Tayarisha Matendo Mema ya Kutosha kwa ajili ya Hatima Yako

Nimefanya kazi nyingi miongoni mwenu na, bila shaka, Nimenena baadhi ya matamshi pia. Hata hivyo Sina budi kuhisi kwamba maneno Yangu na kazi Yangu havijatimiza lengo la kazi Yangu ya siku za mwisho kikamilifu. Maana katika siku za mwisho, kazi Yangu si kwa ajili ya mtu au watu fulani, bali ili kufafanua tabia Yangu ya asili. Hata hivyo, kutokana na sababu nyingi—pengine ukosefu wa muda au shughuli nyingi za kazi—watu hawajapata ufahamu wowote kunihusu kutokana na tabia Yangu. Kwa hivyo, Ninaanza mpango Wangu mpya, katika kazi Yangu ya mwisho, na kufungua ukurasa mpya katika kazi Yangu ili wale wanaoniona watajipiga kifuani na kulilia na kuombolezea bila kukoma kwa sababu ya uwepo Wangu. Hii ni kwa sababu Ninaleta mwisho wa wanadamu duniani, na kuanzia sasa na kuendelea, Ninaweka wazi tabia Yangu yote mbele ya wanadamu, ili wote wanijuao na wale wote wasionijua waweze kuyafurahisha macho yao na kuona kwamba kweli, Nimekuja katika ulimwengu wa kibinadamu, Nimekuja duniani ambapo vitu vyote vinazidi kuongezeka. Huu ni mpango Wangu, na “kukiri” Kwangu kwa pekee tangu Niwaumbe wanadamu. Nawaomba mzingatie kwa makini kila Ninachokifanya, maana kiboko Changu kinawakaribia wanadamu tena, kwa wale wote wanaonipinga.

Pamoja na mbingu, Ninaanza kazi ambayo ni lazima Niifanye. Na kwa hiyo Ninapenya kati ya misururu ya watu na kupita kati ya mbingu na ardhi, bila ya yeyote kutambua miendo Yangu au kuyatambua maneno Yangu. Kwa hivyo, mpango Wangu unaendelea kusonga mbele kwa urahisi. Ni kwamba hisia zenu zote zimekufa ganzi kiasi kwamba hamtambui hatua za kazi Yangu. Lakini kwa kweli siku moja itakuja ambapo mtatambua nia Zangu. Leo, Ninaishi pamoja nanyi, na Ninasumbuka pamoja nanyi, na kwa muda mrefu Nimekuja kuelewa mtazamo walio nao wanadamu kunielekea. Nisingependa kuzungumza zaidi kuhusu jambo hili, sembuse kutoa mifano zaidi ya suala hili linaloumiza. Natumai tu kwamba mtayakumbuka yale yote ambayo mmeyafanya, ili tuweze kulinganisha maelezo yetu siku tutakapokutana tena. Nisingependa kumshutumu yeyote miongoni mwenu kwa njia isiyo ya kweli, kwa sababu daima Nimekuwa Nikitenda kwa njia ya haki, bila upendeleo, na kwa heshima. Bila shaka, Natumai pia kwamba nyinyi mnaweza kuwa wazi waadilifu, na kutofanya lolote lililo kinyume na mbingu na ardhi na dhamiri yenu. Hili ndilo jambo la pekee Ninalowaomba mfanye. Watu wengi huhisi kusumbuka na kuona haya kwa sababu wametenda makosa mabaya, na wengi wanajionea aibu kwa sababu hawajawahi kutenda tendo lolote zuri. Tena wapo pia wengi ambao, mbali na kutahayari kwa ajili ya dhambi zao, wanakuwa wabaya zaidi, wakiitoa kabisa barakoa inayoficha sura zao mbaya—ambayo haikuwa bado imewekwa wazi kikamilifu—ili kujaribu tabia Yangu. Sijali, wala sitilii maanani yoyote matendo ya mtu yeyote. Badala yake, Mimi hufanya kazi Ninayopaswa kufanya, iwe kukusanya habari, kuzunguka katika nchi au kufanya jambo ambalo linanipendeza. Katika nyakati muhimu, Mimi huendelea na kazi Yangu miongoni mwa wanadamu kama ilivyopangwa awali, bila kuchelewa au kuwa mapema hata kidogo, na kwa urahisi na kwa makini. Hata hivyo, katika kila hatua ya kazi Yanu, watu wengine wanawekwa pembeni, kwa sababu Ninadharau hali yao ya kujipendekeza na hali yao ya kujifanya wanyenyekevu. Wale wanaonichukiza sana hakika watatelekezwa, iwe ni kwa kupenda au kwa kutopenda. Kwa ufupi, Ningependa wale wote Ninaowadharau wawe mbali sana Nami. Ni dhahiri kwamba, Sitawahurumia wale waovu ambao wamebaki katika nyumba Yangu. Kwa kuwa siku ya adhabu ya mwanadamu inakaribia, Sina haraka ya kuzitupa nje zile nafsi zote zinazostahili dharau kutoka katika nyumba Yangu, kwa kuwa Nina mpango Wangu mwenyewe.

