Majukumu ya Viongozi na Wafanyakazi (6)
Leo tutaendelea kushiriki juu ya majukumu ya viongozi na wafanyakazi na juu ya udhihirisho mbalimbali wa viongozi wa uwongo. Katika mkutano uliopita, tulishiriki juu ya kipengele cha sita cha majukumu ya viongozi na wafanyakazi. Maudhui makuu ya kipengele hiki ni yapi? (Kipengele cha sita ni “Kuendeleza na kukuza kila aina ya watu wenye talanta wanaostahili ili wote wanaofuatilia ukweli waweze kuwa na fursa ya kupata mafunzo na kuingia katika uhalisi wa ukweli haraka iwezekanavyo.”) Wakati uliopita, tulishiriki hasa juu ya kanuni za nyumba ya Mungu za kuwaendeleza na kuwakuza watu, na kwa nini nyumba ya Mungu huwaendeleza na kuwakuza watu. Pia tulichanganua matatizo yaliyopo kwa viongozi wa uwongo linapokuja suala la kuwaendeleza na kuwakuza watu wenye talanta wa aina mbalimbali. Basi udhihirisho mkubwa wa viongozi wa uwongo ndani ya vipengele hivi viwili ni upi? Kwa nini tunasema wao ni viongozi wa uwongo? Kuna vipengele viwili hasa. Kipengele kimoja ni kwamba viongozi wa uwongo hawaelewi kanuni za kuwaendeleza, kuwakuza, na kuwatumia watu wa aina mbalimbali, wala hawazitafuti kanuni hizi. Hawajui ni vipengele vipi vya ubora wa tabia vilivyo muhimu kwa watu kuwa navyo au ni vigezo vipi vilivyo muhimu kutimiza ili kuwa kiongozi au mfanyakazi. Kwa hivyo, wanawatumia watu ovyoovyo kwa kuzingatia mawazo na fikira zao wenyewe. Suala lingine zito ni kwamba baada ya kuwaendeleza, kuwakuza, na kuwatumia watu hawa, hawafuatilii wala kukagua kazi yao, wala hawajui jinsi wanavyoendelea vizuri, au kama wanafanya kazi halisi, au kama wanaweza kutimiza majukumu yao, au tabia yao ikoje, au kama wajibu ambao watu hawa wanafanya unawafaa, na hawazingatii kama watu wanaowaendeleza, kuwakuza, na kuwatumia wanafikia kiwango kinachohitajika na wanapatana na kanuni—hawakagui kamwe mambo haya. Viongozi wa uwongo hufikiri kwamba ni suala la kuwaendeleza watu tu, kuwapangia kazi, na basi, na kwamba majukumu yao basi yametimizwa. Hivi ndivyo viongozi wa uwongo hufanya kazi yao, na huu pia ni mtazamo na maoni yao wanapofanya kazi. Basi, je, dhihirisho hizi mbili kuu za viongozi wa uwongo yanaweza kuthibitisha kwamba hawatekelezi na hawawezi kutekeleza majukumu yao linapokuja suala la kuwaendeleza, kuwakuza, na kuwatumia watu? (Ndiyo.) Viongozi wa uwongo hawakagui kazi wala hawawachunguzi watu wa aina mbalimbali, na sembuse kuwa makini linapokuja suala la ukweli na kanuni, wakilinganisha udhihirisho na hali za watu wa aina mbalimbali na ukweli wanaouelewa na kanuni zinazohitajika na nyumba ya Mungu; pia hawawezi kupambanua kama ubinadamu na sifa bainifu za watu wa aina mbalimbali zinapatana na kanuni zinazohitajika za nyumba ya Mungu za kuwatumia watu. Kwa sababu hizi, wamechanganyikiwa na ni hobelahobela hasa linapokuja suala la kuwaendeleza na kuwatumia watu na kuwapangia kazi, na wanachofanya ni kufanya mambo kwa njia isiyo ya dhati tu na kufanya kazi ya juu juu kwa kuzingatia mawazo na fikira zao. Kwa kuwa hali iko hivi, ikiwa viongozi wa uwongo wataombwa kuwatumia watu wa aina mbalimbali kwa busara na ipasavyo kwa kuzingatia ubinadamu na sifa zao bainifu, je, wanaweza kufanikisha hili? (Hapana, hawawezi.) Hebu tuweke kando kwa sasa jinsi ubora wa tabia wa viongozi wa uwongo ulivyo. Tukiangalia tu mtazamo wao kwa kazi na njia na mbinu zao za kufanya kazi, na ukweli kwamba hawafanyi kazi yoyote halisi kabisa, bali hushughulikia tu mambo ya jumla na kufanya kazi kidogo ya juu juu inayowaweka katika umaarufu, na ukweli kwamba hawafanyi kabisa kazi ya kuwapa watu ukweli, na hawajui jinsi ya kutumia ukweli kutatua matatizo—yote haya yanatosha kuthibitisha kwamba viongozi wa uwongo hawawezi kufanya kazi halisi ya kanisa. Kwa kuzingatia tu ukweli kwamba viongozi wa uwongo hawafanyi kazi halisi, au kujihusisha kwa kina na ndugu na dada ili kutatua matatizo halisi, na badala yake hujikweza na kutoa amri, inaweza kuthibitishwa kwamba hawawezi kutekeleza vipengele vyote vya kazi ya kanisa vizuri ili kuwaendeleza na kuwakuza watu kwa ajili ya nyumba ya Mungu.
Kipengele cha Saba: Kuwatenga na kuwatumia watu wa aina tofauti kwa busara, kwa kuzingatia ubinadamu na nguvu zao, ili kila mmoja atumike kadiri ya ubora wake (Sehemu ya Kwanza)
Kuwatumia Watu wa Aina Mbalimbali kwa Busara Kulingana na Ubinadamu Wao
Ufahamu wenu ni upi kuhusu jinsi ya kuwapanga na kuwatumia watu wa aina mbalimbali? (Nyumba ya Mungu ina viwango tofauti vinavyohitajika kwa ajili ya watu wa aina mbalimbali wanaoendelezwa na kukuzwa, na watu wanapaswa kuendelezwa na kutumiwa kulingana na kanuni na viwango vya nyumba ya Mungu vya kuwaendeleza watu. Ikiwa watu wengine wanafaa kuwa viongozi na wafanyakazi, basi wanapaswa kukuzwa kama viongozi, wafanyakazi, na wasimamizi; ikiwa watu wengine wana ustadi wa kitaaluma katika fani fulani, basi wajibu wanaofanya unapaswa kupangwa kulingana na ustadi wao wa kitaaluma, ili watengwe na kutumiwa kwa busara.) Kuna yeyote aliye na la kuongeza? (Jambo lingine ni kuwapima watu kulingana na ubinadamu wao. Ikiwa ubinadamu wa mtu ni mzuri kiasi, na anapenda ukweli, na ana uwezo wa kufahamu, basi anafaa kuendelezwa na kukuzwa. Ikiwa ubinadamu wake ni wa wastani, lakini ana sifa bainifu na anaweza kutekeleza wajibu katika nyumba ya Mungu na kutumikia, basi mtu wa aina hii anaweza pia kupewa wajibu unaofaa kulingana na sifa zake bainifu, ili atumike kadiri ya ubora wake. Ikiwa yeye ni mtu mwenye ubinadamu mbaya kiasi na anaweza kusababisha vurugu na usumbufu, basi kumfanya atekeleze wajibu kutaleta madhara zaidi kuliko faida, kwa hivyo haifai kumpangia wajibu.) Ikiwa watu watatofautishwa kulingana na ubinadamu wao, basi maadamu wao si watu waovu, hawasababishi vurugu au usumbufu, na wanaweza kutekeleza wajibu, basi wanapatana na kanuni za nyumba ya Mungu za kuwatumia watu. Aina nyingine ambao haiwezi kutumiwa, mbali na watu waovu na roho waovu, ni wale wenye akili pungufu, yaani, wale wasiotimiza chochote, wasioweza kufanya jambo lolote, wasioweza kujifunza taaluma, wasioweza kushughulikia mambo rahisi ya jumla, ambao hawawezi hata kufanya kazi ya nguvu—watu wenye akili na ubinadamu pungufu hawawezi kutumiwa. Ni watu gani ndio wako katika kundi hili la wenye akili pungufu? Wale wasioelewa lugha ya binadamu, wasio na ufahamu safi, ambao daima huelewa mambo visivyo, ambao hufanya vitu kimakosa, na kutoa majibu yasiyohusiana na maswali, na walio aina moja na mabwege au wenye ulemavu wa akili—hawa wote ni watu wenye akili pungufu. Kisha kuna watu wenye mawazo yasiyoingia akilini ambao huelewa mambo ya kila aina tofauti na watu wa kawaida—wao pia wana tatizo la akili. Je, akili pungufu inajumuisha kutoweza kujifunza chochote? (Ndiyo, inajumuisha.) Basi je, kutoweza kujifunza jinsi ya kuandika makala kunahesabiwa kama kuwa na akili pungufu? (Hapana, hakuhesabiwi.) Watu wa aina hii hawahesabiwi. Chukua kwa mfano kujifunza kuimba na kucheza densi, kujifunza ujuzi wa kompyuta, au kujifunza lugha ya kigeni; kutoweza kujifunza mambo haya hakuhesabiwi kama kuwa na akili pungufu. Basi, kutoweza kujifunza mambo ya aina gani kunaonyesha akili pungufu? Kwa mfano, watu wengine wana maarifa kiasi, lakini hawawezi kujifunza jinsi ya kupanga maneno yao wanapozungumza na wengine. Basi je, watu wa aina hii wanaweza kushiriki juu ya ukweli, kuomba, na kuwasiliana na wengine kwa kawaida wanapomwamini Mungu? (Hapana, hawawezi.) Wanapokuwa na wazo akilini mwao au wanapokuwa katika hali fulani, na wanataka kujifungua na kuzungumza na watu kulihusu na kutafuta njia ya suluhisho, hutafakari kwa siku nyingi, na hawajui pa kuanzia au jinsi ya kujieleza. Mara tu wanapozungumza, wao huchanganyikiwa na kuongea kwa njia iliyovurugika, midomo yao huonekana kana kwamba haziwasikilizi na mawazo yao yametawanyika. Kwa mfano, unawaambia, “Leo hali ya hewa ni nzuri na jua linawaka,” nao watajibu, “Jana kulinyesha na kulitokea ajali ya gari katika barabara ile.” Hawapo kwenye mstari mmoja na wale wanaozungumza nao. Je, mtu wa aina hii ana akili pungufu? (Ndiyo, ana akili pungufu.) Kwa mfano, kama wanaumwa na kichwa na uwaulize kuna shida gani, watasema kwamba moyo wao haujisikii vizuri. Jibu hili halihusiani na swali, sivyo? (Ndiyo, halihusiani.) Huku ni kuwa na upungufu mkubwa wa akili. Kuna watu wengi sana kama hawa. Mnaweza kutoa mfano? (Watu wengine daima hutoka nje ya mada wanapojibu maswali, hawaelewi kabisa kile watu wengine wanachowauliza.) Kutoka nje ya mada mara kwa mara unapozungumza—hii ni akili pungufu. Kisha kuna watu wanaoshindwa kutofautisha kati ya watu wa ndani na watu wa nje wanapozungumza, na wakati mwingine hujisaliti wanapozungumza, bila hata kujua—hii, pia, ni akili pungufu. Kwa mfano, baadhi ya ndugu na dada huishi na wanafamilia wasioamini, wanaowauliza, “mungu wenu huwaambia mfanye nini?” Wanajibu: “Mungu tunayemwamini ni mwema sana. Yeye hutufundisha kuwa watu waaminifu, na kwamba haturuhusiwi kumdanganya yeyote, na ni lazima tuzungumze kwa uaminifu na kila mtu.” Kwa juu juu, inaonekana kana kwamba wanashuhudia kazi anayoifanya Mungu, wakimtukuza Mungu, na kuwafanya wasikilizaji wao wawe na hisia nzuri juu ya waumini na kuwaamini, lakini je, hivi ndivyo ilivyo kweli? Wasioamini watasema nini wanaposikia hili? Watasema, “Kwa kuwa mungu wenu amewaambia muwe watu waminifu, basi tuambieni ukweli: Kanisa lenu lina pesa kiasi gani? Nani anayetoa matoleo mengi zaidi? Kiongozi wa kanisa lenu ni nani? Mna mahali pangapi pa mikutano?” Ungeshtuka kwa hilo, sivyo? Je, watu kama hawa si mabwege? Kwa nini unazungumza na maibilisi na wasioamini kuhusu kuwa mtu mwaminifu? Kwa kweli si lazima uwe mwaminifu kiasi hicho mbele za Mungu. Basi kwa kung’ang’ania ukweli huo na wasioamini, je, si unajisaliti? Je, huku si kujichimbia shimo na kujitegea mtego? Je, wewe si baradhuli? Unapoufungua moyo wako au kuzungumza kwa uaminifu na mtu, ni lazima uzingatie unazungumza na nani—ikiwa ni ibilisi au Shetani, je, unaweza kumwambia kile kinachoendelea kweli? Kwa hivyo linapokuja suala la watu kama hawa, ni muhimu kuwa “wenye hekima kama nyoka, na wapole kama njiwa”—hili ni fundisho la Mungu kwa wanadamu. Baradhuli hawajui kufanya hivi. Wanajua tu kushikilia kanuni, na kusema mambo kama, “Sisi waumini ni waaminifu sana, hatumdanganyi yeyote. Angalieni ninyi wasioamini, mmejaa uongo, ilhali sisi sote tunasema ukweli.” Na baada ya wao kusema ukweli, watu hupata la kuwashikia. Je, huku si wao kushindwa kutofautisha kati ya watu wa ndani na watu wa nje? Je, si ni kuwa na kasoro akilini? Wanaelewa mafundisho fulani lakini hawajui jinsi ya kuyatumia. Wanapiga kelele za kauli mbiu kisha wanahisi kwamba wao ni wa kiroho kweli, na kufikiri kwamba wanaelewa ukweli na wanamiliki uhalisi wa ukweli, na hujionyesha kila mahali, lakini mwishowe, Mashetani na ibilisi hutumia fursa hii na kuitumia dhidi yao. Hii ni akili pungufu.
Tumetoka kuzungumzia aina kadhaa za watu wenye akili pungufu. Aina moja ni wale wasioelewa lugha ya binadamu, na wanaoshindwa kuelewa na kufahamu kiini na hoja muhimu za maneno ya watu wengine; aina nyingine ni watu vichwa ngumu, wasioweza kutimiza chochote, na wasioweza kufahamua kanuni au hoja muhimu haijalishi wanafanyaje; aina nyingine zaidi ni wale walio na maoni ya kushikilia imani kupita kiasi na ya kipuuzi kupita kiasi kuhusu kila kitu. Bado aina nyingine ni wale wasioweza kujifunza chochote, na ambao hawawezi hata kujifunza jinsi ya kuzungumza au kupiga soga, au jinsi ya kueleza mawazo na maoni yao waziwazi ili wengine waweze kuwaelewa; ingawa wanajua kusoma na kuandika kiasi, hawawezi kupanga maneno yao vichwani mwao, au kuzungumza waziwazi, wala hawawezi kueleza maoni sahihi, au kutimiza chochote. Hawa wote ni watu wenye akili pungufu. Haijalishi ni ufundi au ustadi gani wanaojifunza, daima hawawezi kufahamu kanuni na taratibu. Hata wakifanya ufundi au ustadi vizuri pindi fulani, ni kwa bahati nasibu; hawajui jinsi walivyofanya vizuri. Wakati unaofuata wanaposhindwa kuifanya vizuri, hawajui kwa nini imekuwa hivyo pia. Hawawezi kujifunza chochote au kuwa stadi katika hicho. Wakiombwa kujifunza ufundi au ustadi wa kiufundi, haijalishi wanatumia muda gani kujifunza, watafahamu tu nadharia. Wamesikiliza mahubiri kwa miaka mingi sana lakini hawajaelewa ukweli. Wakiombwa kuchukua maneno haya na kauli hizi maalum ambazo nyumba ya Mungu hushiriki mara kwa mara, na kuzigeuza kuwa kanuni na njia ya utendaji, hawataweza kufanya hivyo hata wakifanya kazi mpaka kufa, na haijalishi wanafundishwaje. Hili linathibitisha kwamba watu hawa wana akili pungufu. Watu wengine hupata matokeo yale yale hasa kutokana na kufanya jambo wakiwa na umri wa miaka 50 au 60 kama walivyofanya wakiwa na miaka 30, bila kupata maendeleo yoyote. Hawajafanikiwa kujifunza jambo hata moja maishani mwao. Hawajapoteza muda wao bure, wao ni waangalifu sana na wanajitahidi, lakini hawajafanikiwa kujifunza chochote; hii inaonyesha kwamba wana akili pungufu. Kwa kuzingatia kile ambacho tumeshiriki, upeo wa kile kinachohesabiwa kuwa akili pungufu umekuwa mpana zaidi, sivyo? Je, ninyi wenyewe mngehesabiwa kuwa wenye akili pungufu? (Ndiyo.) Kidogo, kwa kiwango kikubwa au kidogo. Kwa nini Nasema hivyo? Watu wengi wamesikiliza mahubiri kwa miaka mitano, lakini bado hawaelewi ukweli ni nini, au nia za Mungu ni zipi; na watu wengine wamesikiliza mahubiri kwa miaka 10, au hata miaka 20 au 30 na bado hawaelewi uhalisi wa ukweli ni nini na maneno na mafundisho ni nini, midomo yao imejaa mafundisho, na wanayaropoka kwa ufasaha—hili ni tatizo la akili zao. Tukiacha kando ufahamu wa ukweli kwa sasa, hebu tuseme tu kwamba watu huonyesha udhihirisho ufuatao kwa baadhi ya mambo ya nje na mambo ya akili ya kawaida katika maisha ya binadamu: Haijalishi wamekuwa wakifanya jambo kwa miaka mingapi, hali yao, mazingira yao, na mtazamo wao hubaki vile vile kama walipoanza kujifunza, na haijalishi wanaongozwaje, wanafundishwaje, au wanatendaje, bado hawapati maendeleo yoyote. Hii ni akili pungufu.
