Kutanafusi kwa Mwenye Uweza
Kuna siri kubwa sana moyoni mwako, ambayo hujawahi kuifahamu kamwe, kwa kuwa umekuwa ukiishi katika ulimwengu usio na mwanga. Moyo wako na roho yako vimepokonywa na yule mwovu. Macho yako yamezuiwa na giza yasione, na huwezi kuliona jua angani wala ile nyota ya usiku imetametayo. Masikio yako yamezibwa na maneno ya udanganyifu, na huisikii sauti ya Yehova ingurumayo kama radi, wala sauti ya maji mengi yanayotiririka kutoka katika kiti cha enzi. Umepoteza kila kitu ambacho ni chako kwa haki, kila kitu ambacho mwenye Uweza alikupa. Umeingia katika bahari ya mateso isiyokuwa na mwisho, bila nguvu ya kuweza kukuokoa, bila matumaini ya kuendelea kuishi, na kila unachofanya ni kupambana na kukimbia huku na kule tu.… Kuanzia wakati huo na kuendelea, umehukumiwa kuteswa na yule mwovu, mbali sana na baraka za mwenye Uweza, mbali sana na riziki ya mwenye Uweza, ukiitembea njia ambayo huwezi kurudi nyuma tena. Kuitwa mara milioni hakuwezi kuamsha moyo wako na roho yako. Unalala usingizi mzito mikononi mwa yule mwovu, ambaye alikushawishi kuingia katika ulimwengu usio na mipaka bila mwelekeo au vibao vya maelekezo. Katika wakati huo, ulipoteza kutokuwa na hatia na usafi wako wa asili, na ukaanza kuepuka utunzaji wa Mwenye Uweza. Ndani ya moyo wako, yule mwovu anakuongoza katika kila namna na amekuwa maisha yako. Humwogopi tena, humkwepi, wala humtilia shaka; badala yake, unamchukulia kama mungu moyoni mwako. Umeanza kumtukuza na kumwabudu, na ninyi wawili mmekuwa kama wasiotenganishwa kama mwili na kivuli, mkiahidi kuishi na kufa pamoja. Hujui ulikotoka, kwa nini ulizaliwa, au kwa nini utakufa. Unamtazama Mwenye Uweza kama mgeni; hujui asili Yake, sembuse yote ambayo Amekufanyia. Kila kitu kinachotoka Kwake unakitazama kwa uhasama; hukithamini wala hujui thamani yake. Unatembea sambamba na yule mwovu, kuanzia siku uliyopokea riziki ya Mwenye Uweza. Umevumilia maelfu ya miaka ya tufani na dhoruba pamoja na yule mwovu, na unasimama pamoja naye dhidi ya Mungu ambaye alikuwa chanzo cha uzima wako. Hujui kutubu, sembuse kujua kwamba umefika ukingoni mwa kuangamia. Umesahau kwamba yule mwovu amekushawishi na kukutesa; umesahau mwanzo wako. Hivyo ndivyo yule mwovu amekudhuru vibaya sana katika kila hatua ya njia hadi leo. Moyo wako na roho yako vimekufa ganzi na kuoza. Umeacha kulalamika kuhusu masumbuko ya ulimwengu wa mwanadamu; huamini tena kuwa ulimwengu hauna haki. Sembuse kujali kama Mwenye Uweza yupo. Hii ni kwa sababu muda mrefu uliopita ulimwona yule mwovu kuwa baba yako wa kweli na huwezi kutengana naye. Hii ndiyo siri ndani ya moyo wako.
Alfajiri inapofika, nyota ya asubuhi inaanza kuangaza mashariki. Hii ni nyota ambayo haijawahi kuwepo hapo awali, na inaangaza anga tulivu, inayometameta, ikiwasha tena mwanga uliozimwa katika mioyo ya binadamu. Binadamu si wapweke tena kwa sababu ya mwanga huu, ambao unakuangazia wewe pamoja na wengine. Lakini ni wewe peke yako unasalia ukiwa umelala fofofo katika usiku wa giza. Husikii sauti yoyote na huoni mwangaza wowote; huna ufahamu wa ujio wa mbingu mpya na nchi mpya, enzi mpya, kwa sababu baba yako anakwambia, “Mwanangu, usiamke, bado ni mapema. Hali ya hewa ni baridi, kwa hivyo usiende nje, usije ukachomwa machoni kwa mkuki na upanga.” Una imani tu katika maonyo ya baba yako, maana unaamini kwamba baba yako tu ndiye aliye sahihi, kwa kuwa baba yako ana umri mkubwa kuliko wewe na anakupenda sana. Maonyo kama hayo na upendo kama huo unakuelekeza uache kuamini hekaya kwamba kuna nuru ulimwenguni; unakuzuia kujali iwapo ukweli bado upo ulimwenguni humu. Huthubutu tena kutumainia ukombozi kutoka kwa Mwenye Uweza. Umeridhika kuwa katika hali hiyo, hutumainii tena ujio wa nuru, hutazamii tena ujio wa Mwenye Uweza kama inavyosimuliwa katika hekaya. Kwa maoni yako, yote ambayo ni mazuri hayawezi kufufuliwa, hayawezi kuwepo. Machoni pako, kesho ya wanadamu, siku za baadaye za wanadamu, vinatoweka tu, zimeangamizwa kabisa. Unashikilia sana mavazi ya baba yako kwa nguvu zako zote, ukiwa radhi kushiriki taabu zake, ukihofu sana kumpoteza mwenzako wa kusafiri na mwelekeo wa safari yako ya mbali. Dunia hii pana na yenye ukungu ya mwanadamu imewafinyanga wengi wenu, kuwa majasiri na watu wa kujitahidi sana katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya ulimwengu huu. Umewafanya “mashujaa” wengi wasioogopa kifo. Zaidi ya hayo, umetengeneza kundi baada ya kundi la wanadamu waliokufa ganzi na kupoozwa ambao hawajui kusudi la kuumbwa kwao. Macho ya Mwenye Uweza yanamchunguza kila mmoja wa jamii ya wanadamu walio katika mateso makali. Anachosikia ni vilio vya wale wanaoteseka, Anachoona ni kutokua na aibu kwa wale wanaoteseka, na Anachohisi ni kutojiweza na hofu ya jamii ya wanadamu ambayo imepoteza neema ya wokovu. Wanadamu wanakataa utunzaji Wake, wakichagua kutembea katika njia yao wenyewe, na wanajaribu kukwepa uchunguzi wa macho Yake, wakipendelea kuonja uchungu wa bahari kuu hadi tone la mwisho wakiwa na yule adui. Kutanafusi kwa Mwenye Uweza hakusikiki tena na wanadamu; mikono ya Mwenye Uweza haiko tayari tena kuwapapasa wanadamu hawa wa kusikitisha. Mara kwa mara Anawarejesha, na mara kwa mara Anawapoteza tena, na hivyo ndivyo ilivyo kazi Anayofanya kwa kurudia. Kuanzia wakati huo, Anaanza kuchoka, anahisi kuchoshwa, na hivyo Anaisitisha kazi inayoendelea na anaacha kutembea kati ya wanadamu… Wanadamu hawana ufahamu kabisa kuhusu mabadiliko haya, hawajui kuhusu kuja na kuondoka, huzuni na majonzi ya Mwenyezi.
Kila kitu cha ulimwengu huu kinabadilika kwa wepesi kwa mawazo ya Mwenye Uweza, na chini ya macho Yake. Mambo ambayo wanadamu hawajawahi kuyasikia yanakuja kwa ghafla, ilhali vitu ambavyo wanadamu wamevimiliki kwa muda mrefu vinatoweka bila wao kujua. Hakuna anayeweza kutambua mahali alipo Mwenye Uweza, sembuse mtu yeyote kuweza kuhisi kuzidi uwezo wa binadamu na ukuu wa nguvu za maisha za Mwenye Uweza. Yeye ni Mkuu kwa kuwa Anaweza kutambua kile ambacho wanadamu hawawezi. Yeye ni Mkuu kwa kuwani Yeye anayekataliwa na wanadamu na bado Anawaokoa wanadamu. Yeye anajua maana ya uzima na mauti na, zaidi ya hayo, Anajua sheria za kuishi ambazo binadamu, ambao wameumbwa, wanapaswa kuzifuata. Yeye ndiye msingi wa kuwepo kwa mwanadamu, na Yeye ndiye Mkombozi anayewafufua wanadamu tena. Anailemea mioyo yenye furaha kwa huzuni, na kuiinua mioyo yenye huzuni kwa furaha, yote ni kwa ajili ya kazi Yake, na kwa ajili ya mpango Wake.
Binadamu, wakiwa wamepotoka kutoka kwa ugavi wa uzima wa Mwenye Uweza, hawajui kusudi la kuwepo, lakini wanaogopa kifo hata hivyo. Hawana msaada au tegemeo, lakini bado wanasita kufumba macho yao, na wanajitayarisa kuitegemeza miili yao, na roho zisizo na hisia, na kujikokota kuishi maisha duni duniani humu. Wewe unaishi hivyo, bila tumaini, kama wafanyavyo wengine, bila lengo. Ni Yule Mtakatifu wa ngano pekee ndiye Atakayewaokoa watu ambao, wakiwa wanaomboleza katikati ya mateso yao, wanangoja kwa hamu kubwa kuja Kwake. Imani kama hiyo imebaki bila kutimizwa kwa muda mrefu ndani ya wale wasio na fahamu. Hata hivyo, bado wanaitamani sana. Mwenye Uweza ana rehema kwa watu hawa ambao wameteseka sana; wakati huo huo, Anawachukia watu hawa wasio na fahamu zozote kabisa, kwani inabidi Asubiri kwa muda mrefu sana kabla ya kupokea jibu kutoka kwa watu. Anataka kutafuta, kutafuta moyo wako na roho yako, na kukuletea maji na chakula, ili uzinduke na usiwe na kiu au njaa tena. Unapochoka na unapohisi kiasi fulani cha ukiwa wa dunia hii, usijihisi umepotea, usilie. Mwenyezi Mungu, Mwangalizi, atakumbatia kuja kwako wakati wowote. Anakesha kando yako. Anakusubiri urejee, akisubiri siku utakayorejesha kumbukumbu yako ghafla: utakapotambua kwamba ulitoka kwa Mungu, na kwamba, wakati fulani usiojulikana ulipoteza mwelekeo wako, wakati fulani usiojulikana ulilala usingizi njiani, na wakati fulani usiojulikana ulikuwa na “baba”; unapotambua, zaidi ya hayo, kwamba Mwenye Uweza amekuwa akikesha daima, Akisubiri hapo kwa muda mrefu sana, sana kwa ajili ya kurudi kwako. Amekuwa akitamani kwa hamu kubwa, akisubiri itikio lisilo na jibu. Kukesha Kwake ni kwa thamani isiyokadirika, na ni kwa ajili ya moyo wa mwanadamu na roho ya mwanadamu. Pengine kukesha Kwake hakuna kikomo, au pengine kumefika mwisho. Lakini unapaswa kujua hasa ulipo moyo wako na ilipo roho yako sasa hivi.
Mei 28, 2003