Huu ndio wakati Ninapoamua mwisho wa kila mtu, bali si hatua ambapo nilianza kumfinyanga mwanadamu. Mimi huandika maneno na matendo ya kila mtu katika kitabu Changu, moja baada ya lingine, njia ambayo kwayo wameitumia kunifuata, sifa zao asilia, na hatimaye jinsi ambavyo wamejistahi. Kwa njia hii, haijalishi ni mtu wa aina gani, hakuna mtu yeyote atakayeepuka mkono Wangu, na wote watakuwa pamoja na wa aina yake kama Nilivyopanga. Ninaamua hatima ya kila mtu si kwa kuzingatia umri, ukubwa, kiwango cha mateso, sembuse kiwango ambacho kwacho anataka huruma, bali kulingana na ikiwa anao ukweli. Hakuna chaguo lingine ila hili. Sharti mtambue kwamba wale wote ambao hawafuati mapenzi ya Mungu wataadhibiwa pia. Huu ni ukweli usiobadilika. Kwa hivyo, wale wote wanaoadhibiwa wanaadhibiwa kwa ajili ya haki ya Mungu na kama malipo kwa ajili ya vitendo vyao vingi viovu. Sijafanya mabadiliko yoyote katika mpango Wangu tangu uanzishwe. Ni kwamba tu, kwa binadamu, wale ambao kwao Mimi huelekeza maneno Yangu wanaonekana kupungua kwa idadi, sawa na wale Ninaowakubali kwa kweli. Hata hivyo, Ninasisitiza kwamba mpango Wangu haujawahi kubadilika; badala yake, ni imani na upendo wa mwanadamu ambavyo hubadilika daima, kufifia daima, kiasi kwamba kuna uwezekano wa kila mwanadamu kubadilika kutoka kujipendekeza Kwangu hadi kufikia hali ya kunidharau au hata kunitupa nje. Mtazamo Wangu kwenu hautakuwa baridi wala moto, hadi pale Nitakapohisi kuchukizwa na karaha, na hatimaye kutoa adhabu. Hata hivyo, katika siku ya adhabu yenu, bado Nitawaona lakini nyinyi hamtaweza kuniona tena. Kwa kuwa maisha miongoni mwenu yameshakuwa ya kuchosha na ya taabuKwangu, basi, ni wazi kwamba Nimechagua mazingira tofauti ya kuishi, afadhali kuepuka kuumizwa na maneno yenu maovu na kuwa mbali na tabia zenu mbovu kwa namna isiyovumilika, ili msinipumbaze au kunitendea kwa namna ya uzembe tena. Kabla Sijawaacha, lazima bado Ninawasihi mjiepushe kufanya yale ambayo hayaambatani na ukweli. Badala yake, mnafaa kufanya kile ambacho kinawapendeza wote, kile kilicho na manufaa kwa wote, na kile kinachofaidi hatima yenu wenyewe, la sivyo, yule anayeteseka katika maafa hatakuwa mwingine ila wewe.

Huruma Yangu inaonyeshwa kwa wale wanaonipenda Mimi na kujinyima. Kwa sasa, adhabu itakayowapata waovu, ni thibitisho hasa la tabia Yangu ya haki na, hata zaidi, ushuhuda wa hasira Yangu. Msiba utakapofika, wote wanaonipinga watalia watakapokumbwa na njaa na baa. Wale ambao wametenda aina zote za uovu, lakini ambao wamenifuata kwa miaka mingi, hawataepuka kulipia dhambi zao; wao pia, watatumbukia katika maafa, ambayo yameonekana kwa nadra kotekote katika mamilioni ya miaka, na wataishi katika hali ya taharuki na woga daima. Na wale kati ya wafuasi Wangu ambao wamekuwa waaminifu Kwangu watafurahi na kushangilia ukuu Wangu. Watakuwa na ridhaa isiyo na kifani na kuishi kwa raha ambayo Sijawahi kuwapa wanadamu. Kwa sababu Ninathamini matendo mema ya mwanadamu na kuchukia matendo yake maovu. Tangu Nilipoanza kuwaongoza wanadamu, Nimekuwa Nikitamani kwa hamu kupata kikundi cha watu ambao wanafikiria kama Mimi. Wale ambao hawana fikira sawa na Zangu, wakati ule ule, Siwasahau kamwe; Ninawachukia kabisa moyoni Mwangu daima, Nikisubiri nafasi ya kutoa adhabu kwao, jambo ambalo Nitafurahia kuona. Sasa siku Yangu imefika hatimaye, na Sihitaji kusubiri zaidi!

Kazi Yangu ya mwisho si kwa ajili ya kumwadhibu mwanadamu tu bali pia kwa ajili ya kupanga hatima ya mwanadamu. Aidha, ni kwa ajili ya kupokea shukrani kutoka kwa kila mtu kwa yale yote ambayo Nimefanya. Ninataka kila mtu aone kwamba yale yote ambayo Nimefanya ni sahihi na kwamba yote ambayo Nimefanya ni dhihirisho la tabia Yangu; si kwa uwezo wa mwanadamu, sembuse ulimwengu, ambao uliwaleta wanadamu. Kinyume na hili, mimi Ndiye Ninalisha kila kiumbe miongoni mwa vitu vyote. Bila uwepo Wangu, wanadamu wataangamia tu na kusumbuka kutokana na mashambulizi ya misiba. Hamna mwanadamu atakayeona uzuri wa jua na mwezi au dunia ya kijani kibichi; wanadamu watakumbana tu na usiku wenye baridi na bonde kali la uvuli wa mauti. Mimi tu Ndiye wokovu wa wanadamu. Mimi tu ndiye tumaini la wanadamu na zaidi ya hayo; Mimi tu Ndiye mwamba wa uwepo wa wanadamu wote. Bila Mimi, wanadamu watasimama kabisa mara moja. Bila mimi, wanadamu watakumbana na msiba mkuu na kukanyagwa na mapepo wa aina yote, hata kama hamna anayenisikiliza. Nimefanya kazi ambayo haiwezi kufanywa na yeyote yule ila mimi. tumaini Langu la pekee ni kwamba mwanadamu anaweza kunilipa kwa kutenda matendo kiasi mema. Ingawa wanaoweza kunilipa ni wachache, bado Nitahitimisha safari Yangu duniani na Nianze hatua ifuatayo ya kazi Yangu inayotokea, kwa sababu kukimbia kimbia Kwangu miongoni mwa wanadamu kwa miaka hii mingi imekuwa na matokeo mazuri, na Nimefurahishwa sana. Sijali kuhusu idadi ya watu ila kuhusu matendo yao mazuri. Kwa hali yoyote ile, Ninatumaini kwamba mtatayarisha matendo mema ya kutosha kwa ajili ya hatima yenu wenyewe. Huo ndio wakati Nitakaporidhika; la sivyo, hakuna yeyote miongoni mwenu atakayepuka maafa yatakayowafikia. Maafa haya hutoka Kwangu na bila shaka Mimi ndiye Niliyeyapanga. Ikiwa hamwezi kuonekana kuwa wema mbele Yangu, basi hamtaweza kuyaepuka maafa. Wakati wa majonzi, vitendo vyenu havikuchukuliwa kama vinavyofaa kabisa, kwa sababu imani na upendo wenu vilikuwa tupu, na mlijionyesha tu kuwa wenye woga au sugu. Kuhusu hili, Nitafanya hukumu ya mazuri au mabaya tu. Shaka Yangu inaendelea kuwa jinsi kila mmoja wenu hutenda na kujionyesha, kwa msingi ambao Nitatumia kufanya uamuzi kuhusu hatima yenu. Hata hivyo, ni sharti Niseme wazi kwamba: Sitawahurumia tena wale ambao hawakuwa waaminifu Kwangu kabisa wakati wa majonzi, kwa sababu huruma Yangu ina mipaka. Zaidi ya hayo, Simpendi yeyote yule ambaye amewahi kunisaliti Mimi, wala Sipendi kujihusisha na wale ambao hawawajali wenzao. Bila kujali huyo mtu ni nani, hii ndiyo tabia Yangu. Ni lazima Niwaambie hili: Yeyote atakayeuhuzunisha moyo Wangu hatapokea huruma kutoka Kwangu mara ya pili, na yeyote ambaye amekuwa mwaminifu Kwangu atadumu moyoni Mwangu milele.

Iliyotangulia: Ni Kristo wa Siku za Mwisho Pekee Ndiye Anayeweza Kumpa Mwanadamu Njia ya Uzima wa Milele

Inayofuata: Wewe U Mwaminifu kwa Nani?

Ulimwengu umezongwa na maangamizi katika siku za mwisho. Je, hili linatupa onyo lipi? Na tunawezaje kulindwa na Mungu katikati ya majanga?

Mipangilio

  • Matini
  • Mada

Rangi imara

Mada

Fonti

Ukubwa wa Fonti

Nafasi ya Mstari

Nafasi ya Mstari

Upana wa ukurasa

Yaliyomo

Tafuta

  • Tafuta Katika Maneno Haya
  • Tafuta Katika Kitabu Hiki

Wasiliana nasi kupitia WhatsApp