Kuwachagua na kuwatumia watu kwa kuzingatia ubinadamu wao kunalingana na kanuni; basi Niambieni, je, tuwakuze na kuwatumia watu walio na ubinadamu duni, akili pungufu, au kazi ya roho waovu? Hilo halikubaliki kabisa. Mbali na aina hizi kadhaa za watu wasiopatana na kanuni za nyumba ya Mungu za kuwatumia watu, watu wengine wengi wanaweza kutumiwa kwa busara kulingana na ubinadamu wao. Kwa wale wenye ubinadamu wa wastani, ambao ubinadamu wao hauwezi kuitwa mbaya wala mzuri, wanaweza tu kuwa washiriki wa timu wa kawaida. Kwa wale walio na ubinadamu mzuri kiasi, walio na busara kiasi na wenye dhamiri, wanaopenda vitu chanya, walio wanyofu hasa, wana hisia ya haki, na wanaoweza kutetea masilahi ya nyumba ya Mungu, mkazo unaweza kuwekwa katika kuwakuza na kuwatumia watu hawa. Kuhusu iwapo kuwakuza na kuwatumia kama viongozi au viongozi wa timu, au kufanya kazi fulani muhimu, hili linategemea ubora wa tabia na sifa zao bainifu. Huku ni kupima jinsi ya kuwatumia watu wa aina mbalimbali kulingana na ubinadamu wao.
Kuwatumia Watu Wa Aina Mbalimbali Kwa Busara Kulingana Na Uwezo Wao
Hebu tuzungumze zaidi kuhusu jinsi ya kuwatumia watu wa aina mbalimbali kulingana na sifa zao bainifu. Mbali na ubora wa tabia, watu wengine pia wana ustadi fulani wa kitaaluma ambao wamebobea. Neno “sifa bainifu” linamaanisha nini? (Kuwa na ustadi katika fani maalum, kama vile kuweza kutunga muziki, kupiga ala ya muziki, au kuchora picha.) Kuelewa nadharia ya muziki, sanaa, na pia densi na uandishi—hizi zote ni sifa bainifu. Uigizaji na uelekezaji ni sifa bainifu vinavyohusiana na utengenezaji wa filamu, tafsiri ni kipaji cha lugha, na utengenezaji wa video na madoido maalum pia ni sifa bainifu ndani ya fani maalum. Tunapozungumzia sifa bainifu, tunarejelea ustadi wa kitaaluma unaohusiana na kazi kuu ya kanisa. Watu wengine tayari wana kiwango cha msingi cha ustadi, na watu wengine hujifunza mambo haya baada ya kuja katika nyumba ya Mungu. Ikiwa mtu ana ustadi wa msingi lakini ubinadamu wake haufikii kiwango kinachostahili, na yeye ni mmoja wa wale wenye akili pungufu, mtu mwovu, au roho mwovu, basi hawezi kutumiwa. Ikiwa ubinadamu wa mtu unafikia kiwango kinachostahili na ana kipaji ambacho nyumba ya Mungu inakihitaji, basi anaweza kuendelezwa, kukuzwa, na kutumiwa, akapangiwa timu inayolingana na sifa zake bainifu, au inayohusiana na ustadi wa kitaaluma alio nao, na kuanza kazi mara moja. Watu wengine bado hawana kipaji cha kitaaluma, lakini wako tayari kujifunza, na wanashika mambo haraka. Ikiwa ubinadamu wao unafikia kiwango kinachostahili, basi nyumba ya Mungu inaweza kuwakuza na kuwatengenezea mazingira ya wao kujifunza, na watu kama hao wanaweza pia kutumiwa. Kwa muhtasari, ugawaji wa wajibu unategemea ubora wa tabia na sifa bainifu a watu, na kadiri iwezekanavyo, watu wenye sifa bainifu tofauti wanapaswa kupangiwa kufanya kazi ndani ya fani zao za utaalamu, ili waweze kudhihirisha sifa hizi bainifu. Ikiwa sifa zao bainifu hazihitajiki tena na nyumba ya Mungu, wanaweza kupangiwa kufanya chochote wanachoweza kufanya, kulingana na ubora wa tabia na ubinadamu wao; huku kunaitwa kuwatumia watu kwa busara. Ikiwa nyumba ya Mungu bado inahitaji sifa zao bainifu, wanapaswa kuruhusiwa kuendelea kutekeleza wajibu wao katika fani hii, na hawawezi kuhamishwa kiholela, isipokuwa kuna watu wengi sana wanaofanya kazi katika taaluma hii, ambapo katika hali hiyo idadi ya watu inapaswa kupunguzwa kulingana na hali kwa kuwapangia wale walio na uwezo mdogo zaidi katika taaluma yao wajibu mwingine; huku ni kuwatumia watu kwa busara.
Kuna aina fulani ya mtu ambaye hana ujuzi wowote maalum—anaweza kuandika makala kiasi, anaweza kuimba na kupatia, na kujifunza jinsi ya kufanya chochote, lakini yeye si stadi zaidi katika mambo haya. Yeye ni stadi zaidi katika nini? Ana ubora wa tabia kiasi, ana hisia ya haki kiasi, na ana utambuzi katika kuwapima na kuwatumia watu. Zaidi ya hayo, hasa anamiliki ustadi wa kupangilia. Ukimpa mtu kama huyo kazi, anaweza kuwapanga watu waifanye. Wakati huo huo, anamiliki uwezo wa kazi; yaani, ukimpa kazi, ana uwezo wa kuifanya vizuri na kuikamilisha. Ana mpango akilini, wenye hatua na muundo. Anajua jinsi ya kuwatumia watu, jinsi ya kugawanya muda, na nani wa kumtumia kwa kazi hii. Tatizo likitokea, anajua jinsi ya kujadili suluhisho na kila mtu. Anajua jinsi ya kusawazisha na kutatua mambo haya yote. Mtu kama huyu si kwamba anamiliki uwezo wa kazi tu, bali pia anazungumza vizuri kiasi. Maneno yake ni wazi na yenye utaratibu, na hayawachanganyi watu. Anapokuwa amegawa kazi, kila mtu huelewa waziwazi na anajua kile kila mtu anapaswa kufanya; hakuna mtu anayekaa bila kazi na hakuna mapungufu katika kazi. Maelezo yake ya undani wa kazi pia ni wazi na yenye utaratibu kiasi, na kwa masuala magumu hasa, hutoa uchambuzi, ushirika, na kuorodhesha undani ili kila mtu aelewe masuala hayo, ajue jinsi ya kufanya kazi, na ajue jinsi ya kuendelea. Zaidi ya hayo, anaweza pia kushiriki juu ya njia zipi za kutenda zinaweza kuwa na kasoro, ni mbinu zipi za kufanya kazi zitaathiri ufanisi, ni nini watu wanapaswa kuzingatia wakati wa kazi yao, na kadhalika. Yaani, yeye hufikiri zaidi ya wengine kabla ya kuanza kazi—hufikiri kwa undani zaidi, kwa uhalisi zaidi, na kwa upana zaidi kuliko wengine. Kwa upande mmoja, ana akili, na kwa upande mwingine, ana ufasaha. Kuwa na akili kunamaanisha anafanya mambo kwa utaratibu, kwa hatua na kulingana na mpango, na kwa uwazi mkuu. Kuwa na ufasaha kunamaanisha kwamba anaweza kutumia lugha kueleza, waziwazi na kwa njia inayoeleweka, mawazo, mipango, na mahesabu yaliyo akilini mwake, na kwamba anajua jinsi ya kuzungumza kwa urahisi na kwa ufupi, ili wasikilizaji wake wasichanganyikiwe. Anajieleza kwa lugha iliyo wazi, sahihi, ya kweli, na inayofaa hasa. Huku ndiko kuwa na ufasaha. Watu kama hawa wana ufasaha, wanamiliki uwezo wa kazi, ustadi wa kupangilia, na juu ya hayo, wana hisia ya uwajibikaji, na wana hisia ya haki kiasi. Wao sio watu wa kuwapendeza wengine au watu wa kusawazisha mambo tu. Wanapoona watu waovu wakisababisha vurugu na usumbufu kwa kazi ya kanisa, au mabwege na watu duni wasioshughulikia mambo yao ipasavyo na kutenda kwa ujanja, hukasirika, huhisi kuchukizwa, na wanaweza kutatua na kushughulikia matatizo haya mara moja, na kulinda kazi na masilahi ya nyumba ya Mungu. Kuwa na hisia ya uwajibikaji na hisia ya haki—je, udhihirisho huu si sifa bainifu za ubinadamu wa mtu wa aina hii? (Ndiyo.) Watu kama hawa huenda wasiwe wazuri katika kujumuika na watu, au huenda wasiwe stadi sana katika ujuzi wowote maalum wa kitaaluma, lakini ikiwa wanamiliki sifa nilizoeleza punde tu, wanaweza kukuzwa kama viongozi na wafanyakazi. Sifa hizi pia ni sifa zao bainifu, yaani, wana ufasaha, wanamiliki uwezo wa kazi, ustadi wa kupangilia, na wana hisia ya haki kiasi. Kuwa na hisia ya haki ni muhimu sana. Je, watu waovu na wapinga Kristo wana hisia ya haki? (Hapana, hawana.) Wapinga Kristo wana asili ovu; haiwezekani kwao kuwa na hisia ya haki. Jambo jingine muhimu ni kwamba mtu wa aina hii ana ufahamu wa kiroho na uwezo wa kufahamu ukweli; hili linahusiana na ubora wa tabia yake. Sifa bainifu za mtu wa aina hii zinarejelea sifa hizo za ubinadamu na vipawa nilivyotaja punde tu, pamoja na viwango vitatu vya kuwa na uwezo wa kufahamu ukweli, kubeba mzigo kwa ajili ya kanisa, na kumiliki uwezo wa kazi. Watu kama hao wanaweza kukuzwa kama viongozi; hakuna tatizo na hilo. Mbali na kuwa na akili na ubora wa tabia, kiongozi lazima awe na uwezo wa kufahamu ukweli, na awe na ustadi wa kupangilia na uwezo wa kazi katika kazi yake, na pia ufasaha. Watu wengine wana ubora mzuri sana wa tabia, wanamiliki ufahamu wa kiroho, lakini wakati wa kushiriki katika mikutano unapofika, wanavuruga kabisa kile wanachojaribu kusema, hawana kabisa uwezo wa kupanga maneno yao, na kile wanachosema hakina mantiki kabisa. Je, watu kama hao wanaweza kukuzwa kama viongozi? (Hapana, hawawezi.) Watu wengine kwa shida wanaweza kuzungumza na watu wachache sana; wanaweza kushiriki juu ya hali fulani, maoni, na ufahamu wa ukweli, na wanaweza kuwategemeza, kuwapatia, na kuwasaidia wengine, lakini wakiwa karibu na watu wengi zaidi hawathubutu kusema, na huhisi hofu, na wanaweza hata kuwa na wasiwasi hadi kufikia kiwango cha kulia. Je, watu kama hao wanaweza kukuzwa? Kwa mtu wa aina aliye na ubinadamu dhaifu na mwoga kiasi, na aliye na hofu ya umati, ikiwa anamiliki ubinadamu, sifa bainifu, na uwezo wa kufahamu wa kuwa kiongozi, anaweza kukuzwa kuwa kiongozi wa timu au kiongozi wa kanisa. Kwanza wakuzeni na kuwapa mafunzo tu; baada ya wao kupitia kwa kipindi fulani, watapata utambuzi na hivyo kuwa wajasiri zaidi kidogo, na hawataogopa tena kuzungumza au kuwa na hofu ya umati. Kwa muhtasari, linapokuja suala la wale walio na sifa za ubinadamu na sifa bainifu tulizozizungumzia punde tu, wanaweza kukuzwa kuwa viongozi maadamu ubinadamu wao unafikia kiwango kinachostahili. Kama tulivyosema wakati uliopita, ili mtu akuzwe kama kiongozi, si lazima aelewe ukweli wote, aweze kumtii Mungu, awe na moyo unaomcha Mungu, na kadhalika. Si lazima kabisa kutimiza vigezo hivi. Ikiwa mtu anamiliki ubora fulani wa tabia, ana ufahamu wa kiroho, na anaweza kuukubali ukweli, basi anaweza kuendelezwa na kukuzwa. Je, huku si kuwatumia watu kwa busara? (Ndiyo.) Kigezo muhimu zaidi ni iwapo ubinadamu wa mtu unafikia kiwango kinachostahili au la.
Watu wengine, baada ya kusikiliza kile ambacho Nimesema, wanahisi kwamba tayari wanafikia vigezo vya kuwa kiongozi na wanapaswa kuendelezwa. Huu ni uelewa usio sahihi kwa upande wao, sio? Je, kuwa kiongozi ni jambo rahisi namna hiyo? Wanawaza, “Mimi hupanga mambo vizuri, nina ustadi wa kupangilia, na nina ufasaha wa kuongea, kwa kuwa naweza kueleza hata mambo tata zaidi kwa uwazi, kwa hivyo kwa nini nyumba ya Mungu hainiendelezi? Kwa nini akina ndugu hawanichagui kuwa kiongozi? Imekuwaje viongozi wa ngazi za juu wanakosa kuona kwamba nina talanta?” Usijali. Ikiwa kwa kweli unafikia vigezo vya kuwa kiongozi au mfanyakazi, basi punde si punde, utaendelezwa na kuruhusiwa kujifundisha. Jambo la muhimu sasa ni kwamba ni lazima ujifundishe sana katika kutenda ukweli na kushughulikia mambo kulingana na kanuni, na kwa kuchukua hatua uwasaidie wengine, na kutatua matatizo halisi kwa ajili ya watu wateule wa Mungu. Watu wateule wa Mungu wanapoona kwamba una ubora wa tabia na unaweza kutatua matatizo halisi, watakupendekeza na kukuchagua. Ikiwa huchukui hatua ya kufanya kazi halisi kiasi, na unangoja tu siku ambapo utachaguliwa ghafla kama kiongozi au kuendelezwa kama jambo la kipekee na Aliye juu, hilo halitatokea kamwe. Ni lazima ufanye kazi fulani halisi ili kila mtu aione; punde tu kila mtu anapoona sifa zako bainifu na kuhisi kwamba wewe ni mtu anayepaswa kuendelezwa, kustawishwa, na kutumiwa, kiasili watakupendekeza na kukuchagua. Ikiwa unahisi sasa hivi kwamba unafaa kuwa kiongozi, lakini hakuna aliyekuchagua, na nyumba ya Mungu haijakuendeleza, kwa nini iko hivyo? Jambo moja ni hakika: Bado hujatambuliwa machoni pa akina ndugu. Labda ni ubinadamu wako, labda ni ufuatiliaji wako, au labda ni sifa zako bainifu au ubora wako wa tabia. Ikiwa akina ndugu hawatambui au hawaiidhinishi mojawapo ya vipengele hivi, hawatakuchagua au kukupendekeza. Kwa hivyo lazima uendelee kufanya kazi kwa bidii, uendelee kufuatilia na kujifundisha, na unapoelewa ukweli hakika na unaweza kushughulikia mambo kulingana na kanuni, watu watakupendekeza na kukuchagua kiasili; ni hali ya vitu kufuata mkondo wa asili hali ikiwa sawa. Hakuna haja ya kutazamia daima kuwa kiongozi au kulifikiria wakati wote; hili ni tamanio la kupita kiasi. Unapaswa kuwa na moyo wa kawaida, uwe mtu anayefuatilia ukweli, ujali nia za Mungu, na ujifunze kuwa mtiifu na mvumilivu. Huwezi kuufuatilia uongozi kwa upofu; hiyo ni tamaa ya makuu, na hiyo si njia sahihi. Hupaswi kuwa na tamaa hii ya makuu na matamanio wakati wote. Hata kama kwa kweli una ubora wa tabia, ni lazima usubiri hadi uingie katika uhalisi wa ukweli kabla ya kuweza kumudu jukumu la kutumika kama kiongozi au mfanyakazi. Ikiwa huelewi ukweli na hujui jinsi ya kutenda ukweli, basi hata ukichaguliwa kuwa kiongozi au mfanyakazi, hutaweza kufanya kazi yoyote halisi na itabidi utimuliwe na kuondoshwa, jambo ambalo hutokea mara nyingi. Ikiwa unajiona kwamba unafaa kuwa kiongozi, ukiwa na talanta, ubora wa tabia, na ubinadamu wa