. Unafaa kujua hili: Mpango wa Mungu utakaposhindikana na wakati makumbusho Yake na kusihi Kwake hakutapata majibu yoyote, je, atatoa hasira ya aina gani? Hii itakuwa kama kitu ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo awali au hata kusikika na viumbe vyovyote. Na hivyo Nasema, majanga haya hayana mengine ya kulinganishwa nayo na kamwe hayatawahi kurudiwa. Hii ni kwa sababu ni mpango wa Mungu kuwaumba wanadamu mara hii moja tu na kuwaokoa wanadamu mara hii moja tu. Hii ndiyo mara ya kwanza na pia ni ya mwisho. Kwa hivyo, hakuna anayeweza kuelewa nia zenye maumivu na matarajio ya dhati ambayo kwayo Mungu anawaokoa wanadamu kwa wakati huu.

Mungu aliuumba ulimwengu huu na kumleta mwanadamu ndani yake, kiumbe hai ambaye Alimtia uhai ndani yake. Kisha, mwanadamu akaja kuwa na wazazi na jamaa na hakuwa mpweke tena. Tangu mwanadamu alipotazama kwa mara ya kwanza ulimwengu huu unaoonekana, alikusudiwa kuishi ndani ya utaratibu wa Mungu. Ni pumzi ya uhai inayotoka kwa Mungu ambayo inamtegemeza kila kiumbe hai katika kipindi cha ukuaji wake hadi kufikia utu uzima. Wakati wa mchakato huu, hakuna anayehisi kwamba mwanadamu anakua chini ya uangalizi wa Mungu, lakini badala yake anaamini kwamba mwanadamu anafanya hivyo chini ya utunzaji wa upendo wa wazazi wake, na kwamba ni silika yake mwenyewe ya maisha ambayo inaongoza mchakato huu wa kukua kwake. Hii ni kwa sababu mwanadamu hajui ni nani aliyetoa maisha yake, au ni wapi yalikotoka, sembuse hata jinsi ambavyo silika ya maisha inavyoweza kusababisha miujiza. Anajua tu kwamba chakula ndicho msingi wa kuendelea kwa maisha yake, kwamba uvumilivu ndio chanzo cha kuwepo kwake, na kwamba imani zilizopo katika akili yake ndio mtaji ambao kuishi kwake kunategemea. Mwanadamu hajui kabisa kuhusu neema na riziki zitokazo kwa Mungu, na kwa njia hii yeye hupoteza. uzima aliopewa na Mungu bila azma…. Hakuna hata mmoja wa wanadamu hawa amepoteza maisha ambayo Mungu amempa. Mungu anaendelea tu kufanya kazi juu ya mwanadamu, Akiwa hana matarajio yoyote kutoka kwake, kama jinsi ambavyo Amepanga. Anafanya hivyo kwa matumaini kwamba siku moja, mwanadamu ataamka kutoka katika ndoto yake na kwa ghafla atambue thamani na maana ya maisha, gharama aliyolipa Mungu kwa yote ambayo Amempa, na shauku ambayo kwayo Mungu anamngojea mwanadamu ageuke amrudie Yeye. Hakuna mtu yeyote ambaye amewahi kuchunguza siri zinazoongoza asili na kuendelea kwa maisha ya mwanadamu. Ni Mungu tu, ambaye Anaelewa yote haya, kwa ukimya Anavumilia mapigo na maumivu ambayo binadamu, ambaye amepokea kila kitu kutoka kwa Mungu lakini hana shukrani, anampa Yeye. Mwanadamu hufurahia yote ambayo maisha huleta kwa hakika, na, vivyo hivyo, ni “jambo la hakika,” kwamba Mungu anasalitiwa na mwanadamu, Anasahaulika na mwanadamu, na kutozwa kwa nguvu na mwanadamu. Je, inaweza kuwa kwamba mpango wa Mungu una umuhimu kama huo kweli? Je, inaweza kuwa kwamba mwanadamu, kiumbe huyu aliye hai ambaye alitoka katika mkono wa Mungu, ni wa maana namna hiyo kweli? Mpango wa Mungu kwa hakika ni muhimu kabisa; hata hivyo, kiumbe chenye uhai kilichoumbwa na mkono wa Mungu kipo kwa ajili ya mpango Wake. Kwa hivyo, Mungu hawezi kuuharibu mpango Wake kwa sababu Anaichukia jamii hii ya wanadamu. Ni kwa ajili ya mpango Wake na kwa ajili ya pumzi aliyotoa ndiyo maana Mungu anavumilia mateso yote, sio kwa ajili ya mwili wa mwanadamu ila ni kwa sababu ya uhai wa mwanadamu. Yeye anafanya hivyo ili kurudisha pumzi Aliyopulizia ndani ya mwanadamu, wala si kuchukua tena mwili wa mwanadamu

