Unapaswa Kujua Namna Ambavyo Binadamu Wote Wameendelea Hadi Siku ya Leo
Kazi yote ya miaka 6,000 imebadilika kwa utaratibu kulingana na nyakati. Mabadiliko katika kazi hii yamefanyika kulingana na hali za ulimwengu mzima. Kazi ya usimamizi ya Mungu imebadilika tu kwa utaratibu kulingana na mitindo ya kimaendeleo ya binadamu kwa ujumla; haikuwa imepangwa tayari mwanzoni mwa uumbaji. Kabla ya ulimwengu kuumbwa, au punde tu baada ya kuumbwa kwake, Yehova bado hakuwa amepanga hatua ya kwanza ya kazi, ile ya sheria; hatua ya pili ya kazi, ile ya neema; au hatua ya tatu ya kazi, ile ya kushinda, ambapo Angefanya kazi kwanza miongoni mwa kundi la watu—baadhi ya vizazi vya Moabu, na kupitia hili Angeweza kuushinda ulimwengu mzima. Hakuyaongea maneno haya baada ya kuumba ulimwengu; Hakuyaongea maneno haya baada ya Moabu, wala hata kabla ya Lutu. Kazi Yake yote ilifanywa bila kupangwa. Hivi ndivyo hasa kazi Yake yote ya usimamizi wa miaka elfu sita imeendelea; kwa vyovyote vile, kabla ya kuiumba dunia, Hakuwa ameandika mpango kama huo kwa mtindo wa kitu kama “Chati ya Muhtasari wa Maendeleo ya Binadamu.” Katika kazi ya Mungu, Anaonyesha moja kwa moja kile Alicho; Hapigi bongo kuunda mpango. Bila shaka, manabii wengi wametoa unabii mwingi, lakini bado haiwezi kusemwa kwamba kazi ya Mungu daima imekuwa ya kupangwa kwa usahihi; nabii zilitolewa kulingana na kazi halisi ya Mungu kwa wakati huo. Kazi Zake zote Anazofanya ni kazi halisi zaidi. Anatekeleza kazi Yake kulingana na maendeleo ya kila enzi, na inazingatia jinsi mambo yanavyobadilika. Kwa Yeye, kutekeleza kazi ni sawa na kutoa dawa kutibu ugonjwa; Akiwa anafanya kazi Yake, Anaangalia na kuendelea na kazi Yake kulingana na kile Alichoona. Katika kila hatua ya kazi Yake, Anaweza kuonyesha hekima Yake nyingi na kuonyesha uwezo Wake mwingi; Anafichua hekima Zake nyingi na mamlaka Yake makubwa kulingana na kazi ya enzi husika, na kumruhusu yeyote kati ya watu waliorudishwa na Yeye wakati wa enzi hizo kuweza kuiona tabia Yake yote. Anaruzuku mahitaji ya watu na kutekeleza kazi Anayopaswa kuifanya kulingana na kazi ambayo ni lazima ifanywe katika kila enzi; Anaruzuku mahitaji ya watu kulingana na kiwango ambacho Shetani amewapotosha. Ilikuwa hivi wakati Yehova alipowaumba Adamu na Hawa mwanzoni ili kuwaruhusu wamdhihirishe Mungu duniani na kutoa ushahidi kwa Mungu miongoni mwa uumbaji, lakini Hawa alitenda dhambi baada ya kujaribiwa na nyoka; Adamu alifanya vivyo hivyo, na kwa pamoja wakiwa kwenye bustani walikula tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Na hivyo basi, Yehova alikuwa na kazi ya ziada ya kutenda miongoni mwao. Aliuona uchi wao, Aliifunika miili yao kwa nguo zilizotengenezwa kwa ngozi za wanyama. Baada ya hayo, Alimwambia Adamu “Kwa sababu umeisikiliza sauti ya mkeo, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, Nikisema, usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako ... hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” Kwa mwanamke Akasema, “Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.” Kuanzia hapo na kuendelea, Aliwafukuza kutoka kwenye Bustani ya Edeni na kuwafanya waishi nje ya bustani, kama vile binadamu wa sasa afanyavyo duniani. Mungu alipomuumba mwanadamu mwanzoni kabisa, Hakupanga kumfanya binadamu ajaribiwe na nyoka baada ya kuumbwa na kisha kuwalaani binadamu na nyoka. Kwa hakika Hakuwa na mpango wa aina hii; ilikuwa tu ni jinsi mambo yalivyoendelea ndiyo yalimpa kazi mpya ya kufanya miongoni mwa uumbaji Wake. Baada ya Yehova kutekeleza kazi Yake miongoni mwa Adamu na Hawa duniani, binadamu waliendelea kukua kwa miaka elfu kadhaa, mpaka “Yehova alipoona ya kwamba uovu wa mwanadamu ulikuwa mkubwa duniani, na kwamba kila wazo analowaza moyoni mwake lilikuwa ovu tu daima. Na Yehova akajuta ya kwamba alikuwa Amemuumba mwanadamu ulimwenguni, na Akawa na huzuni moyoni Mwake. … Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Yehova.” Kwa wakati huu Yehova alikuwa na kazi mpya zaidi ya kufanya, kwasababu wanadamu aliokuwa Amewaumba walikuwa wamezidisha dhambi baada ya kujaribiwa na nyoka. Kwa mujibu wa hali hizi, Yehova aliichagua familia ya Nuhu miongoni mwa watu hawa na kuinusuru, kisha Akatekeleza kazi Yake ya kuuangamiza ulimwengu kwa gharika. Binadamu wameendelea kukua kwa njia hii mpaka siku ya leo, wakiendelea kupotoka kwa kukithiri, na wakati utakapofika ambapo maendeleo ya binadamu yamefikia kilele chake, hio itaashiria mwisho wa binadamu. Kuanzia mwanzo kabisa hadi mwisho wa ulimwengu, ukweli wa ndani wa kazi Yake siku zote umekuwa hivi na daima utakuwa hivi. Hii ni sawa na jinsi ambavyo watu watakavyoainishwa kulingana na aina zao; hii ni mbali na suala la kwamba kila mtu aliamuliwa kabla kuwa wa kundi fulani; badala yake, kila mtu anaainishwa hatua kwa hatua baada tu ya kupitia mchakato wa maendeleo. Mwishowe, yeyote ambaye hawezi kuokolewa kikamilifu atarudishwa kwa mababu zake. Hakuna kati ya kazi za Mungu miongoni mwa binadamu iliyokuwa tayari imetayarishwa wakati wa uumbaji wa ulimwengu; badala yake, ilikuwa ni maendeleo ya mambo yaliyomruhusu Mungu kutekeleza kazi Yake hatua kwa hatua kwa uhalisi zaidi na kwa kivitendo zaidi miongoni mwa binadamu. Hivi ni kama ambavyo Yehova Mungu hakumwumba nyoka ili kumjaribu mwanamke. Haukuwa mpango Wake mahususi, wala halikuwa jambo ambalo Alikuwa ameliamua kimakusudi kabla; mtu anaweza kusema kwamba hili halikutarajiwa. Kwa hivyo, ilikuwa ni kwa sababu hili kwamba Yehova aliwafukuza Adamu na Hawa kutoka kwenye Bustani ya Edeni na kuapa kutowahi kumwumba binadamu tena. Lakini hekima ya Mungu inagunduliwa tu na watu kwenye msingi huu, kama tu ile hoja Niliyoitaja awali: “Ninatumia hekima Yangu kulingana na njama za Shetani.” Haijalishi jinsi ambavyo binadamu walizidi kupotoka au jinsi nyoka alivyowajaribu, Yehova bado ana hekima Yake; kwa hivyo, Amekuwa Akijihusisha katika kazi mpya tangu Alipouumba ulimwengu, na hakuna hatua yoyote ya kazi hii iliyowahi kurudiwa. Shetani ameendelea kutekeleza njama zake; binadamu wamekuwa wakipotoshwa siku zote na Shetani, na Yehova Mungu pia ameendelea kutekeleza kazi Yake ya hekima siku zote. Hajawahi kushindwa, na Hajawahi kusita kufanya kazi Yake kuanzia uumbaji wa ulimwengu mpaka sasa. Baada ya binadamu kupotoshwa na Shetani, Aliendelea siku zote kufanya kazi miongoni mwa watu ili kumshinda adui Yake anayewapotosha binadamu. Vita hivi vinaendelea kuanzia mwanzo hadi mwisho wa ulimwengu. Kwa kufanya kazi hii yote, Hajawaruhusu tu binadamu, ambao wamepotoshwa na Shetani, kupokea wokovu Wake mkuu, lakini pia Amewaruhusu kuiona hekima Yake, uweza na mamlaka, na hatimaye Atawaruhusu binadamu kuiona tabia Yake ya haki—huku Akiwaadhibu waovu na kuwatuza wema. Amepambana na Shetani hadi siku hii ya leo na Hajawahi kushindwa, kwani Yeye ni Mungu mwenye hekima, na hekima Yake hutumika kulingana na njama za Shetani. Kwa hivyo, sio tu kwamba Mungu anafanya kila kitu mbinguni kitii mamlaka Yake; pia Anafanya kila kitu duniani kikae chini ya mahali Pake pa kuwekea miguu, Anawafanya wale waovu wanaowashambulia na kuwanyanyasa binadamu wajipate katika kuadibu Kwake. Matokeo yote ya kazi yanaletwa kutokana na hekima Yake. Alikuwa hajawahi kufichua hekima Yake kabla ya uwepo wa binadamu, kwani Hakuwa na maadui kule mbinguni, duniani, au katika ulimwengu mzima, na hakukuwa na nguvu za giza zilizoshambulia chochote miongoni mwa viumbe. Baada ya malaika mkuu kumsaliti, Aliwaumba binadamu duniani, na ilikuwa ni kwa sababu ya binadamu ndiyo maana Alianza rasmi vita Vyake vya milenia nzima dhidi ya Shetani, malaika mkuu, vita ambavyo vilizidi kushamiri kwa kila hatua iliyopigwa. Uweza na hekima Yake vinapatikana katika kila mojawapo ya hatua hizi. Ni kwa njia hio tu ndipo kila kitu kule mbinguni na duniani kinaweza kushuhudia hekima ya Mungu, uweza Wake, na hasa uhalisi wa Mungu. Bado Anatekeleza kazi Yake kwa njia ile ile ya kivitendo hadi leo; hata zaidi, Anapoendelea kutekeleza kazi Yake anafichua pia uweza Wake na hekima Yake; Anawaruhusu kuona ule ukweli wa ndani katika kila hatua ya kazi, kuona hasa ni vipi ambavyo mnaweza kuelezea uweza wa Mungu, na hata zaidi, ni vipi ambavyo mnaweza kuelezea uhalisi wa Mungu.
Kuhusu Yuda kumsaliti Yesu, watu wengine wanajiuliza: Je, hili halikuamuliwa kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu? Kwa kweli, Roho Mtakatifu alipanga hili kulingana na hali halisi ya wakati huo. Ilitukia tu kwamba kulikuwepo mtu kwa jina la Yuda ambaye siku zote angebadhiri fedha. Hivyo basi alichaguliwa kutekeleza wajibu huu na kuwa mwenye huduma katika njia hii. Huu ni mfano halisi wa kutumia rasilimali za mahali palepale. Yesu hakujua jambo hili mwanzoni; Alijua hili tu baadaye, baada ya Yuda kufichuliwa. Kama mtu mwingine angeweza kutekeleza wajibu huu, basi mtu mwingine angeweza kufanya hivi badala ya Yuda. Kile ambacho kiliamuliwa tangu mwanzo, kilikuwa kwa kweli, kitu ambacho Roho Mtakatifu alikifanya kwa wakati huo. Kazi ya Roho Mtakatifu siku zote inafanywa moja kwa moja; wakati wowote Anapopanga kazi Yake, Roho Mtakatifu ataitekeleza. Kwa nini sikuzote Nasema kwamba kazi ya Roho Mtakatifu ni ya uhalisi? Kwamba siku zote ni mpya na haijawahi kuwa zee, na siku zote inakuwa na uhai zaidi? Kazi Yake ilikuwa bado haijapangwa wakati ulimwengu ulipoumbwa; hivi sivyo kabisa ilivyofanyika! Kila hatua ya kazi hufikia athari yake bora kwa wakati wake mwafaka, na haziingiliani kwa kila moja. Kuna wakati mwingi ambapo mipango iliyopo akilini mwako haiendani kabisa na kazi ya hivi punde ya Roho Mtakatifu. Kazi Yake si rahisi kama watu wanavyofikiria, wala si ngumu kama watu wengi wanavyofikiria; inajumuisha kuwaruzuku watu wakati wowote na mahali popote kulingana na mahitaji yao ya sasa. Hakuna aliye wazi zaidi kuhusu kiini halisi cha watu kama Yeye, na ni kwa sababu hii mahususi ndiposa hakuna kinachoweza kufaa mahitaji halisi ya watu kama vile ambavyo kazi Yake inavyofanya. Hivyo basi, kutoka kwa mtazamo wa mwanadamu, kazi Yake ilipangwa milenia kadhaa kabla. Anapofanya kazi miongoni mwenu sasa, kulingana na hali zenu, pia Anafanya kazi na kuongea wakati wowote na mahali popote. Wakati watu wako katika hali fulani, Yeye huongea maneno hayo ambayo hasa ndiyo wanayohitaji ndani yao. Ni kama hatua ya kwanza ya kazi Yake, nyakati za kuadibu. Baada ya hayo, Mungu aliendesha kazi Yake kwa kuzingatia kile ambacho watu walidhihirisha, uasi wao, hali chanya zilizojitokeza kutoka kwao na hali mbaya, na vile vile na kikomo cha chini kabisa ambacho watu wangeweza kuanguka wakati hali hizo mbaya zilifikia hatua fulani; na Alitumia vitu hivi ili kupata matokeo bora zaidi kutoka katika kazi Yake. Anatekeleza tu kazi Yake ya kuruzuku miongoni mwa watu kulingana na hali zao za sasa. Yeye Hutekeleza kila hatua ya kazi Yake kulingana na hali halisi za watu. Viumbe vyote vilivyoumbwa viko mikononi Mwake; Angekosaje kuvijua? Mungu hutekeleza hatua inayofuata ya kazi ambayo inapaswa kufanywa, wakati wowote na mahali popote, kulingana na hali za watu. Kazi hii haikupangwa maelfu ya miaka kabla; hii ni dhana ya mwanadamu tu! Anafanya kazi huku Akitazama matokeo ya kazi Yake, na kazi Yake inaendelea kuongezeka na kukua; Anapoendelea kuangalia matokeo ya kazi Yake, Anatekeleza hatua inayofuata ya kazi Yake. Anatumia vitu vingi ili kuibadilisha hatua kwa hatua na kufanya kazi Yake mpya ionekane na watu baada ya muda. Kazi ya aina hii inaweza kuruzuku mahitaji ya watu, kwani Mungu anawajua watu vizuri sana. Hivi ndivyo Anavyotekeleza kazi Yake kutoka mbinguni. Vilevile, Mungu mwenye mwili anafanya kazi Yake kwa njia hiyo hiyo, Akifanya mipango na kufanya kazi miongoni mwa wanadamu kulingana na hali halisi. Hakuna kati ya kazi Zake iliyopangwa kabla ya ulimwengu kuumbwa, wala kupangwa kwa umakinifu kabla ya wakati. Miaka elfu mbili baada ya ulimwengu kuumbwa, Yehova aliona binadamu walikuwa wamepotoka sana kiasi cha kwamba Alitumia kinywa cha nabii Isaya kutabiri kwamba baada ya Enzi ya Sheria kukamilika, Angetekeleza kazi Yake ya kuwakomboa wanadamu katika Enzi ya Neema. Huu ulikuwa ni mpango wa Yehova, bila shaka, lakini mpango huu pia ulifanywa kulingana na hali ambazo Aliziona kwa wakati huo; bila shaka Yeye hakuufikiria mara moja baada ya kumuumba Adamu. Isaya alitabiri tu, lakini Yehova hakuwa amefanya matayarisho ya mapema ya kazi hii wakati wa Enzi ya Sheria; badala yake, Alianza kazi hii mwanzoni mwa Enzi ya Neema, wakati mjumbe alipotokea katika ndoto ya Yusufu ili kumwangazia kwa ujumbe kwamba Mungu angekuwa mwili, na ndipo kazi Yake ya kupata mwili ilianza. Mungu hakuwa, kama watu wanavyofikiri, hakutayarisha kazi Yake ya kupata mwili mara tu baada ya kuumba ulimwengu; iliamuliwa tu kulingana na kiwango ambacho ubinadamu ulikuwa umekua na hali ya vita Vyake dhidi ya Shetani.
Mungu anapokuwa mwili, Roho Wake anamshukia binadamu; kwa maneno mengine, Roho wa Mungu anavaa mwili. Anafanya kazi Yake duniani, na badala ya kuleta naye hatua mbalimbali zilizozuiliwa, kazi hii haina mipaka kamwe. Kazi ambayo Roho Mtakatifu hufanya katika mwili bado inaamuliwa na matokeo ya kazi Yake, na Yeye hutumia mambo haya kuamua urefu wa muda ambao Atafanya kazi akiwa katika mwili. Roho Mtakatifu hufichua moja kwa moja kila hatua ya kazi Yake; Yeye huchunguza kazi Yake anapozidi kuendelea; kazi hii si kitu kisicho cha kawaida kiasi cha kuzidi mipaka ya mawazo ya mwanadamu. Hii ni kama kazi ya Yehova katika kuumba mbingu na nchi na vitu vyote; Aliweza kupanga na kufanya kazi wakati huo huo. Alitenga nuru kutoka kwenye giza, na asubuhi pamoja na jioni vyote vikawepo—hii ilichukua siku moja. Siku ya pili Aliumba mbingu, ambayo pia ilichukua siku moja na kisha Akaiumba nchi, bahari na viumbe vilivyojaa ndani yale, pia ilichukua siku nyingine moja. Hili liliendelea hivyo hadi siku ya sita, wakati Mungu alipomuumba binadamu na kumwacha asimamie viumbe hivi vyote juu ya nchi, mpaka siku ya saba, Alipokuwa amemaliza kuumba viumbe vyote, na Akapumzika. Mungu aliibariki siku ya saba na kuitenga kuwa siku takatifu. Aliamua tu kuanzisha siku hii takatifu baada ya kuviumba viumbe vyote, na wala si kabla ya kuviumba. Kazi hii pia ilitekelezwa moja kwa moja; kabla ya kuviumba viumbe vyote, Hakuamua kuumba ulimwengu kwa siku sita na kupumzika siku ya saba; ukweli hauko hivi hata kidogo. Hakusema hili, wala Hakupanga hili. Kwa vyovyote vile Hakusema kwamba uumbaji wa viumbe vyote ungekamilishwa katika siku ya sita na kwamba Angepumzika katika siku ya saba; badala yake, Aliumba kulingana na kile kilichokuwa kikionekana kizuri Kwake. Mara tu Alipomaliza kuumba kila kitu, tayari ilikuwa ni siku ya sita. Kama ingekuwa ni siku ya tano Alipomaliza kuumba kila kitu, Angepangilia basi siku ya sita kuwa siku takatifu; hata hivyo, Alimaliza kuumba kila kitu katika siku ya sita, na hivyo basi siku ya saba ikawa siku takatifu, ambayo imepitishwa hadi siku ya leo. Hivyo basi, kazi Yake ya sasa inatekelezwa kwa njia hii hii. Anazungumza na kuwaruzuku kulingana na hali zenu. Yaani, Roho huzungumza na kufanya kazi kulingana na hali za watu; Roho huangalia kila kitu na kufanya kazi wakati wowote na mahali popote. Kile Ninachofanya, Ninachosema, Ninachoweka juu yenu, na kuwapa, bila kuacha ni kile mnachohitaji. Kwa hivyo, hakuna kazi Yangu yoyote iliyo tofauti na uhalisi; zote ni halisi, kwani ninyi nyote mnajua ya kwamba “Roho wa Mungu hutazama vitu vyote.” Ikiwa haya yote yangekuwa yameamuliwa kabla ya wakati, je, huoni kwamba mambo yangekuwa yamekwisha kuamuliwa? Unafikiri kwamba Mungu alipanga mipango kwa ajili ya milenia sita nzima na kisha Akaamua kabla binadamu wawe waasi, wapinzani, waongo na wadanganyifu, na wawe na upotovu wa mwili, tabia za kishetani, tamaa za macho, na kujihusisha kwao na mambo yasiyofaa. Haya yote hayakupangwa na Mungu, lakini yalitokana na upotoshaji wa Shetani. Wengine wanaweza kusema, “Je, Shetani pia hakuwa katika mkono wa Mungu? Mungu alikuwa amepanga awali kwamba Shetani angewapotosha binadamu kwa njia hii, na baada ya hapo Angetekeleza kazi Yake miongoni mwa binadamu.” Je, kweli Mungu angepanga awali Shetani awapotoshe binadamu? Mungu ana shauku kubwa tu ya kuwaruhusu binadamu waishi maisha ya kawaida, Angewezaje kweli kuvuruga maisha ya binadamu? Kama ingekuwa hivyo, je, kumshinda Shetani na kuwaokoa binadamu si kungekuwa jitihada za bure? Je, uasi wa binadamu ungewezaje kuamuliwa kabla? Ilikuwa ni kwasababu ya usumbufu wa Shetani kiuhalisia; kwa hivyo ingewezaje kupangwa awali na Mungu? Shetani aliye katika mkono wa Mungu ambaye mnamwelewa ni tofauti sana na Shetani aliye katika mkono wa Mungu ambaye Ninamzungumzia. Kulingana na kauli zenu kwamba “Mungu ni muweza wa yote, na Shetani yupo mikononi Mwake,” hivyo Shetani hangeweza kamwe kumsaliti Yeye. Je, hamkusema kwamba Mungu ni muweza? Maarifa yenu ni ya kidhahania mno na hayaambatani na uhalisi; mwanadamu kamwe hawezi kuelewa fikira za Mungu, wala mwanadamu hawezi kamwe kuelewa hekima za Mungu! Mungu ni muweza; huu si uwongo kamwe. Malaika mkuu alimsaliti Mungu kwa sababu Mungu alimpa sehemu ya mamlaka awali. Bila shaka, tukio hili halikutarajiwa, kama vile Hawa kushindwa na jaribio la nyoka. Hata hivyo, bila kujali jinsi ambavyo Shetani anatekeleza usaliti wake, bado hana uwezo kama Mungu. Kama vile mlivyosema, Shetani ana nguvu tu; haijalishi kile anachofanya, mamlaka ya Mungu daima yatamshinda. Hii ndiyo maana ya kweli ya usemi huu, “Mungu ni muweza, na Shetani yupo mikononi Mwake.” Kwa hivyo, vita Vyake na Shetani lazima vitekelezwe hatua moja baada ya nyingine; aidha, Yeye hupanga kazi Yake kulingana na ujanja wa Shetani. Hivi ni kusema, kulingana na enzi, Anawaokoa watu na kufichua hekima na uweza Wake. Vilevile, kazi ya siku za mwisho haikuamuliwa mapema, kabla ya Enzi ya Neema; kuamuliwa kabla hakufanywi kwa njia ya kawaida kama hii: kwanza, kwa kuifanya tabia ya nje ya binadamu ibadilike; pili, kumweka mwanadamu katika kuadibu na majaribio Yake; tatu, kumfanya mwanadamu apitie jaribio la kifo; nne, kumfanya binadamu apitie nyakati za kumpenda Mungu na aonyeshe azimio la kiumbe kilichoumbwa; tano, kumruhusu binadamu aweze kuona mapenzi ya Mungu na kumjua Yeye kikamilifu; na hatimaye, kumkamilisha binadamu. Hakupanga mambo haya yote wakati wa Enzi ya Neema; badala yake, Alianza kuyapanga katika enzi ya sasa. Shetani yuko kazini, kama vile Mungu alivyo. Shetani anaonyesha tabia yake potovu, huku pia Mungu anazungumza moja kwa moja na kufichua baadhi ya mambo muhimu. Hii ndiyo kazi inayofanywa leo, na kanuni hii hii ya kufanya kazi ilitumika zamani, baada ya ulimwengu kuumbwa.
Kwanza Mungu aliwaumba Adamu na Hawa, na pia Alimwumba nyoka. Miongoni mwa vitu vyote, nyoka ndiye aliyekuwa mwenye sumu nyingi sana; mwili wake ulikuwa na sumu, na Shetani aliitumia sumu hii ili kufaidika nayo. Ni nyoka aliyemjaribu Hawa hadi akatenda dhambi. Adamu alitenda dhambi baada ya Hawa kutenda, na wawili hao waliweza kutofautisha kati ya mema na maovu. Kama Yehova angejua kwamba nyoka angemjaribu Hawa, na kwamba Hawa angemjaribu Adamu, kwa nini Akawaweka wote pale ndani ya bustani? Kama Aliweza kutabiri mambo haya kwa nini Akamwumba nyoka na kumweka ndani ya Bustani ya Edeni? Kwa nini Bustani ya Edeni ilikuwa na tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya? Je, Alikusudia wale lile tunda? Yehova alipokuja, si Adamu wala Hawa aliyethubutu kumkabili Yeye, na ilikuwa ni wakati huu tu ambapo Yehova alijua kwamba walikuwa wamekula tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya na kushikwa katika ujanja wa yule nyoka. Hatimaye Alimlaani nyoka, na Akamlaani Adamu na Hawa pia. Wakati wawili hao walipokula tunda la mti ule, Yehova hakujua kabisa kwamba walikuwa wakifanya hivyo. Binadamu walipotoka hadi kufikia kiwango cha kuwa na uovu na uasherati wa kimapenzi, hadi kufikia hatua ambayo mambo yote waliyokuwa nayo katika mioyo yao yalikuwa maovu na yasiyo ya haki; yote yalikuwa machafu. Kwa hivyo, Yehova alijutia kuwaumba wanadamu. Baada ya hayo, Alifanya kazi Yake ya kuuangamiza ulimwengu kwa gharika, ambayo Nuhu na watoto wake wa kiume walinusurika. Baadhi ya mambo kwa hakika si ya juu na ya kumiujiza kama vile watu wanavyoweza kufikiria. Baadhi wanauliza: “Kwa sababu Mungu alijua malaika mkuu angemsaliti Yeye, kwa nini Alimwumba?” Huu ndio ukweli: Wakati dunia haikuwepo bado, malaika mkuu ndiye aliyekuwa malaika mkuu zaidi mbinguni. Alikuwa na mamlaka juu ya malaika wote kule mbinguni; haya ndiyo yaliyokuwa mamlaka ambayo Mungu alimpa. Kando na Mungu, yeye ndiye aliyekuwa malaika mkuu zaidi mbinguni. Wakati Mungu alipomuumba binadamu baadaye, malaika mkuu alitekeleza usaliti mkuu zaidi dhidi ya Mungu duniani. Nasema kwamba alimsaliti Mungu kwa sababu alitaka kuwasimamia binadamu na kuzidi mamlaka ya Mungu. Ni malaika mkuu ambaye alimjaribu Hawa hadi akatenda dhambi; alifanya hivyo kwa sababu alipenda kuanzisha ufalme wake duniani na kuwafanya binadamu wamsaliti Mungu na kumtii yeye badala Yake. Aliona kwamba kulikuwa na vitu vingi ambavyo vilimtii; malaika walimtii, sawa na vile ambavyo watu wa duniani walivyomtii. Ndege na wanyama, miti, misitu, milima, mito na vitu vyote vilivyomo duniani vilikuwa chini ya utunzaji wa binadamu—yaani, Adamu na Hawa—huku nao Adamu na Hawa wakimtii malaika mkuu. Malaika mkuu kwa hivyo alitamani kuzidi mamlaka ya Mungu na kumsaliti Mungu. Baadaye aliwaongoza malaika wengi kumsaliti Mungu, ambao baadaye walikuja kuwa pepo wachafu mbalimbali. Je, maendeleo ya binadamu hadi siku ya leo hayajasababishwa na upotovu wa malaika mkuu? Binadamu wako tu namna walivyo leo kwa sababu malaika mkuu alimsaliti Mungu na kuwapotosha binadamu. Kazi hii ya hatua kwa hatua haiko karibu kuwa ya kidhahania na rahisi kama vile watu wanavyofikiria hata kidogo. Shetani alitekeleza usaliti wake kwa sababu fulani, ilhali watu hawawezi kufahamu kitu kirahisi kama hicho. Ni kwa nini Mungu aliziumba mbingu na nchi na vitu vyote, na pia Akamuumba Shetani? Kwa kuwa Mungu anamdharau Shetani sana, na Shetani ni adui Yake, kwa nini akamuumba Shetani? Kwa kumuumba Shetani, je, hakuwa Anamuumba adui? Mungu kwa hakika Hakuumba adui; badala yake, Alimuumba malaika, na baadaye malaika akamsaliti Yeye. Hadhi yake ilikuwa kubwa mno kiasi cha kwamba alitaka kumsaliti Mungu. Mtu anaweza kusema kwamba hii ilikuwa ni bahati mbaya, lakini pia lilikuwa ni jambo lisiloepukika. Ni sawa na vile ambavyo mtu bila kuepuka atakufa akiwa na umri fulani; mambo yameendelea tayari hadi kwa hatua fulani. Kunao hata wapumbavu wengine wanaosema: “Kwa sababu Shetani ni adui Yako, kwa nini Ulimuumba? Je, Hukujua kuwa malaika mkuu angekusaliti? Je, Huwezi kutazama kutoka milele hadi milele? Je, Hukuijua asili ya malaika mkuu? Kwa kuwa Ulijua wazi kuwa angekusaliti Wewe, basi kwa nini Ukamfanya kuwa malaika mkuu? Sio tu kwamba alikusaliti, bali pia aliongoza malaika wengine wengi pamoja naye na wakashuka kwa ulimwengu wa wanadamu kuwapotosha binadamu, lakini hadi leo, bado Umeshindwa kukamilisha mpango Wako wa usimamizi wa miaka elfu sita.” Je, maneno haya ni sahihi? Unapofikiria kwa njia hii, hujiweki katika matatizo mengi zaidi kuliko yanayohitajika? Wengine bado husema: “Kama Shetani asingewapotosha binadamu hadi siku ya leo, Mungu asingewaokoa binadamu kwa njia hii. Katika mfano huu, hekima na uweza wa Mungu vyote vingekuwa havionekani; hekima Yake ingejionyesha wapi? Kwa hivyo, Mungu aliiumba jamii ya binadamu kwa ajili ya Shetani; ili kwamba baadaye Mungu aweze kufichua uweza Wake—vinginevyo, binadamu angewezaje kugundua hekima ya Mungu? Kama binadamu asingempinga Yeye na kumwasi Yeye, isingehitajika kwa vitendo Vyake kujionyesha. Kama viumbe wote wangemwabudu Yeye na kumtii Yeye, Asingekuwa na kazi ya kufanya.” Hili lipo mbali zaidi na uhalisi wa mambo, kwani hakuna chochote kichafu kuhusu Mungu, na hivyo basi Hawezi kuumba uchafu. Yeye hufichua vitendo Vyake sasa ili kuweza tu kuwashinda kabisa adui Zake, ili kuwaokoa binadamu, ambao Aliwaumba, ili kuyashinda mapepo na Shetani, ambao wanamchukia, wanamsaliti na wanampinga, ambao walikuwa chini ya utawala Wake na walikuwa Wake mwanzoni kabisa; Anataka kuwashinda hawa mapepo, na katika kufanya hivyo Anafichua uweza Wake kwa vitu vyote. Binadamu na vitu vyote vilivyomo duniani kwa sasa vipo chini ya utawala wa Shetani na chini ya utawala wa waovu. Mungu anataka kufichua matendo Yake kwa vitu vyote ili watu waweze kumjua Yeye, na hivyo kuishia kumshinda Shetani na kuwaangamiza kabisa maadui Zake. Kazi hii yote inakamilishwa kupitia kufichua matendo Yake. Viumbe Vyake vyote vinamilikiwa na Shetani, kwa hivyo Angependa kuufichua uweza Wake kwa viumbe hivyo, na hivyo kumshinda Shetani. Kama Shetani asingekuwepo, Asingehitaji kuyafichua matendo Yake. Kama usingekuwa usumbufu wa Shetani, Angewaumba binadamu na kuwaongoza waishi katika Bustani ya Edeni. Kwa nini Hakuwahi kufichua matendo Yake yote kwa malaika au malaika mkuu kabla ya kusalitiwa na Shetani? Kama malaika na malaika mkuu wangalimjua Yeye, na pia kumtii Yeye pale mwanzoni, basi Asingetekeleza vile vitendo vya kazi visivyo na maana. Kwa sababu ya uwepo wa Shetani na mapepo, watu wanampinga Yeye na wanajazwa tabia ya uasi kwa kiwango cha juu, na hivyo Mungu anataka kufichua matendo Yake. Kwa sababu Anataka kupigana vita na Shetani, ni lazima Atumie mamlaka Yake kumshinda Shetani na kutumia matendo Yake yote kumshinda Shetani; kwa njia hii, kazi Yake ya wokovu Anayotekeleza miongoni mwa binadamu itawafanya watu waone hekima na uweza Wake. Kazi anayofanya Mungu leo ni yenye maana na haifanani hata kidogo na vile ambavyo watu wengine hurejelea wanaposema: “Je, kazi hii Unayofanya haipingani? Je, Hujisumbui tu na huu mfululizo wa kazi? Ulimuumba Shetani, kisha Ukamruhusu akusaliti na kukupinga Wewe. Uliwaumba binadamu, na kisha ukawakabidhi kwa Shetani, na Ukaruhusu Adamu na Hawa wajaribiwe. Kwa sababu uliyafanya mambo haya yote kwa kukusudia, kwa nini Unawachukia binadamu? Kwa nini Unamchukia Shetani? Mambo haya si ya kujitengenezea Mwenyewe? Kuna nini cha Wewe kuchukia?” Watu wengi wapumbavu watasema hayo. Wanatamani kumpenda Mungu, lakini mioyoni mwao wanalalamika kumhusu Mungu—ni mkanganyiko ulioje! Wewe huelewi ukweli, unazo fikira nyingi sana za kimiujiza, na pia unadai kwamba hili ni kosa la Mungu—wewe ni mpumbavu kweli! Ni wewe unayepindisha ukweli; si kosa la Mungu! Baadhi ya watu hata watalalamika tena na tena: “Ni wewe uliyemuumba Shetani, na ni Wewe uliyemrusha Shetani hadi katika ulimwengu wa binadamu na Ukawakabidhi binadamu kwake. Binadamu wana tabia ya kishetani; badala ya kuwasamehe, Unawachukia sana kwa kiwango fulani. Mwanzoni Uliwapenda binadamu kwa kiwango fulani, na sasa Unawachukia sana binadamu. Ni Wewe unayewachukia sana binadamu, lakini ni Wewe pia ambaye Unawapenda binadamu. Ni nini hasa kinaendelea hapa? Je, huu si ukinzani?” Bila kujali ni vipi mnavyoangalia suala hili, hili ndilo lililofanyika mbinguni; malaika mkuu alimsaliti Mungu kwa njia hii, nao binadamu wakapotoshwa kwa njia hii, na wakaendelea mpaka leo kwa njia hii. Bila kujali ni vipi mnavyolisema, hii ndiyo hadithi yote. Hata hivyo, lazima muelewe kwamba Mungu anaifanya kazi ya leo ili kuwaokoa nyinyi, na ili kumshinda Shetani.
Kwa sababu malaika hasa walikuwa wanyonge na hawakuwa na uwezo wowote, walipata kiburi walipopewa mamlaka, hasa malaika mkuu, ambaye hadhi yake ilikuwa ya juu zaidi kuliko ile ya malaika mwingine yeyote. Malaika mkuu alikuwa ndiye mfalme wa malaika wote. Aliwaongoza mamilioni ya malaika, na chini ya Yehova mamlaka yake yalizidi yale ya malaika wengine. Alitaka kufanya hivi na vile, na kuwaongoza malaika hadi kwenye ulimwengu wa binadamu ili kuutawala ulimwengu. Mungu alisema kwamba Yeye Anautawala ulimwengu; malaika mkuu akasema kwamba ulimwengu ulikuwa wake wa kuutawala, na kuanzia hapo akamsaliti Mungu. Mbinguni, Mungu alikuwa ameuumba ulimwengu mwingine. Malaika mkuu akataka kuutawala ulimwengu huu na pia kushuka chini kwenye ulimwengu wa binadamu. Je, Mungu angemruhusu kufanya hivi? Kwa hivyo, Alimpiga malaika mkuu na kumtimua chini hadi katikati ya anga. Tangu alipowapotosha binadamu, Mungu amefanya vita dhidi yake ili kuwaokoa binadamu; Ametumia milenia hizi sita kumshinda. Dhana yenu ya Mungu mwenye uweza haipatani na kazi ambayo Mungu anaifanya kwa sasa; haina uhalisi kabisa, na ni uongo hata zaidi! Kwa kweli, Mungu alitangaza kuwa malaika mkuu ni adui Yake, baada tu ya malaika mkuu kumsaliti Yeye. Ilikuwa ni kwa sababu tu ya usaliti wake ndipo alipowakandamiza binadamu baada ya kuwasili katika ulimwengu wa binadamu, na ilikuwa ni kwa sababu hii ndiyo maana binadamu waliendelea hivyo hadi kwa hatua hii. Kufuatia haya, Mungu alikula kiapo na Shetani: “Nitakushinda wewe na kuwaokoa binadamu, viumbe Wangu.” Shetani hakushawishika wakati wa mwanzo na akasema, “Ni nini kwa hakika unachoweza kunifanyia mimi? Wewe kweli unaweza kuniangusha hadi katikati ya anga? Wewe unaweza kwa kweli kunishinda mimi?” Baada ya Mungu kumwangusha hadi katikati ya anga, Hakumtilia maanani tena na kisha Alianza kuwaokoa binadamu na kufanya kazi Yake mwenyewe, licha ya usumbufu ulioendelea kutoka kwa Shetani. Kila kitu ambacho Shetani angeweza kufanya kilitokana na nguvu alizopewa na Mungu; alichukua vitu hivi pamoja naye hadi katikati ya anga na amevihifadhi hadi leo. Alipomwangusha malaika mkuu hadi katikati ya anga, Mungu alimwangusha hadi kwenye anga lakini hakuchukua mamlaka yake, na hivyo basi aliendelea kuwapotosha binadamu. Mungu, kwa upande mwingine, Alianza kuwaokoa binadamu, ambao Shetani alikuwa amewapotosha baada ya kuumbwa kwao. Mungu hakufichua matendo Yake wakati akiwa mbinguni; hata hivyo, kabla ya kuiumba dunia, Aliwaruhusu watu katika ulimwengu Aliouumba mbinguni kuona vitendo Vyake na hivyo kuwaongoza watu juu mbinguni. Aliwapa hekima na akili, na kuwaongoza watu hao kuishi katika ulimwengu huo. Kwa kawaida, hakuna kati yenu ambaye amewahi kusikia haya awali. Baadaye, baada ya Mungu kuwaumba binadamu, malaika mkuu alianza kuwapotosha binadamu; duniani, binadamu wote walikuwa katika machafuko. Ilikuwa ni wakati huu tu ambapo Alianza vita Vyake dhidi ya Shetani, na ilikuwa ni wakati huu tu ambapo watu waliona matendo Yake. Hapo mwanzo matendo Yake yalifichwa kutoka kwa binadamu. Baada ya Shetani kuangushwa hadi katikati ya anga, alijishughulisha na masuala yake, naye Mungu akajishughulisha Mwenyewe na kazi Yake binafsi, siku zote Akifanya vita dhidi ya Shetani, kila wakati mpaka siku za mwisho. Sasa ndio wakati ambapo Shetani anafaa kuangamizwa. Mwanzoni Mungu alimpa mamlaka, na baadaye Alimtimua hadi katikati ya anga, lakini Shetani alibaki mwasi. Baada ya hapo, aliwapotosha binadamu, lakini Mungu kwa hakika alikuwa ulimwenguni Akiwasimamia binadamu. Mungu hutumia usimamizi Wake wa watu kumshinda Shetani. Kwa kuwapotosha watu, Shetani hutamatisha majaaliwa ya watu na kuvuruga kazi ya Mungu. Kwa upande mwingine, kazi ya Mungu ndiyo wokovu wa binadamu. Ni hatua gani ya kazi ya Mungu mwenyewe ambayo hainuii kuwaokoa binadamu? Ni hatua gani hainuii kuwatakasa watu, kuwafanya watende haki na kuwafanya waishi kwa njia ambayo inaunda taswira inayoweza kupendwa? Shetani, hata hivyo, hafanyi hivi. Yeye huwapotosha binadamu; siku zote anatekeleza kazi zake za kuwapotosha binadamu kote ulimwenguni. Bila shaka, Mungu pia hufanya kazi Yake mwenyewe. Hamtilii maanani Shetani. Haijalishi ni kiasi kipi cha mamlaka ambayo Shetani anayo, mamlaka yake bado yalitoka kwa Mungu; Mungu kwa hakika hakumpa mamlaka Yake yote, na hivyo basi haijalishi ni nini anachofanya, hawezi kumzidi Mungu na siku zote yuko mikononi mwa Mungu. Mungu hakufichua vitendo Vyake vyovyote akiwa mbinguni. Alimpa Shetani kiwango kidogo tu cha mamlaka ili kumruhusu kutekeleza udhibiti wake dhidi ya malaika. Hivyo basi, haijalishi kile anachofanya, hawezi kuzidi mamlaka ya Mungu kwa sababu mamlaka ambayo Mungu alimpa awali ni finyu. Huku Mungu akifanya kazi, Shetani anavuruga. Katika siku za mwisho, usumbufu wake utakomeshwa; vilevile, kazi ya Mungu itakamilika, na aina ya mtu ambaye Mungu angependa kumkamilisha atakuwa amekamilika. Mungu huwaongoza watu kwa njia nzuri; maisha Yake ni maji ya uzima, yasiyopimika na yasiyo na mipaka. Shetani amempotosha binadamu hadi kiwango fulani; hatimaye, yale maji hai ya uzima yatamkamilisha binadamu, na haitawezekana kwa Shetani kuingilia kati na kutekeleza kazi yake. Kwa hivyo, Mungu ataweza kuwapata kabisa watu wake. Shetani angali anakataa kukubali haya sasa; siku zote anapambana na Mungu, lakini Mungu hamtilii maanani. Mungu amesema, “Nitakuwa mshindi juu ya nguvu zote za giza za Shetani na dhidi ya ushawishi wote wa giza.” Hii ndiyo kazi inayopaswa kufanywa katika mwili, na pia ndiyo inayofanya umuhimu wa kupata mwili: yaani kukamilisha hatua ya kazi ya kumshinda Shetani katika siku za mwisho, kuondoa vitu vyote vinavyomilikiwa na Shetani. Ushindi wa Mungu dhidi ya Shetani hauepukiki! Shetani kwa hakika alishindwa kitambo sana. Wakati injili ilipoanza kuenezwa nchi yote ya joka kuu jekundu, yaani, wakati Mungu mwenye mwili alipoanza kufanya kazi Yake na kazi hii ikafanywa kuendelea, Shetani aliweza kushindwa kabisa, kwani kusudi hasa la kupata mwili lilikuwa ni kumshinda Shetani. Mara tu Shetani alipoona kuwa Mungu amepata mwili kwa mara nyingine tena na kuanza kutekeleza kazi Yake, ambayo hakuna nguvu ingeweza kuizuia, kwa hiyo alipigwa na butwaa kuona kazi hii, na hakuthubutu kufanya uharibifu mwingine wowote. Hapo kabla Shetani alifikiria kwamba yeye pia alimiliki hekima nyingi, na alivuruga na kusumbua kazi ya Mungu; hata hivyo, hakutarajia kwamba Mungu angefanyika mwili kwa mara nyingine tena, au kwamba katika kazi Yake, Mungu angetumia uasi wa Shetani kuhudumu kama ufunuo na hukumu kwa binadamu; na hivyo basi kumshinda binadamu na kumshinda Shetani. Mungu ni mwenye hekima kuliko Shetani, na kazi Yake inamzidi Shetani kwa mbali. Hivyo basi, Niliwahi kusema hapo awali kwamba: “Kazi Ninayoifanya inatekelezwa kutokana na ujanja wa Shetani. Mwishowe Nitafichua uweza Wangu na hali ya kutoweza kwa Shetani.” Mungu anapofanya kazi Yake, Shetani anamfuatia kwa nyuma mpaka mwishowe ataangamizwa—hatajua hata kilichomgonga! Ataweza kutambua tu ukweli baada ya kuvunjwa na kupondwapondwa; na wakati huo atakuwa tayari amechomwa kwenye ziwa la moto. Je, hatakuwa ameshawishika kabisa kwa wakati huo? Kwa sababu hatakuwa na njama zozote zingine za kutumia!
Ni kazi halisi ya hatua kwa hatua ambayo mara nyingi inaulemea moyo wa Mungu kwa huzuni juu ya binadamu, kiasi cha kwamba vita Vyake na Shetani vimedumu kwa miaka 6,000. Kwa hivyo Mungu alisema kwamba: “Sitawahi tena kuwaumba binadamu, wala kuwahi tena kuwapa malaika mamlaka.” Kuanzia hapo, wakati malaika walipokuja kufanya kazi duniani, walimfuata tu Mungu ili kufanya kazi fulani. Hakuwahi kuwapa malaika mamlaka. Je, malaika ambao Waisraeli waliwaona walitekeleza vipi kazi yao? Walijifichua katika ndoto na kupitisha maneno ya Yehova. Wakati Yesu alipofufuka siku ya tatu baada ya kusulubishwa, ni malaika ndio waliolisukuma jiwe kando; Roho wa Mungu hakufanya kazi hii yeye binafsi. Malaika waliweza kufanya tu kazi ya aina hii; walifanya tu wajibu wa usaidizi na hawakuwa na mamlaka, kwani Mungu hangewahi tena kuwapatia mamlaka. Baada ya kufanya kazi kwa muda fulani, watu ambao Mungu aliwatumia hapa duniani walichukua nafasi ya Mungu na kusema, “Nataka kuuzidi ulimwengu! Nataka kusimama kwenye mbingu ya tatu! Tunataka utawala wa mamlaka makuu!” Wangekuwa na kiburi baada ya siku kadhaa za kazi; walitaka mamlaka makuu duniani, walitaka kuanzisha taifa jingine, walitaka vitu vyote viwe katika utawala wao na walitaka kusimama katika mbingu ya tatu. Je, kwani hujui kwamba wewe ni binadamu tu unayetumiwa na Mungu? Unawezaje kupaa hadi kwenye mbingu ya tatu? Mungu anakuja duniani kufanya kazi, kimyakimya na bila kujitangaza, na Anaondoka baada ya kukamilisha kazi Yake kimyakimya. Hajitangazi kama vile binadamu wanavyofanya, lakini badala yake Anatekeleza kazi Yake kwa vitendo. Wala haingii kanisani na kujitangaza, “Nitawaangamiza nyinyi nyote! Nitawalaani na kuwaadibu!” Anatekeleza tu kazi Yake binafsi, na kuondoka mara Anapomaliza. Wale wachungaji wa kidini wanaowaponya wagonjwa na kupunga mapepo, wanawafundisha wengine madhabahuni, na kutoa hotuba ndefu na zenye makuu, na kuzungumzia masuala yasiyo halisi, wana kiburi cha ndani! Wao ni vizazi vya malaika mkuu!
Baada ya kufanya kazi Yake ya miaka 6,000 hadi leo, Mungu tayari amefichua matendo Yake mengi, sababu ya msingi ikiwa ni kumshinda Shetani na kuleta wokovu kwa binadamu wote. Anatumia fursa hii kuruhusu kila kitu mbinguni, kila kitu kilicho duniani, kila kitu kinachopatikana baharini, pamoja na kila kitu cha mwisho ambacho Mungu alikiumba ulimwenguni kiweze kuona uweza wa Mungu na kushuhudia matendo yote ya Mungu. Anachukua fursa ya kumshinda Shetani ili kufichua matendo Yake kwa binadamu na kuwaruhusu watu waweze kumsifu Yeye na kuitukuza hekima Yake kwa kumshinda Shetani. Vitu vyote vilivyomo duniani, mbinguni na ndani ya bahari vinamletea utukufu, vinasifu uweza Wake, vinasifu matendo Yake yote na kutamka kwa sauti jina Lake takatifu. Huu ni uthibitisho wa ushindi Wake dhidi ya Shetani; huu ni uthibitisho wa Yeye kumshinda Shetani; na la muhimu zaidi, ni uthibitisho wa wokovu Wake kwa binadamu. Viumbe vyote vya Mungu vinamletea utukufu, vinamsifu Yeye kwa kumshinda adui Yake na kurudi kwa ushindi, na vinamsifu Yeye kama Mfalme mkuu Aliyeshinda. Dhumuni Lake si kumshinda Shetani tu, na ndio maana kazi Yake imeendelea kwa miaka 6,000. Anatumia kushindwa kwa Shetani kuwaokoa binadamu; Anakutumia kushindwa kwa Shetani kufichua vitendo Vyake vyote na kufichua utukufu Wake wote. Atapata utukufu, na umati wote wa malaika utaweza kushuhudia utukufu Wake wote. Wajumbe walio mbinguni, wanadamu walio duniani na viumbe wote walio duniani watauona utukufu wa Muumba. Hii ndiyo kazi Aifanyayo. Viumbe vyake kule mbinguni na duniani vyote vitauona utukufu Wake, na Atarudi kwa ushindi baada ya kumshinda Shetani kabisa na kuwaruhusu binadamu wamsifu Yeye, kwa hivyo Atapata ushindi maradufu katika kazi Yake. Hatimaye binadamu wote watashindwa na Yeye, na Atamwondoa yeyote yule anayepinga au kuasi, hivi ni kusema, Atawaondoa wale wote wanaomilikiwa na Shetani. Kwa sasa unashuhudia matendo mengi sana ya Mungu, ilhali bado unapinga na unakuwa mwasi na hutaki kunyenyekea; unayahifadhi mambo mengi ndani yako na unafanya utakacho; unafuata tamaa zako, na kile upendacho—huu ni uasi; huu ni upingaji. Imani katika Mungu ambayo inatekelezwa kwa ajili ya mwili, kwa ajili ya tamaa za mtu, na kwa ajili ya kile anachopenda mtu, kwa ajili ya ulimwengu, na kwa ajili ya Shetani ni chafu; ni upinzani na uasi. Kuna aina zote tofauti za imani kwa sasa: Baadhi hutafuta hifadhi dhidi ya janga, na wengine hutafuta kupokea baraka, huku baadhi wakitamani kuelewa mafumbo na bado wengine wanajaribu kupata pesa. Hizi zote ni aina za upinzani; hizi zote ni kufuru! Kwa kusema kwamba mtu anapinga au anaasi—je, hiyo hairejelei mambo haya? Watu wengi kwa sasa wanalalamika, wanatoa manung’uniko au kutoa hukumu. Haya yote ni mambo yanayofanywa na waovu; wao ni binadamu wapinzani na waasi; watu kama hao wamemilikiwa na kujawa na Shetani. Watu ambao Mungu anawapata ni wale wanaonyenyekea Kwake kabisa, ni wale ambao wamepotoshwa na Shetani lakini wameokolewa na kushindwa na kazi Yake ya sasa, ni wale ambao wamevumilia dhiki, na ambao hatimaye wamepatwa kabisa na Mungu, hawaishi tena chini ya nguvu za Shetani, wamejiweka huru kutokana na udhalimu, na ni wale ambao wako tayari kuishi kwa kudhihirisha utakatifu—hawa ndio watu watakatifu zaidi; hawa ndio wale watakatifu. Kama matendo yako ya sasa hayalingani na sehemu moja ya mahitaji ya Mungu utaondolewa. Hili halipingiki. Kila kitu kinafanywa kulingana na leo; ingawa Amekuamulia awali na kukuchagua wewe, matendo yako ya sasa bado yataamua matokeo yako. Kama huwezi kwenda sambamba kwa sasa, utaondolewa. Kama huwezi kwenda sambamba kwa sasa, utawezaje kwenda sambamba baadaye? Kwa kuwa sasa muujiza mkubwa kama huo umefanyika kwako, lakini bado huamini. Basi, utamwamini vipi baadaye wakati Atakapomaliza kazi Yake na Hafanyi tena kazi kama hiyo? Kufikia wakati huo, itakuwa ni vigumu zaidi kwako kumfuata! Baadaye, Mungu atategemea mtazamo wako, maarifa yako kwa kazi ya Mungu mwenye mwili, na uzoefu wako ili kubainisha kama wewe ni mwenye dhambi au mwenye haki, au kubainisha kama wewe ndiwe uliyekamilishwa ama ni yule aliyeondolewa. Lazima uweze kuona uwazi sasa. Roho Mtakatifu anafanya kazi hivyo: Anaamua matokeo yako kulingana na tabia yako ya leo. Ni nani anayezungumza maneno ya leo? Ni nani anayefanya kazi ya leo? Ni nani anayeamua kama utaondolewa leo? Ni nani anayeamua kukufanya kuwa mkamilifu? Je, hiki sicho Ninachofanya Mimi mwenyewe? Mimi ndimi Ninayeongea maneno haya; Mimi ndimi Ninayetekeleza kazi hii. Kulaani, kuadibu na kuhukumu watu vyote ni sehemu ya kazi Yangu binafsi. Hatimaye, kukuondoa kutakuwa pia kazi Yangu binafsi. Zote ni kazi Zangu mwenyewe! Kukufanya uwe mkamilifu ni kazi Yangu mwenyewe, na kukuruhusu ufurahie baraka ni kazi Yangu mwenyewe pia. Hizi zote ni kazi Zangu mwenyewe. Matokeo yako hayakuamuliwa awali na Yehova; yanaamuliwa leo na Mungu wa leo. Yanaamuliwa sasa; hayakuamuliwa kabla ya ulimwengu kuumbwa. Baadhi ya watu wapumbavu husema, “Pengine kuna kitu hakipo sawa machoni Pako, na Haunitazami mimi jinsi Unavyopaswa kunitazama. Mwishowe, Utaona vile ambavyo Roho atadhihirisha kila kitu!” Yesu awali Alimchagua Yuda kama mwanafunzi Wake. Watu huuliza: “Angewezaje kumchagua mwanafunzi ambaye angemsaliti?” Mwanzo Yuda hakuwa na nia ya kumsaliti Yesu. Hili jambo lilifanyika tu baadaye. Wakati huo Yesu alikuwa amemchukua Yuda kwa upendo; Alimfanya mtu huyo amfuate Yeye na kumfanya awajibikie masuala yao ya kifedha. Kama Angejua kwamba Yuda angebadhiri pesa, Asingemwacha asimamie pesa hizo. Mtu anaweza kusema kwamba Yesu hakujua mwanzo kwamba mtu huyu hakuwa mwaminifu na alikuwa mdanganyifu, na kwamba aliwadanganya kaka na dada zake. Baadaye, baada ya Yuda kumfuata Yesu kwa muda fulani, Yesu alimwona Yuda akiwadanganya kaka na dada zake na kumdanganya Mungu. Watu waligundua pia kwamba siku zote alitumia pesa kutoka kwenye mfuko wa fedha na kisha wakamwambia Yesu. Yesu alipata habari tu kuhusu haya yote wakati huu. Kwa sababu Yesu alikuwa atekeleze kazi ya kusulubishwa na Alihitaji mtu wa kumsaliti, na Yuda alitokea tu kuwa mhusika mzuri wa wajibu huu, Yesu akasema, “Kutakuwepo miongoni mwenu ambaye atanisaliti Mimi. Mwana wa Adamu atatumia usaliti huu kuweza kusulubishwa na baada ya siku tatu atafufuka.” Kwa wakati huo Yesu hakumchagua hasa Yuda ili aweze kumsaliti Yeye; kinyume chake, Alitumaini kuwa Yuda angekuwa mwanafunzi mtiifu. Bila kutarajia, Yuda aligeuka kuwa mtu mpotovu mwenye tamaa ambaye alimsaliti Bwana, na Akatumia hali hii kumchagua Yuda kwa kazi hii. Kama wanafunzi wote kumi na wawili wa Yesu wangekuwa watiifu, na hakuna mtu kama Yuda ambaye angekuwa miongoni mwao, yule mtu wa kumsaliti Yesu angekuwa hatimaye mtu kutoka nje ya wale wanafunzi. Hata hivyo, kwa wakati huo ilitokea tu kwamba kulikuwa na mmoja kati ya wanafunzi ambaye alifurahia kupokea rushwa—Yuda. Kwa hivyo Yesu alimtumia mtu huyu kukamilisha kazi Yake. Jambo hili lilikuwa rahisi jinsi gani! Yesu hakuwa Amepanga hili mwanzoni mwa kazi Yake; Alifanya tu uamuzi huu mara tu mambo yalipoendelea hadi hatua fulani. Huu ulikuwa ni uamuzi wa Yesu, yaani, uamuzi wa Roho wa Mungu Mwenyewe. Wakati huo ni Yesu aliyemchagua Yuda; wakati Yuda alipomsaliti Yesu baadaye, haya yalikuwa ni matendo ya Roho Mtakatifu ili kuhudumia malengo Yake mwenyewe; ilikuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu kwa wakati huo. Wakati Yesu alipomchagua Yuda, Hakuwa na wazo lolote kwamba Angemsaliti. Alijua tu kwamba alikuwa Yuda Iskariote. Matokeo yenu yanaamuliwa pia kulingana na kiwango chenu cha kutii leo, na kulingana na kiwango chenu cha ukuaji wa maisha, na wala si kulingana na wazo miongoni mwa dhana za binadamu kwamba matokeo yako yalipangwa awali katika uumbaji wa ulimwengu. Lazima uelewe mambo haya waziwazi. Kazi hii yote haitekelezwi kulingana na mawazo yako.