uongozi, lakini nyumba ya Mungu haijakuendeleza na akina ndugu hawajakuchagua, unapaswa kulichukuliaje jambo hilo? Kuna njia ya utendaji hapa unayoweza kufuata. Ni lazima ujijue kikamilifu. Angalia uone kama kiini cha jambo hilo ni kwamba una tatizo katika ubinadamu wako, au kwamba kufichuliwa kwa kipengele fulani cha tabia yako potovu huwachukiza watu; au kama ni kwamba huna uhalisi wa ukweli na huwasadikishi wengine, au kwamba utendaji wa wajibu wako haufikii kiwango kinachostahili. Ni lazima utafakari juu ya mambo haya yote na uone ni wapi hasa unapopungukia. Baada ya kutafakari kwa muda na kupata tatizo lako liko wapi, ni lazima utafute ukweli mara moja ili ulitatue, na uingie katika uhalisi wa ukweli, na ujitahidi kufikia mabadiliko na kukua, ili wale walio karibu nawe wanapoliona, watasema, “Siku hizi, amekuwa bora zaidi kuliko awali. Anafanya kazi kwa uthabiti na anachukulia kazi yake kwa uzito, na anazingatia hasa kanuni za ukweli. Hafanyi mambo kwa haraka au kwa kijuujuu tu, na yeye ni mwangalifu na mwenye kuwajibika zaidi kuhusu kazi yake. Hapo awali alipenda kuzungumza maneno makubwa mara kwa mara, na akijionyesha kila mara, lakini sasa amejishusha zaidi na si jeuri tena. Hata kama anaweza kufanya mambo machache, hajisifu kulihusu, na anapomaliza kitu, hulitafakari tena na tena, kwa hofu ya kufanya kosa. Anatenda kwa uangalifu zaidi kuliko awali, na akiwa na moyo umwogopao Mungu—na muhimu zaidi, anaweza kushiriki kuhusu ukweli ili kutatua matatizo kadhaa. Hakika, amekua.” Wale walio karibu nawe ambao wameshirikiana nawe kwa muda wanagundua kwamba umepitia mabadiliko na ukuaji dhahiri; katika maisha yako ya kibinadamu, mwenendo wako na ushughulikiaji wa mambo, na katika mtazamo wako kwa kazi yako, na katika utendaji wako wa kanuni za ukweli vilevile, unatia bidii zaidi kuliko hapo awali, na una msimamo thabiti katika usemi na matendo yako. Akina ndugu huyaona haya yote na kuyatia moyoni. Labda, basi, utaweza kugombea kama mgombea katika uchaguzi ujao, na utakuwa na tumaini la kuchaguliwa kuwa kiongozi. Ikiwa unaweza kutekeleza wajibu fulani muhimu kwa kweli, utapata baraka ya Mungu. Ikiwa kwa kweli unajitwika mzigo na una hisia kama hiyo ya wajibu, na unataka kubeba mzigo, basi fanya haraka na ujifundishe. Zingatia kutenda ukweli na ufikie hatua ya kutenda kwa kanuni. Punde tu unapokuwa na uzoefu wa maisha na unaweza kuandika makala za ushuhuda, utakuwa umekua kweli. Na ikiwa unaweza kumshuhudia Mungu, basi hakika unaweza kupata kazi ya Roho Mtakatifu. Ikiwa Roho Mtakatifu anafanya kazi ndani yako, inamaanisha kwamba Mungu anakutazama kwa fadhila, na Roho Mtakatifu akikuongoza, fursa yako itakuja hivi karibuni. Unaweza kuwa na mzigo sasa, lakini kimo chako hakitoshi na uzoefu wako wa maisha ni wa juu juu sana, kwa hivyo hata kama ungekuwa kiongozi, ungeanguka kwa urahisi. Ni lazima ufuatilie kuingia katika uzima, utatue matamanio yako ya kupita kiasi kwanza, uwe mfuasi kwa hiari, na ufikie kumtii Mungu kweli, bila maneno ya malalamiko kwa chochote Anachopanga au kupangilia. Unapokuwa na kimo hiki, fursa yako itakuja. Kwamba unataka kubeba mzigo mzito, kwamba una mzigo huu, ni jambo jema. Linaonyesha kwamba una moyo wenye bidii ya kutafuta maendeleo na kwamba unataka kujali nia za Mungu na kufuata mapenzi ya Mungu. Hii si tamaa ya makuu, bali ni mzigo wa kweli; ni wajibu wa wale wanaofuatilia ukweli na lengo la ufuatiliaji wao. Huna nia zozote za ubinafsi na hufanyi kwa ajili yako mwenyewe, bali ni kumshuhudia Mungu na kumridhisha Yeye—hiki ndicho kinachobarikiwa zaidi na Mungu, na Yeye atakufanyia mipango inayofaa. Kwa sasa, jihusishe tu na kufuatilia kuingia katika uzima, timiza wajibu wako ipasavyo kwanza, na kisha uandike makala chache za ushuhuda wa kupitia ili kumshuhudia Mungu. Ikiwa shuhuda zako ni za kweli na za vitendo, watu watakaozisoma watakuheshimu na kukupenda, na watakuwa tayari kushirikiana nawe na kukupendekeza, na hivyo fursa yako itakuja. Kwa hivyo, ni lazima kabisa ujizatiti na ukweli kabla ya fursa kuja. Kwanza uwe na uzoefu wa vitendo, na kisha kiasili utakuwa na ushuhuda wa kweli; matokeo ya wajibu wako yatakuwa bora zaidi na zaidi, na wakati huo, hutaweza kujificha hata kama ungetaka, na akina ndugu walio karibu nawe watakupendekeza. Ni kwa sababu watu walio na uhalisi wa ukweli hawahitajiwi tu na nyumba ya Mungu, bali pia na watu wateule wa Mungu; kila mtu anapenda kushirikiana na watu walio na uhalisi wa ukweli, na kila mtu anapenda kuhusiana na marafiki walio na uhalisi wa ukweli. Ukipitia hadi kiwango hiki, na kila mtu aone kwamba una ushuhuda wa kweli na akiri kwamba una uhalisi wa ukweli, hutaweza kuepuka kuwa kiongozi hata kama ungetaka, na akina ndugu watasisitiza kukuchagua. Je, si hivyo ndivyo ilivyo? Mwana mpotevu anapogeuka na kumrudia Mungu, Mungu hufurahishwa, huwa na furaha, na hufarijika moyoni Mwake. Kama mtu aliye na uhalisi wa ukweli, ungewezaje kutotumiwa na Mungu? Hilo halingewezekana. Nia ya Mungu ni kupata watu wengi zaidi wanaoweza kumshuhudia Yeye; ni kuwakamilisha wote wanaompenda Yeye, na kufanya kikundi cha watu kiwe kamili ambao ni wenye moyo na nia moja na Yeye haraka iwezekanavyo. Kwa hivyo, katika nyumba ya Mungu, wote wanaofuatilia ukweli wana matarajio mema makuu, na matarajio mema ya wale wanaompenda Mungu kwa dhati hayana kikomo. Kila mtu anapaswa kuielewa nia ya Mungu. Hakika ni kitu chanya kuwa na mzigo huu, na ni kitu ambacho wale walio na dhamiri na busara wanapaswa kuwa nacho, lakini si kila mtu ataweza kubeba mzigo mzito. Tofauti hii inatoka wapi? Licha ya vipaji au uwezo wako, na licha ya kiwango chako cha akili kuwa juu kiasi gani, kilicho muhimu ni ufuatiliaji wako na njia unayotembea. Ikiwa ubinadamu wako unafikia kiwango kinachostahili na una ubora fulani wa tabia, lakini wewe si mtu anayefuatilia ukweli, na una ubinadamu mwema tu na hisia fulani ya mzigo, je, unaweza kuifanya kazi ya uongozi wa kanisa vizuri? Je, unahakikisha kwamba unaweza kutatua matatizo kwa kutumia ukweli? Ikiwa huwezi kutoa hakikisho kulihusu, basi bado huna uwezo katika kazi hiyo. Hata kama ungechaguliwa au kupangiwa kuwa kiongozi, bado hungekuwa na uwezo wa kuifanya kazi hiyo, kwa hivyo kungekuwa na faida gani? Ingawa kungeridhisha ubatili wako, kungewadhuru akina ndugu na kuchelewesha kazi ya kanisa. Ikiwa unatimiza vigezo vya kuwa kiongozi au mfanyakazi, na wewe ni mtu anayefuatilia ukweli, na pia una ushuhuda fulani wa kupitia, basi hakika utaweza kufanya kazi nzuri katika kazi ya uongozi, kwa sababu una ushuhuda wa kupitia, wewe ni mtu anayeelewa ukweli, na unaweza kubeba mzigo mzito wa kuwa kiongozi wa kanisa. Kwamba ubinadamu wako unafikia kiwango kinachostahili na pia una sifa fulani bainifu ni vigezo vya msingi tu vya kuendelezwa, kustawishwa, na kutumiwa na nyumba ya Mungu, lakini kama unaweza kufanya kazi nzuri katika kazi ya uongozi inategemea kama una upitiaji halisi na uhalisi wa ukweli—hili ndilo jambo la muhimu zaidi. Watu wengine ni watu sahihi na wanafuatilia ukweli, lakini wameamini kwa miaka mitatu hadi mitano tu na hawana uzoefu wa vitendo. Je, watu kama hao wanaweza kuifanya kazi ya uongozi wa kanisa vizuri? Nahofia hawatafaa kwa kazi hiyo. Wanapungukia wapi? Wanakosa uzoefu wa vitendo na bado hawajafikia kuelewa ukweli. Hata kama wanaweza kusema maneno na mafundisho mengi, bado hawajafikia kiwango cha kutatua matatizo kwa kutumia ukweli. Kwa hivyo, bado hawafai kwa kazi ya uongozi na wanahitaji kuendelea kujifundisha ili kufikia uelewa wa ukweli na kuingia katika uhalisi wa ukweli. Kwa mfano, mtu ambaye ubinadamu wake unafikia kiwango kinachostahili na ambaye ni mwaminifu kiasi, na ambaye hasemi uwongo na kudanganya mara chache, na anayefanya wajibu wake bila kusababisha vurugu au usumbufu, lakini ambaye ni duni katika kufuatilia ukweli; je, mtu kama huyo anaweza kustawishwa kuwa kiongozi au mfanyakazi? Hili lingekuwa jambo gumu sana. Je, mtu anayetimiza vigezo vya kuendelezwa, kustawishwa, na kutumiwa, lakini asiyefuatilia ukweli, angeweza kuwa mtu anayefuatilia ukweli ikiwa angeendelezwa kuwa kiongozi au mfanyakazi? Je, angeweza kuanza kufuatilia ukweli? Je, angeweza kuingia katika uhalisi wa ukweli baada ya kufanya kazi kama kiongozi au mfanyakazi kwa kipindi fulani? Hilo halingewezekana. Haijalishi mtu anatimiza vigezo gani, maadamu yeye si mtu anayefuatilia ukweli, hawezi kabisa kuchaguliwa au kuendelezwa kama kiongozi au mfanyakazi. Ikiwa mtu ana ubinadamu na ubora wa tabia unaofikia kiwango kinachostahili, na pia anaweza kuukubali ukweli na kupitia mabadiliko fulani, basi anaweza kuendelezwa, kustawishwa, na kutumiwa, na matokeo yake, atapata fursa ya kujifundisha, kuingia katika uhalisi wa ukweli, na kuanza njia ya wokovu na ukamilisho. Kwa hivyo, haijalishi ni nani anayeendelezwa na nyumba ya Mungu kuwa kiongozi, mfanyakazi, au msimamizi, lengo si kuridhisha matamanio na tamaa zako za makuu, wala kutimiza malengo yako bora, bali ni kukuwezesha uanze njia ya wokovu na uwe mtu aliyekamilishwa.
Kuhusu wale wasio na akili za kutosha kabisa, wao pia wana nia ya kutekeleza wajibu wao vizuri na wanataka kuyalinda masilahi ya nyumba ya Mungu, lakini wanakosa hekima, hawajui jinsi ya kutenda kulingana na kanuni, na hawawezi kung’amua jambo lolote. Wakati fulani, wanakumbana na kishawishi na kuanguka ndani yake, na matokeo yake, wanasaliti masilahi ya kanisa, wanawasaliti akina ndugu, na kuleta madhara kwa kazi ya nyumba ya Mungu. Tunapaswa kuwashughulikia na kuwatendeaje watu wa aina hii ambao ni wajinga na wenye akili pungufu? Linapokuja suala la wajinga kama hao wasiokuwa na ufahamu wa kiroho na wenye akili pungufu, kila mmoja wao anapaswa kutimuliwa na kuondolewa kutoka katika wajibu wake, na hakuna hata mmoja anayeweza kutumiwa. Ikiwa watu kama hao watatumiwa, wanaweza kuleta shida kwa kazi ya nyumba ya Mungu wakati wowote—kuna mafunzo mengi sana kama haya. Siku hizi, kuna watu wengi ambao kwa nje wana mfano fulani wa mwanadamu, lakini hawawezi kushiriki uhalisi wowote wa ukweli. Wamemwamini Mungu kwa miaka mingi na bado wanabaki katika hali hii. Chanzo cha tatizo hili kinapaswa kuonekana wazi; hili ni tatizo la ubora duni sana wa tabia na ukosefu wa ufahamu wa kiroho. Watu kama hao hawatabadilika haijalishi wanamwamini Mungu kwa miaka mingapi, na hawajapata maendeleo yoyote muhimu licha ya mahubiri yote waliyoyasikiliza. Wanaweza tu kuwekwa kando, ili kutumikia kwa njia yoyote duni wawezavyo. Je, hii ni njia nzuri ya kuwashughulikia au la? (Ni nzuri.) Watu wengine wenye akili pungufu na wasio na uwezo hawawezi kuyaelewa maneno ya Mungu kabisa hata baada ya kuyasoma kwa miaka kadhaa, na wanakosa kuelewa mahubiri licha ya kuyasikiliza kwa miaka kadhaa. Je, bado ni muhimu kuwapa vitabu vya maneno ya Mungu watu kama hao? (La.) Vitabu vya maneno ya Mungu havipaswi kupewa watu wenye akili pungufu, kwa sababu kufanya hivyo ni bure na ni sawa na upotevu, na kitabu chochote walichopewa kinapaswa kuchukuliwa na kurudishwa mara moja. Huku si kuwanyima haki ya kusoma maneno ya Mungu, bali ni kwa sababu akili zao hazitoshi. Hata kama watu kama hao wakiishi maisha ya kanisa, hawawezi kuuelewa ukweli, sembuse kutekeleza wajibu. Watu kama hao ni takataka, sivyo? Mnapaswa kujua jinsi ya kushughulikia takataka. Watu wengine huonekana wanyoofu kabisa kwa nje, lakini akili zao ni duni sana kiasi kwamba hawawezi hata kufanya kazi zozote za nguvu ipasavyo, na wanaharibu kila kitu wanachofanya. Wakiombwa kufanya kazi fulani, hakika wataharibu kitu, kwa hivyo watu kama hawa hawawezi kutumiwa. Ukimwomba achukue ndoo ya maji, ataipindua chupa ya mafuta. Ukimwomba aoshe bakuli, atavunja sahani. Ukimwomba apike, atapika aidha kingi sana au kidogo sana, au kitakuwa na chumvi nyingi au hakitakuwa na chumvi ya kutosha. Wanatia moyo wao katika hilo, lakini haijalishi wanajaribu vipi, hawawezi kulifanya vizuri, na hata hawafanyi kazi nzuri ya kufanya kazi za nguvu. Je, watu kama hao wanaweza kutumiwa? (La.) Kwa hivyo ikiwa hawawezi kutumiwa, wanapaswa kuambiwa wafanye nini? Je, inamaanisha kwamba hawaruhusiwi kumwamini Mungu na kwamba nyumba ya Mungu haiwataki? La, haimaanishi hivyo. Usiwaruhusu tu watekeleze wajibu. Ikiwa hawafanyi ipasavyo mambo yaliyo ndani ya wigo wa maisha ya kawaida ya binadamu—ikiwemo mambo ya kawaida ya kimaisha na shughuli za kila siku—au hawawezi kufanya mambo haya, basi hawafai kutekeleza wajibu katika nyumba ya Mungu.
Ingawa watu wengine hawana ubinadamu mzuri au talanta zozote maalum, sembuse kuweza kustawishwa kuwa viongozi, bado wanaweza kufanya kazi fulani za nguvu. Kwa mfano, kulisha kuku na bata, kulisha nguruwe, na kuchunga kondoo ni kazi wanazoweza kufanya vizuri. Ukiwapa kazi rahisi, wanaweza kuifanya vizuri maadamu wanaitilia maanani, na hivyo watu kama hao wanaweza kutekeleza wajibu katika nyumba ya Mungu. Ingawa ni kazi moja, rahisi, wanaweza kuitilia maanani na kutimiza wajibu, na wanaweza pia kujiwekea masharti kulingana na maneno ya Mungu na kanuni za ukweli. Haijalishi kama kazi ni kubwa au ndogo, au ni muhimu au si muhimu, mwishowe, wanaweza kuifanya vizuri kazi moja waliyopewa. Hawawezi tu kuwalisha kuku vizuri ili watage mayai kama kawaida, bali wanaweza pia kuwalinda kuku wasichukuliwe na mbwa mwitu. Wakimsikia mbwa mwitu akilia kwa kelele, watamwambia msimamizi wao mara moja, wakijitahidi kuepuka mkasa wowote katika utendaji wa kazi na jukumu walilokabidhiwa na nyumba ya Mungu. Wakifanya kazi namna hii basi wamejitolea kiasi, na hii inahesabiwa kama kuweza kutimiza wajibu wao na kufanya kazi vizuri. Kuhusu yaliyosalia—maisha yao ya kibinafsi, na jinsi wanavyojiendesha na kushughulikia mambo—wanapungukiwa kiasi; kwa mfano, hawajui jinsi ya kushirikiana na kuzungumza na wengine, au jinsi ya kushiriki kuhusu hali yao na wengine, na wakati mwingine ni wenye kuudhika bila sababu. Je, hili linahesabiwa kama tatizo? Je, ni sawa kutowatumia kwa sababu ya masuala haya? (La.) Watu wengine wana usafi duni wa kibinafsi; hawaoshi nywele zao kwa angalau siku kumi na kwa ujumla wananuka vibaya. Wengine hupiga kelele kubwa wakila na kunywa huku wale walio karibu nao wakipumzika, na huwa na kelele nyakati zingine pia, kama vile wanapotembea, wakifunga milango, na wakizungumza—hawana adabu na hawana malezi mema. Watu kama hao wanapaswa kutendewaje? Kila mtu lazima awe na uelewa, awasaidie na kuwategemeza kwa moyo wa upendo, ashiriki nao kuhusu ubinadamu wa kawaida ulivyo, na awaruhusu wabadilike kidogo kidogo. Kwa kuwa nyote mko pamoja, mnapaswa kujifunza jinsi ya kuishi pamoja kwa upatano. Watu kama hao wanaweza kutumiwa maadamu wanaweza kufanya kazi yao ipasavyo, na kuubeba mzigo wa kazi, na hawafanyi chochote kinachosababisha vurugu na usumbufu. Watu wengine ni werevu, wana ubora mzuri wa tabia, na wanafanya kazi kwa bidii, na wanaweza kutimiza majukumu yao na kufanya vizuri katika kazi walizopewa, kwa hivyo wanaweza kustawishwa na kutumiwa. Lakini watu wengine wana ubora duni sana wa tabia kiasi kwamba hawawezi hata kufanya kazi moja moja vizuri; wanaweza tu kumudu kulisha kuku, lakini ikiwa pia watalazimika kulisha bata na mabata bukini, watazidiwa na hawatajua jinsi ya kuifanya. Si kwamba hawataki kuifanya vizuri, bali ubora wao wa tabia ni duni sana. Ubongo wao una ukomo wake, wanajua tu jinsi ya kufanya kazi moja, na wakipewa nyingine ya kufanya, hawawezi kuimudu. Hawajui jinsi ya kupanga, kwa hivyo wanaharibu mambo tu. Watu kama hao wanafaa tu kufanya kazi moja kwa wakati mmoja. Usiwape kazi nyingi, kwa sababu hawatakuwa na uwezo wa kuzibeba. Usifikiri kwamba ikiwa wanaweza kufanya kazi moja vizuri, hakika wanaweza kufanya kazi mbili au tatu; si lazima iwe hivyo, na inategemea ubora wao wa tabia. Waache wajaribu kufanya kazi mbili kwanza. Ikiwa wana ubora mzuri wa tabia na wanaweza kuzibeba, basi unaweza kuwapangia kwa njia hii. Ikiwa hawawezi kufanya kazi mbili vizuri kwa wakati mmoja, na wakaziharibu, inamaanisha kuwa ni zaidi ya ubora wao wa tabia, kwa hivyo lazima uwaondolee kazi yao ya pili mara moja. Hii ni kwa sababu kupitia uchunguzi na kipindi cha majaribio, umegundua kwamba wanafaa tu kufanya kazi moja kwa wakati mmoja, badala ya kufanya kazi nyingi ngumu, na kwamba hawana ubora wa tabia kwa hili. Watu wengine ni werevu kiasi na wana ubora mzuri kiasi wa tabia, na ukiwapa kazi kadhaa za kufanya, wanaweza kuzifanya vizuri. Kwa mfano, ukimwomba apike, alishe vifaranga, na asimamie bustani ya mboga, anaweza kuandaa milo kwa wakati kila siku huku akisimamia bustani ya mboga katika wakati wake wa ziada, akiinyunyizia maji na kupalilia bustani mara moja, na kuwalisha vifaranga kwa wakati. Watu wengine wanaweza kusema, “Kwa kuwa wana ubora huu wa tabia, wacha wachukue pia kazi ya kanisa na wawe kiongozi wa kanisa.” Je, hilo lingekuwa sawa? Ingawa ana uwezo wa kubeba kazi fulani za nguvu na za kila siku, linapokuja suala la kuwa kiongozi wa kanisa, hilo linahitaji tathmini tofauti; si kitu kinachoweza kupimwa kulingana na utendaji wake wa kazi hizi rahisi, za nje. Hiyo ni kwa sababu kuwa kiongozi wa kanisa si kazi ya nguvu, lazima ipimwe kwa kanuni za uongozi. Hata hivyo, ikiwa mtu huyu ana ubora wa tabia na talanta ya kuwa kiongozi wa kanisa, na ubinadamu wake ni mzuri kiasi, haingefaa kwako kumpa kazi za nje; huko kunaitwa kuwatumia watu isivyofaa. Kwa juu zaidi, viongozi wa kanisa wanaweza kufanya kazi moja zaidi ya muda mfupi inayohusiana na maisha ya kila siku, na kujishughulisha nayo zaidi kidogo wakati wowote hawana shughuli—hili halitawachosha. Linapokuja suala la mambo madogo, ya kawaida na kazi hizi za nguvu, watu wanaweza kufanya nyingi kadri wawezavyo. Je, kuna yeyote anayeweza kuzibeba zote? Je, kuna yeyote aliye na ubora kama huo wa tabia? (La.) Inaweza kuwa kwamba ubora wao wa tabia na uwezo wao vinatosha, lakini kuna kitu kimoja ambacho hawatakuwa nacho cha kutosha, na hicho ni nguvu. Watu ni viumbe vinavyokufa, nguvu zao zina ukomo, na idadi ya kazi wanazoweza kufanya pia ina ukomo. Watu wenye nguvu nyingi wanaweza kufanya kazi hadi saa kumi na mbili kwa siku, ilhali watu wenye nguvu za wastani wanaweza kufanya kazi kwa saa nane kwa kawaida, na watu wenye nguvu kidogo wanaweza kufanya kazi kwa saa nne au tano tu. Kwa hivyo, iwe unamtumia mtu kufanya kazi za nguvu, kazi ya uongozi wa kanisa, au kazi inayohusisha ustadi wa kitaaluma, lazima uzingatie kile anachofaa zaidi kufanya, na baada ya kumpa kazi inayofaa zaidi, ikiwa hawezi kuifanya, mpe kitu kingine. Ikiwa huwapi kazi kulingana na kile wanachofaa zaidi kufanya, hili ni kosa katika jinsi unavyowatumia watu. Kwa wale watu wasioweza kupewa kipaumbele kwa ajili ya kuendelezwa, kustawishwa, na kutumiwa, hata wakitakiwa kufanya kazi za nguvu, lazima wapewe kazi hizi kulingana na ubora wao wa tabia na uwezo wao. Ikiwa, katika wakati huohuo wanapoifanya vizuri kazi yao moja waliyopewa, bado wanaweza kufanya kazi zingine, basi wanaweza kuombwa kufanya kazi zingine chache za nguvu kwa muda mfupi, maadamu haiathiri kazi yao kuu. Watu wengine wana nguvu kimwili na wanaweza kufanya kazi tatu mfululizo; baada ya kumaliza kazi moja, bado wana nguvu za ziada, na wanakuwa huru wakati mwingi. Lakini viongozi wa uwongo ni vipofu na hawajui jinsi ya kugawanya kazi, na hawajatambua kuwa hili ni tatizo, kwa hivyo wanawapa watu hao kazi moja tu, jambo ambalo ni kosa.
Nilikuwa Nazungumza hivi punde kuhusu watu wenye akili pungufu wasio na ustadi maalum na wanaoweza tu kufanya kazi za nguvu. Pia kuna watu walio na ugonjwa fulani na hata hawawezi kufanya kazi za nguvu, na hupata maumivu ya kichwa, maumivu ya tumbo, au maumivu ya mgongo kila wanapofanya kitu chochote cha kutumia nguvu hata kidogo. Nini kifanyike kuhusu kuwapangia wajibu watu wa aina hii, ikiwa wanafaa kutekeleza wajibu? Ni lazima mtu aangalie vipengele mbalimbali, kama vile hali yao ya afya na pia ubinadamu wao na ubora wao wa tabia, ili kubaini ni wajibu gani wanaofaa kuutekeleza katika nyumba ya Mungu. Ikiwa afya yao ni mbaya sana kiasi kwamba hawawezi kufanya kazi zozote, na wanalazimika kupumzika baada ya kufanya kazi kwa muda, na pia wanahitaji mtu wa kuwatunza, ikiwa hawawezi kutekeleza wajibu ipasavyo wenyewe na ni lazima mtu apangiwe kuwatunza, basi haifai kabisa. Watu kama hao hawafai kutekeleza wajibu, kwa hivyo waache waende nyumbani wapone. Chochote unachofanya, usimtumie mtu yeyote aliye mgonjwa sana kiasi kwamba upepo mkali unaweza kuwaangusha. Ikiwa afya yao si mbaya sana na ni kwamba tu wanaugua maumivu ya tumbo wakila chakula kisichofaa, au wanapata maumivu ya kichwa wakitumia ubongo wao sana, kwa hivyo wanaweza tu kufanya kazi kwa saa tatu au nne chini ya mtu wa kawaida, au kufanya nusu ya kazi ya mtu wa kawaida, basi watu kama hao bado wanaweza kutumiwa maadamu wanatimiza vigezo vingine. Isipokuwa walizungumzie wenyewe na kusema, “Afya yangu ni mbaya sana siwezi kustahimili ugumu huu. Nataka kwenda nyumbani ili nipone. Nitakaporudi, nitarudi na kutekeleza wajibu wangu,” basi kubali hilo bila kuchelewa na usijaribu kuwashauri kuhusu jinsi wanavyofikiri; haitakuwa na athari yoyote hata ukifanya hivyo. Kuna msemo unaosema, “Kwa nguvu chuma hakiwi panga”; imani, azimio, na ufuatiliaji wa kila mtu ni tofauti. Watu wengine wanaweza kusema: “Je, si ni kwamba tu wakati mwingine wanahisi vibaya kidogo na wana nguvu kidogo? Watu wanaweza kuhisi vibaya wakila vitu visivyofaa, lakini baada ya siku kadhaa watakuwa sawa; je, kuna haja yoyote kwao kwenda nyumbani na kupata nafuu? Je, maumivu yao ya kichwa na kizunguzungu hayataisha baada ya kulala vizuri usiku? Je, hawawezi kufanya kazi kama kawaida basi? Je, ni jambo kubwa hivyo?” Linaweza kukosa kuwa jambo kubwa kwako, lakini watu wengine ni tofauti na wengine kulingana na kiwango wanachothamini miili yao, na watu wengine kwa kweli wana shida za kiafya. Katika hali kama hizo, wakiomba warudi nyumbani kupumzika na kupata nafuu, kanisa linapaswa kukubali haraka, lisiwawekee masharti, lisiwafanyie mambo kuwa magumu, na hasa lisijaribu kuwashauri kuhusu jinsi wanavyofikiri. Baadhi ya viongozi wa uwongo huwashughulikia watu kama hao kila mara, kwa kusema: “Angalia kiwango ambacho kazi ya Mungu imefikia sasa. Majanga yanazidi kuwa makubwa, miezi minne yenye rangi ya damu imetokea, na sasa janga la mlipuko limeenea sana kiasi kwamba wasioamini hawana njia ya kuendelea kuishi! Uko katika nyumba ya Mungu, ukitekeleza wajibu wako na kufurahia neema ya Mungu—hutawekwa hatarini na pia unaweza kupata ukweli na uzima—hiyo ni baraka kubwa iliyoje! Shida hii ndogo uliyo nayo si kitu. Lazima uishinde na umwombe Mungu. Mungu hakika atakuponya. Soma tu maneno ya Mungu, jifunze nyimbo chache zaidi za sifa, na ugonjwa wako utapona kiasili ukiutoa akilini mwako. Je, si maneno ya Mungu yanasema, ‘Kukaa katika ugonjwa ni kuwa mgonjwa’? Unakaa katika ugonjwa sasa hivi. Ukiendelea kufikiria kuhusu kuwa mgonjwa, basi ugonjwa utakuwa mbaya. Usipoufikiria, basi ugonjwa wako utatoweka, sivyo? Kwa njia hiyo, utakua katika imani na hutataka kwenda nyumbani kupumzika. Wewe kwenda nyumbani kupumzika kunaitwa kutamani starehe za mwili.” Usijaribu kuwashauri kuhusu jinsi wanavyofikiri, ni upumbavu kufanya hivyo. Hawawezi hata kuvumilia usumbufu mdogo wa muda na wanataka tu kwenda nyumbani kupumzika, na hawawezi hata kushinda ugumu mdogo, jambo linalothibitisha kwamba hawatekelezi wajibu wao kwa dhati. Kwa kweli, watu wa aina hii hawana nia ya kutekeleza wajibu kwa muda mrefu, hawaufanyi kwa dhati yoyote, hawataki kulipa gharama, na sasa hatimaye wamepata fursa na kisingizio cha kutoroka kabisa. Moyoni mwao, wanafurahia kwamba wao ni werevu sana na kwamba ugonjwa huu umekuja kwa wakati unaofaa kabisa. Kwa hivyo chochote unachofanya, usiwashawishi wabaki. Watamchukia yeyote anayejaribu kuwashawishi wabaki, na watamlaani yeyote anayejaribu kubadili nia zao. Je, huelewi hili? Bila shaka, watu wengine kwa kweli ni wagonjwa, na wamekuwa wagonjwa kwa muda mrefu, na wanaogopa kwamba wakiendelea kuvumilia zaidi, maisha yao yatakuwa hatarini. Hawataki kuiletea nyumba ya Mungu shida yoyote, au kuathiri utendaji wa wajibu wa watu wengine. Wanahisi kwamba punde tu afya yao inapowashinda, watalazimika kuwategemea akina ndugu kuwatunza, na wanahisi vibaya kuhusu kuifanya nyumba ya Mungu iwatunze, kwa hivyo kwa busara wao huchukua hatua ya kuomba ruhusa ya kuondoka. Hali hii inapaswa kushughulikiwaje? Vivyo hivyo, kwa kuwaacha waende nyumbani wapumzike bila kuchelewa zaidi. Nyumba ya Mungu haiogopi shida, ila tu haitaki kuwalazimisha watu kinyume na mapenzi yao. Zaidi ya hayo, watu wote wana matatizo fulani ya kibinafsi na halisi. Watu wanaoishi katika mwili wote huugua, na magonjwa ya mwili ni tatizo lililopo katika uhalisi—tunaheshimu ukweli wa mambo. Watu wengine kwa kweli hawawezi kutekeleza wajibu wao kwa sababu ya kuwa na afya mbaya sana, na ikiwa wanahitaji nyumba ya Mungu iwaandalie huduma zinazofaa, au wanahitaji akina ndugu watoe tiba au kutoa mapendekezo fulani ya matibabu, nyumba ya Mungu itafurahi kutoa vitu hivi. Ikiwa hawataki kuisumbua nyumba ya Mungu na wana pesa, njia, na uwezo wa kwenda kutibiwa ugonjwa wao, hilo pia ni sawa. Kwa muhtasari, ikiwa ni kwa sababu afya yao haiwaruhusu kuendelea kutekeleza wajibu wao katika nyumba ya Mungu au kuendelea kustawishwa na nyumba ya Mungu, basi wanaweza kuwasilisha ombi linalostahili, na nyumba ya Mungu italikubali mara moja. Hakuna mtu anayepaswa kujaribu kubadili nia zao, au kuweka masharti, kwani hilo lingekuwa lisilofaa na lisilokuwa na urazini. Hii ndiyo mipango inayofanywa kwa ajili ya watu wa aina hii.
Jinsi ya Kuwachukulia Watu Wachache Walio Maalum
I. Jinsi ya Kuwatendea Watu Ambao Hawashughulikii Kazi Yao Sahihi
Watu wengine wana ubinadamu unaokubalika, wana sifa nzuri na wenye akili, wanazungumza kawaida, kwa kawaida wao huwa na matumaini sana, na wana bidii sana katika kutekeleza wajibu wao, lakini wana kasoro moja, ambayo ni kwamba wao ni wenye hisia kupita kiasi. Wanapokuwa wanamfuata Mungu na kutekeleza wajibu wao kanisani, wao huwakumbuka daima familia na jamaa zao, au wao hufikiria daima kuhusu kula vyakula vizuri vya miji ya kwao, na kutoweza kuvila huwaumiza, jambo ambalo huathiri utendaji wa wajibu wao. Kuna mtu wa aina nyingine, anayependa kuishi peke yake mahali pamoja, akiwa na nafasi yake ya faragha. Anapokuwa na akina ndugu, anahisi kwamba kasi ya kazi ni ya haraka sana na kwamba hana nafasi ya faragha ya kuishi. Yeye huhisi daima akiwa chini ya shinikizo, na daima huhisi kuwa amezuiwa na hana raha kuishi na akina ndugu. Daima anataka kufanya chochote apendacho na kuwa huru kujifurahisha. Hataki kutekeleza wajibu wake pamoja na kila mtu mwingine, na yeye hufikiria daima kuhusu kurudi nyumbani. Daima yeye huona kutekeleza wajibu wake katika nyumba ya Mungu kuwa jambo lisilopendeza. Ingawa ni rahisi kwake kuelewana na akina ndugu na hakuna anayemdhulumu katika nyumba ya Mungu, yeye hupata shida kiasi kufuata ratiba ya kazi na mapumziko—baada ya kila mtu kuamka asubuhi, yeye anataka kulala zaidi, lakini anahisi aibu kufanya hivyo, na wakati kila mtu mwingine anapumzika usiku, yeye hataki kulala na daima anataka kufanya kitu kinachomvutia. Wakati mwingine kuna kitu fulani ambacho anataka kula sana, lakini hakipatikani katika kantini, na anaona aibu sana kukiomba. Wakati mwingine anataka kwenda matembezi, lakini hakuna mtu mwingine anayeuliza kufanya hivi, kwa hivyo hathubutu kujifurahisha. Yeye daima ni mwangalifu na mwenye tahadhari, na anaogopa kuchekwa, kudharauliwa, au kuitwa mtoto. Ikiwa hatekelezi wajibu wake vizuri, wakati mwingine yeye hupogolewa. Anahisi kana kwamba kila siku ana wasiwasi mwingi, kana kwamba anatembea kwenye barafu nyembamba, na hana furaha kabisa. Yeye huwaza, “Nakumbuka kwamba nilipokuwa nyumbani, nilikuwa mtoto mdogo wa familia, huru na bila kuzuiwa, kama malaika mdogo. Nilikuwa na furaha mno! Ninatekeleza wajibu wangu katika nyumba ya Mungu sasa, imekuwaje kwamba alama za jinsi nilivyokuwa zamani zimetoweka? Siwezi tena kufanya chochote ninachotaka, kama nilivyokuwa nikifanya,” na kwa hivyo hawataki kuishi maisha ya aina hii. Lakini hawathubutu kumweleza kiongozi wao jambo hili, na wao hueneza mawazo haya daima kwa watu walio karibu nao, wao daima hutamani nyumbani, na kulia kwa siri kitandani usiku. Ni kitu gani kinachopaswa kufanywa kuhusu watu wa aina hii? Yeyote anayefahamu jambo hilo anapaswa kuliripoti bila kuchelewa, kiongozi anapaswa kuthibitisha mara moja kama ripoti hiyo ni ya kweli au la, na ikiwa ni kweli, mtu huyo anaweza kuruhusiwa kurudi nyumbani. Anafurahia chakula, kinywaji, na ukarimu wa nyumba ya Mungu, lakini bado hataki kutekeleza wajibu wake na daima ananuna, akihisi amekosewa na hana furaha, kwa hivyo mtume aondoke haraka iwezekanavyo. Watu wa aina hii hawana hisia hizi kwa muda mfupi tu, na kisha kuzitatua kwa kutafakari mambo—hiyo siyo hali yao. Nia ya kibinafsi ya watu wengine ni kutekeleza wajibu wao kwa uthabiti, na ingawa wanatamani nyumbani, wanajua hili ni tatizo la aina gani, na wanaweza kutafuta ukweli na kulitatua. Kwa upande wa watu hawa, hakuna haja ya kuwaacha waende au kuwa na wasiwasi juu yao. Hali tunayozungumzia ni wakati watu walio katika miaka yao ya thelathini bado wanatenda kama watoto, bila kukua kamwe, na daima wanabaki bila kutulia. Wao hufanya tu chochote wanachoambiwa kufanya, na wakati hawana la kufanya, wao hufikiria kuhusu kujifurahisha na kupiga gumzo kuhusu mada zisizo na maana, na kamwe hawataki kushughulikia kazi yao rasmi. Wasioamini husema kwamba mtu huimarika akiwa na umri wa miaka 30. Kuimarika kunamaanisha kushughulikia kazi ya mtu rasmi, kuweza kujitwika kazi na kujikimu, kujua kushughulikia mambo rasmi ya mtu, kutumia muda mchache kujifurahisha, na kutochelewesha kazi ya mtu rasmi. Je, “kutenda kama watoto” kunamaanisha nini? Kunamaanisha kutoweza kujitwika kazi yoyote wanayofaa kufanya, daima kutaka kuacha mawazo yao yaende mbali, na daima kutaka kwenda matembezi, kuzurura, kufanya upuuzi, kula vitafunio, kutazama drama, kupiga gumzo kuhusu mambo yasiyo na maana, kucheza michezo, na kutafuta mtandaoni matukio ya ajabu na hadithi zisizo za kawaida. Kunamaanisha kutokuwa na mwelekeo wa kuhudhuria mikutano kamwe, daima kutaka kulala wakati wowote ambapo mikutano inapofanyika, kutaka kulala mara tu wanapohisi kusinzia, na kutaka kula mara tu wanapohisi njaa, kuwa wakaidi na kutoshughulikia kazi yao inayofaa. Watu kama hawa hawawezi kusemwa kuwa na ubinadamu mbaya, ni kwamba tu hawakui kamwe na daima wanabaki kuwa hawajakomaa. Wako hivi wakiwa na umri wa miaka 30, na bado wako hivi wakiwa na miaka 40; hawawezi kubadilika. Wakiomba kuondoka na wasiwe tayari tena kutekeleza wajibu wao, hili linapaswa kushughulikiwaje? Nyumba ya Mungu haiwasihi wabaki. Unapaswa kuwajibu mara moja—waache waondoke mara moja na warudi kati ya wasioamini, na uwaambie wasiseme kabisa kwamba wanamwamini Mungu. Je, watu wasioshughulikia kazi yao inayofaa wanaweza kupata ukweli? Ikiwa unatarajia wakomae katika ubinadamu wao na kuja kushughulikia kazi yao rasmi kupitia kutekeleza wajibu katika nyumba ya Mungu, kuweza kujitwika kipengele muhimu cha kazi, na kisha kuelewa na kutenda ukweli na kuishi kwa kudhihirisha mfano wa mwanadamu, hupaswi kulitegemea hilo kabisa. Utapata watu kama hawa katika kundi lolote. Wasioamini wana jina la utani kwa watu wa aina hii: “watoto wakubwa.” Watu kama hao wanaweza kufikia umri wa miaka 60 bila kuwahi kushughulikia kazi yao inayofaa. Wao huzungumza na kushughulikia mambo kwa namna isiyofaa, daima wanacheka, kutaniana, na kurukaruka, hawafanyi chochote kwa njia ya dhati, na wamedhamiria hasa kujifurahisha. Nyumba ya Mungu haiwezi kuwatumia watu kama hao.
Je, mnafikiri kwamba hawa “watoto wakubwa” ni wabaya? Je, ni watu waovu? (La.) Baadhi yao si watu waovu, ni watu wanyofu kabisa, na si wabaya. Baadhi yao ni wema kabisa na wako tayari kuwasaidia wengine. Lakini wote wana kasoro moja—wao ni wakaidi, wanapenda kucheza, na hawashughulikii kazi yao inayofaa. Kwa mfano, tuseme baada ya mwanamke kuolewa, hajifunzi kufanya kazi yoyote ya nyumbani. Yeye hupika tu chakula wakati ana furaha, lakini sio wakati hana furaha—lazima abembelezwe wakati wote. Mtu akimtaka afanye kitu, lazima ajadiliane na yeye, na lazima asimamiwe. Daima anapenda kujipamba vizuri ili aende nje kufanya ununuzi, akinunua nguo na vipodozi, na kufanyiwa urembo. Anaporudi nyumbani, hafanyi kazi hata moja, na anataka tu kucheza karata na mahjong. Ukimwuliza ratili moja ya kabichi inagharimu pesa ngapi, hajui; ukimwuliza atakula nini kesho, hajui hilo pia; na ukimwambia apike kitu, anakiharibu. Basi, yeye ni hodari zaidi katika jambo gani? Yeye ni hodari zaidi katika mambo kama kujua ni mgahawa upi unaopika chakula kitamu zaidi, ni duka lipi lina nguo za mtindo wa kisasa zaidi, na ni duka lipi linalouza vipodozi vya bei nafuu na vinavyofanya kazi vizuri, lakini haelewi au kujifunza mambo mengine kama jinsi ya kuendesha maisha, au ujuzi unaohitajika katika maisha ya kawaida ya mwanadamu. Je, anakosa kujifunza mambo haya kwa sababu ana ubora wa tabia usio wa kutosha? La, sivyo. Kulingana na mambo ambayo yeye ni hodari katika, ana ubora wa tabia, lakini hashughulikii kazi yake inayofaa. Maadamu ana pesa za kutumia, ataenda nje kula katika migahawa na kununua vipodozi na nguo. Ikiwa kuna upungufu wa sufuria na vikaango nyumbani na akiombwa anunue vingine, atasema, “Kuna chakula kitamu kinachouzwa nje, nina haja gani ya kununua hivyo vyote?” Ikiwa mashine ya kufyonza vumbi nyumbani imeharibika, na aombwe asinunue nguo moja ili kuokoa pesa za kununua mpya, atasema, “Nitakapokuwa nachuma pesa siku zijazo, nitamwajiri tu mfanyakazi wa nyumbani asafishe nyumba, kwa hivyo hakuna haja ya kununua mashine ya kufyonza vumbi.” Kwa kawaida, ikiwa hachezi michezo au mahjong, basi ananunua nguo za mtindo wa kisasa, na hasafishi nyumba kamwe. Huku ni kutoshughulikia kazi ya mtu inayofaa, sivyo? Kisha kuna wanaume wengine ambao, mara tu wanapochuma pesa kiasi, wanazitumia kununua gari au kuzitumia kwa kucheza kamari. Ikiwa kitu kimeharibika nyumbani, hawakirekebishi. Hawaendeshi maisha yao kwa njia inayofaa. Nyumbani kwao, friji yao haifanyi kazi, na mashine yao ya kufua nguo haifanyi kazi pia, mifereji imeziba, na paa linavuja kukinyesha, na hawarekebishi vitu hivi kwa muda mrefu sana. Mnaonaje kuhusu wanaume kama hawa? Hawashughulikii kazi inayofaa. Wawe ni wanaume au wanawake, nyumba ya Mungu haiwezi kutumia aina za watu ambao ni wakaidi kupita kiasi na wasioshughulikia kazi yao inayofaa.
Watu wengine hawashughulikii kazi yao inayofaa kama wazazi, na wanashindwa kuwatunza watoto wao ipasavyo. Matokeo yake, watoto wao huishia kubabuliwa na maji yanayochemka au kugongwa na kukwaruzwa; watoto wengine huishia kuvunjika pua zao, wengine huungua makalio yao kwenye jiko, na wengine huunguza koo zao baada ya kunywa maji yanayochemka. Watu wa aina hii hawako makini katika chochote wanachofanya, na hawawezi kufanya chochote ipasavyo. Hawashughulikii kazi yao inayofaa, wanazembea, ni wakaidi na wanapenda kucheza, na hawawezi kubeba majukumu ambayo mtu anapaswa kubeba. Kama wazazi, hawawezi kutimiza majukumu yao na hawajali. Basi, je, watu kama hao wanaweza kubeba majukumu ambayo watu wa kawaida wanapaswa kubeba wanapotekeleza wajibu katika nyumba ya Mungu? La, hawawezi kabisa. Watu wasioshughulikia kazi yao inayofaa hawawezi kutumiwa. Wakisema hawataki kutekeleza wajibu wao tena na waombe kurudi nyumbani, basi waache waende mara moja. Hakuna anayepaswa kuwalazimisha au kuwasihi wabaki, kwa sababu hili ni tatizo linalohusu asili yao, si dhihirisho la hapa na pale la muda mfupi. Watu hawa walijawa na njozi walipokuja katika nyumba ya Mungu kutekeleza wajibu wao; walifikiri kwamba kutekeleza wajibu na kumfuata Mungu kungekuwa kama kuja katika Bustani ya Edeni, kama kuwa katika nchi nzuri ya Kanaani. Maisha waliyowazia yalikuwa ya kupendeza, kukiwa na vitu vizuri vya kula na kunywa mchana kutwa, uhuru na bila kuzuiwa, na bila kazi yoyote ya kufanywa kabisa. Walitaka kuishi maisha ya starehe bila wasiwasi, lakini yakaishia kuwa tofauti kabisa na vile walivyowazia. Watu hawa wamepitia ya kutosha, na wanahisi kwamba inachosha na haipendezi hapa, na wanataka kuondoka, kwa hivyo waache waende bila kuchelewa, nyumba ya Mungu haiwasihi watu hawa wabaki. Nyumba ya Mungu haiwalazimishi watu, na ninyi hampaswi kufanya hivi pia; huku ni kutenda ukweli na kutenda kulingana na kanuni. Lazima mfanye mambo ambayo yanalingana na kanuni za ukweli, lazima muwe watu wanaoelewa nia za Mungu, watu wenye busara—msiwe watu waliovurugika, au watu wanaotaka kuwafurahisha wengine bila ubaguzi. Washughulikieni watu wa aina hii wasioshughulikia kazi yao inayofaa kwa njia hii—je, huku kunaweza kuchukuliwa kuwa kutokuwa na upendo au kutowapa watu nafasi ya kutubu? (La, hakuwezi.) Mungu ni mwenye haki kwa kila mtu, na nyumba ya Mungu ina haki ya kukuendeleza, kukustawisha, na kukutumia. Ikiwa huko tayari kutekeleza wajibu wako, na unaomba kuondoka kanisani, hilo ni chaguo lako huru, kwa hivyo kanisa linapaswa kukubali ombi lako, halitakulazimisha kabisa. Hili linalingana na maadili, linalingana na ubinadamu, na bila shaka, linalingana hasa na kanuni za ukweli. Hii ni hatua inayofaa sana kuchukua! Ikiwa yeyote atatekeleza wajibu wake kwa kipindi cha muda, na kuona unachosha na ni mgumu, na hafurahii kuufanya tena, na hivyo anataka kuacha wajibu wake na kuacha kumwamini Mungu, Nitakupa jibu dhahiri la jambo hili leo, ambalo ni kwamba nyumba ya Mungu itakubali hili, na haitakulazimisha kamwe kubaki, au kufanya mambo yawe magumu kwako. Hakuna mtanziko kwa hili, na huhitaji kuhisi kana kwamba uko katika hali ngumu, au kwamba umepoteza heshima. Sembuse kuwa ni tatizo kwa nyumba ya Mungu, na nyumba ya Mungu haikuwekei masharti yoyote pia. Zaidi ya hayo, ukitaka kuondoka, basi nyumba ya Mungu haitakushutumu au kukuzuia, kwa sababu hii ndiyo njia uliyochagua, na nyumba ya Mungu inaweza tu kutimiza matakwa yako. Je, hii ni hatua inayofaa ya kuchukua? (Ndiyo.)
Nimeorodhesha hivi punde hali kadhaa ambazo watu hawashughulikii kazi yao inayofaa. Nyumba ya Mungu haiwalazimishi watu hawa; ikiwa hawako tayari kutekeleza wajibu wao au wana matatizo fulani ya kibinafsi na kuomba kutotekeleza wajibu tena, basi nyumba ya Mungu itakubali. Haitawatumia tena, na haitawaaacha watekeleze wajibu. Hivi ndivyo watu kama hao wanavyoshughulikiwa, na ni hatua inayofaa kabisa kuchukua.
II. Jinsi ya Kuwachukulia Akina Yuda
Kuna watu wengine ambao ni waoga sana, na kila wanaposikia kwamba ndugu au dada amekamatwa, wao huogopa sana kukamatwa wenyewe. Inaonekana wazi kwamba wakikamatwa, kuna hatari ya wao kulisaliti kanisa. Watu kama hawa wanapaswa kushughulikiwaje? Je, watu hawa wanafaa kutekeleza wajibu fulani muhimu? (La, hawafai.) Watu wengine wanaweza kusema, “Ni nani anayeweza kuhakikisha kwamba mtu huyu mwenyewe hatakuwa Yuda?” Hakuna anayeweza kuhakikisha kwamba hatakuwa Yuda kamwe akiteswa. Basi, kwa nini nyumba ya Mungu haiwatumii watu waoga ambao wanaweza kuwa akina Yuda? Kwa sababu watu ambao ni waoga dhahiri wanaweza kukamatwa na kujihusisha na usaliti wakati wowote; watu kama hao wakitumiwa kutekeleza wajibu muhimu, kuna uwezekano mkubwa sana kwamba mambo yataharibika. Hii ni kanuni ambayo lazima ieleweke wakati wa kuchagua na kuwatumia watu katika mazingira ya hatari ya China bara. Kuna hali maalum hapa, ambayo ni kwamba watu wengine wameteswa kwa muda mrefu na kwa kiasi kikubwa kiasi kilichohatarisha maisha yao, na hatimaye, kwa kweli hawakuweza kuvumilia tena, kwa hivyo wakawa akina Yuda kwa sababu ya udhaifu na wakasaliti mambo fulani yasiyo muhimu. Hakuna anayeweza kuwang’amua watu kama hao, na watu hawa bado wanaweza kutumiwa. Lakini kuna watu ambao tayari wamejiandalia njia ya kutokea kabla ya kukamatwa. Wamefikiria kwa muda mrefu na kwa kina kuhusu jinsi ya kuhakikisha wanaachiliwa mara moja baada ya kukamatwa bila kulazimika kupitia mateso yoyote—kwanza, kuepuka mateso, pili, kuepuka kuhukumiwa, na tatu, kuepuka kwenda jela. Hivi ndivyo wanavyofikiri. Hawana azimio kwamba ni heri wateseke au wafungwe jela kuliko kuwa Yuda. Wanaweza kujihusisha na usaliti bila hata kuteswa, kwa hivyo, je, inaweza kusemwa kwamba wao tayari ni akina Yuda kabla ya kukamatwa na kufungwa jela? (Ndiyo.) Hawa ndio akina Yuda halisi. Je, kanisa linathubutu kuwatumia watu wa aina hii? (La, halithubutu.) Ikiwa wanaweza kugundulika, lazima wasistawishwe kabisa na kutumiwa. Watu hawa hudhihirishaje tabia zao kwa kawaida? Wao ni waoga sana. Mara tu jambo fulani linapoenda mrama, wao hukwepa majukumu yao katika fursa ya mapema zaidi, na wakati wowote wanapokumbana na hatari ndogo zaidi, wao huacha wajibu wao na kutoroka. Kila wanaposikia kwamba mazingira yamekuwa ya hatari, wao hutafuta mahali salama pa kujificha; hakuna anayeweza kuwapata, na hawawasiliani na yeyote. Kujificha ni kazi wanayoifanya kwa ustadi sana. Hawajali kuhusu matatizo yoyote ambayo kazi ya kanisa inapitia, na wana uwezo wa kuweka kando kazi yoyote muhimu; wao huchukulia usalama wao wenyewe kuwa muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote. Zaidi ya hayo, wanapokabiliwa na hatari, watawafanya wengine wajitokeze na kujihatarisha wakati wowote jambo linapotokea, huku wao wakijilinda. Haijalishi wanawaweka wengine katika hatari kiasi gani, wanahisi kwamba inafaa na ni sahihi kufanya hivi kwa ajili ya usalama wao wenyewe. Pia, wanapokabiliwa na hatari, hawaji haraka mbele za Mungu kuomba, wala hawapangi haraka uhamisho wa akina ndugu au mali ya kanisa ambayo inaweza kuwa hatarini. Badala yake, kwanza wao hufikiria kwa uzito jinsi ya kutoroka, jinsi ya kujificha, na jinsi ya kujinasua kutoka katika hatari. Hata wao huwa wametayarisha mpango wao wa kutoroka—ni nani wa kusaliti kwanza wakikamatwa, jinsi ya kuepuka kuteswa, jinsi ya kuepuka kuhukumiwa kifungo cha jela, na jinsi ya kuepuka dhiki. Wakati wowote wanapokumbana na aina fulani ya dhiki, wao hufa ganzi kwa woga na hawana hata chembe ya imani. Je, si watu wa aina hii ni wa hatari? Wakiombwa wafanye kazi ya hatari, wao hulalamika bila kikomo, wanaogopa na daima hufikiria kutoroka, na hawako tayari kuifanya. Watu wa aina hii tayari huonyesha ishara za kuwa akina Yuda hata kabla ya kukamatwa. Punde tu wanapokamatwa, kuna uhakika kamili kwamba watalisaliti kanisa. Katika kutekeleza wajibu wao katika nyumba ya Mungu, wao ni wenye bidii sana katika kila kitu kinachowapa umaarufu bila kuwaweka hatarini; lakini linapokuja suala la kujihatarisha, wao hurudi nyuma, na ukiwataka wafanye jambo la hatari, hawatalifanya, hawataki kabisa kuwajibika. Punde wanaposikia hatari mahali fulani, kwa mfano, kwamba joka kuu jekundu linafanya ukamataji, au kwamba waumini fulani wamekamatwa, wao huacha kuhudhuria mikutano, wanaacha kuwasiliana na akina ndugu, na hakuna anayeweza kuwapata. Wao hujitokeza tena punde tu uvumi unapotulia na kila kitu kiko sawa. Je, watu wa aina hii wanaweza kutegemewa? Je, wanaweza kutekeleza wajibu katika nyumba ya Mungu? (La.) Kwa nini hawawezi? Hawana hata azimio au nia ya kutokuwa akina Yuda; wao ni waoga tu, wadhaifu, na na ni nyangarika. Watu wa aina hii wana sifa moja bainifu iliyo dhahiri, ambayo ni kwamba haijalishi wana nguvu na uwezo gani, nyumba ya Mungu ikiwatumia, hawatajitoa kamwe kwa moyo wote kutetea masilahi ya nyumba ya Mungu. Je, ni kwamba hawatetei masilahi ya nyumba ya Mungu kwa sababu hawana uwezo wa kufanya hivyo? La, sivyo; hata kama wana uwezo huu, hawatatetea masilahi ya nyumba ya Mungu. Wao ni akina Yuda halisi. Wakati wowote wanapohitaji kuwa na shughuli na wasioamini katika mchakato wa kutekeleza wajibu wao, wao hudumisha mahusiano ya upatano nao na kuhakikisha kwamba wasioamini wanadumisha heshima kubwa, staha na uthamini kwao. Basi, ni gharama gani ambayo kwayo wanapata haya yote? Ni ile ya kusaliti masilahi ya nyumba ya Mungu ili kubadilishana na utukufu na masilahi yao ya kibinafsi. Mtu wa aina hii ni mwoga hasa hata kabla ya kukamatwa, na baada ya kukamatwa kuna uhakika kamili kwamba atajihusisha na usaliti. Nyumba ya Mungu haiwezi kabisa kuwatumia watu kama hawa—akina Yuda hawa—na lazima iwaondoshe haraka iwezekanavyo.
Kuhusu aina ya watu ambao ni Mayuda, ingawa kwa nje hawaonekani kuwa watu waovu, kwa kweli ni watu wenye uadilifu duni sana na tabia ya kiibilisi. Haijalishi wanasikiliza mahubiri au kusoma maneno ya Mungu kiasi gani, hawawezi kuelewa ukweli, wala hawahisi kwamba kudhuru masilahi ya nyumba ya Mungu ndilo jambo la aibu zaidi, la uovu, na la kudhuru sana. Wako tayari kujitokeza linapokuja suala la mambo yanayowafanya waonekane, lakini linapokuja suala la mambo ambayo ni ya hatari, au magumu kushughulikia, wanawaachia wengine wayabebe na kuyashughulikia. Hawa ni watu wa namna gani? Je, si wao ni watu wenye uadilifu duni sana? Watu wengine hununua vitu kwa ajili ya nyumba ya Mungu, na katika kufanya hivyo, wanapaswa kuzingatia masilahi ya nyumba ya Mungu, na kuwa wenye haki na busara. Hata hivyo, aina ya watu ambao ni Mayuda si tu kwamba wanashindwa kutetea masilahi ya nyumba ya Mungu, bali kinyume chake, wanawasaidia wasioamini kwa gharama ya nyumba ya Mungu, na kutosheleza matakwa ya wasioamini katika kila fursa, na wako radhi masilahi ya nyumba ya Mungu yadhurike ikiwa hilo linawasaidia kutafuta kibali kwa wasioamini. Huku kunaitwa kung’ata mkono unaokulisha, na ni kukosa maadili! Je, huku si kuwa na ubinadamu wa kudharauliwa? Je, si hili ni sawa na Yuda kumsaliti Bwana na marafiki zake. Chochote ambacho nyumba ya Mungu inawaagiza wafanye, hawazingatii masilahi ya nyumba ya Mungu. Wanapoombwa kununua kitu, hawatafuti huku na kule na kulinganisha bei, ubora na huduma ya baada ya mauzo ya wauzaji wengi, na kisha kupima chaguo kwa makini na kufanya uhakiki unaofaa, ili waepuke kudanganywa, waiokolee nyumba ya Mungu pesa kidogo, na kulinda masilahi ya nyumba ya Mungu yasidhurike—hawafanyi hivyo kamwe. Ndugu au dada akipendekeza kwamba ingekuwa vyema kutafuta huku na kule, wanasema, “Hakuna haja ya kutafuta huku na kule; muuzaji anasema kwamba vitu vyake ndivyo bora zaidi.” Ndugu au dada anapowauliza, “Basi unaweza kupatana bei na yeye?” wanajibu, “Kwa nini nipatane bei? Tayari ameniambia bei ni ipi, na nikianza kujadiliana na yeye, bila shaka hiyo itakuwa aibu, na itaonekana kana kwamba hatuna pesa. Nyumba ya Mungu ni tajiri, sivyo?” Haijalishi kitu kinagharimu kiasi gani au ubora wake ukoje, maadamu wanaona kinafaa, watamfanya mtu akinunue mara moja, na watamkosoa, kumkemea na hata kumhukumu yeyote anayechelewa kufanya ununuzi huo. Hakuna anayethubutu kusema “hapana” mbele yao, na hakuna anayethubutu kutoa maoni yoyote. Iwe wanafanya shughuli kubwa au ndogo kwa ajili ya nyumba ya Mungu, kanuni zao ni zipi? “Nyumba ya Mungu inahitaji tu kulipa pesa, na iwapo masilahi ya nyumba ya Mungu yanadhurika au la halinihusu. Hivi tu ndivyo ninavyofanya mambo; lazima nianzishe uhusiano mwema na wasioamini. Chochote ambacho wasioamini wanasema ni sahihi, na nitakubaliana nacho. Sitashughulikia mambo kulingana na mahitaji ya nyumba ya Mungu. Iwapo unataka kunitumia, basi fanya hivyo; ikiwa hutaki kunitumia, basi usinitumie—ni juu yako. Hivi tu ndivyo nilivyo!” Je, hii si asili ya kishetani? Watu kama hawa ni watu wa mataifa na wasioamini. Je, wanaweza kutumiwa kushughulikia mambo kwa ajili ya nyumba ya Mungu? Mtu wa aina hii ana elimu fulani, umahiri, na uwezo fulani wa nje, na ni mzuri wa kuzungumza, na anaweza kushughulikia biashara fulani. Lakini haijalishi wanashughulikia mambo gani kwa ajili ya nyumba ya Mungu, bila shaka wanafanya hivyo kiholela na kwa jeuri, wakisababisha madhara kwa masilahi ya nyumba ya Mungu. Pia wao huidanganya nyumba ya Mungu daima na kuficha hali halisi ya mambo, na punde wanapokuwa wamevuruga mambo, nyumba ya Mungu inalazimika ipange mtu wa kurekebisha uharibifu wao. Huu ni mfano halisi wa kula njama na watu wa nje ili kuyasalaiti masilahi ya nyumba ya Mungu. Huku kuna tofauti gani na Yuda kumsaliti Bwana na marafiki zake? Watu wa aina hii wanapotumiwa kutekeleza wajibu, sio tu kwamba wanashindwa kutoa huduma kwa nyumba ya Mungu, bali wanaishia kuwa wabadhirifu na wenye kuleta mkosi. Hawana hata sifa za kuwa watendaji huduma; wao ni watu duni, hakuna lingine! Watu kama hawa ndio hasa watumishi wa Shetani na uzao wa joka kuu jekundu, na punde wanapofichuliwa, wanapaswa kuondolewa na kuondoshwa mara moja. Kama mwumini wa Mungu na mshiriki wa nyumba ya Mungu, hawezi hata kutimiza jukumu lake la kutetea masilahi ya nyumba ya Mungu, je, bado ana dhamiri na busara? Yeye ni duni hata kuliko mbwa wa kulinda!
Aina ya watu ambao ni Yuda hawana neno “Yuda” lililobandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao, lakini matendo na mienendo yao ni ya asili ileile kama ya Yuda, na hupaswi kamwe kuwatumia watu wa aina hii. Ninaposema “hupaswi kuwatumia kamwe”, Ninamaanisha nini? Inamaanisha kwamba hawapaswi kamwe, asilani kukabidhiwa mambo muhimu. Likiwa ni jambo dogo ambalo halina madhara kwa masilahi ya nyumba ya Mungu, ni sawa kuwatumia kwa muda, lakini mtu wa aina hii hakika halingani na kanuni za nyumba ya Mungu za kuwatumia watu, kwa sababu yeye ni Yuda wa kuzaliwa, na asili yake ni mbaya. Kwa ufupi, watu hawa ni watu hatari na hawapaswi kutumiwa kabisa. Kadiri unavyomtumia mtu wa aina hii kwa muda mrefu, ndivyo utakavyohisi wasiwasi zaidi, na ndivyo madhara yatakavyokuwa mengi huko baadaye. Kwa hiyo, ikiwa tayari unaona wazi kwamba wao ni aina ya watu ambao ni Yuda, basi hupaswi kuwatumia kabisa—haya yote ni kweli. Je, inafaa kuwatendea hivi? Watu wengine wanaweza kusema: “Kuwatendea namna hii ni kukosa upendo. Hawajamsaliti yeyote; wanawezaje kuwa Yuda?” Je, unahitaji kusubiri wamsaliti mtu? Yuda alijidhihirisha vipi? Je, kulikuwa na dalili zozote kwamba alikuwa karibu kumsaliti Bwana? (Ndiyo, aliiba pesa kutoka kwa mfuko wa pesa wa Bwana Yesu.) Watu ambao daima husaliti masilahi ya nyumba ya Mungu wana asili sawa na ya Yuda, aliyeiba pesa kutoka kwa mfuko wa pesa. Punde watu kama hawa wanapokamatwa, watafanya usaliti, na kumwambia Shetani kila kitu wanachojua, bila kuficha chochote. Mtu wa aina hii ana kiini cha Yuda. Kiini chake tayari kimefunuliwa na kufichuliwa wazi; hata hivyo, ukimtumia, je, si unajitafutia shida? Je, huku si kuidhuru nyumba ya Mungu kwa makusudi? Watu wengine husema waziwazi, “Mtu yeyote akinipogoa, au mtu yeyote akifanya chochote kinachodhuru masilahi yangu au kuharibu mambo yangu mazuri niliyo nayo hapa, atakiona!” Hasa ni kwamba mtu wa aina hii ana kiini cha Yuda; ni dhahiri sana. Yeye mwenyewe huwaambia wengine kwamba yeye ni Yuda, kwa hivyo mtu wa aina hii hawezi kutumiwa kabisa.
III. Jinsi ya Kuwatendea Marafiki wa Kanisa
Kuna aina nyingine ya watu ambao hawawezi kuhesabiwa kuwa wazuri wala wabaya, na ambao ni waumini kwa jina tu. Ukiwaomba wafanye kitu mara kwa mara, wanaweza kukifanya, lakini hawatajitolea kutekeleza wajibu wao ikiwa hutawapangia. Wakati wowote wanapokuwa na muda wa ziada wanahudhuria mikutano, lakini katika wakati wao wa faragha, haijulikani iwapo wanakula na kunywa maneno ya Mungu, wanajifunza nyimbo, au kuomba. Hata hivyo, wao ni wenye urafiki kiasi kwa nyumba ya Mungu na kanisa. Kuwa wenye urafiki kiasi kunamaanisha nini? Kunamaanisha kwamba ikiwa ndugu na dada watawaomba wafanye jambo, watakubali; kwa ajili ya kuwa waumini wenzao, wanaweza kusaidia kufanya mambo machache, kulingana na uwezo wao. Hata hivyo, wakiombwa watumie nguvu nyingi au walipe gharama ya aina fulani, hakika hawatafanya hivyo. Ikiwa ndugu au dada yuko katika shida fulani na anahitaji wamsaidie, kama vile kusaidia kutunza nyumba mara chache, kupika chakula, au kusaidia kazi ndogondogo mara chache—au mtu huyo anajua lugha ya kigeni na anaweza kuwasaidia ndugu na dada kusoma barua—wanaweza kusaidia kwa jambo la aina hii na wana urafiki kiasi. Kwa kawaida wao huelewana vizuri na wengine na hawana kinyongo na watu, lakini hawahudhurii mikutano kwa mara kwa mara na hawaombi kutekeleza wajibu, sembuse kufanya kazi yoyote muhimu au hata ya hatari. Ukiwaomba wafanye kazi ya hatari, hakika watakataa, wakisema, “Ninamwamini mungu kwa ajili ya kutafuta amani, kwa hivyo nitawezaje kufanya kazi za hatari? Je, huko si kujitafutia shida? Siwezi kamwe kufanya hivyo!” Lakini ikiwa ndugu na dada au kanisa litawaomba wafanye jambo dogo, wanaweza kusaidia na kufanya bidii kidogo, kama rafiki tu. Aina hii ya kujitolea na kusaidia haiwezi kuitwa kutekeleza wajibu, wala haiwezi kuitwa kutenda kulingana na kanuni za ukweli, na sembuse kuitwa kutenda ukweli; ni suala tu la wao kuwa na hisia nzuri kwa waumini wa Mungu na kuwa marafiki kiasi kwao, na kuweza kutoa msaada ikiwa mtu anahitaji msaada. Jina la watu wa aina hii ni lipi? Nyumba ya Mungu inawaita marafiki wa kanisa. Watu wa aina hii ambao ni marafiki wa kanisa wanapaswa kutendewaje? Ikiwa wana ubora wa tabia na vipawa fulani na wanaweza kusaidia kanisa kushughulikia mambo fulani ya nje, basi wao pia ni watendaji huduma na ni marafiki wa kanisa. Hii ni kwa sababu watu wa aina hii hawahesabiwi kama waumini wa Mungu, na nyumba ya Mungu haiwatambui. Na ikiwa hawatambuliwi na nyumba ya Mungu, je, Mungu anaweza kuwatambua kama waumini? (Hapana.) Kwa hiyo, msiwahi kamwe kuwaomba watu wa aina hii wajiunge na safu za wale wanaotekeleza wajibu wa wakati wote. Kuna wale wanaosema: “Watu wengine, wanapoanza kuamini mwanzoni, wana imani haba na wanataka tu kuwa marafiki wa kanisa. Hawaelewi mambo mengi kuhusu kumwamini Mungu, kwa hivyo wanawezaje kuwa tayari kutekeleza wajibu? Wanawezaje kuwa tayari kujitumia kwa moyo wote?” Hatuzungumzii watu ambao wamemwamini Mungu kwa miezi mitatu hadi mitano au hadi mwaka mmoja, bali watu ambao wamemwamini Mungu kwa jina kwa zaidi ya miaka mitatu, au hata kwa miaka mitano au kumi. Haijalishi watu kama hawa wanakiri kiasi gani kwa vinywa vyao kwamba Mungu ndiye Mungu mmoja wa pekee wa kweli na kwamba Kanisa la Mwenyezi Mungu ndilo kanisa la kweli, hilo halithibitishi kwamba wao ni waumini wa kweli. Kulingana na udhihirisho mbalimbali wa watu wa aina hii na namna yao ya imani, tunawaita marafiki wa kanisa. Msiwachukulie kama ndugu au dada—wao si ndugu au dada. Msiwaruhusu watu kama hawa wajiunge na kanisa la wajibu wa wakati wote, na msiwaruhusu wajiunge na safu za wale wanaotekeleza wajibu wa wakati wote; nyumba ya Mungu haiwatumii watu kama hawa. Wengine wanaweza kusema: “Je, Unawabagua watu wa aina hii? Ingawa wanaweza kuonekana vuguvugu kwa nje, kwa kweli ni wenye ari sana kwa ndani.” Haiwezekani kwa waumini wa dhati kumwamini Mungu kwa miaka mitano au kumi na bado wawe vuguvugu; tabia ya watu wa aina hii tayari inafichua kikamilifu kwamba wao ni wasioamini, watu walio nje ya maneno ya Mungu, na wasioamini. Ikiwa bado unawaita ndugu na dada, na bado unasema wanatendewa isivyo haki, basi hayo ni mawazo yako na hisia zako zinazozungumza.
Tunapaswa kuwatendeaje aina ya watu ambao ni marafiki wa kanisa? Wana moyo mwema na wako tayari kusaidia katika kushughulikia mambo machache. Ikiwa wanahitajika, unaweza kuwapa fursa ya kushughulikia mambo machache. Ikiwa wanaweza kufanya kitu, waache wafanye. Kuhusu mambo ambayo hawawezi kufanya vizuri, na ambayo wanaweza hata kuyavuruga, hakika usiwaachie kazi kama hizo, ili kuepuka kuleta shida—huwezi kujiruhusu uhisi kulazimishwa na nia zao njema. Hawaelewi ukweli, wala hawaelewi kanuni. Ikiwa kuna mambo ya nje ambayo wanaweza kushughulikia, waache waendelee. Lakini usiwahi kuwaruhusu washughulikie mambo makuu yanayohusu kazi ya kanisa—katika hali kama hiyo, nia zao njema na msaada wao wa shauku unapaswa kukataliwa. Unapokutana na mtu wa aina hii, shughulika na yeye kwa kijuujuu tu, lakini yaishie hapo; usichukulie mambo kwa uzito na yeye. Kwa nini hupaswi kuchukulia mambo kwa uzito na yeye? Kwa sababu yeye ni rafiki wa kanisa tu, na yeye si ndugu au dada hata kidogo. Je, watu kama hawa wanalingana na kanuni za nyumba ya Mungu za kuwatumia watu? (Hapana.) Kwa hiyo, ikiwa mtu wa aina hii hahudhurii mikutano, hasikilizi mahubiri, au kutekeleza wajibu, hakuna haja ya kumwalika. Ikiwa hali na kunywa maneno ya Mungu au kuomba, ikiwa hatafuti kanuni za ukweli wakati wowote mambo yanapompata, na ikiwa hayuko tayari kujihusisha na ndugu na dada, hakuna haja ya kumtegemeza au kumsaidia. Maneno mawili—usijishughulishe na yeye. Usichukulie mambo kwa uzito na aina ya watu ambao ni marafiki wa kanisa na wasioamini, na usijishughulishe nao. Hakuna haja ya kuhangaika juu yao, na hakuna haja ya kuulizia hali zao. Kwa nini usiulizie hali zao? Kuna maana gani ya kuulizia hali za watu ambao hawana uhusiano wowote nasi? Ni jambo la ziada, sivyo? Je, mnataka kuwajali watu wa aina hii? Labda mnapenda kuwa wadadisi na mnataka kujali, na mnawaza, “Wanaendeleaje sasa hivi? Wameoa au la? Je, wanaendelea vizuri? Wanafanya kazi gani sasa?” Haijalishi wanaendeleaje, hilo halikuhusu. Kuna maana gani ya kujihusisha na hilo? Usijali kuhusu watu hawa hata kidogo, na usitoe maoni juu yao pia. Watu wengine wanapenda kutoa maoni, kama vile: “Unaona? Hawamwamini Mungu ipasavyo, wanaishi maisha ya kukatisha tamaa na kuchosha kila siku, na wanaonekana waliochoka sana na hoi wakati wote,” au “Unaona? Hawamwamini Mungu ipasavyo, kwa hivyo hawana amani, na jambo baya lilitokea katika familia yao tena.” Yote haya ni upuuzi, na hayahitajiki. Jinsi wanavyoishi maisha yao na jinsi wanavyotembea katika njia yao hayakuhusu. Hata usiwataje; hamko katika njia moja nao. Wewe unajitumia kwa dhati kwa ajili ya Mungu na kutekeleza wajibu wako wa wakati wote, unataka tu kufuatilia kupata ukweli na kufikia wokovu, na haijalishi kile ambacho Mungu anasema, unataka kufanya uwezavyo kumridhisha Yeye; watu hao hawana mambo haya mioyoni mwao. Unapoona mitindo miovu, unahisi kuchukizwa na kukerwa nayo, na unahisi kwamba hakuna furaha kuishi katika ulimwengu huu, na unaweza kupata furaha tu kwa kumwamini Mungu; ilhali wao ni kinyume kabisa na wewe: Hili linathibitisha kwamba hawako katika njia moja na wewe. Kanuni ya nyumba ya Mungu ya kumshughulikia mtu wa aina hii ni kwamba ikiwa yuko tayari kusaidia, nyumba ya Mungu inaweza kumpa fursa maadamu hakuna madhara yanayoweza kutokea baadaye. Ikiwa nyumba ya Mungu haina matumizi na yeye kabisa na bado yuko tayari kusaidia, basi ni bora kukataa kwa heshima—usijitafutie shida. Waumini hushiriki juu ya ukweli kila siku na kukubali kupogolewa, lakini bado wanaweza kufanya mambo kijuujuu tu, basi, je, marafiki wa kanisa wanaweza kushughulikia mambo ipasavyo bila malipo yoyote? (Hapana, hawawezi.) Niambieni, je, fikira hii ni kuwawazia watu vibaya zaidi? Je, huku ni kuwatazama watu kwa mtazamo hasi kuzidi kiasi? (Hapana.) Huku ni kuzungumza kulingana na ukweli wa mambo, kuzungumza kulingana na kiini cha watu. Usiwe mjinga, usiwe mpumbavu, na usifanye chochote cha kijinga. Waumini bado wanapaswa kupitia upogoaji, hukumu na kuadibiwa, nidhamu kali, kurudiwa, na kufichuliwa kabla ya utendaji wa wajibu wao ufikie kulingana kidogo kidogo na nia ya Mungu. Rafiki wa kanisa au mtu wa mataifa hakubali ukweli wowote, na anachofikiria tu ni masilahi yake mwenyewe, kwa hivyo ni wema gani unaoweza kutokana na yeye kushughulikia mambo kwa ajili ya nyumba ya Mungu au kwa ajili ya ndugu na dada? Hilo haliwezekani kabisa. Inafaa tu kutojishughulisha na watu wa aina hii, sivyo? (Ndiyo.) Inamaanisha nini, “kutojishughulisha nao”? Inamaanisha kwamba nyumba ya Mungu haiwahesabu kama waumini. Wanaweza kumwamini Mungu vyovyote wanavyopenda, lakini kazi na mambo ya nyumba ya Mungu hayahusiani nao hata kidogo. Wako tayari kusaidia, lakini lazima tupime mambo na kukadiria iwapo wanafaa kuifanya, na ikiwa hawafai, hatuwezi kuwapa fursa hii. Niambieni, je, kutenda kwa njia hii kunalingana na kanuni? Je, tuna haki ya kuwatendea watu kama hawa hivi? Tunayo kabisa!
IV. Jinsi ya Kuwatendea Watu Waliotimuliwa
Kuna aina nyingine ya watu, yaani wale ambao wametimuliwa. Tunapaswa kuwatendeaje? Iwe watu hawa wametimuliwa kwa sababu hawawezi kufanya kazi halisi na wameainishwa kama viongozi wa uwongo, au kwa sababu wanafuata njia ya wapinga Kristo na wameainishwa kama aina ya watu ambao ni wapinga Kristo, ni lazima kuwapangia watu hawa kazi nyingine kwa njia inayofaa, na kuwafanyia mipango inayofaa. Ikiwa wao ni wapinga Kristo ambao wametenda mambo mengi maovu, basi bila shaka wanapaswa kufukuzwa; ikiwa hawajatenda mambo mengi maovu, lakini wana kiini cha mpinga Kristo na wameainishwa kama wapinga Kristo, basi maadamu bado wanaweza kutumika kwa namna fulani bila kusababisha vurugu au usumbufu, hawahitaji kufukuzwa—waache waendelee kutumika na muwape nafasi ya kutubu. Kwa upande wa viongozi wa uwongo ambao wametimuliwa, wapangie kufanya kazi tofauti kulingana na vipawa vyao na wajibu wanaofaa kutekeleza, lakini hawaruhusiwi tena kutumika kama viongozi wa kanisa; kwa upande wa viongozi na wafanyakazi ambao wametimuliwa kwa sababu ubora wao wa tabia ni duni sana na hawawezi kufanya kazi yoyote, pia wapangie kufanya kazi tofauti kulingana na vipawa vyao na wajibu wanaofaa kutekeleza, lakini hawawezi tena kuendelezwa kama kiongozi au mfanyakazi. Kwa nini hawawezi? Tayari wamejaribiwa. Walifunuliwa, na tayari ni wazi kuona kwamba ubora wa tabia na uwezo wa kazi wa watu kama hao unawafanya wasifae kuwa viongozi. Ikiwa hawafai kuwa viongozi, je, hawawezi kutekeleza wajibu mwingine? Si lazima iwe hivyo. Ubora wao duni wa tabia unawafanya wasifae kuwa viongozi, lakini wanaweza kutekeleza wajibu mwingine. Baada ya watu kama hao kutimuliwa, wanaweza kufanya chochote wanachofaa kufanya. Hawapaswi kunyang’anywa haki ya kutekeleza wajibu; bado wanaweza kutumiwa tena punde tu kimo chao kitakapokua hapo baadaye. Wengine wanatimuliwa kwa sababu ni vijana na hawana uzoefu wowote wa maisha, na pia wanakosa uzoefu wa kazi, kwa hivyo hawawezi kujitwika mzigo wa kazi na hatimaye wanatimuliwa. Katika kuwatimua watu wa aina hii, kuna uhuru fulani. Ikiwa ubinadamu wao unafikia kiwango kinachostahili na ubora wao wa tabia unatosha, wanaweza kutumiwa baada ya kushushwa cheo, au wanaweza kuwekwa kufanya kazi nyingine inayowafaa. Punde tu uelewa wao wa ukweli unapokuwa wazi, na wakipata kupitia na uzoefu kiasi wa kazi ya kanisa, watu kama hao bado wanaweza kupandishwa cheo na kustawishwa tena kulingana na ubora wao wa tabia. Ikiwa ubinadamu wao unafikia kiwango kinachostahili lakini ubora wao wa tabia ni duni sana, basi hakuna thamani yoyote ya kuwastawisha, na hawawezi kabisa kustawishwa au kubakishwa.
Miongoni mwa wale walioondolewa, kuna aina mbili za watu ambao hawapaswi kamwe kuendelezwa na kusitawishwa tena. Aina moja ni wapinga Kristo, na nyingine ni wale ambao ubora wao wa tabia ni duni sana. Kisha kuna baadhi ya watu ambao hawahesabiwi kuwa wapinga Kristo, lakini wana ubinadamu duni tu, ni wabinafsi na wadanganyifu, na baadhi ya watu hawa ni wavivu, wanatamani starehe za mwili na hawawezi kuvumilia ugumu. Hata kama watu kama hao wana ubora mzuri sana wa tabia, hawawezi endelezwe tena. Kama wana ubora kiasi wa tabia, basi waache wafanye chochote wanachoweza kufanya, mradi tu mipango inayofaa ifanywe kwa ajili ya hilo; kwa ufupi, usiwaendeleze kuwa kiongozi au mfanyakazi. Mbali na kuwa na ubora wa tabia na uwezo wa kazi, viongozi na wafanyakazi wanahitaji kuelewa ukweli, wawe na mzigo kwa ajili ya kanisa, waweze kufanya kazi kwa bidii na kuvumilia ugumu, na lazima wawe wenye bidii na wasiwe wavivu. Juu ya haya, lazima wawe waaminifu na wanyofu kiasi. Huwezi kamwe kuwachagua watu walio wadanganyifu. Wale ambao ni wapotovu sana na wadanganyifu daima hufanya hila dhidi ya ndugu na dada, viongozi wao wa ngazi za juu, na nyumba ya Mungu. Wao hutumia siku zao kufikiria tu mawazo potovu. Unaposhughulika na mtu kama huyo, lazima kila mara ukisie kile anachofikiria hasa, lazima uendelee kuulizia kile ambacho amekuwa akifanya hivi karibuni hasa, na lazima kila mara umwangalie. Kumtumia mtu kama huyo kunachosha sana na kunaleta mahangaiko mengi. Ikiwa mtu wa aina hii ataendelezwa cheo kutekeleza wajibu, hata akielewa mafundisho kidogo, hatayatekeleza, na atatarajia faida na manufaa kwa kila kazi ndogo anayofanya. Kumtumia mtu kama huyo kunaleta mahangaiko mengi na ni shida sana, kwa hivyo watu kama hao hawawezi kuendelezwa. Kwa hivyo, linapokuja suala la wapinga Kristo, wale walio na ubora duni sana wa tabia, wale walio na ubinadamu mbaya, wale walio wavivu, wanaotamani starehe za mwili na hawawezi kuvumilia ugumu, na wale ambao ni wapotovu wadanganyifu na wadangayifu sana—mara tu watu wa aina hizi wamefichuliwa na kuondolewa baada ya kutumiwa, usiwaendeleze mara ya pili; usiwatumie tena kwa namna isiyofaa baada ya kung’amuliwa. Wengine wanaweza kusema, “Mtu huyu hapo awali aliainishwa kama mpinga Kristo. Tumegundua kwamba amekuwa akifanya vizuri kwa muda sasa, anaweza kushirikiana na ndugu na dada kwa kawaida na hawakandamizi tena wengine. Je, anaweza kuendelezwa cheo?” Usiwe na haraka kiasi hicho—punde tu anapoendelezwa na kupata hadhi, asili yake ya kupinga Kristo itafichuliwa. Wengine wanaweza kusema: “Ubora wa tabia wa mtu huyu ulikuwa duni sana hapo awali; alipoombwa kusimamia kazi ya watu wawili, hakujua jinsi ya kugawa kazi, na mambo mawili yangetokea kwa wakati mmoja, hakujua jinsi ya kufanya mipango inayofaa. Sasa kwa kuwa amekuwa mkubwa kidogo, atakuwa bora zaidi katika mambo haya, sivyo?” Je, dai hili lina ukweli wowote? (Hapana, halina.) Mambo mawili yanapotokea kwa wakati mmoja, mtu huyo huchanganyikiwa na hajui jinsi ya kuyashughulikia. Hawezi kumng’amua yeyote wala kung’amua chochote. Ubora wake wa tabia ni duni sana kiasi kwamba hana uwezo wa kazi wala uwezo wa kufahamu. Mtu kama huyo hapaswi kamwe kuendelezwa kama kiongozi tena. Hili si suala la umri. Watu wenye ubora duni wa tabia bado watakuwa na ubora duni wa tabia watakapokuwa na umri wa miaka themanini. Sio kama watu wanavyowaza, kwamba mtu anapozidi kuwa mkubwa na kupata uzoefu zaidi, anaweza kuelewa kila kitu—hivyo sivyo ilivyo. Watakuwa tu na uzoefu fulani wa maisha, lakini uzoefu wa maisha si sawa na ubora wa tabia. Haijalishi mtu anapitia mambo mangapi au anajifunza mafunzo mangapi, haimaanishi kwamba ubora wake wa tabia utaboreka.
Ikiwa ubinadamu wa mtu ni wa ubinafsi sana, wa udanganyifu sana, na wa uovu sana, na yeye amejaa hila, na anajifikiria mwenyewe tu, je, mtu wa aina hii anaweza kubadilika? Aliondolewa kwa sababu hizi; sasa miaka kumi imepita na amesikiliza mahubiri mengi—je, ubinadamu wake sio wa ubinafsi, wa upotovu na wa udanganyifu tena? Acha Nikuambie: Mtu wa aina hii hatabadilika, atakuwa vilevile miaka 20 mingine ijayo. Kwa hivyo, ukikutana na yeye tena baada ya miaka 20 na umwulize kama bado ni mbinafsi na mdanganyifu kiasi hicho, yeye mwenyewe atakiri. Kwa nini watu wenye ubinadamu mbaya hawatabadilika? Je, wanaweza kubadilika? Tukidhani kwamba wangeweza kubadilika, msingi na masharti ya hilo kufanyika yangekuwa yapi? Lazima waweze kukubali ukweli. Watu wenye ubinadamu duni hawakubali ukweli, na moyoni wanadharau, wanachukia, wanadhihaki, na ni wenye uhasama kwa vitu chanya—hawawezi tu kubadilika. Kwa hivyo haijalishi ni miaka mingapi imepita, usiwaendeleze, kwa sababu hawawezi kubadilika. Inawezekana kwamba katika muda wa miaka 20, watakuwa wamejifunza kuwa watu wajanja zaidi, na hodari zaidi katika kusema maneno matamu na mambo yanayowadanganya wengine. Lakini ukishirikiana na watu hawa na uchunguze matendo yao, utagundua ukweli mmoja, ambao ni kwamba hawajabadilika hata kidogo. Unadhania kwamba baada ya miaka mingi kupita na wamesikiliza mahubiri mengi na kutekeleza wajibu katika nyumba ya Mungu kwa muda mrefu, wanapaswa kuwa wamebadilika—umekosea! Hawatabadilika. Kwa nini? Wamesikiliza mahubiri mengi na kusoma maneno mengi ya Mungu, lakini hawakubali wala kutenda kulingana na sentensi hata moja, kwa hivyo hawajabadilika hata kidogo, haiwezekani kwao kubadilika. Punde watu kama hao wanapofichuliwa na kuondolewa, hawawezi kutumiwa tena, na ukiwatumia, unaidhuru nyumba ya Mungu na ndugu na dada. Ikiwa huna uhakika, angalia tu jinsi wanavyotenda, na uone ni masilahi ya nani wanayotetea wanapokabiliwa na mambo yanayoleta mgongano kati ya masilahi yao wenyewe na masilahi ya nyumba ya Mungu; hawatayatoa masilahi yao wenyewe na kujitolea kikamilifu kutetea masilahi ya nyumba ya Mungu. Ukiliangalia kwa mtazamo huu, hawaaminiki, na hawastahili kuendelezwa na kutumiwa na nyumba ya Mungu. Hiyo ndiyo sababu watu kama hao wameamuriwa kutotumiwa. Je, watu wasiokubali ukweli bado wanaweza kubadilika? Haiwezekani, na ni ndoto ya kipumbavu!
Kuhusu watu ambao ni wavivu, wanatamani starehe za mwili, na hawawezi kuvumilia hata ugumu kidogo, wao wana uwezo mdogo hata zaidi wa kubadilika. Wakati wa kipindi chao kama kiongozi, hawateseki na ugumu wowote, hawavumilii hata ugumu ambao ndugu na dada wa kawaida wanaweza kuvumilia. Katika kutekeleza wajibu wao wanafanya tu mambo kijuujuu—kufanya mikutano na kuhubiri mafundisho fulani, kisha kwenda kulala ili kujitunza. Usiku, wakienda kulala wakiwa wamechelewa hata kidogo, bado watakuwa wamelala fofofo asubuhi wakati ndugu na dada wanapoamka. Hawako tayari kuchoka hata kidogo au kuwa na shughuli nyingi kidogo, au kuvumilia hata ugumu kidogo. Hawalipi gharama yoyote na hawafanyi kazi yoyote halisi. Popote wanapokwenda, punde wanapoona chakula na kinywaji kizuri, wao hufurahi sana kiasi kwamba wao husahau kila kitu kingine, na hawaendi popote, bali wao hubaki hapo wakila, kunywa na kujifurahisha, na bila kufanya kazi yoyote ile. Hawasikilizi wanapopogolewa na Aliye juu, wala hawakubali kumbusho na ufichuzi kutoka kwa ndugu na dada. Wanachagua kuishi maisha kwa njia ya starehe iwezekanavyo, bila kulipa gharama yoyote, na bila kutimiza majukumu yao au kutekeleza wajibu wao, na hivyo wanakuwa nyangarika. Je, watu kama hao wanaweza kubadilika? Watu wa aina hii ni wavivu sana, wanatamani starehe za mwili; hawawezi kubadilika. Hivi ndivyo walivyo sasa na hivi ndivyo watakavyokuwa katika siku zijazo. Watu wengine wanaweza kusema: “Mtu huyo amebadilika, amekuwa akiweka bidii nyingi katika kazi yake kwa muda sasa.” Usiwe na haraka kiasi hicho. Ukimwendeleza awe kiongozi, atarudia tabia zake za zamani—hivyo tu ndivyo alivyo. Yeye ni kama mcheza kamari, ambaye, anapoishiwa na pesa, ataendelea kucheza kamari hata kama atalazimika kukopa pesa, kuuza nyumba yake, au hata kuwauza mke na watoto wake. Ikiwa hachezi kamari siku hizi, inaweza kuwa ni kwa sababu jumba la kamari limefungwa na hakuna mahali pa kuchezea kamari, au kwa sababu marafiki zake wote wa kamari wamekamatwa na hakuna mtu wa kucheza naye kamari tena, au kwa sababu ameuza vitu vyote anavyoweza kuuza na hana pesa iliyobaki ya kuchezea kamari. Punde anapokuwa na pesa mikononi mwake, ataanza kucheza kamari tena na hataweza kuacha—hivyo tu ndivyo alivyo. Vivyo hivyo, wale walio wavivu na wanaotamani starehe za mwili pia hawawezi kubadilika. Punde wanapopata hadhi fulani, watarudia mara moja umbo lao la asili, na sura yao halisi itafichuliwa. Wanapokuwa hawana hadhi, hakuna anayewafikiria sana na hakuna anayewatumikia, na ikiwa hawafanyi chochote, basi wanapaswa kuondolewa, kwa sababu kanisa haliwategemezi watu wazembe, kwa hivyo hawana chaguo ila kufanya mambo fulani shingo upande. Wanafanya mambo tofauti na wengine. Wengine hufanya mambo kwa kujituma, ilhali wao huyafanya bila hiari. Ingawa kwa nje hakuna tofauti, katika kiini kuna tofauti. Wengine wanapokuwa na hadhi, wao hufanya kile wanachopaswa kufanya na wanaweza kutimiza majukumu yao; punde watu hawa wanapokuwa na hadhi, wao hutumia fursa hiyo kufurahia manufaa ya hadhi yao na hawafanyi kazi yoyote, na kiini cha asili yao ya uvivu na kutamani starehe kinafichuliwa hivyo. Kwa hivyo, watu wa aina hii hawatabadilika katika hali yoyote, na punde wanapofichuliwa na kuondolewa, watu kama hao hawapaswi kamwe kuendelezwa na kutumiwa tena—hii ndiyo kanuni.
Kuhusu watu wenye hali tofauti, hizi ndizo kanuni za kuwaendeleza na kuwatumia. Kiwango cha chini kabisa ni kwamba wanaweza kutoa nguvu na kutumikia katika nyumba ya Mungu bila kusababisha vurugu; katika hali hiyo, wanaweza kutekeleza wajibu katika nyumba ya Mungu. Ikiwa hawawezi hata kufikia kiwango hiki cha chini kabisa, basi haijalishi ubinadamu wao na vipawa vyao vikoje, hawafai kutekeleza wajibu, na watu wa aina hii wanapaswa kuondoshwa kutoka kwa safu ya wale wanaotekeleza wajibu. Ikiwa ubinadamu wa mtu ni mwenye kudhuru na ni sawa na ule wa mpinga Kristo, basi punde tu inapothibitishwa kwamba yeye ni mpinga Kristo, nyumba ya Mungu haitamtumia kamwe, wala kumwendeleza au kumsitawisha. Watu wengine wanaweza kusema: “Je, ni sawa kumruhusu atumike?” Inategemea na hali. Ikiwa kutumika kwake kunaweza kuwa na athari hasi na kuleta matokeo mabaya kwa nyumba ya Mungu, basi nyumba ya Mungu haitampa hata fursa ya kutumika. Ikiwa anajua kwamba yeye mwenyewe ni mtu mwovu au mpinga Kristo aliyetimuliwa, lakini yuko tayari kutumika, na atafanya mambo vyovyote vile kanisa linavyompangia afanye, na anaweza kutumika kwa nidhamu bila kudhuru masilahi yoyote ya nyumba ya Mungu, basi katika hali hiyo anaweza kubakishwa. Ikiwa hawezi hata kumudu kutumika ipasavyo, na kutumika kwake kunaleta madhara zaidi kuliko faida, basi hatakuwa hata na fursa ya kutumika, na hata akitumika, nyumba ya Mungu bado haitamtumia, kwa sababu hastahili wala hatimizi vigezo vya kutumika. Kwa hivyo watu wa aina hii hawapaswi kurudi—waache waende popote wanapotaka. Watu wengine wanaweza kusema, “Ikiwa nyumba ya mungu hainitumii, basi nitaihubiri injili mimi mwenyewe, na nitawakabidhi watu ninaowapata kupitia kuhubiri injili kwa nyumba ya Mungu.” Je, hilo lingekuwa sawa? (Ndiyo.) Wengine wanaweza kusema, “Wewe humtumii mtu huyo hata kutumika, kwa hivyo kwa msingi gani wakupe Wewe watu wanaowapata kwa kuhubiri injili? Kwa msingi gani wakuhubirie injili Wewe?” Nyumba ya Mungu haiwatumii kwa sababu ya vipengele mbalimbali. Kimoja ni kwamba hawapatani na kanuni za nyumba ya Mungu za kuwatumia watu. Kingine ni kwamba nyumba ya Mungu haithubutu kuwatumia watu wa aina hii, kwa sababu punde tu wanapotumiwa, kutakuwa na shida zisizoisha. Basi tunapaswa kulielezea vipi suala hili la wao kuwa tayari kuhubiri injili? Kile wanachoshuhudia katika kuhubiri injili ni Mungu, na ni kwa sababu ya maneno ya Mungu na kazi ya Mungu ndiyo wanaweza kuwapata watu. Ingawa watu hawa wamepatikana kupitia kwa mtu huyo kuhubiri injili, hili kwa vyovyote vile halihesabiwi kuwa sifa kwao. Kwa kiwango kizuri zaidi, ni kutimiza tu majukumu yao kama mwanadamu. Bila kujali kama wewe ni mpinga Kristo au mtu mwovu, au kama umeondolewa au umetimuliwa, kutimiza majukumu yako kama mwanadamu ni kitu unachopaswa kufanya. Kwa nini Ninasema kwamba ni jambo unalopaswa kufanya? Umepokea usambazaji mkubwa kiasi hicho wa ukweli kutoka kwa Mungu, na hii pia ni damu ya moyo ya Mungu. Nyumba ya Mungu imekunyunyizia na kukupa mahitaji kwa miaka mingi sana, lakini, je, Mungu anadai chochote kutoka kwako? La. Vitabu vyote mbalimbali vinavyosambazwa na nyumba ya Mungu ni vya bure, hakuna anayepaswa kutumia hata senti moja. Vivyo hivyo, njia ya kweli ya uzima wa milele na maneno ya uzima ambayo Mungu huwapa wanadamu ni ya bure, na mahubiri na ushirika wa nyumba ya Mungu yote ni bure kwa watu kusikiliza. Kwa hivyo, iwe wewe ni mtu wa kawaida au mshiriki wa kikundi maalum, umepokea ukweli mwingi kiasi hicho kutoka kwa Mungu bila malipo, hakika ni sahihi tu kwamba unapaswa kueneza maneno ya Mungu na injili ya Mungu kwa watu na kuwaleta watu mbele za Mungu, sivyo? Mungu amewapa wanadamu ukweli wote; ni nani anayeweza kumudu kulipa upendo mkuu kiasi hicho? Neema ya Mungu, maneno ya Mungu, na uzima wa Mungu havina bei, na hakuna mwanadamu anayeweza kumudu kuvilipa! Je, maisha ya mwanadamu yana thamani kiasi hicho? Je, yanaweza kuwa na thamani kama ukweli? Kwa hivyo, hakuna anayeweza kumudu kulipa upendo na neema ya Mungu, na hiyo inajumuisha wale ambao wameondolewa, wametimuliwa, na kuondoshwa na kanisa—wao pia hawajasazwa. Maadamu una dhamiri, busara, na ubinadamu kiasi, basi haijalishi nyumba ya Mungu inakutendeaje, unapaswa kutimiza wajibu wako wa kueneza maneno ya Mungu na kushuhudia kazi Yake. Hili ni jukumu la watu lisiloweza kukwepwa. Kwa hivyo, haijalishi unawahubiria watu wangapi maneno ya Mungu na injili Yake, au unapata watu wangapi, hili si jambo la kusifiwa. Mungu ameonyesha ukweli mwingi kiasi hicho na bado huusikilizi au kuukubali. Hakika kutumika kidogo na kuhubiri injili kwa wengine ndicho unachopaswa kuwa ukifanya, sivyo? Kwa kuwa umefika hapa leo, je, hupaswi kutubu? Je, hupaswi kutafuta fursa za kulipa upendo wa Mungu? Unapaswa kweli! Nyumba ya Mungu ina amri za utawala, na kuwaondoa watu, kuwatimua, na kuwaondosha ni mambo yanayofanywa kulingana na amri za utawala na kulingana na mahitaji ya Mungu—kufanya mambo haya ni sahihi. Watu wengine wanaweza kusema, “Inaaibisha kidogo kuwakubali kanisani watu waliopatikana kwa kuhubiri injili na wale ambao wameondolewa au kutimuliwa.” Kwa kweli, huu ni wajibu ambao watu wanapaswa kufanya, na hakuna kitu cha kuaibisha. Watu wote ni viumbe walioumbwa. Hata kama umeondolewa au kutimuliwa, na kuhukumiwa kama mtu mwovu au mpinga Kristo, au wewe ni mlengwa wa kuondoshwa, je, bado wewe si kiumbe aliyeumbwa? Punde tu unapoondolewa, je, Mungu bado si Mungu wako? Je, maneno ambayo Mungu amekuambia na mambo ambayo Mungu amekupa yamefutwa kwa mpigo mmoja? Je, yanaacha kuwepo? Bado yapo, ni vile tu huyathamini. Watu wote waliobadilishwa, haijalishi ni ni nani aliyewabadilisha, ni viumbe walioumbwa na wanapaswa kujisalimisha mbele ya Muumba. Kwa hivyo, ikiwa watu hawa ambao wameondolewa au kutimuliwa wako tayari kuhubiri injili, hatutawazuia; lakini haijalishi wanahubiri vipi, kanuni za nyumba ya Mungu za kuwatumia watu na amri za utawala za nyumba ya Mungu hazibadiliki, na hili halitabadilika kamwe.
Miongoni mwa aina hizi kadhaa za watu ambao wameondolewa, wengi hawawezi kutubu kweli na hawapaswi kutumiwa tena. Kuna nafasi tu ya kuwaendeleza na kuwatumia wale walioondolewa au ambao wajibu wao ulibadilishwa kwa sababu walikosa uzoefu wa kazi na hivyo hawakuweza kufanya kazi yao kwa muda. Watu wa aina hii wana ubora wa tabia wa kutosha na hakuna matatizo makubwa katika ubinadamu wao, wana mapungufu madogo tu, tabia mbaya, au mazoea mabaya yaliyorithiwa kutoka kwa familia zao—hakuna hata moja ya mambo haya ambalo ni tatizo kubwa. Ikiwa nyumba ya Mungu inawahitaji, wanaweza kuendelezwa na kutumiwa tena kwa wakati unaofaa; hili ni jambo la busara, kwa sababu wao si watu waovu na hawatakuwa wapinga Kristo. Ubora wao wa tabia unatosha, ni vile tu walikuwa hawajafanya kazi kwa muda mrefu na hawakuwa na uzoefu, kwa hivyo hawakuweza kumudu kazi hiyo, jambo ambalo si tatizo kubwa. Ikiwa waliondolewa kwa sababu hizi, basi wana nafasi ya kuendelea katika siku zijazo na wanaweza kubadilika. Maadamu mtu ana uwezo wa kazi, anamiliki ubora wa tabia, na ubinadamu wake unafikia kiwango kinachostahili, basi katika kipindi ambacho anapitia kazi ya Mungu na kutekeleza wajibu wake, watu wa aina hii watabadilika polepole, ubinadamu wao utabadilika, watakua katika kuingia kwao katika uzima, kutakuwa na mabadiliko fulani linganifu katika tabia yao, na kutakuwa na maendeleo fulani katika uelewa wao wa ukweli. Kulingana na mazingira, wajibu wanaotekeleza, na azimio lao la kibinafsi, watabadilika na kukua kwa viwango tofauti, kwa hivyo inaweza kusemwa kwamba watu wa aina hii ni wa kuendelezwa na kutumiwa. Hizi kwa ujumla ndizo kanuni za kuendelezwa tena na kuwatumia aina kadhaa za watu ambao wameondolewa hapo awali.
Kipengele cha saba cha majukumu ya viongozi na wafanyakazi ni “Kuwatenga na kuwatumia watu wa aina tofauti kwa busara, kwa kuzingatia ubinadamu na nguvu zao, ili kila mmoja atumike kadiri ya ubora wake.” Katika ushirika wetu hivi punde, maana ya kumtumia mtu kadiri ya ubora wake ilielezwa waziwazi. Maadamu kuna thamani hata kidogo ya kumsitawisha mtu, na mradi tu ubinadamu wake unafikia kiwango kinachostahili, basi nyumba ya Mungu itampa fursa. Maadamu mtu anafuatilia ukweli na anapenda vitu chanya, basi nyumba ya Mungu haitamkataa au kumwondoa kiurahisi hivyo. Maadamu ubinadamu wako na ubora wako wa tabia unafikia viwango ambavyo Nimeshiriki kuhusu hivi punde, nyumba ya Mungu hakika itakuwa na nafasi kwa ajili yako ya kutekeleza wajibu, na hakika itakutumia kwa busara, na kukupa nafasi ya kutosha ya kudhihirisha uwezo wako. Kwa ufupi, ikiwa una vipawa na ustadi katika taaluma fulani ambavyo vinahitajika kwa kazi ya kanisa, basi nyumba ya Mungu hakika itakuacha utekeleze wajibu unaofaa. Hata hivyo, ikiwa huna azimio au nia na hutaki kujitahidi kwenda juu, basi fanya tu chochote unachoweza, fanya wajibu fulani ambao uko ndani ya uwezo wako wa kufanya, na si chochote zaidi. Ikiwa una azimu, na unasema, “Ninataka kuelewa na kupata ukweli zaidi, na kuanza njia ya wokovu haraka iwezekanavyo, na kuingia katika uhalisi wa ukweli. Niko tayari kuujali mzigo wa Mungu, niko tayari kubeba mzigo mzito katika nyumba ya Mungu, kuteseka na ugumu zaidi kuliko wengine, kujitumia zaidi na kuacha mengi zaidi kuliko wengine,” na ikiwa unafaa katika nyanja zote, lakini bado hakuna anayekupendekeza, basi unaweza pia kujipendekeza. Je, hilo si jambo la busara? Kwa muhtasari, hizi zote ni kanuni za nyumba ya Mungu za kuwatumia watu wa kila aina, lengo likiwa si lingine ila kuwawezesha watu kuingia katika uhalisi wa ukweli. Je, udhihirisho wa kuingia katika uhalisi wa ukweli ni upi? Ni kuelewa ukweli, kuelewa kanuni za ukweli wakati wa kufanya vipengele mbalimbali vya kazi, na kuweza kutenda ukweli linganifu wakati wa kushirikiana na kila aina ya watu, matukio, na vitu katika maisha ya kila siku, badala ya kuchanganyikiwa na kutojua la kufanya wakati wowote jambo lolote linapokupata—hili ndilo lengo. Kwa kuwa hili ndilo lengo ambalo limewekwa, mnapaswa kulifuatilia!
Huu ndio mwisho wa ushirika wetu juu ya kipengele cha saba cha majukumu ya viongozi na wafanyakazi. Watu wengine wanaweza kusema, “Hujamaliza kufanya ushirika bado, Hujawafichua viongozi wa uwongo kuhusiana na kipengele hiki.” Ningejibu kwamba hakuna haja ya kuwafichua. Kwa upande mmoja, viongozi wa uwongo wana ubora duni wa tabia na hawawezi kufanya kazi halisi; kwa upande mwingine, hawana dhamiri na busara, hawabebi mzigo wowote, hawatilii maanani kazi yao hata kidogo, na hawawezi hata kufanya mambo rahisi vizuri. Wakati wowote wanapokumbana na tatizo tata, au tatizo linalohusiana na kanuni za ukweli, hawawezi kulitofautisha hata kidogo, na sembuse kuweza kung’amua kiini cha tatizo hilo. Kwa hivyo, hakuna haja ya kuwafichua. Hata kama wangefichuliwa, hawangekubali, na lingekuwa ni upotevu wa maneno. Zaidi ya hayo, kuzungumzia mambo ambayo wamefanya kungechefuisha na kuwakasirisha watu sana moyoni. Kuikabidhi kazi muhimu kama hiyo kwa viongozi hawa wa uwongo kulikuwa kosa katika kuwatumia watu. Kutoweza kufanya kazi yao tayari kunawafanya wajihisi kuwa nyangarika, na ikiwa watafichuliwa na kuchanganuliwa, watahisi uchungu zaidi. Kwa hivyo waache viongozi hawa wa uwongo wajipime wenyewe kwa kulinganisha na kuchunguza matatizo yao wenyewe kadiri wawezavyo. Ikiwa unaweza kugundua matatizo yako, angalia kama unaweza kufanya maboresho katika siku zijazo; ikiwa huwezi kuyagundua, basi unahitaji kuendelea kuchunguza, na unaweza pia kuwaomba watu walio karibu na wewe wakusaidie kuchambua na kuainisha. Ikiwa wengine wamefanya ushirika na wewe na umelitilia maanani lakini bado huwezi kugundua matatizo yako mwenyewe, na bado hujui jinsi ya kuyatambua au jinsi ya kuyatatua, basi wewe ni kiongozi wa uwongo kweli na unapaswa kuondoshwa.
Tarehe 6 Machi, 2021