Wote wanaokuja katika ulimwengu huu lazima wapitie maisha na kifo, na wengi wao walipitia mzunguko wa kifo na kuzaliwa upya. Wale wanaoishi watakufa hivi karibuni na wafu watarejea karibuni. Yote haya ni mchakato wa maisha uliopangwa na Mungu kwa kila kiumbe hai. Hata hivyo, mchakato huu na mzunguko huu hasa ni ukweli ambao Mungu anataka binadamu auone: kwamba maisha aliyopewa mwanadamu na Mungu hayana mipaka, na hayazuiliwi na maumbile ya nje, wakati, au nafasi. Hili ndilo fumbo la maisha aliyopewa mwandamu na Mungu, na ni udhihirisho kwamba maisha yalikuja kutoka Kwake. Ingawa watu wengi wanaweza kukosa kuamini kwamba maisha yalitoka kwa Mungu, binadamu bila kujua anafurahia yote kwa Mungu, iwe wanaamini au wanakana uwepo Wake. Iwapo siku moja Mungu kwa ghafla Atabadili moyo na Atake kurudisha yote yaliyomo duniani na kuchukua uzima Aliotoa, basi yote duniani yataisha. Mungu hutumia uzima Wake kukimu vitu vyote vilivyo hai na visivyo hai, na kuleta vyote kwenye utaratibu mzuri kupitia nguvu na mamlaka Yake. Huu ni ukweli ambao hauwezi kufikirika au kueleweka na yeyote, na kweli hizi zisizoeleweka kwa fikira zetu ni udhihirisho halisi na ushahidi wa nguvu za Mungu katika maisha. Sasa hebu Niwaambie siri: Ukubwa wa maisha ya Mungu na nguvu za maisha Yake haziwezi kueleweka na kiumbe chochote kilichoumbwa. Hivi ndivyo hali ilivyo sasa, kama ilivyokuwa awali, na itakuwa hivyo kwa wakati ujao. Siri ya pili Nitakayotoa ni hii: Chanzo cha uhai kwa viumbe vyote hutoka kwa Mungu, bila kujali jinsi wanavyoweza kuwa tofauti katika maumbile au muundo. Hata uwe kiumbe hai wa aina gani, huwezi kwenda kinyume na njia ya maisha ambayo Mungu ameweka. Kwa vyovyote vile, kile Ninachotaka ni mwanadamu aweze kuelewa hili: Bila ulinzi, utunzaji, na utoaji wa Mungu, mwanadamu hawezi kupokea yote aliyokusudiwa kupokea, bila kujali jinsi anavyojaribu kwa bidii au jinsi anavyopambana kwa bidii. Bila ruzuku ya uhai kutoka kwa Mungu, mwanadamu anapoteza thamani ya kuishi na maana ya maisha. Je, Mungu angewezaje kumruhusu mwanadamu, ambaye bila umakini amepoteza thamani ya maisha Yake, Asiwe na wasiwasi kiasi hicho? Kama vile Nilivyosema hapo awali: Usisahau kwamba Mungu ndiye chanzo cha uhai wako. Ikiwa mwanadamu atashindwa kuthamini yote ambayo Mungu Amemfanyia, si tu kwamba Mungu atachukua kile Alichotoa hapo mwanzo, lakini pia Atamfanya mwanadamu amlipe fidia mara mbili ya gharama zote Alizotoa.

Mei 26, 2003

Iliyotangulia: Mnapaswa Kuzingatia Matendo Yenu

Inayofuata: Kutanafusi kwa Mwenyezi

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp